CHADEMA yazungumzia habari iliyochapishwa Raia Tanzania kumhusu Dk Slaa


Ziko habari za uzushi kuhusu Katibu Mkuu Dk. Slaa, zinaandikwa na kuenezwa na Gazeti la Raia Tanzania kwa siku kadhaa mfululizo sasa.

Uongo huo wa Raia Tanzania leo umeendelea kwa kiwango cha juu zaidi kiasi cha gazeti hilo kuandika kuwa eti Katibu Mkuu Dk. Slaa amekabidhi nyaraka za chama kwa dispatch saa 3 usiku juzi.

Wakuu, hakuna uongo uliokubuhu kama huo. Mtakumbuka uongo huo wa kwamba KM Dk. Slaa anarudisha mali za chama zilienezwa usiku wa juzi mitandaoni na mmoja wa waandishi wa habari aitwae Manyerere Jackton.

Kwa bahati nzuri wakati Jackton (mtu ambaye tunaheshimiana kwa sababu ya kikazi na kitaaluma) wakati akijipatia jukumu la kuandika uzushi badala ya habari na kusambaza uongo badala ya taarifa, binafsi nilikuwepo ofisini physically. Nilikanusha kupitia Jamii Forums ambako alidanganya kwa jina lake, huku 'akijiapiza'.

Uongo huo ambao leo umeshadidiwa na Gazeti la Raia Mwema leo, ulisababisha taharuki isiyokuwa ya lazima kwa waandishi wa habari kadhaa ambao walinitafuta (si Raia Tanzania wala Jackton) na nikawaruhusu waje Ofisini wakitaka usiku huo ili waone namna ambavyo wako watu au chombo cha habari kinaweza kujivika kazi ya kusambaza uongo. Kujeruhi na kuua ukweli.

Kazi ya kujeruhi na kuua ukweli hufanywa sana na maadui wakati wa mapambano kama ilivyo sasa katika mchuano wa kisiasa unaoendelea nchini kuelekea Uchaguzi. Maadui wa CHADEMA wako kazini. Lilitarajiwa hilo.

Wakati Raia Tanzania wakikoleza uongo wao kwa kusema eti 'majira ya saa 3.15 hivi' lilifika Gari aina ya Noah maeneo ya ofisini kisha eti watu wawili wakaingia ofisini wakiwa na mkoba mwekundu, muda huo mimi nilikuwa Ofisini. Hakuna kitu cha namna hiyo kilichofanyika. Labda kama Ni Kwenye Ofisi za gazeti hilo.

Naandika haya nikiwa na uchungu. Kwa sababu huwa sijisikii vizuri kabisa kulumbana na wenzangu (senior fellas) kwenye taaluma ya habari. Tena kwenye mambo ya hovyo yanayohusu kuvunja vunja kabisa misingi ya uandishi wa habari i.e accuracy, facts, truth, objectivity etc.

Inapofikia hatua Gazeti kama hilo linashindwa kabisa kusimama kwenye kitu kiitwacho Social Responsible Journalism inatia aibu na kichefuchefu kwa jamii ya watu makini wanaotaka ushindani wa kisiasa unaoendelea nchini ufanyike kwa misingi ya kila mdau kutimiza wajibu wake inavyotakiwa. Uwajibikaji.

Nimalizie kwa kusema yafuatayo; Katibu Mkuu hajajiuzulu. Nafasi yake haiko wazi kama ambavyo gazeti limepotosha.

Agenda ya kuandika uzushi na uongo kuhusu Katibu Mkuu Dk. Slaa na CHADEMA wanayotekeleza Gazeti la Raia Tanzania walioko nyuma yake wanajulikana. Ni agenda ya CCM na Mawakala wao. Wasaliti wa mabadiliko ambao hawajaamini kuwa ndege ya mabadiliko hatimaye inaruka wakiwa wametupwa nje kwa sababu ya usaliti wao wa kufanya kazi za CCM wakiwa ndani ya CHADEMA kabla hawajatimuliwa.

Mojawapo ya malengo ni kuwachanganya wanachama, wapenzi, mashabiki na wafuasi wa CHADEMA katika kipindi hiki muhimu kinachohitaji utulivu wa mwili, akili na roho ili kupanga mikakati ya kumdhibiti adui na kuweka kila kitu sawa kwa ajili ya kusaka ushindi kwenye Uchaguzi mkuu wa mwaka huu.

Inaitwa diversion. Ili badala ya kuendelea kuwa focused kwenye masuala ya msingi eti tuanze kukimbizana na propaganda!

Aidha, baada ya CCM kusambaratikia Dodoma na sasa iko vipande vipande ikiwa ni mwendelezo wa kuanguka kwa 'himaya' hiyo huku Wananchi wakipandisha mori wa mabadiliko kupitia BVR, lengo jingine ni kutaka kuuhadaa umma wa Watanzania kuwa eti CHADEMA nayo imegawanyika. Wanaota.

Mgawanyiko wa chama cha siasa huwa unatokea kwenye vikao pale ambapo maamuzi yanashindwa kufanyika au kufukiwa. Hakujawahi kutokea jambo la namna hiyo ndani ya chama.

Kwa sababu chama kimejenga utamaduni wa kusimamia misingi katika kusimamia na kuendesha masuala yote, kinaendelea kuwa imara kadri tunavyosonga kuelekea Uchaguzi mkuu.

Uimara huu wa CHADEMA kikijiandaa (kwa kushirikiana na vyama wenza katika UKAWA) kwenda kushinda Uchaguzi, kushika dola na kuongoza serikali, ni mpango wa Mungu. Tujiandae kwa propaganda kubwa zaidi ya hizo za Raia Tanzania.

Tutashinda.

Makene

Kauli ya Mwapachu kuhusu Lowasa

JV Mwapachu
JV Mwapachu
Akiwaandikia Wanazuoni anasema...

Ndugu zangu,

Nimekuwa kimya kwa muda mrefu katika mabadilishano ya fikra kwenye mtandao huu ambao kwa hakika, kwa maoni yangu, haubidi kuwa ni wa fikra pevu zisizo shawishika na misimamo ya 'kimalaya ya siasa'. Kama tutaserereka katika msingi huu, basi ni bora Chambi ukafunga virago na kusitish huu mtandao. Nimesoma mabadilishano na mabishano ya fikra kuhusu hali ya siasa nchini mwetu na hususan baada ya Mhe Lowassa kuamua kujiunga na Chadema na kuwa mwakilishi wa UKAWA katika kinyang'ariro cha nafasi ya Urais wa Jamhuri yetu ya Muungano. Sijui nyie wenzangu mmesimama au mmesimamia wapi katika suala hili.

Naomba niseme mwanzoni kabisa kwamba nchi yetu hii leo imefikia mahali ambapo wasomo, wanazuoni kama sisi katika mtandao huu, Hatuna budi kujitokeza na kuhesabika tunamuunga nani mkono katika uchaguzi ujao wa Rais wa Tanzania. Tuwe wakweli na siyo kuendelea kuegemea katika kificho cha 'uhuru' wa wanazuoni katika kutoa maomi na fikra kama vile sisi si wapiga kura au wananchi wanaothamini umuhimu kuhusu uongozi wa nchi yetu. Wakati huo umepitwa na hali halisi ya itikadi na maana muhimu ya uongozi wa Taifa.

Sasa, Mimi binafsi, namuuunga mkono Edward Ngoyai Lowassa. Yako mengi ambayo kazuliwa huyu ndugu yetu; tunaambiwa tangu 1995 wakati Mwalimi Juluis Nyerere alipo tamka kwamba 'huyu kijana ninalo file lake; ana utajiri usiyoelezeka. Ana nyumba kadhaa.' Lakini huyo huyo Baba wa Taifa alimpenda sana Edward na kumpa madaraka ndani ya CCM na baraza la mawaziri. Kama Edward alikwa 'corrupt' swali ni kwaninini Baba wa Taifa hakumchukulia hatua za kisiasa na kisheria? Kwanini aseme hayo aliyoyasema mwaka 1995 wakati Edward Lowassa alikuwa akiongoza kupendwa dani ya CCM, ngazi zote na akitarajiwa ndiye angependekezwa kuw mgombea wa Urais? Jamani, wanazuoni, lazima mtafakari historia na hali halisi ilivyokuwa. Mhe Jakaya Kikwete hakuwa 'the favourite' candidate in 1995. Na Mwalimu alimtaka Ben Mkapa wakati ule awe Rais. Ilibidi Lowassa atoswe ki namna!

Mimi namfahamu Edward. Ninyi mnaujua huo utajiri wake au basi akitoa michango hapa na pale ni pesa zake? Kati yenu mna utajiri zaidi ya Edward. Edward alivumilia na kumsaidia mwenzake (nasita sasa hivi kutumia neno 'rafiki') Jakaya ashinde uteuzi wa mgombea wa CCM hapo 2005. Aliamua hivyo baada ya makubaliano ya 1995. Wapo wengi wa Tanzania waliyojitolea muhanda, wa hali na mali kuungana na Edward kumwezesha Jakaya Kikwete kuwa Rais 2005. Kati yao, ndiyo wamekuwa karibu na Edward katika kinyang'anyiro cha majuzi Dodoma. Imani yao ilikuwa kwamba pamoja na mkanganyiko wa Februari 2008 wa Richmond ambao hauna mashiko yoyote ya ufisadi kwa maana ya rushwa, Rais Kikwete angemfungulia mlango mwenzake Edward kuwa mgombea wa CCM. Badala yake Edward bado akajengewa mzengwe wa utajiri kama Baba wa Taifa alivyofanya 1995. Hivi leo tukichambua nani kati yetu ni tajiri zaidi ya Lowassa tutakuwa na viongozi wanao kidhi mategemeo yetu?

Kuhusu hili swala la Richmond: Hivi baada ya taarifa ya Tume ya Bunge ya Dr Mwakyembe, Serikali litoa majibu. Mbona kwenye tuhum aza Bunge kuhusu Tegeta Escrow imekuwapo taarifa toka kwa Chief Secretary kuhusu suala hilo? Nani aliyejaribu kutoa maelezo ambayo yangemfungisha Lowassa au kumkomboa kwa kitendo chahe cha kujiuzuru kisiasa? Badala yake, wanazuoni wenzangu ambao sidhani kama tunazo facts za kutosha tuanaendelea kumshutumu Lowassa na kuwmona kama vile ni corrupt na kiongozi asiyefaa. It is not fair.

Mimi simlaumu Lowassa kujitoa CCM. Ni haki yake na kajieleza vipasavyo kuhusu maamuzi yake. Je, ni uamuzi wa uroho kuhusu U-Rais? Jamani, wanazuoni, hivi kweli tumefia hatua ya kumwona mtu ana uroho wa Urais? Ili awe au afanye nini ambacho sisi tufunge macho, na siyo tu kutoona, bali pia kuto chukua hatua? Ikifikia hapo, basi hatuna Taifa tena!!

Taifa letu limebahatika kufika hapa lilipofika mwaka huu. Wengi hatukutarajia kwamba yale ambayo tumekuwa tukitafakari na hata kusalia ghafla yameibuka. Sidhani na siamini kwamba ramani ya siasa ya Jamhuri yetu itabaki ilivyo ifikapo Desemba 2015. Ni ishara ya kheri na mwelekeo mwafaka kwa demokrasia ya Taifa letu.Naamini kwa dhati kabisa kwamba Edward Lowassa atakuwa kiongozi ambaye atasaidia ramani hii kuwa na muono mpya.

JV Mwapachu.

---
Unaweza kuendelea kufuatilia mjadala huu Wanazuoni

Ananilea aeleza kwa nini, "Ninamuunga mkono Lowassa kugombea Urais"

Ananilea Nkya
Ananilea Nkya

Mimi Ananilea Nkya tatizo langu kubwa kwa Lowassa lilikuwa ni ufisadi wa Richmond uliotafuna zaidi ya shilingi bilion 172 za wananchi. Baada ya kusikia kauli yake alipohojiwa na wanahabari siku alipojiunga na CHADEMA, na baada ya kujiridhisha kuwa kama alikuwa amehusika na ufisadi wa Richmond leo angelikuwa jela kama Yona na Mramba, namuunga mkono kugombea Urais. Naamini hata Dr Slaa amemkubali Lowassa kuwa mgombea Urais wa vyama vinanyounda UKAWA baada ya kujiridhisha kuwa mamlaka ya juu ilimbebesha Lowassa kashfa ya Richmond ili kunusuru serikali nzima kuanguka.

Lakini zaidi nimeongeza imani yangu kwa Lowassa baada ya kubaini kuwa hata Baba wa Taifa Julius Kambarage Nyerere alimuona kama kijana makini mwenye maono na dhamira safi ya kuwatumikia Watanzania. Mwaka 1995 wakati Rais mstaafu Ali Hassan Mwinyi anamaliza muda wake Nyerere mwandishi wa habari Mwita Matinyi alimuliza Mwalimu Nyerere alikuwa anafikiri ni nani angeweza kumrithi Mwinyi kuiongoza Tanzania. Mwalimu alijibu Matinyi hivi. Nanukuu:
Ni kweli Mzee Mwinyi anaondoka lakini ndani ya CCM kuna viongozi wengi wenye sifa za kuwaongoza Watanzania, kikubwa tu awe na dhamira kwa mfano wapo wakina Warioba, Mzee Msuya na Mark Bomani na wapo vijana hodari na wenye upeo mkubwa sana kama Mkapa, Kikwete na Lowassa ni jambo la heri sana CCM kuwa na watu kama hawa (Majira 26/5/1995) ukurasa wa 3; na Nipashe 26/5/95 ukurasa wa 3).
Pia nikiwa ripota Radio Tanzania Dar es Salaam niliwahi kufanya kazi na Lowassa katika miaka ya 90. Nilivyouona utendaji wake wa kazi zama hizo nashawishika kwamba anafaa kuwa kiongozi wa nchi yetu. Nilishuhudia akijituma kweli kweli kwenye kazi za umma zama hizo.

Kadhalika namuunga mkono Lowassa kwa sababu hagombei Urais kupitia chama cha CCM ambacho kinakumbatia mfumo wa kuwadhawau na kuwafukarisha wananchi huku watawala wachache wakineemeka kwa kutumia rasilimali za nchi kama vile nchi hii ni mali ya watawala, familia zao na marafiki za. Ninaamini kwa kugombea Urais kupitia UKAWA, CCM itapunguziwa dharau na jeuri yake dhidi ya wananchi ambao ndio wenye mamlaka ya mwisho kuhusu hatma ya nchi yetu. Mfano CCM mwaka jana 2014 ilionyesha dharau kubwa sana kwa wananchi kwa kuizika Rasimu ya Katiba iliyotengenezwa kwa kutumia maoni ya wananchi wakati fedha zaidi ya bilioni 130 zilitumika. Kwa kutumia mabilioni hayo bila Katiba Mpya kupatikana ni kufisadi mali za wananchi mchana kweupe. Haikubaliki.

Vile vile namuunga mkono Lowassa kwa kwa sababu anaukataa hadharani umaskini wa kuchongwa ambao watawala wanautumia kwa faida yao ili waendelee kuwanunua wananchi mafukara wakati wa uchaguzi na wakishapata madaraka waendelee kujineemesha na mali za nchi.

Nchi yetu siyo maskini bali watawala wanaendekeza matakwa ya wawekezaji (wakoloni wa zama hizi za utandawazi wizi) ambao wanaliibia taifa rasilimali nyingi na na hatimaye nchi za wawekezaji hao (donors)wanawapoza watawala kwa vijimisaadaa uchwara. Ni aibu sana kwa kiongozi wa Tanzania kijipitisha nchi moja hadi nyingine Marekani, Ulaya, China, India na Ausralia n.k kutembeza bakuli (omba omba kama matonya vile) huku nchi yetu ikiwa na rasilimali tele. Tena wakati watawala wanakwenda kuomba eti wanapanda ndege daraja la kwanza. Huu ni wenda wazimu. Ni kuiaibisha Tanzania na Afrika.

Sina chama cha siasa ninachofungamana nacho kwa sasa, lakini namuunga mkono Lowassa kugombea Urais kupitia UKAWA kwa sababu naamini akiwa Rais wa nchi yetu upuuzi huu wa kuendekeza umaskini kwa kuomba omba nchi za nje huku tukitoa mali za nchi honyo hovyo kwa wageni na kuamini kuwa maendeleo ya nchi yetu yataletwa kwa misaada kutoka nje, kutakomeshwa. Naamini hata hao wakoloni wa zama hizi za utandawazi wizi wanajua Lowassa hatachekacheka nao.

Lakini zaidi namuunga mkono Lowassa kwa sababu Watanzania wakiridhia kwenye sanduku huru la kura hapo Oktoba awe Rais wa Tanzania, vyama vinavyounda UKAWA vitasimamia kuhakikisha kuwa mamlaka ya wanannchi hayaporwi hivyo hovyo tena. Kwa hiyo Rasimu ya Katiba ya wananchi itaheshimiwa na nchi yetu itapata Katiba Mpya inayotokana na maoni ya wananchi. Kwa kufanya hivyo taifa hili litaanza kupiga hatua kubwa ya kuondoa ufukarishwaji wa wananchi walio wengi unaofanya na watawala wa CCM kwa kushirikiana na wakoloni wa zama hizi za utandawazi wizi.

Naridhia andiko langu hili lichapishwe na yeyote anayetaka.

Ananilea Nkya

----

Maoni ya Dk Lwaitama kuhusu UKAWA

Azaveli Lwaitama
Azaveli Lwaitama

Ndugu Wanabidii,

Historia inaonesha kuwa vipindi fulani katika mstakhabali wa nchi unalazimisha kupima nini ni janga zaidi ya jingine. Marehemu Samora Machel na Frelimo walikubali kutia saini Mkataba wa Nkomati wa ushirikiano na Makaburu kama mkakati wa kujinusuru na kutoa nafasi kukabiri janga kubwa kuliko zote wakati huo la kuondolewa serikali ya Frelimo na Renamo ikisaidiwa na Makaburu. Wakomunisti wa Afrika ya Kusini waliingia ubia na ANC ya mabweneyenye weusi ili kutokomeza kwanza ukaburu na mapambano na ubepari yaje baadaye. Katika Vita Kuu ya Dunia ya Pili wakomunisti walishirikiana na mabwenyenye wa mrengo wa kulia na kati kutokomeza janga kubwa zaidi wakati huo la ufashisti, yaani ubepari wa mrengo wa wa kulia kupitiliza. Hivyo hivyo mapambano ya kuleta uhuru wa Tanganyika yalivyo unganisha nguvu za mabwenyenye wazungu na waasia pamoja na zile za wakulima na wafanyakazi wa rangi zote kwa azimio lile la mkutano wa mkuu wa Tanu wa 1958 pale Tabora. Hivyo hivyo Mandela na ANC waliingia "urafiki wa mashaka" na De Clerk kiongozi wamakaburu ili kuondolewa ukaburu kuwe kwa amani ya "kula matapishi" ya kuwalaani huko nyuma kuwa ni wabaya wa Mwaafrika!!

Mabadiriko ya haraka haraka yanayoendelea hapa Tanzania yenye lengo la kuondoa CCM madarakani kama chama dola kinachodumaza na kudhoofisha ushindani wa kisiasa miongoni mwa mabwenyenye watabaka tawala Tanzania ni mbadiliko yatayoleta neema kwa Watanzania wote. Ile tu CCM kudhoofishwa na kujiunga UKAWA kwa Lowasa ni kuvuja kwa pakacha ambayo ni nafuu ya mchukuzi.....Nikuondoa kizingiti kikuu cha kushamiri kwa demokrasia pana na maendeleo endelevu Tanzania ambacho ni kuhodhiwa na ukiritimba wa chama dola cha CCM kinachojinadi kama chama cha mrengo wa kushoto wakati ni chama cha mrengo wa kulia kama vyama vyote vya siasa Tanzania kwa sasa.

Kumeguka kwa CCM-Mambo Leo kama taasisi ya kakundi kawana mtandao ulioingiza serikali ya sasa ya Tanzania madarakani mwaka 2005 ni faraja kwa wote wenye kuitakia mema nchi hii na ni kiashiria cha kukomaa kwa vuguvugu la ukombozi wa pili wa Tanzania utakao chukua sura ya demokrasia zaidi ilikuwa na na maendeleo endelevu zaidi yapatikane kupitia kupatikana nafasi chanya zaidi ya kupitishwa kwa Katiba Mpya kama ilivyopendekezwa ndani ya Rasimu ya Pili ya Tume ya Rais iliyoongozwa na Jaji Warioba. Kwa mara ya kwanza vyama vy siasa vya upinzani kiuhalisia ( tofauti na vile ambavyo vimebebwa na watawala wa sasa kwa lengo la kuua upinzani wa kisiasa kijanja kijanja kama ACT- Wazalendo) sasa vimeunganishwa na kupigania Katiba Mpya iliyotokana na maoni ya wananchi yaliyokusanywa na Tume ya Jaji Warioba ( UKAWA) badala ya kuunganishwa na kutaka kuondoa CCM madarakani pekee.

Ghafla mwanasiasa mwenye nguvu nyingi ndani ya chama cha kifisadi cha CCM, mwanasiasa ambaye umaaarufu wake umetokana na kuongoza mtandao uliouweka utawala wa sasa wa CCM madarakani, Ndugu Edward Lowasa, amekasirishwa na kukatwa jina lake na aliodhani ni rafiki zake ndani ya CCM na kuamua kusema basi na lolote liwe kwa kujiunga na vuguvugu la kupigania katiba mpya!! Naye sasa kang'amua kuwa Katiba ya sasa na ile Pendekezwa ni za ovyo maana haziruhusu kuwepo mgombea huru bila mizengwe. Hasira za Lowasa zimezaa tunda zuri la kug'amua kuwa Watanzania wanaitaji mabadailiko kupitia Katiba Mpya iliyobebwa ndani ya Rasimu ya Pili ya Tume ya Rais iliyoongozwa na Jaji Warioba. Hasira hizi za mkizi ni furaha ya kunguru na ni busara kwa viongozi wa Chadema na UKAWA kwa ujumla kutoongopa "kula matapishi yao" kwa kumkaribisha Ndugu Lowasa ...huyu huyu waliomwita fisadi... kujiunga na UKAWA na kugombea urais. Nafasi ya kihistoria imejitokeza ya kukiondoa CCM madarakani kwa amani!!

Sishangai wasaliti wa vuguvugu la kukiondoa CCM madarakani wanatushauri sisi Watanzania wenye shauku ya kuutumia upenyo huu wa mpasuko ndani ya CCM kukiondoa CCM madaraka!!!Eti tuombe radi kwa" kula matapishi yetu" wote tulio wahi kumwita Lowasa fisadi! Wao wanataka tuendelee kuvumilia kutawaliwa na CCM labda kwa miaka mitano au zaidi hivi mpaka chama kipya cha watakatifu kiitwacho ACT-Wazalendo kitakapo kuwa tayari kututawala badala ya CCM!! Sishangai kusikia ushauri huu kutoka kwa wasaliti hawa ambao kazi yao hata huko nyuma imekuwa nikuudhoofisha upinzani dhidi ya CCM na kukisaidia CCM kiendeleee kuwa madarakani!! Hawa jamaa ni wasomi sana na ni wajanja sana, ilo lazima kulikiri!!!

Sitashanga kama haya ninayoyasema yatapigwa madogo na wasaliti hawa!! Historia itakapoandikwa baada ya UKAWA kupata viti vingi zaidi Bunge lijalo au hata kuuchua urais na kupata Katiba Mpya iliyobebwa ndani ya Rasimu ya Pili ya Tume ya Rais iliyoongozwa na Jaji Warioba itawapa hukumu yao stahiki, wajanja na welevu hawa! Bila shaka wanaoomba UKAWA ishindwe kupata viti vingi Bunge lijalo na iukose urais na hivyo tuendelee kutawaliwa na CCM na wao wapate viti vya kutosha kuwa viongozi wakuu wa eti upinzani muruwa wenye maadili ya Azimio la Arusha Tanzania!! Ni haki yao ya binadamu kuendelea na matumaini haya kama na sisi tulivyo na haki ya kuendelea na matumani yetu ya uwezakano wa ushindi mnono chini ya UKAWA dhidi ya ukiritimba wa chama kimoja chama dola cha CCM!

Mwl. Lwaitama

---

Kauli ya Zitto kuhusu Mnyika "kuhamia ACT-Wazalendo"


KUMEKUWA na tetesi kwenye mitandao ya kijamii kuwa Mbunge wa Jimbo la Ubungo na Naibu Katibu Mkuu (CHADEMA), Bara, John Mnyika, amekihama chama chake na kwenda chama cha ACT-Wazalendo.

Akizungumza issue hiyo hapa mkoani Kigoma, Kiongozi Mkuu wa ACT-Wazalendo amesema hajui chochote kuhusu hilo.

Hata hivyo Zitto amesema kuwa ACT hawawezi kukataa mwanachama na kwamba yeye hana chuki na Mnyika bali zilitokea tofauti za kisiasa baina yao na kuongeza kuwa Mnyika alikuwa anatumiwa na hata yeye mwenyewe alikuwa anajua kuwa anafanya kitu ambacho sio sahihi.

Kauli hiyo ya Zitto huenda ikaendeleza mjadala juu ya Mnyika kuhamia ACT na haitashangaza kama itatokea kutokana na mazingira ya kisiasa yalivyo kwa sasa nchini.

Lowasa arejesha fomu CHADEMA

Naibu Katibu Mkuu Zanzibar Mh Salum Mwalim akimkaribisha Edward Lowassa katika ofisi ya Makamu Mwenyekiti Bara Prof Abdallah Safari.

Chilongola: Ukweli kuhusu Dk Slaa (?)

Ujumbe huu nimeupokea kupitia kundi moja la WhatsApp, na nimeubandika hapa "as is"...

Ukweli kuhusu Dr.Slaa

AN Chilongola (LLM)

Taharuki imetanda juu ya wapi alipo Katibu mkuu wa Chadema Dr.Wilbroad Slaa. kila mtu anazungumza lake kwa kadri anavyoelewa. wengine wakisema yupo kwenye maandalizi ya vikao vya kamati kuu na wengine wakisema amejificha kwa sababu hakubaliani na maamuzi ya kumleta EL kwenye chama.

Mimi kama kada wa chadema wa muda mrefu na mwanasheria mzoefu nimefanya utafiti na nimejiridhisha bila shaka yoyote kuwa hali si shwari ndani ya chadema licha ya juhudi mbalimbali zinazofanywa kuonesha kuwa hakuna tatizo.

Ukweli ni upi? Ukweli ni kuwa Dr.Wilbroad Slaa hakubaliani na maamuzi yaliyofanywa na kamati kuu ya Kumleta EL na kumpa nafasi ya kugombea Urais bila kufanya utafiti wa kutosha. Slaa anadai kuwa maamuzi haya ni ya haraka mno na chama kilitakiwa kijitafakari zaidi kabla ya kumpa ridhaa ya kugombea Urais.

Ikumbukwe siku ya jumapili tar.26 wakati UKAWA wamefanya kikao cha mwisho na EL Dr.Slaa alikuwepo na baada ya hapo akapotea kabisa na hajaonekana hadharani hadi leo.

Ukweli ni kwamba ndani ya kikao kile chs jumapili Slaa alionesha msimamo wake juu ya EL na kudai kuwa watanzania hawatatuelewa wakituona tukipita kumsafisha mtu yuleyule tuliyemchafua awali.

Hivyo Slaa akatoa masharti mawili makubwa. La kwanza ni EL aitishe Press na ajisafishe mwenyewe kabla hajatangaza kuja UKAWA. Aruhusu waandishi wamuulize maswali yote kuhusu Richmond na kashfa nyingine ikiwemo umiliki wa jengo la Ubalozi wa S.Africa na EL ajibu hoja zote kwa maelezo ya kueleweka. Sharti la pili la Slaa ni kuwa EL asupewe nafasi ya kugombea urais kwa sasa kwani ni ngumu kupima dhamir yake kama ni ya kweli. Slaa akapendekeza EL aje CHADEMA na aisaidie UKAWA kuchukua dola bila kugombea Urais.

Lakini Mbowe akampinga sana Slaa na akasema Katibu mkuu hawezi kuweka "ultimutum" ya EL kujiunga na chadema. Mbowe akapuuza mawazo ya Slaa na akaagiza mchakato wa kumpokea uanze mara moja na kesho yake Mbatia akaambiwa atoe tamko la kumkaribisha EL UKAWA.

Hali hii ilimfanya Slaa kujihisi mnyonge na aliyepuuzwa. akahisi hathaminiki ndani ya chama licha ya mchango mkubwa alioutoa kukijenga chadema. jambo la ajabu Mbowe alipopelekewa taarifa hizo alijibu kwa kejeli kuwa liwalo na liwe. yani yuko tayari kumpoteza Slaa na kumkumbatia EL.

Haikujulikana wazi Mbowe ana maslahi gani katika hili la EL na kwanini aamue kuwa na msimamo mkali hivyo wa kumtetea EL.

Inadaiwa tangu jumapili Slaa alipoachana na viongozi wenzie wa UKAWA hadi sasa yupo ndani hajatoka na hakuna mgeni anayeruhusiwa kumuona. Anautumia muda huu kusali na kushauriana na marafiki zake kwa njia ya simu (wengi ni maaskofu) juu ya nini afanye katika kipindi hiki.

Wengi wamemshauri aachane na siasa na ajiuzulu nafasi yake ya SG ndani ya chadema wazo ambalo limeungwa mkono na mkewe Josephine na baadhi ya watu wenye misimamo mikali.

Baada ya ushauri huu mkewe wa Slaa ameonekana kufurahia na ameanza kuelezea kwenye mitandao ya kijamii. Jsna kupitia kundi la Nyakahoja la whatsapp Josephine alisema mumewe ameteseka sana na chama hiki na amekitoa mbali sana. Dr.Slaa alivunjika mkono na hadi sasa ana ulemavu wa kudumu kwa sababu ya kuitetea chadema. yeye mwenyewe alipigwa na kuharibiwa mimba mwaka 2011 kwa sababu ya chadema halafu leo wanapuuzwa kama vile si chochote ndani ya chama.

Anasema ni afadhali Mbowe angesikiliza ushauri wa Slaa wa EL kujisafisha kwanza kabla hajaja chadema maana kuja bila kujisafisha ni kuwaweka viongozi wote wa chadema kwenye mtego.

Madai ya Mbowe kupewa fedha na EL. Yapo madai kuwa Mbowe amehongwa sh. bil 12 ili kumpokea EL. Fedha hizi ameziweka kwenye akaunti yake binafsi na amewawia kidogo wale aliowaona wanaweza kumchallenge. baadhi ya watu waliopata mgao ni wajumbe wa kamati kuu ili kuwaziba mdomo. na si wajumbe wote bali wale wachache viherehere. baadhi yao ni Godbless Lema (anadaiwa kupokea milioni 120), Peter Msigwa (mil 135), Tundu Lissu (mil 180), Salum Mwalimu (Mil 180).

Pesa hizi ndizo zinazodaiwa kuwafumba macho kamati kuu na kuamua kumpitisha EL bila kufikiri mara mbili. Kitu cha ajabu kamati kuu imefunga dirisha la kuchukua fomu na kusema eti kamati kuu inamuunga mkono Lowassa tu.

Huu ni ujinga ambao hata CCM haiwezi kuufanya. Kamati kuu inatakiwa kuwa neutral. kamati kuu haitakiwi kuwa na mgombea. kamati kuu haitakiwi kuzuia watu kuchuku fomu. acha wachukue wengi kadri iwezekanavyo halafu wachujwe abaki mmoja.

Kama EL anajiamini yeye ni bora zaidi na ana nguvu zaidi kwanini anaitumia kamati kuu kuzuia watu wasichukue fomu? Siku chache zilizopita watu walilalamikia kamati kuu ya CCM kuwa ilikua na mgombea wake mbona hawaoni hili la kamati kuu ya chadema?

Ikiwa madai haya ya kuhongwa kamati kuu ni ya kweli basi chadema inaelekea ukingoni katika siasa za nchi hii. jambo la ajabu viongozi wanaodaiwa kuhongwa akiwemo Mbowe hawajakanusha habari hizi. halafu wanatuma ujumbe kw Slaa eti wakamsihi asiondoke. wajumbe wote waliotumwa wakaishia getini na hawakufunguliwa mlango. mlitegemea mfunguliwe mlango wakati kuna madai mmehongwa na hamjakanusha? kanusheni kwanza ndio muende kumuona Slaa. Au mnataka mkamhonge na yeye? Kama msipokanusha habari hizo mkienda mtafungiwa tena nje maana nyumbani kwa Slaa hakitaingia chochote kilicho kichafu.

Response ya Chadema. ni kama vile hawajali yanayoendelea. na bahati mbaya zaidi vijana wa chadema wameanzisha movement ya kumtukana Josephine kuwa yeye ndio anamponza mumewe. kwenye mtandao wa jamiiforums, facebook ma magroup ya whatsapp wanamtukana sana.

kwenye group moja la wabunge wa chadema wameanzisha movement iitwayo "Josephine Bring Back our Dr". wengine wanamwita mwanamke mpumbavu, wengine wanasema ana hasira ya kukosa ufirst lady, lakini wengine wamefika mbali na kudai anatumiwa na TISS na CCM.

Kimsingi madai yote hapo juu hayana mashiko. Josephine hatumiwi na TISS wala CCM. Hana uchungu wa kukosa ufirst lady wala nini. anachofanya ni kutetea haki ya mumewe. haki ya kuthaminiwa, haki ya kuheshimiwa, haki ya kutoa mawazo yake na kusikilizwa.

Hivi mumeo anapuuzwa kwenye vikao vikubwa vya maamuzi halafu unaambiwa waliompuuza wamehongwa fedha na hawajakanusha habari hizo, halafu ukimtetea mumeo unaambiwa unatumika na TISS. this is ridiculous.

Hakuna cha TISS wala CCM mchawi wa chadema ni chadema wenyewe na mchawi wa ukawa ni chadema. Hizi porojo za TISS ni mbinu inayotumika ili Slaa akiamua kutangaza msimamo wake ionekane anatumiwa na CCM. Chadema acheni siasa za kitoto. hivi Slaa aliyepigania chadema zaidi ya miaka 20 akitoa sadaka maisha yake kwenu ndio wa kutumika na TISS leo aache kutumika huyo EL aliyekuja jana? this is very interesting. chadema kitaingia katika rekodi za dunia za kuwa chama cha kwanza kumtilia shaka mwanachama wake wa miaka 20 na kumuamini mwanachama wa siku moja.

Nini kifanyike? Jambo linaloweza kufanyika na kusaidia kuiokoa chadema na UKAWA kwa ujumla ni mediation. zitafutwe mbinu nzuri za kukutana na Slaa na kuongea nae. aeleze yanayomhusu na chama kioneshe concern ya kuyatatua.

pia kwa kuwa Josephine anaonekana kuwa na nguvu kubwa sana kwa Slaa hivi sasa ni bora Watafutwe wanawake wenye heshima ndani ya chama wakaongee nae. kwa mfano Mama Regina Lowassa, mama Ntagazwa na mama Mbatia waende kumuona mwanamke mwenzao waongee nae. hii itasaidia kupunguza hasira za huyu mama maana tangu juzi anatukanwa mitandaoni akidaiwa ndiye anayemzuia Slaa.

Ni vizuri mambo haya yafanyike mapema maana taarifa zilizopo ni kuwa kufikia wiki ijayo kama chama kitakua hakijatoa msimamo kuhusu Slaa basi yeye atatangaza msimamo wake wa kujiuzulu wadhifa wake chadema na kuamua kuachana na siasa kabisa. kisa wataondoka nchini yeye na familia yake kwenda Italia ambapo ataishi huko kwa miaka mitano kabla ya kurudi nchini na kumalizia maisha yake Karatu. mipango ya Slaa kwenda kuishi Italia kwa miaka mitano inaratibiwa na shirika mija la kiroho la kanisa katoliki na maandalizi yanaendelea vizuri.

Hivyo basi ni vema kazi hii ikafanywa mapema na kwa umakini ili tusivuruge kazi yote ya kuijenga Ukawa na kuujenga upinzani nchini. ukweli ni kuwa Slaa akiamua kujiuzulu siasa za upinzani zitapoteza uelekeo na tutashindwa vibaya kwenye uchaguzi mkuu kuanzia udiwani, ubunge hata urais. maana yake ni kuwa kazi yote iliyofanyika kuujenga upinzani inabomolewa siku moja na kuifanya CCM izidi kushamiri. na ikiwa Slaa ataondoka itachukua miska zaidi ya 100 kupata upinzani mwingine wenye nguvu kama huu. hivyo basi juhudi za haraka zinatakiwa.

Mwandishi wa makala haya ni ndugu A.N Chilongola, mwanachama wa chadema na mkurugenzi wa kampuni ya uwakili ya Chilongola &Advocates iliyopo Mabibo Dar. [email protected]

Kauli iliyoandikwa na "Dr Slaa"

screen-shot ya nukuu ya ujumbe wa Dr.W.Slaa
Yericko,

Siasa ya unafiki sipendi. Nimenyamaza lakini naona mnazidi kunichokoza. Ni afadhali mngelikaa kimya kama nilivyonyamaza mimi. Uwongo wowote na upotoshwaji wowote sitauvumilia. Nitaukanusha hapo hapo. Hata kama una lengo lako ambalo silifahamu naomba sana usitumie jina langu. Nimefundishwa uwongo ni dhambi siko tayari kushiriki dhambi hiyo.
sina kikao chochote cha Secretariat sina mpango wowote ninaopanga kuwasilisha popote. Naomba watanzania wapuuze propaganda zote zinazofanyika kwa jina langu.
Ningehitaji kutuma taarifa yoyote kwa umma ningeliita Press Conference Mwenyewe au ningelitumia utaratibu wowote uliouliozoeleka.

Naomba kutoa onyo kwa mtu yeyote awaye, matumizi ya jina la Dr Slaa yakome.
Hiyo ni nukuu ya aliyeandika kwa kutumia akaunti iliyohakikiwa kwa jina la Dk Slaa akijibu ujumbe wa Yericko Nyerere alioandika.
Jioni ya leo Dr. Slaa katibu mkuu wa CHADEMA atawasilisha mpango mkakati wa ushindi mbele ya sekretariet tayari kuelekea cc kesho.
Hatua hiyo inafuatia jopo la wataalamu nane likiongozwa na Dr Slaa kujichimbia kwa wiki nzima kuhariri na kuchakata taarifa mbalimbali za umoja wa vikosi kazi vya vyama vinavyounda UKAWA,
Japo maneno na uzushi mwingi umezagaa mitaani lakini Dr hayumbishwi na hilo, mida ya usiku wa leo atawasilisha ripoti hiyo katika vikao vinavyofanyika kwa siri kubwa ili kuepuka maadui ambao kwasasa tunapigana vita nao usiku na mchana.
Kesho ndio rasmi Dr. Slaa atawasilisha mbele ya cc mipango mkakati hiyo ikiwemo Ilani nk.
Pipoooooooz!!!!
Kauli hizi zimenukuliwa kutoka ukumbi wa majadiliano wa JamiiForums

Nyumbani na Diaspora: Susan Mzee, Kiangio Sekazi, Jessica Che-Mponda


Mangala Band waibuka na muziki wa Kihehe katika ladha ya kisasa

Mangala Band -Tanzania chini ya mwimbaji kiongozi Riziki Msola katika muziki wa asili wenye mahadhi ya ghani ya Kihehe wanaendelea na mikikimikiki ya mwisho kwa ajili kukamilisha video baada ya album kupata mapokezi mazuri.

Hizi ni habari njema kwa wadau wa muziki wa asili nchini Tanzania bila kujali uasilia wao kwa kuwa muziki unaweza kumgusa mtu yeyote.

Kwa wakati huu unakaribishwa kupakua muziki huu mtandaoni au kuagiza cd yako na itakufikia hapo ulipo.

Vyereje leo! Kwani hawakumjua Lowassa?


Khelef Naasor
Khelef Naasor
“Sitapiki nikameza” ni msemo mashuhuri sana katika jamii zetu, ambao mtu huutumia akimaanisha kuwa kamwe hatorudia jambo au kitu ambacho ameshaachana nacho. Kwa bahati mbaya sana, msemo huu ni tofauti na mtazamo wa Chama cha Mapinduzi (CCM) kwani wao sio tu hujitapikia, bali pia hujipaka matapishi hayo kabla hawajaanza tena kuyameza. Uchafu ulioje!

Tukumbushane kidogo. Mnamo tarehe 7 Juni 2015, Waziri Mkuu wa zamani Edward Lowassa aliwasili Zanzibar kwa ajili ya kutafuta watu watakaomdhamini katika harakati zake za kuwania uraisi kwa tiketi ya CCM. Lowassa aliwasili milango ya saa 1:30 usiku katika uwanja wa ndege wa Abeid Amani Karume na kulakiwa na mwenyeji wake ambaye ni mwenyekiti wa CCM mkoa wa Mjini Unguja, Borafya Silima.

Borafya akamtembeza Lowassa na kumtambulisha kwa makada mbalimbali wa CCM ndani ya mkoa huo. Katika kutafuta wadhamini, Borafya alimnadi Lowassa kuwa ni mtu safi asiye na hata chembe ya ubaya. Alimuogesha maji ya utakatifu na kumpaka mafuta ya unabii. Vifijo na nderemo kutoka kwa makada hao vilirindima kila sehemu aliyopita Lowassa kusaka wadhamini. Na hiyo ikawa ni kote Unguja na Pemba alikokwenda kusaka wadhamini, kama ilivyokuwa pia kote Tanzania Bara, chini ya kaulimbiu ya “Safari za Matumaini”.

Kwa mara nyengine, akawa ni Borafya aliyethibitisha kuwa Lowassa alikuwa ni mtu safi na aliyeandaliwa kwa muda mrefu na chama chao. Aliongeza kuwa walikuwa wanamuunga mkono mia-fil-mia na zaidi ya yote yeye binafsi alisema kuwa ana mahaba naye. Hapa sijui ni mahaba ya aina gani aliyonayo mzee huyu kwa Lowassa. Jibu analo mwenyewe, lakini waliokuwa wanafuatilia harakati za akina Borafya wakati wa “Safari ya Matumaini” ya Lowassa, wanataja namna safari hiyo ilivyomimina mapesa mifukoni mwao, wengine wakafikia umbali wa kununua magari na viwanja vya kujenga majumba. Yalikuwa maslahi binafsi, kwa hakika.Mambo yakaenda kama yalivyoenda na hatimaye Lowassa akakatwa ugombea wa CCM na majuzi kuhamia upinzani. Sasa CCM inajikuta ikiwa na wajibu mmoja mbaya sana – kumkana mtu ambaye ilimtangazia usafi wa kinabii na kujinasibisha naye sako kwa bako. Jukumu hili linaonekana kuwa gumu upande wa CCM Taifa, lakini limetupwa moja kwa moja kifuani kwa CCM Zanzibar. Ndio maana jana, tarehe 31 Julai 2015, Borafya akaitisha kikao cha kujipakaza matapishi na kisha kuyameza kwenye ukumbi wa CCM Kisiwandui.

Sasa Lowassa hafai tena, ni mbaya, fisadi na mlafi wa madaraka. Kwa sasa Lowassa ananuka kama mzoga kwenye pua za makada wa CCM. Kisa! Kahama CCM na kuhamia chadema kuendeleza kile kinachoitwa safari yake ya matumaini. Kumkejeli na kumbeza Lowassa kwa makada hawa ni sawa na kula matapishi yao wenyewe waliyokwisha yatapika. Vyereje leo! Kwani hapo mwanzo hawakumjua Lowassa? Au ni kutokana na hili joto la mabadiliko linalowafukuta ndani kwa ndani?

Kujiunga kwa Lowassa na Chadema sio tu kumewaumiza makada wa CCM visiwani Zanzibar, bali hata upande wa Tanganyika pia. Wamegubikwa na mawazo ambayo yanawala na kuzifyonza siha za miili yao. Sasa wanamvisha Lowassa guo la ubaya badala ya lile la ufalme uliotukuka walilomvisha hapo awali. Wanataka kuuaminisha umma kuwa Lowassa hafai, fisadi, mlafi wa madaraka na ni wa kuogopa kama ukoma! Wanatapatapa kama wafa maji.

Kibaya kwa wote ni kwamba wameshindwa kuzisoma alama za nyakati kama alivyoshindwa Mwenyekiti wao wa Taifa, Rais Jakaya Kikwete, kule kwenye vikao vya Halmashauri Kuu na baadaye Mkutano Mkuu, Dodoma. Alikosea takribani kwenye kila hatua kwa kushindwa kwake kuusoma wakati. Huu sio tena ule utawala wa Giningi aliousimulia mwandishi mashuhuri Prof. Said Ahmed Mohammed kwenye tamthilia ya Kivuli Kinaishi – ulimwengu wa cheupe kuitwa cheusi na cheusi kuitwa cheupe. Wana-CCM wanaombeza Lowassa na kumwita fisadi wanapaswa wawajibu Watanzania suali hili: Je, baada ya kujiuzulu kwake uwaziri mkuu kwa sakata Richmond, ufisadi ndani ya serikali ya CCM umepungua au umeongezeka? Watanzania wanajuwa jawabu ya suali hilo na Oktoba 25 watalitoa kwenye sanduku la kura.

Hakuna ubishi kuwa Lowassa ni kipenzi cha Watanzania na ana wafuasi wengi. CCM hupoteza muda mwingi kwa kunukuu maneno ya Julius Nyerere kama kwamba ni Msahafu au Biblia ili kuhalalisha maamuzi yao. Lakini cha kushangaza ni kwamba huchagua nukuu ipi waitumie, ipi waipuuzie. Ni Nyerere huyo huyo pia aliyesema: “Sasa ni vizuri mukasikiliza maoni ya wananchi, jee wananchi wanataka nini? Musidhani munaweza mukapata ushindi mukipuuza maoni ya wananchi, mukasema hili ni letu tu! Hamteui katibu wa chama bali munateua mtu atakayekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano ya Tanzania. Hivyo ni vizuri musikilize wananchi wanataka nini juu ya watu wenu, musipuuze maoni ya wananchi hata kidogo. Chama kitakachopuuza maoni ya wananchi, kinaweza kikalia kilio na asipatikane mtu wa kusaidia kupangusa machozi.”

Kikwete aliwaongoza wenzake kupuuzia maneno hayo ya mwasisi wa chama chao ambaye hutaka waonekane kuwa wanamuheshimu sana hata sasa akiwa kaburini aliko. Kikwete alisahau hata njia ambayo ilimfikisha alipo miaka kumi tu iliyopita, akaongoza genge la kupora haki ya wanachama wa CCM walio wengi. Sasa mpira uko upande wa umma. Inafaa ikumbukwe kuwa serikali ni ya wananchi na siyo ya chama cha siasa. Wananchi ndio wenye mamlaka ya kuchagua nani anafaa kuwa kiongozi wao. Unapofanya kinyume chake, huko ni kuwanyang’anya wananchi madaraka na watakuhukumu.

Narudia. Hakuna ubishi hata kidogo kuwa Lowassa anapendwa na Watanzania walio wengi. Kulikata jina lake katika hatua za awali sio tu kulikuwa ni dharau kwa Lowassa mwenyewe, bali hata kwa wananchi wenyewe ambao kimsingi ndiyo wenye mamlaka. Borafya alisema kwenye mkutano wa kujimezesha matapishi kuwa “CCM ilikuwa ina watu wawili tu ambao walilelewa kiuongozi. Kikwete na Lowassa.” Hakukosea kwenye hilo. Sasa mmoja kasimama upande mmoja na mwengine upande mwengine. CCM ingoji gharika itakayowaangamiza Oktoba 25.

Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mjini Unguja. Borafya Silima, akimpokea Edward Lowassa mwanzoni mwa mwezi Juni kwenye Uwanja wa Ndege wa Zanzibar.
Imeandikwa na Khelef Nassor via HakiNaUmma

Uchaguzi CCM waahirishwa baada ya kukamatwa "kura bandia"

Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Tarime mkoani Mara kimetangaza kuhairisha uchaguzi wa kura za maoni kwa Ubunge na Udiwani baada ya kukamatwa kura zinazodaiwa kupigwa kabla ya muda wa uchaguzi kuanza.

Tamko la kuhairishwa kwa uchaguzi huo imetangazwa na Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Tarime, Rashidi Bogomba wakati alipokuwa akizungumza na wananchama wao nje ya ofisi za wilaya na kusema wamefikia uamuzi wa kuhairisha kura hizo kutokana na kukamatwa kwa masanduku ya kupigia kura yakiwa tayari na kura zilizopigwa jana asubuhi.

“Leo asubuhi zimekamatwa kura zikiwa tayari zimeshapigwa, kutokana na hali hiyo tumelazimika kuhairisha uchaguzi ambao ulipaswa kufanyika leo (jana) hivyo utafanyika kesho (leo), kwa sasa vinafanyika vikao kujadili suala hilo,” alisema.

Mwenyekiti huyo alisema kura hizo zimekamatwa katika vijiji vya Nyamwaga, Masanga, Nyamongo na nyingine katika mitaa ya Bomani, Magena, Romori iliyopo ndani ya Jimbo la Tarime.

Hata hivyo alibainisha kuwa kura hizo zinazodaiwa kupigwa kabla ya muda zilikuwa zimeandaliwa na Katibu wa CCM Wilaya ya Tarime Bernard Nyerembe kwa lengo la kuwasaidia wagombea wawili ambao aliyekuwa mbunge wa Jimbo la Tarime, Nyambari Nyangwine na Gaudensia Kabaka anayewania ubunge katika Jimbo Jipya la Tarime Mjini.

Wanaogombea Ubunge Jimbo la Tarime ni Christopher Kangoye ambaye ni Mkuu wa Wilaya Arusha, Nyambari Nyangwine Mbunge wa Jimbo la Tarime anayetetea jimbo, Pius Marwa, John Gimunta, Maseke Muhono, Lucas Mwita, Paul Matongo na Charles Machage.

Kwa jimbo jipya la Tarime mjini wanaotangaza nia ya Ubunge ni Waziri wa kazi na Ajira Gaudensia Kabaka, Maico Kembaki, Philipo Nyirabu, Jonathani Machango, Ditu Manko na Brito Burure.

Alisema kutokana na tuhuma hizo kumuangukia Katibu wa Wilaya uchaguzi ambao utafanyika leo hautasimamiwa tena na Katibu Nyerembe bali Katibu wa Jumuiya ya Wazazi wa Wiaya ya Tarime Mathias Rugora.

“Katibu huyu kwa sasa tumemkabidhi mikononi mwa Taasisi ya Kuzuwia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) ambao tumewaachia jukumu la kuendesha uchunguzi wake ikiwa ni pamoja na kufuatilia kura hizo zilipigwa na nani na wakati gani wakisaidiwa na Katibu husika.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kipolisi wa Tarime na Rorya, Benedict Mambosasa amethibitisha kukamatwa kwa Katibu huyo wa CCM Nyerembe kukabidhi kwa Takukuru kwa mahojiano ya rushwa kutokana na kutuhumiwa kununuliwa ili kupindisha sheria za uchaguzi.

Kwa upande wake Nyambari Nyangwine anayetetea kiti cha Ubunge amekanusha kuhusika na hujuma hiyo na kubainisha kuwa hakuwa anatambua hatua jambo hilo na kwamba anachojua ni kuwa kura zilipaswa kupigwa leo.

Naye Waziri Gaudensia Kabaka yeye alisema amestushwa na taarifa hizo na kudai huenda ni moja ya mbinu chafu zilizotumika kuwaangusha katika uchaguzi huo.

sema anayetangazania ya Ubunge Jimbo la Tarime mjini wote wakiongea kwa simu wamekanusha kuhusika na kudai hizo ni njama zilizopikwa dhidi yao ili wasiate nafasi ya Ubunge.