Gari la JKT lapata ajali na kuua vijana 6 na kuacha 21 mahututi

Update kutoka Kigoma Live blogKatibu Tawala wa mkoa Kigoma Injinia John Ndunguru (kushoto) akiongoza kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa kigoma kuaga miili ya vijana wa jeshi la kujenga Taifa waliofariki kwenye ajali ya gari juzi nje kidogo ya manispaa ya kigoma ujiji vijana hao wamesafirisha jana kuelekea makwao kwa taratibu za mazishi.


Mkuu wa kambi ya JKT Bulombora kikosi cha 821 Luteni Kanali Mohamed Mketo (kushoto) akitoa heshima kwa vijana wa JKT waliofariki kwa ajali ya gari mkoani Kigoma juzi ambapo vijana hao walisafirishwa jana kuelekea kwenye mikoa yao kwa mazishi.


Baadhi ya wanajeshi wa jeshi la wananchi wa Tanzania na wapiganaji kutoka JKT Bulombora wakitoa heshima kuaga miili ya vijana wa JKT waliofariki kwa ajali ya gari juzi mjini Kigoma. (Picha na Fadhil Abdallah).

KATIBU Tawala wa Mkoa wa Kigoma, Eng. John Ndunguru, leo mchana amewaongoza waombolezaji kuaga miili ya askari saba wa Jeshi la Kujenga Taifa Kikosi cha 821KJ Kambi ya Bulombora mkoani Kigoma, ambao wamefariki dunia jana katika ajali ya gari.

Akiongea kwa niaba ya serikali wakati wa kuaga miili ya askari hao ambao wawili kati yao walikuwa askari wa kudumu na watano wa kujitolea, John Ndunguru, ametoa pole kwa wafiwa wote sambamba na kuwataka wananchi pamoja na uongozi wa jeshi kuwa wavumilivu katika kipindi hiki cha majonzi.

Kabla ya miili ya askari hao kusafirishwa, Mkuu wa Vikosi vya Jeshi mkoani Kigoma Kanali Mamdali Msuya, kwa niaba ya Mkuu wa Majeshi ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania,ametoa shukrani kwa watu wote walioungana na jeshi baada ya tukio hilo vikiwemo vikosi mbali mbali vya majeshi na Hospitali ya Maweni.

Ajali hiyo ilitokea jana jioni majira ya saa kumi na nusu katika kijiji cha Kasaka eneo la mzani, wakati askari hao wakisafiri kutoka kikosini Bulombora kwenda mjini Kigoma kikazi kwa kutumia gari lenye namba 57117 JW 09 mali ya jeshi, ambalo lilipasuka tairi zote za nyuma na kupoteza uelekeo.

Askari waliofariki dunia katika ajali hiyo ni MT 54407 Sajenti Ally Hamidu Kambanga na MT 108155 Abel Tadei Maisha ambao walikuwa askari wa kudumu na wengine AH 6831 SM (Service Man), Eugine Stephano Butati, AH 7190 SM Said Sadala Said, REC (Recruit) Abubakar Salum Washokera, REC Bakari Ramadhani Kibaya na REC Frederick Kahemela Ephrahim.

Askari wengine 22 ambao wamejeruhiwa na kulazwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kigoma, Maweni, kufuatia ajali hiyo, wametajwa kuwa ni Benedicto Ndokeye, Raphael Kibamba, Antanas Emmanuel, Abuu Nzoghe Hassan, Abubakar Mathias Peter, Bakari Sinuki Mwaisunga, Deus Manyanya Charles, Peter Edward Nyanda, Elias Masaga Magesa, Geofrey Peter Malik na King Lucas Kasofu.

Wengine ni Camilius William Hagida, Lameck John, Martin Andrew Lupatu, Steven Denis Mtege, Said Omary Kitogo, Said Suleiman Zuberi, Shabani Idd Zakaria, Victor Adelbert, Jackson John Nyarubi, Mohamed Jackson Nyimbo na Abubakar Hassan Mkubi, ambao kulingana na Mganga Mfawidhi wa Hospitali hiyo Dr.Fadhil Kibaya wengi hali zao zinaendelea vizuri.

(picha via JamiiForums)

Vijana 6a waliokuwa katika mafunzo ya kijeshi ya kujitolea katika kikosi cha 821 JKT Bulombora mkoani Kigoma wamefariki dunia na wengine 21 kujeruhiwa vibaya kutokana na ajali ya gari iliyotokea jioni ya Oktoba Mosi, 2015.

Mganga Mfawidhi wa hospital ya mkoa wa Kigoma Dkt. Fadhil Kibaya amekaririwa na blogu ya Michuzi akisema
"Ni kweli leo majira ya saa moja jioni tumepokea miili minne ya vijana wa JKT ambao waliletwa hapa tayari wamefariki na majeruhi 21. "Wengine wawili wamefariki hapa hapa wakati tukiendelea kuwapa huduma"
Alisema hali za majeruhi hazikuwa nzuri sana kwani wengi waliumia sehemu za kichwa
"Bado tunaendelea na jitahada za kuwapatia matibabu na majina ya waliopoteza maisha pamoja majeruhi tutatoa kesho, sababu majeruhi wengi hawana fahamu"alisema.
Kamanda wa polisi mkoa wa Kigoma Afande Ferdinand Mtui alisema chanzo cha ajali hiyo ni gari la jeshi kushindwa kupanda mlima na kusababisha tairi mbili za nyuma kupasuka.

Alisema ajali hiyo imetokea katika eneo la Kasaka karibu na mizani ambapo lori hilo la jeshi lilikuwa likitoka mjini kwenda kambini likiwa limebeba masanduku ya soda na unga.

Kamati ya ulinzi na usalama ikitembelea vijana wa JKT Bulombora kikosi namba 821 ambao ni majeruhi wa ajali wakiwa wodi namba 7 katika hospital ya mkoa wa Kigoma wakiendelea kupatiwa matibabu
Baadhi ya vijana wa JKT Bulombora kikosi namba 821 ambao ni majeruhi wa ajali wakiwa wodi namba 7 katika hospital ya mkoa wa Kigoma wakiendelea kupatiwa matibabu


Ratiba na tarehe ya uchaguzi kwa majimbo walimofariki wagombeaKaimu Mkurugenzi wa NEC, Emmanuel Kawishe akizungumzia uchaguzi wa madiwani na wabunge ulioahirishwa kutokana na kufariki dunia wagombea, alisema uchaguzi huo utafanyika Novemba 22 mwaka huu.

Uchaguzi huo utahusisha majimbo ya Lushoto na Ulanga Mashariki na kata tano za Bomang’ombe (Hai), Bukene (Shinyanga), Msingi Mkamala (Singida), Muleba (Kagera) na Uyole (Mbeya).
“Mchakato wa uchaguzi huo utakuwa kama ifuatavyo: Uteuzi utafanyiaka Oktoba 12, kampeni Oktoba 13 hadi Novemba 18 isipokuwa siku ya uchaguzi Oktoba 25 na 26 na siku ya kupiga kura itakuwa Novemba 22 mwaka huu” 
alisema Kawishe. [via MTANZANIA]

Waliotibua NCCR-Mageuzi wasema walilipwa na CCM kuhujumu UKAWA
CHAMA cha NCCR Mageuzi kimetibua njama za kuuhujumu na kuufarakanisha Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) zilizolenga pia kusababisha mauaji kwa Mwenyekiti wake, James Mbatia.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Mwenyekiti Mwenza wa Ukawa, James Mbatia aliyefuatana na viongozi wa juu wa chama hicho, alisema mkakati huo uliwahusisha makamishna wa chama hicho waliohudhuria pia mkutano huo, na uliratibiwa na Makamu mwenyekiti wa chama hicho, Leticia Mosore.

Huku akionyesha vielezo vya picha na video, Mbatia ambaye pia ni mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, alidai Mosore ametenda makosa ya jinai yakiwamo ya kupanga njama za kudhuru na mauaji hivyo ushahidi huo unapelekwa polisi kwa hatua zaidi.

Alidai Mosore alianza hujuma hizo Septemba 17 mwaka huu kwa kuzungumza na waandishi wa habari katika Hoteli ya Land Mark Dar es Salaam ambako alitoa waraka uliolaumu hatua ya chama hicho kujiunga na Ukawa.

“Cha kusikitisha ni baadhi ya viongozi wa juu wa chama wanapokwenda kinyume na Katiba na sheria za chama. Tarehe 17 Septemba mwaka huu, Mama Leticia Mosore alizungumza na waandishi wa habari na kumlalamikia mwenyekiti kuwa anadhoofisha chama na amekuwa msemaji wa Chadema,” alisema Mbatia.

Hata hivyo, Mbatia alimtetea Katibu mkuu wa chama hicho aliyekuwapo pia kwenye mkutano huo, akisema hakuzungumzia mambo ya chama bali migongano tu ya Ukawa.

“Katibu Mkuu, Nyambabe Mosena alikuwapo ila hakuzungumzia mambo ya chama bali migongano ya Ukawa ambayo tunakubaliana,” alisema.

Alisema Mosore amekiuka katiba ya chama hicho na kwamba na amesimamishwa uongozi huku hatua nyingine zikifuata.

“Baada ya kikao chake tulimwita katika kikao nilichokiongoza mimi mwenyewe na alijitetea na mengine akakiri. Kikao kile kwa niaba ya Halmashauri Kuu kilimsismamisha uongozi,” alisema.

Aliendelea kumtuhumu Mosore kuwa alikula njama kwa kuwatumia fedha makamishina wa chama hicho kwa ajili ya kupanga mpango wa kumdhuru na kumfarakanisha na Ukawa.

“Alikuwa akituma fedha kwa makamishina hawa na alishirikiana na CCM, ushahidi upo. Kwa mujibu wa Katiba yetu, ukihujumu chama kwenye uchaguzi unafukuzwa uanachama.

“Septemba 17 nilipokea ujumbe wa kutishiwa maisha na kulikuwa na taarifa za wanachama wa chama chetu kuvalishwa sare ili wanivamie na kunidhuru,” alidai Mbatia.

Alisema kutokana na tishio hilo, Mwenyekiti wa Baraza la wadhamini wa chama hicho, Mohamed Tibanyendera alitoa taarifa na kufikisha taarifa Polisi.

Alisema katika mkakati huo waliwatumia makamishina wanne wa chama hicho ambao ni Peterson Mshenyera kutoka Kagera, Rajab Mawaya kutoka Mkoa wa Pwani, Ame Mshindani kutoka Kaskazini Unguja na Rajab Amran kutoka Mwanza kwa kuwalipia fedha za kujikimu (Sh 60,000 kila siku na tiketi za ndege).

Licha ya fedha hizo, alisema makamishina hao walilipwa Sh 400,000 jana na waliahidiwa kupewa Sh milioni 10 kama kiinua mgongo chao na walikuwa wakifanya vikao eneo la Segerea Dar es Salaam kwa kada wa CCM aliyewahi kuwa mkuu wa wilaya (jina linahifadhiwa) tangu Septemba 22.

“Leo (jana) walitakiwa waende Hoteli ya Peacock kusoma waraka walioandaliwa. Lakini kwa kuwa tulikuwa tunawasiliana tangu awali, tuliwachukua na kuwapeleka sehemu nyingine na simu zao zikabadilishwa. Ndiyo maana mlisikia kuwapo mkutano wa habari pale,” alisema Mbatia.

Akizungumzia njama hizo, kamishna wa chama hicho, Peterson Mshenyera alisema alihusishwa tangu Septemba 19.

“Nilihusishwa kwenye mkakati huo siku mbili baada ya kuzungumza na waandishi wa habari. Ninavyo vielelezo kwenye simu yangu. Awali nilisita lakini niliwasiliana na Mwenyekiti na akaniimarishia ulinzi,” alisema Mshenyera na kuongeza:

“Waliongeza makamishna wengine bila kujua kuwa ndiyo wanaharibu. Leo tumelipwa Sh 400,000 na tuliahidiwa Sh milioni 10.”

Huku akisitiza kutomtaja jina, Mshenyera alisema kuna kiongozi wa CCM ambaye ni Mwenyekiti wa Jumuiya mojawapo ya chama hicho aliyekuwa akiratibu njama hizo.

“Siwezi kumtaja kiongozi huyo kwa sababu hawa watu wana hela nyingi, nahofia usalama wangu. Huu waraka una maneno ya kumtukana Lowassa (Edward- mgombea urais wa Ukawa), Sumaye (Frederick- Waziri Mkuu mstaafu) na Ukawa na unavitaka vyama vya CUF na NLD kutopigia kura Ukawa,” alisema.

Alisema baada ya kusoma waraka huo walipanga kusafiri nchi nzima kuutangaza na mpango wa pili ulikuwa ni kuivuruga halmashauri kuu ya chama hicho na mwisho kuuvuruga mkutano mkuu.

“Tumesema hatuwezi kumtukana baba yetu, hatuwezi kukiharibu chama chetu na kutukana Ukawa,” alisema.

Alipotafutwa kwa njia ya simu, Makamu mwenyekiti wa chama hicho, Leticia Mosore alisema hana taarifa za kusimamishwa uongozi wala njama hizo.

“Hizo taarifa siyo za kweli, kwanza mimi naumwa niko nyumbani. Hapa nilipo nasikia baridi nataka kwenda hospitali,” alisema Mosore.

Alikiri kuitwa kwenye kikao cha viongozi wa juu wa chama hicho, Septemba 18, lakini akasema walijadili masuala ya chama.

“Ni kweli tulikuwa na kikao na tulijadili mambo ya chama. Hayo mengine mimi sijui, niko nyumbani naumwa. Wewe ni mwandishi wa pili kunipigia simu kuuliza mambo hayo,” alisema Mosore.

Taarifa ya NACTE kwa umma ya Oktoba Mosi, 2015

Taratibu za usajili wa Taasisi na Vyuo vya Elimu ya Ufundi, Ithibati ya Taasisi na Vyuo vya Elimu ya Ufundi, mitaala iliyoidhinishwa kutumika katika kutoa elimu ya mafunzo ya ufundi, Utambuzi wa idara zinazotoa kozi mpya, usajili wa walimu; Kuongezwa kwa Muda wa Usajili wa Wanafunzi Wanaomba Kujiunga katika Vyuo na Taasisi za Ufundi katika Mwaka wa Masomo 2015/2016 na Kufungua Vyuo na Taasisi za Elimu ya Ufundi 2015/2016.

Maamuzi ambayo yamefanyika yanafafanuliwa zaidi kama ifuatavyo:

1. Usajili wa Taasisi na Vyuo vya Elimu ya Ufundi

Kwa mujibu wa Sheria iliyoanzisha Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (Na. 9 ya mwaka 1997) na Kanuni za Usajili Na. 13 za mwaka 2001, vyuo na taasisi za serikali na zisizo za serikali zinazotoa elimu na mafunzo ya ufundi zinatakiwa kusajiliwa ili ziweze kuendesha mafunzo. Usajili unalenga kuhakikisha kuwa chuo au taasisi ya elimu na mafunzo ya ufundi imeanzishwa kisheria na ina uwezo, nyenzo na rasilimali za kutosha kuwezesha kutoa mafunzo yenye ubora.

Baraza katika kikao chake cha 57 liliidhinisha usajili wa kudumu kwa vyuo na taasisi zipatazo 143 na usajili wa muda kwa vyuo na taasisi 102 na kufanya hadi sasa kufikisha idadi ya vyuo vilivyosajiliwa na Baraza kuwa 567 (Jedwali Na. 1). Baraza linapenda kuukumbusha umma wa Tanzania kusoma katika vyuo na taasisi ambazo zimesajiliwa ambazo zimetimiza masharti na vigezo vya utoaji elimu ili kupata elimu bora. Baraza pia linawataka wale wanaoendesha vyuo kiholela bila usajili kuacha tabia hiyo mara moja na kuchukua hatua kufuata taratibu za kusajili vyuo/ taasisi hizo kwa mujibu wa sheria.

2. Ithibati ya Taasisi na Vyuo vya Elimu ya Ufundi

Baraza pia lina mamlaka ya kutoa ithibati kwa taasisi na vyuo kwa mujibu wa sheria ya Baraza na Kanuni za Ithibati za mwaka 2001. Ithibati hutolewa kwa vyuo vyenye usajili wa kudumu na kutimiza vigezo vya ithibati. Ithibati inahusisha masuala mbalimbali ikiwemo uongozi na utawala wa chuo/taasisi, mpango wa kudhibiti na kusimamia ubora wa mafunzo pamoja na tathmini ya utendaji wa chuo. Katika ithibati Baraza huangalia pia uwezo wa taasisi/chuo wa kuendesha programu za mafunzo kwa viwango vya ubora unaokubalika kimataifa na kimataifa.

Hivyo basi katika kikao chake cha 57 Baraza lilitoa ithibati kwa vyuo na taasisi 27 na kufanya vyuo na taasisi zenye ithibati kufikia 124 (Jedwali Na. 2). Baraza linapenda kutumia nafasi hii kuvitaka vyuo vyenye Usajili wa kudumu kukamilisha vigezo vya ithibati ili kuweza kufikia ngazi ya ithibati ambayo ni ya juu katika utoaji wa mafunzo katika vyuo vya ufundi.

3. Mitaala Iliyoidhinishwa Kutumika Katika Kutoa Elimu na Mafunzo ya Ufundi

Mojawapo ya masharti ya usajili na ithibati ni chuo au taasisi ya elimu na mafunzo ya ufundi kuwa na mitaala iliyoidhinishwa na Baraza. Baraza huratibu uandaaji wa mitaala inayozingatia umahiri kulingana na mahitaji ya soko la ajira na muundo wa tuzo (NTA) ambao unatoa taarifa sahihi juu ya madhumuni na matarajio ya elimu na mafunzo. Kwa vyuo na taasisi zisizo na uwezo wa kuandaa mitaala yake, Baraza limechukua hatua ya kuandaa baadhi ya mitaala ya kitaifa kwa mujibu wa kifungu Na.11 cha Sheria ya NACTE.

Baraza katika kikao chake cha 57 kiliidhinisha mitaala 169 inayozingatia umahiri kutumika katika ufundishaji wa taaluma mbalimbali zitolewazo vyuo na taasisi za ufundi nchini na kufanya jumla ya mitaala ambayo tayari imeidhinishwa kutumika katika vyuo na taasisi za ufundi kufikia 512 (Jedwali Na. 3). Baraza lingependa kuwaomba wananchi kutokusoma katika kozi yoyote itolewayo na chuo au taasisi ya ufundi ambayo haina mtaala ulioidhinishwa na Baraza.

4. Utambuzi wa Idara Zinatoa Kozi Mpya


Baraza pia lina mamlaka ya kuidhinisha Kozi yoyote mpya ambayo chuo/taasisi inataka kutoa ili kuhakikisha kuwa idara itakayotoa mafunzo hayo imefikia vigezo vya utoaji elimu bora kama ilivyoainishwa katika Kanuni za Baraza za Ithibati na Utambuzi wa Idara za 2001.

Katika kikao cha 57 Baraza lilitoa idhini kwa idara 91 kutoka vyuo na taasisi mbalimbali kutoa kuanzisha kozi mpya 62 (Jedwali Na. 4). Tunawaomba wananchi wanaotaka kupata elimu kusoma katika kozi ambazo zimepitishwa na Baraza ili waweze kupata elimu bora na kutambulika kitaifa na kimataifa.

5. Usajili wa Walimu

Baraza pia linatoa usajili kwa walimu wanaofundisha katika vyuo na taasisi za elimu ya ufundi ili kuhakikisha kuwa vyuo na taasisi za elimu ya ufundi zinakuwa na walimu wenye sifa stahiki na wenye uwezo wa kutoa elimu bora kwa wanafunzi.

Katika kikao cha Baraza cha 57 walimu 748 walisajiliwa na kufikisha idadi ya walimu 3325 waliosajiliwa wanaofundisha katika vyuo na taasisi za elimu ya ufundi. Baraza linapenda kuwakumbusha viongozi wa vyuo na taasisi za elimu ya ufundi kuhakikisha kuwa walimu wanaofundisha katika vyuo/taasisi za elimu ya ufundi wana sifa stahiki na waliosajiliwa na Baraza.

6. Kuongezwa kwa Muda wa Usajili wa Wanafunzi Wanaomba Kujiunga katika Vyuo na Taasisi za Ufundi katika Mwaka wa Masomo 2015/2016

Baraza linapenda kuutaarifu umma kuwa muda wa kufanya udahili kwa wanafunzi wanaoomba kujiunga na mafunzo kwa njia ya kielectronic kupitia mfumo wa udahili wa pamoja (CAS) umeongezwa mpaka tarehe 16/10/2015 kwa wanafunzi wenye stashahada wanaotaka kujiunga katika ngazi ya shahada katika elimu ya juu na wale wanaotaka kujiunga katika ngazi za astashahada na stashahada katika kozi za afya. Hivyo Baraza linawaomba wale ambao hawajaomba na wana nia ya kujiunga na mafunzo katika mwaka huu wa masomo watumie nafasi hii kutuma maombi yao sasa.

7. Kufungua Vyuo na Taasisi za Elimu ya Ufundi 2015/2016

Baraza linapenda kuwataarifu viongozi na wamiliki wa vyuo na taasisi za elimu ya ufundi kufungua vyuo na taasisi zao mwezi Novemba 2015 ili kuruhusu wanafunzi kupata fursa nzuri ya kushiriki kikamilifu katika uchaguzi Mkuu ujao utakaofanyika tarehe 25/10/2015. Aidha, kwa vyuo na taasisi ambazo zilishafunguliwa na kuanza masomo, watatakiwa kufunga wiki mbili katika kipindi cha uchaguzi ili kutoa nafasi kwa kila mwanafunzi kushiriki katika uchaguzi na kupiga kura katika eneo alilojiandikisha.

Agizo la Serikali kupitia NACTE kwa Vyuo kuhusu siku ya Kupiga KuraKaimu Katibu Mkuu wa Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE), Dk Adolf Rutayuga ameeleza maamuzi hayo akisema,
“...hili ni agizo la Serikali, kwamba wanafunzi waendelee kwenye likizo mpaka mwezi Novemba watakapofungua ili nao washiriki kikamilifu kwenye Uchaguzi huo Mkuu. Wapewe ruhusa walikokuwa wamejiandikisha sasa kuweza kutumia nafasi yao hiyo kumchagua kiongozi wanayemtaka, ambayo ni tarehe 25 mwezi wa kumi mwaka 2015.
Aidha kwa vyuo na taasisi ambazo zilishafunguliwa na kuanza mafunzo, wanaagizwa kufunga wiki mbili katika kipindi cha uchaguzi ili kutoa nafasi kwa kila mwanafunzi kushiriki katika uchaguzi nak upiga kura katika eneo alilojiandikisha. Hii ina maana kwamba, wiki moja kabla ya tarehe 25 mwezi wa kumi, Vyuo hivi ambavyo vina wanafunzi tayari, wanapaswa kufunga na watakuwa na wiki nyingine moja, baada ya uchaguzi.”
Taarifa ya mwisho katika video hii kutoka EATv inazungumzia agizo hilo...


[video] Kauli ya Wauguzi kuhusu taarifa "Madaktari, Wauguzi wataka mabadiliko"


Madaktari, Wauguzi wataka mabadiliko


TAASISI nne zinazojihusisha na masuala ya afya ya binadamu, zimekubaliana kwa pamoja kuunga mkono mabadiliko katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25 mwaka huu.

Taasisi hizo ni Jumuia ya Madaktari Tanzania (MAT), Chama cha Wauguzi Tanzania (TANNA) Jumuia ya Wafamasia Tanzania (PST) pamoja na Jumuiya ya Madaktari Wasaidizi Tanzania (AMEPTA).

Viongozi wa taasisi hizo walitoa tamko hilo la pamoja katika Ukumbi wa Hoteli ya Mtakatifu Theresa, mjini Bukoba mkoani Kagera jana wakisema wanaunga mkono mabadiliko ya siasa kuelekea uchaguzi mkuu ikizingatiwa sekta ya afya inakabaliliwa na changamoto nyingi, hivyo inahitaji mabadiliko ya siasa kupata muafaka wa afya ya Watanzania.

Akisoma tamko hilo kwa kwa niaba ya wenzake, Rais wa TANNA, Paulo Magesa, alisema wao kama vyama vya kutetea maslahi ya watumishi wa sekta ya afya wanaunga mkono mabadiliko yatakayotokea nchini ingawa hawakuweka wazi mabadiliko hayo ni ya chama kipi cha siasa.

Tamko hilo limebeba kauli mbiu isemayo, “Afya bora kwa wote inawezekana Tanzania, tuamue Oktoba 25”.

Katika tamko hilo, taasisi hizo zimeainisha changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta ya afya ikiwa ni pamoja na ukosefu wa dawa, vifaa tiba na vifaa vya uchunguzi vya kutosha zikisema tatizo hilo linasababishwa na bajeti finyu ya sekta ya afya hususan inayoelekezwa katika upatikanaji wa dawa.

Pia ukosefu wa viwanda vikubwa vya kuzalisha dawa za kutosha zenye ubora stahiki vinavyomilikiwa na serikali na ucheleweshwaji wa malipo kwa ajili ya dawa katika Bohari Kuu ya Dawa (MSD) kutoka serikalini na hivyo kuifanya MSD kushindwa kuagiza dawa za kutosha nje ya nchi.

Changamoto nyingine ni kuwapo msambazaji mmoja wa dawa yaani MSD pekee kwa vituo vyote nchini huku akiwa hajajengewa uwezo wa kutosha na hivyo wakati mwingine kusababisha uchelewaji wa dawa na vifaa tiba katika vituo vya afya.

Akisoma tamko hilo, Magesa alisema hadi kufikia mwaka 2014 uhaba wa wafanyakazi katika sekta ya afya ulikuwa ni asilimia 56, ambayo ni nusu ya wafanyakazi wanaohitajika na hivyo kusababisha watumishi wachache waliopo kufanya kazi kubwa na hata wakati mwingine zilizo nje ya wigo wa majukumu yao.

Magesa alisema wamechukua hatua hiyo madhubuti wakati taifa likiwa katika maandalizi kuelekea uchaguzi mkuu ifikapo Oktoba 25, mwaka huu huku akisisitiza kuwa wanatambua mstakabali na msingi wa mabadiliko ya kweli katika sekta ya afya na hata sekta nyingine za maendeleo zimo mikononi mwa wanasiasa wanaotarajiwa kuchaguliwa, kuanzia madiwani, wabunge na raisi.

Alisema mfano mwaka 2014 pekee, daktari mmoja Tanzania alihudumia wastani wa watu 20,000 tofauti na wastani wa watu 5,000 unaotakiwa kwa mujibu wa kanuni za kitaalamu uliowekwa na Shirika la Afya Duniani (WHO).

Alisema uhaba huo unachangiwa kwa kiasi kikubwa kutokuwapo vyuo vya kutosha kwa ajili ya kutoa mafunzo katika kada za afya ambapo mwaka 2014 vyuo vyote vilitoa wastani wa wahitimu 9,000.
“Kwa malengo ya kuwa na zahanati katika kila kijiji, kituo cha afya kila kata na hospitali kwa kila wilaya nchi nzima tulipaswa kuwa na wastani wa wahitimu 20,000 kwa mwaka kuanzia mwaka 2008 huku pia serikali ikishindwa kuajiri wahitimu wote wanaomaliza katika vyuo vichache vilivyopo.
“Kwa mfano, kwa kada ya udaktari pekee katika wahitimu 700, wahitimu chini ya 300 huajiriwa kila mwaka huku wahitimu 400 waliosoma kwa fedha za serikali wakiwa hawaajiriwi serikalini na hivyo kuamua kufanya kazi nje ya sekta ya afya.
“Hadi mwaka huu wapo wagonjwa wanaolala chini katika hospitali zetu, wapo wanaolala zaidi ya wawili kitanda kimoja na wapo ambao inabidi kuruhusiwa kabla ya kupona vizuri kutoa nafasi kwa wenye hali mbaya zaidi. Hii huwavunja moyo watoa huduma na hata wakati mwingine kushindwa kutoa huduma inayostahili kwa wananchi.
“Zipo sera za huduma bure kwa makundi maalumu, hata hivyo mara nyingine utekelezaji wake umesongwa na uhaba wa dawa na vifaa tiba hata kuleta migogoro kati ya watoa huduma na wahudumiwa.
“Kwa nini tunachukua hatua hii wakati huu kuelekea Uchaguzi Mkuu ifikapo Tarehe 25 Oktoba, jibu ni kwamba tunatambua mustakabali na msingi wa mabadiliko ya kweli katika sekta ya afya na hata sekta nyingine za umma umo mikononi mwa wanasiasa tunaokwenda kuwachagua kuanzia madiwani, wabunge na rais.
“Hivyo tungependa wahudumu au wataalam wa afya na wananchi wote watambue wanapoamua kuacha kupiga kura au wanapopiga kura basi wanaamua mustakabali wa afya yao katika kipindi cha miaka mitano ijayo.
“Hivyo lengo letu kuu ni kuwaelimisha wadau wa afya wote nchini kwamba tusifanye makosa, tuamue afya yetu sasa, tuchague kwa makini, tuchague mabadiliko ya kweli,” alisema rais huyo wa TANNA.
Naye mgeni rasmi katika mkutano huo, Mkuu wa Mkoa wa Kagera, John Mongella alisema baadhi ya changomoto zilizoibuliwa na wataalamu hao wa sekta ya tiba zitatafutiwa ufumbuzi.
“Kweli kama serikali tuna wajibu wa kushughulikia changamoto katika sekta ya afya, sekta hii ni nyeti tunawajibika kutimiza wajibu, baadhi ya changamoto naamini zinawezekana kutatuliwa kama tutajenga utaratibu wa kukaa pamoja na changamoto nyingine ni ubunifu tu ambazo hazihitaji mjadala wa taifa” 

Huduma ya Kwanza wapinga kauli ya UKAWA kuhusu mkutano TangamanoShirika la Huduma ya Kwanza Tanzania Ofisi ya Tanga, limesema viongozi wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) walifanya uamuzi wa kuahirisha mkutano wao uliofanyika uwanja wa wazi wa Tangamano, mkoani Tanga kwa sababu zao na si kwa sababu ya msongamano kama ambavyo iliripotiwa kwenye vyombo vya habari.

Taarifa iliyotolewa na shirika hilo kwa vyombo vya habari na gazeti hili kupata nakala Dar es Salaam jana, ilieleza kuwa;
"Hakuna watu walioumia katika mkutano huo na hakuna ripoti ya tukio hata moja la maafa kwenye hospitali yoyote au kwenye kituo cha afya Tanga kutokana na mkutano huo."
Kwa mujibu wa taarifa hiyo ilieleza kwamba viongozi wa UKAWA waliamua kuahirisha mkutano huo bila kuwahusisha wao wala jeshi la polisi, ambao ni wataalamu kwenye mambo yanayohusu usalama wa raia.

Taarifa hiyo ilieleza kwamba pamoja na kutolewa tamko la kuahirisha mkutano, mgombea urais wa UKAWA (Edward Lowassa) alihutubia kwa muda mfupi na hakukutokea maafa, hivyo angeweza kuendelea kama angependa.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Shirika hilo limewataka wanasiasa kuacha kutumia shughuli za kitaaluma kwa manufaa ya kisiasa hasa katika kipindi hiki cha uchaguzi.

Shirika hilo limesisitiza kwamba katika kipindi cha uchaguzi litaendelea kusimamia usalama wao katika mikutano yote ya kampeni.
"Wananchi waendelee kuhudhuria bila kuwa na woga kuhusiana na usalama wao,"
ilisema taarifa hiyo. Shirika hilo limesema lina wafanyakazi na vitendeakazi vya kutosha kuweza kumudu shughuli za aina yoyote.

Shirika hilo limesisitiza kuwa katika mkutano huo katika Uwanja wa wazi Tangamano, haukuwa na msongamano mkubwa kama ilivyoripotiwa na baadhi ya vyombo vya habari.

Taarifa ya Wizara leo Oktoba Mosi kuhusu Mahujaji

Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa imepokea taarifa za kuwepo Mahujaji wawili kutoka Tanzania ambao wamelazwa katika mojawapo ya hospitali nchini Saudi Arabia baada ya kujeruhiwa kutokana na tukio la mkanyagano wa Mahujaji lililotokea eneo la Mina, Makkah, tarehe 24 Septemba, 2015.

Mahujaji hao ambao wanaendelea kupata matibabu na hali zao zikiendelea vizuri ni Bi. Hidaya Mchomvu na Bi. Mahjabin Taslim Khan

Pia kwa mujibu wa taarifa za Ubalozi Hujaji mwingine anayejulikana kwa jina la Mustafa Ali Mchira amelazwa katika Hospitali ya Ansari Madina katika chumba cha wagonjwa mahututi. Taarifa zinaeleza kuwa Bw. Mchira alipata ugonjwa tangu alipowasili Saudi Arabia na hivyo ugonjwa wake hauhusiani na ajali iliyotokea tarehe 24 Septemba, 2015. 

Vilevile, Serikali ya Saudi Arabia imeanza kutoa taarifa za alama za vidole za Mahujaji waliopata ajali. Hivyo, Ubalozi unazipitia na kuzihakiki taarifa hizo ambazo zitasaidia kuwabaini Mahujaji wetu waliokufa katika ajali hiyo. 

Kutambulika kwa Mahujaji hao waliolazwa, kunatokana na jitihada zilizofanywa na Ubalozi kwa kushirikiana na Tanzania Hajj Mission na Vikundi vya Mahujaji za kutembelea Hospitali zote zilizopo Makkah, Mina, Arafat, Muzdalifa, Jeddah na Taif kwa ajili ya kuwatafuta Mahujaji wa Tanzania waliofariki dunia au kulazwa katika hospitali hizo. 

Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa,
Dar es Salaam.

01 Oktoba, 2015

Tanzania Global Diaspora Week UK 2015


This is to announce to you the ‘Home is best’ Tanzania global diaspora Week UK 2015 and the Tanzania Diaspora Achievement Awards to be held from the 3rd -6th December 2015.

We are showcasing the culture ,trade and investment of Tanzania .This will give opportunities for Businesses to:
  • Have access to several organisations to meet directly with various business people and foreign partners.
  • Access to International buyers of Commodities & produce
  • Access to Service Providers who are interested in doing business in Tanzania
  • An opportunity for Tanzania government and private sector that wants to recruit from the diaspora
We also announce our Tanzania Diaspora community Leaders Gala Dinner and Awards ceremony . The evening provides an opportunity for you to join us in celebrating the vital work of Tanzanians in the Diaspora and friends of Tanzania as well as helping to deliver our mission to bring the UK and Tanzania closer together through our pioneering activities in business, policy and culture.

We present these annual awards to those individuals who exemplify the concept of the ‘Servant Leader’. These awards highlight the links between economic success, professional excellence accompanied by moral leadership, and service to society. By recognising individuals who embody the ‘Servant Leader’ ideal, we seek to encourage widespread recognition and adoption of these values among the global Great lakes community.

For more information please contact
TEL :0776888777/0715241177/00447556130219
[email protected]

Wimbo wa Diamond "CCM Number One" kwa ajili ya kampeni


You are invited to a debate: Political parties on Corruption and Ethics

Twaweza would like to invite you to:

Debate | Political Party debate on the topic Corruption and Ethics


Time: 3:00pm - 5:00pm

Date: Sunday October 4 2015

Venue: Julius Nyerere International Conference Center (JNICC) - Posta

Invited guests

The five political parties fielding the largest number of candidates in the elections (at constituency or ward level) have been invited to send their experts to outline their visions and plans for these critical areas. These representatives will be interrogated by a panel composed of sector experts drawn from civil society.

These debates will be broadcast live by Star TV and Radio RFA.

Registration for this event is essential. Please send your name and media outlet to [email protected] or call +255 768 129974.

Mgombea Ubunge Bariadi kupitia ACT-Wazalendo atekwa


Mgombea ubunge wa Chama cha ACT-Wazalendo katika Jimbo la Bariadi Magharibi, Masunga Nghezo ametoweka kusikojulikana na hajapatikana hadi sasa akiwa katika harakati za kufanya mikutano ya hadhara katika jimbo hilo. 

Mbali na kutoonekana kwa Nghezo, simu yake aliyokuwa akiitumia, ndiyo inatumika kutuma ujumbe wa vitisho kwenda kwa mzazi wa mgombea huyo ikimtaka amkanye mwanae kuachana na siasa vinginevyo familia nzima itadhurika.

Taarifa ya chama hicho iliyotolewa jana kwa vyombo vya habari na Afisa Habari wake, Abdallah Khamis, imesema kuwa Nghezo alitoweka siku ya Jumatatu ya wiki hii akijiandaa kwenda katika mkutano wa hadhara katika kijiji cha Baneni.

Taarifa hiyo inaeleza kuwa kabla ya kutoweka kwake, Nghezo, alienda kumtafuta dereva mwingine wa kumuendesha baada ya yule wa siku zote kwenda msibani na kwamba aliporudi na dereva mwingine aliliacha gari likiwa katika maandalizi ya kufungwa vipaza sauti.

Taarifa imeongeza kuwa baada ya dereva na viongozi wengine wa chama kumaliza kazi ya kufunga vipaza sauti walianza kumtafuta mgombea wao bila mafanikio huku simu yake ikiwa haipatikani hadi jana mzee wake alipopokea ujumbe mfupi wa simu kupitia simu ya mwanae ikimtaka kumkanya mwanae aachane na siasa za Bariadi.

Pia taarifa ya Khamis inaeleza kuwa mzazi wa mgombea, Mzee Nghezo, anazidi kutumiwa ujumbe wenye masharti wakimpa muda wa saa sita kutekeleza masharti yao vinginevyo watamdhuru kijana wake na kisha kuitafuta familia nzima,

Hata hivyo Mwananchi Digital imezungumza na mzazi wa mgombea huyo, Joseph Nghezo ambaye amethibitisha kupotea kwa mtoto wake tangu siku ya Jumatatu.

Mzee Nghezo amesema kuwa siku ya Jumatatu viongozi wa chama cha ACT-Wazalendo walimpigia simu wakitaka kujua kama mtoto wake yupo nyumbani, ndipo alishtuka kwakuwa alijua mwanawe yuko kwenye kampeni.

Ameongeza kuwa baada ya kuulizwa sana juu ya mtoto wake, majirani walimshauri aende akatoe taarifa katika kituo cha polisi.

‘Tumeenda kutoa taarifa katika kituo cha polisi hapa mjini Bariadi na polisi wamechukua maelezo hivyo wanafanya kazi,’ aliongeza Nghezo.

Mwananchi Digital imemtafuta Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Simiyu, Gemini Mushi ili kuthibtisha tukio hilo lakini hakuweza kuzungumza lolote kwakuwa alipopokea simu alisema yuko kwenye kikao.
  • via Mwananchi