Aliyekuwa 'mpambe' wa Godbless Lema 'amwanika'


[video] Lowassa alipohojiwa na Tido Mhando


Rais Kikwete azindua Chuo cha Ukamanda na Unadhimu, Duluti


Mkuu wa Chuo Cha Ukamanda na Unadhimu Meja Jenerali Ezekiel Kyunga kulia akimuonyesha Amiri Jeshi Mkuu Rais Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete maeneo mbalimbali ya Chuo hicho muda mfupi baada ya Rais Kikwete kuzindua Chuo hicho eneo la Duluti nje kidogo ya mji wa Arusha leo.Kushoto ni Mkuu wa Majeshi Jenerali Davis Mwamunyange.

Tamko la THBUB kulaani matukio katika kampeni za Uchaguzi Mkuu

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Tamko la kulaani mauaji na matukio ya uvunjifu wa sheria wakati wa kampeni za uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani huko Tarime

TUME ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) imesikitishwa sana na vurugu za ushabiki wa kisiasa zilizoanza kujitokeza wakati wa mikutano ya kampeni za vyama vya siasa katika sehemu kadhaa nchini.

Matukio ya uvunjifu wa amani na sheria za nchi ambayo yametangazwa na vyombo vya habari hivi karibuni, ni tofauti na jinsi mikutano mikubwa iliyofanyika kwa amani siku za mwanzo za uzinduzi wa kampeni za vyama na wagombea urais wa vyama vya siasa.

Kwa mujibu wa taarifa za vyombo vya habari inaonyesha kwamba kuna ongezeko la vurugu zinazotokea kutokana na wafuasi wa vyama vya siasa kuingiliana katika mikutano ya kampeni na kusababisha vurugu, ama wafuasi hao kupigana.

Tume imepata taarifa ya kutokea vurugu kama hizo ambazo zimesababisha kifo cha mtu mmoja na watu wengine kujeruhiwa kwa kukatwa mapanga, uharibifu wa gari la mgombea ubunge wa jimbo la Tarime mjini, Bi. Esther Matiko. Vurugu hizo zilizowahusisha wafuasi wa

vyama vya CCM na CHADEMA zilitokea kijiji cha Mangucha, jimbo la Tarime Vijijini, Septemba 10, 2015.

Pia Tume imesikitishwa na taarifa za vyombo vya habari zinazoelezea vurugu zilizofanyika hivi karibuni wakati wa kampeni zinazoendelea katika baadhi ya maeneo nchini, yakiwemo majimbo ya uchaguzi ya Kyela, Bunda mjini, Dodoma mjini, Dar es Salaam na Zanzibar.

Matukio haya yote ni ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu, na yanaenda kinyume na Maadili ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani ya Mwaka 2015 yaliyotiwa saini na vyama vya siasa, ambayo yanavitaka vyama vya siasa na wahusika wote kukataa na kulaani vitendo vya vurugu, fujo, chuki, mafarakano, matumizi ya lugha za matusi na kejeli na kubeba silaha yoyote inayoweza kumdhuru mtu.

Tume inalitaka Jeshi la Polisi kuhakikisha linatoa ulinzi wakati wa mikusanyiko yote wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu.

Kila ilipopata fursa ya kukumbusha umuhimu wa amani wakati wa uchaguzi, THBUB imefanya hivyo. Tume inapenda tena kuchukua fursa hii kuwakumbusha viongozi wa vyama vya siasa kuwaasa wanachama na wafuasi wao kuzingatia amani wakati wote wa mchakato wa kampeni na hadi uchaguzi tarehe 25 Oktoba 2015. Aidha, Tume inawakumbusha viongozi wa vyama vya siasa kuacha kabisa kauli zinazoweza kuchochea wafuasi wao kufanya fujo na vitendo vya uvunjifu wa amani.

Kutokana na hali hiyo Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora inalaani vikali vitendo hivyo na kutoa rai kama ifuatavyo:
  1. Vyama vya Siasa, wagombea na wafuasi wao wazingatie Maadili ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani ya Mwaka 2015. Aidha, viongozi wa vyama vya Siasa wawahamasishe na kuwasisitiza wafuasi wao kutanguliza uzalendo zaidi, kuwa na uvumilivu wa kisiasa na umuhimu wa kuilinda amani hasa kipindi hiki cha kampeni na kuelekea upigaji kura.
  2. Wanasiasa wafanye kampeni za kistaarabu na kujiepusha na matamshi au vitendo vitakavyoashiria uvunjifu wa amani vinavyoweza kuwatia hofu wananchi hata washindwe kujitokeza kwenye mikutano ya kampeni.
  3. Wananchi na wafuasi wa vyama kwa ujumla waache jazba na tabia ya kujichukulia sheria mkononi hali inayohatarisha amani na utulivu wa nchi.
  4. Wananchi watambue kuwa wanao wajibu wa kuheshimu uhuru na haki za watu wengine, ikiwemo haki za kuishi na uhuru wa kujumuika na kushiriki katika masuala ya kisiasa.
  5. Jeshi la Polisi lifanye uchunguzi wa kina na kuwafikisha mbele ya vyombo vya sheria wote watakaobainika kuwa walihusika na mauaji, au uharibifu wa mali na vurugu zilizotokea maeneo mbalimbali.
  6. Mwisho, Tume inatoa wito kwa wananchi kutoa ushirikiano kwa Jeshi la Polisi katika kuhakikisha wale wote waliohusika na matukio ya mauaji, vurugu na uharibifu wa mali wanakamatwa na kufikishwa katika vyombo husika ili sheria ichukue mkondo wake.

Imetolewa na:

TUME YA HAKI ZA BINADAMU NA UTAWALA BORA
Septemba 13, 2015

TUME YA HAKI ZA BINADAMU NA UTAWALA BORA
Kitalu Na. 8, Mtaa wa Luthuli
S.L.P 2643, DAR ES SALAAM
Simu: +255 22 2135747/8; 2137125; 2135222
Faksi: +255 22 2111281
Barua Pepe: [email protected]
Tovuti: www.chragg.go.tz

Mnyika: Mimi na Kubenea, moto utawaka Bungeni! - DART na fidia UbungoMadaktari 40% wameacha taaluma – Twaweza: Huduma za Elimu na Afya


Mnyika azungumzia CCM, Taarifa za mwandishi wa Uhuru na waangalizi wa uchaguzi
Polepole: Magufuli na kujikosoa namfananisha na Mwl. Nyerere na tujisahihishe


MAGUFULI NA KAMPENI ZA KUJIKOSOA, NAMFANANISHA NA MWALIMU NYERERE NA KAULI YA TUJISAHIHISHE


Kumekuwa na maoni kutoka kwa wadau mbalimbali kuhusu mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kupitia CCM, Dr. John Pombe Magufuli, kuibua na kuzungumzia mapungufu ya serikali ambayo yeye ni waziri. Baadhi ya watu wanaofuatilia kampeni zake wameenda mbali zaidi na kuhisi kuwa kwa kufanya hivyo, Magufuli anawafanyia kampeni labda bila yeye kujua wapinzani wake katika kinyang’anyiro cha Urais.

Bila shaka, kwa watu wenye mtizamo huo, kampeni za Magufuli zingekuwa zinatawaliwa na maneno yaliyoyajaa sifa nzuri za utendaji wa serikali na chama tawala. Kwa hiyo, kwa mtizamo huo, ni jambo la kushangaza kuona kuwa Magufuli anakosoa serikali aliyomo badala ya kuisifia na kuipamba majukwani. Kwa sababu hiyo, baadhi ya watu wanasema kuwa Magufuli anazungumza kama vile anagombea kupitia vyama vya upinzani.

Maoni ya namna hii pia yamekuwa yakielekezwa kwa katibu mkuu wa CCM, Ndg. Abdulrahaman Kinana, ambaye katika shughuli zake za kisiasa za chama chake katika maeneo mbalimbali hapa nchini amesikika mara nyingi akiikosoa serikali ya chama ambacho yeye ni katibu mkuu. Watanzania watakumbuka kuwa Ndg. Kinana aliwahi kuwaita baadhi ya mawaziri wa serikali hii 'mizigo' na kutaka wawajibishwe kwa kushindwa kutimiza wajibu wao kwa ufanisi. Kwa baadhi ya watu Ndg. Kinana hakufanya vizuri kuikosoa serikali yake hadharani na hasa kwa kuongea kama mpinzani.

Kitendo cha Magufuli na viongozi wa chama chake kuibua mapungufu na kuikosoa serikali yao hadharani inaonekana kama ni lugha ya wapinzani wa kisiasa. Hakika utamaduni huo ni sawa na kujikosoa mwenyewe. Hata hivyo, ili tuweze kuelewa kama kujikosoa ni jukumu pekee la vyama vya upinzani na wagombea wao, inabidi tujiruhusu kuelimishwa na maneno ya hekima aliyekuwa Rais na mpigania uhuru wa Guinea Bissau, kamarade, Amilcar Cabral ambaye alishawahi kusema kuwa kwa kiongozi au anayetaka kuwa kiongozi wa umma sharti awe na mwenendo wa kutoficha ukweli: Kwa maneno yake;

"Hide nothing from the masses of our people.Tell no lies.Expose lies whenever they are told. Mask no difficulties, mistakes, failures. Claim no easy victories."

Tafsiri yake ni kuwa, kiongozi asifiche chochote kwa wananchi. asiseme uongo, afichue uongo kila unapoibuka. Asifiche matatizo, makosa, mapungufu na kushindwa. Asijipe sifa nyepesi nyepesi.” Kutokana na hekima ya Amilcar Cabral ilivyoelezwa hapo juu, ni wazi kuwa anachofanya Magufuli ndicho haswa kinachotakiwa kufanyika. Kwa kufanya hivyo, Magufuli anaonyesha wazi kuwa anajua matatizo na mapungufu yaliyopo na badala ya kuyafunika na kuyapaka rangi anayaweka wazi. Bahati nzuri Magufuli amekuwa akielezea namna atakavyoshughulikia hayo matatizo na mapungufu. Bahati nzuri tabia hii ya Magufuli siyo mpya. Watanzania watakumbuka kuwa hulka hii ya Magufuli ilijionyesha wakati hata alipokuwa waziri chini ya Rais Benjamin Mkapa alipoikosoa Ofisi yake hadharani kwa baadhi ya watumishi wa ofisi hiyo kujimilikishia magari ya umma isivyo halali. Katika kipindi hiki cha kampeni, Magufuli amekuwa akitoa mapungufu ya serikali hata pale ambapo Rais Kikwete yupo.

Sambamba na Amilcar Cabral, Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere aliwahi kuandika kitabu mwaka 1962 kiitwacho "Tujisahihishe" akitaka Watanzania na hasa viongozi wawe tayari muda wote kujisahihisha. Katika kitabu hicho Baba wa Taifa, alisema kuwa “makosa ni makosa bila kujali ni nani ameyafanya. Muhimu ni kuyajua makosa hayo na kujisahihisha.” Katika kitabu hicho, Mwalimu Nyerere aliendelea kusema;

“Kujielimisha ni kujua ukweli wa mambo na kuwa na ujuzi wa sababu mbalimbali za mambo; na kama mambo hayo ni mabaya ni kujua jinsi ya kuyaondoa; na kama ni mema, jinsi ya kuyadumisha. Mpumbavu ni yule anayeyapa mambo sababu zisizo za kweli na kushauri dawa isiyo ya kweli katika kutafuta sababu za matatizo na jinsi ya kuyaondoa(Nyerere, 1962, 5).”

Kwa maelezo hayo ya Baba wa Taifa, ni wazi kuwa Magufuli ameamua kuwa mkweli katika kampeni zake na ameepuka kuwa mpumbavu kama alivyobainisha Baba wa Taifa.

Kujikosoa anakofanya Magufuli kunadhihirisha aina ya Rais tunayemhitaji. Itakuwa ni hatari kubwa kuwa na Rais asiyetayari kujikosoa au kukosolewa. Ni janga kubwa kwa nchi kuwa na Rais ambaye anaamini kuwa yeye ni mtakatifu asiyekosea. Rais wa namna hiyo ni lazima atakuwa ni dikteta na watakodhubutu kumkosoa na kuibua makosa yake watakiona cha moto. Kama historia za nchi mbalimbali inavyoonyesha, hili likitokea, Tanzania itakuwa katika dhahama kubwa.

Maandiko ya vitabu vitakatifu yanatuelekeza kuwa ukamilifu wa binadamu huja kwa kusimama katika ukweli, kujikosoa na kukubali kukosolewa na kuepuka hadaa. Vivyo hivyo, ukamilifu na uhai wa taasisi zinazoundwa na binadamu kama vile vyama vya siasa na serikali lazima viwe na uthubutu wa kujikosoa na kukubali kukosolewa kama anavyofanya Magufuli.

Kwa maelezo hayo hapo juu, ni ni wazi kuwa ukosoaji siyo jukumu pekee la vyama vya upinzani bali ni jukumu la kila mmoja hasa wale wanaotaka kuwa viongozi wetu. Hivyo, badala ya kumshangaa Magufuli kwa kubainisha makosa na mapungufu ya serikali ambayo yeye ni sehemu yake, tujielekeze katika kuwataka wagombea wengine katika nafasi mbalimbali waepuke hadaa na badala yake wafanye kampeni zao kwa kueleza ukweli.

Hadaa katika kampeni zitatupatia viongozi matapeli ambao bila shaka uongozi wao utakuwa wa hadaa kwa wananchi. Kinyume chake kiongozi mkweli na aliye na uthubutu wa kujikosoa anaonyesha kuwa ana uwezo wa kutafuta suluhisho la kweli la matatizo yaliyopo.

Kwa kuitimisha, Magufuli hajachemka katika kuikosoa serikali aliyomo bali, kwa kufanya hivyo, anaonyesha ufahamu wake wa hali halisi ilivyo. Zaidi, anaonyesha kuwa yeye ni mtu aliyetayari kusimamia ukweli jinsi ulivyo na hivyo ndivyo inapaswa kuwa.

Humphrey Polepole
@Twitter