Zahanati ya Wakorea na Wachina nchini Tanzania yafungiwa kutoa huduma


Tathmini ya REDET na TEMCO kuhusu Uchaguzi Mkuu Tanzania 2015TB Joshua akutana na Lowassa
Rehearsal: Kuapishwa kwa Dk John Magufuli na kuagwa Rais KikweteKibanda cha kitakachotumika wakati wa kuapishwa kwa Rais Mteule, Dk John Magufuli kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kesho kutwa kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.


Askari wa Jeshi la Wananchi akiigiza kama Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi nchini, Jenerali Davis Mwamunyange na mwingine akiigiza kama Rais anayemaliza muda wake, Jakaya Kikwete wakati wa mazoezi ya sherehe za kuapishwa Rais wa Awamu ya Tano, Dk John Magufuli kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.

Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Jenerali Davis Mwamunyange (wa pili kulia), Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, Ernest Maangu (wa tatu kulia) na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Sadick wakipiga saluti ulipokuwa unaimbwa wimbo wa Taifa wakati wa mazoezi ya sherehe za kuapishwa Rais wa Awamu ya Tano, Dk John Magufuli kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.

Maofisa mbalimbali wakiwa katika kibanda cha kiapo wakipanga jinsi viongozi watakavyokaa wakati wa sherehe za kuapishwa Rais wa Awamu ya Tano, Dk John Magufuli kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.


Kikundi cha sarakasi kikitumbuiza wakati wa maandalizi hayo

Wasanii kutoka Zanzibar wakicheza ngoma ya kibati wakati wa mazoezi hayo

Mtu aliyeigiza kama Rais Jakaya Kikwete, akiwa amesimama alipokuwa akipigiwa mizinga ikiwa ni ishara ya kuagwa kwa rais huyo kabla ya kuapishwa Rais mpya wa Awamu ya Tano, Dk John Magufuli wakati wa mazoezi hayo.

Viongozi mbalimbali wakiwemo wa vyombo vya ulinzi na usalama wakiwa Jukwaa Kuu wakati wa maandalizi hayo.

Baadhi ya wananchi wakiwa wamesimama wakati wimbo wa Taifa ukipigwa na Bendi ya Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) wakati wa maandalizi hayo.

Mtu aliyeigiza kama Rais Jakaya Kikwete, akielekea kukagua gwaride la heshima la kumuaga wakati wa mazoezi hayo.
  • Tumeshiriksihwa taarifa hii na Richard Mwaikenda/Kamanda wa Matukio blog

Kauli zilizompandisha Yericko Nyerere kizimbani kwa makosa ya mtandaoniMfanyabiashara, Yeriko Yohanesy Nyerere amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, akikabiliwa na mashtaka matano ya kutoa taarifa za upotoshaji kupitia mtandao wa Facebook.

Wakisoma hati ya mashtaka kwa kubadilishana mawakili wa Serikali, Simon Wankyo na Paul Kadushi jana mbele ya Hakimu Mfawidhi, Cyprian Mkeha walidai kuwa mshtakiwa huyo alifanya makosa hayo kinyume na kifungu cha 16 cha Sheria ya Mtandao namba 14 ya 2015.

Wankyo alidai kuwa Oktoba 25, 2015 katika eneo lisilojulikana Nyerere alichapisha taarifa za upotoshaji kupitia mtandao wa Facebook kuwa ‘piga kura leo huku ukikumbuka kifo cha Mwangosi, Mateso ya Ulimboka na Kibanda, mateso ya kijana wetu wa JKT. Ukikumbuka hayo fanya uamuzi sahihi bila ushabiki.’

Wakili huyo wa Serikali alidai kuwa Oktoba 24, 2015 katika eneo lisilojulikana jijini Dar es Salaam mshtakiwa huyo alichapisha taarifa za upotoshaji kupitia mtandao wa Facebook, kuwa Taifa la Tanzania kuanzia leo (yaani Oktoba 24) halihitaji amani, linahitaji haki tu.

Alidai kuwa Oktoba 24, 2015 mshtakiwa huyo alichapisha taarifa za uongo kupitia Facebook kuwa siku ya leo (Oktoba 24) mpaka siku ya kuapishwa Lowassa, taifa hili halihitaji amani bali taifa hili linahitaji haki tu, amani ilishatoweka siku nyingi, kilichosalia ni uvumilivu tu.

Mbali na hayo pia alichapisha taarifa za uongo kuwa, njia sahihi ya kulitibu taifa hili ni kwa dola dhalimu kutenda haki hata kama itawauma.

“Uchaguzi huu ni vita, anayedhani ni demokrasia apimwe akili. Hii ni vita kati ya umma na dola, ni vita kati ya wema na ubaya, ni vita kati ya shibe na njaa , ni vita kati ya masikini na matajiri, CCM siyo chama cha siasa kwa sasa, ni muungano wa kihalifu unaolindwa na baadhi ya watumishi wa vyombo vya dola .

“Umma umekosa amani na furaha , fursa pekee waliyoipata Watanzania wanamjua rais wao wanayekwenda kumchagua kesho (Oktoba 25), jaribio lolote litakalofanywa na CCM na vibaraka wao la kukwamisha matakwa ya umma litaondoa hata ule uvumilivu kidogo walionao Watanzania na kisha vitazaliwa vichaa chongo ambavyo hata risasi na mabomu hayatakizima.

“Kwa siku ya leo (Oktoba 24) mpaka siku ya kuapishwa Lowassa, taifa hili halihitaji amani, bali taifa hili linahitaji haki tu,” yalinukuliwa mahakamani maneno yanayodaiwa ya Yeriko.

Mshtakiwa huyo anadaiwa kuwa Agosti 24, 2015 alichapisha taarifa nyingine ya upotoshaji kupitia mtandao huo wa Facebook akidai, “mipango ya hujuma ya JK toka Ngurdoto Arusha muda huu.

Kikwete yupo Ngurdoto Arusha na wakuu wote wa mikoa na wilaya Tanzania nzima pia wakuu wa vyombo vya dola na wanadhimu mbalimbali,” yalinukuliwa maneno yanayodaiwa ya Yeriko.

“Wakuu wa mkoa wanaelezwa kwanza kuwa NEC kwa kushirikiana na CCM tayari wameshatengeneza kura bandia kwa kutumia mfumo wa kalamu za kichina.

“Pia wanaamuliwa kuhakikisha wanahujumu kampeni za Ukawa kwa kutumia vyombo vya dola, wanaagizwa kuhakikisha kamatakamata ya vijana wa bodaboda wiki moja kabla ya uchaguzi na zaidi ni wakuu hao wa mikoa wanaagizwa wakawaagize ma-DC kote nchini kuhakikisha wanalinda masilahi ya CCM walipo siku ya uchaguzi,” yalinukuliwa maneno yanayodaiwa ya Yeriko.

Yeriko anadaiwa kuwa Septemba 3, 2015 katika eneo lisilojulikana alichapisha taarifa za upotoshaji kupitia mtandao wa Facebook kuhusu uwepo wa akaunti ya benki ya kughushi inayomilikiwa na Mtanzania katika benki ya HSBC tawi la North London ikionesha CCM imemuwekea Dk Slaa E 1.5 milioni kupitia kwa mchumba wake Josephine Mshumbusi ikiwa ni rushwa ili kushinda uchaguzi 2015.

Mawakili hao wa Serikali walidai kuwa mshtakiwa huyo alichapisha taarifa hizo za upotoshaji akiwa na lengo la kupotosha umma katika Uchaguzi Mkuu wa 2015.

Baada ya kusomewa mashtaka hayo, mshtakiwa alikana na Hakimu Mkeha alimtaka mshtakiwa huyo kuwa na mdhamini mmoja ambaye atasaini bondi ya Sh5 milioni.

Upande wa mashtaka ulidai upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika na mshtakiwa alikamilisha masharti hayo ya dhamana na kesi imeahirishwa hadi Desemba Mosi, 2015.

  • [Imenukuliwa kutoka kwenye gazeti la MWANANCHI]

NYONGEZA

Inadaiwa, alichapisha taarifa za uongo kupitia mtandao huo kuwa, 
“siku ya leo mpaka siku ya kuapishwa Lowassa, taifa halihitaji amani, bali taifa hili linahitaji haki tu, amani ilishatoweka siku nyingi, kilichobaki ni uvumilivu tu… njia sahihi ya kulitibu taifa hili ni kwa dola dhalimu kutenda haki hata kama itawauma.”

Inadaiwa Nyerere aliendelea kudai kuwa,
“Uchaguzi huu ni vita, anayedhani ni demokrasia apimwe akili…hii ni vita kati ya umma na dola, ni vita kati ya wema na ubaya, kati ya shibe na njaa, kati ya masikini na matajiri… umma umekosa amani na furaha, fursa pekee waliyoipata watanzania wanamjua rais wao wanayekwenda kumchagua kesho, jaribio lolote litakalofanywa na CCM na vibaraka wao la kukwamisha matakwa ya umma, litaondoa hata ule uvumilivu kidogo walionao watanzania na kisha vitazaliwa vichaa chongo ambavyo hata risasi na mabomu hayatakizima”.

Aidha, anadaiwa siku hiyo hiyo alichapisha taarifa nyingine ya upotoshaji kupitia mtandao ikisema, 
“mipango ya hujuma ya JK toka Ngurdoto Arusha muda huu…Kikwete yupo Ngurdoto Arusha na wakuu wote wa mikoa na wilaya Tanzania nzima pia wakuu wa vyombo vya dola na wanadhimu mbalimbali… wakuu wa mkoa wanaelezwa kuwa NEC kwa kushirikiana na CCM tayari wameshatengeneza kura bandia kwa kutumia mfumo wa kalamu za kichina… pia wanaamuliwa kuhakikisha wanahujumu kampeni za Ukawa kwa kutumia vyombo vya dola, wanaagizwa kuhakikisha kamatakamata ya vijana bodaboda wiki moja kabla ya uchaguzi na zaidi wanaagizwa wakawaagize maDC kote nchini kuhakikisha wanalinda maslahi ya CCM siku yaUchaguzi."

Taarifa ya NHIF ya kuanguka kwa jukwaa lake lililotua kwenye paa la TANESCO

Mkurugenzi wa Masoko na Utafiti wa NHIF,Bw Rehani Athuman akionyesha mchoro wa jengo hilo kwa waandishi wa habari, kushoto ni Mkurugenzi wa Uendeshaji (NHIF), Eugen Mikongoti

Utangulizi:

Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) hivi sasa unaendelea na ujenzi wa majengo katika mikoa mbalimbali nchini, kwa lengo la kujitosheleza kwa majengo ya ofisi na kukidhi mahitaji ya wanachama wake na wadau wengine.Moja ya mikoa ambayo inaendelea na ujenzi huo ni Mbeya, ambako Mfuko unajenga jengo la ghorofa kumi na mbili litakalokuwa na nafasi za ofisi na huduma nyingine ndani yake.

Tukio la Kuanguka kwa jukwaa:


Wakati shughuli hizo za ujenzi zinaendelea, jana mchana katika hali isiyotarajiwa mvua iliyoambatana na upepo mkali ilinyesha mjini Mbeya. Upepo na mvua hizo vilisababisha kuanguka kwa jukwaa la jengo hilo na kutua juu la paa la jengo la ofisi ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) mkoani Mbeya.

Kuanguka kwa jukwaa hilo hakukuwa na madhara yoyote kwa maisha ya binadamu, kwa maana kuwa hakuna mtu aliyepoteza maisha au kupata majeraha. Hata hivyo tukio hilo lilisababisha taharuki kwa wafanyakazi wapatao hamsini waliokuwemo ndani ya jengo hilo na hivyo kusababisha kazi kusimama kwa muda. Aidha tathmini ya awali iliyofanyika katika paa la jengo la TANESCO lililoangukiwa na jukwaa hilo inaonyesha kuwa paa hilo ilipata hitilafu ndogo ambayo itafanyiwa marekebisho kwa gharama za Mkandarasi anayejenga jengo la NHIF.

Hatua za kisualama zilizochukuliwa:


Kama sheria za ujenzi zinavyoagiza, kabla ya kuanza kwa ujenzi wa jengo hilo Mkandarasi alishajenga uzio kuzunguka jengo zima ili kuhakikisha kuwa shughuli za ujenzi hazileti madhara kwa wapita njia au ofisi zilizo jirani. Umakini wa Mkandarasi huyo katika kuzingatia taratibu za tahadhari katika shughuli za ujenzi, umewezesha jengo hilo la ghorofa kumi na mbili kufikia hatua nzuri ya ujenzi bila madhara yoyote kwa wajenzi wenyewe, wapita njia au ofisi za jirani.

Aidha kufuatia tukio la Jumatatu 02/11/2015, Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya umeshamwandikia Mkandarasi anayeendelea na ujenzi katika jengo hilo kuhakikisha kuwa uzio unaozunguka jengo zima unaimarishwa zaidi hususani wakati huu tunapokaribia kipindi cha mvua za masika ili kuepuka uwezekano wa madhara yoyote kwa binadamu wakati shughuli za ujenzi zinaendelea.

Namna Habari ilivyoripotiwa:


Tunapenda kuufahamisha umma kwamba habari zilizoripotiwa jana na baadhi ya vyombo vya habari kwamba jengo la NHIF mkoani Mbeya limeporomoka, zilipotosha ukweli wa tukio hilo, kwani kilichoporomoka siyo jengo, bali ni jukwaa.Tunapenda kusisitiza kuwa tukio hilo limesabishwa na mvua kubwa na upepo uliovuma katika mji wa Mbeya, wala siyo uzembe wa Mkandarasi anayejenga jengo hilo.

Wito kwa Wanachama wa NHIF:


Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya unawaomba wanachama na wadau wake nchini kote waendelee kuwa watulivu na kuvuta subira kwani changamoto ya ufinyu wa ofisi katika mikoa itakuwa imepatwa ufumbuzi baada ya kukamilika kwa ujenzi wa majengo ya unaoendelea hivi sasa katika mikoa mbali mbali nchini.

Imetolewa na:
Mkurugenzi Mkuu,
Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya.


Mkurugenzi wa Uendeshaji (NHIF),Eugen Mikongoti akifafanua jambo wakati akizungumza waandishi wa habari kuhusu kuvunjika kwa uzio wa jengo la mfuko huo linalojengwa mkoani Mbeya kutokana na kukumbwa na mvua na upepo mkali, amesema jengo hilo liko salama kabisa ila uzio unaosaidia kuwakinga wajenzi ndiyo ulioanguka kutokana na upepo huokulia ni Mkurugenzi wa Masoko na Utafiti wa NHIF,Bw Rehani Athuman.


Mkurugenzi wa Uendeshaji (NHIF),Eugen Mikongoti akifafanua jambo wakati akizungumza waandishi wa habari kuhusu kuvunjika kwa uzio wa jengo la mfuko huo linalojengwa mkoani Mbeya.

Rais Kikwete ateua Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi TTCL

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

WIZARA YA MAWASILIANO SAYANSI NA TEKNOLOJIA 

TAARIFA KWA UMMA 

UTEUZI WA MWENYEKITI WA BODI YA WAKURUGENZI WA KAMPUNI YA SIMU TANZANIA 


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, amemteua Prof. Tolly Salvatory Augustin Mbwette kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL) kwa kipindi cha miaka miaka mitatu kuanzia tarehe 12 Oktoba 2015.

Uteuzi huo ni kwa mujibu wa kifungu Na. 9 (4) (a) cha Sheria Na. 20 ya Mwaka 1993 iliyoanzisha Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL). Prof. Tolly Salvatory Augustin Mbwette amekuwa Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Huria Tanzania kwa kipindi cha miaka kumi kuanzia tarehe 13 Aprili 2005 hadi tarehe 13 Aprili 2015. Pia amekuwa Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, kwa taaluma ni Mhandisi ujenzi aliyobobea kwenye maeneo ya Mazingiria, TEHAMA, Utawala na Menejimenti kwa zaidi ya miaka 25 na amesoma Vyuo Vikuu vya Dar es Salaam, Tanzania; IHE Delft, Netherland; na Chuo Kikuu cha London, Uingereza kwa ngazi ya Shahada ya Kwanza, Uzamili na Uzamivu. Pia ameshirikiana na Vyuo Vikuu mbali mbali duniani kutoka Bara la Ulaya, Amerika, Asia na Afrika katika maeneo ya uhandisi, utafiti, TEHAMA, uandishi wa vitabu na majarida mbali mbali.

Imetolewa na:

KATIBU MKUU

Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia

TB Joshua awasili Tanzania kwa uapisho wa Dk Magufuli
Mtume TB Joshua wa Kanisa la Church of All Nations nchini Nigeria ametua jijini Dar es salaam leo  tayari kwa kushuhudia kuapishwa kwa Rais wa Awamu ya Tano Dkt. John Pombe Magufuli siku ya Alhamisi.

Mara tu baada ya kutua uwanja wa Ndeghe wa Kimataifa wa Julius Nyerere, TB Joshua alikwenda Ikulu moja kwa moja kumsalimia Rais Jakaya Mrisho Kikwete kumsabahi na kumpongeza kwa kufanikisha uchaguzi mkuu kwa uhuru na amani, huku akiondoka madarakani akiwa mtu mwenye furaha. TB Joshua amepongeza Rais Kikwete pia kwa kupata Dkt Magufuli kama mrithi wake, akimtaja Rais huyo mpya mteule kama Rais wa Tanzania wa baraka na fanaka tele katika awamu hii mpya.
Rais Jakaya Mrisho Kikwete akimlaki Mtume TB Joshua wa kanisa la Church of All Nations la nchini Nigeria Ikulu jijini Dar es salaam jioni hii. TB Joshua ametua jijini Dar es salaam tayari kwa kushuhudia kuapishwa kwa Rais wa Awamu ya Tano Dkt. John Pombe Magufuli siku ya Alhamisi.


Rais Jakaya Mrisho Kikwete akiongea na Mtume TB Joshua wa kanisa la Church of All Nations la nchini Nigeria Ikulu jijini Dar es salaam jioni hii.
  • Picha na Freddy Maro/Ikulu