Book: Remembering Nyerere in Tanzania - History Memory LegacyAvailable at www.africanbookscollective.com

Cross-posted from Chambi Chachage's blog - Udadisi

Kitabu cha wasifu wa mlinzi wa kwanza wa Mwalimu NyerereKinapatikana: www.africanbookscollective.com

Imenukuliwa kutoka kwenye blogu ya Chambi Chachage - Udadisi

Mmoja wa 5 waliookolewa kwenye machimbo Kahama afariki dunia

Mhanga mmoja kati ya watano wa ajali ya mgodi wa dhahabu wa Nyangalata waliolazwa katika hospitali ya wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga amefariki dunia..

Akithibitisha kifo cha mtu huyo mganga mfawidhi wa hospitali ya wilaya ya Kahama, Dk.Joseph Ngowi amesema hadi jana usiku afya ya mgonjwa huyo ilikuwa nzuri lakini leo asubuhi alianza kutapika mfululizo na ilipofika leo saa sita mchana akafariki dunia.

Nao baadhi ya ndugu wa marehemu wamesema wamepokea kifo cha ndugu ya kwa masikitiko lakini wanamshukuru mwenyezi mungu na sasa wanajiandaa kuusafirisha mwili wa ndugu yao kwenda nyumbani kwao Tarime kwa ajili ya mazishi.

Kwa upande wake mkuu wa wilaya ya Kahama Vitta Kawawa amesema halmashuri yake imepokea taarifa za kifo hicho kwa masikitiko kwa kuwa walikuwa wanafanya jitihada kuhakikisha wahanga wote wanapona na kurejea katika familia zao.
  • via Malunde 1 blog

Hotuba ya Waziri Mkuu Majaliwa ya kuahirisha Kikao cha Kwanza cha Bunge la XI

Waziri Mkuu Mhe. Majaliwa Kassim Majaliwa na mkewe Mama Mary Majaliwa wakisalimiana na viongozi wa mkoa wa Morogoro wakati waliposimama kwa muda mjini Morogoro wakiwa njiani kuelekea Dar es salaam wakitoka Dodoma kwa gari leo Novemba 22, 2015. Kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Dkt. Rajabu Rutengwe. (Picha: Ofisi ya Waziri Mkuu)

HOTUBA YA MHESHIMIWA MAJALIWA KASSIM MAJALIWA (MB), WAZIRI MKUU
WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, WAKATI WA KUTOA HOJA YA KUAHIRISHA MKUTANO WA KWANZA WA BUNGE LA KUMI NA MOJA, DODOMA TAREHE 20 NOVEMBA, 2015


Taarifa ya NHIF kuhusu madai yanayolipwa kwenye vituo vya huduma

MFUKO WA TAIFA WA BIMA YA AFYATAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI KUHUSU MADAI YANAYOLIPWA KWA VITUO VYA KUTOLEA HUDUNA NA MFUKO WA TAIFA WA BIMA YA AFYA TAR 22 NOV 2015.


Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya ni Taasisi ya Serikali iliyo chini ya Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii ambayo ilianzishwa kwa Sheria ya Bunge (SURA 395 Toleo la 2002) ikiwa na jukumu kubwa la kusimamia na kutoa huduma za matibabu kwa wanachama wake.

Kutokana na majukumu hayo, ili NHIF iweze kutoa huduma za matibabu kwa wanachama wake, imesajili vituo 6,347 vya kutolea huduma za matibabu ambapo mbali ya vituo vya wamiliki binafsi, mashirika ya Umma na Madhehebu ya dini, Mfuko pia umesajili vituo vyote vya serikali kuanzia ngazi ya zahanati mpaka ngazi ya Hospitali ya Taifa Muhimbili vimesajiliwa na Mfuko.

Mfuko unalo jukumu la kuvilipa vituo hivi madai ya huduma zilizotolewa kwa wanachama wake kwa kipindi husika huku sheria, taratibu na kanuni zikifuatwa katika ulipaji wa fedha hizo.

Katika kipindi hiki, baadhi ya watoa huduma wamekuwa wakitoa sababu mbalimbali za kushindwa kutoa huduma nzuri ama za kuridhisha kwa wanachama wetu na wananchi kwa ujumla kwa kisingizio cha kukosa fedha hali inayosababisha kukosa dawa, kukosa vifaa tiba na vitendanishi pamoja na kushindwa kuboresha mazingira ya vituo.

Watoa huduma hao wanadai hayo ama wanatoa visingizio vya kukwama huduma katika maeneo yao kutokana na NHIF kuchelewa kulipa fedha fedha za madai ambayo wametibia wanachama wake.

Taarifa hizi zinajenga mazingira kuwa NHIF ni kikwazo katika ufanisi wa vituo hivyo jambo ambalo si la kweli na limebeba taswira ya kuleta chuki baina ya wanachama ama wananchi na chombo chao ambacho kina dhamana ya kuwatibia.

Kwa kuzingatia hali hali iliyopo ya uhitaji mkubwa wa huduma za matibabu na kama alivyoagiza Mheshimiwa Rais John Pombe Magufuli katika hotuba yake ya kufungua bunge la 11 NHIF tayari imechukua hatua zifuatazo;-

  • NHIF tunakanusha kuwa sisi ndio kikwazo ama sababisho la huduma mbovu katika vituo hivyo nah ii inatokana na ukweli kwamba zipo jitihada mbalimbali ambazo NHIF imekuwa ikizifanya kuhakikisha inasaidiana na Serikali katika kuboresha huduma za vituo hivyo ili wananchi kwa pamoja wapate huduma zinazostahili.
  • Kuhusu suala la malipo kwa watoa huduma, NHIF imekuwa ikilipa watoa huduma wake ndani ya muda uliowekwa kisheria na unaoonekana katika mikataba ambayo Mfuko umeingia na watoa huduma hao.
  • Kisheria madai yanatakiwa kulipwa ndani ya muda wa siku 60 tangu yawasilishwe NHIF na muda huu unaweza ukapungua zaidi kutokana na umakini wa kituo husika kwa kuwasilisha madai kwa wakati na yaliyo na usahihi mkubwa.
  • Hata hivyo kwa kuzingatia ufanisi na uboreshaji wa huduma na hasa matumizi ya Mifumo Habari, Mfuko una uwezo wa kulipa madai hayo kwa muda mfupi zaidi.
  • Ili kuwawezesha watoa huduma waweze kulipwa haraka zaidi, Mfuko umeandaa Mfumo wa kielekroniki ambao hospitali zote kubwa zinazolipwa zaidi ya milioni 5 zimeingizwa ili kuharakisha zaidi malipo yanayodaiwa.

Pamoja na jitihada zote hizi mambo yafuatayo yamekuwa yakijitokeza;-

Watoa huduma hasa wa vituo vya Serikali wamekuwa kikwazo kwetu katika ulipaji wa madai yao kutokana na ucheleweshaji mkubwa wa madai wanayodai kwetu


Madai mengi ambayo yamekuwa yakiwasilishwa kwetu yamegubikwa na udanganyifu mkubwa hali inayotufanya kuchukua muda mrefu katika uhakiki wake ikiwemo kuwapigia simu wagonjwa waliopewa huduma za matibabu.


Baadhi ya watoa huduma bado wamekuwa wagumu kutumia Mfumo wa kielekroniki pamoja na kwamba vifaa vyote vinatolewa na NHIF ambapo Mfumo huu ndio unarahisisha uhakiki na kudhibiti udanganyifu.

Madai yamekuwa yakiwasilishwa kwetu yakiwa na mapungufu makubwa ikiwemo kukosekana kwa taarifa muhimu zinazosababisha Mfuko kushindwa kulipa kwa kuwa madai ya namna hiyo hayalipiki.

Jitihada ambazo zinafanywa na Mfuko kukabiliana na hili ni pamoja na;-

Kuwawezesha watoa huduma kwa kuwapa mafunzo katika maeneo ya kazi zao.

Kuhamaisha watoa huduma kuwasilisha madai yao kwa wakati ili yaweze kulipwa kwa wakati.

Aidha, tunapenda kukumbusha na kusisitiza kuwa Mfuko unao utaratibu wa mikopo ya dawa, vifaa tiba, ukarabati wa majengo na miundombinu ya TEHAMA kwa lengo la uboreshaji wa huduma za matibabu katika vituo kiaisi cha shilingi zipatazo bilioni 10 zimekuwa zikitengwa kwa lengo hilo. Hata hivyo muitikio, hususani kwa vituo vinavyomilikiwa na Serikali umekuwa ni mdogo na waliokuwa wengi wamekuwa wakiomba fedha badala ya vifaa jambo ambalo ni kinyume na malengo ya mpango huu.

Kutokana na haya yote, Mfuko unawakata watoa huduma kutoa huduma kwa wanachama wake bila kuelekeza visingizio kwa NHIF ili kwenda na sambamba na maagizo ya Rais wetu katika kuwahudumia Watanzania.

Kuhusu madai ya hivi karibuni kutoka Hospitali ya Rufaa ya Mbeya kuwa wanaudai Mfuko jumla ya shilingi bilioni 2 na kwamba wanaudai Mfuko kutoka mwezi Juni, 2015 Mfuko unakanusha madai hayo kuwa sio ya kweli. Ukweli ni kuwa Mfuko unalipa madai baada ya mtoa huduma kuwasilisha kwenye Mfuko. Madai ya mwisho ya Hospitali hiyo kulipwa ni ya mwezi Agosti, 2015. Madai ya mwezi Septemba, 2015 yamewasilishwa kwenye Mfuko tarehe 4/11/2015 ambayo mpaka sasa yana siku 15 tu. Kwa hiyo Hospitali ya Rufaa ya Mbeya tumewalipa madai yao yote na kwa mwaka huu wa 2015 kuanzia Januari hadi Agosti 2015 tumewalipa kiasi cha shilingi bilioni 4.3.

Mfuko unatumia fursa hii kutoa onyo kali kwa watoa huduma ambao wamekuwa bado wakijihusisha na udanganyifu wa aina yoyote kwa kuwa haitawaonea haya kuwafutia usajili na kuwafikisha katika vyombo vya sheria.

Mfuko pia unazidi kutoa rai kwa watoa huduma kutumia fursa zinazotolewa na Mfuko katika kuhakikisha huduma za matibabu zinaboreshwa kwa wanachama na Watanzania kwa ujumla.

Mwisho.

Imetolewa na,

Kaimu Mkurugenzi wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya

22 Nov, 2015

Mkuu wa Wilaya amfuta kazi Mganga wa zamu Geita

MKUU wa Wilaya ya Bukombe mkoani Geita, Amani Mwenegoha, amemfukuza kazi Dkt. Johanes Makobwe, aliyekuwa zamu wa Hospitali ya Wilaya ya Mjini Ushirombo mkoani Geita usiku wa kuamkia leo kwa uzembe na kukataa kumtibu mtoto mwenye umri wa miezi sita.

Mwenegoha ameiambia FikraPevu kuwa amechukua hatua hiyo ili iwe funzo kwa waganga na wauguzi wengine wanaofanya manyanyaso ya kupokea rushwa na kunyanyapaa wagonjwa hospitalini hapo.

Mkuu huyo amesema alipofika hospitalini hapo saa kumi na mbili asubuhi alimkuta mganga huyo akiwa amelala ndipo akampigia simu Mganga Mkuu wa Hospitali hiyo Dkt. Maja Susuma, aliyefika na kumpatia matibabu mtoto huyo.

Vyanzo vyetu vya habari ndani ya hospitali hiyo vinaeleza kuwa Mkuu huyo wa wilaya amechukua hatua hizo baada ya kupigiwa simu na wazazi wa mtoto aliyefikishwa hospitalini hapo saa kumi za usiku ili kupatiwa matibabu lakini mganga wa zamu alikataa kumtibu.

Sababu zinazotajwa kuwa ndizo zilizosababisha mganga huyo kutomtibu mgonjwa huyo ni madai aliyoyatoa kuwa Mganga ambaye angeingia zamu asubuhi ndiye ambaye angepaswa kumhudumia mtoto huyo.

Chanzo chetu cha habari kimedokeza kuwa, mhudumu huyo wa afya anatuhumiwa kwamba alikuwa amekwenda kuangalia mpira wa mechi ya ligi kuu kati ya Real Madrid C.F na F.C Barcelona iliyochezwa jana usiku Novemba 21, 2015.

Pia anatuhumiwa kuwa alikuwa amekunywa pombe hali ambayo inadhaniwa kusababisha kushindwa kufanya kazi na kutoa majibu yasiyoridhisha kwa wagonjwa.

Hata hivyo mganga huyo wa zamu amekutwa na Mkuu wa wilaya akiwa amelala, huku akikana tuhuma za kuwa alikuwa amekwenda kuangalia mechi ya mpira.
  • Imenukuliwa kutoka FikraPevu

Picha za kumbukumbu: Rais Magufuli alipolizindua rasmi Bunge la XI, 2015


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Joseph Magufuli akisalimiana na wabunge muda mfupi baada ya kuhutubia na kuzindua rasmi Bunge la 11 mjini Dodoma Jumamosi Novemba 20, 2015

MSD yazungumzia vifaa vilivyopelekwa MOI, Muhimbili


BOHARI ya Dawa (MSD) imeanza kupeleka vifaa tiba kwenye Taasisi ya Mifupa ya Muhimbili (MOI), vifaa ambavyo vimenunuliwa na Ofisi ya Bunge kwa agizo alilotoa Rais Dk. John Magufuli.

Vifaa hivyo vilianza kupelekwa juzi katika Taasisi hiyo ili kukabiliana na uhaba alioubaini Rais Magufuli baada ya kufanya ziara ya kushitukiza katika mapema mwezi huu.

Mkurugenzi Mkuu wa MSD, Laurean Bwanakunu akizungumzia kuhusu vifaa hivyo jijini Dar es Salaam juzi wakati wa usambazaji alisema hivyo vyenye gharama ya sh. milioni 251 ni pamoja na vitanda 300, magodoro 300, viti vya kusukuma (wheel chairs) 30, vitanda vya kubebea wagonjwa (stretchers) 30, mashuka 1,695 na mablanketi 400.

Alisema MSD ilianza kupeleka vifaa hivyo MOI mwishoni mwa wiki na kuwa itaendelea kutoa vifaa hadi wiki hii inayoanza leo.

Fedha hizo zilizotumika kununulia vifaa hivyo zilitokana na agizo la Rais Dk. John Magufuli alilolitoa wakati akilihutubia bunge mjini Dodoma mwishoni mwa wiki ambapo alilitaka bunge kutumia sh. milioni 15 tu kwa ajili ya kujipongeza na kiasi hicho kilichobaki kitumike kununulia vifaa hivyo.

Dott Mwaibale
__________ MWISHO ___________


TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Agizo alilolitoa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli la kutaka fedha zilizochangwa na wadau mbalimbali kwa ajili ya kugharamia hafla ya wabunge zipelekwe Katika hospitali ya Taifa Muhimbili kwa ajili ya kununulia vitanda na magodoro ya wagonjwa wanaolala chini limetekelezwa.

Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Sefue amesema fedha hizo zimefanikisha kupatikana vitanda 300 vya wagonjwa pamoja na magodoro yake, shuka 600, Baiskeli za kubebea wagonjwa na vifaa vingine na kwamba hivyo vyote tayari vimepelekwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili.

Balozi Sefue ameuagiza uongozi wa Hospitali hiyo kuhakikisha vitanda vyote vinafungwa kesho jumapili na kwamba atakwenda kuvikagua siku ya jumatatu vikiwa tayari vinatumiwa na wagonjwa waliokua wanakosa vitanda vya kulalia na kulazimika kulala chini.

Wadau mbalimbali walichanga fedha kiasi cha shilingi milioni 225 kwa ajili ya kugharamia hafla ya wabunge baada ya uzinduzi rasmi wa bunge la 11 lakini Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli aliagiza fedha hizo zitumiwe kwa kiasi kidogo kisichozidi shilingi milioni 15 na nyingine zipelekwe hospitali ya Muhimbili kutatua tatizo la uhaba wa vitanda.

Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano IKULU,

Novemba 21, 2015.Taarifa ya ziara ya Katibu Mkuu Kiongozi kesho katika hospitali ya Muhimbili

Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Sefue atafanya ziara katika Hospitali ya Taifa Mhimbili Kesho Jumatatu (23 Novemba, 2015) kuanzia majira ya saa nne asubuhi.

Ziara hiyo ni kwa ajili ya kukagua utekelezaji wa maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyeagiza fedha zilizochangwa ajili ya hafla ya wabunge zitumike kununulia vitanda vya wagonjwa katika hospitali hiyo.

Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasilino, IKULU

20 Novemba, 2015

Salam za Shigongo kwa Wabunge 2015

Bunge la Jamhuri ya Muungano.
Mimi ndugu yenu sijambo, naendelea kusukuma mbele gurudumu la maendeleo kujenga nchi yetu. Nawapongezeni sana kwa ushindi mkubwa mlioupata ambao leo umewawezesha kutuwakilisha Watanzania wote katika Bunge la Jamhuri ya Muungano, muhimili namba mbili katika nchi yetu.

Najua mmepita katika safari ndefu, wengi wenu mna majeraha, hayo yote yamepita, sasa ni kazi moja tu; kuwawakilisha vyema wananchi waliowatuma ili muweze kulisogeza taifa letu mbele kwa kuisimamia vyema serikali na zoezi zima la utungaji wa sheria.

Nawapongezeni sana kwa uchaguzi wa Spika Mheshimiwa Job Ndugai, Naibu Spika Mheshimiwa Dk. Tulia Mwansasu na pia Mheshimiwa Waziri Mkuu wa 10 wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Majaliwa Kassim Majaliwa. Hongereni sana.

Najua mtawakumbuka sana wabunge wenzenu ambao hawakupata nafasi ya kurejea bungeni, kama David Kafulila, kijana aliyejitolea kwa nguvu zake zote na hata kuhatarisha maisha yake mwenyewe katika Sakata la Escrow, lakini wananchi wa jimbo lake wakamuona alikuwa mbunge wa taifa si mbunge wao, wakamkata.

Pia mtawakumbuka sana wabunge walioaga dunia kama Deo Filikunjombe, Dk. Abdallah Kigoda, Celina Kombani, Kapteni John Komba, Mariam Mfaki, Clara Diana Mwatuka, Mungu azilaze roho zao mahali pema peponi, ni vyema mkasimama hata kwa dakika moja kuwakumbuka na ninamwomba Mungu wa Mbinguni, atuinulie watu wengine kama wao katika Bunge hili, watakaokuwa tayari kusimama kidete kutetea maslahi ya wanyonge.

Baada ya kusema hayo nielezee dhumuni la kuwaandikia barua yangu, kwani imekuwa ni desturi yangu sasa kuandika barua moja kila wiki, naandika barua hii kuwakumbusheni juu ya jukumu lililowapeleka Dodoma na matarajio ya wananchi waliowatumeni kazi, najua mnafahamu lakini si jambo baya kukumbushana ili asiwepo mtu atakayedhani amekwenda Dodoma kufaidi maisha, akabweteka kwa sababu ya heshima anayoipata hivi sasa kama mbunge, miaka mitano si karne, 2020, mtakutana na wananchi kwenye boksi la kura, yasije yakawapata yaliyowapata ambao hawakurejea.
Ndugu zangu waheshimiwa wabunge wa Jamhuri ya Tanzania, Mmepata bahati ya kuwa wabunge wa kwanza wa Bunge la 11 la awamu ya tano chini ya Rais Dk. John Pombe Magufuli, mmeupata ubunge katika kipindi ambacho uchumi wa nchi yetu katika robo ya pili ya mwaka 2015 unakuwa kwa kasi ya asilimia 7.9, hii ni kasi nzuri kwani kuanzia mwaka 2002 -2014 uchumi wa taifa hili hili ambao ninyi ni wabunge wake ulikuwa ukikua kwa wastani wa asilimia 6.72.

Waheshimiwa wabunge,

Wakati uchumi wa nchi yetu ukikua kwa asilimia 7.9, nchi nyingi za Afrika zinasuasua sana nyuma yetu, kasi ya ukuaji wa uchumi wetu kwa mujibu wa taarifa za benki ya dunia umezidi mataifa makubwa duniani kama China ambayo uchumi wake umekuwa kwa asilimia 6.9 tu! Na India ni asilimia 7, kwangu mimi hii ni dalili nzuri inayonyanyua matumaini yangu kwamba, hata kama hali ni mbaya hivi sasa, kama serikali itasimamiwa vizuri na Bunge ambalo ninyi ni wabunge wake, hakika tumekaribia kufika katika nchi ya ahadi.

Kwa nini nimeamua kuwaandikia barua hii? Waheshimiwa wabunge, pamoja na takwimu zote zilizoko hapo juu ambazo zinaashiria mema huko tuendako, ni ukweli ulio wazi kwamba ukuaji wa uchumi wetu haujaonekana kwenye meza ya chakula na maisha ya Mtanzania wa kawaida.
Katika nchi yetu yenye jumla ya watu wasiopungua milioni 48, milioni 12 kati yao bado wanaishi katika umaskini mkubwa, hizi ni takwimu za mwaka 2015! Huduma za afya bado ni mbaya, watu wengi wanakufa kwa magonjwa yanayoweza kutibika, elimu yetu bado ni duni, watumishi wetu wa umma bado hawalipwi vizuri na wamevunjika moyo, huduma za maji na umeme vijijini bado ni duni, vifo vya akina mama na watoto bado viko juu.

Sarafu yetu inazidi kuporomoka, imeshuka kwa karibu asilimia ishirini ikilinganishwa na thamani ya dola ya Kimarekani! Jambo ambalo limesababisha kupanda katika bei ya vitu vinavyoagizwa nje ya nchi na kufanya mfumuko wa bei ambao mwaka 2011 ulikuwa asilimia 20 ukashuka mpaka asilimia 4, Juni 2015, upande tena mpaka asilimia 6.4 jambo ambalo limechangiwa pia na kupanda kwa vyakula.

Waheshimiwa wabunge mnaingia bungeni Tanzania ikiwa na tatizo kubwa sana la ajira, takwimu zikionyesha kwamba karibu nguvu kazi ya vijana 800,000 huingia sokoni kila mwaka, soko ambalo halina ajira kwa ajili yao! Hili ni tatizo kubwa sana kwa taifa kama Tanzania ambalo vijana wake wengi wametegemezwa kuwa mara wamalizapo vyuo (ambazo hivi sasa ni vingi kila kona ya nchi) kutakuwa na ajira za kuwapa.

Nawaandikieni barua hii kuwakumbusheni ndugu zangu juu ya jukumu kubwa mlilonalo kwa taifa na watu wenu, hakika haiko sababu ya ninyi kusherehekea kuwa wabunge, kwani ushindi wenu ndiyo mwanzo wa kazi kubwa mliyonayo mbele, ambayo kwa mtu mwenye uzalendo wa kweli kwa taifa lake ubunge ni mzigo. Najua mmeingia Bungeni kwa kupitia vyama mbalimbali, wengine mmeteuliwa, najua mnazo tofauti mbalimbali, zikiwemo za dini, rangi, kabila na itikadi, nawaombeni sasa muweke tofauti zenu zote pembeni na kusimama pamoja kama wawakilishi wa watu ili kuisimamia Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania vyema iweze kutimiza majukumu yake.
Kuendelea kusimama na U-CCM, U-Chadema, U-Cuf, U-NCCR MAGEUZI, hakika hakutaisaidia lolote Tanzania yetu na watu wake, hivi sasa ninyi ni wawakilishi wa Watanzania, simamieni maslahi ya watu wa taifa hili na maslahi ya taifa kwa ujumla wake.

Mnapoingia bungeni katika kipindi hiki ambacho taifa letu linakabiliwa na hali ngumu ya uchumi, kukiwa hakuna fedha za kutosha kujiendesha, si jambo jema hata kidogo kuendelea kugawanyika, umoja peke yake ndiyo utaweza kubadilisha mambo. Najua ninyi nyote ni wazalendo kwa taifa lenu,
basi uonyesheni uzalendo wenu kwa vitendo ili kuhakikisha uwepo wenu Bungeni kwenye Bunge la 11 unakuwa ni wa kihistoria, wengi wenu ni vijana, matarajio yangu ujana, elimu na vipaji mlivyonavyo mtavitumia vizuri katika kuhakikisha vipaumbele vya taifa hili vinaandaliwa vyema kwa faida ya waliopo na watakaofuata baada ya sisi.

Nasi tulioko huku nje ya Bunge hatutawaachia mzigo huu peke yenu, tutatimiza wajibu wetu kama Watanzania wawajibikaji. Tutapiga kelele kila tutakapoona mambo hayaendi sawa, ufisadi unafanyika hadharani na rasilimali za taifa hili zinatumiwa na watu wachache kwa faida yao wao na familia zao, huu kwetu utakuwa ni uzalendo kwa taifa ambalo tumeapa kulitetea wakati wote na kuvitetea vyama vyetu pale tu vinapostahili.

Tanzania inasonga mbele, ilipo leo ni bora kuliko ilikokuwa jana, kama uchumi wetu ukiendelea kukua jinsi unavyokua kwa kasi, nina uhakika tutawapita waliokuwa mbele yetu wakiwa wamekaa! Hili halitakuja kama zawadi bali matokeo ya matendo yetu mema tutakayoyafanya, ninyi Bungeni na sisi huku nje ya Bunge, sote tuna wajibu wa kujenga taifa letu. Baada ya kusema haya niwatakieni bunge jema lenye mafanikio na nimtakie Mheshimiwa Spika Job Ndugai hekima na Busara za kuliendesha bunge hili vizuri, vivyo hivyo kwa msaidizi wake, pia waziri mkuu wetu mpya ambaye ni msimamizi wa shughuli zote za serikali Bungeni, namtakia kila la kheri.

Mungu ibariki Tanzania,
Mungu libariki Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Wabariki wabunge wote na wape moyo wa kizalendo na hekima za kuwafikiria wananchi wa taifa hili katika maamuzi yao.

Wasalaam,
Eric Shigongo James
...............................................
BARUA KALI

Ombi la mtandao wa Wanawake na Katiba kwa Serikali ya Rais Magufuli

Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake na Katiba na Uchaguzi, Profesa Ruth Meena (kushoto) akizungumza na wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari leo jijini Dar es Salaam. Kulia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania.
MTANDAO wa Wanawake na Katiba na Uchaguzi umeitaka Serikali ya Awamu ya Tano iliyopo chini ya Rais Dk. John Pombe Magufuli ijenge misingi imara itakayoondoa mazingira kandamizi kwa jamii ya chini hasa kwa akinamama. Aidha umeitaka serikali kuhakikisha inasimamia ipasavyo suala zima la uwajibikaji na kupambana na vitendo vya kifisadi ambavyo ndivyo vinavyowakandamiza wananchi.

Kauli hiyo imetolewa leo jijini Dar es Salaam na jopo la viongozi wanaounda mtandao huo likiongozwa na Mwenyekiti wa Umoja wa Mtandao, Profesa Ruth Meena walipokuwa wakitoa tathmini juu ya mtazamo wa mtandao huo baada ya Uchaguzi Mkuu na suala zima la usawa wa jinsia kwa wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari.

Akizungumza katika mkutano huo, Mkurugenzi Mtendaji wa Mfuko wa Wanawake Tanzania, Mary Rusimbi ambaye ni mjumbe wa Mtandao wa Wanawake na Katiba na Uchaguzi alisema serikali ya awamu ya tano ina kila sababu ya kumjali mwanamke na kutambua kuwa anamchango mkubwa katika maendeleo ya uchumi.

Alisema Serikali hainabudi kujenga misingi imara ya uwajibikaji wa kweli na kutambua makundi mbalimbali ya jamii kwa jinsia zote. "...Tunataka haki yetu iwe haki kweli kweli na itambulike huku ikiwa nautekelezaji wa vitendo na kwa uhakika," alisisitiza Bi. Rusimbi.

Alisema kuwa wangependa kushuhudia idadi ya kutosha ya wanawake inaingia katika ngazi mbalimbali za uongozi na vyombo vya maamuzi ili waweze kuingiza changamoto zao na kuzisemea ipasavyo kwa lengo la kupatiwa ufumbuzi.

Kwa upande wake Prof. Meena akizungumzia mtazamo wa mtandao baada ya Uchaguzi Mkuu juu ya ushirikishwaji wa wanawake katika kugombea nafasi anuai za uongozi alisema bado kuna changamoto kubwa kwa kundi hilo kwani kulingana na matokeo ya sasa Tanzania itafikia usawa wa 50/50 mwaka 2055.

Alisema licha ya ongezeko la fursa ya vitimaalum kupandishwa hadi kufikia asilimia 40 bado fursa hizo zinachangamoto kubwa kwani viti hivyo ndani ya vyama hutolewa kwa wanawake kama aina fulani ya zawadi jambo ambalo huwazuia wanawake hao kusimamia ajenda zao za msingi kwa kuhofia kuonekana wasaliti. "...Viti hivi maalum hutolewa na vyama na vyama ndio vyenye ushawishi na misimamo hivyo wanawake hawawezi kusimamia hoja zao ipasavyo...," alisema Prof. Meena.

Aidha Profesa Meena alivitaka vyombo vya habari kusaidia kubeba ajenda za wanawake na kukemea mfumo dume ili kuibadili jamii ambayo bado inamtazamo hasi juu ya wanawake na uwezo wao. Alisema wanawake walijitokeza kwa wingi katika uchaguzi huu licha ya kwamba ndani ya vyama vyao bado kuna aina fulani ya ugumu katika kuwapa nafasi kundi hilo.

Naye Mjumbe wa Mtandao huo, Dk Ave-Maria Semakafu aliitaka serikali kuendelea kuondoa vikwanzo na changamoto mbalimbali katika jamii ambazo bado zinamtesa mwanamke. Alisema huduma za elimu bado mtoto wa kike anachangamoto jambo ambalo linamnyima kufikia malengo yake huku huduma nyingine za maji na utafutaji wa nishati ya kuni ikiwa ni mzigo kwa mwanamke.

Mkurugenzi Mtendaji wa Mfuko wa Wanawake Tanzania, Mary Rusimbi (kushoto) ambaye ni mjumbe wa Mtandao wa Wanawake na Katiba na Uchaguzi akizungumza na wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari leo jijini Dar es Salaam. Kulia ni Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake na Katiba na Uchaguzi, Profesa Ruth Meena.

Mjumbe wa Mtandao huo, Dk. Ave-Maria Semakafu (kulia) akizungumza na wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari leo jijini Dar es Salaam.

Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania akisisitiza jambo kwenye mkutano na wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari leo jijini Dar es Salaam. Kutoka kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa Mfuko wa Wanawake Tanzania, Mary Rusimbi na Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake na Katiba na Uchaguzi, Profesa Ruth Meena

Baadhi ya wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari wakifuatilia mkutano wao na viongozi wa Mtandao wa Wanawake na Katiba na Uchaguzi leo jijini Dar es Salaam.

Baadhi ya wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari wakifuatilia mkutano wao na viongozi wa Mtandao wa Wanawake na Katiba na Uchaguzi leo jijini Dar es Salaam.

*Imeandaliwa na www.thehabari.com