[update] Mgombea Ubunge Lushoto, Mohamedi Mtoi atutoka!
MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), jana ameongoza mamia ya wananchi wa Jimbo la Lushoto mkoani Tanga, wakati wa mazishi ya aliyekuwa mgombea wa jimbo hilo, marehemu Mohamed Mtoi.

Katika mazishi hayo, Mbowe aliiomba Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ihairishe uchaguzi wa jimbo la Lushoto ili waweze kuanza mchakato wa kutafuta mgombea mwingine wa kuziba nafasi iliyoachwa na marehemu Mtoi ambaye alifariki kwa ajali ya gari juzi.

Alisema uchaguzi wa Oktoba, mwaka huu katika jimbo hilo hauwezi kufanyika hadi utaratibu wa kupata mgombea mwingine utakapokamilika ukihusisha vyama vyote vilivyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).

Marehemu Mtoi alizikwa katika Kijiji cha Mkuzi.

Mazishi hayo, yalihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa chama hicho, wakiwamo wabunge waliomaliza muda wao ambao ni Joseph Selasini (Rombo), John Mnyika (Ubungo), Halima Mdee (Kawe), Makamu Mwenyekiti, Profesa Mwesiga Baregu, Kaimu Katibu Mkuu Zanzibar, Salum Mwalimu na Hassan Hassanali mgombea ubunge Jimbo la Dodoma.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa Chadema, Mnyika alisema kifo hicho ni pengo kubwa kwao na kuwataka wenzao wa CUF kuwafuta machozi kwa kumuunga mkono mgombea wao ambaye watamsimamisha baadae.

“Niseme tumepoteza jembe, nawaomba CUF watufute machozi katika hili kwa kumuunga mkoano mgombea atakayeteuliwa,” alisema.

Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya CUF, Gogola Shechonge akizungumza kuhusu

kauli ya Mnyika kutaka waachiwe jimbo hilo, alisema wamewekeana utaratibu juu ya kuachiana majimbo.
  • OSCAR ASSENGA, LUSHOTO via gazeti la MTANZANIA, Septemba 15, 2015

-------------------------

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Ofisi ya Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kupitia Idara ya Habari na Mawasiliano, kwa masikitiko makubwa inatangaza msiba wa aliyekuwa Mgombea Ubunge Jimbo la Lushoto ambaye pia alikuwa Ofisa Mwandamizi wa Makao Makuu ya Chama, Ndugu Mohamed Kanyawana Shemg'ombe Mtoi akiratibu Kanda za Chama Taifa.

Kamanda Mtoi alifariki dunia baada ya kupata ajali, Jumamosi ya Septemba 12, mwaka huu, eneo la Magamba alipokuwa njiani kurejea nyumbani kwao Mkuzi baada ya shughuli za kampeni jimboni humo.Ofisi ya Katibu Mkuu na Chama kwa ujumla kimempoteza mmoja wa wanachama, mtendaji na kiongozi mahiri kabisa katika wakati ambapo mchango wake ulikuwa ukihitajika sana.

Mazishi ya Ndugu Mohamed yamepangwa kufanyika Leo saa 7 mchana nyumbani kwao Mkuzi, Lushoto ambapo Mwenyekiti wa Chama Taifa, Mheshimiwa Freeman Mbowe atashiriki.

Chama kwa kushirikiana na familia kinafanya uratibu wa msiba huo na taarifa zaidi zitaendelewa kutolewa.Pamoja na mambo mengi, Ndugu Mohamed atakumbukwa sana kwa namna alivyoratibu na kusimamia uendeshaji wa Kanda za Chama kupitia idara yake chini ya Kurugenzi ya Oganaizesheni, Mafunzo na Uratibu wa Kanda.Kama inavyojulikana, dhana ya kuendesha chama kupitia Kanda, imekuwa ni utekelezaji kwa vitendo wa mojawapo ya sera muhimu za chama, iitwayo Mfumo Mpya wa Utawala, hivyo Ndugu Mohamed alikuwa aliaminika na kupewa majukumu makubwa ya kuhakikisha chama kinathibitisha kwa Watanzania kuwa mawazo mbadala ya mabadiliko yanawezekana kwa manufaa ya taifa letu.Wasomaji wa kupitia njia mbalimbali za mitandao ya kijamii na baadhi ya magazeti, watakumbuka namna Mohamed alivyokuwa na mchango mkubwa katika kupigania chama kutokana na imani yake kubwa katika kupigania mabadiliko na kutoyumba.
Chama kinatoa pole kwa familia ya Ndugu Mohamed kwa kumpoteza baba, mmoja wa nguzo muhimu na mtu wa karibu katika maisha yao. Tunaomba Mwenyezi Mungu awafanyie wepesi na kuwapatia moyo wa ujasiri katika wakati huu mgumu.

Aidha chama kinatoa salaam za pole kwa ndugu, jamaa, marafiki wa Mohamed halikadhalika viongozi, wanachama, wapenzi, mashabiki wa CHADEMA na Watanzania wote walioguswa na msiba huo.

Inna lillahi wa inna ilayhi raji'un.

Imetolewa leo Jumapili, Septemba 13 na;

Tumaini Makene
Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano
CHADEMA


Nimesoma kwa masikitiko na majonzi kuhusu ajali iliyompata kaka Mohamedi Mtoi aliyekuwa akiwania Ubunge katika jimbo la Lushoto kwa tiketi ya CHADEMA na mwavuli wa UKAWA.

Nimesikitika sana kusikia kuwa ameaga dunia.

Nilimfahamu Mtoi kupitia mawasiliano ya intaneti baada ya yeye kuniandikia kwa utani na baadaye nikagundua kuwa alikuwa mmoja wa wanafunzi wa mama yangu katika Chuo cha Ualimu Korogwe.

Tangu nifahamiane naye kwa miaka mitatu, tumekuwa tukiwasiliana hapa na pale hasa kwa machapisho yake kadha wa kadha aliyokuwa akiyatuma na kwa salamu alizokuwa akinitumia punde anapoonana na kumjulia hali Mama yangu.

Moja ya mawasiliano yangu na Mtoi 😟
---------- Forwarded message ----------
From: Mohamedi Mtoi <[email protected]>

Date: 2012-03-27 10:14 GMT-07:00 Subject: 

Re: BINTI UKO KIMYA SANA WANGU! 

To: Subi <[email protected]>

Pouwa wangu.Yangu ni +255 713 246764. Siku moja moja tunavutiana waya na kuyachana mawingu kwa mwangwi wa dhahabu.Barikiwa leo, mimi naingoja kesho kama roho zitakuwa hai.​

---------- End of forwarded message ----------

Tulipunguza mawasiliano mwaka huu mzika kutokana na yeye kujikita zaidi na kwa kina katika siasa za mrengo aliouona unafaa, na kutokana na mimi kutokutaka kusimama katika upande wowote wa kisiasa, nilimtakia heri na mafanikio na kumtaarifu kuwa tutampima kauli zake kwa matendo yake endapo atapata ridhaa ya kutuongoza. Tuliahidiana kukutana na kusalimiana familia zetu kunako majaaliwa, lakini sasa ameondoka kabla hatujaonana tena ana kwa ana.

Nimempoteza rafiki aliyekuwa hachoki kunieleza mawazo na msimamo wake na nia yake ya kuleta mabadiliko katika nafasi yoyote atakayojaaliwa na Mwenyezi Mungu pale atakapofanikiwa kusema mawazo yake atakavyo.Familia ya Mtoi Mohamedi
Familia ya Mtoi

Uchaguzi Mkuu: Ilani ya CCM 2015 - 2020


Bibi wa Mkuranga ang'aka na uchaguzi huu akilinganisha na enzi za mkoloni


Mbasha azungumza baada ya Gwajima kumjibu Dk Slaa

Emmanuel Mbasha katika uzinduzi wa kampeni za CCM, Jangwani kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu 2015

Siku chache baada ya Mchungaji Kiongozi wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima kujibu mapigo ya aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Wilbrod Slaa, sasa Emmanuel Mbasha ambaye ni mume aliyetengana na mkewe, Flora Mbasha amerejea madai yake kwamba, Gwajima alisimamia mchakato mzima wa yeye na mkewe kutengana.

Akizungumza na Risasi Jumamosi katika mahojiano ya takribani dakika thelathini juzi jijini Dar, Mbasha alisema alimshuhudia Gwajima, Jumanne wiki hii akitupa shutuma kwa Dk. Slaa tena kwa kuyaanika mambo yake ya ndoa, yeye akashangaa sana.

“Na mimi leo nataka kumjibu Gwajima kama yeye naye alivyojitokeza kumjibu Dk. Slaa. Gwajima niliwahi kumshutumu kwa kuhusika na kuvunjika kwa ndoa yangu. Leo hii anasimama kwa kujigamba akisema Slaa si msafi, yeye ana usafi gani?.

“Lakini kiko wapi sasa! Hata huyo Flora mwenyewe ameshamkimbia, yuko kwingine. Kwa hiyo kama ishu ni uchafu, Gwajima pia si msafi. Ana mambo anajua alikuwa akiyafanya kwa mke wangu, mimi nayajua na nina ushahidi.”

Hata hivyo, Mbasha hakufafanua, Flora amemkimbia Gwajima kivipi? Na huko kwingine alikokwenda ni kwa nani na kwa sababu gani!

ANA MAZITO YA GWAJIMA

Lakini alikwenda mbele zaidi kwa kusema: “Naomba leo niseme kwamba nina mambo mazito sana ya Gwajima ambayo siku ikifika nikienda kuyasema kanisani kwake waumini wake watashangaa wote. Muda bado haujafika lakini ukifika nitamlipua.”

Risasi Jumamosi: “Je, kuibuka kwako upya tukisema umetumwa na chama kimoja cha siasa umchafue Gwajima, utasemaje?”

Mbasha: “Kwani ye’ alitumwa na nani? Mimi nimeibuka kwa sababu hata yeye ameibuka. Kama angesimama pale (ukumbi wa Hoteli ya Landmark) akasema mambo yake bila kukosoa ndoa ya Dk. Slaa hata mimi nisingepanua kinywa kusema. Hawezi kusema siri za mwenzake kama mtumishi. Tena anasema mpaka ishu ya Dk. Slaa kulala ndani ya gari.”

“Nimeamua kusema kwa sababu yeye amemwona mwenzake si msafi. Yeye usafi wake ni upi? Niliachana na Flora, akaenda kwake, yeye akampokea. Angekuwa msafi angemshauri Flora kwamba alichofanya si kizuri. Hapo ningesema ni msafi.”

AMKUMBUSHA GWAJIMA KUHUSU MOROGORO

“Gwajima akumbuke kabla ya ukaribu wetu haujafa, mimi, Flora na yeye tulikwenda Morogoro kwa ajili ya huduma ya Mungu. Nini kilitokea? Lakini sijasema. Ajitokeze anijibu na mimi halafu nitasema nini kilitokea. Kwa sasa sitoi risasi zote, nasubiri ajibu.”

NDANI YA MITANDAO

Ndani ya mitandao mbalimbali ya kijamii, majibu ya Gwajima kwa Dk. Slaa yamekuwa gumzo. Timu ya Mbasha imemtupia shutuma kali Gwajima ikikumbushia mgogoro wa Flora na mumewe huku kundi jingine la Gwajima likitetea kuwa, hakuna uhusiano wowote wa mgogoro wa Mbasha na mkewe na majibu ya Gwajima kwa Dk. Slaa.

GWAJIMA SASA

Juzi, gazeti hili lilimsaka kwa njia ya simu Mchungaji Gwajima ili aweze kujibu shutuma za Mbasha ambazo ni kama ameziibua upya lakini simu yake haikuwa hewani.

Hata hivyo, katika mkutano wake na wanahabari Jumanne, Gwajima alisema: “…kwa hiyo Dk. Slaa si msafi. Dk. Slaa huyu wa leo si yule wa mwaka mmoja uliopita! Lakini ukiangalia kwa makini sana, si yeye, matatizo yapo kwa yule mke wake, amemkamata.”

Pia, Gwajima alianika siri akidai kuwa, Dk. Slaa aliwahi kutupiwa virago nje akalala kwenye gari baada ya kubaini kuwa, ameridhia, Chadema kumpokea waziri mkuu wa zamani, Edward Lowassa na kugombea urais.

Flora Mbasha katika Kongamano la BAWACHA/CHADEMA 2015

FLORA NAYE ANA MAMBO MENGI

Wakati Mbasha akirusha madai hayo huku akisema mkewe amemkimbia Gwajima na yuko kwingine, kwa upande wake, Flora aliwahi kusema: “Nina mambo kibao ya Mbasha, nikiyasema watu watashangaa! Lakini siku zote mimi namwachia Mungu tu. Yeye ndiye muweza wa yote.”

MKE WA DOKTA SLAA

Kuhusu madai ya kumfukuza mumewe nje na kulala kwenye gari, mke wa Dk. Slaa, Josephine Mushumbuzi aliwahi kusema: “Najiuliza nini kinaendelea, kuna mambo mwanamke huwezi kumfanyia mwanaume. Mume atabaki kuwa mume tu siku zote.”

SLAA AHOFIA

Kuhusu madai ya kukatiliwa kuingia ndani ya nyumba na mkewe na kulala ndani ya gari, Dk. Slaa alipoulizwa kihabari, alisema: “Mambo hayo ni ya kifamilia sana. Sitaki tu kuzungumzia mambo ya familia za watu nikiyasema utatokea mpasuko! Tuache tu.”
  • Imenukuliwa kutoka GPL

Hatua iliyofikiwa na NEC katika maandalizi ya vifaa vya uchaguzi


Tume ya Taifa ya Uchaguzi NEC imesema karatasi za kupigia kura kwenye uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 25 mwaka huu, zinatarajiwa kuwasili nchini Septemba 29, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya kuleta vifaa vya uchaguzi.

Akizungumza na Waandishi wa Habari jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa ununuzi na ugavi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Eliu Njaila amesema matayarisho ya vifaa vya kupigia kura yanaenda vizuri, ambapo amebainisha kwamba baadhi ya vifaa muhimu vinavyohitajika vimeshaanza kuwasili.

Amevitaja baadhi ya vifaa hivyo kuwa ni vituturu (vibanda) vya kupigia kura, mihuri na vitabu ambavyo vimeshaanza kusambazwa mikoani ambapo ya shilingi Bilioni 41.6 kwa ajili ya vifaa hivyo tayari yamekamilika.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi huyo, karatasi za kupigia kura pekee ndizo zinazoagizwa kutoka nje ambapo amesema vifaa vingine muhimu vimepatikana hapa nchini baada ya kutangazwa zabuni.

Aidha, bwana Njaila amewataka wananchi kutokuwa na hofu kuhusu upatikanaji wa vifaa hivyo ambapo amesema vyote vitapatikana na hakutakuwa na upungufu.

Karipio la CUF kuhusu vurugu za CCM

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Chama Cha Wananchi (CUF) kinalaani vikali na kwa nguvu zote kitendo cha Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuvuruga mkutano wa kampeni wa Mgombea Urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CUF, Maalim Seif Sharif Hamad uliokuwa ukifanyika jana tarehe 11 Septemba, 2015 kwenye Viwanja vya KwaBinti Amrani, jimbo la Mpendae, Wilaya ya Mjini Unguja.

Kwa makusudi kabisa, wakati mkutano wa kampeni unaendelea na Mgombea Urais, Maalim Seif, akiwa kwenye jukwaa anahutubia, vijana wa CCM walipita kwenye mkutano huo wakiwa na gari la matangazo lenye namba Z 458 GC ambalo lilikuwa linapiga muziki kwa sauti ya juu na kusababisha kuingiliana sauti na hotuba ya mgombea.

Kitendo hicho cha uchokozi wa makusudi kilizua tafrani kubwa miongoni mwa wananchi waliokuja kuhudhuria na kusikiliza mkutano huo. Kutokana na hekima na busara kubwa alizo nazo Maalim Seif aliamua kukatisha hotuba yake na kuteremka juu ya jukwaa na hivyo kuuvunja mkutano huo kabla ya muda wake. Busara na hekima za Maalim Seif ziliepusha shari iliyokuwa ikitafutwa na CCM kwa makusudi.

CUF tumesikitishwa zaidi na hatua ya Polisi wakitumia gari mbili za defenders kuipatia ulinzi mbele na nyuma ya gari hiyo ya matangazo ya CCM wakati inafanya uchokozi huo wa makusudi. Hatukutegemea kitendo hicho kufanywa na Polisi. Tulitegemea Polisi ambao ndiyo wenye dhamana ya kusimamia amani na utulivu kwenye maeneo ya mikutano ya kampeni kuwazuia vijana hao wa CCM na gari yao wasipite eneo lile. Badala yake Polisi ndiyo waliowapa ulinzi vijana hao wa CCM kuendesha hujuma na uchokozi wao.

Baada ya tukio hilo, Mjumbe wa Timu ya Kampeni ya CUF, Ismail Jussa, aliwasiliana kwa njia ya simu na Kamishna wa Polisi Zanzibar na kumueleza juu ya tukio hilo.

CUF tunasema tumesikitishwa na hatua ya Polisi kwa sababu Polisi wakiongozwa na Kamishna wa Polisi Zanzibar, CP Hamdani Omar Makame, waliitisha kikao kati yao na vyama vya CUF na CCM siku ya Ijumaa, tarehe 28 Agosti, 2015 hapo Ziwani kwenye makao makuu ya jeshi hilo Zanzibar na kuzungumza namna bora ya kushirikiana baina yetu ili kuepusha vitendo vya vurugu na fujo na kuhakikisha tunaendesha kampeni na harakati nyengine za uchaguzi kwa salama na amani.

Ni kwa sababu ya mazungumzo hayo ndiyo maana CUF tokea siku ya uzinduzi wa kampeni zetu tarehe 9 Septemba hadi jana kwenye mkutano huo wa Mpendae tumekuwa tukiwaeleza wafuasi wetu na wananchi kwa ujumla juu ya umuhimu wa kushirikiana kutunza amani na utulivu nchini kwetu. Hatukutegemea kwamba wakati sisi tunafanya hivyo, wenzetu waendelee na vitimbi vyao vinavyolenga kuchafua amani na utulivu ulioonekanwa tokea tumeanza kampeni.

CUF leo hii tutaiandikia Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) kuwaeleza juu ya uchokozi huu wa CCM, kuwataka wakionye Chama Cha Mapinduzi juu ya vitendo vyake hivi na pia kuwataka Tume kusimamia ratiba ya kampeni ambayo tulikubaliana kwa pamoja baina ya vyama vyote vya siasa, Tume yenyewe na Jeshi la Polisi katika mkutano ulioandaliwa na ZEC tarehe 4 Septemba, 2015. Pia tutamuandikia Kamishna wa Polisi kumueleza malalamiko na masikitiko yetu kutokana na kitendo cha Polisi wake kushindwa kuwazuia vijana hao wa CCM na badala yake kuwalinda ili waweze kufanikisha uchokozi wao.

Mwisho, CUF tunaendelea kusisitiza kwamba tukiwa chama makini kinachojiandaa kuongoza Serikali ya Umoja wa Kitaifa baada ya kupewa ridhaa na wananchi wa Zanzibar tutalinda amani na utulivu uliopo na hatutoingia katika mtego wa njama za CCM ambao wamedhamiria kuvuruga amani iliopo baada ya kukata tama juu ya uwezekano wa kushinda uchaguzi.

CUF tunaendelea kutoa wito kwa wanachama na wafuasi wetu na wananchi wote kwa ujumla kufuata sheria na pia maelekezo ya viongozi wetu katika kutunza amani na utulivu wakati wote wakijua kwamba tunaelekea katika ushindi mkubwa kwenye uchaguzi mkuu wa tarehe 25 Oktoba, 2015.

HAKI SAWA KWA WOTE

ISMAIL JUSSA
MKURUGENZI WA MAWASILIANO – TIMU YA KAMPENI YA CUF
ZANZIBAR – 12 SEPTEMBA, 2015

Taarifa kuhusu Watanzania walioko Mecca kulikoanguka msikiti

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI 
 
Taarifa ya kuanguka Msikiti Makhah-Saudi Arabia, Watanzania Salama.

Kufuatia mvua ilioambatana na upepo mkali na kusababisha kuanguka kwa mashine ya ujenzi wa upanuzi wa eneo la Tawaf ulipo msikiti wa Makkah, msikiti huo umeanguka na kusababisha vifo vya mahujaji.

Kwa mujibu wa Televisheni ya Saudi Arabia, Saudi TV hadi sasa watu 107 wamefariki dunia na wengine takriban 200 wamejeruhiwa.

Kufuatia ajali hiyo, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa kupitia Ofisi za Ubalozi Riyadh unathibitihsa kuwa Mahujaji wa Tanzania wameanza kuwasili Jeddah kuelekea Makkah leo tarehe 12 Septemba 2015 wakitokea Madina. Hadi sasa Wizara haijapokea taarifa ya Watanzania waliopoteza maisha wala kujeruhiwa kwenye ajali hiyo.

MWISHO.

Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali kwa Umma,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa,

12 Septemba, 2015

Maagizo ya BASATA kwa wasanii "wanaotumiwa vibaya kisiasa"

Katika siku za hivi karibuni kumeibuka wimbi la wasanii kuvunja maadili, kukaidi adhabu na kutumia lugha chafu kwa makusudi katika kazi za Sanaa hususan muziki hali ambayo imezua malalamiko, masikitiko na hofu kwa jamii ambayo ni walaji wa kazi za Sanaa.

Lugha hiyo chafu ambayo inajidhihirisha kwa matusi ya wazi, maneno ya uchochezi, kashfa, kejeli, dharau na udhalilishaji wa kada mbalimbali za kijamii wakiwemo viongozi wa kitaifa inaonesha wazi kulenga katika kuigawa jamii na kufifisha amani, upendo, uzalendo na ustaarabu tuliokuwa nao watanzania.

Ieleweke kwamba kwa mujibu wa misingi ya Sanaa Duniani kote kazi zote za Sanaa zinapaswa ziwe ni zenye kuonya, kuelimisha, kuadabisha, kukosoa, kuburudisha, kuhamasisha na kuchochea maendeleo chanya katika jamii na siyo kuigawa au kuivuruga jamii.

Ndiyo maana msanii anayefanya kazi zake kwa kuzingatia misingi ya Sanaa anatambuliwa kuwa ni kioo cha jamii, kiongozi na pia ni mwalimu wa yale yote yaliyo mema katika jamii inayomzunguka.
Kinyume na misingi hiyo ya Sanaa, baadhi ya Wasanii, studio za kurekodia na kutengenezea muziki, vyombo vya habari vya kielektroniki na mitandao ya kijamii ama kwa kutumiwa au kwa utashi wao binafsi wamekuwa wakijihusisha na Sanaa zenye viashiria vya uchochezi na kuvunja misingi ya weledi katika Sanaa hususan katika kipindi hiki cha kampeni na maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa Rais, wabunge na madiwani.

Aidha, baadhi ya Wasanii wamekuwa wakitumiwa na baadhi ya vyama vya Siasa au wagombea na kujikuta wakitumiwa vibaya na kuvunja misingi ya Sanaa kwa faida za kisiasa. BASATA linapenda kutoa maagizo yafuatayo:
  1. Wasanii wana haki zote za kikatiba na kidemokrasia kushiriki shughuli za Siasa lakini wanawajibika kwa kiwango cha hali ya juu kulinda misingi ya weledi, maadili, miiko na hadhi yao kama inavyofanyika katika tasnia zingine.
  2. Wasanii wanapaswa kutambua kwamba kuna maisha na Taifa baada ya uchaguzi mkuu. Umoja wa kitaifa na umoja baina ya wasanii wa kada zote za Sanaa ndiyo utakuwa msingi mkuu wa kuendelea kusukuma gurudumu la maendeleo ya Sekta ya Sanaa na Taifa kwa ujumla pasipo kugawanyika katika misingi ya itikadi za kisiasa
  3. Wasanii wasitumie nafasi na umaarufu wao kuligawa taifa, kukashifu viongozi wa kitaifa, kudharau mamlaka, vyama na makundi mbalimbali katika jamii kwa kile kinachoitwa ushabiki wa kisiasa. Ieleweke kuwa Serikali haitafumbia macho wale wote watakovunja sheria, kanuni na taratibu. Tukumbuke kuwa hakuna mtu aliye juu ya sheria.
  4. Ijulikane kuwa wasanii kama kundi muhimu katika kipindi cha kampeni za kisiasa ni sawa na watu wengine wanaopewa kazi ili kutimiza lengo lililokusudiwa. Wasanii wasitumiwe kama vyombo tofauti na watu wengine.
BASATA linatoa onyo kali kwa msanii yeyote atakayeendelea kukaidi, kuvunja maadili na kusambaza kwa njia yoyote ile kazi ya Sanaa yenye ukengeufu wa maadili.

BASATA linawatakia wasanii wote utekelezaji mwema wa maagizo haya lakini kubwa kuliko yote kutambua kwamba tunatakiwa kujenga mshikamano, umoja wa kitaifa na kustawisha amani tuliyonayo ambapo ikitoweka itaathiri ufanisi wa Wasanii na kuirejesha itatugharimu sana.

Sanaa itumike kulinda amani, kujenga upendo, umoja wa kitaifa na mshikamano baina ya makundi mbalimbali ya kijamii.

SANAA NI KAZI TUIKUZE, TUILINDE NA KUITHAMINI

Godfrey L. Mngereza
KATIBU MTENDAJI, BASATA

Taarifa ya kukamatwa kwa walioshambulia wafuasi, magari ya CCM


TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Polisi Mkoa wa Dodoma tunawashikilia watu wanne na wengine tunaendelea kuwatafuta kutokana na tuhuma za Kujeruhi, Kuharibu Mali na Kufanya fujo. 

Hii ni kutokana na jana tarehe 11.09.2015 majira ya saa 18:30 Wanachama na Wafuasi wa Chama cha Chadema waliokuwa wanatoka kwenye Mkutano wa Kampeni uliokuwa umehutubiwa na Viongozi wa Chadema akiwepo Mh. E. Lowasa katika Viwanja vya Barafu walipofika maeneo ya njia panda ya NAM Hotel Dodoma walianza kuwatukana na kuwashambulia kwa mawe wanachama na Wafuasi wa CCM waliokuwa wanatokea kwenye mkutano wa Kampeni maeneo ya Msalato.
Kutokana na vitendo hivyo ambavyo ni kinyume na sheria, kanuni, taratibu na maadili ya uchaguzi walisababisha watu wanne kupata majeraha na magari manne kupata uharibifu wa kuvunjwa vioo. Magari yaliyovunjwa vioo ni kama ifuatavyo:-
1. T 180 AFE Toyota L/Cruiser mali ya CCM ambalo limevunjwa kioo cha dirisha la kushoto.
2. T627 BEJ Toyota L/Cruiser mali ya CCM limevunjwa kioo cha mbele
3. T 844 ACG Nissan Patrol mali ya CCM limevunjwa kioo cha mbele
4. T 841 AJS Toyota Double Cabin ambalo limevunjwa kioo cha mlango wa kushoto.

Wanaoshikiliwa kutokana na vitendo hivyo ni:-
1. JUMA S/O BIKA, MIAKA 40, MGOGO MKAZI WA MIYUJI NA KATIBU MWENEZI WILAYA YA DODOMA.
2. FULGENCE S/O MAPUNDA, MIAKA 37, MNGONI MKAZI WA SINZA DAR ES SALAAM.
3. GEORGE S/O MWINGIRA, MIAKA 25, MNGONI, MKAZI WA KINONDONI – KIGOGO
4. DEOGRATIAS S/O PETER, MIAKA 26, MCHAGA, MKAZI WA KIMARA BARUTI.

Watuhumiwa wengine wanaendelea kutafutwa ili wote waweze kufikishwa mahakamani.
Nitoe wito kwa Viongozi wa Vyama wawaelimishe Wanachama na Wafuasi wao kujiepusha na vitendo kama hivi ambavyo ni kinyume na sheria, kanuni, taratibu na maadili ya Uchaguzi. Pia watambue wanapokwenda na kurudi kwenye mikutano ya kampeni barabara wanazotumia bila kufuata sheria wanawatia hofu na kuwanyima haki watu wengine wanaotumia barabara hizo. Pia wawaelimshe wanapokutana na wenzao wa vyama vingine waache kutumia lugha chafu, kuwafanyia vurugu, kupiga na kuharibu mali.

Hii ni kutokana na baadhi yao kutumia Waendesha bodaboda ambao huendesha pikipiki zao kwa fujo na kuyumba barabara nzima jambo linalowafanya watumiaji wengine kushindwa kutumia huduma hii bila karaha.

Kama Jeshi la Polisi Dodoma tutaendelea kuwachukulia hatua wale wote watakaoacha kutii sheria, kanuni, taratibu na maadili ya uchaguzi.

Taarifa ya Uhuru Publications kuhusu mwandishi aliyejeruhiwaLEO ASUBUHI, MWANDISHI AMBAYE PIA NI MPIGAPICHA WA MAGAZETI YA UHURU,MZALENDO NA BURUDANI YANAYOCHAPISHWA NA KAMPUNI YA UHURU PUBLICATIONS, CHRISTOPHER LISSA, ALIPATA TAARIFA ZA MAANDAMANO YA WALIOTAJWA KUWA WAFUASI WA CHAMA CHA DEMOKRASIA NA MAENDELEO (CHADEMA) WALIOKUWA WAMEKUSUDIA KUANDAMANA KWENDA MAKAO MAKUU YA CHAMA CHAO.

LISSA ALIMFAHAMISHA MHARIRI WAKE JUU YA TAARIFA HIZO, AMBAPO MHARIRI
ALIMTAKA KUFUATILIA TUKIO HILO.

MWANDISHI HUYO ALIONDOKA OFISINI SAA 2:50 ASUBUHI MPAKA KINONDONI ENEO AMBAKO WAANDAMANAJI WALIKUWA WAMEPANGA KUANZIA MAANDAMANO YAO.

WAANDAMANAJI WALICHELEWA KUFIKA ENEO TAJWA NA ILIPOTIMU SAA 5.00
NDIPO WALIFIKA WAKIWA KWENYE BASI NA KUSHUKA KUANZA MAANDALIZI YA
MAANDAMANO HUSIKA.

WAANDAMANIJI HAO WALIANZA MAANDAAMO MUDA MFUPI BAADAYE KUELEKEA
OFISI ZA MAKAO MAKUU YA CHADEMA ZILIZOPO MTAA WA UFIPA, KINONDONI.

HUKU WAKIWA NA MABANGO YALIYOKUWA NA UJUMBE TOFAUTI AMBAPO MWINGI ULIKUWA UKIKEMEA KITENDO CHA MGOMBEA URAIS WA CHADEMA, EDWARD LOWASSA, KUTUMIA UDINI KUOMBA KURA KANISANI. ITAKUMBUKWA KWAMBA LOWASSA ALIOMBA KURA HIVI KARIBUNI ALIPOKUWA MJINI TABORA, AMBAPO ALIFANYA HIVYO KATIKA KANISA LA KILUTHERI.

BAADA YA KUNDI HILO LA WAANDAMANAJI KUFIKA, LILIKWENDA MOJA KWA MOJA HADI KATIKA MLANGO WA KUINGIA KWENYE OFISI ZA CHAMA HICHO, AMBAPO MWANDISHI WETU ALIANZA KUTEKELEZA JUKUMU LAKE AKIWA NA WAANDISHI WENGINE.

HATA HIVYO KATIKA HALI YA KUSHANGAZA LISSA PAMOJA NA WAANDISHI WENZAKE WA HABARI, WALIKAMATWA NA WALINZI WA CHAMA HICHO, AMBAPO WENZAKE WALIACHIWA BAADA YA KUJITAMBULISHA KUWA WANATOKA VYOMBO VYA HABARI.

LAKINI CHA KUSHANGAZA LISSA ALIPOJITAMBUSHA KUWA ANATOKA GAZETI LA UHURU NDIPO WALIPOSEMA KWAMBA ‘HUYU NDIYE TULIYEKUWA TUNAMTAFUTA’ NA KUANZA KUMPIGA KWA NGUMI MAGONGO NA VYUMA NA KUMSABABISHIA MAJERAHA NA KUHARIBU KAMERA, HUKU WAKIMPORA SIMU YAKE YA MKONONI NA ‘WALLET’ ILIYOKUWA NA JUMLA YA SH. 80,000.

AIDHA ALIPOKUWA AKIPIGWA WAHUSIKA WALISIKIKA WAKISEMA TUWASUBIRI
WAKUBWA NA MUDA MFUPI BAADAYE ALIINGIA MSEMAJI WA CHAMA HICHO, BONIFASCE MAKENE, DIWANI WA UBUNGO CHADEMA, AMBAYE PIA ANATUHUMIWA KUMSHAMBULIA MLINZI WA DK. WILLIBROD SLAA, MUDA HUO HUO PIA ALIPITA MHE. JOHN MNYIKA ALIYEKUWA NA KIKAO NA WAANDISHI WA HABARI.

KWA MUJIBU WA MWANDISHI LISSA ALIYEELEKEZA NA KUMUINGIZA KWENYE CHUMBA CHA MATESO NI DIWANI HUYO WA UBUNGO AKIWA PAMOJA NA WALINZI WENGINE AMBAO WALIKUWA WAKIMPIGA.

AKIWA KATIKA CHUMBA HICHO ALIENDELEA KUPIGWA NA BAADAYE ALIPEWA KADI ZA CHADEMA NA KUANZA KUSHURUTISHWA KUSHIKA HIZO KADI NA ATAMKE MBELE YA KAMERA YA VIDEO ILIYOKUWA IKIMREKODI KWAMBA YEYE AMETUMWA NA KATIBU MKUU WA CHAMA CHA MAPINDUZI (CCM), ABDULRAHMAN KINANA NA VIONGOZI WA CCM KUANDAA MAANDAMANO HAYO, AMBAPO PAMOJA NA KUSHURUTISHWA HUKO ALIKATAA NA KUSHIKILIA MSIMAMO WAKE KWAMBA ALIKUWA AKITETEJELEZA MAJUKUMU YAKE YA UANDISHI WA HABARI NA SI VINGINEVYO.

WAKIWA WANAAENDELEA KUMSHURUTISHA GHAFLA WALIINGIA POLISI NA WATEKAJI WALISTUKA NA KUMWELEZA ASISEME KWAMBA ALIKAMATWA NA YUKO NDANI, HIVYO WALIMTOA NA KUTOKA NAYE NJE PAMOJA NA WATU WENGINE HUKU AKILINDWA NA WALINZI WA CHADEMA.

POLISI WALIPOFIKA NA KUOMBA KUFANYA UPEKUZI KUTOKANA NA TAARIFA ZA KUWEPO MWANDISHI WA UHURU, ANAYESHIKILIWA NDANI YA OFISI, WALIRUHUSIWA KUFANYA HIVYO HUKU LISA AKIWA NJE NA WALINZI WA CHADEMA WALIOMTAKA KUTOJITAMBULISHA AU KUSEMA CHOCHOTE WAKATI POLISI WAKIWEPO ENEO HILO.

BAADA YA POLISI KUONDOKA WALISIKIA WAKISEMA KWAMBA ‘DILI’ YETU
HAIJAFANIKIWA NA KUINGIA NAYE NDANI TENA NA KUMWELEZA MNYIKA ALIYEKUWA AKIZUNGUMZA NA WAANDISHI WA HABARI KWAMBA WAMEMKAMATA MWANDISHI WA UHURU AMBAYE NI MUANDAAJI WA MAANDANAMO HAYO.

BAADA YA KUPATA TAARIFA HIYO, MNYIKA ALIWAAMBIA WAANDISHI WA HABARI
WAKATI HUO LISA AMBAYE ALIOKUWA AMESHIKISHWA KADI NYINGI ZA CHADEMA, ALISHURUTISHWA KUSEMA KWAMBA NDIYE ALIYEANDAA MAANAMANO HAYO NA KWAMBA ASIPOSEMA HIVYO HATATOKA MZIMA.

PAMOJA NA VITISHO HIVYO, LISSA ALIKATAA NA KUSHIKILIA MSIMANO WAKE
KWAMBA ALIFIKA ENEO HILO KUFANYA KAZI YAKE YA UANDISHI WA HABARI NA SI VINGINEVYO. BAADHI YA WAANDISDHI WALISIKIKA WAKISEMA KWANINI MWENZAO ALIKUWA AKISHURUTISHWA KUSEMA MANENO HAYO.

WALINZI HAO WAONEKANA KUKIRI KWAMBA ZOEZI LAO LIMESHINDIKANA NA WENGINE WALITAKA APIGE NA HADI KUFA ILI KUPOTEZA USHAHIDI, LAKINI WENGINE WALIGOMA WAKISEMA HAPO NI MAKAO MAKUU YA CHAMA.

BAADA YA KUTOFAUTIANA WENYEWE KWA WENYWE WALIMRUHUSU LISSA AONDOKE NA NDIPO ALIPOONDOKA NA GARI LILILOKUWA NA WAANDISHI WA HABARI WA AZAM MOJA KWA MOJA KWENDA KITUO CHA POLISI, OYSTERBAY AMBAKO ALITOA MAELEZO YAKE.

TUNASIKITIKA KWAMBA CHADEMA WAMEAMUA KUFANYA SIASA CHAFU
ZINAZOTUHUSISHA KATIKA HARAKATI ZAO AMBAZO ZIMESHINDWA KUFANIKISHA KUWASHAWISHI WATANZANIA ILI WAWACHAGUE.

AIDHA, TUNALAANI VIKALI KITENDO HICHO KILICHOFANYWA NA KUNDI LA
MAOFISA NA WALINZI WA CHAMA HICHO, KUINGILIA UHURU WA VYOMBO VYA HABARI. CHADEMA WAMEFANYA UNYAMA HUO DHIDI YA MWANDISHI WETU, LAKINI CHAMA CHA MAPINDUZI HAKIJAWAHI KUFANYA HIVYO. HIVYO TUKIO HILI LIMEONYESHA PICHA HALISI CHA CHAMA HICHO AMBACHO KINALILIA KUWAONGOZA WATANZANIA.

WAKATI TUNALAANI UNYAMA HUO, TUNAAMINI VYOMBO VYA HABARI VITAKEMEA TUKIO HILI, LAKINI PIA TUNAAMINI HATUA STAHIKI ZA VYOMBO VYA DOLA IKIWEMO POLISI VITACHUKUA HATUA DHIDI YA WALIOHUSIKA NA UNYAMA HUO.

DAIMA CCM IMEKUWA IKIENDESHA KAMPENI ZA KISTAARABU KATIKA KIPINDI HIKI CHA UCHAGUZI MKUU TOFAUTI NA CHADEMA. UONGOZI WA UPL UNATOA POLE KWA LISSA NA KUMTAKIA MATIBABU MEMA.

RAMADHANI MKOMA,
KAIMU MHARIRI MTENDAJI,
UHURU PUBLICATIONS LIMITED.

Buriani mwandishi mzee Godfrey Mngodo

Godfrey Mngodo
Godfrey Mngodo

Wadau, nimepokea kwa huzuni habari ya kifo cha Mzee Godfrey Mngodo, aliyewahi kuwa mtangazaji Voice of America na Radio Tanzania. Mzee Mngodo alikuwa rafiki wa marehamu baba yangu, Dr. Aleck Che-Mponda. Walikuwa wote Voice of America walipoaanzisha Idhaa ya Kiswahili. Mzee Mngodo pia aliwahi kunifundisha Mass Communication nikiwa mwanafunzi Tanzania School of Journalism. Mzee Mngodo alinichekesha sana aliponiambia kuhusu ziara ya Mwalimu Nyerere nchini Marekani wakati wa Uhuru mwaka 1961. Mzee Mngodo alikuwa ni Press Secretary wa ziara. Basi waandishi wa habari wa USA walimwandama Mwalimu. Mwalimu kachoka na kwa hasira kaanza kuongea kiswahili. Waandishi ha wakamkimbilia Mzee Mngodo, "eti, anasemaje!' Mzee Mngodo anasema ilibidi atunge maana Mwalimua alikuwa anawachamba hao waandishi.

Poleni sana wanafamilia kwa msiba wa kufiwa na mzee wenu.

Rest in eternal peace, Mzee Godfrey Mngodo.
Idhaa ya Kiswahili ya Sauti ya Amerika inamkumbuka aliyewahi kuwa mtangazji wake Mzee Godfrey Mngodo aliyefariki dunia Ijumaa Septemba 11.
Godfrey Mngodo alikuwa mtangazaji wa kwanza wa idhaa ya Kiswahili ya sauti ya Amerika ilipoanzishwa mwaka 1962 .
Kwa mujibu wa taarifa za mtoto wa marehemu, Kinyemi Mngodo, Marehemu Mzee Godfrey Mngodo amefariki katika hospitali ya Dar Group jijini Dar es salaam baada ya kuugua kwa muda maradhi ya figo.
Taratibu za mazishi zinafanyika nyumbani kwa mtoto wa marehemu Yombo Vituka jijini Dar es salaam lakini taarifa za awali zinaeleza kuwa marehemu anatarajiwa kuzikwa kijijini kwake Muheza mkoani Tanga.
Mzee Godfrey Mngodo aliyezaliwa Februari 7 mwaka 1939 pia alikuwa miongoni mwa watangazaji wa mwanzo wa iliyokuwa Tanganyika Broadcasting Corporation kabla ya kubadilishwa na kuwa Redio Tanzania Dar es salaam.
Atakumbukwa pia kama mwanzilishi wa chumba cha habari mara kilipoanzishwa kituo cha utangazaji cha Dar es salaam Televisheni , DTV mwaka 1994 na aliendelea kutumikia kituo hicho baada ya kuanzishwa pia kituo cha CHANNEL TEN kama Msimamizi wa habari na baadaye Meneja rasilimali watu mpaka alipostaafu mwishoni mwa mwaka 2008.
Idhaa ya Kiswahili ya Sauti ya Amerika inatoa pole kwa ndugu na jamaa na Marafiki wa Marehemu Godfrey Mngodo.