Kwa kuwa Lowasa yupo CHADEMA sasa haya maswali ya miaka 7 yatajibiwa?


MJADALA juu ya Edward Lowassa, mbunge wa Monduli, kuhama Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kujiunga na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), unaendelea kushika kasi.

Hili limetokea muda mfupi baada ya vyama vinavyounda Muungano wa Kutetea Katiba ya Wananchi (UKAWA), kunukuliwa wakimkaribisha Lowassa ndani ya umoja huo.

Katika mitandao ya kijamii na vyombo vya habari, ndani na nje ya nchi, mjadala umekuwa ukarimu wa vyama vya upinzani kwa Lowassa. Wapo wanaohoji:
 • Ni lini Lowassa amekuwa swahiba wa upinzani? 
 • Ni lini CHADEMA imeanza kuamini kuwa Lowassa ni mtu safi, mwadilifu na mchapakazi? 
 • Ni lini kimeanza kuamini kuwa Lowassa amesafishika kutoka katika lindi la tuhuma za ufisadi? 
 • Lini CHADEMA kimeanza kuamini kuwa Lowassa alionewa katika sakata la kashfa ya Richmond?
 • Je, hatua ya CHADEMA kumbeba Lowassa inalenga nini? 
Haya ndiyo maswali ambayo wananchi wanajiuliza na ambayo yanastahili kupatiwa majibu.

Akisoma tamko la vyama vinavyounda UKAWA – NCCR- Mageuzi, Chadema, Chama cha Wananchi (CUF) na National League for Democrats (NLD) – mbele ya waandishi wa habari, James Mbatia, mmoja wa wenyeviti wa UKAWA alisema, “…tunamkaribisha Lowassa UKAWA ili kukamilisha kazi ya kuing’oa CCM.” Mkutano kati ya waandishi wa habari na viongozi wakuu wa UKAWA, ulifanyika makao makuu ya CUF, Buguruni, jijini Dar es Salaam, Jumatatu wiki hii.

Hizi ndizo hoja ambazo wananchi wanataka ufafanuzi wake. CHADEMA na wale wote wanaomuunga mkono Lowassa kuamua kuondoka na minyororo ya utumwa ya CCM, wanatakiwa kuyatolea ufafanuzi.

Kwa mfano, wananchi wanapaswa kuelezwa, hoja juu ya uadilifu wa Lowassa au uchafu, siyo hoja tena jambo la mjadala kwa sasa. Lowassa amekuwa kimya miaka saba, hawezi kuibuka na kusema leo akasikilizwa.

Hata wale wanaompinga nje ya CHADEMA na kumwita “fisadi,” hawawezi kuwa na hoja ambazo zitamuumiza Lowassa. Hapa hoja kuu ni ujio wake ndani ya CHADEMA na UKAWA, ikiwa ni mwanzo wa mafuriko au ukame.

Lakini kitendo cha Lowassa kukaribishwa UKAWA kuwa mgombea urais, kitasaidia:
Kupatikana taarifa kuhusu ushiriki wa Lowassa katika sakata la umeme wa Richmond.
 1. Tutapata kufahamu nani aliyeisajili kampuni hiyo nchini? 
 2. Je, ni kweli ilisainiwa na Samwel Sitta, wakati alipokuwa mkurugenzi wa kituo cha uwekezaji nchini (TIC)?
 3. Tutapata kufahamu kwa nini Bunge lilimtuhumu kuhusika katika kuingiza nchi kwenye mkataba huo? Kwa nini Dk. Harisson Mwakyembe, aliyekuwa mwenyekiti wa Kamati Teule ya Bunge, iliyochunguza mkataba wa Richmond, alidai kuwa Lowassa alihusika na mkataba huo?
 4. Pamoja na kwamba Dk. Mwakyembe ameshindwa kuthibitisha kuwa Lowassa amepokea rushwa ili kuipatia kazi kampuni hiyo, bado ni muhimu yeye akaeleza, sababu zilizoipa kazi ya kufua umeme Richmond, wakati haikufanyiwa uchunguzi.
 5. Nani aliyeamrisha kutoa mkataba kwa Richmond na sababu zake? Alilipwa kiasi gani? 
 6. Je, akiwa Waziri Mkuu ambaye anatajwa katika Ibara ya 52 na 53 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano kuwa ndiye mwenye “udhibiti, usimamiaji na utekelezaji” wa shughuli za kila siku za serikali alitenda yote hayo kwa maelekezo ya nani? Au aliagizwa na rais?
 7. Uhusika wa Rais Jakaya Kikwete, katika suala hilo ukoje? Je, pale aliposema, “hakuna jambo nililolifanya ambalo wewe Rais Kikwete hukulifahamu au hukunituma kuhusu Richmond/Dowans” alilenga nini?
 8. Kueleza kwa nini alinyamazia pendekezo la aliyekuwa waziri wa nishati na madini, Dk. Ibrahim Msabaha, kuwa TANESCO iingie mkataba na Richmond! Wala hajawahi kukana hadharani au kutoa maelezo ya kilichosababisha kampuni hiyo ya kitapeli kupata mkataba katika giza la upendeleo. Hajaeleza alihusika vipi na suala hilo na hatua alizochukua.
 9. Kueleza hatua alizochukua kuhakikisha Sheria ya Manunuzi ya Umma (PPRA), inafuatwa.
 10. Kueleza kilichosababisha kujiuzulu uwaziri mkuu wakati anadai hakuwa na makosa. Je, alitaka kumfurihisha nani au alidaganywa na Kikwete? Hili ni muhimu akalieleza kwa kuwa baadhi ya wafuasi wake wanaamini kuwa Lowassa hakujiuzulu kwa sababu ya kuwajibika kutokana na makosa ambayo yeye, akiwa kiongozi na ofisi yake, walifanya kuhusiana na Richmond. Au hakujiuzulu kwa sababu alikubaliana na madai yaliyotolewa na Dk. Mwakyembe.
 11. Je, alijiuzulu kwa sababu aliamini kulikuwa na mkakati wa kumuondoa katika kiti chake; mkakati huo ulisukwa kwa ustadi mkubwa na baadhi ya wakubwa serikalini, akiwamo Sitta. Alijiuzulu kwa sababu aliamini Kamati Teule ya Bunge, haikutoa nafasi ya kujitetea? Alijiuzulu kupinga kile alichoita, “kutotendewa haki.”

 12. Tarehe 7 Februari 2008, Lowassa alisema, “…nimetafakari kwa makini sana jambo hili, nikajiuliza hivi kulikoni mpaka watu wazima wenye uwezo wao, watu maarufu wenye heshima zao, mpaka wafike mahali waache jambo la msingi kama hilo; kulikoni?” Aliongeza, “mimi nadhani tatizo, ni uwaziri mkuu. Nadhani tatizo ni uwaziri mkuu. Kwamba ionekane waziri mkuu ndio amefanya haya, tumuondolee heshima au tumwajibishe.”

  Kwamba Lowassa aliamua kujiuzulu badala ya kujitetea bungeni, ni fursa nyingine kwake kueleza kuwa akina Dk. Mwakyembe walisema “uongo” bungeni.

 13. Anapaswa kuumbua uongo huo hoja kwa hoja ili kulipa taifa nafasi ya kuuona ukweli. Pamoja na yeye kujiuzulu, serikali imeshindwa kutekeleza maazimio 11 ya Bunge, likiwamo Azimio Na. 11, linalohusu Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma (1995). Pamoja na kujiuzulu, bado viongozi waandamizi wenye dhamana ya kisiasa serikali wanaendelea na biashara zao binafsi wakiwa madarakani, jambo ambalo lina mgongano wa kimaslahi.
 14. Pamoja na yeye kujiuzulu, kwa nini serikali imeshindwa kufanya maandalizi ya majadiliano ya kina kuhusu suala hilo ndani na nje ya Bunge? Kwa nini imeshindwa kuunda kikundi kazi kufuatilia hili?
 15. Kwa nini waraka wenye mapendekezo ya kurekebisha sheria ya maadili ya viongozi wa umma, (Sura 398), ambao ulifikishwa hadi katika ngazi ya kujadiliwa na kamati ya makatibu wakuu (IMTC) haujakamilishwa? Mapendekezo ya waraka huo yanadaiwa yangesaidia kuweka utaratibu mahsusi kwa viongozi waandamizi wenye dhamana ya kisiasa na watendaji wa ngazi ya juu katika utumishi wa umma, kutenganisha shughuli zao za biashara na uongozi wa umma. Lengo ni kuepusha migongano ya kimaslahi katika utendaji wao. Lakini hakuna kilichofanyika na waraka haujakamilika.
Imeandikwa na Anaandika Saed Kubenea via MwanaHALISI ONLINE

Huduma ya kununua LUKU itakosekana nchi nzima Agosti 1 - 2, 2015


Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Felchesmi Mramba amesema kesho na keshokutwa hakutakuwa na huduma ya ununuzi wa umeme kupitia LUKU nchi nzima.

Hatua hiyo inatokana na kubadilisha mfumo wa uuzaji na usambazaji wa umeme kwa wateja kutoka Luku kwenda mfumo mpya wa 3E.

Alisema hayo juzi wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini hapa kuhusu taarifa zilizosambaa kuwa huduma hiyo haitakuwapo kwa siku saba na kufafanua kuwa huduma hiyo itakosekana kwa saa 24 tu.
“Mfumo huu wa LUKU haukidhi vizuri mahitaji ya wateja kutokana na kushindwa kuhudumia wateja wengi kwa wakati mmoja, lakini mfumo 3E unaweza kuhudumia wateja wengi zaidi”
Amewaomba wateja kuwa wavumilivu katika kipindi hicho cha kufanya marekebisho hayo ya mfumo. Mramba alisema mfumo wa 3E utaongeza ufanisi, ikiwa ni pamoja na wateja wote kupata huduma kwa urahisi na haraka kuliko hapo awali.

How to make juice/tea from pineapple skin and Turn watermelon rinds into pickles

Take notes from the video below...Avanti Communications: TTCL launches 100% National broadband coverage across Tanzania


LONDON--(BUSINESS WIRE)--TTCL, Tanzania's leading telecoms operator, announce this week exciting new digital capabilities with the launch of 100% national broadband coverage. Thanks to their new high speed satellite broadband service, homes and businesses now have the opportunity to enjoy a broadband connection to the internet of up to 15Mb speeds wherever they are in the country.

The launch of these services will also help a growing number of young people play a part in the global digital economy. This new generation of digital entrepreneurs can develop their ideas and collaborate with others to build their online businesses from even the most remote locations of Tanzania.

TTCL has designed its tariffs to suit the needs of the most demanding of individuals or businesses.

Peter Ngota, Chief Sales and Marketing Officer at TTCL, commented: “We are proud to announce the complete coverage of Tanzania with fast broadband services. It is appropriate that, hard on the heels of the recent Global Entrepreneurship Summit (GES 2015), we are able to support the entrepreneurial spirit of Tanzania.

“We know that fast reliable broadband is essential to develop our next generation of business leaders in the digital economy. No matter where they are TTCL provides broadband connectivity using all suitable technologies. This positions TTCL to support the national growth agenda for Tanzania and MDGs. Both Avanti and TTCL share the same commitment to quality, and together, we will help entrepreneurs grow allowing Tanzania to reach its full digital potential from today.”

Matthew O'Connor, Chief Operating Officer at Avanti Communications, commented: "We are very happy that TTCL has chosen Avanti to provide satellite-based broadband to its customers across the whole of Tanzania. The digital development of a modern economy needs full national coverage with modern broadband to prevent the emergence of a digital divide. TTCL are in the forefront of those companies delivering broadband to all areas for the benefit of as many homes, businesses and entrepreneurs, as possible."


Katuni za leo 31.07.15 kuhusu "siasa za Tanzania"


TAKUKURU yamsaka Mbunge aliyekimbia; Yafikisha vigogo 3 CAMARTEC kortini

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Arusha, imewaburuza mahakamani vigogo watatu wa Kituo cha Zana za Kilimo na Teknolojia (Camartec), kwa tuhuma za matumizi mabaya ya ofisi.

Ilidaiwa mbele ya Hakimu Patricia Kisinda wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Mfawidhi Wilaya ya Arusha/Arumeru kuwa, watuhumiwa hao walitoa zabuni ya matengenezo ya gari kwa kampuni ya Mbilinyi Auto Garage ambayo malipo yake yalikuwa Sh. 24,820, 000.

Mawakili wa Takukuru, Monica Kijazi na Rehema Mteta, walidai kuwa utaratibu wa kutoa zabuni ya matengenezo ya gari hiyo aina ya Toyota Land Cruizer ulikiuka Sheria ya Manunuzi na matumizi mabaya ya ofisi kinyume cha Sheria ya Takukuru.

Vigogo walioburuzwa mahakamani hapo ni Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Camartec, Elifariji Makongoro, Ofisa Manunuzi Absalom Nnko na Kaimu Ofisa Usafiri, Pythias Ntella.

Walidaiwa kwa kukiuka sheria hizo waliisababishia hasara Camartec ya Sh. 24, 820,000.
Hata hivyo, watuhumiwa hao wote walikana kutenda makosa hayo.

Mahakama ilisema kosa wanalotuhumiwa watuhumiwa hao lina dhamana na hakimu alitaja masharti kuwa ni lazima wadhaminiwe na watu wawili wenye vitambulisho kwa kila mmoja na kuweka bondi ya Sh. milioni 30 au mali isiyohamishika yenye thamani ya kiasi hicho cha fedha.

Watuhumiwa wote walifanikiwa kutimiza masharti na hivyo kupata dhamana hadi Agosti 24, mwaka huu kesi hiyo itakapoanza kusikilizwa ushahidi wa awali. [NIPASHE]

Pinda, Chambiri
Pinda, Chambiri

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoani Manyara, imemhusisha Mbunge wa Babati Mjini, Kisyeri Chambiri (pichani kulia), na tuhuma za kutoa hongo katika kura za maoni ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Takukuru inadai kuwa mbunge huyio alinusurika kukamatwa juzi usiku akiwa na wapambe wake waliokuwa wanagawa rushwa.

Kamanda wa Takukuru mkoani Manyara, Mogasa Mogasa, alisema Chambiri akiwa na wezake watatu ambao wanashikiliwa na taasisi hiyo, alinusurika kwa kutimua mbio usiku majira ya saa nne na kuacha kitita chaSh. 500, 000 alizokuwa nazo katika kijiji cha Kiongozi akitaka kuzigawa kwa baadhi ya watu wake.

Pia taarifa ya kamanda huyo ilieleza kuwa Chambiri alifanikiwa kukimbia akiwa na viongozi kadhaa wa kijiji hicho ambao kamanda huyo hakuta kuwataja majina, akisema kuwa wanaendelea kutafutwa na kumtaka Chambiri ajisalimishe.

Kamanda huyo aliwataja waliyokamatwa kuwa ni Samuel John Barani ambaye ni Katibu wa Uchumi na Fedha CCM wilaya; Thomas Cosmas Darabe na Ally Ayubu Ramadhani, ambao walikuwa na mgombea huyo katika harakati hizo.

Kamanda Mogasa paliongeza kuwa baada ya watuhumiwa hao kukutwa katika eneo hilo na Chambiri kutokomea, walifanikiwa pia kukamata makaratasi yenye majina ya watu waliokuwa wameandaliwa kwa ajili ya mgawo huo.

Hata hivyo, alisema wanaendelea na mahojiano watuhumiwa hao na kwamba baada ya taratibu kukamilika watafikishwa mahakamani na kuongeza kuwa wanalishikilia gari la mbunge huyo.

Chambiri alipoulizwa, alikana kuhusika na kudai kuwa ni mbinu zinazotumiwa na baadhi ya watu wasiyomtakia mema.

Aidha, alidai kuwa yeye kama mgombea na mtetezi wa jimbo hilo, amekuwa akipata taarifa mara kwa mara za kupangiwa njama kama hizo ili kudhoofisha juhuddi zake za kurejea madarakani.

“Hivi walishindwaje kunikamata wakati wanadai walitukuta tukiwa ndani kama siyo uzushi, mimi nafahamu kuna watu wamewekwa kunichunga hata kama naenda nyumbani kisa tu mimi nisichanguliwe, na hiyo ni baada ya kuona watu wameonyesha upendo kwangu,” alisema Chambiri. [NIPASHE]

NEC: Fomu za Urais, Ubunge, Udiwani Tanzania 2015 kuanza kutolewa kesho


Fomu za kugombea nyadhifa mbalimbali za uongozi nchini Tanzania katika uchaguzi wa Oktoba mwaka huu zinaanza kutolewa kesho na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).

Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji Mstaafu, Damian Lubuva amesema:
 1. Fomu za Urais, Ubunge na Udiwani zitatolewa hadi Agosti 21, 2015.
 2. Fomu ya Urais itatolewa bure lakini itarudishwa kwa dhamana ya shilingi milioni moja na wadhamini 200 kutoka mikoa yote ya Tanzania ikiwemo mikoa miwili ya Zanzibar.
 3. Fomu za Ubunge gharama yake ni sh.50,000 wakati zile za Udiwani sh.5000.
 4. Fomu hizo zitachukuliwa katika Ofisi za Wilaya.
 5. Wanaochukua na kurudisha fomu wazingatie kutokuambatana na kundi kubwa ambalo linaweza kusimamisha shughuli za watu wengine.

Maswali yazidi majibu kuhusu Dk Slaa, Mnyika...


Hofu imetanda ndani ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na wananchi kwa ujumla kutokana na kutoonekana kwa Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk. Willibrod Slaa, katika matukio mawili makubwa ya kisiasa yanayohusu mustakabali wa chama hicho.

Dk. Slaa hakuonekana siku ya kihistoria Jumanne wiki hii, iliyokuwa maalum kwa Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, kutangaza kujivua uanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kujiunga CHADEMA.

Kadhalika, Dk. Slaa hakuonekana jana makao makuu ya chama wakati Lowassa alipofika kuchukua fomu ya kuwania urais kupitia chama hicho akitarajiwa kuwakilisha Umoja wa Kutetea Katiba ya Wananchi (UKAWA), katika hafla iliyotikisa jiji la Dar es Salaam na kuhudhuriwa na viongozi wa juu wa CHADEMA.

Hata hivyo, Dk. Slaa alihudhuria kikao cha dharura cha kamati kuu ya CHADEMA Jumapili iliyopita ambacho kiliendelea hadi usiku wa manene na hoja kuu ikiwa ni kujadiliana na Lowassa na kumpokea katika chama hicho.

Dk. Slaa alionekana katika baadhi ya picha zilizovuja kutoka katika kikao hicho akiwa na viongozi waandamizi wa CHADEMA huku akijadili jambo na Lowassa, ambaye katika siku za hivi karibuni ambekuwa gumzo kubwa baada ya kubadili upepo wa siasa za Tanzania.

Tangu juzi kumekuwa na mijadala mirefu ndani ya mitandao ya kijamii, juu ya aliko Dk. Slaa, wengine wakibashiri kuwa ameamua kuacha siasa.

Hata hivyo, Dk. Slaa mwenyewe hajawa radhi ama kupokea simu yake au kujitokeza hadharani kujibu maswali ya umma juu ya kinachomsibu.

Mbali na kutokuonekana CHADEMA, Dk. Slaa pia hakuonekana kwenye mkutano wa UKAWA, uliofanyika Jumatatu wiki hii makao makuu ya Chama cha Wananchi (CUF), ambao wenyeviti wenza wa umoja huo walimkaribisha Lowassa kujiunga nao.

Wakati wa Dk. Slaa akiadimika kwenye hadhara, viongozi waandamizi wa CHADEMA kwa nyakati tofauti wameithibitishia NIPASHE kuwa kila kitu “kimedhibitiwa” kuhusu tetesi kwamba kiongozi huyo amesusa.
“Sikiliza brother, Dokta yuko freshi. Kila kitu kinakwenda kama tulivyopanga. Hakuna ukweli wa lolote juu ya madai eti Dokta anakwenda CCM,” 
kilisema chanzo chetu kilichoomba kutotajwa kwa sasa.

Wakati hali ikiwa hivyo, kuna taarifa kwamba Dk. Slaa anashinikizwa sana na watu wa ndani ya familia yake ambao wanadaiwa kusumbuliwa zaidi na ubinafsi, hasa baada ya mabadiliko ya kisiasa ambayo yamekikumba chama hicho kufuatia kujiunga kwa Lowassa.

Watu hao wa ndani wa familia ya Dk. Slaa wanadaiwa kuwa walikuwa wamejiandaa kuwa sehemu ya harakati za katibu mkuu huyo kuwania tena urais mwaka huu kama ilivyokuwa mwaka 2010.
“Sisi tunawaza jinsi ya kuivunjavunja CCM, lakini wapo watu wanawaza jinsi ya kuwa sijui nini sijui nani?
Hapa tunatafuta njia ya kuing’oa CCM hata kama ni kwa kutumia nguvu ya shetani,”
 alisema kiongozi mmoja wa CHADEMA.

Lowassa aliamua kujiunga CHADEMA baada ya kuchoshwa na siasa zilizojaa chuki za kumzuia kuingia kwenye kinyang’anyiro cha kusaka tiketi ya kuwania urais kupitia CCM.

Katika hatua nyingine, Mwanasheria wa CHADEMA, Tundu Lissu, aliliambia NIPASHE kwamba, Dk. Slaa alishiriki vikao vyote muhimu vilivyoafiki, Lowassa kujiunga na chama hicho.
“Jana (juzi) usiku nilikuwa naye na wiki hii alishirika kikao cha kamati kuu ambacho mliona picha kwenye mitandao,” 
alisema.

Alipoulizwa alipo, Dk. Slaa, Lissu hakutoa majibu ya moja kwa moja zaidi ya kusema kwamba akiwapo mwenyekiti kwenye kikao chochote inatosha na siyo lazima, viongozi wote wa kitaifa wawepo.

Kuhusu Naibu Katibu wa CHADEMA, Tanzania Bara, John Mnyika na yeye kutoonekana katika mikutano hiyo, alijibu kwa kifupi kwamba anaumwa.

Licha ya kutafutwa mara kadhaa kupitia simu yake ya mkononi juzi na jana, Dk. Slaa hakupatikana badala yake mtu mmoja mwanamke alipokea na kusema mpigaji amekosea namba.

Alipotumiwa ujumbe mfupi wa maneno ili aeleze kilichomsibu kushindwa kuhudhuria matukio muhimu ya kumkaribisha Lowassa pia hakujibu.
 • Taarifa hii imenukuliwa kutoka NIPASHE

Mahakama yafuta kesi ya IPTL, PAP dhidi ya Kafulila

Mhe Kafulila akiwaaga wananchi wa Nguruka jana baada ya kumaliza mkutano wake wa hadhara alipokwenda kuchukua fomu NCCR-Mageuzi ya kuwania Ubunge.

MAHAKAMA Kuu Kanda ya Dar es Salaam imetupilia mbali kesi namba 301 iliyofunguliwa na Kampuni ya kufua Umeme ya IPTL, PAP pamoja na Mkurugenzi wa Kampuni ya PAP Bw Harbinder Singh Sethi dhidi ya Mbunge wa Kigoma Kusini, Mhe David Kafulila.

Kesi hiyo illikuwa ikidai kuwa Kafulila alichafua jina kampuni hizo na mhusika wake kwamba walichota zaidi ya shilingi bilioni 300 kwenye akaunti ya Tegeta escrow kinyume cha sheria na taratibu.

Katika shauri hilo, Kampuni ya IPTL, PAP na Herbinder Singh Sethi walitaka Mahakama imwamuru Kafulila ailipe fidia ya sh. 310bn kwa kuchafua jina la kampuni na mkurugenzi huyo.

Katika kesi hiyo Kafulila alikuwa akitetewa na taasisi za kisheria za Legal & Human Rights Centre pamoja na kituo cha Human Rights Defenders.

Akitoa uamuzi huo mbele ya mawakili wa Human Rights Defenders na Legal & Human Rights Center wakiongozwa na wakili Mtobesya huku mawakili wa IPTL, PAP na Sethi wakiwa hawakufika mahakamani, Jaji Rosemary Teemba alisema Mahakama Kuu imejiridhisha kwamba kampuni ya IPTL, PAP na Mkurugenzi wao Harbinder Sethi hawakuwa na hoja za msingi kuthibitisha madai yao kama msingi wa kufungua kesi mahakama kuu na hivyo kwa kuzingatia hayo, Mahakama Kuu kanda ya Dar es salaam inatupilia mbali shauri hilo.

"Tuliomwita Lowasa 'fisadi' tumuombe radhi"

Ananilea Nkya (kulia) akipokea tuzo mwaka 2010 kutoka kwa aliyekuwa Balozi wa Marekani nchini Tanzania, Alfonso E. Lenhardt. (picha: tovuti ya Ubalozi wa Marekani)

Ni nukuu ya mchango uliotolewa kwenye ukumbi wa majadiliano wa Mabadiliko Forum...
Nimemsikiliza Edward Lowassa kwenye you tube tuliyowekewa humu jukwaani akiulizwa maswali na wanahabari kuhusu kashfa ya Richmond iliyotokea alipokuwa Waziri Mkuu miaka minane iliyopita. Kulingana na majibu aliyoyatoa hata mimi kama mwanahabari niliwahi kumwita fisadi kwa sababu ya kashfa hiyo. Lakini kulingana na maelezo aliyoyatoa ninakiri nilifanya dhambi maana kumsingizia mtu uongo ni dhambi na binafsi baada ya kusikia upande wake mimi kwa upande wangu namuomba radhi.

Kumbe kinara wa kashfa ya Richmond alikuwa bosi wake. Lo! Sasa inaingia akilini ni kwa nini TOR za Mwakyembe hakikumuweka Lowassa kama sample ya kuhojiwa kashfa ya Richmond ilipotokea. Lakini kwa unyenyekevu Lowassa alijiuzulu kuinusuru serikali nzima isianguke. Mungu mwema miaka minane baadaye ukweli kamili wa Richmond unajulikana. Kama ulichokisema ni kweli Lowassa, Mungu atakupigania kwa sababu ni wewe na Mzee Mwinyi peke yenu mna rekodi ya kujiuzulu kuonyesha uwajibikaji kutokana na nafasi zenu na siyo kosa mlilolitenda ninyi wenyewe. Viongozi wengine mpaka umma upige kelele sana ndipo wajibaraguze kujiuzulu mfano kashfa ya escrow 2014. Sasa ninaelewa ni kwa nini baadhi ya watu wana hofu baada ya LOwassa kukubaliwa na UKAWA kuwa mgombea Urais.

Namshukuru sana aliyetuwekea hii you-tube huku jukwaani maana baadhi yetu ambao hatuko site tungeweza kuendelea kufanya uchambuzi wetu kwa kutumia habari nusu nusu tulizopewa miaka iliyopita kuhusu kashfa ya Richmond.

Ananilea Nkya
Unaweza kufuatilia michango mingine 25+ (kutoka kwa wachangiaji 14 hadi wakati wa kuchapishwa post hii) katika mjadala huo kwa kujiunga mabadilikotanzania 

Tamko la CCM Zanzibar kuhusu yatokanayo na maamuzi ya Dodoma 2015

*audio ya maswali na majibu imepachikwa hapo chini baada ya taarifa kwa maandishi.

Katibu wa CCM Wilaya ya Mjini Ndg Mohammed Omar Nyawanga akisoma Tamko la Mikoa Mnne ya CCM Unguja kuhusuana na Mhe Edward Lowassa. kwa Waandishi wa habari na Makada wa CCM Afisi Kuu ya CCM Zanzibar leo. (picha: ZanziNews blog)

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

(PRESS RELEASE)
NDUGU WANAHABARI!
WANACHAMA NA MAKADA WENZANGU WA CCM!
ASALAM ALEYKUM!

Awali ya yote, kwa niaba ya Wanachama na Makada wenzangu tuliokusanyika hapa leo, ninapenda kuchukua fursa hii kumshukuru Molla wetu mtukufu mwingi wa rehemu kwa ukarimu wake na kutujaalia afya njema na uwezo wa kukutana nanyi hapa leo. Pili ninapenda kuwashukuru kwa dhati Wahariri na Wanahabari kutoka Vyombo mbali mbali vya Habari vya hapa Zanzibar, kwa kukubali kuitika wito wetu huu maalumu.

Sisi tuliowaita hapa ni Wanachama na Makada wa CCM. Baadhi yetu ni viongozi wa CCM wa ngazi mbali mbali za Chama, wakiwemo Wajumbe wa Halmashauri Kuu za CCM za Wilaya, Mikoa na Taifa. Kwa kuzingatia nasabu yetu hio, ndio maana mkutano huu tumeamua kuufanyia katika jengo letu hili la Afisi Kuu ya CCM Zanzibar.

Lengo kubwa la kuwaiteni hapa leo, ni kuwaelezea hisia na msimamo wetu kama wanachama na viongozi wa CCM ambao kwa kuzingatia wajibu na majukumu tuliyonayo katika Chama, sisi ndio wasimamizi wakuu wa Siasa, Sera na Itikadi ya CCM hapa Zanzibar.

Hivyo basi, kwa kuzingatia hali ya Kisiasa iliyojiri hapa nchini, tangu kumalizika kwa Mkutano Mkuu Maalumuwa CCM wa Taifa uliofanyika tarehe 12 na 13/7/2015 mjini Dodoma, na kumchagua Mhe. Dk. John Pombe Joseph Magufuli kuwa mgombea wa CCM wa Kiti cha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kumthibitisha Mhe. Samia Suluhu Hassan kuwa mgombea mwenza na uhusika wetu katika maamuzi hayo ya Chama, tumeona ipo haja na umuhimu mkubwa wa kuitisha mkutano huu na kupitia kwenu kuwaeleza wanachama wenzetu wa CCM na Watanzania kwa jumla, hisia na muono wetu juu ya mustakabali wa Chama chetu na hatima ya Taifa letu.

Kama tunavyofahamu mapema mwezi Mei 2015, Chama chetu kilitangaza ratiba ya mchakato wa uteuzi wa wagombea wa CCM katika chaguzi za Vyombo vya Dola. Ratiba hio ilihusu uteuzi wa mgombea wa kiti cha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Wabunge, Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar pamoja na Madiwani.

Mchakato wa uteuzi wa wagombea wa CCM wa Kiti cha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Rais wa Zanzibar, ulianza tarehe 3/6/2015 hadi 2/7/2015, kwa wanachama kuchukua na kuresha fomu za maombi. Baada ya hapo vikao vya uchujaji vilianza kuanzia tarehe 4/7/2015 na kumalizika tarehe 13/7/2015. Jumla ya Wanachama wa CCM 42 walijitokeza kuchukua fomu za maombi na kati yao 38 walifanikiwa kukamilisha masharti yaliyotakiwa na kurejesha. Miongoni mwao walikuwemo Makamu wa Rais, Waziri Mkuu, Mawaziri Wakuu Wastaafu, Mawaziri, Majaji Wakuu Wastaafu, Mabalozi, Mawaziri na hata wanachama wa CCM wa kawaida tu (wakulima, wafugaji n.k).

Kwa kuzingatia Katiba na Kanuni za Chama chetu, kikao cha kwanza kabisa cha uchujaji wa wagombea niKamati ya Usalama na Maadili ya ngazi husika. Hivyo, kwa wagombea wa Kiti cha Rais, Kamati ya Usalama na Maadili ya Taifa ndicho chombo cha kwanza kabisa chenye wajibu wa kuchambua kwa makini ubora wa wanachama wanaoomba Uongozi, ama viongozi wanaoteuliwa katika ngazi mbali mbali za Chama, kabla vikao vinavyohusika havijatoa idhini ya kuwaruhusu wateuliwe kugombea uongozi huo ama kushika nafasi zilizo kusudiwa.

Kikao cha pili ni Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM ya Taifa, ambayo chini ya ibara ya 119(6)(b) ya Katiba ya CCM ya mwaka 1977, Toleo la 2012, imepewa jukumu la kufikiria na kutoa mapendekezo yake kwa Halmashauri Kuu ya CCM ya Taifa juu ya majina ya wanachama wasiozidi watano wanaoomba kugombea kiti cha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Ndugu Wanahabari!

Tumelazimika kuvinukuu vifungu hivyo vya Katiba na Kanuni ya Uongozi na Maadili ya CCM, kwa sababu huo ndio msingi uliofuatwa na Chama chetu katika uteuzi wa Wagombea wa Kiti cha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kinyume na maelezo ya baadhi ya watu wasioitakia mema CCM na kwa kuzingatia maslahi yao binafsi wanataka kuwaaminisha Watanzania kwamba, mchakato huo uligubikwa na mizengwe, chuki na kila aina ya ubabaishaji, jambo ambalo sio la kweli.

Tunayasema haya sio kwa ushabiki wala kushawishiwa na mtu au kiongozi yeyote wa CCM. Bali ukweli ni kwamba sisi wenyewe tulikua sehemu ya mchakato huo na tulishiriki katika kila hatua ya utekelezaji. Na kama ni kushawishiwa basi baadhi yetu tulishawishiwa kumuunga mkono huyo ambaye leo analalamika kuwa, CCM haikumtendea haki. Sio siri, baadhi yetu tulikubali kumsaidia na kufanya kampeni kubwa ya kuwaomba wanachama wenzetu wa CCM wakubali kumdhamini katika Mikoa mbali mbali ya nchi yetu. Tulifanya hivyo tukifahamu vyema matakwa ya Katiba na Kanuni za Chama chetu kwamba, mwisho wa siku vikao halali vya Chama ndio vyenye wajibu na mamlaka ya kufanya maamuzi kwa kuzingatia Katiba na Kanuni za Chama chetu.

Hata hivyo, wengi hapa hatujashangazwa hata kidogo na kwa kweli tulitegemea kuona kile kilichotokea tarehe 28/7/2015 kwa ndugu yetu Waziri Mkuu wa zamani, Kada na Kiongozi wa muda mrefu wa CCM Edward Ngoyai Lowassa, kujitoa katika CCM na kujiunga na Chama cha upinzani cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kwa madai kwamba, CCM imeuonea na haikumtendea haki! 

Tunasema hivyo kwa sababu tulianza kupata mashaka pale tuliposikia kauli zake wakati akijibu maswali ya baadhi ya Waandishi wa habari kwamba, katika mchakato wa uteuzi wa mgombea wa CCM wa Kiti cha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ndani ya Chama, kwa upande wake hakuna kushindwa wala kikao chenye uwezo wa kukata jina lake. Kimsingi, kauli hio sio tu ni ya kukidhalilisha Chama chetu bali vile vile ni uasi! Kwani ndugu Lowassa anafahamu vyema wajibu wa mwanaCCM na mamlaka ya kila kikao ndani ya Chama. Iweje leo atamke tena hadharani kwamba, CCM ni lazima imteue yeye kuwa mgombea wake na hakuna mwanachama mwengine ye yotemwenye sifawala uwezo wa kumudu kuliongoza Taifa letu zaidi ya yeye tu peke yake!

Aidha, ni jambo la ajabu sana kuona kuwa, wale waliokua maadui zake wakubwa kisiasa,wakiwemo Viongozi Wakuu wa Vyama vya upinzani ambao walizunguka ndani na nje ya nchi kulichafua jina lake na CCM, leo hii bila haya wala soni ndio wanaosimama mbele ya Vyombo vya Habari na kupaza sauti zao eti CCM imemuonea na kumdhalilisha Lowassa! Kama hio haitoshi, wapo wale wanaodiriki kututisha, eti nyuma yake lipo kundi kubwa la wanaCCM ambao wapo tayari kumfuata popote pale aendapo.

Ili kujibu madai hayo, na kwa kupitia kwenu Waandishi wa Habari, tunapenda kutumia fursa hii kumueleza ndugu Edward Ngonyai Lowassa pamoja na wote wanaomuunga mkono hususan Viongozi na wanachama wa UKAWA, kwamba:-

a) Sisi wote tuliyopo hapa leo na maelfu ya wanaCCM waliyo nyuma yetu hususan katika Mikoa yote ya Zanzibar, tulimuunga mkono Lowassa katika azma yake ya kuomba kuteuliwa na CCM kuwa mgombea wake wa Kiti cha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, sio kwa sababu ya uzuri wa suara yake au utajiri alionao hapana! Bali ni kwa sababu ya Siasa, Sera na Ilani ya Chama alichokiamini na kukipigania, yaani CCM. Hivyo, kwa kuwa sasa ameamua kujitenga na CCM, basi nasi tumeamua kujitenga naye na kamwe hatuko pamoja naye.

b) CCM ni muumini wa Haki za Binadamu, usawa na utawala wa sheria. Hivyo, kujiondoa kwa Lowassa katika CCM ni sawa na ilivyokua wakati wa kujiunga kwake. Ni suala la hiari yake na wala hatuna ugomvi naye. Ila tunamkumbusha tu kwamba, inawezekana kabisa umaarufu alionao sasa umejengwa kutokana na CCM, lakini haiwezekani kabisa kuwa, umaarufu wa CCM umejengwa au kutokana na yeye. Ndio maana tunasema, Chama kwanza mtu baadae”.

c) CCM ni Chama chenye mamilioni ya wanachama na maelfu ya viongozi, wenye hekima, busara, mapenzi na uadilifu mkubwa kwa wananchi. Bado kinaamiwa na kukubalika miongoni mwa wananchi wengi wa Tanzania. Wingi huo wa wanachama wake haitokani na wala haujaletwa na utajiri wa Viongozi wake. Bali unatokana na uimara wa Siasa, Sera na Itikadi yake., Hivyo, hasara ya kweli kwa CCM sio kumpoteza tajiri mmoja anaetaka kubadili Sera na Itikadi ya CCM kwa maslahi yake binafsi na marafiki zake, bali ni kuwapoteza mamilioni ya wanachama wake ambao wanachoshwa na viongozi walafi na wanafiki ndani ya CCM!

d) Kwa kuzingatia ukweli huo ni wazi kwamba, uamuzi wa Lowassa kujiondoa ndani ya CCM sio jambo la kukishtua Chama chetu, viongozi wala wanachama wake. CCM kamwe haiwezi kudhoofika wala kupasuka. Aidha, hii sio mara ya kwanza kwa CCM kuondokewa na Kiongozi Mwandamizi na kujiunga upinzani. Mwaka 1989, CCM iliwafukuza uanachama jumla ya viongozi waandamizi 11 akiwemo Waziri Kiongozi Mstaafu wa Zanzibar, Seif Shariff Hamad. Akafuatia Agostino Lyatonga Mrema, ambaye alijiunga na NCCR-Mageuzi. Mwaka jana 2014, CCM ilimfukuza uanachama aliyekua Mwakilishi wa Jimbo la Kiembesamaki kwa tiketi ya CCM Mansoor Yussuf Himid. Hivyo, kama wahenga walivyonena tunamuambia Lowassa, “Kama mvuvi wa pweza tukutane mwambani” !

e) Tunawashangaa sana Viongozi wa baadhi ya Vyama vya Upinzani hasa vile vinavyounda umoja wa UKAWA na hususan Viongozi na Wanachama wa CHADEMA kwa namna wanavyoendelea kuendesha Siasa za ubabaishaji na ulaghai kwa Watanzania. Kwa hakika ni jambo la aibu na kufedhehesha sana kuona kwamba, hata baada kufikisha umri wa miaka 23, tangu kuanzishwa rasmi kwa Vyama vya Upinzani hapa nchini (1992), bado Vyama hivyo hadi leo hii vimeshindwa kuandaa wagombea wenye uwezo wa kuwaongoza Watanzania na kuishia kudaka mapumba yanayotoka CCM?Mara nyingi tumewasikia wakijitoa kimasomaso kwakukariri nusu nusu kauli ya Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius K. Nyerere kwamba, “Watanzania wanahitaji mabadiliko na wasipoyapata ndani ya CCM watayafuata nje ya CCM”. Kwa bahati mbaya sana wasia huo wa Baba wa Taifa unakaririwa nusu nusu.Naomba kuwakumbushaViongozi wa UKAWA kwamba, Wasia huo wa Baba wa Taifa kwa Watanzania unaendelea kwa kutamka kwamba “Rais wa Tanzania anaweza kutoka Chama cho chote kile, lakini Rais bora wa nchi yetu atatoka CCM!

Mwisho kabisa, ninapenda nimalizie kwa kumpongeza sana Mhe. Dk. John Pombe Joseph Magufuli kwa kuteuliwa kuwa mgombea wa CCM wa kiti cha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kuteuliwa kuwa mgombea mwenza, pamoja na wanachama wengine wote waliojitokeza kutangaza nia hatimaye kuchukua fomu za kuomba kuteuliwa kugombea nafasi ya kiti cha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa heshima kubwa waliyoipatia CCM na kubwa zaidi kwa kukubali kupokea bila kinyongo maamuzi ya Chama na kudumisha umoja na mshikamano miongoni mwa wanaCCM.

KIDUMU CHAMA CHA MAPINDUZI!

Malalamiko ya kutokuridhishwa na mwenendo wa kampeni Kibamba


Mwanamuziki wa Tanzania aadhibiwa na BASATA kwa "kudhalilisha nchi"


Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) kama msimamizi na mratibu wa sekta ya Sanaa nchini limemfungia msanii wa Muziki wa Kizazi Kipya Zuena Mohamed kwa jina la kisanii Shilole kufanya shughuli za sanaa nchini kwa muda wa mwaka mmoja kuanzia tarehe 24/07/2015 hadi tarehe 24/07/2016.

Itakumbukwa kuwa mnamo tarehe 09/05/2015 akiwa katika onyesho lake la Muziki nchini Ubelgiji alikiuka maadili ya kazi ya sanaa mbele ya hadhira ya wapenda sanaa za Tanzania na hivyo akadhalilisha utu wake na jamii ya Kitanzania kimaadili. Pia itakumbukwa kwamba mnamo mwezi Oktoba, 2013 BASATA ilimuonya na akakiri kwa kuomba msamaha kwa tabia yake ya kucheza bila kuzingatia utu na maadili awapo jukwaani.

BASATA ilimpa nafasi ya kutoa maelezo yake kwa nini asichukuliwe hatua za kinidhamu kwa kitendo chake cha kudhalilisha maadili, utu na sanaa ya Tanzania lakini akakaidi kutoa maelezo. Hivyo basi BASATA imejiridhisha kwamba alikiuka maadili ya kazi ya sanaa kwenye onesho lake la huko Ubelgiji makusudi na amekiuka Sheria, Kanuni na Taratibu za uendeshaji wa Sanaa.

Hivyo basi kutokana na ukiukwaji huo wa sheria na kanuni za uendeshaji wa shughuli za sanaa nchini, Baraza la Sanaa la Taifa chini ya Kanuni ya 30(1)(d) ya G.N 322 ya 2005 limemsimamisha kujishughulisha na kazi za Sanaa nchini kwa muda wa Mwaka Mmoja tokea tarehe 24/07/2015.

Hivyo haruhusiwi kufanya au kushiriki kwa namna yoyote ile shughuli yoyote ya onesho la sanaa nchini au nje ya nchi. Iwapo atafanya kinyume cha hayo kutapelekea kupewa adhabu zaidi ikiwa ni pamoja na yeyote yule utakaye shirikiana naye.

Ni matumaini ya Baraza la Sanaa la Taifa kwamba wasanii na waandaaji wa shughuli za sanaa wataendelea kutambua umuhimu wa kufuata sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa.

Sanaa ni kazi, tuipende na kuithamini

Godfrey Mngereza
KATIBU MTENDAJI


Taarifa ya Asubuhi Njema ya ChannelTEN 31.7.2015