Sheikh Salum atangaza kuonekana kwa mwezi na kuanza kwa mfungo

Waislamu wa Tanzania leo wanaungana na waislamu wenzao Duniani kote kuanza mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani.

Imeripotiwa katika vyombo rasmi vya habari kuwa Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam Al-Haj Mussa Salum ameutangazia umma kuwa mwezi umeonekana katika maeneo mbalimbali ikiwa ni pamoja na mkoa wa Mtwara nchini Tanzania.

Tunawatakia Waislamu wote mfungo mwema na mwezi mtukufu wa Ramadhani.

Iko namna, si bure...

Gari ya abiri ikitoka Wete kwenda Chake Chake ikiwa katika maeneo ya Ole - Kianga, Juni 2015. (Picha na Abdi Suleiman, Pemba  via ZanziNews blog)

Waraka wa Luteni mstaafu Mberito Magova kwa CCM kuhusu Uchaguzi Mkuu 2015

CHAMA CHA MAPINDUZI

MCHAKATO, MKAKATI NA MWENENDO WA KUFANIKISHA UCHAGUZI MKUU WA DOLA KWA NAFASI YA (RAIS, WABUNGE NA MADIWANI) KWA MWEZI OKTOBA, 2015 TANZANIA
IMEANDALIWA NA LT. MK MAGOVA (MST) WA JWTZ NA CCM.
WA => “LYASA, IMAGE, KILOLO, IRINGA TANZANIA”

TAREHE 08 JUNI 2015

1.0     UTANGULINZI:
Tanzania ni taifa lenye mfumo wa vyama vingi vya siasa kidemokrasia, kwa mujibu wa Katiba ya (Jamhuri ya muungano wa Tanzania)ya mwaka 1977 toleo la mwaka 1992 mpaka sasa 2015.
Mpaka sasa kuna vyama vya siasa 20 ambavyo vimesajiliwa kisheria kwa mujibu wa Katiba ya nchi na vyama vyote vilivyo na usajili wa kudumu wanayo haki ya kusimisha wagombea (Urais, Wabunge na Madiwani) katika mchakato huu wa uchaguzi wa mwaka huu wa Oktoba, 2015.

Watanzania tuko huru kwa mujibu wa Katiba ya nchi, kugombea nafasi yeyote ya (Urais, Ubunge na Udiwani) kwa kuzingatia sheria za Tume ya uchaguzi bila vurugu wala shari.Wagombea wote ni lazima wazingatie Katiba na Kanuniya Tume ya uchaguzi na sheria za nchi. Pia bila kuingilia shughuli za vyombo vya Dola vya ulinzi na usalama (JWTZ, JKT, POLICE, MAGEREZA, UHAMIAJI  NA FIRE BRIGED), wakati wa shughuli za uchaguzi na kuwaheshimu wapiga kura.

Vyombo vya habari, ni vyombo muhimu sana kutoa habari juu ya mwenendo wa chaguzi. Pia vyombo vya habari ni kupata habari toka kwa mihimili ya Dola na kupeleka habari kwa wananchi, ili kutoa habari kwa wananchi kwa kutumia (TV, Radio na Magazeti) ili kujua mchakato na mwenendo wa uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani.

Waraka huu waelimishwe wana CCM kwa vikao au mikutano ya ndani.

2.0     MCHAKATO, MKAKATI NA MWENENDO WA UCHAGUZI:
2.1     Kwa mujibu wa Chama Cha Mapinduzi mchakato na mkakati wa mwenendo wa uchaguzi huazia kwa wanachama wa CCM kwa kutoa kura za maoni kwenye (Kata, Majimbo na Wilaya) na vikao vya kuwajadili wagombeawote waliogombea Urais, Ubunge na Udiwani kwa mujibu wa (Katiba na Kanuni ya uchaguzi)ndani ya CCM.

2.2      Vikao vya(Kamati ya maadili, Kamati ya sekretarieti, Kamati ya siasa, Halmashuri kuu na Mkutano mkuu) kwa ngazi ya Kata, Wilaya na Mkoa kwa kuwajadili (Wbunge na Madiwani) na kupendekeza kwenda ngazi za juu kwa uteuzi wa wagombea. Baada ya kuteuliwa watapambana na wagombea wa vyama vya upizani, kwa kunadi (Itikadi, Sera, Malengo, Mipango na Ilani)kwa kila Chama. Wananchi wataamua ni mgombea wa chama gani wanamtaka na kumchagua.

2.3     Kwa ngazi ya taifa kuna mchakato wavikao vya (Organazesheni, Sekretarieti, Kamati kuu, Halmashuri kuu na Mkutano mkuu) kwa ngazi ya taifa kwa kuwajadili wagombea Uraisbaada ya kudhaminiwa na wana CCM kwa zaidi ya mikoa 25 kwa (Tanzania bara na Zanzibar). Ndipo vikao hupendekeza na kuteua mgombea mmoja wa CCM kugombea Urais kwa kupambana na wagombea Uraisna vyama vya upizani. Wpiga kura watamchagua wanayemtaka kwa mujibu wa kukubalika kwa (Itikadi, Sera, Malengo, Mipango na Ilani) kwa Chama Cha Mapinduzi.

3.0     MAMBO YA KUZINGATI KWA WAGOMBEA WOTE WA (URAIS, UBUNGE
 NAUDIWANI) KWA CHAMA CHA MAPINDUZI:
3.1       Wananchi wakumbushwe mchakato wa historia ya utawala wa Tanzania.
A.      Tanzania ni taifa la muungano wan chi za (Tanganyika na Zanzibar) ambazo zote zilitawaliwa na wakoloni mbalimbali.
B.      Tanganyika na Zanzibar kulikuwa utawala wa kimila kwa kuongozwa na (Watemi, Watwa na Machifu) tangu mwaka 800 hadi mwaka 1885, wakoloni. Wajerumani walikuja mwaka 1880 na warabu waliingia  Zanzibar  tarehe 25/08/1896.
C.      Wananchi wazalendo wa Tnganyika walipinga wakoloni wa Ujerumani chini ya utawala wa Karl Peters, vilianza vita vya majimaji tangu tarehe 04/08/ 1905 hadi 1907 viliongozwa na Kinjikitile Bokero Ngwale kwa ukanda wa Ngarambe Matumbi. Walipigana (Mtwara, Lindi, Ruvuma, Pwani, Morogoro na Iringa)
D.     Vita kuu ya kwanza ya Dunia walipigana tangu mwaka 1914 hadi mwaka 1918.
E.      Vita kuu ya pili ya Dunia walipigana tangu mwaka mwaka 1939 hadi 1945.
F.       Tanganyika ilitawaliwa na Wajermani tangu mwaka 1885 hadi mwaka 1919.
G.      Waingereza walitawala tangu mwaka 1920 hadi mwaka 1961.
3.2        Tanganyika kupata uhuru na Zinzibar kufanya mapinduzi.
3.3        Mchakato wa kujitawala watanzania, mpaka sasa ni juhudi za
wananchi wanzalendo wa kujitolea bila malipo mpaka sasa.
A.    TANU ilipigania (haki, usawa, uhuru na kujitawala) tangu mwaka 1954 hadi mwaka 1961, mpaka sasa tunaishi kwa amani na utulivu.TANU iliongozwa na (Mwalimu Julius Kambarage Nyerere)
B.    ASPilipigania (haki, usawa, uhuru na kujitawala)tangu mwaka 1857 na kufanya mapinduzi Januari, 1964 wananchi wazalendo walijitolea bila malipo kufanya mapinduzi dhidi ya utawala wa Sultan toka Oman.ASPiliongozwa na (AbeidAmani Karume).
C.     Kwa uongozi wa mwenyekiti wa TANU.Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere (Baba wa Taifa)na mwenyekiti wa ASP.Hayati Abeid Amani Karume. Walihamasisha wananchi wa(Tanganyika na Zanzibar) kuungana Aprili, 1964 na kuwa Tanzania hadi sasa.
D.    Vyama vya siasa vya TANUnaASPni vyama vilivyoandaa uimara wa CCM katika (kutawala, kuongoza na kusimamia kwa nidhamu vyombo vya ulinzi usalama) kwa manufaa ya umma wa Tanzania.
E.     CCM tangu kuanza kazi ya kutawala mwaka 1977 ni chama chenye historia katika ulimwengu kwa mambo yafutayo:-
1)      Kiliimarisha uchumi wa taifa katika sekta za (kilimo, ufugaji, uvuvi, viwanda, biashara na wajasiriamali)
2)      Kiliimarisha na kusimamia vyombo vya (ulinzi na usalama)kwa kulinda wananchi, mali na mipaka ya nchi(anga, maji na nchi kavu).
3)      Kiliimarisha sekta za (elimu, afya, mawasilano, nishati, madini na siasa)
4)      Kufundisha wapigania uhuru wa nchi mojawapo wa nchi za kusini mwa Afrika(Angola, Mozambiki, Zimbabwe, Namibia na Afrika Kusini)ili kujitawala kidemokrasia. Makamanda na wapiganaji wa jeshi la JWTZ  walikufamashuja 101kwa kusaidia Mozambiki na makaburi yako Nambele Mtwara. Kwa hiyo wananchi wajue hitoria ya CCM juuya amani na utulivu.
5)      CCM ilipigana vita vya Kagera (Tanzania na Uganda)kwa kuvamiwa na majeshi ya Uganda kwa kuongozwa na Nduli Idd Amin tarehe 25,10/1978 na mapambano ya vita yalianza rasimi kuanzia (Miziro, Mtukula na Kakuto) tarehe 22/01/1979  hadi tarehe 25/07/1978. Hadi kuwakomboa Waganda.
6)      Daraja la mto Kagera lilivunja tarehe 25/10/1978  na kujengwa hadi kukamilika tarehe 03/11/1978 na majeshi ya JWTZ  yalianza kuvuka na kuanza mapambano.
7)      Mojawapo wa makamanda wa vita vya kung’oa utawala wa Dikteta Nduli Idd Amin wa Uganda ni kama wafuatao:-
A.      Mwalimu Julius JK Nyerere alikuwa (Amiri Jeshi Mkuu) wa vita vya Kagera.
B.      Abud Jumbe Mwinyi alikuwa makamu wa kwanza wa Rais Tanzania
C.      Rashid Mfaume Kawawa alikuwa makamu wa pili wa Rais Tanzania.
D.      Edward Moringe Sokoine alikuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano
E.       Jeneral Abdalah Twalipo Mkuu wa majeshi (JWTZ) wakati wa vita vya Kagera kati ya (Tanzania na Uganda).
F.       Jeneral David Msuguli alikuwa Kamanda mkuu wa vita mstari wa mbele.
G.     Brigedia Silas Mayunga –Mti Mkavu alikuwa Brigedi Kommanda wa 206 KV kwa upande wa Kakunyu kelekea Mbarara Uganda.
H.      Brigedia John Keats Walden alikuwa Brigedi Kommanda wa 207 KV Miziro kuelekea Masaka Uganda .
I.        Brigedia Mwita Chacha Marwa—Kambale Mamba alikuwa Brigedi Kommanda wa 208 KV upande wa Mtukula kuelekea Masaka Uganda.
J.        Kuna mafisa na wapiganaji walipigana vita vya Kagera usiku na mchana kwa (ushupavu na ujasiri) na walikufa mashujaa 601na kuzikwa Kaboya Bukoba Kagera, mpaka sasa familia za mashujaa hao wanaishi kwaa shida.
K.      Wananchi  waliandaliwa mafunzo ya Mgambo na JWTZili kwenda kupigana vita na majeshi ya kivita toka Uganda.

4.0          MCHAKATO NA MWENENDO WA VYAMA VYA SIASA TANZANIA:
4.1          Tanzania kuna mchakato wa historia wa vyama vya siasa tangu mwaka 1977
mpakaSasa mwaka huu wa 2015, lakini CCM ina mchakato ufutao:-
A.      Mwaka 1977 vyama vya TANUna ASPwanachama wa vyama hivyo walaamwua
kuunga na kuwa (CCM => CHAMA CHA MAPINDUZI) mpaka sasa ni chama tawala.
B.      Lengo la kuungana CCMna ASPilikuwa ni kuimarisha (upendo, umoja, undugu,
mshikamano, uelewano, uzawa, uhuru, uzalendo na mahusiano bora)
C.      Kuimarisha masuala ya (amani, utulivu, ulinzi, usalama na kubinafasi).
D.     Kulaani, kukemea na kupinga masuala ya (siasa uchwara, udini, ukabila, ubaguzi wa
 rangi, ulevi wa madaraka, rushwa, hongo na takrima).
4.2       Tangu mwaka 1977 kulikuwa na mfumo wa chama kimoja tawalana kusimamia
vyombo vya ulinzi na usalama cha CCMhadimwaka1992.Ulipoanza mfumo wa
vyamavingi vya siasa mpaka sasa.
A.      CCM mwaka 1992 ilitoa maoni kwa wanachi wapige kura kuwa na mfumo wa vyama vingi au uendelee mfumo wa chama kimoja.
B.      Matokeo ya kura za maoni, wananchi 80% walitaka uendelee mfumo wa chama kimoja kutawala na wananchi 20% walitaka mfumo wa vyama vingi vya siasa.
C.      Mchakato wa vikao vya CCM vilianza kujadili na kufanya upembuzi yakinifu ili kufikia muafaka. CCMilimwita Mwalimu JK Nyerere (Baba wa Taifa)atoe maoni yake juu ya maoni ya wananchi. Alisema kuwa,kwa mujibu wa haki ya Demokrasia ni kwamba, wengi wape lakini kwa sasa duniani nchi nyingi kuna mfumo wa vyama vingi.Tanzania haiwezi kujitenga na mataifa kiuchumi na kisiasa. Kwa hiyo wananchi waelimishwe kuwe na mfumo wa vyama vingi vya siasa ili kuepukana na vurugu za watu wachache katika taifa, amani na utulivu ndani ya umma vitatoweka. Kwa hiyo wachache wanaopenda mfumo wa vyama vingi wakubalike.
4.3          Chaguzi kuu chini ya mfumo wa vyama vingi vya siasa tangu mwaka1995 hadi
uchaguzi wa mwaka 2010 ni kama ufutao:-
A.      Uchaguzi wa mwaka 1995 CCMkilipata 69% na vyama vya upizani walipata 31%, CCM kilishinda.
B.      Uchaguzi wa mwaka 2000CCMkilipata 71% na vyama vya upizani walipata 29%, CCM kilishinda.
C.      Uchaguzi wa mwaka 2005 CCMkilipata 82% na vyama vya upizani walipata 18%, CCM kilishinda.
D.     Uchaguzi wa mwaka 2010 CCMkilipata 61% na vyama vya upizani walipata 39%, CCMkilishinda.
4.4        Kwa mchakato huo wa mwenedo wa uchaguzi mkuu wa Dola tangu mwaka 1995 hadi
2010 Chama Cha Mapinduzi kilishinda. Je! Uchaguzi wa Oktoba,2015 ni chama kipi
kitashinda. Wana CCMni kuwa makini na hakuna kugawanyika na kukisaliti Chama Cha
Mapinduzi.Isipokuwa kwa kaulimbiu ya (umoja ni ushindi) izingatiwe.
4.5        Ushindi wa CCM kwa mwaka huu utatokana na kufanya vikao vya ndani kwa kutumia
jumuiya za CCM(WAZAZI, UWT na UVCCM)kuratibu takwimu za wapiga kura, wapenzi,
wakerketwa na washabiki wa CCM. Bila hivyo uchaguzi ni kulikoni ni lazima CCM kuwa
imara kwa kampeni.
5.0          CCM NI KUWA NA DHANA YA (UKWELI NA UWAZI)
5.1        Wajibu wa wagombea wa ngazi zote ni kueleza ukweli juu ya mapungu, matatizo, shida,
malalamiko na kero kwa wananchi (wakulima, wafugaji na wavuvi)wapewe maeneo ya
kufanyia shughuli zao za kilimo, mifugo na uvuvi. Siyo kuwanyang’anya maeneo yao na
kupewa wageni.
5.2       Wagombea kuwaeleza (wafanya biashara, wajasilia mali, mama lishe,machinga,
bodaboda, wasafirishaji wa ndege, meli, magari ya maroli na mabasi, mafuta, maji,
umeme, mawasiliano, na biashara nyingine) wazingatie sheria, za kulipa kodi na
kupewa maeneo ya biashara.
5.3       Wagombea kuwaambia haki zao (watumishi, wafanyakazi, walimu, madaktari, majeshi,
wastaafu, wazee, walemavu, wanawake wenye mimba, watoto, vijana kupata ajira,
matibau na dawa kuwa na ubora)
5.4       Wagombea kuwaeleza ukweli juu ya tuhuma zilizojitokeza juu ya wizi wa fedha za wananchi (ESCROW, ITPL, RUSHWA WIZI na EPA) licha watuhumiwa kesi zao ziko
mahakamani na vyombo vya sheria.
5.5       Wananchi wawe makini sana kuwachagua viongozi ambao si waadilifu, pia viongozi wa
 TAMISEMI kuratibu takwimu mbalimbali  za(wazee, wanaume, wanawake, walemavu,
watoto, vijana, vifaa vya usafiri, zana za kilimo, ukubwa wa maeneo, mifugo, makazi,
kaya, idadi ya shule, vituo vya afya, zahanati, haspitali, mashamba,  na miundombinu
mbalimbali) kwa Tanzania uchumi mkubwa uko vijijini ambako kuna watu wengi sana.
5.6        Suala la uwajibikaji juu ya (usawa, haki za binadamu na utawala bora) ni jukumu la
mihimili ya Dola (Serikali kuu, Bunge na Mahakama) kutenda haki kwa wananchi.
Mihimili ya Dola siyo kutuhumiana na kashifa, hasa wakiwa bungeni, huo si utawala
bora ila ni ukiukaji wa maudhui na maadili katika taifa letu.
5.7        Wananchi wawe makini kuwachagua viongozi watakaokuwa makini juu ya kusimamia
mazingira na matibabu kwenye vituo vya afya na hospitali pia kunakuwa na dawa za
kutosha, ambazo zina kiwango chenye ubora. Pia viongozi watakaochaguliwa wawe
makini sana juu ya bidhaa feki zinazoingizwa kwa njia za panya.
5.8        Viongozi na watendaji waache masuala ya dhuluma na kutotenda haki kuwalipa watu
sitahil zao iwapo fedha zitatolewa na serikali kwa shughuli za maendeleo ya jamii,
malipo ya safari na uhamisho au malipo kwenye matibabu.
5.9        Wananchi wawachague viongozi watakaosimamia haki za mahakama kuhukumu
mapema watu wenye makosa ya jinai, kuliko watu kulundikana mahabusu zaidi ya miaka
mitano bila kuhukumiwa, serikali inazidi kujenga Magereza kwa gharama. 

A.      MWISHO WANANCHI WAAMBIWE KWAMBA:-
B.      Serikali ni wananchi au umma ndio wanaolipa kodi kwa ajili ya maendeleo ya taifa.
C.      Hazina na BoT ni haki ya wananchi ambao hulipa kodi na VAT si haki ya mihimili ya Dola, fedha ni kwa ajili ya maendeleo na kujenga miundombinu mbalimbali kwa wananchi.

D.     Wananchi waambiwe kwamba(nchi na watu ni taifa) bila nchi na watu hakuna taifa. Kwa sasa kuna baadhi ya viongozi na watendaji hawajali kusimamia taifa katika masuala ya maendeleo, kwa manufaa ya taifa.
E.      Wananchi wawe makini kuangalia mali asili kama vile (wanyama, misitu, ndege, madini, maji na mazingira) ni jukumu la wananchi sehemu zao hasa vijini.
F.       Wananchi wawe makini kwa wagombea wanaotoa rushwa, hongo na takrima hawana sifa ya kuwaongoza wananchi katika taifa letu ila wana sifa ya kuhujumu uchumi.
G.     Wananchi wawe huru kuchagua kiongozi anayekuwa karibu na wanachi kwa kusikiliza na kupokea kero zao na ushauri  wakati wote siyo viongozi wa kushinda kwenye Baa hafai.
H.     Watanzana wote wajue kwamba, amani (haicheziwi, haikosewi na haijaribiwa) kwani amani ikitoweka ni (majuto, kufa, kuhangaika na kuimbia nchi yako) watu wote ni (kufikiri, kutafakari na chambua) nini maana ya (usawa, uhuru, uzalendo, demokrasia, kubinafasi, haki za binadamu na utawala bora) katika taifa letu la Tanzania vitazingatiwa.

+Kaulimbiu yetu tunahitaji (amani, siri, miiko, utulivu, upendo, mshikamano, umoja, uelewano, kukubaliana, ulinzi na usalama)ni kuzingatia wakati wa uchaguzi bila vurugu wala shari+

                                           --------------------------------------------
Lt Mberito Kimvelye Magova (mst)
(MBEKIMA)
KADA WA ELIMU YA JAMMI

=MUNGU IBARIKI TANZANIA, AFRIKA NA ULIMWENGU KWA UJUMLA=

[update] Jaji Agustino Ramadhani achukua fomu ya CCM ya kuwania Urais Tanzania 2015

18.06.2015*Achukua fomu CCM na kusema; “Chema chajiuza
*Atamba ana uwezo wa kutosha kuiongoza nchi
*Ni nguli wa sheria, mwanajeshi na kiongozi wa diniJAJI Mkuu Mstaafu wa Tanzania, Augustino Ramadhani (70) ambaye kwa sasa ni Rais wa Mahakama ya Afrika, amepandisha joto la urais ndani ya CCM, baada ya jana kuchukua fomu ya kuomba kuteuliwa na chama hicho kupeperusha bendera ya CCM katika uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu.

Mara baada ya kuchukua fomu, Jaji Ramadhani ambaye pia ni mwanajeshi aliyestaafu akiwa na cheo cha Brigedia Jenerali, kiongozi wa dini akiwa Mchungaji wa Kanisa Anglikana na mwanamichezo mahiri, alisema amejitokeza kwa kuwa ana uwezo wa kutosha katika kuongoza nchi.

Pia ameahidi kuyaangalia mapendekezo ya wananchi yaliyoachwa kwenye Katiba inayopendekezwa iwapo atapata ridhaa ya kuongoza nchi kwani katiba ni ya wananchi.

"Sina makeke ndiyo maana nimeongozana na watu wachache kuja kuchukua fomu, siku zote chema chajiuza," alisema.

Alisema yeye ni mtu safi na hajawahi kutajwa mahali popote kuhusika na ufisadi kutokana na kuwa na mapenzi wa kuitumikia nchi yake na atahakikisha anashughulika na tatizo la rushwa na ufisadi katika nchi.

Akiwa ameongozana na mkewe, Saada Mbarouk Ramadhani ambaye ni mwanajeshi wa ngazi ya juu mwenye cheo cha Luteni Kanali, alisema ana uzoefu wa kutosha ndio maana anaomba dhamana ya chama na wananchi ili aweze kuwa kiongozi mkuu wa nchi."Nina vigezo vya kutosha na nia uwezo najiamini, nataka nipate nafasi ya kuteuliwa na chama na baadaye niwe kiongozi mkuu wa Nchi ili kwa pamoja tuijenge nchi yetu," alisema

Jaji Mstaafu Ramadhani, tofauti na wagombea wengine zaidi ya 35 waliomtangulia kuchukua fomu CCM, hakujieleza, bali alitaka kuulizwa tu maswali na waandishi wa habari.

"Mimi sikuitisha kikao cha kutangaza nia ninataka waandishi waniulize maswali tu," alisema.

Alipoulizwa kama anaona kuna mgombea yeyote ambaye ni tishio kwake alisema, yeye ni Brigedia Jenerali hawezi kuogopa chochote.

Pia alipohojiwa akiwa rais atawezaje kuondoa tatizo la rushwa na ufisadi na hata tatizo la mauji ya watu wenye ulemavu wa ngozi, alisema matatizo hayo yote yatatafutiwa dawa mapema kwani hata alipokuwa Jaji Mkuu alizunguka mikoa 15 ambapo alikutana na wakuu wa mikoa na wilaya na walizungumzia suala hilo.

"Suala la rushwa na ufisadi ni mtoto pacha sheria zipo ni utekelezaji tu unaotakiwa," alisema.

Alisema tatizo la mauaji ya walemavu wa ngozi serikali inajitahidi na wale waliohusika wamefikishwa mahakamani wengine wamehukumiwa adhabu ya kifo na kinachosubiriwa ni utekelezaji wa adhabu hizo.

Alisema elimu zaidi inatakiwa kutolewa ili wananchi wafahamu viungo vya albino havileti utajiri.

Pia alipohojiwa kwamba, wakati akiwa kama Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Marekebisho ya Katiba kuna mapendekezo ya wananchi yaliachwa, atafanyaje akipata nafasi ya kuongoza nchi?

Alijibu kwa kusema Katiba ni ya wananchi si ya kwake, na atasikiliza matakwa ya wananchi kama wakihitaji yarudishwe basi yatarudishwa.

Alipohojiwa amekuwa mwanachama wa CCM tangu lini alisema ameingia kwenye siasa mwaka 1969. Alisema alikuwa mwanachama wa Umoja wa Vijana wa TANU tangu Agosti, mwaka 1969 wakati huo akiwa mwanafunzi wa Sheria katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.


Akiwa chuoni wakati akikaribia kumaliza shahada yake akatuma maombi ya kujiunga na jeshi na na akaulizwa kama ni mwanachama wa TANU akasema ni mwanachama wa Vijana wa TANU akaambiwa lazima awe mwanachama wa Tanu ndipo ajiunge na Jeshi.

Alisema alikwenda kufuatilia kadi ya TANU na alifanikiwa kuipata na aliendelea kuwa na mwanachama wa CCM hadi mwaka 1992 wakati mfumo wa vyama vingi vya siasa ulipoanza na Katiba kukataza Majaji kuwa wanachama wa vyama vya siasa.

Jaji Mstaafu Ramadhani alisema alipostaafu Ujaji mwaka 2011 alirudi tena na kuwa mwanachama wa CCM. Pia alipopata tu shahada ya chuo kikuu alijiunga na jeshi moja kwa moja na mwaka 1971 aliteuliwa kuwa Luteni Usu kwa alikaa makao makuu ya Jeshi na ilipoanzishwa Brigedi ya Faru mkoani Tabora.

Alisema Rais wa Zanzibar wakati huo, Mzee Aboud Jumbe alimuita arudi Zanzibar ili awe mwanasheria mkuu lakini alitaka kujifunza kwanza kabla ya kushika nafasi hiyo.

Mwaka 1978 akawa Naibu Jaji Mkuu wa Zanzibar na wakati wa Vita baina ya Tanzania na Uganda alikwenda vitani na alirejea Zanzibar mwishoni mwa mwaka 1979 na ndipo akateuliwa kuwa Jaji Mkuu wa Zanzibar.

Alipotoka Zanzibar aliteuliwa kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufaa Nchini kwa miaka 20, baadaye Jaji Mkuu miaka mitatu na nusu akastaafu na sasa ni Rais wa wa Mahakama ya Haki za Binadamu Afrika.

Historia yake


Jaji Augustino Ramadhani alizaliwa Desemba 28, 1945 mjini Unguja, Zanzibar akiwa mtoto wa pili kati ya wanane waliozaliwa kwa wazazi wake. Baba yake ni Mathew Douglas Ramadhani, raia wa Zanzibar aliyefariki dunia mwaka 1962 na mama yake, Bridget Ramadhani alifariki dunia mapema mwaka huu.

Watu wengi hushangaa kuona au kusikia ana majina mawili ya dini tofauti. Augustino (jina la Kikristo) na Ramadhani (jina la Kiislamu). Lakini ukweli wa mambo ni kuwa yeye ni Mkristo wa dhehebu la Anglikana na ni mchungaji wa kanisa hilo.

Elimu ya msingi aliianzia wilayani Mpwapwa Mkoa wa Dodoma katika Shule ya Msingi Mpwapwa mwaka 1952 -1953 darasa la kwanza na la pili. Baadaye alihamia mkoani Tabora na kusoma darasa la tatu na la nne katika Shule ya Mingi “Town School” mwaka 1954 – 1956. Mwaka 1957 – 1958 alisoma darasa la la sita na la saba katika Shule ya Msingi Kazel Hill (sasa inaitwa Shule ya Msingi Itetemia), kabla ya kurudi Mpwapwa ambako alikamilisha darasa la nane mwaka 1959.

Aijiunga na Shule ya Sekondari ya Wavulana Tabora mwaka 1960-1965 kwa ajili ya elimu ya kidato cha kwanza na nne pamoja na elimu ya kidato cha tano na sita. Baada ya kumaliza elimu ya sekondari alipata fursa ya kujiunga katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam akianza kusomea Sheria. Shahada hii nyeti aliisoma kuanzia mwaka 1966 hadi alipohitimu Machi 1970 na baada ya kuhitimu alijiunga na Jeshi la Kujenga Taifa kwa mujibu wa sheria na aliajiriwa katika Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), kufanya kazi za uanasheria.

Kwa mtu mwenye shahada ya chuo kikuu enzi za miaka ya 1970, kupanda vyeo kilikuwa kitu cha lazima. Jeshi halikuwa na wasomi wengi kama ilivyokuwa katika sekta nyingine na kila aliyekuwa na elimu kubwa alikuwa mtu muhimu.

Ndiyo maana haikushangaza kwamba mwaka 1971 tayari alikuwa Luteni (nyota mbili) akiwa kambi ya Mgulani na miaka sita baadaye akahamishiwa Brigedi ya Faru mkoani Tabora wakati huo akiwa tayari ni Meja.

Kutoka hapo, alifanya kazi jeshi na uraiani kwa vipindi tofauti hadi alipostaafu na sasa kujiona ameshakomaa katika nyanja nyingi, hivyo yuko tayari kuvaa viatu vya Rais wa Awamu ya Nne anayemaliza muda wake, Rais Jakaya Kikwete.

Anakuwa Mzanzibari wa tatu kujitosa Urais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania mwaka huu, wengine wakiwa Mtoto wa Mwasisi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Balozi Ali Karume na mwanadiplomasia aliyewahi kuwa Waziri wa Fedha wa Zanzibar na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Tanzania, Amina Salum Ali ambaye kwa sasa ni Balozi wa Umoja wa Afrika (AU) huko Marekani.

Taarifa ya Sifa Lubasi, HabariLEO Dodoma

------------
17.06.2015


Jaji Mkuu Mstaafu Agustino Steven Laurence Ramadhani amekabidhiwa fomu ya kuwania Urais wa Tanzania kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi huko mjini Dodoma leo.

Jaji Ramadhani amekumbusha kuwa aliwahi kuwa askari kwa cheo cha Luteni Usu mwaka 1971 na hatimaye Brigedia Jenerali na kupambana natika vita vya Uganda. Pia amesema mwaka 1978 alikuwa Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar.

Alisema kuwa baadaye aliteuliwa kuwa Jaji Mkuu Zanzibar na hatimaye Tanzania Bara hadi kustaafu kwake, na kwamba hadi sasa ni Jaji Mkuu wa Afrika na ni Mtanzania wa kwanza kushika nafasi hiyo, hivyo kutokana nafasi yake aliyokuwa nayo anasema ana uzoefu na ana uwezo na sifa za kuwa Rais wa Nchi hii. Amekumbusha pia kuwa ni msafi asiye na tuhuma za rushwa.

Alipoulizwa kuhusu suala la mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi (albino) kwa kusema kuwa akiwa Rais atahakikisha inatolewa elimu kwa wananchi ili kuondoa imani potofu ya kuwa viungo vya albino vinampa mtu utajiri au cheo.

Aidha akiwajibu waandishi wa habari kuhusu kuwa na wafuasi wengi wakati wa kuchukua fomu, alisema, "sipendi makeke wakati wa kuchukua fomu. Kibaya chajitembeza na kizuri chajiuza."

Jaji Ramadhan amekabidhiwa fomu kadhaa zikiwemo za kupeleka mikoani kuomba wadhamini mikoani na kisha kuzirudisha kwenye ofisi za Chama hicho Mjini Dodoma. [taarifa kwa mujibu wa blogu ya Ruvuma]
Serikali yazindua tovuti ya "Wananchi" kwa ajili ya kutoa dukuduku

WIZARA ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo kupitia Idara ya Habari- MAELEZO, imekamilisha kazi ya kuboresha Tovuti ya Wananchi na sasa iko hewani.

Akizungumza na waandishi wa habari kwenye ofisi za Wizara hiyo, Mkurugenzi wa MAELEZO Assah Mwambene, aliwataka wananchi kuitumia tovuti hiyo kupitia anuani ya www.wananchi.go.tz kuwasilisha hoja zao Serikalini ili ziweze kupatiwa majibu.

“Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo kupitia Idara ya Habari- MAELEZO, imekamilisha kufanya maboresho ya tovuti ijulikanayo kwa jina la Tovuti ya Wananchi” alisema Mwambene na kuongeza:

“Lengo letu sasa ni kutaka wananchi badala ya kuhangaika sana, akiwa sehemu yoyote ya nchi hii anaweza kuuliza swali kupitia mtandao wa intaneti kwa anuani ya www.wananchi.go.tz

Alisema mwananchi akiingia kwenye tovuti hiyo atakutana na sehemu ya kuweka hoja yake kuuliza swali, kutoa maoni, kutoa pongezi, kuwasilisha malalamiko yake na moja kwa moja yatapokelewa na MAELEZO na kufanyiwa kazi.

“Mwananchi anaweza kuandika swali moja kwa moja kwenye taasisi anayotaka swali lile liende, kwa mfano kama anataka swali lile liende Wizara ya Ardhi anaweza akaandika” alisema Mwambene na kuongeza:

“Sisi tutapata taarifa kwamba ameleta swali na tutalipeleka kwenye taasisi husika na tutaangalia na kuona je swali hilo limejibiwa ama halijajibiwa”.

Mwambene alifafanua kuwa kila siku MAELEZO itajua ni wizara gani ama taasisi gani ya Serikali imepelekewa swali gani na swali hilo limejibiwa au la.

Alisema tovuti hiyo ni chombo muhimu katika mabadiliko ya sayansi na teknolojia na itamfanya mwananchi asilazimike kutembea kutoka kwenda wizara moja hadi nyingne ama taasisi ya Serikali kushughulikia malalamiko yake.

Alitoa mfano kuwa hata mwananchi akitaka kujua jinsi ya kupata viza au huduma nyingine inayotolewa na Serikali ataweza kupatiwa majibu ndani ya muda mfupi sana kupitia tovuti hiyo ya Wananchi.

“Baadaye kuna jambo lingine ambalo bado tunalifanyia tathimini, ni suala la kwamba wanaanchi wanaweza kutumia simu zao za mkononi kutuma maswali na kupokea majibu” alisema Mwambene.

Alibainisha kuwa tathimini hiyo ikikamilika hivi karibuni, watatoa namba ambayo mwananchi anaweza kutumia ujumbe mfupi wa simu ya mokononi kutuma hoja yake Serikalini na kupatiwa majibu kupitia njia hiyo.

“Ni tovuti ambayo tunapenda wananchi waitumie ili kupunguza gharama na muda mwingi sana kwa mfano mtu kusafiri, kupanda gari kwenda wizarani au taasisi ya umma kufuatilia shida yake.Hivyo anaweza kutumia simu yake ya mkononi” alisema Mwambene na kuongeza:

“Lengo letu ni kwamba wananchi waone kama hiyo ni fursa muhimu ya mawasiliano na waone kuwa sasa hivi wanaweza kutuandikia ujumbe kuuliza swali au malalamiko na yatatufikia na kufanyiwa kazi”.

Mwambene alisema Wizara imejipanga vya kutosha kuhakikisha kwamba Serikali inawasiliana na wananchi wake kwa kusikiliza shida zao na kuzipatia majibu.

“Hii ni Serikali ya wananchi na lazima tuwasiliane na wananchi kwa njia yoyote ambayo ni rahisi kuwafikia na Serikali imeona hii ni njia rahisi zaidi kuwafikia kupitia mtandao huu wa Tovuti ya Wananchi” alisema.

Tovuti ya Wananchi imewahi kufanya kazi katika miaka iliyopita na baadaye ilisimama lakini sasa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo imeifanyia marekebisho makubwa na iko hewani.

Rais Kikwete aelekea India kwa ziara ya Kiserikali

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete yuko njiani kwenda India ambako atafanya ziara rasmi ya Kiserikali ya siku nne katika Jamhuri ya India kwa mwaliko wa Rais wa India, Mheshimiwa Pranab Mukherjee. Ziara hiyo, inaanza rasmi jioni ya leo, Jumatano, Juni 17, 2015.

Wakati wa ziara yake, Rais Kikwete ambaye anafuatana na Mama Salma Kikwete, mbali na kukutana na Rais Mukherjee kwa mazungumzo rasmi ya Kiserikali, atakutana kwa mazungumzo na Makamu wa Rais, Mheshimiwa Mohammad Hamid Ansari na Waziri Mkuu Narendra Damordadas Modi, ambaye aliingia madarakani rasmi Mei 26, mwaka jana, 2014 akiwa Waziri wa 15 wa Jamhuri ya India baada ya chama chake cha Bharatiya Janata Party (BJP) kushinda uchaguzi mkuu.

Ziara hii itakuwa ya pili kwa Rais Kikwete kutembelea India katika miaka 10 ya uongozi wake. Mwaka 2008, Rais Kikwete, akiwa Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika (AU), alitembelea India ambako alikuwa Mwenyekiti Mwenza wa Mkutano wa Kwanza wa Wakuu wa Nchi za Afrika na India (India-Africa Forum) uliofanyika mjini New Delhi, mji mkuu wa India pamoja na Waziri Mkuu wa India wakati huo, Mheshimiwa Manmohan Singh.

Wakati wa ziara yake, Rais Kikwete atatembelea miji ya New Delhi na Jaypur (Pink City of India) na miongoni mwa shughuli zake ni kukutana na Watanzania ambao wanaishi India, kukutana na wafanyabiashara wakubwa wa India wenye kutaka kuwekeza Tanzania na na kufungua Mkutano wa Kwanza wa Wafanyabiashara wa Tanzania na India (1st Indian-Tanzania Business Forum).

Mbali na wafanyabiashara, kiasi cha wanafunzi 2,500 wa Kitanzania wanasoma katika vyuo vikuu vya India kwa ufadhili wa Serikali za Tanzania na India. Hawa ni mbali na maelfu ya wanafunzi ambao wanajisomesha wenyewe katika vyuo vikuu vya nchi hiyo.

Rais pia atakutana kwa mazungumzo na Mtendaji Mkuu wa Shirika la Ndege la India, Air India, kwa nia ya kulishawishi shirika hilo kuanzisha tena safari za ndege kati ya nchi hizo mbili, atakutana na Mtendaji Mkuu wa Benki ya ICICI, benki kubwa binafsi kuliko zote katika India, ambayo inataka kuingia ubia na Benki ya Posta Tanzania, atakutana na Mkurugenzi wa Kampuni ya Infrastructure Leasing and Financial Services ambayo inataka kujenga barabara ya kisasa kabisa kati ya Dar es Salaam na Chalinze na miradi mikubwa ya maji.

Aidha, Rais Kikwete atakutana na kuzungumza na Mwenyekiti wa Kundi la Makampuni ya Hospitali za Apollo ambayo inataka kujenga hospitali kubwa na ya kisasa Kigamboni, Dar Es Salaam.

Rais Kikwete pia atatembelea kiwanda cha kutengeneza matrekta cha Fiat New Holland ambacho kimekuwa kinashirikiana kwa karibu na Kampuni ya Biashara ya Jeshi la Kujenga Taifa ya SUMA JKT na baadaye kutembelea Shirika la Taifa la Viwanda Vidogo la India.

Rais Kikwete ataungana na Waziri Mkuu Modi kushuhudia utiaji saini wa mikataba minne kati ya Tanzania na India katika maeneo ya utalii, maji na miundombinu.

Ziara ya Rais Kikwete katika India inatoa nafasi ya kuimarisha uhusiano wa kihistoria, wa karibu na wa kirafiki ambao una historia ndefu na ya karne nyingi na ambao uliimarishwa zaidi na uhusiano rasmi ambao ulianzishwa miaka 54 iliyopita. Kimsingi uhusiano huo umejengwa katika misingi ya biashara na mahusiano ya watu kwa watu.

India ndiyo nchi inayofanya biashara kubwa zaidi duniani na Tanzania. Mwaka 2013-14, biashara hiyo ilikadiriwa kufikia dola za Marekani bilioni nne. Mbali na uhusiano wa biashara, Watanzania wengi wamekuwa wanasaka huduma za afya na elimu katika India. Inakadiriwa kuwa tokea mwaka 1999 kiasi cha Watanzania 4,100 wamepata huduma za afya katika hospitali za Apollo pekee.

Inakadiriwa kuwa kuna wananchi kati ya 50,000 na 60,000 wenye asili ya India (PIO’s) ambao wanaishi na kufanya kazi katika Tanzania.

Imetolewa na;

Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu – Dar es Salaam.
17 Juni, 2015.