Raia hawa wote wa Burundi wanasubiri kuingia Tanzania


Hali halisi ya eneo la mpakani ambapo raia wanaokimbia kutoka Burundi wamekwama wakisubiri kuvushwa ili kuingia hifadhini nchini Tanzania.

Huduma ya kuziba tundu la moyo bila kupasua kifua yaanza Tanzania

Baadhi ya Waandishi wa habari wakifanya kazi yao na kuelekezwa namna (Cath Lab) mtambo wa kufanya uchunguzi na kuzibua mishipa ya damu inayopeleka damu kwenye moyo na pia kuziba matundu ndani ya moyo bila kufungua kifua.

Mwezi Mei tarehe 9, mwaka 2015, Tanzania imeandika historia nyingine baada ya kufanya Tiba ya moyo bila ya kufanya upasuaji kwa kuziba matundu yaliyoko kwenye moyo kwa kutumia “kifaa maalum” bila kufungua kifua kama ilivyozoeleka.

Tiba hii inafanyika kwa mara ya kwanza nchini kupitia Idara ya Tiba na Upasuaji Moyo ya Hospitali ya Taifa Muhimbili ikishirikiana na madaktari bingwa kutoka Hospitali ya Prince Sultan Cardiac Centre iliyoko Riyadh nchini Saudi Arabia ambao watakuwepo Muhimbili kwa siku tisa kuanzia tarehe 9 hadi 16 Mei, mwaka huu.

Madaktari hawa wamekuja kupitia taasisi ya Al Mutanda Islami Trust ya Uingereza. Akizungumza na wanahabari, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili Dkt. Hussein Kidanto amesema jumla ya wagonjwa zaidi ya 20 wanatarajiwa kupatiwa tiba hii.

Taaluma ya matibabu inabadilika kwa kasi kubwa sana duniani na ili Hospitali ya Taifa Muhimbili iweze kuenda sambamba na kasi hiyo ni muhimu na lazima kufanya ushirikiano na nchi ambazo zimepiga hatua kubwa kwenye nyanja mbalimbali za matibabu, amesema Dkt. Kidanto.

Tiba hii inafanyika kwa kutumia kifaa maalumu cha kuzibia sehemu yenye tundu kwenye moyo kupitia mishapa ya damu kufika kwenye tundu liliopo kwenye moyo ambao mtoto anazaliwa nayo. Kuna faida nyingi kufanya kwa tiba hii ambapo mgonjwa hatakaa wodini muda mrefu akisubiri kupona kidonda cha upasuaji ukilinganisha na kama angefunguliwa kifua, amesema Dkt. Kidanto. Aliongeza kuwa mara baada ya mgonjwa kupata tiba hii mgonjwa anaweza kuruhusiwa ndani ya siku moja hadi mbili na kuondoka kuendelea na shughuli zake za kawaida.

Katikati ni Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili Dkt. Hussein Kidanto akizungumza na waandishi wa habari. Kushoto kwake ni Prof. Jameel Alata ambaye ni Daktari Mwelekezi wa Magonjwa ya Watoto ambaye ameongoza timu ya madaktari bingwa kutoka Hospitali ya Prince Sultan Cardiac Centre iliyoko Riyadhi nchini Saudi Arabia ambao watakuwepo Muhimbili kwa siku tisa kuanzia tarehe 8 hadi 16 Mei, mwaka huu. Aliyepo mwisho kulia ni Sheikh Said Ahmed Abri ambaye ni Mwenyekiti Mtendaji wa Shirika lisilo la Kiserikali la Kiislam la hapa nchini liitwayo Dhi Nureyn Islamic Foundation na shirika hili ndilo lililoratibu timu hii ya madaktari kuja kutoa huduma.

Aprili mwaka huu, Tanzania iliandika historia ya kwanza kwa kuzibua mishipa ya damu inayopeleka damu kwenye moyo na kuweka kifaa maalumu kinachoitwa (stent) ambapo mtambo maaluum wa Cath Lab unatumika baada ya kufanya uchunguzi wa kuangalia mishipa ya damu inayoenda kwenye moyo jinsi unavyofanya kazi, na kama kuna mshipa umeziba uweze kuzibuliwa.

Tangu kuanzishwa kwa huduma hii mwezi uliopita jumla ya wagonjwa 31 walifanyiwa uchunguzi wa mishipa ya damu ya moyo na wagonjwa wanne waliweza kuzibuliwa mishipa yao ya moyo na kuwekewa stent ambapo damu iliweza kupita vizuri katika mishipa ya moyo, wagojwa wawili walihitaji upasuaji wa moyo wa haraka kuweza kutibiwa mishipa yao ya damu ya moyo kwa njia ya upasuaji. Ifikapo julai 31 mwaka huu tunatarajia idadi ya wagonjwa mia moja watapata huduma hii.

Dkt. Kidanto amesema kasi hii ya kutoa huduma hizi inatarajia kuleta tija kwa wagonjwa wenyewe, taifa na wafanyakazi ambao wanaona maendeleo mazuri ya wagonjwa wanaowahudumia inaongezeka. Huduma hizi mbili kuanzia kwenye uchunguzi hadi tiba hazijawahi kufanyika popote hapa nchini isipokuwa hapa Hospitali ya Taifa Muhimbili kupitia idara yake ya Tiba na Upasuaji Moyo.

“Kwa misingi hiyo, Tanzania imeandika historia ya pekee na uenda kasi ya kupeleka wagonjwa nje ya nchi ikapungua kwa kiasi kikubwa kwa wale watakaohitaji huduma hii kwa vitendo”
amesema Dkt. Kidanto.

“Moja wapo ya malengo yetu ni kuhakikisha tunashirikiana na taasisi za kitaaluma rafiki na kuwakaribisha kuja kufanya kazi na sisi katika mazingira yetu na hivyo kujenga uwezo hapa hapa nchini kwa watu wengi zaidi kuliko ambayo tungepeleka watalaam wetu wachache kwao kujifunza” alisema Dkt. Kidanto.

Dkt. Kidanto amesema, hadi kufikia Aprili mwaka huu jumla ya wagonjwa 453 wamefanyiwa upasuaji wa moyo ambapo wagonjwa 110 wamefanyiwa uchunguzi wa mishipa ya damu ya moyo. Utaratibu huu wa kushirikiana na wataalam mbali mbali kutoka nje utaendelea tena 16/05/2015-22/05/2015 kwa wataalam wa moyo kutoka Medical University of South Carolina chuo kikuu kabisa cha jimbo la South Carolina, Marekani kupitia Madaktari Afrika.

Tunatarajia kupokea kundi jingine liitwalo Save A Child’s Heart kutoka Israel Juni 28-Julai 5 2015. Na kama tulivyo eleza awali haya ushirikiano huu una dhumuni la kutoa huduma kwa wagonjwa wetu na mafunzo kwa wataalam wazawa hapahaoa nchini, amesema Dkt. Kidanto.
Watu 80 Simiyu wanaongea hovyo hovyo, waishiwa nguvu, waumwa vichwa

Hali ya taharuki imewakumba wananchi katika wilaya ya Meatu Mkoani Simiyu, baada ya kuibuka ugonjwa wa hajabu uliowakumba wananchi hao ambao dalili zake ni kuongea ovyo, kuishiwa nguvu pamoja na kuumwa kichwa.

Bado haijajulikana ni aina gani ya ugonjwa kutokana na baadhi ya waathirika waliofikishwa katika vituo vya afya kupimwa na kubainika hawana ugonjwa wowote na badala yake kubaki wakiweweseka.

Mkuu wa wilaya hiyo, Erasto Sima alisema kuwa ugonjwa huo ulianza usiku wa kuamkia tarehe 02 Mei 2015, katika kata za Mwandoya, Mwabusalu, Lingeka, Mwakisandu, Tindabuligi, Pamoja na Lubiga.

Sima alieleza kuwa tangu kuibuka kwa ugonjwa huo idadi ya wagonjwa imezidi kuongezeka kila siku, ambapo alibainisha kuwa mpaka jana wamefikia jumla ya wagonjwa 80 kutoka katika Kata hizo.

Aidha sima aliongeza kuwa timu ya wataalamu, wahudumu wa afya, pamoja na madaktari kutoka katika hospitali ya wilaya hiyo, tayari wamewasili katika kata hizo kwa kushirikina na wataalamu wa afya waliopo ili kuongeza nguvu kutoa huduma ya kwanza.

Alisema kuwa wagonjwa mbalimbali ambao wamekuwa wakiletwa wamekuwa wakionyesha dalili na kuishiwa nguvu, kuongea maneno yasiyoeleweka, kuwapiga wenzio, kugongwa na kichwa, kutokwa na mafua, ikiwa pamoja na kukohoa kikohozi kikavu.

Alieleza kuwa ofisi ya Mganga Mkuu wa Mkoa iliwasili baada ya kutokea kwa ugonjwa huo, ambapo sampuli zilichukuliwa kwa ajili ya kupelekwa katika hospitali ya rufaa Bugando iliyoko Mkoani Mwanza kwa ajili ya vipimo ili kubaini ni aina gani ya ugonjwa.

Alisema kuwa taarifa alizozipata ambazo hana uhakika nazo kutokana na kutokudhibitishwa na wataalamu, kuwa ugonjwa huo unaambukizwa na wanyama wa porini kwa kile alichoeleza baadhi ya waathirika wanapakana na pori tengefu la Maswa.

Hata hivyo aliongeza kuwa awali walipata taarifa kutoka kwa wananchi kuwa kabla ya kutokea ugonjwa huo kwao mifugo ikiwemo ng’ombe ilikuwa ikishika na ugonjwa huo kwa kuweweseka hadi kupoteza uhai.

Aliongeza kuwa bado hawajatambua ikiwa ugonjwa huo unaambukizwa kwa hewa, au kushikana mikoni kwa kile alichoeleza bado wanasubiri majibu ya vipimo vilivyochukuliwa katika hospitali ya rufaa ya Bugando.

“Bado hatujatambua dalili zake ni nini? Unaambukizwaje?.. kutokana na vipimo vilivyopelekwa vikiwa bado havijarejeshwa…lakini huduma ya kwanza inaendelea kutolewa na tumeongeza nguvu za kutoa huduma hizo” 
alisema Sima.

Aliongeza kuwa ugonjwa huo unawapa watu wa marika yote wakiwemo watoto, huku akieleza kuwa Afisa Mifugo na Misitu ametumwa katika ameneo hayo ili kuchunguza kama ugonjwa huo unasababishwa na wanyama kama ilivyoelezwa na wananchi hao.

Kuhusu ugonjwa kuhusishwa na imani za kishirikina,  Mkuu huyo wa Wilaya alikanusha habari hizo na kueleza kuwa hakuna dalili ambazo zimeoneshwa kuwa ugonjwa huo unatokana na imani za ishirikina.

Aliongeza kuwa baadhi ya wagonjwa ambao wamefika kupatiwa huduma kutokana na ugonjwa huo, walikutwa na magonjwa mengine mbalimbali ukiwemo ugonjwa wa malaria ambao alisema walitibiwa na kupona hadi kuruhusiwa kwenda nyumbani.

Alipotafutwa, Mganga Mkuu wa Wilaya hiyo, Majeda Kihulya alikataa kuongelea suala hilo, huku akieleza kuwa majibu ya vipimo vilivyopelekwa Bugando yatakapoletwa na Mkuu wa Wilaya husika ndiye atakayetoa taarifa katika vyombo vya habari.

Basi la Dar Express laungua motoKamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Jafari Ibrahimu amesema basi la kampuni ya Dar Express lililokuwa likitokea Dar es Salaam kwenda Arusha, leo mchana limeteketea kwa moto eneo la Kwamakocho, Kijiji cha Kimange, wilayani Bagamoyo, Mkoa wa Pwani. Eneo la Kwamakocho lipo katikati ya eneo la Mandela na Mbwewe mkoani Tanga.

RPC Jafari Ibrahimu amesema kuwa abiria wote waliokuwemo ndani ya basi hilo wako salama. Chanzo cha moto huo bado hakijajulikana na akasema uchunguzi unaendelea.

  • via ITV

Timu zilizoshuka, zilizopanda daraja Ligi Kuu ya Soka


Timu za African Sports (Tanga), Majimaji (Ruvuma), Toto Africans (Mwanza), na Mwadui (Shinyanga) zitacheza Ligi Kuu msimu ujao.


Timu za Polisi Morogoro na Ruvu Shooting ya Pwani zimeteremka daraja, zitashiriki ligi daraja la kwanza msimu ujao.

[update] Meli ya Mv Maendeleo

Mv Maendeleo ikiwa imetegesha katika katika eneo la bandari ya Mkoani Pemba.

Meli ya Mv Maendeleo imetia nanga salama katika bandari ya Unguja ikitokea kisiwani Pemba baada ya kukwama kwa muda wa saa kadha katika eneo la bandari ya Mkoani.

Akizungumza kwa njia ya simu kutoka bandarini Unguja na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazanzibari nchini Marekani (ZADIA) Bwana Omar Haji Ali, Afisa wa ngazi za juu katika MV Maendeleo alithibitsha kuwa meli hiyo imetia nanga ikiwa na abiria wote salama.

"Siwezi kuzungumza sana kwa sasa kwa vile bado tumo katika harakati za kushusha abiria", alisema afisa huyo na kuongeza kuwa atakuwa katika nafasi nzuri zaidi ya kuongea baadaya mkutano na maofisa wa ngazi za juu wa Serikali ya Zanzibar utakaofanyika mara tu baada ya kumaliza kuwashusha wa abiria.

Mawasiliano ya Ndugu Omar Ali na maofisa wa ngazi za juu katika Serikali ya Zanzibar na MV Maendeleo, yanakuja katika juhudi za kuwapatia taarifa za uhakika wanachama wa ZADIA na Wazanzibari kwa ujumla nchini Marekani, kufutia hofu na mtafaruku uliojitokeza miongoni mwa wanajumuiya hiyo baada ya habari za kukwama kwa meli hiyo kisiwani Pemba.

Bwana Ali amewataka Wanajumiya kutokuwa na hofu yoyote juu ya ndugu na jamaa zao waliokuwa katika meli hiyo, kwani abiria wote wamefika salama u salmini.

Meli ya Mv Maendeleo ilikwama baada ya kukosea njia wakati ikitoka katika banndari ya Mkoani kisiwani Pemba ikiwa na abiria zaidi ya 260.

Bado haijajulikana rasmi ni hasara gani za kiuchumi zilizosababishwa na mkwamo huo wa abiria ambao baadhi yao walikuwa katika safari za kibiashara.

Taarifa zaidi baada ya mazungumzo na maofisa wa ngazi za juu wa MV Maendeleo.


  • Tumeshirikishwa taarifa hii mpya/update na blogu ya Swahilivilla


--------

Tujikumbushe: Mafuriko ya mvua Dar mwaka 2011


[video] Zoezi la uokozi lilivyofanyika jijini Dar es Salaam


Inaripotiwa kuwa watu nane wamepoteza maisha -- 6 Kinondoni na 2 Temeke -- huku wengine 12 wakiokolewa kutoka kweenye nyumba zao baada ya kuzingirwa na maji eneo la Kinondoni Mkwajuni jijini Dar es Salaam.

Kituo cha ITV kilikuwepo katika zoezi hilo kama inavyooneshwa kwenye video iliyopachikwa hapo.

Rambirambi zatolewa Congo kwa askari WatanzaniaMashirika ya kutetea haki za binaadamu mashariki mwa Congo DR, yametoa rambimbi kwa serikali ya Tanzania na wananchi wake huku mili ya askari wawili waliouawa wakilinda amani huko DRC ikisafirishwa kutoka Beni hadi Entembe na kurejeshwa nchini kwa maziko.

Rais Kikwete ziarani Algeria

Rais was Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete akilakiwa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Algeria Mheshimiwa Abdelmalek Sellal alipowasili mjini Algiers, mji mkuu wa Algeria, mchana wa leo, Jumamosi, Mei 9, 2015 kuanza ziara rasmi ya Kiserikali ya siku tatu katika nchi hiyo rafiki wa miaka mingi wa Tanzania kwa mwaliko wa Rais Abdelaziz Bouteflika.

Rais was Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amewasili mjini Algiers, mji mkuu wa Algeria, mchana wa leo, Jumamosi, Mei 9, 2015 kuanza ziara rasmi ya Kiserikali ya siku tatu katika nchi hiyo rafiki wa miaka mingi wa Tanzania kwa mwaliko wa Rais Abdelaziz Bouteflika.

Rais Kikwete amewasili katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Algeria akitokea New York, Marekani, ambako kwa wiki nzima amekuwa anaendesha vikao vya Jopo la Watu Mashuhuri Duniani ambao wanatafuta jinsi gani dunia inaweza kujiandaa vizuri zaidi kukabiliana na majanga ya afya, na hasa magonjwa ya milipuko, katika siku zijazo kufuatia balaa la ugonjwa wa Ebola katika nchi za Afrika Magharibi za Guinea, Liberia na Sierra Leone.

Kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Houari Boumediene mjini Algiers, Rais Kikwete amepokelewa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Algeria Mheshimiwa Abdelmalek Sellal kabla ya kuelekea kwenye Kasri ya Kirais ya Zeralda ambako amefikia.

Baadaye jana jioni, Rais Kikwete ameweka shada la maua kwenye Mnara wa Taifa kwa heshima ya wanamapinduzi waliopoteza maisha yao katika vita vya ukombozi wa kuwania uhuru wa Algeria kutoka kwa Wafaransa.

Algeria ilipata uhuru kutoka kwa Wafaransa mwaka 1962 baada ya vita kali ya ukombozi ya miaka minane, ambako pia wananchi wanaokadiriwa milioni mbili walipoteza maisha yao.

Baadaye, Rais Kikwete pia amembelea Jumba la Makumbusho la Mashujaa wa Vita ya Ukombozi mjini Algiers.

Kesho, Jumapili, Mei 10, 2015, Rais Kikwete atahudhuria dhifa ya kitaifa ambayo itaandaliwa kwa heshima yake na Waziri Mkuu ambaye atafanya naye mkutano rasmi kabla ya dhifa.

Baadaye, Rais atakwenda kwa mazungumzo rasmi ya Kiserikali na Rais Abdelaziz Bouteflika, ambaye mwaka jana alichaguliwa tena kwa mara ya nne kuongoza Algeria tokea alipochaguliwa kuwa Rais kwa mara ya kwanza mwaka 1999 baada ya kutumikia kama Waziri wa Mambo ya Nje ya nchi yake kwa miaka mingi. Tokea 1999, alichaguliwa tena 2004, mwaka 2009 na mwaka jana.

Tanzania na Algeria zimekuwa marafiki wa karibu kwa miaka mingi tokea uhusiano ulipoanzishwa na waanzilishi wa mataifa hayo mawili, Hayati Mwalimu Julius Nyerere na Hayati Ben Bella. Kwa hakika, Algeria ilikuwa moja ya nchi chache duniani zilizoisaidia sana Tanzania wakati wa Vita ya Kagera dhidi ya Idi Amin.

Tanzania pia imekuwa inapata misaada mikubwa kutoka Algeria katika sekta za gesi a elimu na katika kitendo kilichothibitisha ukaribu kati ya Tanzania na Algeria, mwaka 2010, Algeria iliifutia Tanzania kiasi cha dola za Marekani milioni 144. Kiasi hicho kilikuwa ni pamoja na deni la awali la dola milioni 58.03, deni ambalo liliongezeka kwa sababu ya mikopo ya mafuta ambayo Tanzania ilikuwa inapata kutoka Algeria na riba.


Bendera za Tanzania na Algera zikiwa zimepamba jiji la Algiers, Algeria, ambako Rais was Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amewasili mchana wa leo, Jumamosi, Mei 9, 2015 kuanza ziara rasmi ya Kiserikali ya siku tatu katika nchi hiyo rafiki wa miaka mingi wa Tanzania kwa mwaliko wa Rais Abdelaziz Bouteflika. 

Rais was Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete na ujumbe wake wakiongea na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Algeria Mheshimiwa Abdelmalek Sellal alipowasili mjini Algiers, mji mkuu wa Algeria, mchana wa leo, Jumamosi, Mei 9, 2015 kuanza ziara rasmi ya Kiserikali ya siku tatu katika nchi hiyo rafiki wa miaka mingi wa Tanzania kwa mwaliko wa Rais Abdelaziz Bouteflika.

Ombi la mawasiliano ya Maulid Kambaya

Msomaji mmoja wa wavuti.com ametuma ombi ambalo naliwasilisha kwenu, mwenye majibu tafadhali mfahamishe kupitia kisanduku cha maoni hapo chini:

Nna hamu sana kuwasiliana na waandazi wa kipindi cha Kumepambazuka Kiswahili kitokacho siku za Jumamosi, saa 1:30 hadi saa 3:00 za asubuhi. Tafadhali niunganishe na Maulid Kambaya ambaye ni mdau mkubwa wa lugha yetu hii.
Wakatabahu,
MWANAGENZI, Mswahili.