Taarifa ya Wizara ya Afya kuhusu hali ya kipindupindu Tanzania

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

WIZARA YA AFYA NA USTAWI WA JAMII

TAARIFA KWA UMMA KUHUSU HALI YA UGONJWA WA KIPINDUPINDU NCHINI

Utangulizi

Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii inapenda kutoa taarifa kwa umma, kuhusu hali ya ugonjwa wa kipindupindu katika mikoa ya Dar es Salaam na Morogoro. Ugonjwa wa kipindupindu katika mkoa wa Dar es Salam umeripotiwa katika Manispaa ya Kinondoni kuanzia tarehe 15 Agost, 2015. Tangu ugonjwa uanze hadi tarehe 20 Agosti 2015 idadi ya wagonjwa walioripotiwa ni 56 na vifo vya watu watatu (3). Wagonjwa walioathirika wanatokea maeneo ya Tandale, Mikocheni, Saranga, Kijitonyama, Makumbusho, Ubungo, Kigogo, Manzese, Kawe na Kimara katika Manispaa ya Kinondoni. Mkoani Morogoro wagonjwa nane (8) wameripotiwa na kifo cha mtu mmoja na wanatokea katika maeneo ya Kilakala na Mzinga Juu.

Kutokana na hali hii, Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii inapenda kutoa tahadhari ya Ugonjwa huu kwa wananchi wote wa nchini na hasa kwa mkoa wa Dar es Salaam, Morogoro na mikoa ya jirani.
Kipindupindu ni ugonjwa hatari unaoambukizwa kwa kula chakula au kinywaji chenye vimelea vya “Vibrio cholera” ambavyo ndivyo husababisha ugonjwa wa kipindupindu. Vimelea hivi hupatikana kwenye kinyesi na matapishi ya mgonjwa wa kipindupindu au kwenye kitu chochote kimechafuliwa na kinyesi au matapishi ya mgonjwa.

DALILI KUU ZA UGONJWA WA KIPINDUPINDU

Dalili kuu za ugonjwa wa kipindupindu ni pamoja na kuanza ghafla kuharisha mfululizo kinyesi cha majimaji meupe kama maji ya mchele na kunaweza kuambatana kutapika, kulegea, kusikia kiu, midomo kukauka, na kuishiwa nguvu. Mgonjwa anaweza kupoteza maisha endapo hatapataa huduma yoyote ya tiba katika muda mfupi na hasa kutokana na kuishiwa maji.

Hatua zilizochukuliwa

i. Kufungua kambi za wagonjwa wa kipindupindu katika Manispaa zote tatu za Dar es Salaam ambapo kwa Kinondoni kambi ipo Mburahati, Ilala kambi ipo kituo cha afya Buguruni na Temeke katika Hosipitali ya Temeke.
ii. Kutoa dawa, vifaa vya maabara na vifaa kinga
iii. Kupima vipimo vya maabara na kubaini aina ya vimelea vinavyosababisha ugonjwa
iv. Kupeleka timu za watalaam kutoka ngazi ya Mkoa na Taifa kusaidiana na timu za Manispaa husika.
v. Kutoa mafunzo kwa watumishi wa afya kuhusu ufuatiliaji na matibabu ya ugonjwa wa kipindupindu
vi. Kutoa elimu ya afya kwa jamii kuhusu namna ugonjwa unavyoenezwa na hatua za kuchukua ili kujikinga na maambukizo ya ugonjwa huu
vii. Kutembelea maeneo yote walikotoka wagonjwa na kuhimiza kuzingatia kanuni za afya.
viii. Ufuatiliaji katika ngazi ya kaya walizotoka wagonjwa na pia kunyunyuzia dawa kwenye vyanzo vya maji (chlorine) na vyoo vya shimo na maji yaliyotuama
ix. Ukaguzi wa biashara za vyakula na vinywaji (Mama na Baba lishe).
x. Kushirikisha idara ya maji katika kuchukua sampuli kwenye vyanzo vya maji ya bomba na visima kwa ajili ya kufanya uchunguzi wa kimaabara.
xi. Kuimarisha ukaguzi na upimaji wa afya za wauza vyakula katika migahawa na mama/baba lishe

Hata hivvo Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kwa kushirikiana na uongozi wa mikoa iliyoathiriwa itaendelea kufuatilia kwa karibu sana hali ya ugonjwa huu ili kuhakikisha kuwa ugonjwa huu unadhibitiwa mapema na kumalizika kabisa hapa nchini.

NJIA ZA KUDHIBITI KUENEA KWA UGONJWA HUU:

Wananchi wanashauriwa kuzingatia yafuatayo ili kujikinga na ugonjwa huu:

i. Epuka kula chakula kilichopoa au kuandaliwa katika mazingira yasiyo safi
ii. Nawa mikono yako kwa sabuni na maji safi kwa maji yanayotiririka:-
– kabla na baada ya kula
– baada ya kutoka chooni
– baada ya kumnawisha mtoto aliyejisaidia
– baada ya kumhudumia mgonjwa
iii. Epuka kusalimiana kwa kushikana mikono
iv. Kunywa maji yaliyo safi na salama – yaliyochemshwa au kutiwa dawa
v. Hakikisha mazingira yako yanakuwa safi wakati wote hasa chooni
vi. Usile tunda au kitu chochote bila kukisafisha kwa maji safi na salama
vii. Hakikisha unatumia choo kwa ufasaha na wakati wote
viii. Toa taarifa kituo cha Afya kilicho karibu na wewe endapo utapatwa na ugonjwa wa kuharisha au kutapika

Hitimisho

Wizara inapenda kuwatahadharisha wananchi kufuata kanuni za Afya, kama vile kunawa mikono na sabuni baada ya kutoka chooni na kabla ya kula chakula pamoja na kunywa maji yaliyo chemshwa au kutibiwa na dawa ya aina ya klorini.

Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali
Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii
Tarehe 20, August, 2015

Mkuu wa Mkoa wa Dar apiga marufuku kuzomea wafuasi wa vyama vya siasa
ACT yamtangaza mgombea Urais Tanzania 2015 na kupokea waliohama CHADEMASehemu ya mwisho: Maoni ya Mndeme kuhusu aliyosema Polepole

Mkanganyiko wa Kauli na Misimamo ya Humphrey Polepole kuhusu UKAWA na Mh Lowasa: Sehemu ya Nne
Katika sehemu ya nne ya makala hii, ninaendelea na kipengele cha MAGEUZI na MABADILIKO ambacho ndugu Humphrey Polepole (HP) amekitumia sana katika uwasilishaji wake katika kuwapinga UKAWA kama kundi la kisiasa na mgombea wao ambaye kwa lugha nyepesi ameamua "kumvua nguo" ili akataliwe na wapiga kura. Iwapo hukunisoma kwenye sehemu tatu za mwanzo, nakushauri uzisome kwanza ili upate msingi wa nitakachojadili hapa. Sehemu zote tatu za kwanza zapatika kwenye blodg yangu ya www.mwalimumm.blogspot.com na kwenye www.wavuti.com
Sehemu ya tatu ya makala hii niliandika kwa kirefu kidogo kuhusu dhana ya mabadiliko na uhalisia wake kwenye maisha na mazingira ya utawala wa kidemokrasia kama wa nchi yetu. Kwa lugha nyepesi, mabadiliko yanawezwa kutazamwa kama TUKIO au MCHAKATO wa muda mfupi wenye lengo la kubadilisha kilichopo. Kwa upande mwingine MAGEUZI ni MCHAKATO wenye lengo la kubadili mfumo. Kama nilivyosema jana, unaweza kufanya mabadiliko bila mageuzi lakini huwezi kufanya mageuzi bila kuanza na mabadiliko.


Jana nilijenga hoja kwamba katika mazingira halisi, mabadiliko mengi ya mifumo ya utawala wa kisiasa, yanaangukia katika kundi la mabadiliko yasiyopangwa (unplanned change). Msukumo wa mabadiliko ya kisiasa hayahitaji wasanifu (archtect) wa kuwafundisha watu jinsi ya kubadilika bali watu huamua kutafuta mbadala wakisukumwa na mambo wasiyoridhishwa nayo chini ya hali ilivyo kinyume na matarajio yao toka kwa watawala. Mifano ya hili ni mingi Afrika na kwinginko. Wako wanaowatisha watu kwamba namna hii ya mabadiliko ni hatari na wanaifananisha na nchi za Libya na Syria lakini hawasemi pia kwamba kuna nchi kama Tunisia, Misri, Kenya, Zambia na kwingineko ambako mabadiliko yalifanyika na yamepelekea nchi hizo kufanya MAGEUZI. Kabla sijaingia kwenye hoja ya MAGEUZI, niongeze kitu kidogo kuhusu dhana ya mabadiliko niliyoizungumzia jana:


 1. Pamoja na ukweli wa kwamba watu wana sababu na kiu ya mabadiliko, uzoefu na utafiti unaonesha kwamba watawala huwa ni waoga na hawapendi mabadiliko. Jana nilieleza kidogo kwa nini mabadiliko huwa yanakabiliana na pingamizi kubwa. Wakati mwingine watu hawa wanaogopa hata wasichokijua (the fear of unknown) na hutafuta kila sababu ya kuonesha kwa nini mabadiliko siyo ya msingi na waendeleze hali iliyoko.


Nakumbuka miaka 9 iliyopita nilikua nafanya kazi na taasisi moja kama kiongozi wa mabadiliko (Change Management leader) kupelekea utumiaji wa mifumo ya TEHAMA kwenye mahospitali yaliyo chini ya mashirika ya dini ili kuboresha huduma na upatikanaji wa taarifa sahihi za afya. Nilipokua nawasiliasha mada yangu kwenye kundi la watalamu wa tiba kwenye hospitali mojawapo, daktari mmoja bingwa wa mangonjwa ya kina wanawake baada ya kunisikiliza kwa muda aliniuliza swali. Naomba nimnukuu, "Kijana wangu MM, mimi nimefanya kazi kwa miaka 30 kama daktari wa wanawake bila kutumia kompyuta. Leo unapotaka kuniwekea kompyuta niitumie wakati namtibu mgonjwa wangu, yenyewe inahusika vipi katika kumtibu mwanamke?". Nikiwa kama kijana asiye na uzoefu wa kufanya kazi katika sekta ya afya hili swali halikua jepesi na ilihitajika kulitazama katika kile kilichokua tayari kimeonekana kwa watumishi hawa: kwamba hawakutaka matumizi ya kompyuta maana walihisi inawaingilia "kumi na nane zao".


 1. Watu waliozoea mfumo wa utawala ni wagumu sana kukubalia tafakuri tofauti (different thinking) lenye lengo ya kuleta mabadiliko: labda hayo mabadiliko wawe wameyaanzisha wao. Ni ngumu sana mtu aliyelelewa kwenye mfumo na ameneemeka nao; umemfanya anakula na kusaza; unambeba kwa kila hali; halafu akatamani kuubadilisha hata kama hauna faida kwa wengine. Hawezi kufanya hivyo kwani hawana uhakika iwapo mfumo mpya utamwezesha yeye "kuendelea kuishi karibu na mbingu wakati wenzake wanaisogelea jehanamu". Hivyo watu wanaotaka mabadiliko wategemee upinzani mkubwa sana toka kwao na huwa wana hoja nzito zenye ushawishi. Hili ni kwa watawala na wanufaika wa mfumo hata kama sio watawala.


 1. Nikupe mfano: watanzania tunalalamika sana kwamba huduma za jamii ni mbaya na zimejaa rushwa. Ukitaka umeme lazima uhonge na hata kama unao ukipata hitilafu kupata mafundi kwa wakati lazima "uwe unajua mtu au unajulikana". Hivyo hivyo na kwenye maji. Hospitali hapafai na watu wanaomba Mungu wasiumwe kwani ukiumwa kutibiwa bila kujuana na mtu ni majaliwa. Kuna watu wanaomba usiku na mchana wasikumbane na chochote cha kuwafanya wafike kituo cha polisi bila kujali wao ndio washtaki au ndio washatakiwa. Maana wako ambao wana uzoefu wa kufika kituo cha polisi kwenda kutafuta haki na kujikuta wewe ndio unaingizwa "lock-up" kwa kuwa aliyewanyima haki "yuko karibu na system". Unaweza kujikuta hata kabla hujasikilizwa, unakua umeshatishwa vya kutosha, viatu umeambiwa uvue na ujitambulishe na kusema shida yako ukiwa umechuchumaa.


Pamoja na wanayokutana na hayo, wako watu wakitaka umeme hata kama kunahitajika nguzo kumi kufikia unapokwenda, wanainua tu simu na kesho yake mafundi wanaanza kazi. Wako watu ambao wakitaka maji wakiongea na "mkuu fulani" wanaletewa hadi bomba la ziada. Wako watu ambao wakiugua mawasiliano yanafanyika na kabla mgonjwa (yeye au ndugu) hajafika hospital kila kitu kimeshaandaliwa kwa ajili yake kupata matibabu. Wako watu wakikumbana na uhutaji wa kwenda kituo cha polisi: iwe wao ni wakosaji au wakosewa, polisi ni mahali salama sana kwao. Anasikilizwa na "anapata msaada" anaouhitaji. Usitegemee hata siku moja watu wa aina hii watawaunga mkono kundi linalodai mabadiliko: "eti mifumo iboreshwe na watu wote wapate haki na huduma kwa usawa bila upendeleo na uonevu". Watawapinga hao wenye wazo hilo hata ikiwezekana kwa kutumia "ngumi, kichwa na fimbo/bakora".


 1. Kwa mifano hii na niliyotoa jana, niseme tu kuwa, hua inahitaji "ukichaa fulani hivi na ung'ang'anizi" wa kutokukata tamaa katika kuyatafuta na kuyapata mabadiliko watu wanayoyadai toka kwa watawala. Iko hivyo na imekua hivyo sehemu nyingi duniani.


MAGEUZI
Makala iliyotangulia niligusia maana na dhana jumla ya mageuzi. Unapozungumzia mageuzi ya kisiasa au kiutawala wa nchi, hili ni jambo kubwa sana. Mageuzi yanatumia muda mrefu na hayafanywi kwa kushtukiza. Yanahitaji taifa kujipanga kimkakati na kutafuta aina fulani ya maridhiano katika makundi ya kijamii ili kuyafikia.


Kwa mfano, unapozungumzia haja ya mageuzi kwa nchi kama yetu unagusa maeneo mengi sana. Tuna shida na ubovu ulioota manyoya karibu kwenye kila eneo hasa vikichangiwa na mfumo wa utawala/uongozi. Unapotazama matatizo au changamoto hizi utagundua kwamba ni ngumu sana kukabiliana nazo kwa mifumo na taratibu tulizojiwekea sasa. Ziko changamoto zingine zinahitaji tu utayari na maamuzi lakini mifumo hairuhusu. Hivyo, ili kukabiliana na haya, tunahitaji MAGEUZI ya kiutawala na mifumo itakayotupelekea kuwa na nchi mpya tunayoitamani. Jambo hili liligusiwa na baadhi ya watia nia wa nafasi ya urais wa CCM na walifanya watu wengi kuvutiwa na mawazo yao (hili ni mada inayojitegemea).


Labda tujiulize MAGEUZI yanahitaji nini? Yako mambo mengi nasiwezi kudanganya kwamba naweza kuyaainisha yote hivyo nitataja machache tu ninayoona yanaendana na msingi wa mada yangu.


 1. Mageuzi huanza na kupata hamasa kupitia Mabadiliko: Nilipotoa tafsiri ya mageuzi jana nilinukuu tafsiri ya lugha ya kikoloni inayosema mageuzi "mabadiliko yaliyofikia ukamilifu" (transformation is a complete change). Nilisema kwamba hakuna mageuzi kabla ya mabadiliko na huwezi kufanya mageuzi bila kuanza na madiliko. Ukiweka mtazamo huu katika tafsiri nyepesi, utasema MAGEUZI ni MCHAKATO wenye kujumuisha MTIRIRIKO/MFULULIZO wa MABADILIKO yenye nia ya kufikia MFUMO mpya wenye sura ya maboresho tofauti na ambavyo mambo yamekua yakifanyika.


  1. Nitoe mfano: Wengi wetu tumemfahamu ndugu HP kupitia tume ya mabadiliko ya Katiba. Tume hii ilifanya kazi kubwa ya kukusanya maoni na waliendelea na kazi kubwa ya kuyatetea matokeo ya kazi yao dhidi ya waliokua wanayapinga hadi pale tume yao "ILIPOKATWA". Dhamira ya kuwa na katiba mpya, imejengwa katika kufanya MAGEUZI ya kimfumo kwa vile tumethibitisha kwamba hali tuliyonayo haiwezi kutusaidia kutatua wingi wa changamoto tulizonazo. Katika kulitatua hilo, tumeona pa kuanzia ni kuwa na mwongozo (road map) ambao katika huo mengine yote yatasimamishwa na kuimarishwa. Mwongozo huo ni katiba yenye kuainisha mambo tunayohitaji katika mfumo mpya.


  1. Kazi hii ya kuandaa katiba mpya waliyofanya akina HP ilitokana na maamuzi ya Rais kwamba tuanze mchakato huo. Ila Rais haikuibuka tu na kusema tunataka katiba. Kwanza yeye mwenyewe katiba mpya halikua jambo la msingi alipokua anatafuta uongozi mwaka 2010. Nina kumbukumbu ya kauli yake wakati wa kampeni za uchaguzi mwaka 2010 (nikimsikiliza kupitia Clouds FM) akisema wazi kwamba nchi yetu haihitaji katiba mpya.  Kama vile haitoshi, hii haikua ajenda ya chama chake. Tunajua kwamba msukumo wa kutaka katiba mpya ulikua ni ajenda kubwa ya vyama vya upinzani katika uchaguzi huo wakiendeleza madai ambayo yamekuwepo kwa muda mrefu.


  1. Baada ya hapo hatua zingine zilifuata hadi kufikia bunge maarufu na la kihistoria hasa kutokana na "tabia, kauli na mienendo" ya waheshimiwa waliojaliwa kuwa wajumbe. Historia ya yaliyotokea sote tunaijua.


Kwa kuyasema haya, nathibitisha tu kwamba HUWEZI KUPATA MAGEUZI BILA KUANZA NA MABADILIKO. Mabadiliko ndio hatua ya kwanza katika kuelekea kwenye MAGEUZI na haijalishi sana mabadiliko hayo yamefanywa kiusahihi kiasi gani au yamechukua muda mfupi au mrefu kiasi gani. Mabadiliko pekee ndio yanayoanza kuibua hari na kiu ya kwenda mbele kuelekea mageuzi. Watanzania wengi hasa wasio na elimu kubwa katiba mpya haikua jambo kubwa kuliko yote yanayowakabili. Ila pale rais alipoamua KUBADILIKA kutoka kwenye msimamo wa HATUHITAJI KATIBA MPYA kwenda kwenye msimamo wa TUNAHITAJI KATIBA MPYA, kila mtu alihamasika na hata ambao hawakuwahi kuiona katiba waliiona kwa mara ya kwanza. Vijana wangesema "katiba imekua issue". Kupiga gari "stata" ni hatua ya KWANZA na ya LAZIMA kabla hujaielekeza injini nini cha kufanya kukupeleka unapota kwenda.


 1. Mageuzi yanahitaji Uongozi wenye Dhamira:  ukitazama milichoelezea kwenye namba moja hapo juu, utaona kwamba swala la uongozi ni la muhim sana katika kufanikisha mageuzi. Uongozi wenye dhamira ya kweli ya mabadiliko ni wa lazima kuelekea kwenye uhalisia wa mageuzi munayoyataka.
  1. Uongozi ndio unaweza kufanikisha mchakato wa mageuzi, kuuchelewesha na hata kuuzuia. Hili liko dhahiri kwenye mchakato uliofanya na tume ya kina HP. Tumeona jinsi ambavyo uongozi ulisaidia kunzisha safari ya mageuzi na ikafanikiwa. Hata hivyo tumeona kwamba, uongozi (kwa maana ya chama na seriakali yake) haukua "umejilipua" kwa maana ya kutaka kuruhusu MAGEUZI makubwa yatokee kulingana na dhamira na kiu ya wananchi. Kwa lugha nyingine, vijana wangesema "wamelinzisha huku wakiwa hawajajiandaa wala kujua litaagharimu kiiasi gani". Wameanzisha mchakato lakini baadaye wakaona kuna "maslahi" mengi yanakwenda kuingiliwa au kuzibwa na hivyo wakaanza kupambana tena kuzuia MABADILIKO ambayo ni hatua muhim ya kuelekea MAGEUZI (rejea hoja yangu ya upinzani wa mabadiliko).
  1. Uongozi lazima uwe na dhamira ya kweli ya kutaka mageuzi hata kama wako watakaogharamika kwa mageuzi hayo. Huwezi kusema unataka mageuzi wakati unaongozwa na utawala unaoyapinga mageuzi hayo au kukubali tu baadhi ya mabadiliko na kukataa mengine. Kumbuka mageuzi ni mabadiliko yaliyokamilia; hivyo kuzuia baadhi ya mambo yanayohitajika hakutakamilisha mageuzi tarajiwa na itakua ni sawa na "kuzuia mafuriko kwa mkono" au "kuzuia nguvu ya kimbunga kwa kanga"


 1. Mageuzi yana gharama kubwa: watu wanapotaka mageuzi ni lazima watambue kuna gharama kubwa sana katika kuyapata. Hivyo ni lazima wakae chini na kutafakari vema kabla ya kuanza "SAFARI YA MAGEUZI". Pamoja na kwamba kiu ya mageuzi inaanza kwa mamauzi ya mlipoko wa mabadiliko (unplanned change), ni lazima kutumia mfumo wa "planned change" katika kuyafikia mageuzi. Ni lazima kufanya tathimini sahihi na kuwa na makubaliano na maridhiano.


  1. Ukitazama mchakato wa katiba mpya uatona kabisa kwamba moja ya changamoto ya kuyafikia mageuzi tunayoyataka ni hali ya kutojianda baada ya maamuzi ya mabadiliko kufanyika. Hatukujiandaa kirasilimali na hatukujipa nafasi ya kutosha kutafuta muafaka wa jinsi tunayafikia mageuzi. Matokeo yake kumekua na gharama kubwa ambazo hatukizitegemea na mchakato "umekwenda likizo yenye malipo" lakini isiyo na muda maalumu.


  1. Kwa upande wa watu binafsi, utaona kuna watu wameogopa kupoteza nafasi zao. Nakumbuka gazeti moja lilimnukuu mmoja wa watangaza nia wa urais wa CCM akiwa mkoa wa Shinyanga. Pamopja na mambo mengine alinukuliwa "akiwatisha" aliokua anaowamba udhambini kwamba wakikubali upinzani washinde mwaka huu kutakua na hatari na mingoni mwa hatari hizo ni kuondolewa kwa "vyeo vya  ukuu wa wilaya". Kule Kenya baada ya utekelezaji wa katiba mpya uliopeleka mamlaka zaidi kwa wananchi (devolution), wako watu walikua na vyeo kama "machifu" ambao ni sawa na wakuu wa wilaya. Hawa wote walipoteza kazi nchi nzima na halikua jambo jepesi.


 1. Mageuzi yanahitaji muda: Ili kuyafikia mageuzi kunahitajika muda wa kutosha kuhakikisha msingi umetengemaa na kila tofali la mabadiliko linawekwa mahali sahihi maana kama kukikosewa mahali gharama ya kuvunja na kuanza upya ua kukarabati ni kubwa sana. Hivyo hakuhitaji haraka na maamuzi ya kulipuka yanayoendeshwa na hisia na miheuko.


  1. Kwenye mchakato wa katiba yetu tumeliona hili. Katika harakati za CCM kuhakikisha inapatikana katiba "inayokidhi matakwa ya chama", mchakato mzima umeleta shida, umekua na gharama kubwa na uliingilia hata mandalizi ya uchaguzi mkuu
  2. Uharaka uliosukumwa na dhamira zingine, ulipelekea maamuzi ya kugeuza tu bunge la kawaida kuwa la katiba bila kutazama kwa undani madhara yake na kilichotokea wote twakijua na ni historia.
  3. Uharaka wa kutaka kufikia mageuzi ya katiba mpya, uliliweka taifa katika hali ngumu ya kifedha kwani kulikua na matumizi makubwa ya mchakato huu kuliko matarajio
  4. Uharaka ulipelekea tume ya kina HP ambayo ilikua bado yatakiwa sana kufanikisha mchakato, "KUKATWA" kukiwa bado asubuhi kabisa na viongozi wao kulalamika kwamba kulikua na sintofahamu kwenye namna kazi ya ilivyohitimishwa


 1. Kuelekea MAGEUZI, kuna mahali pa kuanzia na tunawatumia watu wa jamii ileile
  1. Jamii inapohitaji mageuzi ni yenyewe inahusika na mageuzi husika. Jamii ndio wasanifu na wajenzi kuelekea kwenye mageuzi. Tunapozungumzia mageuzi ya kiutawala na mifumo katika taifa, pamoja na ukweli kwamba huenda sisi wenyewe ndio waharibifu wa mambo, bado ndio tutahusika katika harakati za mageuzi. Hatutegemei kuingiza watu toka nchi jirani kutusaidia kuleta mageuzi. Niliwahi kuambiwa habari ambazo sijazithibitisha kwamba kuna Rais wa nchi moja aliunda tume ya kuchunguza tuhuma za rushwa na alidhamiria kupambana nayo. Alipoletewa repoti na tume yake na kuipitia, aliiamua kuifungia kabatini na kwenda kunywa pombe kwanza kwani kila aliyemjua serikali ikiwa ni pamoja na wasaidizi wake wa karibu, walitajwa kama wahusika wakuu wa rushwa. Hata hivyo katika uongozi wake, alifanikiwa kubadili baadhi ya mambo kwa kuwatumia watu walewale waliotajwa kuhusika na rushwa


  1. Safari ya mageuzi sio lazima iletwe na watu wapya kwa maana ya sura mpya, bali inaletwa na watu walewale. Kinachohitajika tu ni NIA YA DHATI ya ya kuleta mageuzi na UONGOZI THABITI WENYE NIA NA UTAYARI wa kuleta mageuzi. Haya mawili ndio ya msingi na kuyatafuta tunapotaka kuamua au kuchagua ni nani wa kutuongoza kuelekea kwenye mageuzi tunayoyataka. Ushawishi unaosambaa kwamba mtu au watu waliokua sehemu ya mfumo usiotaka mageuzi hawawezi kusaidia au kuongoza kuleta mageuzi una ukakasi. Ushawishi huu waweza kuwa wa kweli pale tu mtu au watu hao wanakosa mambo mawili niliyoyataja: yaani Nia ya dhati na Uongozi thabiti wenye nia na utayari wa mageuzi.


Ninakuachia wewe msomaji uliyesoma mfululizo wa makala hizi, upime na kuchuja ukweli kuhusu msimamo na kauli za ndugu HP kuhusu Mabadiliko na Mageuzi. Pia ujaribu kuhitimisha dhana nzima ya Maadili, Ukweli, Haki na Mabadiliko kama inavyosimimiwa na HP dhidi ya UKAWA na EL. Waweza kujiuliza mambo kadhaa:


Moja: Ni kweli kwamba Tanzania kwa sasa haihitaji mabadiliko ya uongozi kwa maana ya chama kinachotawala kwa maana ya sera mpya, fikra mpya, utaratibu mpya na misimamo tofauti na ulioko?


Mbili: Kati ya CCM (walioikata katiba ya kina HP/wananchi) na UKAWA (walioitetea na wanaoitetea katiba ya kina HP/wananchi), nani yuko kwenye nafasi nzuri ya kuleta mageuzi iwapo tutawachagua kuongoza nchi katika uchaguzi ujao?


Tatu: Kwa hali tuliyonayo sasa, je, twahitaji mtu mmoja anayedaiwa ni msafi kama njia pekee ya kuelekea mageuzi au tunahitaji mabadiliko ili kuelekea mageuzi?


Nne:  Kwa nini HP anamwandama EL kwa kauli kali na ngumu kama vile wana ugomvi wa jambo binafsi? Je hii ni sehemu ya MAGEUZI?


Tano: Kama EL alitoa maoni yake kinyume na matakwa ya HP, nini ulikua msingi wa kutafuta maoni? Walikua wanatafuta maoni yanayofanana toka kwa kila mtu? Je, kupambana na waliotoa maoni yao kinyume na wengi, ilikua moja ya majukumu ya wanatume kama yeye?


Sita: Kama hatukuruhusiwa kutoa maoni tofauti kwenye mchakato wa katiba, sasa tunatafuta maridhiano na makubaliano ya nini? Mwisho wa kazi ya tume ilikua ni uzito wa maoni ya mtu mmoja mmoja au ni jumuisho la mambo yaliyoonekana yana uzito zaidi kwenye jamii?


Saba: Ni kweli kwamba adui mkubwa kuliko wote wa katiba mpya na maadili yake alikua EL pekee? Na hata kama ilikua hivyo, ni dhambi gani leo akikubaliana na aliowapinga?


Nane: Kama leo twashabikia HP kumvua EL nguo hadharani kwa misingi ya kutetea maadili na mageuzi, je, tuko tayari kesho kushabikia akimvua nguo Rais wetu akitoka madarakani au kuwavua wengine ambao atakua na "mapambano binafsi" kama afanyavyo kwa EL?


Sitaendelea na Mada hii.


Mwalimu MM ni mhadhiri katika kitengo cha Sayansi ya ya Kompyuta ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Mtafiti wa mifumo ya TEHAMA (ICT) katika Huduma za Afya (Health Informatics). Unaweza kuwasiliana naye kupitia [email protected] na kusoma makala zake kupitia: http://mwalimumm.blogspot.com

UN yapanda zaidi ya miti 2,000 ili kuunusuru mlima Kilimanjaro

Mgeni rasmi Mwakilishi wa Makamu wa Rais, Waziri wa nchi ofisi ya Makamu wa Rais anayeshughulikia Mazingira, Binilith Mahenge (wa pili kushoto) akiwasili kwenye kijiji cha Marua kata Kiruavunjo, mkoani Kilimanjaro kwa ajili kupanda miti ikiwa ni sehemu ya shamrashamra ya maadhimisho ya miaka 70 ya Umoja wa Mataifa na kupokelewa na Mratibu Mkazi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa na Mwakilishi wa Shirika la Maendeleo (UNDP) nchini, Alvaro Rodriguez (wa pili kulia) pamoja na Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Celestine Mushy (kushoto). (Picha zote: Zainul Mzige/modewjiblog).

*Sehemu ya Shamra shamra za maadhimisho ya miaka 70 ya Umoja wa Mataifa

Na Mwandishi wetu, Moshi

MASHIRIKA ya Umoja wa Mataifa yaliyopo nchini yameadhimisha miaka 70 ya kuundwa kwa umoja huo kwa kupanda zaidi ya 2000 katika miteremko ya mlima Kilimanjaro.

Kazi ya kupanda miti ilifanywa na wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa na wadau wao ikiwemo serikali ya Tanzania pamoja na wanakijiji.

Kazi ya kupanda miti iliongozwa na Mratibu Mkazi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa na Mwakilishi wa Shirika la Maendeleo (UNDP) nchini, Alvaro Rodriguez akishirikiana na Mwakilishi wa Makamu wa Rais, Waziri wa Nchi ofisi ya Makamu wa Rais anayeshughulikia Mazingira, Binilith Mahenge.

Shughuli hizo za kupanda miti zilifanyika katika kijiji cha Maruwa.

Akizungumza wakati wa shughuli hiyo Waziri Mahenge alisema kwamba amefurahishwa na hatua iliyochukuliwa na Umoja wa Mataifa ya kuadhimisha miaka 70 kwa kuwakumbusha washirika wao wa maendeleo suala la mazingira.

“Ni kawaida kuadhimisha kuundwa kwa Umoja wa Mataifa Oktoba 24 kila mwaka. Mwaka huu ni tofauti na zaidi ya tofauti umekuwa maalumu kwa namna yake kwa kuwa tunaadhimisha miaka 70 ya uwapo wa Umoja wa Mataifa.” alisema Waziri Mahenge.

Balozi wa Ireland nchini Tanzania, Bi Fionnuala Gilsenan akiwasili kwenye sherehe ya kupanda miti katika kijiji cha Marua ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 70 ya Umoja wa Mataifa na kusalimiana na Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Idadi ya watu duniani (UNFPA) nchini, Dkt. Natalia Kanem.
Hata hivyo alikumbusha kwamba wakati tunaadhimisha miaka 70 ni vyema wadau wa maendeleo wakaangalia historia na kujipanga kimkakati katika kusonga mbele kimaendeleo kwa kujali mazingira.

Alisema kwamba pamoja na hoja ya kujali mazingira pia serikali itaendelea kushirikiana na mashirika ya Umoja wa Mataifa katika mambo mbalimbali ya maendeleo.

Akizungumzia umuhimu wa siku hiyo ya kupanda miti, Rodriguez, alisema kauli mbiu ya wa mwaka huu ni “Sayari Moja Watu Bilioni 7: Utunzaji Mazingira ni Wajibu Wetu”, umerandana na shughuli hizo za upandaji miti.

Alisema kitendo cha upandaji miti kunaonesha wajibu wa kwanza wa kuhami mazingira ya sayari yetu kwa manufaa ya kizazi kijacho cha wanadamu.

Alisema mabadiliko ya tabia nchi si utani yapo kweli na ipo haja ya kuendelea kuwapo kwa juhudi za makusudi za wakazi wa dunia hii kulinda mazingira kwa ajili ya amani maendeleo na ustawi.

Mgeni rasmi Mwakilishi wa Makamu wa Rais, Waziri wa nchi ofisi ya Makamu wa Rais anayeshughulikia Mazingira, Binilith Mahenge akisoma hotuba kwa niaba ya Makamu wa Rais kwenye sherehe za upandaji miti katika kijiji cha Marua ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 70 ya Umoja wa Mataifa.

Kwa upande wake balozi wa Ulaya alisema upandaji miti katika mteremko wa mlima Kilimanjaro kuadhimisha miaka 70 ya Umoja wa Mataifa ni alama muhimu katika mapambano ya wanadamu kulinda mazingira.

Alisema ishara hiyo muhimu inaelekeza Umoja huo na wadau wake wa maendeleo kuchukua tahadhari za kutosha kulinda mazingira na inakwenda sanjari na malengo endelevu ya milennia (SDGs) ambayo yana mada tano za kuangaliwa katika mazingira kuliko yale ya awali ambayo yalikuwa na mada moja tu.

Msemaji wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa, Hoyce Temu alisema kwamba upandaji miti uliofanyika ni moja ya shughuli kadhaa zitakazofanywa na Umoja huo kuadhimisha miaka 70 toka kuanzishwa kwake.

Shughuli nyingine itakayofanywa ni kusafisha soko la Temeke, mashindano ya uchoraji kwa vijana na maadhimisho ya siku yenyewe.


Mratibu Mkazi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa na Mwakilishi wa Shirika la Maendeleo (UNDP) nchini, Alvaro Rodriguez akitoa salamu za Umoja wa Mataifa katika sherehe ya upandaji miti kwenye kijiji cha Marua ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 70 ya Umoja wa Mataifa zilizofanyika mkoani Kilimanjaro.

Sikiliza kionjo cha hotuba ya Kiswahili ya Mratibu Mkazi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa na Mwakilishi wa Shirika la Maendeleo (UNDP) nchini, Alvaro Rodriguez hapa chini.Mkuu wa Jumuiya ya Umoja wa Ulaya, Balozi Filiberto Sebregondi akizungumza kwenye sherehe ya upandaji miti katika kijiji cha Marua ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 70 ya Umoja wa Mataifa zilizofanyika mkoani Kilimanjaro.


Wakufunzi kutoka chuo cha Ualimu Moshi wakitoa burudani kwenye hafla ya kupanda miti katika kijiji cha Marua ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 70 ya Umoja wa Mataifa.


Pichani juu na chini ni baadhi ya wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa na wanakijiji wa kijiji cha Marua walioshiriki sherehe za upandaji miti ikiwa ni Shamra shamra ya kusheherekea miaka 70 ya Umoja wa Mataifa.
Mgeni rasmi Mwakilishi wa Makamu wa Rais, Waziri wa nchi ofisi ya Makamu wa Rais anayeshughulikia Mazingira, Binilith Mahenge akipanda mti katika kijiji cha Marua karibu na miteremko ya mlima Kilimanjaro, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 70 ya Umoja wa Mataifa yaliyofanyika mkoani Kilimanjaro.


Afisa Misitu wa mkoa wa Kilimanjaro, Emanuel Kiyengi (kulia) akitoa maelezo kwa mgeni rasmi, mabalozi na viongozi wa serikali katika eneo maalum lililotengwa kwa ajili ya kupanda miti 200 zoezi lililoendeshwa na Umoja wa Mataifa nchini katika kusheherekea miaka 70 ya Umoja wa Mataifa.


Mgeni rasmi Mwakilishi wa Makamu wa Rais, Waziri wa nchi ofisi ya Makamu wa Rais anayeshughulikia Mazingira, Binilith Mahenge akiteta jambo na Mratibu Mkazi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa na Mwakilishi wa Shirika la Maendeleo (UNDP) nchini, Alvaro Rodriguez.


Mgeni rasmi Mwakilishi wa Makamu wa Rais, Waziri wa nchi ofisi ya Makamu wa Rais anayeshughulikia Mazingira, Binilith Mahenge (wa tatu kushoto) akikata utepe kuashiria uzinduzi wa eneo maalum lililotengwa kwa ajili ya kupanda miti 2000 katika kijiji cha Marua karibu na miteremko ya mlima Kilimanjaro. Wanaoshuhudia tukio hilo ni Mratibu Mkazi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa na Mwakilishi wa Shirika la Maendeleo (UNDP) nchini, Alvaro Rodriguez (wa pili kushoto), Mkuu wa ofisi ya Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO), Zulmira Rodrigues (kushoto), Mkuu wa mabalozi, ambaye pia ni Balozi wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (DRC), Juma Halfan Mpango (wa nne kushoto), Balozi wa Ireland nchini Tanzania, Bi Fionnuala Gilsenan (wa tano kushoto), Mkuu wa Jumuiya ya Umoja wa Ulaya, Balozi Filiberto Sebregondi (wa nne kulia), Mkuu wa wilaya ya Moshi, Novatus Makunga ( wa tatu kulia), Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Celestine Mushy ( wa pili kulia) pamoja na Afisa Tawala Mkuu katika ofisi ya Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro, Omari Msuya.


Mkuu wa wilaya ya Moshi, Novatus Makunga akishiriki zoezi la kupanda miti katika kijiji cha Marua.


Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Celestine Mushy (kushoto) akitoa maelekezo kwa Mkuu wa ofisi ya Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO), Zulmira Rodrigues (kulia) wakati wa zoezi la upandaji miti.


Mkuu wa ofisi ya Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO), Zulmira Rodrigues akishindilia udongo kwenye mti aliopanda katika eneo lake.


Kaimu Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo (UNDP), Titus Osundina akishiriki zoezi la upandaji miti katika kijiji cha Marua mkoani Kilimanjaro.


Balozi wa Ireland nchini Tanzania, Bi Fionnuala Gilsenan akishiriki zoezi la kupanda miti lililoendeshwa na Umoja wa Mataifa ikiwa ni sehemu ya kusheherekea miaka 70 tangu kuanzishwa kwake duniani.


Afisa Habari wa Kituo cha Habari cha Umoja wa Mataifa (UNIC), Usia Nkhoma Ledama akishiriki zoezi la kupanda mti katika kijiji cha Marua.Wakinamama wa kijiji cha Marua wakipozi miti yao wakati wakielekea kuunga mkono juhudu za Umoja wa Mataifa katika kukabiliana na mabadiliko ya Tabianchi.


Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Celestine Mushy (kulia) wakitazama jambo na Mkuu wa ofisi ya Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO), Zulmira Rodrigues wakati wa zoezi la kupanda miti katika miteremko ya mlima Kilimanjaro kijiji cha Marua mkoani Kilimanjaro.


Baadhi ya maafisa wa Wizara ya Mambo ya Nje na Umoja wa Mataifa wakijadiliana jambo na mshehereshaji wa hafla hiyo.


Mgeni rasmi Mwakilishi wa Makamu wa Rais, Waziri wa nchi ofisi ya Makamu wa Rais anayeshughulikia Mazingira, Binilith Mahenge akikata utepe kuzindua jiwe la kumbukumbu la miaka 70 ya Umoja wa Mataifa kwenye eneo maalum lililopandwa miti 2000 katika kijiji cha Marua, mkoani Kilimanjaro. Wanaoshuhudia tukio hilo ni Mratibu Mkazi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa na Mwakilishi wa Shirika la Maendeleo (UNDP) nchini, Alvaro Rodriguez (kulia), mabalozi wanaowakilisha nchi zao Tanzania pamoja na viongozi mbalimbali wa Serikali.


Zoezi la uzinduzi likiendelea.


Mgeni rasmi Mwakilishi wa Makamu wa Rais, Waziri wa nchi ofisi ya Makamu wa Rais anayeshughulikia Mazingira, Binilith Mahenge katika picha ya pamoja na mabalozi waalikwa, viongozi wa Serikali na wakuu wa mashirika ya Umoja wa Mataifa Tanzania.


Picha ya pamoja ya wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa na mgeni rasmi.


Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Idadi ya watu duniani (UNFPA) nchini, Dkt. Natalia Kanem akipata picha ya kumbukumbu na wanakijiji wa kijiji cha Marua.

DMV All Stars video - Najivunia

Msiba wa Bi Khadija Kube

Msiba wa Bi Khadija Kube
Bi. Khadija Ismail Kube
Tunasikitika kutangaza kifo cha ndugu yetu Bi. Khadija Ismail Kube maziko yatafanyika siku ya Ijumaa 21 -08-2015, saa 4.00 asubuhi nyumbani kwao mtaa Aggrey. Kariakoo msikiti wa Qiblatein mwenyezimungu amlaze mahala pema peponi.

Taarifa zimetolewa na Masjid Qubah, Segerea Mwisho, Dar es Salaam.

Innalilahi Wainna Iilahi Rajiunn!

----
Taarifa hii imewasilishwa kwetu na "Msema Kweli"

Ireland yawapa ufadhili wa masomo Watanzania 14

Balozi wa Ireland nchini Tanzania, Bi. Fionnuala Gilsenan, akizungumzia kuhusu ufadhili kwa Watanzania wanaokwenda vyuo mbalimbali vya ndani na nje ya nchi. Sherehe hizo zimefanyika Alhamisi, Agosti 20, 2015 kwenye ofisi za ubalozi huo Masaki jijini Dar es Salaam.
SERIKALI ya Ireland kupitia Ubalozi wake nchini Tanzania, leo Agosti 20, 2015 imekabidhi scholarship kwa Watanzania 14 ambao watakwenda kusomea kozi mbalimbali za shahada ya uzamili (masters) ambapo wanne kati yao wakienda kusoma vyuo vikuu nchini Ireland.

Akikabidhi hati hizo za ufadhili wa masomo, Balozi wa Ireland nchini Tanzania, Bi. Fionnuala Gilsenan, alisema utaratibu wa kutoa ufadhili kwa wataalamu mbalimbali ni jambo la msingi kutokana na ukweli kwamba ujuzi watakaoupata unaweza kuliletea taifa maendeleo.
“Ufadhili huu ni sehemu ya Mpango wa Mafunzo wa Kila Mwaka (Fellowship Training Programme), katika sukuma mbele maendeleo ya nchi washirika wetu, tunadhani tunao wajibu wa kusaidia pia kuwaelimisha watalaamu wao,” 
Aliwataja wanufaika wanne waliobahatika kwenda ng’ambo kuwa ni Stella Zakayo Munisi, Meneja Rasilimali Watu na Utawala wa Shirika la Sikika, ambaye anakwenda kusomea shahada ya uzamili (Organizational Development and Change) na Cosmas Joseph Mworia, Ofisa Ushirika na Ofisa Ufuatiliaji na Ukadiriaji katika Kilimo wa Halmashauri ya Wilaya Kondoa anayekwenda kusomea shahada ya uzamili katika Kilimo Endelevu na Maendeleo Vijijini (Sustainable Agriculture and Rural Development). Wawili hao wanakwenda katika Chuo Kikuu cha Dublin.

Flavian Majenga Lihwa, Mratibu Programu ya Elimu wa Shirika la Care Tanzania yeye anakwenda Chuo Kikuu cha Dublin Institute of Technology kuchukua shahada ya uzamili katika Maendeleo Endelevu (Sustainable Development) na Zabron Elias Masatu, Mganga Mkuu wa Wilaya (DMO) ya Misenyi yeye anakwenda Chuo Kikuu cha Taifa cha Ireland Maynooth (NUIM) kuchukua shahada ya uzamili ya Immunolojia na Afya (Immunology and Global Health).

Wanufaika wengine 10 wa mwaka huu, kozi na vyuo wanavyokwenda vikiwa kwenye mabano ni, Siwajibu Ally Selemani Malenge, Kaimu Ofisa Kilimo/Umwagiliaji na Ushirika wa Wilaya ya Kigoma (Chuo Kikuu cha Sokoine – Elimu ya Kilimo na Ushauri ‘Agricultural Education and Extension’); Edita Byangwamu Rutatora Kokwijuka, Ofisa Kilimo Daraja la Kwanza kutoka Wilaya ya Muheza (Chuo Kikuu cha Sokoine – Kilimo); Doreen Elias Mangesho, Mhasibu Mkuu wa CCBRT (Chuo Kikuu cha Dar es Salaam – Utawala wa Fedha); Elinlaa Michael Kivaya, Mchumi wa Kilimo wa Wilaya ya Ngorongoro (Chuo Kikuu cha Sokoine – Kilimo na Uchumi Mtambuka ‘Agriculture and Applied Economics’); na Joshua Julius Musimu, Mkufunzi wa Kilimo Daraja la Pili kutoka Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika (Chuo Kikuu cha Sokoine – Uchumi wa Kilimo ‘Agricultural Economics’).

Wengine ni Fredrick Pius Massawe, Ofisa Kilimo Daraja la Kwanza kutoka Ofisi ya Katibu Tawala Mkoa wa Kilimanjaro (Chuo Kikuu cha Sokoine –Kilimo); Samuel Korinja Olekao, Mratibu wa Kinnapa Development Programme (Chuo Kikuu cha Sokoine – Utunzaji wa Maliasili na Kilimo Endelevu); Eva Emmanuel Mbambale, Ofisa Program wa Sikika (Chuo Kikuu cha Makerere,Uganda – Afya ya Jamii); Iddi Alfani Shekabugi, Mchumi Daraja la Kwanza katika Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika (Chuo Kikuu cha Mzumbe – Uchumi na Fedha kwa Maendeleo); na Felix Lyope Lubuga, Ofisa Utafiti wa Taasisi ya Afya Ifakara (Chuo Kikuu cha Dar es Salaam – Afya ya Jamii).

Awali, Balozi Fionnuala aliwatunuku vyeti wanufaika wengine 10 waliomaliza mwaka 2013 na 2014 katika fani mbalimbali.

Hao ni Deogratias Gabriel Rugarabamu, Ofisa Tabibu wa Wilaya ya Kilindi (Chuo Kikuu cha Tumaini, KCMC – Medical Entomology and Clinical Parasitology); Pudensiana Clement Panga, Ofisa Uvuvi kutoka Wizara ya Mifugo na Maendeleo ya Uvuvi (Chuo Kikuu cha Sokoine – Sayansi ya Chakula); Fatma Ally Mwasola Libaba, Ofisa Utafiti (Lishe) kutoka Taasisi ya Chakula na Lishe (Chuo Kikuu cha Sokoine – lishe ya Binadamu); Rubea Mohammed Ali, Mkuu wa Idara katika Wizara ya Kilimo na Maliasili, Zanzibar (Chuo Kikuu cha Sokoine – Elimu ya Kilimo na Ushauri ‘Agricultural Education and Extension’); na David Eliatosha Lekei, Ofisa Kilimo Wilaya ya Hai (Chuo Kikuu cha Sokoine – Elimu ya Kilimo na Ushauri ‘Agricultural Education and Extension’).

Wengine waliohitimu mwaka 2014 ni John Nobert Kirway, Mkufunzi Mkuu wa Mifugo wa Wizara ya Mifugo na Maendeleo ya Uvuvi, Arusha (Chuo Kikuu cha Sokoine –Tropical Animal Production); Teddy Frederick Dionis Mamboleo, Ofisa Utafiti (Lishe) kutoka Taasisi ya Chakula na Lishe (Chuo Kikuu cha Sokoine – Lishe ya Binadamu); Adam Khamis Haji, Ofisa Mipango na Utawala, Wizara ya Kilimo na Maliasili, Zanzibar (Chuo Kikuu cha Sokoine – Maendeleo Vijijini); Jacob Polycarp Ngowi, Mkufunzi wa Masuala ya Mifugo kutoka Wizara ya Mifugo na Maendeleo ya Uvuvi (Chuo Kikuu cha Sokoine –Tropical Animal Production); na Mussa Said Bakari, Meneja wa Maeneo Tengefu – Pemba kutoka Wizara ya Kilimo na Maliasili, Zanzibar (Chuo Kikuu cha Sokoine – Utunzaji wa Maliasili na Kilimo Endelevu).

Mpango huo wa Mafunzo wa kila Mwaka unahusisha Mfuko wa Misaada wa Ireland (Irish Aid) kupitia program ya maendeleo ya Ubalozi huo nchini Tanzania.

Wanufaika wa mpango huo wameteuliwa na washirika wa maendeleo wa Ireland nchini Tanzania, zikiwemo wizara mbalimbali za Serikali, halmashauri za wilaya na mashirika yasiyo ya kiserikali, ambayo shughuli zao zinawiana na maeneo ya vipaumbele vya Irish Aid, hususan Kilimo, Afya, Lishe na Utawala.

Aidha, wanufaika wote ni watendaji wa kati ambao baada ya kuhitimu masomo yao watarejea kwenye mashirika na taasisi zao kutumia ujuzi walioupata kwa manufaa ya jamii.
“Kwa wanufaika watakaokwenda kusoma nchini Ireland, program inatoa fursa nzuri ya kujifunza katika hadhi ya kimataifa na kunufaika na hazina kubwa ya nyenzo za tafiti zinazotolewa kwenye Vyuo Vikuu na Taasisi za Teknolojia za Ireland,” 
“Inatarajiwa kwamba mafunzo ya wataalamu hawa yatachangia kwa kiasi kikubwa maendeleo ya Tanzania, na kuendelea kuimarisha ushirika wa kielimu baina ya Ireland na Tanzania.”
Ireland, kupitia Mfuko wa Misaada (Irish Aid), imekuwa ikidhamini Mpango huo wa Mafunzo nchini Tanzania kwa miaka 40 sasa ambapo program hiyo imekuwa msingi wa msaada katika kuzijengea uwezo nchi zinazoendelea na inaendana na mkakati wa kupunguza umaskini wa nchi washirika wa Ireland, hasa lengo likiwa kuwapatia wataalamu elimu ya juu ili waendeleze taasisi zao.


Baadhi ya wanufaika wa ufadhili huo wakimsikiliza Balozi wa Ireland (hayuko pichani).


Baadhi ya wafanyakazi na wageni waalikwa wakimsikiliza Balozi Gilsenan.


Deogratias Gabriel Rugarabamu, Ofisa Tabibu wa Wilaya ya Kilindi, akipokea cheti cha shukrani baada ya kuhitimu shahada ya uzamili ya Medical Entomology and Clinical Parasitology katika Chuo Kikuu cha Tumaini, KCMC .


Balozi Fionnuala Gilsenan wa Ireland akimpongeza Rubea Mohammed Ali, Mkuu wa Idara katika Wizara ya Kilimo na Maliasili, Zanzibar baada ya kuhitimu shahada ya uzamili katika Chuo Kikuu cha Sokoine katika Elimu ya Kilimo na Ushauri (Agricultural Education and Extension).


David Eliatosha Lekei, Ofisa Kilimo Wilaya ya Hai akipokea cheti cha shukrani kutoka kwa Balozi wa Ireland nchini, Bi.Fionnuala Gilsenan baada ya kuhitimu shahada ya uzamili kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine katika Elimu ya Kilimo na Ushauri (Agricultural Education and Extension).


Mshereheshaji akisoma majina ya wanufaika.


Stella Zakayo Munisi, Meneja Rasilimali Watu na Utawala wa Shirika la Sikika, akipokea hati ya ufadhili kwenda kusomea shahada ya uzamili kuhusu Organizational Development and Change katika Chuo Kikuu cha Dublin, Ireland. 

 • Imeandaliwa na www.brotherdanny.com. Simu 0656-331974
 • Tumeshirikishwa picha na habari na Daniel Mbega