Mbowe akabidhi ambulances 2 kwa hospitali za Machame, Hai

Wananchi wakiwa wamezingira magari hayo wakiyatizama kwa karibu.

Mbunge wa jimbo la Hai Mhe. Freeman Mbowe ametoa magari mawili ya kubebea wagonjwa (Ambulance) yaliyotolewa na kwa ajili ya kukabidhiwa kwa viongozi wa hosptali ya wilaya ya Hai pamoja na hosptali ya Machame inayosimamiwa na KKKT. Magari hayo yalikabidhiwa mbele ya wananchi waliofika katika viwanja vya soko la Kuni.

Pia, alitoa fedha taslimu zaidi ya shilingi milioni kumi kwa ajili ya ukarabati wa soko, shule na barabara.

Mbowe ambaye pia ni Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa alikamilisha hayo katika ziara yake kwenye maeneo tofauti ya Jimbo la Hai.Ndani ya magari hayo ya kubebea wagonjwa.


Mbunge wa jimbo la Hai,Freeman Mbowe akikabidhi nyaraka mbalimbali za magari hayo kwa Baba Mchungaji Asanterabi Swai ambaye pia ni mkuu wa jimbo kwa niaba ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheli Tanzania (KKKT).


Watumishi wa hosptali ya wilaya ya Hai,wakiondoka katika viwanja hivyo mara baada ya kukabidhiwa gari hilo.


Mbunge wa jimbo la Hai, Freeman Mbowe akikabidhi funguo wa gari kwa mganga mkuu wa wilaya ya Hai, Dkt Paul Chaote, msada uliotolewa kwa ajili ya hosptali ya wilaya ya Hai.
Baadhi ya wananchi waliofika kushuhudia makabidhiano ya msaada huo wa magari ya kubebea wagonjwa.


Mbunge wa Jimbo la Hai, Freeeman Mbowe akizungumza na wananchi mara baada ya kukabidhi msaada wa magari mawili ya kubebea wagonjwa.

Taariaf ya Dixon Busagaga/Michuzi blog - Kanda ya Kaskazini.

Wananchi washangaa wenzao kuwashambulia polisi IringaJumamosi, Aprili 11, 2015 -- VURUGU kubwa zimetokea leo katika eneo la Ipogolo mjini Iringa na kulazimisha askari wa kikosi cha kutuliza ghasia (FFU) kutumia mabomu ya machozi kuthibiti vurugu baada ya mtoto wa miaka kata 6 kugongwa na gari wakati akifanya biashara ya kuuza mboga mboga.

Wananchi wanaosadikika kuwa na hasira kali walianza kuwashambulia askari polisi waliofika kuchukua mwili huo kwa mawe kwa madai ya kuchelewa kufika eneo la tukio.

Wakizungumzia tukio hilo kwa mwandishi wa habari hizi, baadhi ya wananchi walisema kuwa mtoto huyo aligongwa majira ya saa 7 mchana na zaidi ya saa moja baada ya kutoa taarifa polisi ndipo walipofika eneo la tukio jambo lililowakwaza wananchi hao.

Walisema tayari baadhi ya askari waliopo eneo hilo la stendi kuu ya Ipogolo kwa kushirikiana na wananchi walifanikiwa kulikamata gari ambalo lilisababisha ajali hiyo.

Alisema Neema Sanga kuwa wakati tukio la kugongwa mtoto huyo likitokea, alikuwa jirani na eneo hilo katika msiba na kuwa wakati akiwa ameingia ndani ya nyumba hiyo yenye msiba kusaidia kugawa chakula, ghafla alipata taarifa kuwa wananchi wameanza vurugu kwa kuchoma moto matairi katika barabara hiyo kuu ya Iringa - Kilolo.

Hata hivyo alisema kuwa tukio hilo lilichukua zaidi ya dakika 45 polisi hao wa FFU kufika na kuanza  kutuliza vurugu hizo kwa kupiga mabomu ya machozi kuwatawanya wananchi zaidi ya 500 waliokuwa wamekusanyika eneo hilo kuzuia magari kuendelea kupita katika barabara hiyo huku baadhi yao wakitaka kufunga barabara kuu ya Mbeya - Iringa ambayo haihusiki kabisa na eneo lililotokea tukio hilo.

"Ni kweli mtoto kagongwa na gari na kufa tukio ambalo ni la kusikitisha sana na polisi baada ya kupigiwa simu wamefika eneo la tukio na kuchukua maiti ya mtoto huyo lakini tunajiuliza kwa nini vijana hao walianza kuwapiga mawe polisi na kufanya vurugu wakati gari lililogonga mtoto huyo likiwa limekamatwa..." alihoji Bi Sanga
Bi Sanga alisema wakati mwingine polisi wanalalamikiwa kuwa wanatumia nguvu zaidi ila kwa tukio hilo lawama zake anazipeleka kwa wananchi wenzake ambao walionyesha kufanya vurugu kwa kuchoma moto barabara hiyo ya lami na kupiga polisi huku wakitambua wazi polisi siyo waliosababisha ajali hiyo.

Naye John Kalinga aliiomba serikali kupitia Wizara ya Miundombinu kuangalia uwezekano wa kuweka matuta katika eneo hilo kwa madai kuwa hii ni ajali ya pili kutokea na kusababisha vifo toka eneo hilo lilipowekwa lami.

Mwandishi wa habari hizi alishuhudia baadhi ya vijana wakikimbilia kujificha katika nyumba moja iliyopo eneo hilo ambayo ilikuwa na msiba huku baadhi yao wakijifungia katika maduka na baa zilizopo eneo hilo kabla ya polisi kuwafuata na kuwakamata huko walikojificha na kuwaacha wale waliokimbilia msibani.

Kamanda wa polisi wa mkoa wa Iringa, Ramadhan Mungi hakuweza kupatikana kuzungumzia tukio hilo huku idadi ya vijana waliokamatwa kwa tuhuma za kuhusika katika vurugu hizo zaidi ya 20 walionekana wakipakiwa katika magari ya polisi.Askari wa FFU wakiwa katika msako wa kuwasaka waliohusika na vurugu hizo eneo la Ipogolo mjini IringaMoshi wa bomu la machozi ukiwa angani

Bomo la machozi likilipuka anganiAskari wa zimamoto wakizima moto katikati ya barabara ya Iringa - Kilolo leo


Askari wa jeshi la Zimamoto na uokoaji mjini Iringa akisaidia kumvusha mzee ambae alikuwa akikimbia mabomu na kujificha mtaroni

Mzee huyo akimpongeza askari kwa wema wake

Baadhi ya watuhumiwa wa vurugu hizo wakipakiwa katika gari la FFU
Magari ya polisi yakisafirisha watuhumiwa wa vurugu kwenda kituo cha polisi kati


Askari wa kikosi cha kutuliza ghasia FFU mchana huu wametumia mabomu ya machozi kuwatawanya wananchi waliokuwa wameziba barabara ya Iringa -Kilolo kwa kuchoma mataili


Wananchi hao wamefikia uamuzi huo Baada ya mtoto kugongwa na gari kwa zaidi ya saa Moja bila maiti kutolewa.


Kutokana na hali hiyo wananchi hao wa Eneo la Ipogolo walilazimika kuchoma moto barabara hiyo huku waliochoma mataili Kabla ya Polisi kutumia mabomu ya machozi kuwatawanya  • Taarifa tumeshirikishwa na Francis Godwin/MatukiodaimaBLOG

[audio] Mhitimu wa Chuo Kikuu abambwa makaburini akitimiza masharti ya mganga ili apate ajira

Dhana ya uchawi, ulozi na ushirikina ni kama imani nyingine. Ikishamwingia mtu, ni vigumu sana kumtoka hata ikiwa amesoma katika ngazi na kiwango cha juu. Dhana hii kwa bahati mbaya haijalishi pia jinsi/jinsia, kabila, rangi ya ngozi wala tabaka jingine maadamu umeikubali, matokeo yake  ndiyo kuongezeka kwa vitendo vinavyodhuru wengine hata kuwapotezea uhai.

Bofya kitufe cha pleya hapo chini umsikilize binti anayedai kuhitimu Chuo Kikuu mwaka jana lakini akalazimika kufuata ushauri wa mama yake wa kumwona mganga kwa lengo la kumwezesha kupata ajira...

Taarifa: Rais Kikwete amteua Lukumay (Katibu - Rufaa za Zabuni) na Makombe (Kamishna - Udhibiti Fedha Haramu)

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amemteua Bwana Kissiok Ole Mbille Lukumay kuwa Katibu Mtendaji wa Mamlaka ya Rufaa za Zabuni za Umma.

Aidha, Rais Kikwete amemteua Bwana Onesmo Hamis Makombe kuwa Kamishna wa Kitengo cha Kudhibiti Biashara ya Fedha Haramu.

Taarifa iliyotolewa Alhamisi, mjini Dar es Salaan na Ofisi ya Katibu Mkuu Kiongozi (KMK), Balozi Ombeni Sefue, inasema kuwa uteuzi wa maofisa hao wawili ulianza Ijumaa ya Machi 27, 2015.

Kabla ya uteuzi wake, Bwana Lukumay ambaye ana diploma in Materials Management na ni Certified Supplies Professional na pia ana MBA (Procurement and Logistics) alikuwa Ofisa Ugavi Mkuu na Kaimu Katibu Mtendaji wa Mamlaka ya Rufaa za Zabuni za Umma.

Naye Bwana Makombe kabla ya uteuzi wake alikuwa Kaimu Kamishna, Kitengo cha Kudhibiti Biashara ya Fedha Haramu. Kielimu, Bwana Makombe ana shahada za B.Com, CPA na MBA (Finance and Human Resources Management).

Imetolewa na;
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu – Dar es Salaam.

10 Aprili,2015

Rais Kikwete apokea ripoti ya uchunguzi wa "Operesheni Tokomeza"
Rais Kikwete amepokea ripoti kutoka kwa Jaji Mstaafu, Hamis Msumi ambaye alikuwa mwenyekiti wa Tume iliyoteuliwa na Rais Kikwete kuchunguza ukiukwaji wa sheria, kanuni na hadidu za rejea za utekelezaji wa 'operesheni tokomeza' iliyokuwa chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii wakati wa uongozi wa Waziri, Balozi Khamis Kagasheki.

Tume hiyo ilipewa jukumu la kupendekeza sheria stahiki za kuchukuliwa dhidi ya watakaobainika kuhusika na uvunjifu huo na kushauri namna bora ya utekelezaji wa operesheni kama hiyo hapo baadaye.

Tume hiyo ilitembelea mikoa 20 na kupokea maoni katika wilaya 38.

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete leo, Ijumaa, Aprili 10, 2015 amepokea Ripoti ya Uchunguzi wa Operesheni Tokomeza katika halfa fupi ilifanyika Ikulu, Dar es Salaam.

Mara baada ya kupokea Ripoti hiyo, Rais Kikwete ameishukuru Tume kwa kazi nzuri na kuongeza kuwa amefurahi kuwa suala zima la Operesheni Tokomeza sasa limefika mwisho wake.

Aidha, Rais amesema kuwa Serikali itaisoma Ripoti hiyo na katika wiki mbili itatoa maelezo ya jinsi Ripoti hiyo itakavyoshughulikiwa.

Rais Kikwete amepokea Ripoti hiyo kutoka kwa Balozi Jaji (mstaafu) Hamisi Amiri Msumi, Mwenyekiti wa Tume ambayo Rais Kikwete aliiteua Mei Mosi, mwaka jana, 2014, na kuitaka ichunguze tuhuma mbali mbali za uvunjifu wa Sheria, Kanuni, Taratibu na Hadidu za Rejea za Utekelezaji wa Operesheni Tokomeza.

Aidha, Rais Kikwete aliipa Tume hiyo jukumu la kupendekeza hatua stahiki za kisheria za kuchukua dhidi ya watakaobainika kuhusika na uvunjifu huo. Vile vile, Rais aliiagiza Tume hiyo ishauri namna bora ya utekelezaji wa Operesheni kama hiyo hapo baadaye.

Rais Kikwete pia aliipa Tume hiyo Hadidu za Rejea sita ambazo pia ziliainishwa katika Taarifa ya Serikali Nambari 131 ya 2014. Hadidu za Rejea hizo ni kama zifuatazo:

(a) Kuchunguza namna Operesheni Tokomeza ilivyotekelezwa;

(b) Kuchunguza iwapo maafisa waliotekeleza Operesheni Tomokeza walizingatia sheria, kanuni, taratibu na hadidu za rejea walizopewa;

(c) Kuchunguza iwapo maofisa waliotekeleza Operesheni Tokomeza walivunja sheria, kanuni, taratibu na hadidu rejea walizopewa.

(d) Kuchunguza iwapo kuna watu waliokiuka sheria yoyote wakati wa utekelezaji wa Operesheni Tokomeza na iwapo hatua zilizochukuliwa na maofisa wa Operesheni Tokomeza dhidi ya wakosaji hao na mali zao zilikuwa sahihi;

(e) Kupendekeza hatua zinazostahili kuchukuliwa dhidi ya maafisa wa Operesheni Tokomeza waliokiuka sheria, kanuni, taratibu na hadidu za rejea za Operesheno Tokomeza; na

(f) Kupendekeza mambo yanayopaswa kuzingatiwa wakati wa kupanga na kutekeleza Operesheni nyingine kama hii, ili kuepuka malalamiko mengine yasitokee.

Jaji Msumi amemweleza Rais Kikwete kuwa katika kutelekeza majukumu yake, Tume ilitembelea mikoa 20 na wilaya 38 na kupokea malalamiko mbali mbali kutoka kwa wafuatao:

(a) Viongozi wa Serikali ikiwa ni pamoja na mawaziri wanne waliojiuzulu kutokana na sakata hilo;
(b) Watekelezaji wa Operesheni; na

(c) Walalamikaji/wahanga wa Operesheni.

Jaji Msumi amemweleza Rais Kikwete kuwa Ripoti ya Tume ina Juzuu kumi, Juzuu ya kwanza ikiwa ni Muhtasari wa Taarifa ya Tume, Juzuu ya pili ikiwa ni Taarifa yenyewe ya Tume, Juzuu ya tatu hadi ya tisa ikiwa ni Mwenendo wa Ushahidi (Proceedings) na Juzuu ya kumi ikiwa ni vielelezo vilivyotolewa na mashahidi.

Mwisho.

Imetolewa na;
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu – Dar es Salaam.

10 Aprili, 2015

Aonavyo Wakudata: Wahapahapa vs Wakujakuja...


Mapitio ya magazeti kwenye Tv, Aprili 11, 2015