Katuni tulizopata, Jumapili 9.8.2015

    

Lowasa kuhamia CHADEMA: Maoni ya Prof. Mbele kuhusu yanayosemwa

[...] Edward Lowassa amejitoa CCM na kuibukia CHADEMA (UKAWA). Tayari amezua zogo. Watu wanarusha makombora kwake, kwa CHADEMA, na kwa UKAWA. Wanasema kwa nini CHADEMA impokee mtu ambaye wamekuwa wakimtukana kama fisadi mkubwa.

Ajabu ni kwamba hakuna mahakama yoyote ambayo imemwona Lowassa kuwa fisadi. Amehukumiwa na hisia za watu pamoja na majungu ya magazetini, katika blogu, na vijiweni. Amekosewa haki ya msingi, kwa mujibu wa tangazo la kimataifa la haki za binadamu, haki ya kwamba mtu anayetuhumiwa au kushtakiwa kwa kosa, lazima ahesabiwe kuwa hana kosa hadi mahakama ithibitishe vinginevyo.

Kwa hivi, wote wanaomwita Lowassa fisadi, au waliomwita fisadi (wakiwemo CHADEMA) wajirekebishe. Wamtendee haki Lowassa. Hadi mahakama ithibitishe, Lowassa ana haki ya kuonekana hana kosa, na kuingia kwake CHADEMA hakuna dosari.

Kwa CHADEMA na UKAWA kumkaribisha Lowassa ni sahihi kabisa. Ni jambo la busara CHADEMA wamwombe radhi kwa kumtukana kwa miaka mingi, yaishe. Na yeye ameonyesha roho nzuri kwa kuja kwenye chama chao, bila kinyongo. Ameonyesha moyo unaoendana na mafundisho ya dini yetu ya u-Kristu ya kuwasamehe wanaotutendea mabaya.

Kwa upande wa CCM ni kwamba Lowassa muda wote wamekuwa naye bega kwa bega. Alikuwa mkuu wa idara yao ya mambo ya nje. Hata baada ya kukatwa kwenye uchaguzi wa mgombea urais, hawakumtukana. Lakini ghafla, baada ya yeye kuhamia CHADEMA (UKAWA) wameanza kumtukana, kwamba ni kapi. Vigogo wa CCM wanaohamia upinzani wanatukanwa kwamba ni makapi.
Imenukuliwa kutoka kwenye blogu yake - Hapa Kwetu.

Tadhahari kuhusu matapeli "wanaopitisha" watu kupata uongozi CCM

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Mchakato wa kuwapata wagombea wa nafasi ya Ubunge, Uwakilishi na Udiwani ndani ya CCM ulioanza tarehe 15/07/2015 unaendelea vizuri na unakaribia katika hatua za mwisho za uteuzi. Kwa nafasi ya Ubunge na Uwakilishi tunategemea kufanya uteuzi tarehe 13/08/2015.

Kutokana na mchakato huo, kuna baadhi ya maeneo kuna malalamiko ya hapa na pale. Iwapo kuna mwanachama ambae hakuridhaka na mchakato ulivyoendeshwa kwenye eneo lake apeleke malalamiko yake kwenye ngazi ya juu ya ngazi iliyosimamia mchakato husika.

Pamekuwa na utamaduni unaojengwa wa makada wetu kulalamika barabarani na wakati mwingine kushawishi wanachama kulalamika kwenye vyombo vya habari na kwingineko, utaratibu huo sio wa chama chetu, Chama kinazo taratibu za kushughulikia malalamiko yatokanayo na michakato hii. Tunashauri taratibu hizo zifuatwe. Katika kufikia hatua hiyo wanachama wanaombwa kuwa watulivu.

Kumetokea pia wimbi la matapeli wanaotumia majina ya viongozi, na baadhi yao wamesajili simu zao kwa majina ya viongozi wakizitumia kwa kuwatapeli wagombea wanaotafuta nafasi za uongozi kwa kuwaahidi watatumia nafasi zao kuwapitisha majina yao katika vikao vinavyotarajiwa kuanza hivi karibuni.

Chama Cha Mapinduzi kinawatahadharisha wanachama ambao watapata simu hizo kuzipuuza na kuwa waangalifu dhidi ya matapeli hao.

Hakuna njia ya mkato kupata uteuzi ndani ya CCM zaidi ya kufuata kanuni na taratibu za Chama. Njia yoyote ya mkato ni utapeli na hauna nafasi ndani ya CCM.

Zipo taarifa za uhakika kuwa kuna baadhi ya makundi ndani ya UKAWA yamepanga na wameanza kuratibu zoezi la kutengeneza kadi feki (za bandia) za CCM na kuzigawa kwa watu wao ili baadaye asipopita mgombea wao ionekane Wana CCM wanakihama chama chao kwa kuzirudisha kadi hizo kwenye shughuli mbalimbali za vyama hivyo vinavyounda UKAWA.

Taarifa hii inafanyiwa kazi ndani ya chama na kwa wakati huu tunawaomba wananchi wawe makini na waangalifu wasije ingizwa kwenye uhalifu huu usiokuwa na tija.

Kwa taarifa hii, tunawaomba wanachama wa CCM na wapenzi wa Chama chetu kutokuwa na hofu na hila hizo na wawe macho kuzibaini mbinu hizo chafu na kuzitolea taarifa kwa vyombo vinavyohusika.

Imetolewa na:-

Nape M. Nnauye,
KATIBU WA HALMASHAURI KUU YA TAIFA
ITIKADI NA UENEZI
08/08/2015

Mbunge CUF afariki ajalini

Clara Mwatuka
Clara Mwatuka 
Aliyekuwa Mbunge wa Viti maalumu CUF mama Clara Mwatuka amefariki dunia baada ya gari lake kupinduka lilipokuwa linashuka Makonde Plateu kuelekea Ndanda.

Gari hili lilikuwa linaendeshwa na dereva wake, ambaye inasemekana ni mwanaye. Maiti ipo chumba cha maiti cha Ndanda Regional Referral hospital.


Habari kuhusu safari ya Prof. Lipumba nchi jirani

Picha hii imepigwa jana toka Kigali, Rwanda: Prof-Lipumba na Wakala wa Usalama, kijana wa Kinyarwanda (picha: MwanaHALISI Online)
SIRI kuu ya kujiuzulu uenyekiti katika Chama cha Wananchi (CUF), Prof. Ibrahim Lipumba, imeanza kufichuka.

Taarifa kutoka serikalini, ofisi kuu ya CCM, Lumumba, Idara ya Usalama wa taifa (TISS) na kwa watu waliokaribu na Prof. Lipumba mwenyewe zinasema, kiongozi huyo amejiuzulu ili kulinda ajira ya mmoja wa maswahiba wake wakubwa serikalini.

“Prof. Lipumba amejiuzulu baada ya wakubwa ‘kufika bei’ ili kulinda kibarua cha mmoja wa vigogo kutoka idara nyeti serikalini, ambaye ni swahiba wake wa karibu,” ameeleza mmoja wa viongozi wajuu kutoka serikalini.

Haijafahamika kiasi gani cha fedha alicholipwa, ili kumshawishi kujiondoa katika wazifa wake, ingawa kuna taarifa kuwa zaidi ya Sh. 3.7 bilioni zimetumika kwa kazi hiyo.

Aidha, taarifa zinasema, Prof. Lipumba amelazimika kujiuzulu baada ya kuahidiwa madaraka makubwa katika serikali ijayo, ikiwa Chama Cha Mapinduzi (CCM), kitafanikiwa kushika madaraka ya dola.

Miongoni mwa vyeo ambavyo Prof. Lipumba ameambiwa atakabidhiwa, ni kufanywa kuwa waziri wa fedha katika serikali ya John Magufuli au kuwa mshauri mkuu wa uchumi wa serikali hiyo.

Kupatikana kwa taarifa kuwa Prof. Lipumba amelambishwa donge kubwa ili kusaliti mageuzi, zimekuja siku tatu baada ya mwanasiasa huyo aliyekuwa akiheshimika nchini kutangaza kujiuzulu kwa kile alichoita, “kusutwa na dhamira yake.”

Alisema, ameamua kujiuzulu wazifa wake wa unyekiti baada ya viongozi wenzake wanne kutoka jumuiko la vyama vinavyounda Umoja wa Kutetea Katiba ya Wananchi (UKAWA), kumkaribisha ndani ya umoja huo, mwanasiasa mashuhuri nchini, Edward Lowassa na kisha kumteuwa kuwa mgombea wake wa urais.

Vyama vinavyounda UKAWA, ni NCCR- Mageuzi, CUF, National Democrat League (NLD) na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

Lowassa alijiunga na Chadema baada ya viongozi wakuu wa UKAWA, akiwamo Pro. Lipumba, James Mbatia, Freeman Mbowe na Dk. Emanuel Makaidi, kukutana na kufikia makubaliano ya pamoja kuhusu jambo hilo.

Vyanzo vya taarifa vinasema, Prof. Lipumba alikutana mara kadhaa na kwa faragha na Lowassa kwa lengo la kumshawishi kujiunga na umoja huo.

Miongoni mwa mikutano hiyo, ni pamoja ule uliofanyika Jumamosi ya tarehe 4 Aprili, majira ya saa 5 asubuhi, ofisini kwa Lowassa, Mikocheni jijini Dar es Salaam.

Katika mkutano huo, Prof. Lipumba alimhakikishia Lowassa kuwa UKAWA wako tayari kumpokea na kumkabidhi bendera yake katika kinyang’anyiro cha urais cha Oktoba. Alitumia mkutano huo kumkandia Dk. Willibrod Slaa kwa kudai kuwa siyo mtu mwenye sifa za kuwania nafasi hiyo, kwa madai kuwa ni mtu asiyeaminika.

Hata hivyo, Lowassa alimuonya mwanasiasa huyo kuwa makini na kauli zake kwa kuwa zitaweza kuwagawa. Alisema, anamfahamu vyema Dk. Slaa na hana matatizo naye.

Habari zinasema, mara baada ya Prof. Lipumba kujiuzulu, aliondoka nchini kuelekea Rwanda kwa kazi maalumu aliyopewa na CCM.

Akiongea na Azam Televisheni, Prof. Lipumba amekiri kuwa nchini Rwnada na kuongeza, “niko huku kufanya utafiti wa jinsi Rwanda ilivyofanikiwa kiuchumi,” jambo ambalo linathibitisha madai kuwa atakuwa mshauri wa uchumi au Waziri wa Fedha katika serikali ya CCM.

Mtoa taarifa anasema, Prof. Lipumba ameondoka nchini na walinzi maalum ambao amekabidhiwa kama sehemu ya makubaliano ya mradi wake na serikali.

Anasema, “…hii habari ya Lipumba imethibitisha kile nilichokisema siku za nyuma, Lipumba anatumika. Ni kibaraka… Tena hukutana naye nyumbani kwake.

“Nilipoona Prof. Lipumba yuko UKAWA nilipata mashaka makubwa, lakini nilikuwa na ahueni kwa sababu niliambiwa Maalim Seif Sharif Hamad, alishawatahadharisha wenzake wasimshirikishe Lipumba kwenye mambo nyeti ya UKAWA kwa sababu haaminiki.”


Tamko la Wizara kuhusu mgogoro na madereva na Serikali

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

WIZARA YA KAZI NA AJIRA

TAARIFA KWA UMMA

TAMKO LA SERIKALI KUHUSU HATUA ZILIZOCHUKULIWA KUSHUGHULIKIA MGOGORO WA MADEREVA

1.0 Tarehe 9/4/2015 ulifanyika mgomo wa madereva nchini uliohusu malalamiko na kero mbali mbali za madereva. Katika kuzipatia ufumbuzi kero hizi, tarehe 2/5/2015 Mhe. Mizengo Peter Kayanza Pinda, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, aliunda Kamati ya Kudumu ya Kutatua Matatizo katika Sekta ya Usafirishaji yenye Wajumbe kutoka Serikalini, Umoja wa Madereva na Vyama vya Madereva, pamoja na Wamiliki wa Vyombo vya Usafirishaji. Kutokana na vikao vilivyofanywa na Kamati hiyo iliundwa Kamati Ndongo ya kushughulikia haki na maslahi ya madereva.

2.0 Kufuatia vikao vya Kamati ya Kudumu na Kamati Ndogo vilivyofanyika tarehe 12/5/2015, 19/5/2015, 21/5/2015 18/6/2015, 19/6/2015 na 23/6/2015, tunapenda kutoa taarifu kwa wadau wote wa sekta hii ya usafirishaji pamoja na wananchi wote kwa ujumla kwamba hadi sasa hatua zifuatazo zimeshakwisha kutekelezwa:

2.1 Serikali kwa kushirikiana na Viongozi wa Vyama vya Wafanyakazi Madereva na Viongozi wa Umoja wa Wamiliki wa Vyombo vya Usafirishaji nchini imeboresha Mkataba wa Ajira wa Madereva. Mkataba ulioboreshwa uliidhinishwa na wadau katika kikao kilichofanyika tarehe 23/6/2015 na ilikubalika kwamba Mkataba huo uanze kutumika tarehe 1/7/2015. Aidha, ilikubalika kwamba hatua za kutekeleza Mkataba huo iwe ni katika kipindi cha miezi mitatu hadi tarehe 30/9/2015 ili kuwapa nafasi waajiri na madereva kuhuisha mikataba yao ya zamani na kutumia mipya na madereva watakaoajiriwa kuanzia tarehe 1/7/2015 waendelee kutumia mikataba mipya.

2.2 Kwa kuzingatia hoja ya kuimarisha umoja wa madereva, Serikali imewezesha kuundwa kwa vyama vya wafanyakazi vya madereva viwili ambavyo ni Chama cha Wafanyakazi Madereva wa Malori Tanzania (CHAMAWATA) kilichosajiliwa tarehe 28/5/2015 na Chama cha Wafanyakazi Madereva Tanzania (TADWU) kilichosajiliwa tarehe 25/6/2015. Uwepo wa Vyama hivyo utawawezesha Madereva kushiriki ipasavyo katika majadiliano ya pamoja na wamiliki wa vyombo vya usafirishaji kwa lengo la kuboresha maslahi na haki za madereva.

2.3 Serikali kupitia Wizara ya Kazi na Ajira imeendelea kutoa elimu ya sheria za kazi kwa Viongozi wa Vyama vya Wafanyakazi vya Madereva, Viongozi wa Umoja wa Wamiliki wa Vyombo vya Usafirishaji,na baadhi ya Wamiliki wa vyombo vya usafirishaji kama ilivyoelekezwa na Kamati ya Kudumu. Vikao vya uelimishaji vilifanyika tarehe 19/5/2015, 18/6/2015 na 23/7/2015. Elimu ya sheria za kazi itaendelea kutolewa kwa madereva na wamiliki wa vyombo vya usafirushaji nchi nzima kwa ajili ya kuimarisha utekelezaji wa sheria, kanuni, na taratibu za kazi.

2.4 Ili kudhibiti tatizo la kughushi mikataba ya ajira linalofanywa na baadhi ya wamiliki wa vyombo vya usafirishaji, ilikubalika kuwepo na nakala tatu za mkataba kwa ajili ya mwajiri, dereva na SUMATRA. Aidha, katika utoaji wa leseni mpya kwa vyombo vya usafirishaji, SUMATRA itoe leseni baada ya wamiliki wa vyombo vya usafirishaji kuwasilisha nakala ya mkataba wa ajira wa dereva ulioboreshwa.

3.0 Aidha, katika kikao cha kutoa elimu ya sheria za kazi kilichofanyika tarehe 7/8/2015. Serikali na viongozi wa Vyama vya wafanyakazi vya madereva pamoja na viongozi wa umoja wa wamiliki wa vyombo vya usafirishaji walikubaliana kwamba kikao kingine cha Kamati ya Kudumu ya Waziri Mkuu kifanyika siku ya Alhamisi tarehe 13/8/2015.

4.0
Hitimisho: Serikali inapenda kutoa wito kwa Wamiliki wa vyombo vya usafirishaji, viongozi wa vyama vya wafanyakazi vya madereva pamoja na madereva wote nchini kutekeleza makubaliano yaliyokwishafikiwa hadi sasa. Aidha, Serikali pamoja na Taasisi zake itaendelea kutoa elimu pamoja na kufuatilia makubalianao yaliyofikiwa na hatua za kisheria zitachulikwa dhidi ya wale watakaokiuka utekelezaji wa makubaliano hayo.

IMETOLEWA NA
KATIBU MKUU
WIZARA YA KAZI NA AJIRA

8/08/2015.

Kura za maoni CCM: Wabunge waliokubali matokeo na waliokata rufani

CCM imesema haitarudia makosa ya mwaka 2010 ya kutengua uamuzi wa wanachama, lakini itahitaji kuwa na moyo mgumu baada ya makada wengi kukata rufaa kupinga matokeo ya kura za maoni.

CCM inamalizia hatua ya mwisho ya mchakato wake wa ndani wa kupata wagombea ubunge na udiwani kwa vikao vya Kamati Kuu na Halmashauri Kuu vitakavyopitia majina ya makada wote walioshinda kwenye kura za maoni, ambazo zilitawaliwa na tuhuma za rushwa na ukiukwaji wa taratibu.

Vikao hivyo huwa vinaweza kutengua ushindi wa kada kwenye kura za maoni kwa kuangalia rufani zinazopinga mchakato, tuhuma za rushwa na ukiukwaji wa taratibu.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alisema wamepokea malalamiko mengi kuhusu ukiukwaji wa kanuni za uchaguzi katika upigaji wa kura za maoni.

“Kumekuwa na utamaduni wa kulalamika barabarani wakati mwingine kushawishi wanachama kulalamika kwenye vyombo vya habari na kwingineko. Utaratibu huu si wa chama chetu,” alisema Nape.

“Tunashauri taratibu zifuatwe. Katika kufikia hatua hii tunawaomba wanachama wawe watulivu.”

Alisema wanachama wamejaa mjini Dodoma wakijaribu kushawishi wajumbe kuhusu rufaa zao, lakini akasema kinachotakiwa kiwasilishwe ni malalamiko yao, ushahidi wa kutosha katika ngazi husika.”

Nape pia alisema kumezuka wimbi la matapeli linalowalaghai makada walioshindwa katika kura za maoni kuwa watoe fedha ili wawasaidie rufaa zao kwenye vikao hivyo.

Alisema matapeli hao wamesajili namba za simu za viongozi wa CCM na kwamba yeye ni mmoja wa viongozi walioathirika na utapeli huo kwa namba yake ya simu ya mkononi kutumika.

“Wanawataka kutoa fedha ili waweze kuwasaidia na tayari tumeshawanasa baadhi yao na kuwakabidhi polisi. Wawe makini wasikubali kutapeliwa fedha zao na kama wana malalamiko wafuate utaratibu uliowekwa,” alisema.

Pamoja na Nape kutotaja idadi ya rufaa zilizowasilishwa, Mwananchi iliongea na makada 16 ambao walithibitisha kuwa wanasubiri uamuzi wa vikao hivyo baada ya kutuma barua zao kupinga matokeo.

Mwananchi imeshuhudia makada waliobwagwa katika kura hizo, wakiwemo mawaziri wakiwa kwenye viunga vya jengo la makao makuu ya CCM mjini hapa.

Baadhi ya makada hao ni mbunge wa Busega, Dk Titus Kamani aliyeangushwa na Dk Raphael Chegeni. Kamani aliiambia Mwananchi kuwa amekata rufani kupinga matokeo ya kura za maoni kwa kuwa mchakato ulitawaliwa na rafu nyingi na anaamini yeye ni mshindi.

Mwingine aliyekuwa mjini hapa ni Juma Kilimba na David Jairo waliobwagwa Iramba Magharibi, Asumpta Mshama aliyeangushwa kwenye Jimbo la Nkenge.

Wabunge waliokata rufani

Vigogo wengine walioangushwa kwenye kura hizo ni Naibu Waziri wa Maji, Amos Makala (Mvomero), ambaye alisema amelazimika kukata rufaa baada ya kutoridhishwa na mchakato ulivyoendeshwa, ikiwa ni pamoja na baadhi ya viongozi wa CCM kutumika kumwangusha.

Alisema kulikuwa na hujuma wakati wa uchaguzi na baadhi ya viongozi wa chama walitumia mwanya huo kumjengea mazingira ya ushindi mpinzani wake.

Mbunge mwingine, Said Nkumba (Sikonge) alisema amekata rufani ili haki itendeke kwa kamati husika, baada ya kubaini kuwepo kwa njama za makusudi za kumwangusha hasa baada ya uongozi wa wilaya kuamuru upigaji wa kura urudiwe katika maeneo ambayo alionekana ameshinda. Madai kama hayo yalitolewa na Gregory Teu (Mpwawa) ambaye alikata rufaa akisema haki haikutendeka na kulikuwa na mchezo mchafu. Mbunge wa Dodoma Mjini, Dk David Mlole alisema ikiwa Kamati Kuu ya CCM itashindwa kuitendea haki rufaa yake, ataachana na masuala ya siasa.

Naye mbunge wa Morogoro Kusini –Mashariki, Dk Lucy Nkya alisema iwapo rufaa yake haitashinda, atakubaliana na matokeo na hatahama chama kwa sababu ya kushindwa katika kura za maoni.

Mshama alidai kuwa amehujumiwa katika mambo mengi yaliyojitokeza kwenye mchakato huo, ikiwamo baadhi ya washindani wake kupotosha kwenye vyombo vya habari kuhusu siku ya kura ya maoni.

“Jambo hilo liliwafanya baadhi ya wapigakura wangu kutojitokeza, hivyo kunifanya nikose kura zao. Nimefanya mambo mengi katika jimbo hili ambalo watu wake wanapenda elimu walinifurahia. Siamini kama wamenikataa, hizi ni hujuma,” alisema Mshama.

Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi Dk Titus Kamani alisema anavyojua ni kwamba yeye ndiye mshindi.

“Hivi wewe unaongea nini? Mimi najua nimeshinda sasa unasemaje nikuambie plan B yangu wakati nimeshinda mimi. Siwezi kushindwa na wala sijasikia kwamba nimeshindwa,’’ alisema Dk Kamani

Naye Nyambari Nyangwine, mbunge wa Tarime, alisema alisema mambo hayakuwa mazuri kwenye matokeo ya kura za maoni.

“Mimi siwezi kuhama chama kwani kutumikia wanaume wawili ni kazi kubwa. Unajua naamini Kamati Kuu itatenda haki tu,’’ alisema

Ally Kibona Mbunge wa Ileje alisema anaiomba CCM iwe makini na rafu ambazo zinachezwa ndani ya chama hicho hususan kipindi cha uchaguzi ikiwemo kuanza kampeni kabla ya muda wake.

Mbunge wa Jimbo la Mbinga Mashariki mkoani Ruvuma, Gaudance Kayombo alisema kwamba yeye alishakata rufaa baada ya kutokubaliana na matokeo hayo ila hafikirii kukihama chama tawala.

Wakubali matokeo

Wakati makada hao wakisubiri kwa hamu uamuzi wa vikao vya juu vya chama, baadhi ya vigogo walioshindwa wamesema wamekubaliana na matokeo na hawana mpango wa kukata rufaa.

Wabunge hao ni pamoja na Dastan Mkapa (Nanyumbu), Dk Muhammed Seif Khatibu (Uzini), Mathias Chikawe (Nachingwea), Gaudensia Kabaka, Adam Malima (Mkuranga) na Salehe Pamba (Pangani).

Vikao vya uteuzi

Nape alisema jana kuwa vikao vya Taifa vya chama hicho vilianza jana na sektarieti itakaaa kwa siku mbili, ikifuatiwa na Kamati Kuu ya Taifa na Halmashauri Kuu itakayokutana Jumatano na Alhamisi.

“Kwa nafasi ya ubunge na uwakilishi tunategemea kufanya uteuzi Agosti 8 (Alhamisi),”alisema Nape.

Polepole: Nitasimama na kukampeni kumkataa mgombea wao wa urais

Humphrey Polepole
Humphrey Polepole
Mjumbe wa Iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Humphrey Polepole amesema yupo tayari kufanya kampeni za kumpinga mgombea urais wa Chadema na Ukawa, Edward Lowassa kwa madai kuwa ana doa linalomzuia kuwania nafasi hiyo.

Polepole ameibuka kuwa maarufu tangu kumalizika kwa Bunge la Katiba, akishiriki kwenye midahalo kadhaa kuhusu mchakato wa kuandika Katiba mpya, akitofautiana na msimamo wa CCM wa kubadilisha Rasimu ya Katiba.

Akizungumza na Mwananchi jana, Polepole alisema Lowassa anayeungwa mkono na vyama vya NCCR-Mageuzi, Chadema, CUF na NLD vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), ana tuhuma za ufisadi na ni mmoja wa makada wa CCM walioipinga Rasimu ya Katiba.

Polepole alisema msingi wa kuzaliwa kwa Ukawa ni kutaka Katiba mpya yenye maoni ya wananchi, hivyo Chadema kumpokea Lowassa ni sawa na kukiuka misingi hiyo.
“Nimeshirikiana na Ukawa na viongozi wao kama Watanzania kuhakikisha Taifa letu linapata Katiba mpya na inayotokana na maoni ya wananchi. CCM ambao walikuwa ndiyo wana mkakati na wenye maamuzi ya mwisho katika kukwamisha maoni ya wananchi. Watu hao (wa CCM) hawastahili kupewa uongozi iwe ndani ya CCM au hata ndani ya Ukawa... Hawana dhamira njema na Taifa letu, watuhumiwa mengine nitaelewa, lakini kwenye la Katiba nilikuwepo na ninajua mchango wao wa kutukwamisha. Niliweka maoni yangu kwamba CCM ikiwachagua hao nitapiga kampeni ya kuwakataa. Hawakupita CCM na mmoja wapo ni Lowassa.”
Alisema amepoteza imani na Ukawa kwa kukubali kuikiuka misingi ambayo awali waliisimamia.
“Nina haki ya kutokubaliana na msimamo wa Ukawa na ikibidi nitasimama na kupiga kampeni ya kumkataa mgombea wao wa urais,” 
Katika Bunge la Katiba, wajumbe kutoka CCM walilazimisha kuondolewa kwa baadhi ya mapendekezo kwenye Rasimu ya Katiba, ikiwa ni pamoja na pendekezo la kutaka muundo wa Muungano uwe wa serikali tatu.

Baadhi ya viongozi na wanachama CCM Arusha wahamia CHADEMA

Onesmo Ole Nangole (kulia) akizungumza na waandishi wa habari. Kushoto ni Isaac Joseph "Kadogoo" (picha: Pamela Mollel, ARUSHA)
Chama cha Mapinduzi kimeendelea kupoteza wanachama baada Mwenyekiti wa chama hicho Mkoa wa Arusha, Onesmo Nangole pamoja na Katibu Mwenezi wa Mkoa huo, Isaac Joseph kutangaza rasmi kujiunga CHADEMA.

Uamuzi huo ulitangazwa jana jijini Arusha katika moja ya hoteli maarufu ambapo viongozi hao walipata wasaa wa kupokelewa na uongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).
“Nasema CCM imekosa misingi iliyounda chama hiki. Hakuna haki yoyote inayotendeka. Imekuwa chama cha watu fulani ambao wamekuwa wakichukua maamuzi ya kukurupuka kwa faida yao.”
Nangole ambaye ameitumikia CCM toka mwaka 1977,  anakuwa mwenyekiti wa pili wa mkoa kukihama chama hicho.

Wiki iliyopita, aliyekuwa mwenyekiti wa CCM mkoa wa Singida, Mgana Msindai na ambaye pia alikuwa Mwenyekiti wa Wenyeviti wa CCM Taifa, alihamia CHADEMA.

Katibu Mwenezi wa CCM mkoa wa Arusha, Isaac Joseph maarufu kama Kadogoo alisema kudhirisha kuwa CCM sasa inaendeshwa kwa masilahi ya watu wachache, mchakato wa kumpata mgombea Urais wa CCM uligubikwa na mizengwe na kusema kuwa kama kanuni na taribu zingefuatwa ni Edward Lowasa ndiye angechaguliwa katika mchakato ule.

Pia alisema hawezi kukaa na kuongoza katika chama ambacho wafuasi wake wamekihama, huku akidai kuwa kwa Arusha mjini alikuwa na wafuasi elfu ishirini na saba na waliojitokeza kupiga kura ya maoni ya kumpendekeza mgombea ubunge kupitia CCM ni elfu tano:
“Siwezi kubaki kuongoza katika chama ambacho kinabaka demokrasia Uongozi wa CCM watafute viongozi wengine wa kuongoza chama hicho siko tayari na siwezi tena”
Mwenyekiti wa CHADEMA Wilaya ya Arusha Magoma Derick Magoma akiwapokea wanachama hao kutoka CCM na kuhamia rasmi CHADEMA anawakaribisha wote wanaoijisika kuunga nao na kuleta mabadiliko ya kweli kwa maslahi ya Taifa kwa ujumla
“Tunawakaribisha wote wanaotaka kuhamia CHADEMA, mlango upo wazi muda wowote na siku yoyote. Muda wa mabadiliko ni sasa.”
Kadi za uanachama zikichomwa moto

Zaidi ya wafugaji 300 warudisha fomu CCM na kuhamia CHADEMA Monduli


Zaidi ya wanachama mia tatu wa CCM kutoka jamii ya kifugaji katika kata ya Engaruka wilaya ya Monduli wamerudisha kadi za CCM na kujiunga na CHADEMA huku wakidai maamuzi yao yametokana na utashi wao binafsi kwa kuzingatia hali halisi ya kisiasa ilivyo hivi sasa.

ITV ilifika katika kijiji cha Engaruka na kushuhudia mamia ya wanachama waliokusanyika katika mkutano wa hadhara kukusanya kadi za CCM kuzichoma moto na kuchukua kadi za CHADEMA huku wakiainisha sababu zilizofanya kufikia maamuzi hayo.

Akizungumza baada ya kuwapokea wanachama hao, akiwemo mwenyekiti wa kijiji cha Engaruka, Lewanga Kivuyo, mwenyekiti wa BAVICHA wilaya ya Monduli, Yasini Shabani amesema CHADEMA ni chama kinachozingatia haki ya kila binadamu na kila mwanachama.

Kada maarufu wa CHADEMA, Julius Karanga amewataka wananchi kuwa wavumilivu kwa kuwa mabadiliko yana changamoto nyingi za kukatisha tamaa kutoka kwa mahasimu, lakini akawatia moyo kuwa, kwa nguvu ya Mungu watayashinda.

Misa ya kumbukumbu ya Mzee Luangisa


Mchungaji Butiku akiongoza misa ya shukurani na arubaini ya marehemu Mzee Samuel Luangisa iliyofanyika siku ya Jumamosi Aug 8, 2015 Mount Vernon, New York na kuhudhuriwa na ndugu, jamaa na marafiki kutoka kila pembe ya Marekani.


Mrs Luangisa, mke wa marehemu akifuatilia misa.


Wanafamilia wakifuatilia misa.


Wajukuu wa marehemu wakifanya onesho la kumenzi babu yao.


Mtoto wa marehemu Mao Luangisa akitoa salamu za shukurani.


Mwenyekiti wa Jumuiya ya Watanzania New York Hajji Khamis akiongea machache huku akisisitiza upendo na mshikmano kwenye Jumuiya za Watanzania hususani zile zilizopo nje ya Tanzania kwani kwa kufanya hivyo Jumuiya zitakua imara.


Mchungaji Butiku akiongoza misa.


Wakati wa maakuli.

Kwa picha zaidi bofya HAPA

Lowasa ahudhuria Mkutano wa Baraza Kuu la CUF

Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wa UKAWA kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Mh. Edward Lowassa akiwapungua Wanachama na Wafuasi wa Vyama UKAWA waliofurika kwenye Makao Makuu ya CUF.
ALIYEKUWA Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Prof. Ibrahimu Lipumba amepotea kwenye uwanja wa siasa.

Hali hiyo imejitokeza leo asubuhi wakati mgombea urais kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Edward Lowassa alipotembelea Ofisi Kuu ya CUF Bunguruni, Dar es Salaam kwa mara ya kwanza.

Katika Uchaguzi Mkuu Oktoba 25 mwaka huu, Lowassa anawakilisha vyama vinne vinavyounda UKAWA ambavyo ni Chadema yenyewe, CUF, NCCR-Mageuzi pamoja na NLD.

Lowassa alifika kwenye ofisi za CUF saa 12.40 mchana lengo likiwa ni kuzungumza na viongozi wa chama hicho akiwa ni mwakilishi wao kupitia UKAWA.

Katika Safari hiyo walikuwepo pia wenyeviti wenza wa UKAWA -Freeman Mbowe (Chadema), James Mbatia (NCCR- Mageuzi) na Emanuel Makaidi (NLD).

Viongozi wengine ni Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif; Naibu Katibu Mkuu wa CUF, Magdalena Sakaya; Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu; Naibu Katibu Mkuu Chadema Zanzibar, Salum Mwalimu na wabunge wanaotoka vyama vinavyounda UKAWA.

Tofauti na ilivyotarajiwa kwamba, kujiuzuru kwa Prof. Lipumba kungesababisha mpasuko ndani ya CUF, badala yake maelfu ya wanachama wa CUF walifurika katika ofisi za chama hicho mapema leo kuanzia saa tatu asubuhi.

Hakukuwa na vikundi vya watu katika majadiliano kuashiria kujadili kuhusu kuondoka kwa Prof. Lipumba, badala yake nyimbo za kumsifu Lowassa na Ukawa zilitawala.

Baada ya Lowassa kukaribishwa na mwenyeji wake Maalim Seif, alisema, “…kwanza nawapa pole kwa Lipumba kuondoka,” kauli hiyo iliyopokelewa na maelfu ya wanachama wa CUF waliofurika katika ofisi hizo kwa kusema “Hatumtakiii…..Lipumba aende zake.”

Lowassa aliendelea “nilikuwa sijamaliza kusema. Nawapongeza kwa uvumivu wenu na umoja wenu katika kipindi hiki baada ya kuondoka Lipumba.

“Nimepata faraja sana kujiunga na Ukawa japo kumekuwa na misukosuko ndani ya UKAWA. Ni lazima tuwe wamoja, mtunze kadi zenu za kupigia kura. Mwaka huu lazima tushinde tena kwa kura asilimia 90 ili wakiiba asilimia 10 tusisikie,” amesema Lowassa.

Hata hivyo Maalim Seif amesema, “tumepata faraja kubwa sana kutembelewa na Lowassa. Hii ni kuthibitisha UKAWA bado tupo pamoja. Hakuna kurudi nyuma, mbele kwa mbele mpaka Lowassa aingie Ikulu. Zanzibar tupo tayari Maalim Seif ndiye rais. Tunasubili aapishwe.”

Kwa upande wake Duni amesema, wagombea wa UKAWA hawapo kwa nia ya kusaka madaraka peke yake kama ambavyo inaelezwa bali kuhakikisha CCM inaondoka madarakani na kila Mtanzania anapata haki sawa katika kunufaika na rasilimali za nchi yake.

“Kama mnavyojua, nilikuwa waziri serikalini. Juzi nimeamua kuachia madaraka baada ya kushauriana na viongozi wangu wa CUF ili nijiunge na Chadema kuhakikisha CCM inaondoka madarakani. Tayari nimeandika barua kwa rais ya kuachia madaraka. Na juzi tu nimetoka kumuaga rasmi,” amesema Duni huku akishangiliwa na ummati.

Hata hivyo, katika mkutano huo Mbowe amewaambiwa wananchi na wafuasi wa UKAWA kuwa, “hii safari ya mabadiliko tumeipigania kwa miaka 25. Wapo waliopoteza maisha, kuachika, kufilisiwa, vilema na wenye kesi katika safari hii. Imekuwa ngumu. Akitoka kiongozi kati yetu akaona malengo yetu hayaendani nae. Huyo hatufai.

“Leo tuna wagombea waliojiunga na Chadema hivi karibuni na wanagombea urais na umakamu. Chadema hatugombei vyeo. Tupo tayari kufanya kazi na wenzetu bila kujali wamejiunga lini na chama.”

Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu kwenye mkutano huo amewatoa hofu wananchi kuhusu uvumi unaoenezwa kwenye mitandao kwamba “mgombea urais na mgombea mwenza wake ni lazima wawe wanachama kupitia vyama wanavyogombea kwa muda wa miezi mitatu.”

“Katiba zote mbili za Tanzania na Zanzibar ninazo hapa. Hakuna Katiba wala Sheria inayosema mgombea wa urais na makamo wake ni lazima watimize muda wa miezi mitatu tangu kujiunga na chama wanachokiwakilisha katika uchaguzi huu. Huu ni uzushi.”

Lissu amesema, masharti yanayotolewa na katiba hizo ni kwamba, mgombea wa urais na makamu wake ni lazima wateuliwe na chama cha siasa chenye usajili wa kudumu.

Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wa UKAWA kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Mh. Edward Lowassa akikumbatiana na Mgombea Urais wa Zanzibar wa UKAWA kupitia Chama cha Wananchi CUF, Maalim Seif Sharif Hamad, kabla ya kuelekea kwenye Makao Makuu Chama cha Wananchi CUF, Buguruni jijini Dar es salaam leo August 9, 2015, kulikofanyika Mkutano wa Baraza Kuu la Chama cha Wananchi CUF. CHANZO OTHMAN MICHUZI


Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wa UKAWA kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Mh. Edward Lowassa na Mgombea Urais wa Zanzibar wa UKAWA kupitia Chama cha Wananchi CUF, Maalim Seif Sharif Hamad na Wenyeviti wenza wa UKAWA, Mh. James Mbatia na Dkt. Emmanuel Makaidi wakitembelea kuelekea Makao Makuu Chama cha Wananchi CUF, Buguruni jijini Dar es salaam leo August 9, 2015, kulikofanyika Mkutano wa Baraza Kuu la Chama cha Wananchi CUF.Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wa UKAWA kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Mh. Edward Lowassa na Mgombea Urais wa Zanzibar wa UKAWA kupitia Chama cha Wananchi CUF, Maalim Seif Sharif Hamad, wakiwapungia wafuasi wa Vyama vinavyounda UKAWA wakati wakielekea kwenye Makao Makuu Chama cha Wananchi CUF, Buguruni jijini Dar es salaam leo August 9, 2015, kulikofanyika Mkutano wa Baraza Kuu la Chama cha Wananchi CUF. Wengine walioambatana nao ni Wenyeviti wenza wa UKAWA, Mh. James Mbatia na Dkt. Emmanuel Makaidi.


Sehemu ya Wafuasi na Wanachama wa Chama cha Wananchi CUF, wakiwa wamejipanga Barabarani tayari kwa kumlaki, Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wa UKAWA kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Mh. Edward Lowassa, alipokuwa akielekea Makao Makuu Chama cha Wananchi CUF, Buguruni jijini Dar es salaam leo August 9, 2015, kulikofanyika Mkutano wa Baraza Kuu la Chama cha Wananchi CUF. 
Wanachama wa Chama cha Wananchi CUF wakifurahia Ugeni huo.


Sehemu ya Viongozi wakuu wanaounda UKAWA, wakiongozwa na Mgombea Urais wa Zanzibar wa UKAWA kupitia Chama cha Wananchi CUF, Maalim Seif Sharif Hamad, Mwenyekiti wa Chama cha NCCR - Mageuzi, Mh. James Mbatia, Mwenyekiti wa Chama cha NLD, Dkt. Emmanuel Makaidi, wakimsuburia Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wa UKAWA kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Mh. Edward Lowassa.


Umati wa Watu ukiwapokea Viongozi wao.


Umati nje ya Makao Makuu ya CUF.


Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wa UKAWA kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Mh. Edward Lowassa akiwapungia mkono wafuasi wa Vyama vinavyounda UKAWA wakati wakielekea kwenye Makao Makuu Chama cha Wananchi CUF, Buguruni jijini Dar es salaam leo August 9, 2015, kulikofanyika Mkutano wa Baraza Kuu la Chama cha Wananchi CUF.
Mgombea Mwenza wa Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wa UKAWA kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dkt. Juma Haji Duni akiwasili kwenye Makao Mkuu ya CUF.


Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wa UKAWA kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Mh. Edward Lowassa akisalimiana na Mgombea Mwenza wake, Dkt. Juma Haji Duni.

Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi CUF na Mgombea Urais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad akiwahutumbia maelfu ya wanachama na wafuasi wa Vyama vinavyounda UKAWA, nje ya jengo la Makao Makuu Chama cha Wananchi CUF, Buguruni jijini Dar es salaam leo August 9, 2015, kabla ya kufanyika Mkutano wa Baraza Kuu la Chama cha Wananchi CUF.

Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Mh. Freeman Mbowe akiwahutumbia maelfu ya wanachama na wafuasi wa Vyama vinavyounda UKAWA, nje ya jengo la Makao Makuu Chama cha Wananchi CUF, Buguruni jijini Dar es salaam leo August 9, 2015, kabla ya kufanyika Mkutano wa Baraza Kuu la Chama cha Wananchi CUF.


Mwenyekiti wa Chama cha NCCR - Mageuzi,Mh. James Mbatia akiwahutumbia maelfu ya wanachama na wafuasi wa Vyama vinavyounda UKAWA, nje ya jengo la Makao Makuu Chama cha Wananchi CUF, Buguruni jijini Dar es salaam leo August 9, 2015, kabla ya kufanyika Mkutano wa Baraza Kuu la Chama cha Wananchi CUF.

Mgombea Mwenza wa Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wa UKAWA kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dkt. Juma Haji Duni akiwahutumbia maelfu ya wanachama na wafuasi wa Vyama vinavyounda UKAWA, nje ya jengo la Makao Makuu Chama cha Wananchi CUF, Buguruni jijini Dar es salaam leo August 9, 2015, kabla ya kufanyika Mkutano wa Baraza Kuu la Chama cha Wananchi CUF.


Mwanasheria wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Mh. Tundu Lissu akiwahutumbia maelfu ya wanachama na wafuasi wa Vyama vinavyounda UKAWA, nje ya jengo la Makao Makuu Chama cha Wananchi CUF, Buguruni jijini Dar es salaam leo August 9, 2015, kabla ya kufanyika Mkutano wa Baraza Kuu la Chama cha Wananchi CUF.
Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wa UKAWA kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Mh. Edward Lowassa akiwahutumbia maelfu ya wanachama na wafuasi wa Vyama vinavyounda UKAWA, nje ya jengo la Makao Makuu Chama cha Wananchi CUF, Buguruni jijini Dar es salaam leo August 9, 2015, kabla ya kufanyika Mkutano wa Baraza Kuu la Chama cha Wananchi CUF.


Mwenyekiti wa Chama cha NLD, Dkt. Emmanuel Makaidi akimpongeza Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wa UKAWA kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Mh. Edward Lowassa mara baada ya kuhutubia.


Wakielekea kwenye Mkutano wa Baraza Kuu la Chama cha Wananchi CUF.


Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi CUF na Mgombea Urais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad, akiwa pamoja na Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Mh. Freeman Mbowe, Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wa UKAWA kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Mh. Edward Lowassa, Mgombea Mwenza wa Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wa UKAWA kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dkt. Juma Haji Duni pamoja na Naibu Katibu Mkuu wa CUF, Mh. Magdalena Sakaya wakati wa Mkutano wa Baraza Kuu la Chama hicho, uliofanyika August 9, 2015, kwenye Makao Makuu Chama cha Wananchi CUF, Buguruni jijini Dar es Salaam.


Sehemu ya Wajumbe wa Mkutano wa Baraza Kuu la Chama cha Wananchi CUF.

  • Tumeshirikishwa picha, taarifa hii na Othman Michuzi