Mahojiano ya kwanza ya Waziri Mkuu Majaliwa baada ya kuteuliwaMtizamo wa Kipanya kuhusu Waziri Mkuu, WabungeGazeti na NIPASHE lilivyoandika jana na leo: "Waziri Mkuu ni Kasim Majaliwa"


Novemba 18, 2015 

Waziri Mkuu hadharani


Hatimaye kazi ya kutambua jina la waziri mkuu ajaye imekuwa rahisi zaidi baada ya majina ya watu wanaotajwa kuwa ndiyo walio mbioni kuteuliwa na Rais Dk. John Magufuli kushika nafasi hiyo kupungua hadi kubakia sita.

Taarifa za uhakika ambazo Nipashe imezipata zimebainisha kuwa hivi sasa, majina yaliyo na nafasi kubwa ya kuwa miongoni mwa wale watakaotajwa na Rais Magufuli ni pamoja na Mbunge wa Ruangwa mkoani Lindi, Kassim Majaliwa na pia Jenista Mhagama wa Jimbo la Peramiho mkoani Ruvuma.

Chanzo hicho kimefichua kuwa wabunge wengine wanne walio katika orodha itakayotoa jina la Waziri Mkuu ni Mbunge wa Bagamoyo aliyekuwa Waziri wa Elimu, Dk. Shukuru Kawambwa; Mbunge wa Chemba aliyekuwa Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, Juma Nkamia; Mbunge wa Mtwara Vijijini aliyekuwa Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Tamisemi), Hawa Ghasia na Mbunge wa Jimbo la Newala aliyekuwa Waziri katika Ofisi ya Rais (Utawala Bora), Kapt. George Mkuchika.

Chanzo kimeihakikishia Nipashe kuwa katika orodha hiyo ya wabunge sita, mmoja wao atakuwa Waziri Mkuu na wengi wataduwazwa kwani siyo miongoni mwa wale maarufu wanaotajwatajwa kwa zaidi ya wiki moja sasa.

Hadi sasa, majina ambayo yamekuwa yakitajwa mara kwa mara na taarifa zao kusambazwa kwenye mitandao mingi ya kijamii ni pamoja na Mbunge wa Jimbo la Isimani (Iringa), William Lukuvi; Mbunge wa Iramba Magharibi (Singida), Mwigulu Nchemba; Mbunge wa Bumbuli (Tanga), January Makamba; Mbunge wa Jimbo la Kyela (Mbeya), Dk. Harrison Mwakyembe, Mbunge wa Musoma Vijijini, Profesa Sospeter Muhongo; Mbunge wa Iramba Mashariki (Singida), Lazaro Nyalandu na pia Mbunge wa Tunduru Kaskazini, Mhandisi Ramo Makani.

Ratiba iliyotolewa wiki iliyopita ilionyesha kuwa Rais Magufuli atawasilisha jina la waziri mkuu wa serikali yake keshokutwa ili wabunge wapate nafasi ya kumpigia kura (waziri mkuu huyo) na kisha kufuatia shughuli ya kuzindua rasmi Bunge hilo la 11.

Chanzo kiliiambia Nipashe kuwa jina hilo la waziri mkuu linafahamika na tayari kuna harakati kadhaa zimeanza kuchukuliwa kuhakikisha kuwa kila kitu kinakwenda vizuri.

“Kinachosubiriwa sasa ni kwa Spika wa Bunge kupelekewa jina hilo tu… hakuna mwenye ujasiri wa kulitaja wazi kwani mwenye jukumu hilo ni rais mwenyewe,” chanzo kiliiambia Nipashe.

Hata hivyo, chanzo hicho kiliainisha sifa kadhaa muhimu ambazo ndizo zimeipa Nipashe ujasiri wa kutambua kuwa waziri mkuu ajaye ni kati ya majina sita, yakiwamo ya Jenista na Majaliwa.

KWA NINI NI KINA MAJALIWA?

Sifa hizo muhimu za mtu atakayetambulishwa bungeni kuwa ndiye waziri mkuu, kwa mujibu wa chanzo chetu, ni pamoja na mahala atokako. Kwamba, yeye hatoki katika mikoa ya kanda za magharibi, ziwa wala kaskazini.

Sifa ya pili ya mtu huyo ni kutowahi kujitokeza katika mbio za kuwania urais ndani ya Chama Cha Mapinduzi.

“Sifa muhimu ya tatu kwa mtu huyu ni kwamba, hajawahi kudhaniwa kushika nafasi hiyo na hivyo, atakapotajwa bungeni watu wengi wataduwazwa,” chanzo kilieleza.

Kadhalika, sifa ya nne ya mtu huyo atakayetajwa kushika nafasi hiyo ya uwaziri mkuu ni kwamba, amewahi kushikilia nafasi ya uwaziri/naibu waziri katika serikali ya awamu ya nne ya Rais Jakaya Kikwete iliyomaliza muda wake Novemba 5, 2015.

“Naye alikuwamo katika kundi la mawaziri na manaibu waziri waliomaliza na Rais Kikwete,” chanzo kilifafanua.
Kwa kuzingatia sifa hizo, ndipo Nipashe ilipofanya uchunguzi binafsi na kubaini maijina sita ya wale wanaoendana na sifa hizo.

Kwanza, mikoa isiyokuwa ya ziwa, nyanda za juu na kaskazini ni ya Kanda ya Kati, ambayo ni Singida na Dodoma; Mashariki na Pwani ambayo ni Morogoro, Pwani na Dar es Salaam na pia mikoa ya Kusini ambayo ni Lindi, Mtwara na Ruvuma.

Aidha, wabunge wanaotoka kwenye mikoa hiyo huku wakiwa na sifa ya kuwamo katika orodha ya mawaziri wa mwisho wa Rais mstaafu Kikwete, wasiowahi kuwania urais na pia wanaowexza kushangaza wengi pindi mmoja wao akitajwa kuwa waziri mkuu ni Nkamia wa Chemba (Dodoma), Dki. Kawambwa wa Bagamoyo (Pwani), Majaliwa wa Ruangwa (Lindi), Ghasia wa Mtwara Vijini (Mtwara) na Jenista wa Peramiho (Ruvuma).

UTABIRI WA WABUNGE 
 
Wakati chanzo cha Nipashe kikitaja sifa zinazowagusa kina Majaliwa, wabunge mbalimbali walioongea na Nipashe kwa sharti la kutotajwa majina yao wamesema ni vigumu kutabiri kwani Rais Mgufuli ni msiri na hadi sasa, kuna taarifa kuwa tayari ameshawatimua watu kadhaa waliojaribu kumuendea kwa nia ya kujipendekeza kwake ili awakumbuke au kupeleka majina ya watu wao.

“Magufuli ni kiongozi tofauti sana… hakuwa na mtandao wowote uliomsaidia kuingia Ikulu na hivyo mambo mengi ni ya siri, hayavuji kirahisi,” mbunge mmoja wa CCM aliiambia Nipashe jana.

Mbunge mwingine alisema katika uteuzi wa mawaziri wakuu waliopita, ilikuwa rahisi kubashiri kwa sababu taarifa mbalimbali zilikuwa zikiwafikia kabla hata ya tangazo rasmi bungeni, lakini sasa hali ni tofauti.

"Hivi sasa wabunge wa CCM hatujui lolote ... safari hii Rais (Magufuli) amefanya siri na wengi hatujui kinachoendelea," alisema.

Hata hivyo, baadhi ya wabunge walieleza sifa za watu ambaoe wanatamani wapewe nafasi hiyo, huku wengine wakitaja majina ya William Lukuvi aliyekuwa

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kuwa anafaa, na wengine wakiwataja aliyekuwa Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba, Mbunge wa jimbo la Musoma Vijijini, Prof. Sospeter Muhongo na Mbunge wa Muheza, Adadi Rajabu.

Mbunge wa Mtera, Livingstone Lisinde, alisema hawezi kutabiri jina, lakini angependa Waziri Mkuu awe ni mwanasiasa makini, mwadilifu na mwenye kuchukua hatua za haraka.

Mbunge wa Nkasi Kaskazini, Ali Kessy, alisema anatakiwa mfuatiliaji wa mambo ya kila siku, awe mkali na kwamba katika uendeshaji wa serikali, kamwe asibague watu, makundi na afanye kazi kwa matakwa ya kanuni, sheria na katiba ya nchi.

"Wananchi wamechoshwa na hatua ya serikali kuwahamisha watumishi wanaoharibu sehemu moja na kuwapeleka kwingine. Hivyo ni lazima Waziri Mkuu ajaye awe na sifa ya kuwachukulia hatua za kisheria watu wa aina hiyo na asiwaogope… hata kama kuna undugu na urafiki," alisema Kessy.

MATARAJIO WAZIRI MKUU WA MAGUFULI 
 
Baada ya uteuzi wa Mwanasheria Mkuu alioufanya siku ya kuapishwa kwake (Alhamisi), Magufuli alisubiri saa chache tu kabla ya kutembea kwa miguu kutoka ofisini kwake hadi katika jingo la Wizara ya Fedha ambako alifanya ziara ya kustukiza, akiingia kila ofisi kuona shughuli za ujenzi wa taifa zinavyoendelea.

Ni wazi kwamba kwa kufanya hivyo, Magufuli anaonyesha kuwa Waziri Mkuu wake atapaswa kuwa mtu wa vitendo zaidi na siyo maneno mengi.

Kadhalika, utoaji wa maamuzi kuanzia siku ya kwanza ni sifa muhimu ya kile alichokuwa akikisisitiza wakati wa kampeni kuwa kamwe, hatavumilia mawaziri wanaopenda majibu ya ‘tuko mbioni’, ‘tuko kwenye mchakato’, ‘tuko kwenye hatua nzuri’ wala ‘tuko kwenye hatua za mwisho’. Ni kazi tu.

Aidha, Magufuli ameshaoonyesha vilevile kuwa Waziri Mkuu wake atakuwa ni mtu wa kutoa maamuzi kwa kasi. Sifa hii inatokana na muda alioutumia katika kutangaza jina la Mwanasheria Mkuu na pia siku ya kuanza kwa Bunge la 11.

Magufuli pia ameshafanya kikao kizito na makatibu wakuu, naibu makatibu wakuu, gavana wa Benki Kuu (BoT) na Kamishna wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA). Katika kikao hicho, alitoa maelekezo kadhaa yaliyofichua sifa nyingine muhimu atakazokuwa nazo Waziri Mkuu wake na pia mawaziri wengine.

Rais Magufuli aliagiza pia kufutwa mara moja kwa safari za nje za mawaziri na viongozi wengine wa juu serikalini na kwenye taasisi za umma.

Aliagiza kuwa masuala yote ya nje ya nchi yatekelezwe na mabalozi waliopo huko na kwamba, kukiwa na ulazima, basi safari hizo ni lazima ziidhinishwe na yeye (Rais) au Katibu Mkuu Kiongozi, Ikulu. Rais Magufuli aliagiza kuwa anachotaka ni kuona viongozi wakifanya ziara nyingi kwa wananchi vijijini na kuwatatulia kero zao. Hii ni dalili nyingine ya wazi kuwa Waziri Mkuu ajaye hatakuwa mtu wa kusafiri nje mara kwa mara na badala yake, atakuwa ni mtu wa kuwa karibu na wananchi huku akisimamia shughuli za serikali kwa umakini zaidi.

Katika hili, ipo sifa nyingine anayotarajiwa kuwa nayo Waziri Mkuu mpya, ambayo ni kuwa na jicho la ziada kuhakikisha kuwa serikali haipati hasara kwa kuuziwa vitu kwa bei ya juu kuliko iliyopo sokoni.

Sifa nyingine muhimu kwa Waziri Mkuu ni kuwa mzoefu wa kukabili changamoto za hoja moto za wapinzani bunegni kwani katika Bunge lijalo, kambi ya upinzani itakuwa na wabunge 121. Kwa sababu hiyo, ni wazi kwamba mtu atakayeteuliwa na Rais Magufuli kwa nafasi ya Waziri Mkuu ni lazima atakuwa na sifa ya kukabiliana na maswali ya wabunge machachari wa upinzani pale inapobidi, ikiwamo wakati wa maswali ya papo kwa papo.

Kwa ujumla, kama ilivyowahi kuripotiwa katika gazeti hili, sifa muhimu za ujumla kwa Waziri Mkuu wa Magufuli zatarajiwa kuwa ni uadilifu, kwa maana ni lazima awe mtu asiyekuwa na chembe ya kashfa, hasa zinazohusiana na rushwa kama ilivyo kwa mwenyewe (Rais Magufuli); Kujiamini kiasi cha kutoa maamuzi magumu na kwa wakati kwa ajili ya maslahi ya taifa; kufanya kazi kwa pamoja na siyo kusaka umaarufu binafsi kiasi cha kumpiku Rais; Uwezo wa kusimamia utekelezaji wa mipango ya serikali na pia Kukubalika ndani na nje ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).


Waziri Mkuu ni Kassim Majaliwa?


Novemba 19, 2015

Wakati kitendawili cha nani atakuwa Waziri Mkuu katika Serikali ya awamu ya tano ya Rais Dk. John Magufuli, kikitarajiwa kuteguliwa leo, kuna kila dalili mteule wa nafasi hiyo anatarajiwa kuwa Mbunge wa Ruangwa (CCM), Kassim Majaliwa.

Majaliwa alikuwa Naibu Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Ofisi ya Waziri Mkuu wakati wa serikali ya awamu nne chini ya Rais Jakaya Kikwete.

Siyo jina kubwa kwenye medani ya siasa na aliingia katika medani hiyo mwaka 2010 baada ya kuchaguliwa kuwa Mbunge wa Ruangwa na kuteuliwa kushika wadhifa huo serikalini na kudumu nao hadi Rais Kikwete alipong’atuka.

Habari zilizopatikana kutoka ndani ya duru za serikali zinasema Rais Magufuli anataka kuteua mtu mpya atakayetekeleza kauli mbiu yake ya `Hapa kazi tu’.

Rais Magufuli atamkabidhi Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, Job Ndugai, jina la Waziri Mkuu leo asubuhi, ambaye atalitagaza na baadaye jioni kupigiwa kura.

Uchunguzi wa Nipashe kupitia vyanzo vyake mbalimbali umebaini kuwa Waziri Mkuu huyo, ambaye atalazimika kupitishwa na bungeni kupitia kura zitakazopigwa leo kabla Magufuli hajalizindua Bunge hilo kesho, umebaini kuwa jina la mteule huyo halijawa wazi kwa watu wengi, tofauti na walioteuliwa kushika nafasi hiyo katika serikali iliyopita ya awamu ya nne.

Kumbukumbu zinaonyesha kuwa Rais Kikwete alipoingia madarakani mwaka 2005, watu wengi walitabiri kwa usahihi kuwa angemteua Edward Lowassa, kuwa Waziri Mkuu.

Na hicho ndicho kilichotokea, kwani siku chache baadaye, jina la Lowassa liliwasilishwa bungeni na mwishowe akapitishwa na wabunge kwa kishindo kuwa Waziri Mkuu.

Kadhalika, inaelezwa vilevile kuwa hata baada ya Lowassa kujiuzulu kufuatia sakata la mitambo ya kufua umeme ya Richmond, wengi walitabiri kuwa Mizengo Pinda, angeteuliwa na Rais Kikwete kuwa Waziri Mkuu. Na ndivyo ilivyokuwa.

Hata hivyo, Nipashe imebaini kuwa hivi sasa tetesi kuhusiana na jina la Waziri Mkuu wa Serikali ya Dk. Magufuli, ziko tofauti sana kulinganisha na vile ilivyokuwa katika uteuzi wa Lowassa ambaye sasa yuko Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na Pinda.

Hata hivyo, Nipashe imethibitishiwa na chanzo cha uhakika kuwa Majaliwa ndiye anayepewa nafasi kubwa kushika wadhifa huo.

Majaliwa anaaminika kuwa ameonekana kuwa ana uwezo wa kuendana na kasi aliyoanza nayo Rais Magufuli katika kuhakikisha kuwa ahadi zote zilizotolewa wakati wa kampeni zinatimizwa.

Kwanini karata dume itamwangukia Majaliwa?

Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili umegundua viashiria kadhaa ambavyo vinadokeza kuwa Majaliwa ndiye atashika nafasi ya Waziri Mkuu.

Kwanza, ni kitendo chake cha kushika wadhifa wa Naibu Waziri kwenye ofisi ya Waziri Mkuu kwa miaka mitano, kumemfanya kuvuna uzoefu wa kufanya shughuli za taasisi hiyo na kukidhi vigezo vya kuaminiwa kupewa nafasi hiyo.

Pia ukizingatia kuwa Majaliwa ndiye aliyekuwa na jukumu la kusimamia masuala ya elimu kwenye Tamisemi, ambayo ni miongoni mwa ahadi kubwa za Rais Magufuli.

Ikumbukwe kuna suala la utekelezaji wa ahadi ya elimu bure kuanzia darasa la kwanza hadi kidato cha nne.

Kutokana na uzoefu wake wa kuongoza masuala ya elimu kwenye Ofisi ya Waziri Mkuu, kunamwongezea sifa ya kushika nafasi hiyo.

Kutokana na ukweli kuwa sifa mojawapo ya Waziri Mkuu anatakiwa kuwa mtu ambaye anaujua mfumo wa serikali, ndiyo maana kunafanya jina la Majaliwa kutajwa kushika nafasi hiyo.

Nipashe pia limedokezwa uwezekano wa Majaliwa kuteuliwa kushika nafasi hiyo umeongezwa na taarifa kuwa hata staili yake ya maisha katika siku za karibuni imebadilika.

Kuna taarifa zimedokeza kuwa familia yake yote kwa sasa iko mjini Dodoma huku kukiwa na ulinzi mkali kwenye nyumba ya serikali anayoishi eneo la Mikocheni jijini Dar es Salaam.

“Mheshimiwa na familia yake wamekwenda Dodoma tangu Jumapili iliyopita. Nyumbani kwake hakuna mtu kwa sasa,” alidokeza mmoja wa wafanyakazi wa Ofisi ya Waziri Mkuu, ambaye hata hivyo, siyo msemaji wake rasmi.

Mmoja aliye karibu na Majaliwa, naye aliiambia Nipashe hajawasiliana na kwa njia ya simu na Majaliwa tangu Jumapili iliyopita.

“Unajua ninafahamiana na Mheshimiwa Majaliwa kwa miaka mingi. Huwa ninamsaidia shughuli zake nyingi. Siyo kawaida yake kutojibu simu. Hata kama hatapokea, basi ni mwepesi kupiga baadaye. Nadhani kuna kitu hapa. Nina wasiwasi. Ila yote kheri kama mambo yatamnyookea,” alidokeza rafiki yake wa karibu, ambaye hakupenda jina lake litajwe gazetini.

Pia kutajwa kutokana na ukweli kuwa Majaliwa anatoka Mkoa wa Lindi ambao Kanda ya Kusini kunafanya awe na nafasi kubwa.

Kutokana na ukweli kuwa suala la jiografia huzingatiwa ingawa siyo la kikatiba, lakini uwezekano wa Waziri Mkuu kutoka Kanda ya Ziwa ni mdogo.

Wengine wanaopewa nafasi kubwa

Chanzo kimoja kiliidokeza Nipashe juzi kuwa awali waziri mkuu huyo atakayetajwa leo, ana ishara kubwa nne zinazomwezesha yeyote kumtambua.

Sifa hizo ni pamoja na mahali atokako ambako siyo Kanda za Magharibi, Ziwa wala Kaskazini.

Sifa ya pili ya mtu huyo ni kutowahi kujitokeza katika mbio za kuwania urais ndani ya CCM; sifa yake ya tatu ni kwamba hajawahi kudhaniwa kushika nafasi hiyo na sifa ya nne amewahi kushikilia nafasi ya uwaziri/naibu waziri katika serikali ya awamu ya nne ya Rais Kikwete iliyomaliza muda wake Novemba 5, mwaka huu.

Pamoja na Majaliwa, wengine wanaoangukia kwenye kundi hilo ni Mbunge wa Peramiho aliyekuwa Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Jenister Mhagama, Mbunge wa Kibakwe aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, George Simbachawene na Mbunge wa Bagamoyo aliyekuwa Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa.

Wengine waliomo katika orodha hiyo ya wabunge saba wanaotajwa kuwa wanaweza kupewa nafasi hiyo ni Mbunge wa Newala, Kapteni George Mkuchika, ambaye alikuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Utawala Bora), aliyekuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (TAMISEMI), Hawa Ghasia na pia Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Vijana na Michezo, Juma Nkamia.

Majina mengine yanayotajwa 

Pamoja nao hao, wengine ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakitajwa tajwa ni William Lukuvi, aliyekuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi; aliyekuwa Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba; Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini, Profesa Sospeter Muhongo, Mbunge wa Muheza, Adadi Rajabu; aliyekuwa Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba na pia aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu.

YANAYOJIRI BUNGENI

Kwa mujibu wa ratiba ya Bunge, jina la Waziri Mkuu litajulikana leo baada ya Rais Magufuli kuliwasilisha ili wabunge walipigie kura.

Baadhi ya wabunge walisema hivi sasa ni vigumu, bali kila mbunge kwa sifa anazozijua atataja mtu anayefikiri kuwa anafaa kuwa Waziri Mkuu na siyo rasmi kutoka ndani ya Chama.

"Ninachokiona Rais huyu amerudisha hadhi ya Ikulu kama taasisi, mambo yanakwenda kwa siri sana, ni vigumu sana kuvuja tofauti na serikali iliyopita, yapo yaliyovuja mapema, hii inatokana na kwamba Rais huyu aliingia madarakani kwa nguvu zake na Chama na siyo mtandao wa watu ambao analazimika kuwasikiliza," alisema mmoja wa wabunge hao.

Kwa mujibu wa ratiba, leo asubuhi itakuwa ni kupiga kura za Naibu Spika, baada ya wabunge wote kumaliza kula viapo vya kuthibitisha kuutumikia umma na kuilinda na kuitetea Katiba.

Mbunge wa kuteuliwa, Dk. Tulia Ackson ndiye anayewania nafasi hiyo kupitia CCM wakati Mbunge wa Urambo Magharibi (CUF), Magdalena Sakaya, atapeperusha bendera ya vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).

Vyama hivyo ni Chadema, CUF, NCCR-Mageuzi na NLD.

[update] Picha za Sherehe ya kuapishwa Waziri Mkuu

Kasim Majaliwa akielekea Bungeni leo kabla hajajua kuwa jina lake ndiyo lililopendekezwa kuwa Waziri Mkuu
YAH: SHEREHE ZA KUMUAPISHA WAZIRI MKUU MTEULE

Sherehe za kumuapisha Mhe. Majaliwa Kassim Majaliwa, Waziri Mkuu Mteule zitafanyika katika Ikulu ndogo ya Chamwino Mkoani Dodoma tarehe 20 Novemba, 2015 kuanzia saa 4.00 Asubuhi.

Sherehe hizo zinafanyika siku moja baada ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitisha jina lake kwa kura nyingi kuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kufuatia uteuzi uliofanywa na Mhe. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Kwa mujibu wa ratiba ya sherehe hizo, Wageni waalikwa wote wanapaswa kuwasili katika Ikulu ya Chamwino kuanzia majira ya saa mbili asubuhi.

Sherehe hizo zinatarajiwa kuhudhuriwa na wageni mbalimbali wakiwemo Marais Wastaafu, Mawaziri Wakuu wastaafu na waheshimiwa wabunge.

Imetolewa na Idara ya Habari MAELEZO

19 Novemba, 2015

[UPDATE/TAARIFA MPYA Novemba 20, 2015]Rais Dkt. John Pombe Magufuli, akimwapisha Mhe. Majaliwa Kassim Majaliwa, kuwa Waziri Mkuu wa awamu ya tano, wakati wa sherehe hizo zilizofanyika leo Nov 20, 2015 kwenye Viwanja vya Ikulu ndogo Chamwino mjini Dodoma.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.John Pombe Magufuli akimuapisha Kassim Majaliwa Kassim kuwa Waziri Mkuu wa Tanzania baada ya uchaguzi Mkuu uliofanyika hivi karibuni, hafla ya kiapo ilifanyika leo Ikulu ya Chamwino Mkoa wa Dodoma

Rais Dkt. John Pombe Magufuli, akimkabidhi nyaraka za Serikali baada ya kumwapisha Mhe. Majaliwa Kassim Majaliwa, kuwa Waziri Mkuu wa awamu ya tano, wakati wa sherehe hizo zilizofanyika leo Nov 20, 2015 kwenye Viwanja vya Ikulu ndogo Chamwino mjini Dodoma.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.John Pombe Magufuli akimkabidhi hati ya kiapo Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa Kassim baada ya uchaguzi Mkuu uliofanyika hivi karibuni, hafla ya kiapo ilifanyika leo Ikulu ya Chamwino Mkoa wa Dodoma

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, akimpongeza Waziri Mkuu mpya wa awamu ya Tano, Mhe. Majaliwa Kassim Majaliwa baada ya kuapishwa rasmi leo kwenye Viwanja vya Ikulu ndogo Chamwino mjini Dodoma, leo Nov 20, 2015.

Rais Dkt. John Magufuli (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Makamu wake, Mhe. Samia Suluhu Hassan (kushoto) na Waziri Mkuu Majaliwa Kassim Majaliwa, baada ya kuapishwa Waziri huyo Mkuu kwenye Viwanja vya Ikulu Ndogo Chamwino mjini Dodoma leo.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.John Pombe Magufuli (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Makamo wa Rais wa jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan (kushoto) na Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa Kassim (kulia) baada ya kuapishwa rasmi kushika wadhifa wake huo na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.John Pombe Magufuli katika Ikulu ya Chamwino Mkoani Dodoma leo.
Sehemu ya wageni waalikwa waliohudhuria sherehe hizo...

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.John Pombe Magufuli (katikati)akiwa katika picha ya pamoja na familia ya Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa Kassim (watatu kushoto mstari wa nyuma) baada ka kuapishwa rasmi leo katika viwanja vya Ikulu ya Chamwino Mkoani Dodoma,

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, akisalimiana na Mbunge wa Ilemela, Angelina Mabula kwenye viwanja vya Ikulu ndogo Chamwino wakati wa sherehe za kuapishwa Waziri Mkuu mpya wa awamu ya Tano, Mhe. Majaliwa Kassim Majaliwa zilizofanyika leo Nov 20,2015 mjini Dodoma.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, akizungumza na mtoto Majaliwa mtoto wa Waziri Mkuu mpya kwenye viwanja vya Ikulu ndogo Chamwino wakati wa sherehe za kuapishwa Waziri Mkuu mpya wa awamu ya Tano, Mhe. Majaliwa Kassim Majaliwa zilizofanyika leo Nov 20,2015 mjini Dodoma.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, akisalimiana na kuwapongeza baadhi ya Wabunge wapya wa bunge la 11, walipokutana kwenye viwanja vya Ikulu ndogo Chamwino wakati wa sherehe za kuapishwa Waziri Mkuu mpya wa awamu ya Tano, Mhe. Majaliwa Kassim Majaliwa zilizofanyika leo Nov 20, 2015 mjini Dodoma.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, akisalimiana na Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Singida, Martha Mlata, kwenye viwanja vya Ikulu ndogo Chamwino wakati wa sherehe za kuapishwa Waziri Mkuu mpya wa awamu ya Tano, Mhe. Majaliwa Kassim Majaliwa zilizofanyika leo Nov 20,2015 mjini Dodoma.

Makamu wa Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akimpongeza Waziri Mkuu mpya wa awamu ya Tano, Mhe. Majaliwa Kassim Majaliwa baada ya kuapishwa rasmi leo kwenye Viwanja vya Ikulu ndogo Chamwino mjini Dodoma, leo Nov 20, 2015.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, akisalimiana na Mbunge wa Peramiho, Mhe Jenister Mhagama, kwenye viwanja vya Ikulu ndogo Chamwino wakati wa sherehe za kuapishwa Waziri Mkuu mpya wa awamu ya Tano, Mhe. Majaliwa Kassim Majaliwa zilizofanyika leo Nov 20,2015 mjini Dodoma.

Waziri Mkuu mpya wa awamu ya Tano, Mhe. Majaliwa Kassim Majaliwa, akimpongezwa na mkewe baada ya kuapishwa rasmi leo kwenye Viwanja vya Ikulu ndogo Chamwino mjini Dodoma, leo Nov 20, 2015.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, akisalimiana na Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Mjini Magharibi, Asham Abdallah Juma, kwenye viwanja vya Ikulu ndogo Chamwino wakati wa sherehe za kuapishwa Waziri Mkuu mpya wa awamu ya Tano, Mhe. Majaliwa Kassim Majaliwa zilizofanyika leo Nov 20,2015 mjini Dodoma.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, akisalimiana na Mbunge wa Nzega, Hussein Bashe, kwenye viwanja vya Ikulu ndogo Chamwino wakati wa sherehe za kuapishwa Waziri Mkuu mpya wa awamu ya Tano, Mhe. Majaliwa Kassim Majaliwa zilizofanyika leo Nov 20,2015 mjini Dodoma.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, akisalimiana na Mbunge wa Shinyanga mjini Stephen Masele , kwenye viwanja vya Ikulu ndogo Chamwino wakati wa sherehe za kuapishwa Waziri Mkuu mpya wa awamu ya Tano, Mhe. Majaliwa Kassim Majaliwa zilizofanyika leo Nov 20,2015 mjini Dodoma.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, akisalimiana na Mbunge Mchengerwa kwenye viwanja vya Ikulu ndogo Chamwino wakati wa sherehe za kuapishwa Waziri Mkuu mpya wa awamu ya Tano, Mhe. Majaliwa Kassim Majaliwa zilizofanyika leo Nov 20,2015 mjini Dodoma.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, akisalimiana na Mbunge wa Viti maalum Kaskazini Unguja, Angela Malembeka, kwenye viwanja vya Ikulu ndogo Chamwino wakati wa sherehe za kuapishwa Waziri Mkuu mpya wa awamu ya Tano, Mhe. Majaliwa Kassim Majaliwa zilizofanyika leo Nov 20,2015 mjini Dodoma.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wananchi waliohudhuria sherehe hizo kwenye viwanja vya Ikulu ndogo Chamwino wakati wa sherehe za kuapishwa Waziri Mkuu mpya wa awamu ya Tano, Mhe. Majaliwa Kassim Majaliwa zilizofanyika leo Nov 20,2015 mjini Dodoma.

Picha: Ikulu, Ofisi ya Makamu wa Rais na Father Kidevu blog

Amwua mdogo wake baada ya kumkuta akimbaka nguruweKijana wa miaka 16 mkazi wa kijiji cha Mbwila wilayani Ludewa mkoani Njombe Simon Dastan amefariki dunia baada ya kupigwa kwa fimbo na kaka yake baada ya kukutwa akifanya ngono na nguruwe.

Kamanda wa Polisi mkoa wa Njombe, Wilbroad Mtafungwa alisema kuwa kijana huyo aliuawa baada ya kaka yake kusikia kuwa ameidhalilisha familia yao kwa kufanya mapenzi na mnyama na kuanza kumchapa kwa fimbo, hivyo kusababisha kutoka damu nyingi na hatimaye kufariki dunia.

Job opportunities at SUA
Wazanzibari waandamana London, Uingereza


Ni video ya maandamano yalioandaliwa na Jumuiya ya Wazanzibari waishio nchini Uingereza, kutaka Uingereza iingilie kati na kuweka shindikizo kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ili kuhakikisha mshindi wa uchaguzi wa Rais wa Zanzibar anatangazwa na kuapishwa,. Mandamano yalifanyika siku ya Alhamis Novemba 19, 2015 jijini London.

Bunge laridhia chaguo la Rais Magufuli la Kasim Majaliwa kuwa Waziri Mkuu
Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania leoa limempitisha Mbunge wa Jimbo la Ruangwa, Mhe. Kassim Majaliwa kuwa Waziri Mkuu wa Serikali ya Awamu ya Tano baada ya jina lake kupelekwa Bungeni na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli.

Mhe. Majaliwa amepitishwa kwa kura 258 sawa na asilimia 73.5% ya kura zote za ndiyo.

Idadi ya wabunge ilikuwa ni 394, waliosajiliwa 369, na waliohudhuria Bunge ni 351. Apigiwa kura 258. Zilizoharibika ni 2, na kura za hapana zilikuwa 91.

Majaliwa (CCM) jina lake lilitajwa katika ukumbi wa Bunge - Dodoma na Spika wa bunge hilo, Job Ndugai aliyeahirisha kikao cha bunge kwa dakika 45 kwa ajili ya kuandaa utaratibu wa Bunge kuthibitisha jina hilo kwa kulipigia kura.

Bahasha iliyobeba jina la Waziri Mkuu iliwasilishwa na mpambe wa Rais katika ukumbi wa Bunge huku ikiwa imefungwa kwa bahasha tatu tofauti na ikiwa imeandikwa kwa mkono na Rais mwenyewe, hali inayoonesha usiri mkubwa wa kuzuia kuvuja kwa jina la mteuliwa kabla ya kutajwa bungeni.

Kassim Majaliwa alizaliwa Desemba 22, mwaka 1960 na kupata elimu katika Shule ya Msingi Mnacho kati ya mwaka 1970-1976 kabla ya kujiunga na shule ya sekondari ya Kigonsera kati ya mwaka 1977- 1980.

Mwaka 1991-1993 alijiunga na Chuo Cha Ualimu Mtwara (Mtwara TTC). Alijiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mwaka 1994 na kuhitimu mwaka 1998 kabla ya kujiunga na Chuo Kikuu cha Stockholm nchini Sweden kwa masomo ya juu.

Amehudumu katika nafasi mbalimbali tangu mwaka 1984 alipojiunga na utumishi wa umma kama mwalimu mkoani Lindi, Katibu wa Chama cha Waalimu Wilaya, Katibu chama waalimu Mkoa na Mkuu wa Wilaya.

Mwaka 2010 alichaguliwa kuwa mbunge wa jimbo la Ruangwa mkoani Lindi kabla ya Rais Mstaafu, Jakaya Kikwete kumteua mwaka 2012 kuwa Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali ya Mitaa (TAMISEMI) anayeshughulikia elimu.

Kiongozi huyu pia mbali na kufanya kazi katika nafasi mbalimbali serikalini, alipitia Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) katika kambi ya Makutopora.

Waziri Mkuu Mteule wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Majaliwa Kassim Majaliwa, akitoka kwenye ukumbi wa bunge mjini dodoma jana mara baada ya kuthibitishwa uteuzi wake na bunge. (Picha: Francis Dande)


Waziri Mukuu Mteule, Majaliwa Kassim Majaliwa, akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kuteuliwa na kuthibitishwa na bunge mjini Dodoma jana, ambapo anatarajiwa kuapishwa leo Ikulu ya Chamwino.


Waziri Mkuu Mteule wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Majaliwa Kassim Majaliwa, akitoka kwenye ukumbi wa bunge mjini dodoma jana mara baada ya kuthibitishwa uteuzi wake na bunge.

Waziri Mkuu Mteule akiwashukuru wabunge mara baada ya kumthibitisha.

Dkt. Tulia Ackson Mwansasu achaguliwa kuwa Naibu Spika wa Bunge


Naibu Spika wa bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Tulia Ackson, akiapa kiapo cha utii mara baada ya kuchaguliwa na wabunge kwenye nafai hiyo mjini Dodoma.
Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, limempitisha Dkt. Tulia Ackson Mwansasu (CCM) kuwa Naibu Spika wa Bunge kwa kura 250 (sawa na 71.2%) dhidi ya mpinzani wake, Mhe. Magdalena Hamisi Sakaya (CUF) aliyepata kura 101 (sawa na 28.8%).

Idadi ya Wabunge iliyotakiwa ni 394, waliosajiliwa 369, akidi (quorum) ni 184 na waliohudhuria ni 351. Hakukuwa na kura iliyoharibika.
Wabunge wa CCM wakishangilia kumpongeza Naibu Spika wa bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Tulia Ackson (wanne kulia) nje ya ukumbi wa bunge mjini Dodoma. (picha: Francis Dande)


Ushauri wa Dk Kigwangallah wa namna ya kudhibiti dawa za kulevya

Wabunge wa Songea Mjini (CCM), Leonidas Gama (kushoto), Nzega Vijijini (CCM) Dkt. Hamis Kigwangallah (katikati) na Sixtus Mapunda wa Mbinga Mjini (CCM) wakibadilishana mawazo nje ya ukumbi wa Bunge mjini Dodoma muda mfupi kabla ya kuanza kwa mkutano wa Bunge la XI 
Mbunge mteule jimbo la Nzega vijijini Dkt Hamisi Kigwangalla (CCM) ametoa ushauri kwa wizara husika juu ya udhibiti wa kuvuja kwa madawa serikalini na kwenda kwenye maduka binafsi.

Kupitia ukarasa wake facebook Kigwangalla amesema #‎SasaKaziTuChangamoto ya Udhibiti wa Kuvuja Madawa Kutoka Mfumo wa Serikali Kwenda Kwenye Maduka ya Watu Binafsi ni Katika Mambo ambayo mgombea Urais wa CCM, Ndg. John Pombe Magufuli alionesha kuwa yanamkera sana. Hivyo wananchi wanasubiri kuona nini kitafanyika kutatua changamoto hii...kuna 'expectation gap' ambayo ni lazima izibwe ndipo watu wasadiki kushuhudia ‪#‎MabadilikoYaKweli.

Nimesikia kuna mkakati wa kutaka kuondoa maduka yote jirani na hospitali za serikali. Si wazo baya sana lakini ninaamini na ninajua kwa hakika kabisa kuwa kuna suluhisho bora zaidi ya hilo.

Inawashangaza watu wengi kuwa kwenye pharmacy za watu binafsi nje tu ya hospitali kuna dawa za kutosha za kila aina wakati kwenye pharmacy ya serikali ndani ya hospitali hakuna! Kuna watalamu wetu wanadhani suluhisho ni kuzuia uwepo wa pharmacy karibu zaidi na hospitali. Ninafahamu kwa mfano, kuna tafiti zimefanyika pale Muhimbili kuhusiana na idadi ya dawa zilizopo ukilinganisha na pharmacy mojawapo pale nje; matokeo ya utafiti huo yakawa, Muhimbili kuna dawa tofauti tofauti 850 (lines), wakati kwenye hiyo pharmacy kuna dawa tofauti tofauti takriban 3200!

Unaweza kusema si busara kuziondoa pharmacy hizi wakati tunajua kabisa kwenye hospitali yetu pale hakuna dawa za kutosha, maana itakuwa ni usumbufu kwa wagonjwa wanaoagizwa kutafuta dawa fulani ambayo Muhimbili haipo. Unaweza kusema kuwa aina mbalimbali zaidi ya 2300 za madawa zimeibiwa kutoka Muhimbili, na mimi hapo utanipa shida sana kukuelewa. Na nitakuuliza, zimepitia wapi pamoja na ulinzi uliopo? Na kama ziliwahi kuweza kutoka nje ya hospitali mpaka pharmacy, kwani pharmacy hiyo ikihamia Kariakoo ama Posta kutakuwa kuna ugumu gani wa 'wezi' hao wa madawa kuzifikisha huko pia kama wameweza kuzitoa?

Nadhani njia hii ni too 'mechanical' na haitoondoa tatizo zaidi ya kuzalisha tatizo lingine 'la usumbufu kwa wagonjwa'.

Nini kifanyike kudhibiti dawa zisikosekane kwenye mfumo wa afya?
  1. Tuhakikishe tuna dawa za kutosha kwenye Idara ya Bohari ya Dawa (MSD) kwa kuongeza 'capacity' yake kununua 'lines' nyingi zaidi za dawa kuliko ilivyo sasa, ambapo MSD inaweza ku-supply only 65% ya mahitaji. 
  2. Bohari ijiendeshe kibiashara.
  3. Tuweke 'color code' kwenye dawa zote za serikali kwenye bohari; mfano labda dawa za serikali ziwe na rangi ya 'pink' pekee, na rangi hii iambatane na 'bar code', na kuwe na 'task force' maalum ya ukaguzi wa pharmacy za binafsi na ikitokea dawa ya serikali ikakutwa kwenye pharmacy yoyote ile kuwe na adhabu kali.
  4. Bohari ya Dawa (MSD), kwa makubaliano maalum na hospitali husika, iruhusiwe kufungua pharmacy zake kwenye hospitali zote nchini ili iuze moja kwa moja kwa wateja. Tunaweza kuanza na hospitali chache za mfano - kama Muhimbili, Amana, Mwananyamala, Temeke, Sekou Toure, Za Rufaa za Mikoa na baadhi ya Wilaya, Vituo Vya Afya na Zahanati; Ili kuliko wateja wa hospitali za serikali kwenda kununua dawa kwa bei ya kurusha kwenye pharmacy za watu binafsi kule nje wanunue kwa bei nafuu ya serikali ndani ya hospitali zetu. 
  5. Tuongeze kasi ya kusajili wananchi wote kwenye Mfumo wa Bima ya Afya kwa Wote ili kuongeza financing kwenye mfumo wa afya wa serikali zaidi ya kutegemea bajeti tu. 
  6. MSD wakiishakuwa na pharmacy yao ndani ya health facility watakaa na wataalamu na menejimenti ya hospitali husika na kuorodhesha madawa wanayohitaji na MSD kuhakikisha yapo kwenye pharmacy yao kwenye kituo husika.
Mwisho.

Tumeshirikishwa na JamiiMoja blog