Katuni tulizozipata Agosti 12, 2015


Maadhimisho ya Siku ya Vijana, Mnazi Mmoja, Dar


Maandamano yakiongozwa na bendi ya jeshi la polisi
Baadhi ya vijana kutoka shule mbalimbali wakiandamana kuingia katika viwanja vya mnazi mmoja wakati wa maadhimisho ya siku ya kimataifa ya vijana duniani iliyoadhimishw jijini Dar es Salaam. Mashirika mbalimbali ya mataifa yanayofanya shughuli za vijana ni kamaUNFPA, IYF, UNIC, ILO, RESTLESS DEVELOPMENT, YUNA, AMREF, MARIE STOPES, pamoja na PSI.(Picha zote na Geofrey Adroph)

Mgeni rasmi Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Prof. Elisante Ole Gabriel (wa tatu kutoka kushoto) pamoja na viongozi wengine wakipokea maandamano ya vijana wakati wa maadhimisho ya siku ya kimataifa ya vijana duniani iliyoadhimishwa katika Viwanja vya Mnazi Mmoja leo jijini Dar es Salaam. Wa kwanza kushoto ni Mkurugenzi Maendeleo ya Vijana Bw. James Kajugusi na wapili kushoto ni Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia idadi ya watu duniani (UNFPA) Bibi. Natalia Kanem.

Mgeni rasmi Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Prof. Elisante Ole Gabriel pamoja viongozi wengine wakipokea maandamano ya vijana wakati wa maadhimisho ya siku ya kimataifa ya vijana duniani iliyoadhimishwa katika Viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam.Viongozi katika meza kuu wakiimba wimbo wa Taifa wakati wa maadhimisho ya siku ya kimataifa ya vijana duniani iliyoadhimishwa katika Viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam.Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia idadi ya watu duniani (UNFPA) Bi. Natalia Kanem akizungumza na vijana wakati wa Maadhimisho ya siku ya kimataifa ya vijana duniani katika Viwanja vya Mnazi Mmoja. Katika hotuba yake aliweza kuzungumzia maswala ya watoto wa kike kubeba mimba wakiwa na umri mdogo ambao unapelekea kuacha masomo kutokana na ujauzito huo pia aliwasisitiza vijana kuwa na umoja kwani ndio nguvu kazi ya Taifa.Mwendeshaji wa Sherehe hiyo Bi. Usia Nkhoma ambaye ni Afisa Habari wa Kituo cha Habari cha Umoja wa Mataifa (UNIC) akizungumza jambo na vijana walioshiriki maadhimisho ya siku ya kimataifa ya vijana duniani katika Viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam.Mkurugenzi Maendeleo ya Vijana kutoka Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Bw. James Kajugusi(wa nne kutoka kulia) akimkaribisha mgeni rasmi kuzungumza na vijana wakati wa maadhimisho ya siku ya kimataifa ya vijana duniani katika Viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam.Wa tatu kutoka Kulia ni Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Prof. Elisante Ole Gabriel, Wa kwanza kulia ni Msaidizi wa Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia idadi ya watu duniani (UNFPA) nchini Tanzania Bi. Hashina Begum na wa pili kutoka kulia ni Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia idadi ya watu duniani (UNFPA) Bi. Natalia Kanem.Naibu Katibu Mkuu kutoka Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Prof. Elisante Ole Gabriel (kushoto) akitoa shukrani kwa wawakilishi wa Umoja wa Mataifa katika maadhimisho ya siku ya kimataifa ya vijana duniani yaliyofanyika katika Viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam. Wa kwanza kulia ni Msaidizi wa Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia idadi ya watu duniani (UNFPA) nchini Tanzania Bi. Hashina Begum na wa pili kutoka kulia ni Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia idadi ya watu duniani (UNFPA) Bi. Natalia Kanem.Naibu Katibu Mkuu kutoka Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Prof. Elisante Ole Gabriel akiwahutubia vijana walioshiriki maadhimisho ya siku ya kimataifa ya vijana duniani leo katika Viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam. Katika hotuba yake aliwasisitiza vijana kujitokeza katika uchaguzi unaotegemea kufanyoka mwezi wa kumi mwaka huu ili kuchagua viongozi makini watakaoweza kutetea masuala ya vijana na pia aliwasisitiza vijana kufanya kazi za kujitolea.Msaidizi wa Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia idadi ya watu duniani (UNFPA) nchini Tanzania Bi. Hashina Begum akiwasalimia vijana walioshiriki maadhimisho ya siku ya kimataifa ya vijana duniani katika Viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam.Bw. Hesein Melele(wa kwanza kuli) kijana ambaye ni mwakilishi wa asasi ya vijana chini ya umoja wa mataifa (YUNA) akiwasilisha maazimio yaliyofikiwa na vijana wakati wa kongamano lililofanyika Agosti 10 mwaka huu kujadili ujumbe wa siku ya kimataifa ya vijana duniani na kuandaa maazimio yaliyowasilishwa kwa mgeni rasmi leo katika Viwanja vya Mnazi Mmoja walipokua wakiadhimisha siku ya kimataifa ya vijana duniani.Mwanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Jangwani, Tatu Ahmed akitoa shukrani kwa wageni waalikwa waliofika katika Viwanja vya Mnazi Mmoja walipokua wakiadhimisha siku ya kimataifa ya vijana duniani.
Mratibu wa Mkoa wa Dar es Salaam kutoka asasi ya vijana chini ya umoja wa mataifa (YUNA), Rahim Nasser akiwatolea ufafanuzi vijana waliofika kwenye banda la Umoja wa Mataifa katika maadhimisho ya siku ya kimataifa ya vijana duniani Viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam.Mgeni rasmi Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Prof. Elisante Ole Gabriel akimsikiliza kwa makini Mratibu wa Mkoa wa Dar es Salaam kutoka asasi ya vijana chini ya umoja wa mataifa (YUNA), Rahim Nasser alipotembelea kwenye banda la Umoja wa MataifaMkufunzi wa Ujasiriamali/Biashara wa Program ya anzisha na imarisha biashara yako (SIYB) iliyochini ya Shirika la Kazi Duniani (ILO), Bw. MacDonald Lanzi (wa pili kutoka kulia) akimfafanulia jambo Mgeni rasmi Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Prof. Elisante Ole Gabriel. Wa pili kushoto ni Msaidizi wa Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia idadi ya watu duniani (UNFPA) nchini Tanzania Bi. Hashina Begum na wa kwanza kutoka kulia ni Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia idadi ya watu duniani (UNFPA) Bi. Natalia Kanem.Mshauri na Mkufunzi wa Ujasiriamali/Biashara wa Program ya anzisha na imarisha biashara yako (SIYB) iliyochini ya Shirika la Kazi Duniani (ILO), Bw. Lawrence Ambokile(mwenye koti jeusi) akitoa ufafanuzi kwa Mgeni rasmi Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Prof. Elisante Ole Gabriel alipotembelea banda iloMgeni rasmi Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Prof. Elisante Ole Gabriel akisaini kitabu katika kwenye moja ya bada la PSI Tanzania katika Viwanja vya Mnazi Mmoja walipokua wakiadhimisha siku ya kimataifa ya vijana duniani. kushoto ni Dkt. Benedict NyiroMwakilishi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia idadi ya watu duniani (UNFPA) Bi. Natalia Kanem akisaini kitabu katika kwenye moja ya bada la PSI Tanzania katika Viwanja vya Mnazi Mmoja walipokua wakiadhimisha siku ya kimataifa ya vijana duniani. kushoto ni Dkt. Benedict NyiroMsaidizi wa Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia idadi ya watu duniani (UNFPA) nchini Tanzania Bi. Hashina Begum akisaini kitabu katika kwenye moja ya bada la PSI Tanzania katika Viwanja vya Mnazi Mmoja walipokua wakiadhimisha siku ya kimataifa ya vijana duniani. kushoto ni Dkt. Benedict NyiroOfisa Habari wa Kituo cha Taarifa cha Umoja wa Mataifa Tanzania (UNIC), Stella Vuzo(wa kwanza kushoto), Meneja mradi wa ICS Bi. Imisa Masinjila(wa pili kutoka kushoto), Mkurugenzi wa Utamaduni kutoka Wizara hiyo Prof. Hermas Mwansoko(wapili kutoka kulia) pamoja na Imisa Masinjila wakizungumza jambo maadhimisho ya siku ya kimataifa ya vijana duniani katika Viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam.Msaidizi wa Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia idadi ya watu duniani (UNFPA) nchini Tanzania Bi. Hashina Begum(wa kwanza kushoto) pamoja na Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia idadi ya watu duniani (UNFPA) Bi. Natalia Kanem(katikati) wakizungumza jambo na Mkurugenzi Maendeleo ya Vijana kutoka Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Bw. James Kajugusi wakati wa maadhimisho ya siku ya kimataifa ya vijana duniani katika Viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam.Msaidizi wa Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia idadi ya watu duniani (UNFPA) nchini Tanzania Bi. Hashina Begum pamoja na Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia idadi ya watu duniani (UNFPA) Bi. Natalia Kanem wakiwa kwenye picha ya pamoja na baadhi ya vijana waliofika kwenye maadhimisho ya siku ya kimataifa ya vijana duniani katika Viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam.Bw. Hesein Melele(katikati) kijana ambaye ni mwanachama wa asasi ya vijana chini ya umoja wa mataifa (YUNA) akiwa kwenye picha ya pamoja na vijana wenzake ambao ni Rehema Pascal(kushoto) pamoja na Felister

Vijana kutoka vikundi mbalimbali wakitoa burudani wakati wa maadhimisho ya siku ya kimataifa ya vijana duniani katika Viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam.

Vijana wakifuatilia kwa makini matukio mbalimbali yaliyokua yakiendelea wakati wa maadhimisho ya siku ya kimataifa ya vijana duniani katika Viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam.
 • Tumeshirikishwa picha,taarifa hii na Geofrey Adrop / Pamoja Pure blog

Mbunge wa Sikonge ahamia CHADEMA


CUF: Orodha ya walioteuliwa kugombea uwakilishi

WAGOMBEA WA CUF WA UWAKILISHI WALIOTEULIWA NA BARAZA KUU LA UONGOZI TAIFA

WILAYA YA MJINI

Amani
Khamis Rashid Abeid

Chumbuni
Maulid Suleiman Juma

Jang’ombe
Ali Haji Mwadini

Kikwajuni
Mohd Khalfan Sultan

Kwahani
Hassan Juma Hassan

Shaurimoyo
Amina Rashid Salum

Magomeni
Yussuf Idrissa Mudu

Malindi
Ismail Jussa Ladhu

Mpendae
Ali Hamad Ali

WILAYA YA MAGHARIBI ‘A’

Bububu
Yussuf Omar Muhine

Mfenesini
Saleh Khamis Omar

Mtoni
Rashid Soud Khamis

Mto Pepo
Nassor Ahmed Nassor

Mwera
Salim Sleyum Abeid

Welezo
Salim Mussa Haji

WILAYA YA MAGHARIBI 'B'

Chukwani
Mansour Yussuf Himid

Dimani
Moh’d Hashim Ismail

Fuoni
Said Salim Said

K/Samaki
Moh'd Nassor Moh'd

Kijito Upele
Ussi Juma Hassan

M/Kwerekwe
Abdillah Jihad Hassan

Pangawe
Suleiman Simai Pandu

WILAYA YA KASKAZINI ‘A’
Chaani
Dunia Haji Pandu

Kijini
Haji Mwadini Makame

Mkwajuni
Haji Kessi Haji

Nungwi
Hassan Jani Massoud

Tumbatu
Makame Haji Makame

WILAYA KASKAZINI ‘B’

Bumbwini
Zahran Juma Mshamba

Donge
Salum Khamis Malik

Kiwengwa
Hassan Khatib Kheir

Mahonda
Mwinshaha Shehe Abdalla

WILAYA YA KATI
Chwaka
Arafa Shauri Mjaka

Tunguu
Khamis Malik Khamis

Uzini
Asha Simai Issa

WILAYA YA KUSINI

Makunduchi
Simai Ameir Haji

Paje
Asha Abdu Haji

WILAYA YA MICHEWENI

Konde
Issa Said Juma

Micheweni
Subeti Khamis Faki

Tumbe
Mmanga Moh'd Hemed

Wingwi
Rufai Said Rufai

WILAYA YA WETE

Gando
Said Ali Mbarouk

Kojani
Hassan Hamad Omar

Mtambwe
Habib Ali Mohd

Mgogoni
Abubakar Khamis Bakar

Wete
Iss-haka Ismail Shariff

WILAYA YA CHAKE CHAKE

Chake Chake
Omar Ali Shehe

Chonga
Khamis Rashid Khamis

Ole
Hamad Massoud Hamad

Wawi
Khalifa Abdalla Ali

Ziwani
Moh'd Ali Salim

WILAYA YA MKOANI

Chambani
Moh’d Mbwana Hamad

Kiwani
Hija Hassan Hija

Mkoani
Seif Khamis Moh’d

Mtambile
Abdalla Bakar Hassan

Taarifa ya TANESCO kuhusu makubwa iliyoyafanya


TANESCO YAFANYA MAKUBWA KUBORESHA SEKTA YA UMEME NCHINI

1.Kuongeza Uzalishaji Umeme

Kwa kuzingatia ukuaji wa sekta ndogo ya umeme hapa nchini na mahitaji makubwa ya umeme yanayoongezeka kwa kasi, Serikali iliweka mikakati mahsusi kuongeza uzalishaji wa umeme hadi kufikia MW 2,780 Mwaka 2015/16. Katika kipindi cha 2005 – 2015, Serikali ya Awamu ya Nne ilifanikiwa kuongeza uwezo wa mitambo ya kuzalisha umemekatika Gridi ya Taifa kutoka MW 891 zilizokuwepo mwaka 2005 hadi kufikia MW 1,501.24 mwaka 2014 sawa na ongezeko la asilimia 68.5. Mpaka kufikia Julai, 2015 uwezo wa mitambo ya kuzalisha umeme katika Grid ya Taifa ulipungua na kufikia MW 1,246.24 kutokana na kukoma kwa baadhi ya mikataba ya wazalishaji binafsi ambao wamekuwa mzigo kwa Shirika kutokana na gharama kubwa. Kuongezeka kwa uwezo wa mitambo ya kuzalisha umeme katika Gridi ya Taifa kwa kipindi cha Awamu ya Nne kutokana na utekelezaji wa mipango na miradi mbalimbali ya kuzalisha umeme. Juhudi zilizochangia mafanikio hayo ni pamoja na:

(i) Kukamilika kwa Mtambo wa kuzalisha umeme MW 100 – Ubungo I: Mtambo huo upo katika eneo la TANESCO-Ubungo Dar es Salaam. Mtambo huu una uwezo wa kufua umeme wa MW 100 kwa kutumia gesi asilia na ulifunguliwa rasmi na Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania MweziNovemba, 2008.

(ii) Kukamilika kwa Ujenzi wa Mtambo wa Kufua Umeme, MW 45 – Tegeta: Ujenzi wa mtambo huo unaotumia gesi asilia una uwezo wa kufua umeme wa MW 45 ulikamilika na kuanza kufua umeme Mwezi Desemba, 2009.

(iii) Kukamilika kwa Ujenzi wa Mtambo wa Kufua Umeme, MW 105 – Ubungo II: Mtambo huu unatumia gesi asilia kufua umeme wa MW 105, upo katika eneo la TANESCO – Ubungo Jijini Dar es Salaam na ulizinduliwa rasmi na aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini Mh. Prof. Sospeter M. Muhongo Mwezi June, 2012.

(iv) Kukamilika kwa Mtambo wa kuzalisha umeme MW 60 – Mwanza: Ujenzi wa mtambo huo umekamilika na ulizinduliwa rasmi na Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tarehe 06 Septemba, 2013. Mtambo huu umesaidia kuboresha upatikanaji wa umeme na kuimarisha gridi ya Taifa katika mikoa ya Kanda ya Ziwa.

(v)Kukamilika kwa Mradi wa Umeme wa Somanga Fungu, MW 7.5: Mitambo ya kufua umeme wa MW 7.5 kwa kutumia gesi asilia iliyopo Somanga Fungu mkoani Lindi ilizinduliwa na Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mwezi Agosti, 2010. Mitambo hiyo inafua umeme unaosambazwa katika miji ya Bungu, Kibiti, Kilwa Kivinje, Kilwa Masoko, Kindwitwi, Muhoro, Nangurukuru, Somanga, Tingi, Utete, Nyamwange, maeneo ya Njia Nne na Hospitali ya Mchukwi.

(vi) Mchango wa Wazalishaji Wadogo wa Umeme katika Gridi ya Taifa: Katika kipindi cha 2005 hadi 2015, wazalishaji wadogo wa umeme waliingia mikataba ya kuuziana umeme na TANESCO ambapo umeme wa MW 8 ununuliwa. Wazalishaji hao ni ni TANWAT – MW 1; TPC – MW 3; na Mwenga Mini Hydro – MW 4.

(vii) Kuboresha Huduma ya Umeme Katika Maeneo yaliyopo Nje ya Gridi ya Taifa: Katika kipindi cha 2005 hadi 2015, utekelezaji wa mipango mbalimbali ya ukarabati na ufungaji wa mitambo mipya ya kufua umeme kwa kutumia mafuta katika maeneo ambayo bado hayajaunganishwa katika gridi ya Taifa imefanyika. Ukarabati wa mitambo ya kufua umeme kwa kutumia mafuta ulifanyika kwenye vituo vya Mpanda, Kigoma, Masasi, Mafia, Songea, Tunduru, Ngara na Biharamulo. Aidha, Serikali kupitia TANESCO ilinunua mitambo mipya 19 ya kufua umeme kwa kutumia dizeli iliyofungwa katika vituo vya Kasulu (1.25 x 2), Kibondo (1.25 x 2), Kigoma (1.25 x 5), Loliondo (1.25 x 4), Namtumbo (0.32 x 1), Songea (1.9 x 1) na Sumbawanga (1.25 x 4). Mitambo hiyo mipya iligharimuEURO milioni 35.94 sawa na Shilingi bilioni 57.5. Pia kuna wazalishaji binafsi waliowekeza katika maeneo yaliyopo nje ya gridi ambao ni Ngombeni – MW 1.4 na Andoya Hydro MW 0.5.

(viii) Kukamilika kwa Mradi wa Mawengi wenye Uwezo wa Kuzalisha kW 300 kwa Kutumia Maporomoko Madogo yaMaji: Mradi huo uliopo Wilayani Ludewa ulizinduliwa na Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mwezi Novemba, 2011, ambapo hadi kufikia Mwezi Octoba, 2014 zaidi ya kaya 1,153 zilikuwa zimeunganishiwa umeme.

Kukamilika kwa miradi hiyo kumewezesha upatikanaji wa umeme wa uhakika nchini na kufanikisha kuondoa mgawo wa umeme hususan kuanzia Mwaka 2012 na hivyo kuboresha ufanisi wa utekelezaji wa shughuli mbalimbali za kiuchumi na kijamii.

Pamoja na kukamilika kwa miradi hiyo, pia kumekuwepo na mikakati mbalimbali ya kuongeza uzalishazi wa umeme kwenye Gridi ya Taifa na je ya Gridi ya Taifa kama ifuatavyo;

(i) Utekelezaji wa Mradi wa Kinyerezi I – MW 150 kwa Kutumia Gesi Asilia: Serikali imefanya juhudi kupunguza utegemezi wa mitambo ya kufua umeme kwa kutumia mafuta ambayo ni ghali. Hatua zilizochukuliwa ni pamoja na kuamua kwa dhati na kwa kutumia fedha za Watanzania kutekeleza mradi wa Kinyerezi - I (MW 150). Mradi huo unaojumuisha ujenzi wa njia za umeme za msongo wa kV 220 (Kinyerezi - Kimara) na kV 132 (Kinyerezi - Gongolamboto) utatumia gesi asilia na utagharimu Dola za Marekani milioni 183.30, sawa na Shilingi bilioni 293.28. Utekelezaji wa Mradi huo ulianza Mwezi Januari, 2013 na unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa Mwezi Agosti, 2015.

(ii) Mradi wa kupeleka umeme miji ya Mpanda, Ngara na Biharamulo (ORIO): Mradi huu unajumuisha ufungaji wa jenereta mbili (2) zenye uwezo wa MW 1.25 katika kila mji, ukarabati wa njia za umeme zilizoharibika na ujenzi w njia mpya za umeme. Awamu ya kwanza ya mradi (development) ilianza September, 2010; na wamu ya pili ya mradi ambayo ni Utelelezaji, Uendeshaji na Matengenezo (Implementation and Operation & Maintenance Phase) ilianza Septemba, 2012. Hadi sasa mchakato mzima wa tenda kwa ajili ya kuwapata wakandarasi kwa ajili ya utelezaji wa mradi huu umekamilika na kazi ya utekelezaji ilianza mwezi Oktoba, 2013. Pia kumekuwa na mafunzo kwa ajili ya wajasiriamali wadogo na wa kati pamoja na mafunzo ya uongozi wa miradi.

(iii) Mradi wa Kufua Umeme Rusumo na Njia ya Kusafirisha Umeme: Mradi huu unahusisha ujenzi wa kituo cha kufua umeme wa MW 80 kwa kutumia maji. Mpaka sasa uchambuzi yakinifu umekamirika, Ripoti ya mazingira kwa upande wa usambazaji kutoka BENACO mpaka mpakani Rusumo tayari imekamirika na kibari cha kuendeleza mradi kinasubiriwa kutoka NEMC. Mchakato wa kupata njia ardhi kwa ajili ya njia ya usafirishia umeme toka Rusumo mpaka Nyakanazi ya kV 220 tayari umeanza.

(iv) Mradi wa Kufua Umeme Kakono Hydro MW 87: Mradi huu unahusisha ujenzi wa kituo cha kufua umeme wa MW 87 kwa kutumia maji. Mpaka sasa uchambuzi yakinifu umekamilika, Ripoti ya mazingira ya kituo cha kuzalisha umeme na njia ya kusafirisha umeme toka Kakono hadi Kyaka ipo tayari na imewasilishwa NEMC Mwezi Mei, 2015 kwa ajili ya kupata kibali ya kuendeleza mradi. Gharama ya mradi inakadiriwa kuwa Dola za Kimarekani Milioni 379.4 na unatarajiwa kukamilika 2019.

1. Kujenga na Kuimarisha Njia za Usafirishaji na Usambazaji Umeme

Katika kipindi cha kuanzia 2005 – 2015, juhudi kubwa zimefanyika kuimarisha njia za usafirishaji na usambazaji wa umeme ili kuwezesha nishati hiyo kuwafikia watumiaji kwa ubora na kwa wakati wote na kuweza kukidhi ongezeko la mahitaji ya umeme nchini. TANESCO imefanya ukarabati na kujenga miundombinu ya usafirishaji na usambazaji umeme. Ukarabati huu umefanyika na unaendelea kufanyika katika mikoa mbalimbali inayopata umeme kupitia Gridi ya Taifa. Kazi hii inafanyika kwa fedha za ndani na kwa ufadhili kutoka wahisani mbalimbali wakiwemo Benki ya Dunia, Benki ya Maendeleo ya Afrika, Shirika la Marekani linalotoa misaada kwa nchi maskini (MCC), Korea Kusini na JICA. Miradi hiyo ni pamoja na ifuatayo;

(i) Kukamilika kwa Mradi wa Kuboresha Kituo cha Taifa cha Kusimamia Mfumo wa Umeme wa Gridi (National Grid Control Cetre): Mradi huu ulianza mwaka 2009 na kukamilika mwaka 2012. Mradi huu ulihusisha ubadilishaji wa mfumo wa zamani SCADA na ufungwaji wa mfumo mpya wa SCADA/EMS. Mradi pia ulihusisha ununuzi, ufungwaji na majaribio ya ‘National Grid Control Center (GCC) – Ubungo, DSM na ufungwaji wa vifaa vingine viambatanavyo na mfumo huo katika nchi nzima. Gharama za Mradi huo ni Euro milioni 3.04 na Dola za Marekani 622,394 sawa na jumla ya Shilingi bilioni 7.4.

(ii) Mradi wa kuboresha mifumo na upatikanaji wa umeme katika Jiji la Dar es Salaam (TEDAP na Finish Project):Mradi wa TEDAP unahusisha ujenzi wa njia msongo wa 132kV ya kilomita 7 kutoka Ubungo – Makumbusho na kituo cha kupoozea umeme cha Makumbusho cha 132/33kV chenye uwezo wa 2 X 45MVA. Mradi huu umekamilika na kuondoa tatizo la umeme mdogo “Low Voltage” na kukatika katika katika maeneo ya Wilaya ya Kinondoni. Pia ulihusisha ujenzi wa vituo vipya vya kupoozea umeme maeneo ya katikati ya jiji, Kipawa, Mburahati, Mikocheni na Oysterbay, ukarabati wa vituo vya kupoozea umeme maeneo ya Chang’ombe, Kariakoo, Kurasini, Mbagala, Ubungo na ujenzi wa njia za umeme za kilomita 51.7 za msongo wa kilovolti 132 na kilomita 83 za msongo wa 0.4kV unaotegemewa kukamika ifikapo Mwezi Disemba, 2015.

Mradi wa Finish umehusisha kujenga njia ya usafirishaji umeme chini ya ardhi ya 132kV kutoka Ilala hadi City Centre Kujenga kituo cha kupoozea umeme cha 132/33/11kV chenye uwezo wa 2x45MVA, ujenzi wa njia ya umeme chini ya ardhi kwa ajili ya kuunga kituo cha Kariakoo – Railway – Sokoine na kituo cha zamani cha City Centre, kuanzisha kituo cha kuongozea mifumo ya usambazaji umeme katika msongo wa kV 33 na kV 11 (distribution SCADA). Mradi huu ulishaanza na unategemewa kukamilika ifikapo Mwezi Septemba, 2015.

(iii)Ujenzi wa Njia Mpya ya Kupeleka Umeme Zanzibar ya Msongo wa kV 132 na Kupeleka Umeme Pemba kutoka Tanga ya msongo wa kV 33: Mradi wa kupeleka umeme Zanzibar ulizinduliwa rasmi tarehe 10 Aprili 2013 na umeboresha usafirishaji umeme wa uhakika katika visiwa vya Zanzibar. Mradi ulihusisha ujenzi wa waya wa majini (Submarine cable) wa njia ya kilomita 39 ambao ulimalizika mwanzoni mwa mwezi Machi 2013. Pia waya wa juu (Overhead line) wa njia ya kilomita 37 ambao ulimalizika mwishoni mwa mwezi February 2013. Pia kukamilika mradi wa kupeleka umeme Pemba ambao ulizinduliwa rasmi tarehe 9 Mei, 2013 na umeboresha upatikanaji umeme wa uhakika katika kisiwa cha Pemba. Kazi hii ilihusisha kutandaza waya wa majini (submarine cable) yenye urefu wa kilomita 90.

(iv) Kuimarisha mfumo wa njia za usafirishaji na usambazaji katika Mikoa ya Arusha na Kilimanjaro (TEDAP): Mradi huu ulihusisha ufungwaji wa Transformer mpya katika vituo vya kupoozea umeme vya Boma Mbuzi, Mt. Meru, Kiltex, Njiro B, Sakina, Themi, Trade School na Unga Ltd. Pia ujenzi wa njia za usambazaji wa umeme katika miji ya Arusha kilomita 143 na Kilimanjaro kilomita 25, ukarabati wa kituo cha kupoozea umeme cha Kiyungi na ujenzi wa njia ya usafirishaji ya umeme ya kilomita 70 ya msongo wa kilovolti 132 kutoka Kiyungi – Njiro, Ujenzi wa kituo kipya cha kupoozea umeme cha KIA cha 132/33kV na ujenzi wa njia ya usafirishaji ya msongo wa 66kV Kiyungi (TPC) Moshi hadi Makuyuni Himo. Mradi huu tayari umekamilika.

(v) Mradi wa Makambako - Songea kV 220: Mradi huo unahusisha ujenzi wa njia yenye urefu wa kilomita 250 na kujenga vituo vya kupoozea umeme 220/132/33kV vya Makambako, Madaba na Songea. Mchakato wa kutafuta wakandarasi wa mradi wa ujenzi wa njia kuu pamoja na vituo vya kupoozea umeme umekamilika na taarifa ya tathmini imewakilishwa kwenye bodi ya zabuni kwa ajili ya kupata kibali hatimaye ipelekwe SIDA; na kujenga kilomita 900 za njia za usambazaji katika miji ya Makambako, Njombe, Ludewa, Songea, Namtumbo, Mbinga, Mbamba Bay, na vijiji vilivyopo karibu na njia ya kusafirishia umeme. Mchakato wa kutafuta wakandarasi wa mradi wa ujenzi wa njia za kusambaza umeme mijini na vijijini umekamilika na umepata kibali kutoka bodi ya dhabuni. Umepelekwa SIDA kwa ajili ya kupata kibali cha kuingia mkataba na mkadarasi aliyeshinda. Wakandarasi wa mradi huu tayari wameanza kazi za awali katika eneo la mradi na kazi inaendelea. Mradi huu unagharamiwa na Serikali ya Sweden kupitia Shirika la Maendeleo la Sweden (Sida) kwa kiasi cha Swedish Kroner milioni 500, sawa na Shilingi bilioni 112. Kwa upande wa usambazaji, mradi umekamilika kwa zaidi ya asilimia 5 na mradi kwa ujumla unatarajia kukamilika mwaka 2017.

(vi) Mradi wa Iringa - Shinyanga kV 400 (Backbone): Mradi huu ni wa kuimarisha Gridi ya Taifa ambapo kukamilika kwake kutapunguza upotevu wa umeme na kuongeza uwezo wa kusafirisha umeme wa kutosheleza mahitaji ya Kanda ya Kaskazini Magharibi. Taratibu za kumpata mtaalamu mshauri wa masuala ya ufundi, sheria na fedha alishapatikana na ameanza kazi; taratibu za manunuzi ya vifaa vya usambazaji umeme (cables na waya) zimekamilika na vifaa vimeanza kuwasili na mtaalamu wa usimamizi wa mradi ameanza kazi. Vilevile, Serikali kupitia TANESCO imeanza kulipa fidia katika maeneo ya mradi. Aidha, Mshauri wa mradi, Kampuni ya Fitchner ya Ujerumani anaendelea na kazi ya kusanifu njia ya usafirishaji umeme na vituo vya kupozea umeme. Gharama za mradi zinakadiriwa kuwa Dola za Marekani milioni 650, sawa na Shilingi bilioni 1,040. Mradi unatarajiwa kukamilika Mwaka 2016.

(vii) Mradi wa Dar es Salaam – Chalinze – Tanga – Arusha kV 400: Serikali kupitia TANESCO imedurusu usanifu wa mradi (redesigning) ili uanzie Dar es Salaam kupitia Chalinze hadi Arusha badala ya kuanzia Morogoro. Mwezi Juni, 2012 TANESCO na mkandarasi Kampuni ya TBEA ya China walisaini mkataba wa marekebisho (EPC addendum), kwa lengo la kuongeza uwezo wa kusafirisha umeme kutoka Dar es Salaam. Mradi huu utatekelezwa kwa mkopo wa takribani Dola za Marekani milioni 770, sawa na Shilingi bilioni 1,232 kutoka Benki ya Exim ya China na unatarajiwa kukamilika mwaka 2017.

(viii) Mradi wa ujenzi wa njia ya umeme ya kV 220 ya Bulyanhulu – Geita – Nyakanazi: Mwezi Januari, 2011 Serikali ilisaini mkataba wa mkopo na Taasisi ya fedha ya BADEA ya Misri na OFID ya Saudi Arabia. Lengo ni kutekeleza mradi wa ujenzi wa njia ya umeme kV 220 kutoka Bulyanhulu hadi Nyakanazi kupitia Geita. Kazi ya kuandaa zabuni za kandarasi za ujenzi ilikamilika mwezi Juni, 2012. Maeneo kwa ajili ya kujenga vituo vya kupoozea umeme tayari yamepatikana na hatua za kuanza kuwalipa wananchi walioathirika na mradi zipo katika hatua za mwisho. Mradi utagharimu Dola za Marekani milioni 53, sawa na Shilingi bilioni 84.8 na unatarajiwa Mwaka, 2017.

(ix) Mradi North – West Grid kV 400: Serikali imeamua kubadilisha msongo wa njia hiyo ya kusafirisha umeme kutoka kV 220 hadi kV 400 kwa lengo la kuimarisha mfumo na upatikanaji wa umeme katika Mikoa ya Geita, Kagera, Katavi, Kigoma, Mbeya, Rukwa na Shinyanga ili kukidhi matarajio ya shughuli mbalimbali za kiuchumi katika maeneo hayo. Maombi ya mkopo yamewasilishwa katika Benki ya Exim ya China kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo. Gharama za mradi zinakadiriwa kuwa Dola za Marekani milioni 259.2 na unatarajiwa kukamilika Mwaka, 2018

(x) Mradi wa electricity – V: Mradi huu ulitekelezwa kwa mkopo kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) na ulihusisha usambazaji wa umeme katika vijiji, miji midogo na Makao Makuu ya Wilaya katika Mikoa ya Geita (Bukombe), Mwanza (Magu na Kwimba) na Simiyu (Bariadi) na kukarabati vituo vikubwa vya kupozea umeme kwenye mikoa ya Dar es Salaam na Arusha. Gharama za mradi ni Dola za Marekani milioni 31, sawa na Shilingi bilioni 49.6.Mradi umehusisha ujenzi wa km 480 wa njia za kilovolti 33, km 251 wa njia za volti ndogo (0.4kV) na ufungaji wa transifoma 109 za kilovolti 33/0.4 na uwezo wa kVA 50 hadi 315 juu ya nguzo; ufungaji wa taa za barabarani na kuunganisha wateja wapatao 8,600 katika mikoa ya Mwanza, Simiyu, Shinyanga na Geita; ukarabati wa vituo vya kupozea umeme. Kuongeza Transfoma ya mbili yenye uwezo wa 33/11kV, 15MVA; kubadilisha Switchgear zote za nje za 33kV na 11kV na kuweka za ndani pamoja na kuongeza njia za kusambaza umeme kwa wateja; kuimarisha mfumo wote wa umeme ndani ya kituo; kubadilisha Transifoma ya 33/11kV, 15MVA iliyoungua pamoja na kubadilisha kizima umeme (CB); kuongeza Transifoma 2 za 132/33kV, 50MVA; kurefusha switchgear ya 132kV na njia nyingine ya kupeleka umeme wa 132kV katika kituo cha Kiyungi; Kujenga switchgear mpya ya 33kV yenye njia zaidi ya kusambaza umeme na kuweka mfumo mpya wa kidigitali wa kuendesha kituo na kusimamia uzimaji na uwashaji. Mradi huu unategemea kukamilika ifikapo Mwezi Septemba, 2015.

(xi) Mradi wa Kujenga Njia za kusambaza Umeme: Mradi huu unahusu ujenzi wa njia za msongo wa kV 33, kV 11 na kV 0.4 kwa ajili ya kusambaza umeme katika Mikoa ya Dodoma, Iringa, Manyara, Mbeya, Morogoro, Mwanza, Njombe na Tanga. Jumla ya kilomita 1,068 kati ya kilomita 1,335 zimekamilika za njia ya kV 33, kV 11, na kilomita 1,094.4 kati ya kilomita 1,368 zimekamilika kwa njia za kV 0.4. Sehemu ya miradi iliyokamilika kwa Mkoa wa Dodoma ilihusisha jumla ya vijiji 46 katika Kijiji cha Mkoka, Wilayani Kongwa.

(xii)Mradi wa Kujenga Njia ya Pili ya Umeme kutoka Dar es Salaam kwenda Unguja: Mradi huu ulihusika na ujenzi wa njia ya umeme ya kV 132 kutoka Ubungo hadi Ras-Kilomoni na utandazaji wa nyaya za umeme chini ya bahari kutoka Ras-Kilomoni hadi Mtoni – Unguja.. Gharama za mradi huo ni Dola za Marekani milioni 50, sawa naShilingi bilioni 80 na tayari umekamilika.

(xiii)Mradi wa Kuunganisha Gridi ya Taifa na Gridi za nchi nyingine: Upembuzi yakinifu wa mradi wa kuunganisha Gridi ya Taifa na gridi za nchi za Zambia na Kenya (ZTK project) ulikamilika kwa upande wa Tanzania kwa ufadhili wa Serikali ya Norway. Aidha, Benki ya Dunia, Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) na JICA zimekubali kufadhili utekelezaji wa mradi huo katika kipande cha Singida hadi Namanga. Fedha zinaendelea kutafutwa kwa ajili ya utekelezaji wa sehemu ya mradi kutoka Kabwe hadi Mbeya. Kukamilika kwa mradi huu kutawezesha biashara ya umeme kati ya Tanzania na nchi za Afrika Mashariki na Afrika ya Kusini. Gharama za mradi huu ni Dola za Marekani milioni 642. Mradi huu unatarajiwa kukamilika 2018.


This is cool! How make fruit salad quickly


Taarifa ya Wizara kuhusu aliyekufa akihofiwa kuwa na 'ebola'

Utangulizi

Ugonjwa wa Ebola umeendelea kuenea katika nchi za Afrika ya Magharibi ambapo hadi sasa nchi tatu ambazo ni Guinea, Liberia na Siera Leone, zimeendelea kutoa taarifa za wagonjwa wapya. Aidha, mpaka tarehe 19 Julai 2015, idadi ya wagonjwa waliothibitishwa kuwa na ugonjwa huu ni 27,705 na vifo 11,269. Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii imejiandaa vyema kudhibiti ugonjwa huu iwapo utaingia nchini ikiwa ni pamoja na kutengeneza mpango kazi wa udhibiti wa ugonjwa huu wa miaka mitatu kuanzia 2015 hadi 2017.

Historia ya Mgonjwa

Mnamo tarehe 9 Agosti 2015, mgonjwa mwenye umri wa miaka 39 kutoka katika kambi ya wakimbizi ya Nyarugusu alipokelewa katika hospitali ya Mkoa wa Kigoma Maweni akiwa na dalili za kutokwa na damu sehemu mbalimbali za mwili hasusan kwenye fizi, macho na masikio. Vile vile alikuwa na dalili za kuchoka na mwili kuwasha. Mgonjwa huyu hakuwa na homa. Alipata matibabu katika hospital hiyo na kwa bahati mbaya mnamo tarehe 10 Agosti, 2015 mgonjwa huyu alifariki dunia. Mgonjwa huyu alikuwa hana historia ya kusafiri kutoka nje ya mkoa wa Kigoma wala kutembelewa na mtu aliyesafiri kutoka nchi za Afrika Magharibi zenye ugonjwa wa Ebola.

Mgonjwa huyu alikuwa ni mkimbizi wa kutoka nchi ya Burundi ambaye ameishi katika kambi ya Nyarugusu kwa miaka mitatu. Mgonjwa huyu alikuwa mmojawapo wa wakimbizi waliokuwa wasafirishwe katika mpango wa kawaida chini ya Shirika la Kimataifa linalohudumia wakimbizi kwenda Marekani. Safari hiyo ilikuwa ianze tarehe 9 Agosti 2015.

Hatua zilizochukuliwa
 1. Mgonjwa huyu alipatiwa matibabu katika hospitali ya Maweni Kigoma mpaka mauti ulipomkuta.
 2. Uongozi wa Afya Kigoma unafuatilia ndugu wa karibu wa mgonjwa huyu, pamoja na wahudumu wa Afya waliomuhudumia mgonjwa huyu kuona kama wataonyesha dalili zinazofanana na ugonjwa aliokuwa nao mgonjwa huyu. Ufuatiliaji huo umeanza tarehe 9 Agosti 2015. Mpaka leo hakuna mtu mwingine, aliyeonyesha dalili za ugonjwa huu.
 3. Sampuli ya mgonjwa huyu imechukuliwa na kupelekwa kwenye maabara ya Taifa ya Afya ya Jamii, ya Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii iliyopo Dar es Salaam kwa uchunguzi zaidi ili kujua chanzo cha ugonjwa huu.
 4. Mazishi ya marehemu huyo yamefanyika chini ya uangalizi wa Afya mkoa, kwa kuzingatia Utaratibu wa Kanuni za Kimataifa za kuzuia maambukizi.
Hitimisho

Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii inapenda kuwahakikishia wananchi kuwa mpaka sasa, hakuna uthibitisho wowote kuwa mgonjwa huyu amekufa na ugonjwa wa Ebola. Aidha kwa kuwa ugonjwa bado unaendelea nchi za Afrika Magharibi, Wizara inazidi kusisitiza wananchi kuchukua tahadhari za kujikinga na ugonjwa wa Ebola na magonjwa mengine ya kuambukiza. Ikiwa ni pamoja na
Kuepuka kugusa au kuingiwa na mate, damu, mkojo, jasho, kinyesi, machozi na majimaji mengine yanayotoka mwilini mwa mgonjwa mwenye dalili za ugonjwa wa Ebola kupitia sehemu zenye michubuko au vidonda.

 • Kuepuka kushughulikia maiti ya mtu aliyekufa akiwa na dalili za ugonjwa wa Ebola; badala yake watoe taarifa kwa uongozi wa kituo cha kutoa huduma za Afya kwa ushauri. Wataalam watasimamia maziko ikiwa kifo kitatokea.
 • Wananchi waepuke mila na desturi zinazoweza kuchelewesha kupata huduma muhimu na kuzidi kueneza ugonjwa wa Ebola.
 • Kutoa taarifa mapema kwa viongozi wa Serikali na watoa huduma za Afya katika ngazi zote pale anapotokea mtu mwenye dalili za ugonjwa wa Ebola.
 • Kuwahi katika vituo vya kutolea huduma za Afya pale mtu anapohisiwa kuwa na dalili za ugonjwa huu.
 • Kunawa mikono mara kwa mara ili kuepuka kusambaza ugonjwa ikiwa mtu atakuwa ameshika mgonjwa au mazingira yenye maambukizi.
 • Kutumia kemikali za kuua vijidudu kutakasa mikono.
Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii itatoa taarifa pindi majibu ya maabara yatakapopatikana.

Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali – Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii
12 Agosti, 2015

Kulenga na kuendesha baiskeli juu ya reli

Ephrahim Maxson akipita juu ya reli kwa baiskeli huko Nguruka, Kigona

Magufuli aagiza, "Walemavu na wanafunzi wavuke bure"

Magufuli akizungumza na wakazi wa Mtwara juzi
Serikali imeagiza wanafunzi na watu wenye ulemavu katika Manispaa ya Mtwara Mikindani na kata ya Msangamkuu, watasafiri bure kwenye kivuko cha Mv Mafanikio.

Kauli hiyo ilitolewa juzi na Waziri wa Ujenzi, John Magufuli, wakati akimkaribisha Rais Jakaya Kikwete kuzindua kivuko hicho.

Alisema wanafunzi wote waliovaa sare za shule hawatatozwa nauli kutokana na kundi hilo kuwa tegemezi.
“Walemavu na wanafunzi watavuka bure bila kutozwa hata shilingi 10, ili mradi tu awe amevaa sare za shule na walemavu pia hawatatozwa pesa yoyote na kwa wengine ni lazima tuendelee kuchangia mafuta ili kivuko hiki kitusaidie na kuwa endelevu,” 
Magufuli alisema kivuko hicho chenye uwezo wa kubeba abiria 100 pamoja na magari kimegharimu Sh. milioni 3.3, fedha kutoka serikalini.
via NIPASHE

Wakati umefika CCM itengenishe vichwa vya kuvaa kofia zake?


Kwa muundo wa sasa wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais wa nchi tulie naye hivi sasa ndiye pia mwenyekiti wa chama hicho kwa ngazi ya Taifa.

Ili kukuza demokrasia, ni vizuri tukazitafakari vyema changamoto zinazomkabili yule anayevaa kofia hizo mbili, ili tufikie muafaka wa kupendekeza kuendelea kofia zote mbili kuvaliwa na mtu mmoja au la.

Pamoja na uwezekano wa chama cha upinzani kushika madaraka, lakini kwa sasa tujadili urais na uenyekiti wa CCM kwani ndiyo mfano uliopo.

Kwa muktadha huo, ni vizuri tukazamisha fikra zetu katika kuangalia madhara ya mkwamo wa uendeshaji na usimamizi wa demokrasia huku kofia mbili zikiwa pamoja katika kichwa cha mtu mmoja.

Kwa mtazamo ulio wazi, kuna uzito mkubwa kwa Rais wa nchi kukidhi matakwa ya uenyekiti wa chama hasa katika kipindi hiki ambacho changamoto za kisiasa hazina msimu na nyingi zinahitaji uamuzi au ridhaa ya mwenyekiti.

Urais wa Tanzania ni jukumu la kuwatumikia Watanzania wote, wenye vyama na wasio na vyama; tena wote wanatarajia kutendewa haki bila ya kubaguliwa kwa misingi ya utashi wao katika vyama.

Kwa siasa za kisasa ukijumlisha na mizengwe yake, ziko sababu za msingi za kukibakisha cheo cha uenyekiti wa chama katika kichwa cha Rais ili kuepuka migogoro inayoweza kujitokeza ndani ya chama wakati yeye Rais akiwa amebarizi Ikulu.

Kwa upande wa pili, majukumu ya urais yanamtosha Rais pekee na si busara hata kidogo kuendelea na hali iliyo sasa ya kumvika kofia ya uenyekiti wa chama kwa sababu zifuatazo:

Mosi, uwezekano wa kofia mbili hizi kutenganishwa upo tena bila ya kuleta madhara yoyote.

Ushahidi wa hilo ni pale Rais mpya anapoingia madarakani huku uenyekiti wa chama Taifa ukiendelea kubakia kwa Rais anayemaliza muda wake kwa muda wa miaka miwili.

Hivi kama imewezekana kofia hizo kutenganishwa kwa miaka miwili, kuna uzito gani kuzitenganisha moja kwa moja?

Kama chama kinaweza kubakia chini ya uenyekiti wa Rais aliyestaafu kwa miaka miwili mpaka utakapofanyika uchaguzi mwingine wa viongozi wa chama na huyu Rais mpya akabakia kuwa salama au vinginevyo, je, kuna hoja gani itakayojengwa juu ya kutowezekana kutenganishwa kofia mbili hizo?

Pili, kutenganisha kofia mbili hizo ili kuondosha malalamiko na kujenga demokrasia ya kweli. Watanzania leo hii hawana tatizo juu ya mali za Serikali kutumiwa ili kuboresha taasisi ya urais, na wala hawana tatizo juu ya gharama za huduma za Rais.

Lakini Watanzania hao hao hawako tayari mali zao kuziona zikitumika kwa maslahi ya CCM pekee, kwani tayari Watanzania walichagua mfumo wa vyama vingi vya siasa.

Pindi Rais wa nchi (mwenyekiti wa chama) akialikwa katika shughuli za kichama ni vigumu taasisi ya urais kuacha kutumia fedha za umma kwa masilahi ya chama kwa sababu bado mtu ni yuleyule. Ili kuepusha tatizo hilo ni vizuri CCM kikatenganisha kofia hizi mbili.

Watanzania hawapendi ‘masihara’ ya kisiasa yamlenge moja kwa moja Rais wa nchi. Na ukweli ni kwamba, kitendo cha Rais wa nchi kuvaa kofia ya uenyekiti wa chama kinamkosesha kinga ya kejeli za wanasiasa kwa mwanasiasa mwenzao.

Anaposimama Mwenyekiti wa chama pinzani kisha akamshutumu, kumdharau au hata kumkejeli kisiasa Mwenyekiti wa chama ambacho kinaongoza serikali (chama tawala) ambaye pia ndiye Rais wa nchi, hapo ni moja kwa moja Serikali imedharauliwa kwa sababu mwenyekiti huyo ndiye kiongozi mkuu wa nchi.

Tatu, kuwapoteza viongozi wazuri wenye uwezo mkubwa wa kuongoza Serikali lakini hawana uwezo au historia katika uongozi wa chama.

Kwa mfano, chama katika mchakato wake kimemtafiti mmoja miongoni mwa wagombea halafu kikagundua ana uwezo usiotiliwa shaka katika kuongoza serikali.

Lakini kitendo cha urais kuunganishwa na uenyekiti wa chama, chama kitalazimika kumtafiti mgombea huyu katika uwezo au historia (uzoefu) ya uongozi wake katika chama.

Chama kikijiridhisha kwamba hana historia yoyote ya uongozi katika chama, kuna uwezekano mkubwa chama kikamkataa huyu ambaye anao uwezo wa kuongoza serikali, lakini hana uzoefu wa kuongoza chama kwa kiasi cha kubebeshwa zigo la uenyekiti wa chama.

Hapo ndipo ninapoendelea kusema kwamba umefikia wakati sasa kofia mbili hizi zitenganishwe.

Ifahamike kwamba hata viongozi na wanachama wa CCM wenye uelewa wa kufahamu mamlaka za kiserikali na utendaji wake, pia wanamtazama Rais wa nchi kwa vyeo vyake vyote

Wanamtazama kwa vyeo hivi: kiongozi mkuu wa nchi, kiongozi mkuu wa Serikali, Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama.

Utaona kwa nguvu hizi alizonazo Mwenyekiti wake, zinamzuia mjumbe wa vikao vya chama kunyanyua mdomo wake kuhoji masuala muhimu ya chama.

Lakini kama kofia mbili hizi zitatenganishwa, Rais wa nchi atabakia na nguvu zake hizo na Mwenyekiti wa chama kwa ngazi ya Taifa atabakia na uenyekiti wake, na hivyo itakuwa rahisi na wepesi kwa wanachama kuhoji masuala muhimu ya chama.

Kuna tofauti unapomhoji mtu kama Mwenyekiti tu wa chama na unapomhoji Mwenyekiti huyohuyo anapokuwa ni Amiri Jeshi Mkuu.

Kwa muktadha huo, utaona mantiki ya kazi za kusimamia chama kwa nafasi ya Mwenyekiti Taifa zingepangiwa mtu mwengine na Rais wa nchi akaachwa asimamie yale ambayo yana maslahi na Watanzania wote

Nihitimishe tafakuri yangu kwa kuwashauri wana CCM kwamba, umefika wakati sasa kutafakari kwa kina umuhimu wa kuzitenganisha kofia mbili hizo ili kumpa nafasi Raisi kushughulika zaidi na taasisi ya Uraisi.

Endapo itashindikana kwa haraka kukubaliana kuzitenganisha kofia hizo mbili, basi muombeni Mwenyekiti wa chama chenu aendelee na wadhifa huo kwa miaka miwili na asijiuzulu kumpisha mwenzake kama ilivyo ada kwa sasa.

Makala ya Prof. Lipumba akiwa Rwanda iliyochapishwa gazetini Mwananchi

Prof. Lipumba
Prof. Lipumba
Baada ya kujiuzulu kuwa Mwenyekiti wa Taifa wa CUF nimerejea katika shughuli za utafiti. Tangu mwaka 2011 nilipokutana na Balozi wa Rwanda nchini Tanzania, nilimueleza nia yangu ya kufanya utafiti wa nini Tanzania inaweza kujifunza kutoka Rwanda.

Sikupata fursa ya kufanya utafiti huo. Baada ya kuamua kun’gatuka uongozi wa siasa, nimepata fursa ya kuendelea na utafiti huo kwa lengo ya kutoa ushauri wa mambo ambayo Tanzania inaweza kujifunza kutoka Rwanda bila kuathiri harakati za kujenga demokrasia na kuheshimu haki za binadamu.

Mtanzania yeyote anapofika Kigali kwa mara ya kwanza atastaajabu usafi wa mji na uzuri wa barabara. Hakuna takataka na huwezi kuona mifuko ya plastiki mitaani. Utengenezaji na uagizaji wa mifuko ya plastiki umepigwa marufuku. Hakuna maeneo yenye vibanda vya ovyo ovyo (slums). Mji una amani na utulivu. Unaweza kutembea usiku bila kuogopa kuporwa au kuvamiwa na vibaka. Kigali ni mji wenye amani lakini pia una askari wengi mitaani wenye nidhamu. Hata vijijini hakuna nyumba zilizoezekwa kwa nyasi.

Wananchi wa Rwanda chini ya uongozi wa Rais Paul Kagame wamefanikiwa kuibadilisha nchi iliyokumbwa na mauaji ya kimbari mwaka 1994, kuwa nchi yenye amani na utulivu. Katika kipindi cha siku 100 kuanzia Aprili 7 1994, wananchi milioni moja waliuawa. Idadi ya watu nchini Rwanda mwaka 1994 ilikuwa milioni saba.

Pamoja na watu milioni moja kuuawa, milioni mbili walilazimika kuwa wakimbizi. Kulikuwa na watoto wengi yatima wasiokuwa na ndugu yeyote. Katika historia ya mauaji ya kimbari hakuna nchi iliyoshuhudia mauaji ya watu wengi kwa muda mfupi kama ilivyotokea Rwanda. Kurejesha amani na utulivu peke yake ni mafanikio makubwa.

Rwanda pia imepata mafanikio makubwa ya kiuchumi na kijamii. Kati ya mwaka 2000 na 2014, pato la taifa limeongezeka kwa wastani wa asilimia 7.7 kila mwaka. Wanyarwanda milioni 1 wamefanikiwa kujinasua kutoka kwenye lindi la umaskini wa kutupwa. Katika kipindi hiki wastani wa pato la kila mwananchi limeongezeka karibu mara mbili licha ya kuwa na kasi ya juu ya ongezeko la idadi ya watu.

Hakuna nchi iliyofanikiwa kurudisha amani na kukuza uchumi kwa muda mfupi baada mauaji makubwa na kusambaratika kwa taifa kama ilivyofanya Rwanda. Mafanikio haya yalitegemea misaada ya fedha kutoka nchi wahisani. Serikali ya Rwanda iliweza kutumia misaada hiyo vizuri. Zaidi ya hapo imeweka mkakati wa kupunguza kutegemea misaada ya nje.

Mwaka 2000 bajeti ya Serikali ya Rwanda ilitegemea misaada kwa asilimia 48.3. Ilipofika mwaka 2013, kutegemea misaada ya nje katika bajeti ya serikali kumepungua na kufikia asilimia 30.2.

Rwanda imejitahidi katika kupambana na ufisadi mkubwa na rushwa ndogondogo. Baadhi madereva wa malori kutoka Tanzania waliotoa rushwa kwa askari wa barabarani wamefikishwa mahakamani na kufungwa.

Taarifa ya Shirika la KimaTaifa (Transparency International) linalochunguza rushwa linaonyesha kuwa mwaka 2014, Rwanda ilipata alama 49 kati ya 100 na kuwa nchi ya 55 kati ya nchi 175 kwa kuwa na rushwa kidogo. Tanzania ilipata alama 31 kati ya 100 na kuwa nchi ya 119.

Rwanda ni nchi ndogo isiyokuwa na ufukwe wa bahari lakini imefanya marekebisho ya sera zake na hivi sasa ni nchi ya tatu kwa ushindani wa kiuchumi katika bara la Afrika baada ya Mauritius na Afrika ya Kusini. Tanzania ni ya 21. Katika nchi 144 zinazofanyiwa tathmini ya ushindani wa kiuchumi, Rwanda ni ya 62 na Tanzania ni ya 121.

Taarifa ya Benki ya Dunia kuhusu wepesi wa kufanya biashara ya mwaka 2014 inaonyesha Rwanda ni nchi ya 32 kati ya nchi 189 wakati Tanzania ni nchi ya 145. Mwaka 2005 Rwanda ilikuwa ya 158. Tovuti ya Rais Kagame inaonyesha kuwa inachukua saa sita kuanzisha na kusajili kampuni. Nchini Tanzania inachukua siku 26.

Wastani wa miaka ya kuishi umeongezeka kutoka miaka 51mwaka 2000 na kufikia miaka 65 mwaka 2012. Asilimia 73 ya Wanyarwanda wana bima ya afya. Watoto wote wanajiunga na shule za msingi na asilimia 72.7 wanamaliza shule za msingi.

Rwanda imefanikiwa katika kuleta usawa wa jinsia. Asilimia 64 ya wabunge ni wanawake. Zaidi ya theluthi moja ya mawaziri ni wanawake.

Matumizi ya kompyuta na mtandao yanaanzia shule za msingi. Katika nchi yenye eneo la kilomita za mraba 24,670, imetandaza nyaya za mtandao wa intaneti kilomita 2229.

Rais mwenyewe

Rais Kagame ni msimamizi wa karibu wa utekelezaji wa miradi ya maendeleo. Hasumbuliwi na itikadi anajali matokeo. Ana kumbukumbu ya mambo mengi yanayoendelea Rwanda. Kwa mfano anajua watu wazima wangapi wataotarajiwa kufundishwa kusoma na kuandika katika kila wilaya. Au ng’ombe wangapi watakaopandishwa na mbegu bora katika eneo lipi.

Viongozi wa serikali wanaingia na kuweka saini mkataba unaoitwa ‘imihigo’ kwa Kinyarwanda unaoeleza majukumu watakayoyatekeleza. Mikataba hii pia inawekwa saini na Rais Kagame mwenyewe. Usipotekeleza mkataba wako unapoteza kazi yako. Dhana ya imihigo inatokana na utamaduni wa Rwanda wa mtu kutoa ahadi katika jamii anayoishi ya kutekeleza majukumu aliyopanga na asipofanya hivyo jamii inamdharau na anakosa heshima.

Mpango Mkakati wa Rwanda wa kujenga uwezo wa utekelezaji (Strategic Capacity Building Initiative) unalenga kujenga uwezo wa serikali kutekeleza vipaumbele vichache lakini muhimu katika kuchochea maendeleo. Sekta zinazopewa kipaumbele na mpango huu ni kilimo, nishati, madini na uwekezaji.

Mkakati huu unazingatia malengo ya mpango wa pili wa maendeleo wa Rwanda unaolenga kubadilisha mfumo wa uchumi wa Rwanda na kuongeza tija, kuongeza uzalishaji sekta ya kilimo na kuleta maendeleo vijijini, kuongeza ajira kwa vijana na kuimarisha utawala bora na uwajibikaji.

Ni rahisi kuhitimisha kuwa maendeleo yaliyopatakana Rwanda ni matokeo ya kuwa na kiongozi mwenye dira na mamlaka ya kidikteta. Haiwezekani Rais kwenye nchi yenye mfumo wa demokrasia kuweza kupata mafanikio yaliyopatikana Rwanda. Kuwa na mipango inayoeleweka na kuisimamia kikamilifu hakuitaji kuwa na Rais dikteta. Kunahitaji rais mwadilifu na muwajibikaji. Mfumo imara wa demokrasia unahitaji uwajibikaji na uadilifu.

Ili tuwe na maendeleo yanayowaletea neema wananchi wote tunahitaji demokrasia ya kweli na siyo utawala wa kidikteta. Demokrasia ya kweli inawapa fursa wananchi kuchagua viongozi wanaowataka katika uchaguzi ulio huru na wa haki.

Hata hivyo haitoshi kuwa na uchaguzi huru. Serikali iliyochaguliwa lazima iwajibike kwa wananchi. Asasi muhimu za serikali inayowajibika na utawala bora ni pamoja na Bunge lenye mamlaka ya kuisimamia na kuiwajibisha serikali, mahakama huru zinazotenda haki, tume huru ya uchaguzi, mkaguzi na mdhibiti wa mahesabu ya serikali, tume yenye uwezo wa kupambana na rushwa, utumishi serikalini wenye weledi, mfumo wa kodi na ukusanyaji mzuri wa mapato ya serikali na usimamizi mzuri wa matumizi ya serikali.

Bunge la Rwanda linaisimamia serikali, mbunge hawezi kuwa waziri

Tanzania ni tajiri wa mali ya asili kuzidi Rwanda. Tunaweza kukuza uchumi unaoongeza ajira na kuwaletea neema wananchi wote ikiwa tutakuwa na uongozi wenye dira na sera mwafaka na usimamizi madhubuti wa utekelezaji wa mipango ya maendeleo.

Rais tutakayemchagua Oktoba 25 2015 anaweza kujifunza kutoka kwa Rais Kagame kuhusu usimamizi wa utekelezaji wa miradi ya maendeleo. Mapema baada ya kuchaguliwa anaweza kukutana na Rais Kagame akajifunza uzoefu wa Rwanda kuhusu umuhimu wa kuweka vipaumbele na usimamizi wa utekelezaji.

Profesa Ibrahim Lipumba
via Gazeti la Mwananchi