Nyumba ya mwania Ubunge yavamiwa na kubomolewa


Kundi la watu wasiojulikana usiku wa kuamkia leo wamevamia na kuibomoa nyumba ya mgombea ubunge wa chama cha wananchi CUF jimbo jipya la nanyamba wilaya ya mtwara vijijini, twahiri saidi baada ya kushindwa kurudisha fomu ya ubunge na kutokomea kusiko julikana huku simu zake za mkononi zikiwa hazipatikani.

Wakizungumza kwa masikitiko baadhi ya viongozi wa chama hicho na wanachi wa jimbo la Nanyamba wamesema mazingira aliyotoweka mgombea huyo yanaonyesha wazi kuna mchezo mchafu umefanywa ili kutoa fursa kwa mgombea wa CCM, Abdallah Chikota kupita bila kupingwa katika jimbo hilo.

Akizungumzia tukio hilo katibu kata wa CUF kata ya Milango Minne eneo analotoka mgombea huyo, amesema mwisho wa kuwasiliana na mgombea huyo ilikuwa majira ya saa saba akimuhimiza kuwahisha fomu kwa msimamizi wa uchaguzi.

Hata hivyo anasema majibu ya mgombea huyo yalionyesha wazi kuna jambo baada ya kudai hawezi kuacha ajira yake na kuingia kwenye kinyang’anyiri cha uchaguzi wakati viongozi wa CUF taifa walimuaidi kumpa shilingi milioni 30 kwa ajili ya uchaguzi na wameshindwa kufanya hivyo na baada ya maneno hayo simu zake hazikuweza kupatikana mpaka muda huu.

Kwa upande wake mkurugenzi wa halmashauri ya maji wa nanyamba oscar ng’itu ambaye aliongozana na mkuu wa kituo cha polisi nanyamba alitembelea nyumba iliyobomolewa na kutoa agizo kwa wananchi kuwataja watu waliyohusika na tukio hilo vinginevyo mkono wa sheria utachukua mkondo wake.
 • Taarifa hii imenukuliwa kutoka ITV

Kafulila amwekea pingamizi mgombea Ubunge kutoka CCM

MGOMBEA Ubunge kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi, CCM, Jimbo la Kigoma Kusini, Hasna Sudi Mwilima, amewekewa pingamizi na mbunge anayemaliza muda wake katika jimbo hilo kwa tiketi ya Chama cha NCCR-Mageuzi, David Kafulila.

Mgombea huyo amewekewa pingamizi hilo kwa kushindwa kujaza fomu kwa kufanya makosa matatu ya kisheria.

Kwa mujibu wa chanzo chetu cha habari: 
 1. Kosa namba moja kwenye fomu 8B ametumia majina matatu tofauti: HASNA SUDI KATUNDA MWILIMA, HASNA MWILIMA na HASNA S. K. MWILIMA.
 2. Aidha kosa namba mbili kwenye tamko la wadhamini imeandikwa amedhaminiwa kuteuliwa tarehe 25.10.2015 badala ya tarehe 21.8.2015.
Sheria inamtaka mgombea ajaze majina yake kamili na kwa mazingira hayo mgombea huyo hajulikani majina yake kamili ni yapi, vinginevyo anatakiwa kupeleka document iitwayo “deed poll” inayotambua majina yote hayo kuwa ni yake.

Kufuatia mkanganyiko huo David Kafulila jana jioni aliweka pingamizi dhidi ya mgombea huyo na kudai kuwa anapswa kuenguliwa kwenye uchaguzi mkuu ujao.

CHADEMA Kishapu wavamia ofisi kupinga mgombea


Muda mfupi kabla mgombea ubunge kwa tiketi ya CHADEMA jimbo la Kishapu mkoani Shinyanga Bw. Fred Mpendazoe kurudisha fomu, baadhi ya wanachama wa chama hicho wameandamana na kuvamia ofisi ya chama kwa madai kuwa hawakubaliani na kitendo cha kamati kuu ya wilaya kubadilisha matokeo ya kura za maoni na kumtangaza mgombea wasiyemtaka kugombea nafasi hiyo.

Wakizungumza na ITV baadhi ya wanachama hao wamedai kutokubaliana na mapendekezo ya kamati kuu kubadilisha jina la mgombea wao Bw. Donald Kahema waliyekuwa wamemchagua kwa kura mia mbili tisini dhidi ya Fred Mpendazoe aliyepata kura kumi na moja hali inayoonyesha baadhi ya viongozi wanakitumia chama vibaya kwa maslahi binafsi na kutishia kuvuruga chama ambacho wananchi walikiamini kwa muda mrefu kuwa kinaweza kuleta mabadiliko ya kidemokrasia.

Aidha katibu muenezi chadema wilaya ya kishapu Bw. Martin Ganja amekiri kuwepo kwa hali hiyo huku akidai kuwa kamati kuu imekiuka na kupora haki za msingi za wapiga kura na yeye kama kiongozi atasimama imara na kuhakikisha kuwa anapigania haki na maslahi ya wanachama.

Kwa upande wake mwenyekiti wa chadema wilaya ya kishapu Bw. Paulo Magembe amesema kimsingi wanachama wana haki ya kudai haki zao huku akidai kuwa kamati kuu ina wajibu wa kuona ninini wanachama wake wanahitaji ili kukiepusha chama kuingia katika migogoro inaoweza kusababisha chama kuanguka katika uchaguzi mkuu ujao.
 • Imenukuliwa kutoka ITV

Mbunge CHADEMA, Silinde apata ajali akirejesha fomuDavid Silinde
David Silinde

Mbio za Ubunge: Ahama vyama 3 ndani ya juma moja

Modestus Kilufi
Modestus Kilufi
WIMBI la hama hama kutoka katika vyama vya siasa, lililowakumba zaidi makada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) waliokatwa katika kura za maoni kwenda vyama vya upinzani, limeingia katika hatua mpya, baada ya kada mmoja kujikuta akihamia vyama vitatu ndani ya wiki moja, akisaka fursa ya kugombea ubunge.

Mwanzoni mwa wiki hii, kada huyo wa CCM, mbunge anayemaliza muda wake katika Jimbo la Mbarali, Modestus Kilufi, alianza kuhama chama hicho kikubwa na kikongwe katika viwanja vya Ruanda Nzovwe jijini Mbeya, ambako alitangaza kuhamia CHADEMA.

Kilufi aliyeangushwa katika kura ya maoni ndani ya CCM, alichukua hatua hiyo katika mkutano wa hadhara wa kumtambulisha mgombea wa urais wa CHADEMA, Edward Lowassa, ambaye naye alihamia huko baada ya kuanguka katika kinyang’anyiro cha kusaka mgombea urais kupitia chama hicho tawala.

Hata hivyo, Kilufi ambaye hajatimiza hata wiki moja tangu ahamie CHADEMA na kupokewa na uongozi wa Taifa wa chama hicho na mgombea urais wake, jana alikwenda katika Ofisi ya Msimamizi wa Uchaguzi na kuchukua fomu ya kuwania ubunge kupitia chama cha ACT-Wazalendo.

Msimamizi Akithibitisha hatua hiyo ya Kilufi, Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Mbarali, Adam Mgoi, alisema mbunge huyo aliyemaliza muda wake, ni miongoni mwa wagombea wanane waliochukua fomu kugombea ubunge ambapo amewakilisha chama cha ACT Wazalendo.

Akizungumzia hatua hiyo ya mwanachama wake mgeni, Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Mbeya, Joseph China, alidai Kilufi ni msaliti anayeendeshwa na msukumo wa watu wachache.

China alidai Kilufi ni miongoni mwa wanasiasa wasio na msimamo na wasio wazalendo kwa Taifa lao, ndiyo sababu anapigania maslahi yake binafsi badala ya maslahi ya Watanzania wanyonge.

Hata hivyo, ujio wa Kilufi ndani ya ACT ulionekana kuleta mkanganyiko, baada ya uongozi ngazi ya wilaya kugawanyika katika kukubaliana na hatua hiyo. Mwenyekiti wa ACT, Anzuruni Anzuruni alisema anachojua ni kuwa mwanachama aliyechukua fomu kupitia chama hicho ni James Kamanga na Kilufi hamtambui.

Wakati Mwenyekiti wa ACT akitoa kauli hiyo, Katibu wake, Erasto Sanga, alithibitisha kumpokea Kilufi na kutengua uteuzi wa mgombea wa kwanza. Gazeti hili baada ya kujiridhisha kwa Msimamizi wa Uchaguzi, Mwenyekiti wa Chadema na uongozi wa ACT, lilimtafuta Kilufi tangu mchana mpaka jioni, lakini simu zake zote ziliita bila majibu.
 • via HabariLeo

Mndeme: Wanasiasa, viongozi wasituchanganye kwa hoja na hisia dhaifu

Tunapoelekea uchaguzi, wanasiasa na viongozi wasituchanganye Watanzania kwa hoja na hisia dhaifu za kutugawa!!
Mojawapo ya jambo linaloshangaza sana kila tunapokaribia uchaguzi mkuu, hasa kwa miaka kama 15 iliyopita, ni kujitokeza kwa hoja ninazoweza kuziita "za kijinga, dhaifu, mbovu na zenye nia ovu" na lengo la kuwajengea watanzani hisia mbaya dhidi ya umoja na utengamano wetu. Hoja hizi ni zile zinazolenga kuingia "miroho na mipepo" ya udini, ukabila, ukanda, udhehubu, na umikoa katika kutafuta kukubalika na kupata kuungwa mkono. Kwa wale waliopata bahati za kuishi kwenye nchi zenye matatizo hayo kama Nigeria, Kenya, na kwingineno, wanajua kabisa kwamba Tanzania hakuna hayo matatizo "kiivyo" na tunapotumia muda kuyaongelea, ni "kukuza ujinga uonekane ni hekima".
Katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2010 Tanzania ilishuhudia siasa mbaya na chafu nadhani kuliko kipindi chochote kile kwenye historia ya nchi yetu.  Zilikua siasa chafu kwa sababu pamoja na madhaifu mengine, siasa zilijengeka katika ushawishi wa udini na ukabila. Tulishuhudia baadhi ya wagombea wakisimama majukwaani na kufanya kazi ya kuwatisha watu kwa kitu ambacho hatukukiona wala kikijua. Badala ya kutangaza sera na ilani za vyama vyao kama msingi wa kuomba kura, baadhi ya wagombea walisimama majukwaani wakiwashawishi wananchi kwamba kuna udini na ukabila katika siasa na kampeni. Walipiga hatua mbaya zaidi kwa kuanza kuelezea habari za damu kumwagika wakati sisi wananchi wala hatukuyaona hayo waliyokua wanahubiri wao. Matokeo ya kampeni hizi tunayajua na ni kwa jinsi gani uchaguzi ule ulijaa kila aina ya matisho na wasiwasi na kupeleka hata idadi ya wapiga kura kuwa ndogo zaidi katika historia za uchaguzi ukilinganisha na watu waliojiandikisha. Baada ya uchaguzi wa 2010, nchi yetu ilijikuta katika migogoro na mivutano mikubwa iliyosababishwa na wanasiasa waliotumia udini kama mtaji wao wa kupata kura.
Sitasahau siku chache kabla ya siku ya uchaguzi tulishududia simu zetu za mikononi zikipokea ujumbe mfupi (SMS) uliojaa matisho ambayo sitamani kuyanukuu tena. Ilikua asubuhi na mapema nikiwa stendi kuu ya mabasi Ubungo nilipoanza kupokea ujumbe ule na ulinipa simanzi siku nzima nikiitafakari mwelekeo wa nchi yangu. Nilipata hasira na mamumivu sana na nikatamani ningekua na uwezo wa kuwasulubisha wahusika. Hasira yangu iliongezeka nilipogundua ujumbe huo umetumwa kariku kwa kila mtu anayemiliki simu ya mkononi na malalamiko yaliko. Sikua na la kufanya na nilichoweza kufanya ni kuwalaani waliohusika na kwa kuwa hawajahi kutubu kwa watanzania kwa kosa lile, ninaamini laana yangu bado inawaandama na itawaandama hadi watakapotubu. Kitu cha ajabu kuliko vyote, jambo lile "lilipotezewa" kirahisi tu kama vile "sio issue" kwa usalama wa nchi na kama vile hatuna vyombo husika vya kufuatilia na kutoa maelezo.
Inasikitisha kwamba mwaka huu tena uchaguzi unapokaribia hoja za ukabila, ukanda, udini na hata udhehebu zinaanza kuibuliwa. Nimekua nikisikiliza wenye madaraka na wanasiasa wakianza kutoa maonyo ya kidini na kikabila bila kutueleza msingi wa maonyo haya. Nimesoma kwenye mitandao ya kijamii jinsi watu wanavyojenga hoja za miheuko yao ya kisiasa ka misingi ya mambo haya ambayo ni hatarishi sana. Nimeona watu wakijibizana kwenye mitandao ya kijamii juu ya kiongozi gani ni dini gani na ni wa kanda gani. Huku ni kujitoa akili kwa taifa lililostaarabika kama letu.
 • Kwa nini mwamko wa kuongelea udini na ukabila kwa viongozi umeibuka kipindi hiki cha uchaguzi?
 • Wapi kumefanyika siasa za kidini na ni nani wanahusika?
 • Kama wako watu wanaoeneza udini na ukabila kwa nini wasionywe hao na kuwashughulikiwa kisheria.
 • Haya mahubiri ya udini, ukabila, udhehebu, ukanda yanahubiriwa kwa manufaa ya nani na kwa hasara ya nani?
 • Ni kwa nini mahubiri haya yanatolewa na kila kiongozi kwa sasa? Wamantisha nani au wanamtaadharisha nani?
 • Wapi wanasiasa na viongozi hawa walikwenda wananchi wakawaambia tatizo lao kubwa dhidi ya serikali yao ni udini na ukabila?
Katika maisha ya kijamii ya watu wanaoishi pamoja kama watanzania, kuna tofauti na manung'uniko mengi ambayo watu binafsi au makundi ya watu wanaweza kuwa nayo kulingana na mambo kadha wa kadha na zingine hakuna awezaye kuzitolea maelezo ya kueleweka. Mambo kama hayo sio vema kuyakuza na kuyatibua kama hayajaibuka maana kufanya hivyo ni kujiharibia sisi wenyewe.
 • Ya nini kuongelea uhatari wa ugonjwa ambao haupo wala hakuna taarifa ya mtu aliyeugua? Ya nini kuhubiri kuhusu uhatari wa ugongwa wa ebola kila siku wakati watanzania hawajawahi kukutana nao na tuna magonjwa mengine kama malaria na kipindupindu ambayo ndiyo tungetamani kusikia habari za kujikinga na tiba zake?
 • Ya nini kuongelea na kuukuza udini wakati wa kampeni? Umaskini wetu na matatizo yetu yamesababishwa na udini na ukabila? Vilio vya wamama wanaokosa huduma bora za uzazi; vijana waliokosa elimu na ajira; wazee wanaokosa matunzo; mishahara midogo; kukosa huduma za maji na umeme; vimesababishwa na ukabila na udini?
 • Kwa nini tusiongelee mambo ya msingi? Kwa nini wanasiasa waiongelee kutumia muda vizuri? Kwa nini wasiongelee watu kujisomea vitabu ili kupata maarifa? Kwa nini wasiongelee watu kufanya kazi kwa bidii? Kwa nini wasiongelee ubunifu na uvumbuzi?
 • Mbona watu wanakosa amani kwa kuporwa na vibaka kila siku na wakuu hawa hawaongelei tatizo hili sugu kila mara?
 • Mbona usiku ukiingia mitaa haipitiki kwa usalama mbovu na wakuu hawa hawaliongelei kila siku?
 • Badala ya kuimba ngonjera za udini na ukabila na ukanda ambavyo havipo kwa nini wasingeimba umuhim wa  usafi wa nyumba, mitaa na miji ili watu wachukie uchafu na tukae mazingira masafi?
Wataalamu wa saikologia na matangazo ya biashara (marketing) wanatuambia kwamba, mtu akilisikia jambo kila wakati, analizoea na analipa umuhim hata ambao hakua nao kabla. Kusikia jambo kila wakati kunalipandikiza kwenye akili, fkira, hisia na maamuzi ya mtu. Na mbinu hii ndio inatumiwa kuwafanya watu wavutiwe na huduma fulani. Ndio mana Tigo au Voda au Airtel hawaachi kutuwekea matangazo yao yaleyale kila siku kwenye vyombo vya habari maana wanataka kuingiza bidhaa zao ndani ya mioyo yetu ili tujenge mapenzi nazo. Dhana hii hufanya kazi hata kwa mambo maovu pia. Mtu abaye kwa hisia zake anahisi kuonewa au kunyimwa haki au kutothaminiwa (hata kama sio kweli), unapokuja na kuanza kumwelezea kwamba kuna mtu au watu wanamsababishia hayo (hata kama hawako), unayapa matatizo haya uzito na uhalisia nafsini mwake.
Roho hii ya kuhubiri mambo ambayo yako kihisia zaidi kwenye jamii yetu, ndio inayowaendesha hawa wahubiri wa mgawanyiko. Wanataka kuingiza kwenye mioyo ya watu ili kuipa uzito na watu waachane na mambo ya msingi waanze kujadili "tofauti zao na migawanyiko ambayo ni ya kihisia zaidi". Wahubiri hawa wa siasa dhaifu wanajifanya wanaongea kwa hekima kuelezea hatari ya udini na ukabila na ukanda  wanachofanya ni kukuza na kuzipa umuhim hoja hizi kwa manufaa yao kisiasa
Ushauri:
 • Wanasiasa acheni hofu za kushinda uchaguzi kwa kuongelea mambo yasiyo halisia na ambayo yanalenga kubomoa.
 • Watanzania wasiwasikilize watu wanaohubiri udini, ukabila, ukanda, udhehebu na kingine chochote cha kututenganisha kama taifa la watu wamoja.
 • Kila mwanasiasa bila kujali chama na cheo chake atakayesimama na kuanza kuongelea mambo haya tumnyamazishe na kumwambia hatutaki kusikia habari hizo maana sio matatizo kwetu.
 • Mwanasiasa atakayegoma kutusikiliza, tumlazimishe atuambie msingi wa hoja yake. Asituambie habari hizi kijumla jumla tu na kutupa tahadhari tusiozielewa
 • Akikataa kutusikiliza, tumzomee na kumwambia "hoja za udini na ukabila na ukanda sio dili kwetu".."tunahitaji majibu ya matatizo yetu; hayo ya uchochezi sio saizi yetu"..."tulisikiliza hoja hizo 2010 na zikataka kutuangamiza kama taifa. Hatuzitaki tena"
 • Wakiendelea kuleta ubishi tuwaambie, "sasa wewe endelea kuongea hayo, ila kuwa na hakika kwamba tutatumia KICHINJIO KUKUKATA wewe na chama chako"
 • Tusiwanyamazie wanaongelea mambo haya iwe kwenye mikutano, kwenye mitandao au kwingine popote pale. Tuwafanye wajue hatutaki habari za kutugawanya maana twajua madhara yake na hatuna haja ya kuendelea kupewa mifano na taadhari
Hoja za udini, ukabila, udhehebu, ukanda, umikoa na nyingine kama hizo ni hoja za kijinga, dhaifu na hazina mashiko kwa taifa letu. Tusiziendeke na wanasisa waachane nazo. Tunataka waongelee mambo ya msingi yanayotuhusu na suluhisho lake na sio kutujengea hofu na fikra za kubaguana na kuchukiana bila sababu huku wakidhani tutawahesabu wana hekima kwa kufanya hayo.
Nitaendeleza mada hii

Mwalimu MM ni mhadhiri katika kitengo cha Sayansi ya Kompyuta ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Mtafiti wa mifumo ya TEHAMA (ICT) katika Huduma za Afya (Health Informatics). Unaweza kuwasiliana naye kupitia [email protected] na kusoma makala zake kupitia: http://mwalimumm.blogspot.com

Waliokuwa CHADEMA Ludewa wachoma moto kadi na kuhamia ACT-Wazalendo

Kadi na nyaraka za CHADEMA zikichomwa moto
*Wafanya Maandamano Makubwa. Wachoma Moto Kadi

* Ofisi ya CHADEMA Wilaya almanusra ichomwe Moto; Viongozi wakimbia na kutelekeza ofisi

WANACHAMA zaidi ya 500 wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Wilayani Ludewa Mkoani Njombe wamekihama chama hicho na kujiunga na chama cha ACT Wazalendo wakipinga hatua ya uongozi wa juu wa chama hicho kukata jina la mshindi wa kwanza wa kura za maoni Bw. Ocol Haule na kumteua aliyekuwa mshindi wa pili katika mchakato huo Bw Bartholomeo Mkinga.

Wanachama hao ambao kutoka kata mbali mbali za wilaya ya Ludewa wamefanya maandamano hayo ya amani leo kuelekea ofisi ya CHADEMA wilaya huku wakitishia kuichoma moto ofisi hiyo baada ya viongozi wake kuifunga, kuitelekeza na kukimbia kunusuru maisha yao. 

Wakizungumzia hatua hiyo ya kupinga maamuzi ya chama ngazi ya taifa wanachama hao Bi Hongera Gama, Taukile Mapunda na aliyekuwa Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake (BAWACHA) wilaya ya Ludewa Bi. Sophia Mtega walisema kuwa wanachama walikuwa na imani kubwa na mshindi wa kura za maoni kwani alifanya kazi kubwa ya kukijenga chama na sio huyo waliomuacha katika kura za maoni .

“Kinachoendelea sasa hivi ndani ya CHADEMA ni ufisadi mtupu,” alisema Bi. Gama akiongeza kuwa yeye binafsi alitoka CCM na kujiunga na Chadema kutokana na mapungufu yaliyokuwepo ndani ya CCM ila kinachoendelea kwa sasa ndani ya Chadema anajuta kuingia Chadema na hivyo ameamua kuhama chama hicho kumfuata mtu wao waliyemchagua popote atakakokwenda .

“ Mwenendo wa chadema kwa sasa ni wa ovyo zaidi kuliko chama chochote cha siasa hapa nchini tulikuwa tukishuhudia CCM watu wakikatwa ila leo ndani ya Chadema imekuwa ni kawaida kuona wale waliochaguliwa na wanachama kukatwa na watu wachache akiwemo mwenyekiti wa Taifa wa chama hicho Freeman Mbowe …..tumechoka tunahitaji kwenda kupata Demokrasia ya kweli ACT Wazalendo siyo ndani ya CHADEMA”

Huku Bw Mapunda akidai kuwa siasa za ukabila zinaendelea kukitesa CHADEMA na kuwa suala hilo la ukabila na kuwakumbatia mafisadi ndilo ambalo linaendelea kukitafuna chama hicho pia siasa za ukanda na kukumbatia ufisadi imekuwa ni kawaida Chadema.

Hivyo alisema katika kuhakikisha wana CHADEMA wilaya ya Ludewa na kote nchini wanapinga siasa za ukanda na zile za kuwachukua watu wenye tuhuma za ufisadi kugombea ndani ya chama hicho ni lazima wanachadema kuungana kupinga hali hiyo kwa kuhama ndani ya chama hicho na kujiunga na ACT Wazalendo.

Aliyekuwa mwenyekiti wa BAWACHA wilaya ya Ludewa Bi Mtenga alisema kuwa uonevu na rushwa vimechangia wanachama na wananchi kukosa imani kabisa na chama hicho na sasa badala ya  kuwa chama cha wanyonge kimekuwa ni chama cha wenye pesa na mafisadi jambo ambalo wao kama wananchi wa chini hawapo tayari tena kukaa ndani ya CHADEMA.

Akimkaribisha mgombea ubunge huyo aliyekatwa ndani ya CHADEMA Bw Haule na wanachama zaidi ya 500 wa chadema , katibu wa ACT wazalendo wilaya ya Ludewa Bw Alfred Ulaya alisema kuwa pia alipata kuwa kiongozi ndani ya CHADEMA wilaya ya Ludewa ila alihama pamoja na viongozi wengine kutokana na siasa za chuki ndani ya chama hicho na hatua ya kukumbatia ufisadi.

Hivyo alisema wanachama hao hawajachelewa kujiengua na chadema na kujiunga na chama cha ACT wazalendo kwani ni chama chenye misingi bora na chama pekee chenye malengo sahihi ya kulikomboa Taifa na Chadema na pamoja na umoja wao wa vyama vinavyo unda katiba ya wananchi (UKAWA) ni CCM B hivyo lazima watanzania wapenda mabadiliko lazima kuchagua ACT Wazalendo.

Katibu huyo alisema kwa wanachama wote ambao wamejiengua na CHADEMA na kujiunga na ACT wazalendo wakiwemo makatibu na wenyeviti wa kata zaidi ya 10 waliojiunga na ACT wazalendo na viongozi wengine watakuwemo ndani ya chama hicho na vyeo vyao kama walivyotoka Chadema.

Kwa upande wake mgombea huyo aliyeenguliwa kugombea ubunge mbali ya kushinda kura za maoni Bw Haule alisema kuwa kimsingi aliyeteuliwa kugombea nafasi hiyo alikuwa amewaandikia barua baadhi ya viongozi ngazi ya wilaya ya kuwaahidi kuwapa pesa, kufungua duka la vifaa mbali mbali pamoja na kuwahonga pikipiki barua ambayo aliinasa na kuwaonyesha wanachama hao.

Pia alisema kimsingi baada ya kuenguliwa kugombea nafasi hiyo alitaka kukaa kimya kama aliyekuwa Katibu Mkuu wa CHADEMA Dk Slaa ila akaona kukaa kimya bado si jibu na hivyo kuamua kujiunga na ACT wazalendo na kuweka uozo huo wazi.

Bw Haule alisema kuwa kwa sasa atahakikisha anazunguka jimbo nzima kufikisha kilio chake kwa wana Chadema na kupinga kwa nguvu zote wagombea wa udiwani na ubunge wa Chadema kupewa kura na kuwa kwa sasa uhai wa Chadema katika wilaya hiyo umekufa rasmi .Wanachama wa CHADEMA wilaya ya Ludewa mkoa wa Njombe wakiandamana kupinga maamuzi ya chama hicho kukata jina la mshindi wa kura za maoni na kumteua aliyeshindwa ,mbali ya kuandamana pia wanachama hao zaidi ya 500 walikihama chama hicho na kujiunga na ACT Wazalendo


Wanachama wa CHADEMAwaliohamia ACT wazalendo wakiwa na mabango ya kukituhumu chama hicho kwa kukiuka Demokrasia


Wanachadema wakiwa nje ya ofisi ya ACT Wazalendo ambako walifika kuomba kujiunga huko


Kadi za CHADEMA zikiteketezwa kwa moto


WanaCHADEMA  wakiwa na mabango


Hasira za kukatwa kwa mshindi wa kura za maoni Ludewa


WanaCHADEMA  wakijiandaa kwa maaandamano ya amani kujiengua na CHADEMA na kujiunga ACT Wazalendo


Bango likimtaka aliyeteuliwa na chama kwenda kugombea jimbo la Hai kwa Mbowe


Mwanzo wa maandamano ya kujiengua na CHADEMA


Wana CHADEMA katika maandamano ya kupinga uonevu ndani ya chama


Tuhuma dhidi ya CHADEMA Taifa


WanaCHADEMA  katika maandamano ya kupinga mshindi kutemwa


WanaCHADEMA  waliojiengua na kujiunga na ACT wazalendo wakiwa nje ya ofisi ya Chadema wilaya ya Ludewa


Barua ya tuhuma za mteuliwa kutoa ahadi ya rushwa hii hapa


Varua ikionyeshwa kwa wanahabari na WanaCHADEMA


Ni jaziba kwa wana CHADEMA  Ludewa


WanaCHADEMA wakiwa nje ya ofisi ya chama wilaya walikokwenda kurudisha kadi kabla ya kuhamia ACT wazalendo


Aliyekuwa mwenyekiti wa BAWACHA wilaya ya Ludewa akionyesha kadi ya ACT wazalendo


Aliyeenguliwa Bw Haule akiwapongeza WanaCHADEMA kwa kuhamia pamoja ACT wazalendo


WanaCHADEMA  wakirudisha kadi za chamna hicho na kujiunga na ACT wazalendo


Baadhi ya nguo na kadi zikiandaliwa kuchomwa moto


Katibu wa ACT wazalendo Ludewa Alfred Ulaya akionyesha kadi za CHADEMAWanachadema wakijipata kuhamia ACT wazalendoKadi zikiwa zimekusanywa kwa kuchomwa moto


Mwana CHADEMA  akichoma moto kadi za CHADEMA Ludewa kupinga uonevu ndani ya chama hicho


Hivi ndivyo kadi zinavyoteketezwa kwa moto baada ya wana CHADEMA  kujiengua na chama hicho na kujiunga na ACT Wazalendo
Mabango ya kuagana na CHADEMA  kwa wana Ludewa
Bango likionyesha CHADEMA kura za CHADEMA  Urais X ,Ubunge X na Udiwani X huku likimaliza kwa kusema msituchagulie


Mwanachama wa CHADEMA  akiongea kwa jazba juu ya hali ya mambo ndani ya CHADEMA kabla ya kujiunga na ACT Wazalendo


Ofisi ya CHADEMA  wilaya ikiwa imefungwa wakati wanachadema walipofika kurudisha kadi zao


Kadi ya ACT baada ya kuhama CHADEMA


Makada wapya wa ACT kutoka CHADEMA


Aliyekuwa mshindi wa kura za maoni akionyesha barua nyenye siri nzito za mteuliwa kununua nafasi hiyo


Bw Haule akijiandaa kuchoma moto vifaa vyake vya CHADEMA kabla ya kujiunga na ACT Wazalendo
 • Tumeshirikishwa taarifa hii na Francis Godwin/MatukiodaimaBlog, Ludewa