Ushauri wa Josias kwa serikali ya Magufuli jinsi VETA itakavyowapa vijana ajira

Baada ya mchakato mzima wa Kampeni kukamilisha na hatimaye Serikali kuundwa na Chama cha Mapinduzi kupitia kwa aliyekua mgombea wake wa Urais Mh. Dkt. John Pombe Magufuli tunapaswa kuungana wote na kutoa mawazo yenye lengo la kujenga uchumi wa Nchi Yetu.

Kumekuwepo na tatizo sugu la ukosefu ama kuwa na miundombinu mibovu mbalimbali ya Elimu Kama Madarasa, Maktaba, Mabweni, Maabara, Madawati nk. Ukosefu wa miundombinu hii umekwamisha ama kudumaza utoaji wa Elimu nchini.

Binafsi napenda kuishauri Serikali ya awamu ya Tano kuwekeza katika kuimarisha Elimu ya ufundi (VETA) na kuweka sera madhubuti itakayowabana wahitimu wa vyuo vya ufundi kujitolea kama sehemu yao ya mafunzo lakini pia ikiwa kama sehemu ya Kujitolea kujenga Taifa.

Mitaala ya Elimu ya ufundi Kama itatolewa kwa kipindi cha miaka miwili basi mwaka mmoja utumike kwa mafunzo darasani na mwaka mmoja kwa mafunzo kwa vitendo yaani( FIELD). Wanachuo wote wa VETA hata kama watasoma bure lakini wakatakiwa kufanya field kwa mwaka mzima watakua wameshiriki kwa kiwango kikubwa katika Ujenzi wa Taifa letu.

Mfano wanafunzi 10,000 wakichukua mafunzo ya ufundi kwa mwaka kwa uwiano tuu wa mafundi uashi 5000 na mafundi seremala 5000 kisha baada ya masomo ya mwaka mmoja wakaenda field kwa Mwaka mmoja kujenga Shule, hospitali, vituo vya afya, kutengeneza samani za ofisi tutapunguza gharama kiasi gani?

Nchi Yetu tuna raslimali nyingi ikiwemo raslimali watu lakini hatujaweza kuiendeleza. Naomba tuwekeze katika kuendeleza raslimali tulizo nazo kwa manufaa ya Taifa letu.

Baada ya kuhitimu mafunzo ya miaka miwili tunao uwezo wa kuwatengenezea ajira vijana hawa na kuwawezesha mitaji inayotokana na shughuri zao katika jamii kwa kujitolea kwa mwaka mzima.

Hebu fikiria Serikali inaagiza samani za ofisi kiasi gani kwa mwaka? Pesa kiasi gani inatumika? Vipi kama vijana waliohitimu VETA mafunzo ya miaka miwili tena kwa kujitolea kujenga Taifa kwa mwaka mzima wakisajiriwa na kampuni na kupata soko la uhakika toka Serikali na kuachana na uagizwaji wa samani za kichina tutapunguza tatizo la ajira kwa kiwango gani?

Vipi kama vijana walio soma ufundi uashi na kujitolea kujenga Taifa kwa mwaka mzima wakapewa mikataba ya kujenga nyumba kama za NHC na Majengo mengine mengi tutapunguza tatizo la ajira kwa kiwango gani?

Tuna amini Serikali ya awamu ya Tano ipo makini na inalenga kila MTU afanye kazi kutimiza kauli mbiu ya "HAPA KAZI TU"

Mawaziri, Wabunge, na viongozi wote wa Serikali onyesheni ubunifu kulifanya Taifa letu lisonge mbele.

Kwa Leo inatosha.

HapaKaziTu

Josias Charles

Ratiba ya shughuli za Mkutano wa Kwanza wa Bunge 2015


Mbunge asitisha msaada wa "mabasi ya wanafunzi" kwa kushindwa uchaguzi

Aliyekuwa mbunge wa Jimbo la Mikindani, mkoani hapa, Hasnein Murji, amesitisha huduma ya usafiri kwa wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Naliendele kufuatia kushindwa ubunge katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 25.

Murji aligombea jimbo hilo kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM).

Alikuwa akitoa usafiri kwa wanafunzi wa shule hiyo tangu mwaka 2011 alipochaguliwa kuwa mbunge wa jimbo hilo.

Wakizungumza na Nipashe kwa nyakati tofauti shuleni hapo, wanafunzi hao walisema kuwa kitendo cha kutochaguliwa mbunge huyo kimewaathiri kiusafiri.

‘Tangu alipochaguliwa kuwa mbunge wa jimbo hili, alitoa magari mawili ambayo yalikuwa yanapokezana, tulikuwa hatulipi nauli, tulikuwa tunawahi vipindi kwa sababu tulikuwa na uhakika wa usafiri,’ alisema mmoja wa wanafunzi hao.

Walisema usafiri wa daladala ni mchache, lakini pia wanatozwa nauli ya Sh. 500 badala ya Sh. 200.
Walidai kuwa wakati mwingine wazazi wanashindwa kumudu gharama na kushindwa kufika shuleni kwa sababu ya kukosa nauli.

Walisema hivi sasa wanafunzi wanaofanya mitihani ya kumaliza kidato cha nne wanalazimika kupanda mabasi ya Tandahimba na Newala ili kuwahi kufanya mitihani.

Kharim Mohamed, ni mwanafunzi wa kidato cha tatu, alisema kuwa ukosefu wa usafiri wa uhakika unawafanya wachelewe vipindi na hukaa kituoni kwa saa tatu wakingoja usafiri.

Awali Mwalimu mkuu wa shule hiyo, Hittu Rashid, alisema shule hiyo ilianza mwaka 1997, na tatizo la usafiri kwa shule hiyo limekuwa la muda mrefu. ‘Miaka ya nyuma kabla sijahamia hapa, niliambiwa kwamba wanafunzi walikuwa wakitumia malori ya mchanga kama usafiri wa kuja shuleni, na mwanafunzi mmoja alipata ulemavu baada ya kuvunjika mguu wakati akipanda gari,’ alisema.

Alisema, tangu kuwepo kwa usafiri wa uhakika wanafunzi wake wamekuwa na mahudhurio mazuri darasani na utoro ukipungua.

‘Kutoka mjini kuja hapa shuleni ni kilomita 12, na kutokana na tatizo la usafiri kwa wanafunzi wangu aliyekuwa mbunge aliona tatizo hili akaamua kuwasaidia, zaidi ya wanafunzi 50 walikuwa wakipanda magari yake bure,’ alisema.

Alipoulizwa na Nipashe kuhusu kusitisha usafiri huo, Murji, alikiri kuchukua hatua hiyo tangu Jumatatu iliyopita kwa madai kuwa alikuwa akitoa huduma hiyo kama mbunge wao, lakini sasa sio mbunge tena ni mfanyabishara kama walivyo wengine.

Aliwataka wamuombe mbunge wao wa sasa awasaidie.

Hata hivyo, alisema atatoa magari kwa ajili ya kwenda Mikindani kwa wananchi wote na nauli yake itakuwa Sh. 200 bila kujali umri wa mtu.

Akizungumzia mpango wa kuwasaidia wanafunzi hao hata kwa kuwatoza nauli ili kupunguza makali ya usafiri, Murji alisema: ‘Kwa kuwa mimi sio mbunge wao tena nafikiria kama nitaweza huenda nitawapelekea, lakini sijajua itachukua muda gani kurejesha usafiri shuleni hapo,’ alisema.

Babu Seya na Papii Kocha wakata rufaa katika Mahakama ya Afrika


Mwanamuziki, Nguza Viking maarufu kama Babu Seya na mwanaye, Johnson Nguza ‘Papii Kocha’, wametua katika Mahakama ya Haki za Binadamu Afrika (AFCPHR) Arusha.

Wanamuziki hao wamekata rufaa dhidi ya adhabu waliyohukumiwa mwaka 2004 ya kutumikia kifungo cha maisha gerezani.

Kupitia shauri lao lililowasilishwa mahakamani na kupewa namba 006/ 2015, wanaiomba Mahakama ya Afrika kutoa uamuzi kuwa haki zao zilivunjwa.

Kwa sababu hiyo wanaomba waachiwe huru na kulipwa fidia.

Katika shauri hilo pia wameomba wawezeshwe kupata msaada wa sheria na.

Pia wanataka Mahakama hiyo iteue wataalamu watakaotoa ufafanuzi wa hoja za kesi yao na kuisaidia kufikia wajibu wake.

Miongoni mwa hoja za walalamikaji hao zilizowasilishwa mahakamani hapo ni pamoja na kwamba mwenendo wa shauri lao haukufanyika kwa kuzingatia haki,.

Vilevile wanadai hati ya mashtaka dhidi yao ilikosewa kuandikwa tarehe ambayo tuhuma za makosa yao zilidaiwa kufanywa hivyo wakashindwa kutayarisha utetezi wao.

Pia wanadai mahakama iliyowatia hatiani ilijielekeza katika ushahidi wa upande wa mashtaka pekee usioshirikisha ushahidi mwingine.

Wanadai kwamba Serikali ya Tanzania kupitia maofisa wake, ilivunja misingi ya haki za binadamu na sheria za kimataifa.

Wanadai pia kwamba mlalamikiwa alivunja Ibara 1,2, 3, 5, 7(1)b), 13 na 18(1) ya Mkataba wa Afrika kuhusu Ubindamu na Haki za Binadamu.

Malalamiko mingine ni kuwa baada ya kukamatwa hawakuelezwa mapema kuhusu mashtaka waliyokuwa wakituhumiwa nayo.

Wanadai kwa sababu hiyo waliwekwa chini ya ulinzi kwa siku nne bila kuwa na mawasiliano na kupata fursa ya kuonana na mwanasheria au mtu mwingine ye yote.

Wanadai wakiwa chini ya ulinzi polisi waliwatesa na kuwatukana na baadaye ofisa mmoja wa polisi aliwaeleza kuwa wanatuhumiwa kwa ubakaji.

Walalamikaji hao raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), walikuwa wakiishi na kufanya kazi ya muziki Dar es Salaam.

Wanadai kwamba mashtaka dhidi yao yalitungwa na hivyo hukumu iliyotolewa haikujikita katika ushahidi wenye nguvu katika sheria.

Nguza na wanawae watatu walikamatwa Oktoba 12, mwaka 2003 na kufikishwa kituo cha Polisi cha Magomeni Dar es Salaam.

Baadaye walipandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Oktoba 16 mwaka 2003.

Watuhumiwa hao pamoja na mwingine aliyejulikana kwa jina la Mwalimu walishtakiwa kwa tuhuma 10 za ubakaji.

Pia walikabiliwa na mashtaka 11 ya kunajisi watoto 10 wenye umri wa miaka sita na nane. Watuhumiwa wote walikana mashitaka yao.

Baada ya kusikilizwa kesi hiyo, Mahakama ya Kisutu Dar es Salaam ilitoa hukumu Juni 25, mwaka 2004.

Iliwatia hatiani kwa kifungo cha maisha jela huku mtuhumiwa wa tano, Mwalimu akiachiwa huru.

Walikata rufaa Mahakama ya Rufaa Tanzania Oktoba 30 mwaka juzi ambako wafungwa wawili Francis Nguza na Nguza Mbango walishinda rufaa yao.

Hata hivyo, Babu Seya na Papii Kocha walijigonga mwamba na kurudishwa jela kwa kuhukumiwa kifungo cha maisha.

JINSI WALIVYOTIWA HATIANI

‘Babu Seya’ na ‘Papii Kocha’ walihukumiwa kifungo cha maisha jela mwaka 2004 baada ya kupatikana na hatia ya ubakaji na kuwanajisi watoto wa Shule ya Msingi Mashujaa, Sinza Dar es Salaam.

Babu Seya na wanawe walidaiwa kutenda makosa 10 ya kubaka watoto hao wa shule ya msingi waliokuwa na umri kati ya miaka sita na minane.

Mahakama iliwatia hatiani kwa makosa mengine 11 ya kulawiti watoto wa kike wenye umri huohuo kati ya Aprili na Oktoba 2003.

Juni 25, 2004, Hakimu Mkuu Mkazi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam aliwatia hatiani Babu Seya na wanae kwa hatia ya kubaka na kulawiti.

Januari 27 mwaka 2005, Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Thomas Mihayo alitupilia mbali rufaa yao iliyokuwa ikipinga hukumu dhidi yao.

Hukumu hiyo ilitolewa na aliyekuwa Hakimu Mkuu Mkazi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Addy Lyamuya aliyewatia hatiani kwa makosa yote waliyokuwa wameshitakiwa nayo Juni 25, mwaka 2004.

Awali mwaka 2004, baada ya kukutwa na hatia katika kesi hiyo, Babu Seya, Papii Kocha na wakili wao, Mabere Marando walikata rufaa ya pili ambayo ilitupiliwa mbali.

Mwaka 2010 waliomba tena rufaa ambayo marejeo yake yalisikilizwa na kutolewa hukumu Februari 2010.

Mahakama iliridhia hukumu ya kifungo cha maisha kwa Babu Seya na Papii Kocha huku ikiwaachia huru watoto wake wawili, Nguza Mbangu na Francis Nguza.

Rais Dk Shein na Makamu wa Kwanza wa Rais, Maalim Seif wateta


Ripoti ifuatayo ni ya Salma Said, mwandishi wa habari akizungumza na DW Kiswahili

Katuni kuhusu Rais Magufuli 'anavyowakimbiza' watu kwa staili yake


Chama kipya cha siasa Tanzania chapata usajili wa muda


Chama kipya cha siasa kijulikanacho Tanzanian Patriotic Front (TPF MASHUJAA), leo kimepata usajili wa muda nchini.

Akizungumza jijini Dar es Salaam, Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji Francis Mutungi amekitaka chama hicho kuzingatia katiba ya chama, sheria ya vyama vya siasa pamoja na kujali mawazo ya wanachama wake.

Julius K. Nyerere - Umuhimu wa kufuata misingi ya sheria katika uongozi


Taarifa ya Meru Logistics: Tunasafirisha mizigo kutoka Uingereza hadi TanzaniaKaribu Meru Logistics kwa huduma nzuri, safi, zenye uhakika na haraka kutuma mizigo kutoka UK kwenda Tanzania.

Wasiliana nasi pia kama unahitaji chochote kutoka UK kama vile magari, matractor, fridge, TV, Vyombo nk. tuta kusaidia kununua na kukutumia mpaka Tanzania bila tatizo lolote na vitafika salama kabisa.

Bei za kutuma mizigo ni kama ifuatavyo:

20' CONTAINER TO DAR /MOMBASA FROM £1,300

40' CONTAINER TO DAR /MOMBASA FROM £1,800

4X4 TO DAR/MOMBASA FROM £850

SALOON CARS TO DAR/ MOMBASA FROM £750

AIR CARGO TO DAR £5 A KILO

AIR CARGO TO ZNZ £4 A KILO

INCLUSIVE CLEARANCE

TO COLLECT CARGO LONDON FROM £25

TO COLLECT CARGO OUTSIDE LONDON FROM £50

ONCE YOU PAY HERE IN UK YOU DONT PAY ANYTHING IN TANZANIA

(UKIISHA LIPA UK UNAKWENDA TU KUCHUKUA MZIGO WAKO)

Address in UK: 
Unit 12 Manor Way Business Centre
Marsh Way, Rainham, Essex
RM13 8UG

COLLECTION POINT IN DAR IS:

DAR FREE MARKET, ALI HASSAN MWINYI ROAD

OYSTER BAY NEAR KENYAN EMBASSY & DSTV

Telephone: +44 (0) 1708554632
Email: [email protected]
Website: www.merulogistics.com
Instagram: @merulogistics
Facebook: Meru Logistics

CUSTOMER SATISFACTION GUARANTEED!

Taarifa ya DAWASCO kuhusu kutuhumiwa kusambaza maji yenye kinyesi

Mnamo tarehe 08/11/2015 Magazeti ya Mzalendo na Majira yaliandika habari zilizolenga upotoshaji na taharuki kwa wananchi na hususani watumiaji wa Maji kwa mkoa wa Dar es salaam wanaohudumiwa na DAWASCO.

Katika gazeti la Mzalendo lilikuwa na kichwa cha habari “Wengi Dar watumia maji yenye kinyesi” na upande wa gazeti la Majira lilibeba kichwa cha habari “Maji machafu yaathiri Dar”. Ndani ya habari hizo waandishi wameelezea shirika la Majisafi na Majitaka Dar es salaam (DAWASCO) kama moja ya chanzo cha ugonjwa wa kipindupindu kwa kuwa maji hayo yameathirika na kinyesi.

Gazeti la Majira 08/11/2015 ukurasa wa 3 inanukuliwa “Kwa kiasi kikubwa Maji ya jiji yamekuwa yameathirika na kinyesi cha binadamu”. mwisho wa kunukuu. Aidha nukuu nyingine kwenye gazeti la Majira inasomeka “Wananchi wa jiji la Dar es salaam wamekuwa wakipata Majisafi na salama kutoka mamlaka ya Majisafi na salama (DAWASCO) kwa aslimia 30 tu”.

Ikumbukwe pia maeneo makubwa ambayo wagonjwa wa kipindupindu wanatoka ni maeneo ambayo yameathirika na wizi wa maji kwa kiasi kikubwa na mapambano hayo bado yanaendelea kuhakikisha wizi wa maji unakwisha maeneo hayo ni pamoja na Manzese, Buguruni ,Kigogo , Mburahati , Kinondoni mkwajuni pamoja na Tandale.Jitihada zilizofanywa na Dawasco katika kudhibiti ugonjwa huu hususa ni watumiaji Maji ni pamoja na Kupeleka huduma ya maji BURE kwa maeneo yaliyoathirika zaidi na mlipuko huo kupitia utarartibu wa Manispaa uliowekwa.
  • Kutoa Elimu kwa wananchi kupitia vyombo vya habari , machapisho, pamoja na vikao vya pamoja na watendaji wa Mitaa, Bwana Afya kwa maeneo yaliyoadhirika.
  • Kuanza kwa usajili rasmi wa magari yanayofanya biashara ya maji (water bowsers) ili kulinda afya ya mtumiaji. Zoezi lilianza tarehe 01 October 2015 na idadi ya Magari 120 yameshasajiliwa hadi sasa.Kuondoa maunganisho yasiyo halali ambayo yanafanywa na baadhi ya wananchi “vishoka” , ambayo yanapeleka huduma ya Maji kwa baadhi ya maeneo yanayoadhirika zaidi.
Dawasco inasikitika kwa taarifa hizo za upotoshaji kwani tangu kuibuka kwa ugonjwa wa Kipindupindu jitahada mbali mbali zimefanyika kwa kushirikiana na Mamlaka husika ikiwemo Wizara ya Afya , Ofisi ya Waziri Mkuu kitengo cha maafa ,kikosi cha kupambana na ugonjwa wa kipindupindu katika Ofisi ya Mkuu wa mkoa na taaisi nyingine nyingi zenye kutetea ustawi wa Afya ya Jamii.

Dawasco inapenda kuwakumbusha vyombo vya habari kuzingatia weledi na utashi katika kuteleza majukumu yao ya kila siku ili kuwapatia wananchi taarifa zilizo sahihi na zenye ukweli siku zote.

Tunaamini kosa la namna hiyo halitajirudia tena ili kuepusha adha na usumbufu kwa wananchi kama ulivyojitokeza kipindi hiki.

“Dawasco mbele kwa mbele”

Bi Everlasting Lyaro
Kaimu Meneja Uhusiano - Dawasco

[update] Rais Magufuli ghafla aibukia Muhimbili akitokea Aga Khan alikomjulia hali Dk BisimbaUPDATE/Taarifa Mpya

TAARIFA YA IKULU KWA VYOMBO VYA HABARI

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Joseph Magufuli , leo mchana amefanya ziara ya kushtukiza katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili na kukutana na hali ya kumsikitisha.

“ Rais  amesikitishwa na kuhuzunishwa na hali ya huduma kwa wagonjwa hususan wanaolala chini. Pia amekasirishwa na hali ya kutokujali wala kushughulikia vifaa vya kufanyia kazi ambapo amekuta mashine muhimu za uchunguzi wa magonjwa kama vile MRI na CT-SCAN zikiwa hazifanyi kazi kwa muda wa miezi miwili sasa, ilihali mashine kama hizo katika Hospitali za binafsi zinafanya kazi na wagonjwa wanaelekezwa kwenda kutafuta huduma huko”. Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Sefue amesema na kutoa maelekezo yafuatayo :

Rais amevunja Bodi ya Hospitali ya Taifa ya Muhimbili ambayo ilishamaliza muda wake na amemteua Prof. Lawrence Mseru, kukaimu nafasi ya Mkurugenzi Mkuu wa Muhimbili kuanzia kesho tarehe 10 Novemba, 2015.

Dkt. Hussein L. Kidanto ambaye ndiye anayekaimu hivi sasa, amehamishiwa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii ambako atapangiwa kazi nyingine.

Balozi Sefue pia amesema,   Rais ametoa wiki moja na kwa vyovyote si zaidi ya wiki mbili kwa uongozi mpya wa Muhimbili kuhakikisha kuwa mashine zote za uchunguzi wa magonjwa ambazo hazifanyi kazi zinafanya kazi na kuhudumia wananchi kama ipasavyo.

Tayari Wizara ya Fedha imetoa shilingi bilioni 3 kwa ajili ya kazi hiyo na kulipa madeni ya ukarabati wa mashine za uchunguzi wa magonjwa nchini.

Hata hivyo Katibu Mkuu Kiongozi amesema kuanzia sasa hospitali zote nchini zinatakiwa kutenga fedha kutoka kwenye mapato yao wenyewe na kuhakikisha mashine na vifaa vyote vya kazi vinafanya kazi wakati wote (Regular Maintenance).

Balozi Sefue pia metumia nafasi hii kuwaagiza watendaji na viongozi wote katika sehemu za kazi kuhakikisha wananchi wanahudumiwa ipasavyo na kazi za umma zinatekelezwa ipasavyo.

“Hakutakuwa na huruma kwa watumishi wa Umma wasiojali wananchi na mahitaji yao” Amesisitiza Balozi Sefue.

………Mwisho………

Imetolewa na;

Premi Kibanga,
Mwandishi wa Habari wa Rais Msaidizi,
Ikulu – Dar es Salaam.
9 Novemba, 2015


(video credit: Robert Okanda)

(video credit: Mroki Mroki / Father Kidevu blog)

Rais Dk Magufuli akimjulia hali Dk Helen Kijo-Bisimba
Rais Dk Magufuli akimjulia hali Dk Helen Kijo-Bisimba
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wa awamu ya tano Dk. John Magufuli amefanya ziara ya kushitukiza katika hospitali ya Taifa Muhimbili kujionea hali ya utoaji huduma kwa wagonjwa inavyoendelea. Akiwa hapo, pia alimjulia hali Mhe. Beatrice Shelukindo alielazwa wodi ya MOI baada ya kuvunjika mguu siku ya kuapishwa Rais katika viwanja vya Karimjee.

Awali Rais Magufuli alifika katika hospitali ya Aga Khan kumjulia hali Mkurugenzi wa LHRC, Dk Hellen Kijo-Bisimba anayepatiwa matibabu na vipimo katika hospitali hiyo kutokana na ajali iliyompata jana.


Rais Magufuli katika moja ya wodi za hospitali ya Muhimbili
Rais Magufuli katika moja ya wodi za hospitali Muhimbili
Tofauti na ziara yake ya ghafla katika Wizara ya Fedha aliyoifanya mwishoni mwa juma lililopita ambapo alikagua ofisi na kubaini kutokuwepo baadhi yao muda wa kazi kisha kuzungumza na wanahabari, leo Rais Magufuli aliongozana na uongozi wa hospitalini hapo kuwajulia tu hali wagonjwa na kuzungumza nao.

Mafuguli amesema ameamua kufanya hivyo kwa lengo la kujionea na kusikia changamoto zinazowakabili wananchi wakati wanaopata huduma za matibabu katika hospitali hiyo. Moja kati ya changamoto ambazo alikutana nazo ni pamoja na kuambiwa kuwa baadhi ya mashine za kuchukulia vipimo zilikuwa hazifanyi kazi kwa kipindi cha zaidi ya miezi miwili.

Rais Magufuli ambaye alishangiliwa na wagonjwa baada ya kufika katika hospitali hiyo aliagiza watendaji katika hospitali hiyo kuhakikisha wanatatua tatizo la mashine kutofanya kazi kwa kuwa hakupewa sababu msingi zinazosababisha tatizo hilo ili hali zinafanya kazi katika hospitali binafsi.

Aliweza kutembelea wodi ya wazazi pamoja na wodi za watu waliopata ajali ya vyombo mbalimbali vya moto.Rais Magufuli katika maeneo ya hospitali Muhimbili
(video credit: Robert Okanda)

Taarifa ya Bodi kuhusu awamu ya pili ya mikopo na kukanusha uvumi

BODI YA MIKOPO YA WANAFUNZI WA ELIMU YA JUU

AWAMU YA PILI YA WANAFUNZI WALIOPANGIWA MIKOPO KWA 2015/2016

Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu inapenda kuutaarifu umma kuwa kuna taarifa zinazosambazwa na baadhi ya mitandao ya kijamii kuwa Bodi haitatoa mikopo kwa waombaji wapya kwa mwaka wa masomo 2015/2016. Taarifa hizo si za kweli na hivyo Bodi inauomba umma kuzipuuza.

Aidha, Bodi ya Mikopo inapenda kutoa taarifa kwamba hadi sasa imekwishawapangia mikopo jumla ya waombaji mikopo wenye sifa 40,836 wa mwaka wa kwanza. Katika awamu ya kwanza, Bodi ilitoa orodha yenye jumla ya waombaji 12,282 waliofanikiwa kupata mikopo na katika Awamu ya Pili iliyotolewa tarehe 9 Novemba, 2015 jumla ya waombaji 28,554 wamepangiwa mikopo.

Majina ya waombaji waliofanikiwa kupata mikopo kutoka katika awamu zote mbili yanapatikana kupitia mtandao wa Bodi wa olas.heslb.go.tz na tovuti ya Bodi (www.heslb.go.tz). Aidha, orodha hizo pia zimetumwa vyuoni kwa ajili ya taratibu za usajili.

Lengo la Bodi ni kuhakikisha kuwa wanafunzi wa mwaka wa kwanza wenye sifa kupata mikopo katika mwaka wa masomo 2015/2016, ambao ni 50,830, wanapata mikopo.

Aidha, Bodi inapenda kuwasihi waombaji wa mikopo kuwa watulivu wakati mchakato wa upangaji wa mikopo kwa wanafunzi wenye sifa unaendelea.

Imetolewa na:

MKURUGENZI MTENDAJI
BODI YA MIKOPO YA WANAFUNZI WA ELIMU YA JUU