NIPASHE yaeleza ilivyoweza kubashiri kwa usahihi jina la Waziri Mkuu, Majaliwa

Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa CCM, Dkt John Pombe Magufuli akimnadi mgombea Ubunge wa jimbo la Ruangwa,Mh.Kassim Majaliwa, kwenye mkutano wa kampeni Oktoba 12, 2015
Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa CCM, Dkt John Pombe Magufuli akimnadi mgombea Ubunge wa jimbo la Ruangwa,Mh.Kassim Majaliwa, kwenye mkutano wa kampeni Oktoba 12, 2015
Baada ya Rais Dk. John Magufuli, kuvunja ukimya kwa kumteua Kassim Majaliwa, kuwa Waziri Mkuu wa Serikali ya awamu ya tano jana, hatimaye imefahamika ni kwa nini mbunge huyo wa Ruangwa mkoani Lindi alikuwa na kila sababu ya kupata nafasi hiyo.

Majaliwa aliyekuwa hatajwi sana katika orodha ya watu waliobashiriwa kushika nafasi hiyo, alishangaza wengi baada ya jina lake kutajwa na Spika wa Bunge, Job Ndugai na kuibua shangwe kubwa.

Uchunguzi uliofanywa na Nipashe ukiwahusisha pia baadhi ya watu walio karibu na Majaliwa umebaini kuwa naibu waziri huyo wa zamani wa Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) ameipata nafasi hiyo siyo kwa bahati kama ambavyo baadhi ya watu wanaweza kudhania, bali ni kutokana na msururu wa sifa zinazokidhi aina ya Waziri Mkuu anayeendana na Rais Magufuli.

Awali, Novemba 2 mwaka huu ikiwa ni muda mfupi tu baada ya Dk. Magufuli kutangazwa kuwa mshindi wa nafasi ya urais kufuatia asilimia 58.46 ya kura halali alizopata dhidi ya wapinzani wake akiwamo Edward Lowassa aliyewakilisha muungano wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), Nipashe ilitaja sifa kadhaa za Waziri Mkuu wa serikali ya awamu ya tano na kwa namna ya kipekee, zote sifa hizo zilizotolewa na wachambuzi wazoefu wa masuala ya siasa nchini, zinaendana moja kwa moja na Majaliwa.

“Ana sifa karibu zote zinazomfaa kuwa Waziri Mkuu wa Magufuli… hiki ndiyo kigezo kikubwa kilichombeba hadi akateuliwa kushika nafasi hiyo,” mmoja wa wachambuzi hao aliiambia Nipashe jana.

Baadhi ya wachambuzi wa masuala ya kisiasa wanahusisha pia uteuzi wa Majaliwa na dhamira ya Rais Magufuli katika utekelezaji wa ahadi zake alizotoa wakati wa kampeni za kuwania urais wakati wa uchaguzi mkuu.

Inakumbukwa kuwa maeneo 10 ambayo Magufuli alitangaza wazi kuwa amepania kuyashughulikia aingiapo madarakani ni pamoja kubana matumizi ya serikali, kuongeza mapato ya serikali kuboresha mfumo wa utendaji na ufanisi na kupitia kodi na ushuru unaowaumiza wakulima, wafugaji na wavuvi.

Pia kupitia upya baadhi ya sheria, kuorodhesha kero za wananchi, kuunda serikali ndogo, kumaliza kero za watumishi wa umma, utekelezaji wa ilani ya CCM na kupendekeza muundo wa kitaasisi ili kutekeleza ahadi yake ya kutoa Sh. milioni 50 kwa kila kijiji.

UADILIFU

Ili Dk. Magufuli atimize ahadi zake na hasa ile ya kupambana na ufisadi na rushwa, ilikuwa ni lazima awe na Waziri Mkuu asiyekuwa na chembe ya kashfa, hasa zinazohusiana na rushwa.

Katika miaka ya hivi karibuni, ikiwamo ya awamu ya nne ya uongozi wa nchi hii, kuliibuka kashfa kadhaa za ufisadi na rushwa kiasi cha kuitikisa serikali ya Rais Jakaya Kikwete mara kadhaa kutokana na vitendo vya aina hiyo.

Kashfa hizo ni pamoja na ile ya uchotwaji fedha katika akaunti ya Benki Kuu ya Malipo ya Madeni ya Nje (EPA), ukodishwaji wa mitambo ya umeme ya kampuni ya kufua umeme ya Richmond, ripoti chafu ya Msimamizi na Mkaguzi wa Fedha za Serikali (CAG) na ile ya ufisadi wa fedha za akaunti ya Tegeta Escrow kwenye Benki Kuu (BoT).

Lowassa aliwajibika kufuatia kashfa ya Richmond mwaka 2008 wakati Pinda alinusurika kwenye kashfa ya Escrow baada ya kusafishwa na Bunge. Hali hiyo inatajwa kuwa ni sababu mojawapo kubwa iliyomfikisha Majaliwa alipo sasa kwani inaelezwa kuwa kama alivyo Rais Magufuli, naye hana doa lolote kubwa linalohusisna na rushwa na ufisadi.

UKANDA

Kwa kuwa Dk. Magufuli anatokea katika mkoa wa Geita, ambao uko Kanda ya Ziwa,4 ilibashiriwa wazi kuwa Waziri Mkuu wa Serikali ya awamu ya tano atakuwa na uwezekano mdogo wa kuteuliwa kutoka katika kanda hiyo au zile za jirani.

Pamoja na ukweli kuwa, Tanzania ni miongoni mwa nchi chache duniani ambazo zimefanikiwa kupiga vita ukabila, lakini bado suala hilo limekuwa likichukuliwa kwa tahadhari kubwa.

Wafuatiliaji wa masual ya siasa nchini, wanaamini kwa vyovyote vile, Rais Magufuli atakuwa ameangalia jiografia ya nchi na kuhakikisha kuwa msaidizi wake mkuu wa shuguhuli za serikali anatoka sehemu nyingine ya nchi na siyo kwenye ukanda wao wala jirani na huko. Majaliwa anatokea mkoa wa Lindi ambao uko katika Kanda ya Kusini.

“Hii ni sababu isiyojadiliwa sana, lakini ni muhimu na kwa namna yoyote ile Rais aliizingatia katika uteuzi wake,” mchambuzi mmoja aliiambia Nipashe jana.

KUJIAMINI, MTU WA MAAMUZI MAGUMU

Mtu aliyetarajiwa kuwa Waziri Mkuu katika serikali ya Rais Dk. Magufuli alitakiwa kuwa na sifa ya kujiamini na uwezo mkubwa wa kutoa maamuzi magumu pale inapobidi.

Kutokana na unyeti wa kazi yenyewe na changamoto zinazokabili taifa kwa sasa, mtu wa sifa hii alikuwa na nafasi kubwa ya kuteuliwa na Magufuli kwani ndiyo pekee inayompa uhakika kuwa ni mtu asiyeyumba. Watu wanaomfahamu Majaliwa kwa karibu wanamuelezea kuwa yuko vizuri katika eneo hili na hivyo, kwa vyovyote vile, sifa hii pia imembeba kwa kiasi kikubwa.

Inaelezwa vilevile kuwa sifa nyingine ya Majaliwa ni uwezo mkubwa alio nao pia katika kujibu maswlai kwa ufasaha, tena bila kutanguliza ‘blaa blaa’ za kisiasa kwa masuala ya msingi. Hili alishalionyesha wakati wa kujibu maswali yaliyoelekezwa kwenye wizara yake bungeni na sasa natarajiwa pia kulionyesha zaidi wakati wa kipindi cha maswali ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu na pia wakati serikali itakapokuwa na hoja za kujibu, hasa kutoka kambi ya upinzani yenye wabunge 121.

ASIYEMZIDI RAIS MAGUFULI KWA UMAARUFU

Hii inatajwa kuwa ni sifa mojawapo kubwa na muhimu iliyombeba Majaliwa. Inalaezwa kuwa mara zote, uzoefu unaonyesha kuwa watu wengi waliowahi kushika wadhifa wa Waziri Mkuu ni wale wanaosifika kwa utekelezaji zaidi na siyo wenye kusaka umaarufu. Watu hawa hutakiwa kutekeleza wajibu wao kwa weledi na umakini mkubwa, lakini bila ya kumzidi Rais aliyeko madarakani kwa sifa au umaarufu huo.

Rekodi za nyuma zinaonyesha kwa mfano, nyota ya siasa ya Mwalimu Nyerere ilikuwa juu kisiasa licha ya kufanya kazi na mawaziri wakuu tofauti waliokuwa wachapakazi kwelikweli kama Rashid Mfaume Kawawa, Edward Moringe Sokoine, Cleopa Msuya na Salim Ahmed Salim.

Hata Joseph Warioba na John Malecela waliposhika wadhifa huo kwenye awamu ya pili chini ya Rais Mwinyi au Frederick Sumaye alipofanya kazi kwa miaka 10 na Rais mstaafu wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa, bado nyota za marais wao zilikuwa juu.

“Magufuli alipaswa kuwa na Waziri Mkuu asiye na nyota kali ya umaarufu kuliko yeye ili kuhakikisha kuwa malengo ya serikali yake yanatimia na siyo msaidizi wake kutumia nafasi hiyo katika kujijenga kisiasa,” mchambuzi mwingine wa siasa aliiambia Nipashe.

UWEZO KUSIMAMIA UTEKELEZAJI

Sifa mojawapo ya Waziri Mkuu mpya chini ya Dk. Magufuli ilitarajiwa kuwa ni uwezo wa kusimamia na utelekezaji wa dhati wa mipango ya serikali.

Kwa mujibu wa Dk. Magufuli, yeye hana nafasi na mawaziri wanaoendekeza kauli za ‘mchakato’, ‘tuko mbioni’ wala ‘tuko katika hatua nzuri’, bali anachotaka ni vitendo zaidi katika utekelezaji. Na mwenyewe Magufuli amedhihirisha hilo katika utendaji wake kwenye wizara mbalimbali alizowahi kuongoza, ikiwamo aliyomaliza nayo ya Ujenzi.

Dk. Magufuli alijizolea sifa kubwa kutokana na utendaji wake, hasa katika kusimamia ujenzi wa barabara sehemu mbalimbali nchini na bila kusahau alipokuwa Wizara ya Ardhi na ile ya Mifugo na Uvuvi.

Waziri Mkuu Majaliwa anatajwa kuwa ni mmoja wa wachapakazi makini na ambaye, wengi wanamtarajia ataendeleza moto wake wa kazi aliouonyesha katika kusimamia elimu akiwa Tamisemi na kumfikia Rais Magufuli au kumzidi kama mwenyewe alivyoahidi sifa za mawaziri wake zitakavyokuwa wakati wa kampeni za uchaguzi. Magufuli anatarajiwa pia kufanya vizuri zaidi kwani Tamisemi bado iko chini ya ofisi yake.

KINARA WA KWELI SHUGHULI ZA SERIKALI BUNGENI

Tangu kuanza kwa mfumo wa vyama vingi nchini Tanzania, miongoni mwa viongozi wanaokumbana na changamoto kali za wapinzani bungeni ni mawaziri wakuu.

Hawa ndiyo wamekuwa na kibarua cha kuwa vinara katika kukabili shinikizo kutoka kwa wapinzani, hasa katika kufafanua masuala ya utendaji. Majaliwa anaelezewa na wabunge wengi kuwa yuko vizuri katika eneo hili.

KUKUBALIKA NDANI, NJE CCM

Dk . Magufuli wakati akiteua Waziri Mkuu mpya, alitarajiwa kumtaja mtu mwenye sifa hii ya kukubalika na kuheshimika ndani na nje ya CCM. Wachambuzi wa masuala ya siasa wanasema Majaliwa anayo sifa hii na ushindi wake wa kishindo bungeni baada ya jina lake kuwasilishwa ni ishara kwamba kweli anakubalika, wakiamini kuwa atatekeleza kwa dhati ahadi zake na pia kulinda maslahi ya chama chake pindi atakapotakiwa kufanya hivyo.

MTU ASIYEWAZIA URAIS

Pamoja na dhamira njema ya Rais Kikwete ya kuwatumikia vizuri Watanzania, lakini moja ya matatizo yaliyomkabili ilikuwa ni kitendo cha baadhi ya mawaziri kuunda mitandao ya maandalizi ya urais kwa ajili ya uchaguzi mkuu uliopita wa 2015.

Mara baada ya kuingia madarakani mwaka 2005, baadhi ya watendaji wa serikali na wale wa CCM walianza kazi ya kuandaa mikakati na kutengeneza mitandao ya kumrithi Rais Kikwete.

Mitandao hiyo ilisababisha kuporomoka kwa utendaji wa baadhi ya mawaziri na mbaya zaidi, kulitokea kutoelewana na hata kuwapo kwa migawanyiko ya wazi.

Inaelezwa kuwa kufuatia hali hiyo, kulizuka mtindo wa baadhi ya mawaziri kubaki na kazi moja ya kuchafua wenzao huku wengine wakihangaika kujijenga kisiasa badala ya kufanya kazi waliyotumwa na rais na matokeo yake kushuka kwa utendaji katika baadhi ya wizara.

Hali hiyo ilisababisha Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuwaomba Rais mstaafu Ali Hassan Mwinyi, aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa chama hicho, Pius Msekwa na Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, kufanya kazi ya kusuluhisha makundi ndani ya chama hicho. Ni wakati huo pia ndipo mawaziri kadhaa walitajwa wazi na Kinana kuwa ni ‘mizigo’ kwani utendajni wao ulikuwa ukilalamikiwa na wananchi karibu katika kila kona na kudhoofisha chama chao.

Majaliwa hatajwi kuwa mmoja wa watu wanaojikweza na kujipatia umaarufu kwa nia ya kutaka kuwania urais siku moja. Hii ni sababu nyingine inayotajwa kuwa imembeba hadi kuwa mrithi wa Mizengo Pinda kwa nafasi ya uwaziri mkuu.

UZOEFU SERIKALINI

Wasifu wa Majaliwa unahusisha utumishi wa miaka kadhaa katika ofisi mbalimbali za serikali, akiwahi kuwa mwalimu, mkuu wa wilaya, ubunge hadi kuwa naibu waziri wa Tamisemi. Waziri Mkuu kwa kawaida ndiye mtendaji mkuu wa serikali. Na ndiyo maana ni muhimu akawa na uelewa mpana wa namna serikali inavyofanya kazi na mifumo yake.

Mathalani, Waziri Mkuu anayemaliza muda wake, Mizengo Pinda, kabla ya kushika wadhifa huo, alikuwa na uzoefu mkubwa wa utumishi serikalini kwa kufanya kazi kwenye Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Ikulu na kuwa Naibu Waziri na waziri kamili wa masuala ya Tamisemi.

Pia mawaziri wakuu waliomtangulia waliwahi kushika nyadhifa mbalimbali serikalini kabla ya kupata nafasi hiyo. Na ndiyo maana Majaliwa amepata nafasi hii kwani uzoefu wake siyo haba, ijapokuwa hakuwahi kushika nafasi ya uwaziri kamili.

MAWAZIRI WAKUU WALIOTANGULIA

Kabla ya Majaliwa aliyeidhinishwa kwa kishindo bungeni jana, wengine waliowahi kuwa mawaziri wakuu ni pamoja na Julius Nyerere (1961-1962), Rashid Kawawa (1962 na 1972-1977) Edward Sokoine (1977-1980, 1983-1984), Cleopa Msuya (1980-1983, 1994-1995), Salim Ahmed Salim (1984-1985), Joseph Sinde Warioba (1985-1990), John Malecela (1990-1994), Frederick Sumaye (1995-2005), Edward Lowassa (2005-2008) na Mizengo Pinda (2008-2015).

Imenukuliwa kutoka kwenye gazeti la NIPASHE la Novemba 20, 2015

Tope lazuia safari za magari barabara ya Kibondo - Kakonko - Nyakanazi


Muonekano wa tope zito na magari madogo ya abiria na makubwa yakiwa yamekwama katika msururu mrefu, baada ya mvua zinazoendelea kunyesha wilayani Kakonko mkoani Kigoma na kuleta tope lenye utelezi mkubwa katika eneo hilo na kufanya magari kupenya kwa shida baada ya magari mengine kukwama.

Baadhi ya abiria na madereva wanasema safari zao kuelekea mkoani Kigoma kupitia barabara ya Kibondo - Kakonko – Nyakanazi wakati wa mvua hukumbwa na changamoto ya matumizi, na kuiomba serikali kuifanyia matengenezo ili iweze kutumika wakati wote bila shida.[video] Spika Ndugai alipowaamuru "Tokeni nje" waliokuwa wanabwagiza "Maalim Seif. Maalim Seif"Wabunge wanaounda "Umoja wa Katiba Ya Wananchi", UKAWA wametolewa nje ya ukumbi wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania leo, Ijumaa, Novemba 20, 2015 baada ya kusisitiza kutokutambua ujio wa Dk Shein bungeni na kuanza kuzomea huku wakisema kwa kurudia, "Maalim Seif. Maalim Seif. ..."

Wabunge hao awali walitoa msimamo wao wa kutokubali Dk Ali Shein kuhudhuria Bunge hilo wakati rais John Magufuli atakapoingia bungeni kulihutubia kwa kuwa hawamtambui kama rais wa Zanzibar wakishikilia kuwa, kwa mujibu wa Katiba, muda wake wa uongozi umekwisha.

Kelele za kuzomea zomea ziliibuka ghafla wakati Rais Dk Shein alipoingia bungeni hali iliyoondoa utulivu Bungeni.

Hata hivyo, Mbunge pekee wa upinzani, Zitto Kabwe (ACT – Wazalendo) alibaki ndani ya Bunge kwa na kuendelea kusikiliza hotuba ya Rais Magufuli, ambaye naye alimsifu kwa msimamo wake.

Awali, wabunge hao walimuandikia barua Spika wa Bunge wakihoji uhalali wa hotuba ya Rais bungeni endapo Dk Shein atahudhuria Bunge hilo kama Rais wa Zanzibar.

UKAWA wameendelea kushinikiza Tume ya Taifa ya Uchaguzi ya Zanzibar (NEC) kumtangaza mshindi wa nafasi ya Urais wa Zanzibar, huku mgombea wa CUF Maalim Seif Sharif Hamadi akidai kuwa ameshinda kutokana na kura halali alizokusanya kwenye vituo vyote.

Spika wa bunge, Job Ndugai aliwataka wabunge hao waache kuzomea na badala yake wakae chini lakini baada ya agizo lake kutokuitikiwa alivyotaka, alitoa amri ya kuwaamuru watoke nje kwa hiari yao kabla nguvu ya dola haijatumika kuwatoa.

Rais Magufuli aagiza "zile fedha zote zilizokuwa zimechangwa...zikanunue vitanda vya wagonjwa"


Baada ya kulihutubia na kulizindua bunge la 11 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt JOHN POMBE MAGUFULI amehudhuria hafla fupi iliyoandaliwa kwa ajili ya wabunge katika viwanja vya Bunge Mjini Dodoma na kuagiza fedha zilizochangwa kwa ajili ya kugharamia hafla hiyo zipelekwe Katika Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa ajili ya kununulia vitanda vya wagonjwa.

Mheshimiwa Magufuli ametoa agizo hilo baada ya kupokea taarifa kuwa wadau mbalimbali wamechanga kiasi cha shilingi milioni 225 kwa ajili ya kugharamia hafla ya wabunge katika siku ya uzinduzi wa Bunge.

Dkt Magufuli amesema alipata taarifa za kuwepo kwa michango hiyo ya fedha na kutoa maelekezo kuwa zitumike kwa kiasi kidogo kwa ajili ya hafla hiyo na sehemu kubwa zipelekwe katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili ili zikatumike kununulia vitanda na hivyo kupunguza tatizo la wagongwa wanaolala chini kutokana na uhaba wa vitanda unaikabili hospitali hiyo.

“Nilipoambiwa kwamba zimechangwa shilingi milioni 225 zimekusanywa kwa ajili ya sherehe, nikasema fedha hizo zipelekwe katika hospitali ya Taifa Muhimbili zikasaidie kununua vitanda” alisema Dkt Magufuli na kusisitiza kuwa “kwa kufanya hivyo tutakua tumejinyima sisi wenyewe lakini tutakua tumewanufaisha wenzetu ambao wanamatatizo makubwa yanayoweza kutatuliwa kwa fedha hizo”.

Awali akitoa taarifa ya michango hiyo Ofisa wa Spika wa Bunge Bwana SAID YAKUBU amesema jumla michango iliyopatikana na shilingi milioni 225 na kwamba fedha zilizotumika katika hafla hiyo ni shilingi milioni 24 tu baada ya kuzingatia maagiza ya Rais Magufuli.

Katika Hafla hiyo Rais Magufuli amekabidhi vyeti vya kutambua mchango wa wadau waliochangia fedha wakiwemo Benki za NMB, CRDB na Benki ya Afrika pamoja na Mifuko ya Hifadhi ya Jamii ya PSPF na PPF.

Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano IKULU
November 20, 2015

Habari nyepesi nyepesi kuhusu Mawaziri Wakuu wa Tanzania

Add caption
Kassim Majaliwa anakuwa Waziri Mkuu wa pili kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu baada ya Mizengo Pinda.

Hadi sasa ni Waziri Mkuu mmoja tu amewahi kushika wadhifa huo akiwa katika serikali mbili tofauti, Rashid Mfaume Kawawa- Tanganyika na Jamhuri ya Muungano.

Ni Mzanzibari mmoja tu amewahi kushika wadhifa huo, Dk Salim Ahmed Salim.

Ni Waziri Mkuu mmoja tu aliyetumikia nafasi hiyo kwa miaka kumi, Frederick Sumaye (1995-2005)

Ni watu wawili tu waliotumikia nafasi hiyo kwa vipindi viwili tofauti, Edward Sokoine (1977-1980, 1983-1984) na Cleopa Msuya (1980-1983-1994-1995).

Ni Waziri Mkuu mmoja tu aliyekufa akiwa madarakani, Edward Sokoine (1984).

Ni Waziri Mkuu mmoja tu aliyejiuzulu kwa kashifa, Edward Lowassa (2008).

Ni Mawaziri Wakuu wawili tu waliojivua uanachama wa chama tawala, Edward Lowassa na Frederick Sumaye (kutoka CCM 2015)

Ni Mawaziri Wakuu wawili tu waliotokea vyama vya wafanyakazi, Julius Nyerere na Kassim Majaliwa.

Mmoja kati ya hawa ni Waziri Mkuu na mwingine ni mtoto wa Rais wa Kwanza
---
Nyepesi hizi ni kutoka kweney mazungumzo ya Watanzania via WhatsApp

Tangazo la kazi Happy Valley Day Care Center


Karibu na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Plot No. 214, Boma Road
P.o. Box 4664 Morogoro, TANZANIA.

Simu: 0783400701/0714022038
Barua Pepe: [email protected]
Tovuti:www.happyvalleyschools.blogspot.com


TANGAZO LA NAFASI YA KAZI

Happy Valley Day Care Center iliyopo Morogoro mjini karibu na ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro inatangaza nafasi (1) ya kazi ya mwalimu wa elimu ya awali.

Majukumu ya mwalimu wa awali yatakuwa yafuatayo
 • Kuwapokea watoto wafikapo shule na kuhakikisha wamerudi salama majumbani mwao 
 • Kuwafundisha watoto elimu ya awali 
 • Kuwahudumia watoto katika mahitaji yao mbalimbali 
 • Kuandaa michezo ya watoto na kuwasimamia wanapocheza 
 • Kutoa taarifa za watoto kwa wazazi kupitia shajara /diary za watoto 
 • Kuhakikisha usalama wa watoto wakati wote 
 • Kuhakikisha usafi wa watoto wakati wote 
 • Kuandaa ripoti za mitihani za watoto. 
 • Kufanya kazi nyingine yoyote ile inayoendana na taaluma ya elimu ya awali atakayoelekezwa na mkuu wake wa kazi. 

Sifa za Muombaji

 • Awe anapenda watoto 
 • Awe angalau na cheti cha ualimu wa elimu ya awali kutoka chuo kinachotambulika 
 • Awe na uwezo wa kuongea na kuandika kwa ufasaha lugha ya Kiingereza na Kiswahili 
 • Awe na umri usiopungua miaka (25) 
 • Awe mbunifu katika kuandaa michezo ya watoto 
 • Awe na ujuzi wa kuwaelewa watoto kwa haraka 
 • Awe na uwezo wa kujituma kuliko kuamrishwa 
 • Mwenye uzoefu wa kufundisha watoto atapewa kipaumbele 
Tuma maombi yako kupitia anwani ya barua pepe (E-mail) inayoonekana hapo juu. Pamoja na barua yako ya maombi, ambatanisha CV yako na nakala za vyeti vyako. Mwisho wa kutuma maombi ni tar 1/12/2015. Kwa maelezo zaidi piga kupitia namba za simu zinaonekana hapo juu.

Mawasiliano ya barabara za Ulowa, Ushetu, Uyogo na Kahama Mjini yakatikaMawasiliano kati ya Kata za Ulowa, Ushetu na Uyogo katika Halmashauri ya Ushetu Wilayani Kahama yamekatika baada ya barabara ya kwenda katika maeneo hayo kukatika kutokana na kushindwa kukamilishwa kwa madaraja yanayounganishwa maeneo hayo

Meneja wa wakala wa barabara Mkoa wa Shinyanga, TanRoads Augustin Philip amesema barabara hiyo ilikwama kupitika kutokana na mkandarasi aliyekuwa akijenga madaraja katika eneo hilo kuchelewa kumaliza.

Juzi wakazi wa kata hiyo walikumbwa na adha ya usafiri katika eneo hilo hali iliyolazimika kuvushwa kwa kubebwa begani kwa gharama ya shilingi 2,000/= kwa mtu mmoja baada ya eneo lililokuwa limetengwa barabara ya muda kujaa maji.

Philip amesema jana Ofisi yake imepiga kambi katika eneo hilo kutengeneza eneo jingine litakalotumika kwa muda kupitisha wananchi pamoja na magari ambayo zaidi ya wiki moja yalikuwa hayavuki katika eneo hilo hali iliyosababisha kupokezana abiria wa kutoka Kahama Mjini na wale wa maeneo ya kata hizo.

Hata hivyo madhara mengine yaliyojitokea kutokana na kukwama kwa ujenzi huo wa madaraja katika eneo hilo ni shughuli za utendaji wa Halmashauri ya Ushetu ambao, kwa mujibu wa Mkurugenzi wake Isabela Chilumba, ili kufika katika maeneo hayo watumishi wake walilazimika kuzunguka kupitia kata za Mapamba ama Bulungwa.

Nyumba na makazi yaendelea kubomolewa Mbezi Beach, KinondoniKijiko cha Manispaa ya Kinondoni kikibomoa nyumba ya Deus Kisisiwe iliyopo Block J Mtaa wa Libermann Mbezi Beach jijini Dar es Salaam, leo.

Hotuba ya kwanza ya Magufuli ndani ya Bunge kama Rais


Rais Dk. John Magufuli akilihutubia bunge mjini Dododma jana wakati akilizindua bunge hilo.

HOTUBA YA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, MHESHIMIWA JOHN POMBE JOSEPH MAGUFULI, AKIFUNGUA RASMI BUNGE JIPYA LA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, DODOMA,
20 NOVEMBA 2015

Mheshimiwa Spika;
Niko hapa leo kutimiza matakwa ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ibara ya 91 Ibara ndogo ya kwanza inayonitaka kulihutubia na kulifungua rasmi Bunge hili. Naomba nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujalia uzima na afya njema, na kutuwezesha kuwepo hapa siku ya leo. Aidha nitumie fursa hii kuwakumbuka wenzetu ambao, kwa namna na nafasi mbalimbali, walishiriki katika mchakato wa uchaguzi huu na kwa bahati mbaya walipoteza maisha yao kabla ya mchakato haujakamilika. Kwa hao wote waliotangulia mbele za haki ninamuomba Mwenyezi Mungu azirehemu roho zao na awape pumziko la amani. Nitumie nafasi hii kuwapa pole ndugu na jamaa ambao ndugu zao walifariki na wengine kupata ulemavu wakati wa mchakato wa uchaguzi huu.

Taarifa ya Wizara leo Novemba 20, 2015 kuhusu mahujaji wa Tanzania nchini Saudi Arabia

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

WIZARA YA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA KIMATAIFA


TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

TAARIFA ZAIDI KUHUSU MAHUJAJI KUTOKA TANZANIA WALIOFARIKI AU KUJERUHIWA HUKO SAUDI ARABIA


Mahujaji wengine wane (4) kutoka Tanzania ambao walikuwa miongoni mwa wale waliokuwa hawaonekani tangu ajali ya kukanyagana kwa mahujaji ilipotokea Makkah nchini Saudi Arabia tarehe 24 Septemba 2015 wametambuliwa kuwa, ni miongoni mwa mahujaji waliofariki dunia. Kutambuliwa kwa mahujaji hao kunafanya idadi ya mahujaji wa Tanzania waliopoteza maisha katika ajali hiyo kufikia thelathini na mbili (32).

Majina ya Mahujaji hao kutoka kikundi cha Khidmat Islamiya ni:-
1. Abdul Idd Hussein
2. Adam Abdul Adam
3. Rashida Adam Abdul
4. Khadija Abdukhalik Said

Aidha, hadi sasa mahujaji saba (7) kutoka Tanzania bado hawajulikani walipo na jitihada za kuwatafuta bado zinaendelea. Majina ya Mahujaji hao ni:
1. Burhani Nziru Matata
2. Farida Khatun Abdulghani
3. Juma Jecha Jaku
4. Laila Manunga
5. Nassor Mohammed Hemed
6. Saleh Mussa Said
7. Shabinabanu Ismail Dinmohamed

Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa,
Dar es Salaam
20 Novemba, 2015