Kenyan verbally abused "because you are black" in Finland

A shocking video of a black Kenyan woman being verbally abused by a white woman in Finland for being ‘black’ has caused a stir on social media.

The racial attack was filmed from the Kenyan woman’s car and the white woman is seen standing next to her victim’s car and spewing out a barrage of insults. In the video, the visibly angry white woman says: “I am a Finnish woman. You are a f***ing African woman”.

“You are zero. You are not human in my eyes. You know what happens in our country. Why all come rape our country? We are in trouble because of black people”.

“Just try to leave good here, work. Don’t use our facilities,” she adds.

The unidentified Kenyan woman then responds to the insults: “I am a nurse, by profession. I treat people in the hospital. Why are you attacking me? What did I do to you?”. To which the Finnish woman retorts, “Because you are black. This country will be like this. Because you are black and I’m white”.

After the barrage of insults, the Kenyan woman says “thank you” to to the white woman as she’s leaving, to which she curtly responds “You are welcome, but not in my country.”

The video...


Nyumba zachomwa moto ikihusishwa na siasa


Wanaompinga Magufuli wanataka nini hasa?

Rais Magufuli, kama alivyosema mwenyewe, hakutoa ahadi zilizolenga kujipatia kura tu wakati wa kampeni, bali kuhakikisha anazitekeleza kwa vitendo kwa faida ya Watanzania.

Hata hivyo, tunaona katika mitandao ya kijamii na hata kwenye vyombo vya habari baadhi ya Watanzania wachache wakionekana kutomuunga mkono Rais Magufuli.

Wanaompinga Magufuli wanataka nini hasa?

Je, wanataka tuendelee kuwa taifa ambalo matajiri hawalipi kodi isipokuwa wanaokamuliwa zaidi ni watu masikini, wenye kipato cha chini na wafanyakazi? Je, wanataka watu waliouziwa viwanda na mashamba waendelee kuyahodhi hata kama wameshindwa kuyaendeleza kwa mujibu wa mikataba?

Yaani wanachukia dhana nzima ya kufufua viwanda vya zamani na kuanzisha vipaya? Je, wanataka tuendelee na watendaji serikalini wasiowajibika ipasavyo ambao wamegeuza sekta ya umma kuwa sehemu ya kuchuma badala ya kuitumikia kwa faida ya wananchi wote?

Wanakataa asipambane na wala rushwa, wanataka alee wazembe katika utumishi wa umma na pia wanataka asizibe mianya ya uchakachuaji wa fedha za umma? Swali letu kwa wanaoonekana kutokuwa upande wa rais ni hili. Je, uzalendo wao ni kuunga mkono kitu gani?

Baadhi ya watu hawa, kwa miaka nenda rudi wamekuwa wakijinadi kwamba wanachukia ufisadi. Je, sasa wanaposhindwa kuunga mkono rais anayeahidi kupambana na ufisadi tuwaeleweje?

Maandalizi ya Wizara ya mwongozo wa muundo, mfumo na utaratibu wa elimu bure ifikapo Januari

KATIBU Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Sifuni Mchome, amesema wizara yake inaandaa mwongozo utakaotoa maelekezo juu ya muundo, mfumo na utaratibu nyumbufu utakaohakikisha kuwa ifikapo Januari mwakani, elimu ya msingi inatolewa bila malipo.

Profesa Mchome aliyasema hayo juzi jioni katika kikao na watendaji wakuu wa taasisi zote na vyuo vilivyopo chini ya wizara yake katika kuhakikisha wanatekeleza maagizo ya Serikali ya Awamu ya Tano. Chini ya Rais John Magufuli, Serikali imetangaza kuwa kuanzia mwakani itatoa elimu bure kuanzia elimu ya msingi hadi kidato cha nne.

Profesa Mchome alisisitiza juu ya utekelezaji wa kutoa elimu bure bila kuathiri ubora wa elimu itakayotolewa na kuziagiza taasisi zinazohusika pamoja na walimu kushughulikia kero zao katika ngazi mbalimbali ikiwemo upatikanaji wa nyumba za walimu.

Alisema wizara yake inatarajia kuongeza uandikishwaji wa watoto wa awali kutoka asilimia 45 mwakani hadi asilimia 100 ifikapo mwaka 2020. Katika kikao hicho ambacho pia kilijadili mwelekeo wa Sera na Mipango ya Elimu katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Tano, Profesa Mchome alisema wizara inajipanga kuhuisha taratibu za kujiunga na taasisi zinazotoa elimu msingi na mafunzo katika ngazi mbalimbali.

Profesa Mchome alitoa vipaumbele elekezi 20 vya utekelezaji katika kuboresha sera na mipango ya elimu kwa kipindi cha miaka mitano kutoka 2015 hadi 2020. “Wizara ina mpango wa kuandaa mfumo, muundo na taratibu nyumbufu za kutoa elimu ya awali na elimu ya msingi bila malipo ili kuongeza uandikishwaji wa watoto wa awali kutoka asilimia 45 mwaka 2015 hadi asilimia 100 ifikapo mwaka 2020,” alisema Profesa Mchome.

Aidha, Profesa Mchome alisisitiza kuhuisha sifa na kutambua sifa zinazohitajika katika mifumo na taasisi tofauti ili kuongeza udahili ili asilimia 20 ya wahitimu wa elimu ya msingi wawe wakijiunga na elimu ya sekondari huku asilimia 80 wakiendelea na mafunzo ya ufundi.

Alisema lengo la mpango huo ni kuhakikisha kuwa asilimia 70 ya wahitimu hao wanaweza kujiajiri na kuajiriwa ili kukidhi mahitaji ya soko hasa ikizingatiwa kwamba Serikali ya Awamu ya Tano imekusudia kupeleka nchi katika uchumi wa viwanda.

Pia aliziagiza taasisi zilizo chini ya wizara kuhuisha mipango yake kufikia malengo ya uongozi wa Dk Magufuli ikiwemo kuongeza nafasi za wanafunzi kujiunga na taasisi mbalimbali na wakati huo huo ubora wa elimu inayotolewa iwe chachu ya maendeleo.

Alizitaka taasisi hizo na vyuo kuhakikisha kuwa wanaweka msisitizo katika masomo ya sayansi ili kuandaa wanasayansi wa kutosha katika kumudu mahitaji ya soko la uchumi wa viwanda.

Aliviagiza vyuo vya elimu ya juu kukaa pamoja ili kujadili mahitaji ya kitaifa na kuandaa programu zitakazokidhi mahitaji hayo na kuitaka Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu kupitia upya vigezo vya utoaji wa mikopo kulingana na vipaumbele vya mahitaji ya soko.

Rais Magufuli asitisha maadhimisho ya siku ya UKIMWI kitaifa

Rais John Magufuli amesitisha maadhimisho ya siku ya UKIMWI kitaifa ambayo yalikuwa yafunguliwe mkoani Singida leo na kufikia kilele chake Desemba mosi mwaka huu mjini humo.

Badala yake Rais Dk Magufuli ameagiza fedha zote ambazo zilitengwa na serikali pamoja na wahisani mbalimbali kwa ajili ya maadhimisho hayo zielekezwe kununua vifaa tiba na vitendanishi.

Ofisa Habari Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa Tume ya Taifa ya Kudhibiti UKIMWI (TACAIDS), Nadhifa Omar, alisema Rais ametoa agizo hilo leo wakati maandalizi kwa ajili ya ufunguzi wa maonesho yaliyoanza Novemba 24 yakiendelea.

“Rais ameagiza kusitisha maadhimisho ya mwaka huu ya siku ya UKIMWI duniani ambapo kitaifa yalikuwa yafanyike Desemba mosi, mwaka huu mjini Singida na kutaka fedha za maandalizi zielekezwe katika manunuzi ya vifaa tiba kwa ajili ya hospitali nchini,”alisema Omary.

Omary alisema serikali ilitenga kiasi cha shilingi milioni 18 kwa ajili ya maadhimisho hayo huku kila mshiriki katika maonesho hayo akichangia kiasi cha shilingi laki tano.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Dar es Salaam juzi, Mwenyekiti Mtendaji wa Tume ya Taifa ya Kudhibiti UKIMWI (TACAIDS), Dk Fatma Mrisho alisema maadhimisho ya mwaka huu yakuwa yatanguliwe na maonesho ya wadau yatakayojumuisha huduma mbalimbali zikiwamo za utoaji elimu na burudani.

Dk Mrisho alisema huduma nyingine zilizopangwa kutolewa katika maadhimisho hayo ya wiki moja ni upimaji wa hiari wa watu zaidi ya 3,500 wanaoishi na virusi vya Ukimwi na utoaji ushauri nasaha, upimaji wa shingo ya uzazi, sukari, uzito, damu na kupata elimu itakayotolewa kupitia vikundi vya sanaa na burudani.

Maadhimisho ya mwaka huu yanachagizwa na kaulimbiu ya ‘Tanzania bila maambukizi mapya ya VVU, vifo vitokanavyo na UKIMWI na ubaguzi na unyanyapaa inazewekana.’

Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dk Parseko Kone aliwaambia waandishi wa habari ofisini kwake hivi karibuni kuwa maadhimisho hayo yanatarajiwa kuanza Novemba 24 mwaka huu kwenye viwanja vya Peoples Club ambapo uzinduzi utakuwa Novemba 25 kabla ya kilele, Desemba mosi.

Hii ni mara ya tatu tangu Rais Dk Magufuli aingie madarakani kuzuia maadhimisho yanayogharimu fedha nyingi na sherehe na fedha zake kuelekeza ikanunulie vifaa tiba mahospitalini.

Awali Rais aliagiza fedha zilizotengwa kwaajili ya hafla ya uzinduzi wa Bunge zaidi ya shilingi Milioni 225 ziende kununulia vitanda vya hospitali ya taifa Muhimbili.

Aidha Rais pia alisitisha maadhimisho ya siku ya Uhuru Desemba tisa mwaka huu na badala yake watu wafanye kazi katika maeneo yao ya kazi hasa usafi wa mazingira.

Kigogo wa chama cha siasa anatafutwa na polisi kwa kumnajisi mwanaye wa mwaka mmoja

Kigogo mmoja wa CCM wilayani Rombo anadaiwa kumnajisi mtoto wake mwenye umri wa mwaka mmoja.

Mama mzazi wa mtoto huyo alidai kuwa tukio hilo lilitokea Novemba 17, usiku nyumbani kwao Mwanga walipokuwa wamelala na alishtuka baada ya kusikia sauti ya mtoto akilia kutokea chumba kingine.

“Nilipoamka nilikwenda kwenye kile chumba na kumkuta mwanangu akitokwa na damu sehemu zake za siri, nilimchukua na kumpeleka Kituo cha Afya cha Mwanga,” alidai mama huyo.

Alidai kuwa daktari aliyemtibu alithibitisha kuwa alikuwa amenajisiwa.

Hata hivyo, alisema baada ya mumewe kufanya kitendo hicho, aliondoka na kwenda kwenye kituo chake cha kazi alichohamishiwa hivi karibuni cha wilayani Rombo.

“Daktari alipompima na kukuta kalawitiwa alimtibu na kumpa dawa za maumivu na kuniambia nikatoe taarifa polisi ili mume wangu akamatwe, lakini hadi sasa hajakamatwa,” alidai na kuongeza:

“Tangu amefanya kitendo hiki hajawasiliana na mimi na tayari nilishafungua jalada polisi. Nadhani alidhamiria kufanya kitendo hiki, amemuumiza mtoto,” alidai mama huyo.

Hata hivyo, Kamanda wa Polisi mkoani Kilimanjaro, Flugence Ngonyani alisema mtuhumiwa bado anatafutwa na polisi kisha afunguliwe mashtaka ya ubakaji.

“Ni kweli tukio hilo nimelisikia na utaratibu unaendelea ili akamatwe na kutoa maelezo dhidi ya tuhuma zinazomkabili. Pia, kama kuna mtu anajua alipo, atusaidie ili tuweze kumkamata na kumfikisha mahakamani,” alisema Kamanda Ngonyani:

“Tunawaomba wananchi mtusaidie katika hili, kitendo alichokifanya huyu baba si cha kufumbiwa macho, lazima atafutwe na akamatwe.”

Zanzibar: Ni nani alitangulia kuyatangaza matokeo ya kura za urais?

NINAANDIKA haya kwa sababu nimebaini wasomaji wengi wameshiba taarifa za uongo na propaganda nyepesi kuhusu kilichotokea hata kusababisha anayeitwa Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha, kutokwa na akili za kawaida, na kuamua kuchukua hatua ya “peke yake” inayoendelea kuichumia nchi mgogoro wa kisiasa.

Ni hatua yake ya kufuta uchaguzi mzima wa Zanzibar – Wazanzibari walimchagua Rais, Wawakilishi na Madiwani wa wadi za Zanzibar Oktoba 25.

Tena niseme wazi ninarudia kudurusu yaliyotokea baada ya kujiridhisha kuwa nisipofanya hivi, sitakuwa nimetenda haki kwa ukamilifu wake. Kwa kutotenda hivyo, nawapa ushindi wanasiasa wachache wachovu wanaotaka kupindisha ukweli kwa maslahi binafsi ya kisiasa.

Nimewahi kuapa kwa jina la mola muumba wa vyote ardhini na angani, ndani ya uhai wangu, sitavumilia ukweli kupotoshwa, kwa yale ninayoyajua kwa uhakika wake.

Lakini pia, ninapenda kusema, nimeguswa mno na majadiliano ya Wahariri katika mjumuiko wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) kuhusu kilichotokea hata Jecha akachukua hatua ile ya peke yake.

Ni “peke yake” kwa sababu mpaka sasa hakuna ushahidi wowote uliotolewa na yeyote ndani ya Tume kwamba alitumwa na Tume ambayo maana yake ni yeye mwenyekiti, makamu wake na makamishna kufanya alichokifanya; wala Tume haikupata kujadili suala lolote tangu wananchi walipomaliza kupigakura, hata iwe walifikia kuamua kufuta uchaguzi wote nchini.

Kitendo cha Wahariri kujadiliana kupitia gurupu lao mahsusi la WhatsApp, ni chema. Tatizo ni kuona baadhi yao wanaeneza ninachoona ni upotoshaji na propaganda ambazo ndizo zinatumiwa na uongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar kujenga kesi dhaifu.

Angalia, Mhariri kwa kutetea ujinga, anahusisha hatua ya Jecha kufuta uchaguzi uliogharimu karibu Sh. 9 bilioni, na hatua ya Maalim Seif Shariff Hamad, anayepigania haki yake ya kuongoza Zanzibar, kutangaza mwelekeo wa kura zake za ushindi.

Huu ni upotoshaji wa kwanza uso maana. Tuseme Maalim Seif amekosea kufanya alichokifanya Oktoba 26 asubuhi, hilo litakuwa kosa lake binafsi linalopaswa kuchukuliwa kijinai.

Ni juu ya wachunguzi wa serikali, Jeshi la Polisi, kumshughulikia. Wangemhoji, wakamrekodi maelezo, wakafungua jalada la tuhuma na kuliwasilisha kwa Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) wa Zanzibar, ambaye akiona tuhuma zina msingi na ushahidi, atafungua mashitaka dhidi yake.

Hivi adhabu inayomstahilia (kama ni sahihi) Maalim Seif aliyegombea urais na “kuchaguliwa” na wananchi kwa mujibu wa matokeo yaliyokwishatangazwa na wasimamizi wa vituo majimboni, inajuzu vipi kuangushiwa wapigakura?

Iko wapi hapo haki ya wapigakura wa Zanzibar kama wanaadhibiwa wao waliopewa haki na Katiba ya Zanzibar ya 1984, kwa kosa lisilowahusu?

Kwani wao ndio waliofanya hicho anacholaumiwa mgombea kufanya? Walifanyia wapi wananchi waliopigakura? Wanasingiziwa ubaya usiowahusu. Kwa hakika watu wasio na hatia yoyote zaidi ya kutumia haki yao ya kikatiba, wanadhalilishwa isivyostahiki.

Maneno niliyoyawekea wino mzito nataka yaeleweke vizuri. Wale wanaojenga hoja ya kumlaumu Maalim Seif na kumtia makosani eti amejitangaza mshindi, wajue kwamba kila kituo cha uchaguzi kilichokuwa na wapigakura wasiozidi 350, kilihesabu kura za urais, pamoja na zile za uwakilishi na udiwani. Na wakahesabu za Rais wa Jamhuri na Wabunge.

Msimamizi alijaza fomu za kura hizo, akawasainisha mawakala wote waliokuwa kituoni, naye akasaini. Akabandika fomu ukutani nje kwa ajili ya umma kujua. Waangalizi, kama tulivyoshuhudia waandishi wa habari, nasi tuliangalia kuthibitisha kile tulichoshuhudia wakati kura zinahesabiwa na kujumlishwa majimboni.

Katika hali kama hiyo, ni nani katangaza matokeo? Ni nani alitangulia kuyatangaza matokeo ya kura za urais? Asemaye ni Maalim Seif, huyo ana lake dhidi ya mwanasiasa huyu kipenzi cha umma.

Maalim Seif, mgombea urais, alipata fomu za majimbo yote 54 (majimbo 18 Pemba na 36 Unguja). Asipate vipi wakati sheria ya uchaguzi inaruhusu na safari hii timu yake ilisimamia kijasusi zipatikane kupitia mawakala wake vituoni? Akajumlisha kura za majimboni, akaona anatimiza idadi ya kura za kumshinda Dk. Ali Mohamed Shein. Tunaelewana?

Labda hamjui nyie, viongozi wa CCM wanatafutana uchawi, ni nani aliruhusu Maalim Seif azipate fomu za majimbo yote? Hamjui baadhi ya mawakala wa CUF walikimbizwa kiroho mbaya na mazombi (askari wasio nidhamu wa serikali) wazisalimishe fomu zisimfikie mgombea. Walichofanikiwa siku zote CCM, kimewashinda safari hii; wanalizana mjue!

Mhariri mzima anashauri kwa njia ya swali, “Maalim Seif akamatwe?” Nani amezuia hili kutendwa?

Kwanini asikamatwe kama amekosa; hata mara moja hajajiweka juu ya sheria. Anakamatika na kushitakika. Mbona ameshashitakiwa sana.

Maalim Seif amekaa gerezani pasina kuhukumiwa na mahkama. Huyu ni mpigania haki za Wazanzibari na nchi yao, hahofii mahkama wala gereza. Amepata kuyasema haya hadharani. Hajabadili kauli.

Juma Duni Haji, mwanasiasa mahiri kwa lugha ya kujengesha hisia wananchi, na kuzidodosa takwimu na tawala dhalimu Tanzania, ameshasema haya mara kadhaa. Nimeyasikia kwenye kampeni za uchaguzi uliofanyia mwezi uliopita.

Hawa wawili wamesema sana hawaogopi yote mawili – mahkama na gereza. Duni alikaa gerezani miaka mitatu mfululizo wakati huo alishatuhumiwa kuua askari mjini Wete, Mkoa wa Kaskazini Pemba, katika siku ambayo kwa hakika alikuwa mjini Unguja.

Maalim Seif alishakaa gerezani sana tu. Alisingiziwa kumshika askari shababi (kijana barubaru) na kumnyang’anya bunduki akiwa na wafuasi wake kadhaa eneo la Jang’ombe. Wenyewe wanasema wameshauawa bado kuzikwa.

Juwa usiyejua kwamba Sheria ya Uchaguzi Na. 11 ya Zanzibar ya 1984, Kifungu 88, inamtaka msimamizi wa uchaguzi jimboni “(a) haraka atamtangaza mgombea aliyepata wingi wa kura halali zilizopigwa kuwa amechaguliwa; na (b) atapeleka taarifa ya maandishi kwa mgombea aliyeshinda; na (c) atatoa taarifa ya matokeo kwa Tume, nayo itayapeleka matokeo, pamoja na idadi ya kura alizopata kila mgombea katika jimbo kutangazwa katika Gazeti Rasmi.”

Ni hawa wasimamizi walikuwa na matokeo ya kura za urais wakawasilisha Tume wakiwa wameshabandika fomu kwenye kuta za vituo majimboni. Walikuwa wameshathibitisha matokeo ya uchaguzi kwenye maeneo yao.

Hatua hiyo imefanywa pasina malalamiko ya mgombea yeyote akiwemo wa CCM. Ila wakubwa watatu wa CCM walifika Tume Oktoba 27, na barua ya malalamiko. Walisikilizwa, waangalizi wakiwepo, lakini wakatoka kapa, hakuna walichokipata.

Hapo, wakaandaa hila – eti makamishna walipigana ngumi, kura zilizidi wapigaji, nyingine ziliokotwa mitaani, eti Maalim Seif alitoka Afrika Kusini na kura bandia.

Kote hawana hoja ya kisheria. Kote wamejidhalilisha na kuumbuka. Hata mpango wao wa kuchakachua matokeo kisiwani Pemba ulishindwa baada ya kukosa wakala wa kuwasaidia kutengeneza matokeo ya kumpiku Maalim Seif.

Kilichobaki baada ya njia hizo kushindwa, ni kimoja tu – yale ya kutokabidhi serikali kwa vikaratasi. Walisema na kurudia, si kada mmoja wala wawili, wengi wao. Wakamtweza nguvu Jecha akafanya ujecha wake, leo amebakia peke yake ndani kwake, nje hakutokeki, kuchungu. Wao wasema wamsubiri atangaze siku ya uchaguzi mpya. Haweshi ubabe, na ndiyo demokrasia yao. Hawa kwa siasa chafu hawawezekani.
  • via MwanaHALISI Online

Wananchi waomba Magufuli awalinde baada ya kumkamata muuguzi kwa "kuiba dawa za kituo cha afya"

Kagoma Hamis akizungumzia walivyokamata dawa hizo na kuita polisi waliofika muda mfupi na kukamata dawa ambao walimkamata mtuhumiwa 
Katika hali hali isiyokuwa ya kawaida baadhi ya wakazi wa kata ya Kambarage manispaa ya Shinyanga wamefanikisha kukamatwa kwa muuguzi mkunga katika kituo cha afya cha Kambarage mjini Shinyanga akituhumiwa kuiba dawa za kituo hicho.

Mashuhuda wa tukio hilo la aina yake wameiambia Malunde1 blog kuwa limetokea jana majira ya saa tano asubuhi katika eneo la kituo cha afya Kambarage Shinyanga baada ya wananchi takribani saba kumtilia shaka muuguzi huyo aliyejulikana kwa jina la Joseph Nkila waliyemuona akitoka kituoni hapo akiwa ameficha mfuko waliohisi kuwa ni dawa za serikali.

Muuguzi amekamatwa na wananchi akiwa na kopo moja la dawa aina ya paracetamol na chupa mbili za dawa ya maji aina ya Erythromycin Syrup.

Wakisimulia jinsi walivyomkamata, Rashid Shaban na Kagoma Hamis kati ya wananchi saba wanaofanya shughuli zao karibu na kituo hicho cha afya wameiambia Malunde1 blog kuwa kwa muda mrefu wamekuwa wakikerwa na mchezo mchafu wa muuguzi huyo ambaye mara nyingi amekuwa akionekana na maboksi ya dawa yenye nembo ya MSD na mara nyingi amekuwa akiegesha gari lake kwenye eneo lao la kazi na kisha kupakia dawa hizo kwenye gari jingine na ndipo jana walipoamua kuchukua hatua.

Wamesema jana kama kawaida yake alifika eneo hilo na kisha kushusha mfuko na kuuweka kwenye gari jingine na kumpa maelekezo dereva wa gari hilo na kuondoka haraka kutoka eneo hilo na kumuacha dereva wa gari hilo la pili, ndipo walipoamua kuzuia gari hilo na kumbana dereva aliyewaonesha dawa na kudai kuwa huwa wanazisafirisha kwenda kijijini.

Hamis aliiomba serikali kuwahakikishia usalama wa maisha yao kwani sasa wanapata vitisho baada ya kufichuo uovu huo. Amesema kutokana na uwepo wa serikali makini ya rais Magufuli, wameamua kujitoa muhanga ili kuokoa jamii kwa kuamini kuwa serikali itawahakikishia usalama wao.

Kaimu mganga mkuu wa manispaa ya Shinyanga Dkt Mhana Raphael akitoa taarifa kwa waandishi wa habari leo
Kaimu Mganga Mkuu wa manispaa ya Shinyanga Dkt Mhana Raphael amesema ni kweli muuguzi huyo amekamatwa na dawa hizo ambazo hazina nembo ya MSD ingawa uchunguzi wa awali wamebaini kuwa ni dawa za kituo hicho.

‘Sisi kama uongozi wa Mkoa na Halmashauri kwenye usimamizi wa dawa hatufanyi utani. Tunaviachia vyombo vya dola vifanye kazi yake kwa maana ya kuchunguza ili kubaini ukweli ili hatua stahiki zichukuliwe,”ameongeza Dkt Raphael.

Kamanda wa jeshi la polisi mkoa wa Shinyanga Justus Kamugisha amethibitisha kukamatwa kwa muuguzi huyo na kusema bado wanaendelea kumhoji juu ya hilo.
  • Imeandikwa na Kadama Malunde via Malunde1 blog

Kauli ya Mtatiro kuhusu Mkuu wa Wilaya, Makonda kuwasweka rumande maafisa ardhiNdugu zangu, muda huu nimeona kwenye mitandao kadhaa watu wakifurahia hatua ya Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni ndugu yetu Paul Makonda kutoa amri (ambayo imetekelezwa) ya kuwaweka ndani wataalam wa ardhi ambao walishindwa kufika eneo la kazi kwa wakati.

Binafsi siungi mkono kitendo cha watendaji kuchelewa maeneo ya kazi lakini zaidi ya yote siungi mkono kitendo cha mkuu wa wilaya kuwaweka ndani watendaji kwa kosa la kuchelewa kazini.

Madhara ya kuwachekea wakuu wa wilaya pale wanapotoa amri zinazokiuka haki za msingi za wafanyakazi ni makubwa mno. Huko nyuma tulizoea mambo haya kufanywa na wakuu wa wilaya enzi za Nyerere, hatutarajii hadi leo wakuu hawa kuendesha wilaya zao kwa amri.

Ni muhimu sana masuala ya kazi yaendeshwe kwa sheria na kanuni za kazi na huyo mtu anayefurahia mamlaka (haramu) ya ma DC kuweka watu ndani atakuwa na matatizo makubwa. Watu wanapaswa kuwekwa ndani kama wamefanya makosa kwa mujibu wa sheria na si kama apendavyo DC.

Tuijenge nchi yetu kimfumo zaidi kuliko ki-amri, nchi zinazoendeshwa kwa amri amri huwa hazifiki kokote, kama tutashindwa kujijenga kimfumo katika miaka hii mitano tukategemea kuendesha nchi kwa amri, matamko na mikwara - ikifika 2020 tutaulizana nini kilifanyika na sote tutabaki kusimulia matamko lukuki yaliyotolewa.

Nimalizie tena kwa kuwakumbusha kuwa "Afrika itajengwa na mifumo imara, watu imara hawawezi kuijenga Afrika maana siku moja watakufa, na kama watakufa bila kuacha mifumo imara - yale yote waliyoyafanya yatapotea haraka ".

Ndugu yetu DC, Paul Makonda, tujengeeni mfumo imara utakaofanya wafanyakazi wote kuwa kazini kwa wakati, (msijijenge ninyi) watu imara na amri lukuki!

Mtatiro J.


Kauli ya Ikulu kuhusu taarifa za "ratiba ya maadhimisho ya Siku ya Uhuru"


Agizo la Katibu Mkuu kwa niaba ya Rais kuhusu dawa za Serikali

Mkurugenzi wa Bohari ya Dawa (MSD), Cosmas Mwaifwani ameagizwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dkt. Donan Mmbando kwa niaba ya Rais, kuhakikisha kuwa dawa zote za Serikali zinakuwa na utambulisho maalum ili endapo zitakutwa katika maduka ya dawa binafsi, hatua za kisheria zichukuliwe dhidi ya wamiliki wa maduka hayo.

MSD inahudumia hospitali za Serikali tu na vituo vyake na kamwe dawa ambazo husambazwa na MSD hazipaswi kuuzwa kwa wamiliki wa maduka ya dawa binafsi. Hili ni katazo la kisheria, hivyo ni kosa la jinai kwa dawa za Serikali kukutwa kwa wamiliki wa maduka ya dawa binafsi. 

Mkurugenzi huyo alikiri kuwa ni kweli wapo watumishi wasio waaminifi ambao wamekuwa wakiiba dawa hizo.

Aidha, Mkurugenzi huyo aliongezea kuwa, MSD itafungua maduka ya dawa makubwa karibu na mahospitali ya Serikali ili kurahisisha zaidi upatikanaji wa madawa kwa urahisi ikiwa ni sambamba na kusambaza madawa hayo kote nchini katika vituo vya afya kwa wakati, ili wananchi wote wenye uhitaji wa madawa waweze kupata bila tabu yoyote ile.

Mkurugenzi huyo ametoa namba maalumu ya simu, ambayo haitatozwa gharama (bure) itakayobandikwa kwenye vituo vya afya na mahospitali yote ya serikali kwa dhumuni la kumwezesha mwananchi kutoa taarifa MSD endapo atapata taabu kupatiwa dawa.  

Maelezo ya Wizara kuhusu ugonjwa wa pamba "Fusarium Wilt Disease"

TAARIFA KUHUSU UGONJWA WA MNYAUKO FUSARI WA PAMBA NA MBEGU ZISIZOOTA


Serikali imewataka wachambuaji na wasambazaji wa mbegu za pamba kuacha kuwasambazia wakulima mbegu zilizozalishwa katika maeneo yaliyobainika kuwa na ugonjwa wa mnyauko fusari (Fusarium Wilt Disease). Kauli hiyo imetolewa leo na Mkurugenzi wa Huduma za Usimamizi, Bodi ya Pamba Tanzania, Bwana James Shimbe.

Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari, Bwana Shimbe amesema, ugonjwa wa mnyauko fusari unaweza kudhibitiwa ikiwa wakulima wa pamba watatumia mbegu bora kutoka kwa wasambazaji wanaotambulika na Bodi ya Pamba Tanzania.

Akizungumzia tatizo la kuenea kwa ugonjwa huo Bwana Shimbe amesema kwa kiasi fulani limetokana na baadhi ya wachambuaji wasio waaminifu kuendelea kusambaza mbegu za pamba za kupanda ambazo zinaweza kuwa zimetoka katika maeneo yaliyobainika kuwa na ugonjwa wa mnyauko fusari.

“Tulishatoa maelekezo kwa kuwataka wasambazaji wa mbegu za pamba za kupanda kutosambaza mbegu zilizozalishwa katika maeneo yenye ugonjwa.”

Hivyo tunaendelea kusisitiza kuwa wakulima wawe makini wanapo nunua mbegu kutoka kwa wasambazaji wasiotambulika na watoe taarifa haraka kwa Bodi wanapoona mbegu hizo hazioti ili hatua za haraka zichukuliwe za kupeleka mbegu zingine mbadala ili kuendana na msimu wa kilimo.

Aidha, Bwana Shimbe amewataka wachambuaji wa pamba ambao ndio wasambazaji wa mbegu kuacha mara moja kuwasambazia wakulima mbegu ambazo zimetoka kwenye maeneo yaliyobainika kuwa na ugonjwa na badala yake mbegu za pamba hizo zisindikwe kuzalisha mafuta ya kula kama walivyokuwa wameelekezwa na Bodi hapo awali.

“ Bodi ilishatoa maelekezo kwa wachambuaji wote wa pamba kote nchini, kutenga mbegu za pamba za kupanda msimu huu wa kilimo kutoka maeneo yaliyo salama kwa kuziwekea lebo ili kuzitofautisha na zile zinazotoka kwenye maeneo yaliyobainika kuwa na ugonjwa, ambapo zile zinazotoka katika maeneo yenye ugonjwa zisitumike kama mbegu za kupanda, bali zisindikwe kupata mafuta ya kula kama sehemu ya kudhibiti kusambaa kwa ugonjwa, na zile mbegu ambazo zimetoka kwenye maeneo yasiyo na ugonjwa zisambazwe kwa wakulima kwa ajili ya kupanda kwenye mashamba yao baada ya kufanyiwa majaribio ya uotaji (seed germination test) na taasisi inayohusika na udhibiti wa ubora wa mbegu (TOSCI)”

Aidha, mbegu zinazofaa kutumika kwa sasa ni UKM08 iliyofanyiwa utafiti na Kituo chetu cha Utafiti cha Ukiriguru, ambayo ubora wake umethibitishwa na Taasisi ya Kudhibiti Ubora wa Mbegu (TOSCI) na inauwezo wa kuhimili magonjwa pamoja na uzalishaji wenye tija zaidi. Mbegu hiyo itakuwa inaiondoa kwenye uzalishaji ile ya zamani ya UK 91 ambayo imepungua ubora wake. Katika msimu huu wa kilimo wa 2015/16 Mbegu ya UKM08 itaendelea kuzalishwa kwa wingi (seed multiplication) katika maeneo salama yasiyo na ugojwa wa mnyauko fusari katika mkoa wote wa Singida na wilaya ya Nzega na Igunga, mkoa wa Tabora.

Bwana Shimbe ametoa wito kwa wakulima na wadau wote wa pamba nchini kufuata kanuni za kilimo bora cha pamba ikiwa ni pamoja na kutumia mbegu bora za pamba. Aidha, baadhi ya mawakala wa ununuzi wa pamba mbegu na wakulima wenye tabia ya kuchanganya pamba mbegu na maji, mchanga, chumvi na kemikali zingine kama vile “mafuta ya kenge” kwa madai ya kuongeza uzito kwenye pamba yao waachane na tabia hiyo potofu, kwani kwa kufanya hivyo kunachangia kuoza kwa kiini cha mbegu na kuharibu ubora wake na hivyo kusababisha mbegu kutokuota.

Imetolewa:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali
Wizara ya Kilimo Chakula na Ushirika
Kilimo Complex
1 Mtaa wa Kilimo 15471

DAR ES SALAAM

Ombi la Jukwaa Huru la Wazalendo kwa Rais na Wabunge kuhusu kubana matumizi

Mwenyekiti wa Jukwaa hilo, Ally Salum Hapi akizungumza na Waandishi wa habari leo katika hoteli ya Travertine, Magomeni jijini Dar es Salaam akiwa na Katibu wake, Mtela Mwampamba (kulia)

JUKWAA HURU LA WAZALENDO

TAMKO LA JUKWAA KWA VYOMBO VYA HABARI

Ndugu Wanahabari,

Mbele yenu sisi tuliowaita hapa ni Jukwaa Huru la Wazalendo ambalo limeitisha mkutano huu ili kufikisha yale tuliyoyakusudia kuwaeleza umma wa watanzania.

Sote tunatambua kuwa nchi yetu imetoka katika uchaguzi mkuu ambao umetupatia viongozi wapya wa awamu ya tano ya uongozi wa taifa letu chini ya Dr. John Pombe Joseph Magufuli. Tunapenda kuwapongeza watanzania wote kwa uchaguzi wa amani na utulivu. Aidha kwakua ndio mara yetu ya kwanza kuzungumza nanyi tunapenda kuwapongeza wanahabari wote kwa kazi nzuri ambayo mmekua mkiifanya kabla, wakati na baada ya uchaguzi mkuu nchini. Tunawashukuru sana.

Mkutano wetu huu umebeba madhumuni makubwa mawili.

Kwanza ni kumpongeza Mh. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa hotuba yake aliyoitoa Bungeni siku ya ufunguzi wa Bunge la 11 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mnamo tarehe 19/11/2015. Tunaiunga mkono Hotuba yake ambayo kwa kweli ilikuwa imebeba Uzalendo, Ujasiri, dira ya kweli ya maendeleo ya taifa letu na muuelekeo mpya wa Serikali ya awamu ya tano. Mambo yote aliyozungumzia Mh. Rais yamebeba maslahi mapana ya nchi yetu na yanalenga kuijenga Tanzania mpya ambayo waasisi wa Taifa letu Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Abeid Amani Karume walikusudia kuijenga.

Pili, pamoja na mambo mengi yaliyogusiwa na hotuba ya Mh. Rais, eneo la kubana matumizi na kupunguza matumizi yasiyo ya lazima kwa Serikali ni moja katika mambo ambayo Jukwaa hili limeamua kuyaunga mkono kwa vitendo. Mh. Rais alitoa mchanganuo wa eneo moja tu la safari za nje na jinsi lilivyo ligharimu Taifa mabilioni ya shilingi na kuahidi kuwa serikali ya awamu ya tano chini ya uongozi wake itajikita katika kupunguza matumizi yasiyo ya lazima.

Aidha Mh. Rais ameanza kutekeleza kwa vitendo ahadi yake hiyo ya kupunguza matumizi yote yasiyo ya lazima Serikalini, ikiwemo hafla, warsha, makongamano na safari za nje.

Jukwaa Huru la Wazalendo, linatambua kuwa kwa miaka kadhaa mbunge wa Kigoma Mjini Mh. Zitto Kabwe amekuwa na msimamo wa kutokupokea posho za kitako tangu akiwa mbunge wa Kigoma Kaskazini katika Bunge la 10. Pamoja na Mh. Zitto, Jukwaa pia limepokea taarifa za baadhi ya wabunge wa Bunge la 11 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania walioamua kuunga mkono juhudi za Mh. Rais za kupunguza matumizi yasiyo ya lazima serikalini kwa kukataa hadharani kupokea posho ya kitako ya mbunge (sitting allowance).

Mnamo tarehe 23/11/2015, mbunge wa Singida Magharibi (CCM) Mh. Elibariki Imanuel Kingu alimwandikia barua Katibu wa Bunge akieleza msimamo wake wa kukataa kulipwa posho ya kitako ya Bunge (sitting allowance) katika kipindi chote cha miaka mitano (2015 - 2020). Huyu anakuwa ni mbunge wa pili baada ya Mh. Zitto Kabwe kutoka hadharani na kukataa posho ambazo msingi wake ni unyonyaji wa wanyonge na ubadhirifu wa kodi za wananchi.

Jukwaa linapenda kumpongeza Mh. Kingu Mbunge kwa ujasiri wake na Uzalendo kwa Taifa lake, uliomfanya kuunga mkono juhudi za Mh. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa vitendo.
Jukwaa linatambua ya kwamba, mapambano ambayo Mh. Kingu Mbunge ameyaanzisha ni makubwa, magumu na yanahitaji kuungwa mkono na watanzania wote wanaoipenda nchi yao bila kujali itikadi za vyama. Tunafahamu, wapo baadhi ya wabunge wabinafsi na wasio na huruma na wanyonge wa Taifa letu ambao hawajafurahishwa na hatua hii ya wabunge kama Zitto na Kingu ya kukataa posho ya kitako. Baadhi ya wabunge wameanza kumpigia simu na kumtumia jumbe (sms) za vitisho mh. Elibariki Kingu (MB) na wengine wakibeza kuwa anatafuta cheo.

Jukwaa linalaani hatua za wabunge hao wanaopinga nia njema ya Mh. Elibariki Kingu na Mh. Zitto Kabwe kwa uamuzi wao wa kukataa posho za kinyonyaji na hivyo basi, Jukwaa linawaomba wananchi wote majimboni, kuwataka wabunge wao waliowachagua kueleza misimamo yao hadharani juu ya kuunga mkono hatua ya kukataa posho kama njia ya kupunguza matumizi ya Serikali yasiyo ya lazima.

Jukwaa linafahamu ya kwamba, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ndiye mwenye mamlaka ya mwisho ya kuidhinisha masharti ya kazi za kibunge na stahiki wanazopaswa kulipwa katika kazi hiyo.

Kwa heshima na unyenyekevu mkubwa, tunamuomba na kumshauri Mh. Rais John Pombe Magufuli atakapokuwa anaidhinisha masharti na stahiki hizo, atusaidie kuifuta kabisa posho ya kitako ya wabunge (sitting allowance).

Aidha, Jukwaa linamuomba mh. Rais kuzipitia na kutoa agizo la kufutwa kwa posho zote zisizo za lazima zinazolipwa kwa watumishi wa umma wa kada mbalimbali yakiwemo mashirika ya umma.

Jukwaa letu linatoa wito kwa wabunge wote bila kujali vyama vyao, kuungana na Mh. Kingu(MB) na Mh. Zitto(MB) katika kukataa malipo ya posho ya kitako ili kupunguza mzigo mkubwa ambao Serikali inaubeba kuhudumia wabunge. Fedha hizi ni vyema zielekezwe katika kutatua kero za wananchi vijijini kama vile ukosefu wa maji, madawati, vitanda vya Hospitali n.k.

Tunasisitiza kwamba, Ubunge ni Utumishi,na wala sio Utukufu. Kazi ya Mbunge ni kuwawakilisha wananchi wake na si kuwanyonya. Tufike mahali kama Taifa tuwe na nidhamu ya matumizi ya kodi za wananchi na mgawanyo sawa wa keki ya Taifa. Kuendelea kulipana posho hizo ni ishara ya unyonyaji, dhuluma na kuongeza pengo kati ya wenye nacho na wasionacho nchini. Jambo hili linakuza chuki na hasira miongoni mwa wananchi wa hali ya kawaida dhidi ya viongozi wao na serikali kwa ujumla.

Tunawaahidi kuwa Jukwaa litaendeleza harakati (movement) na vuguvugu hili kwa kuanzia na Bunge kwasababu ndio wawakilishi wa wananchi. Tutaendelea kupaza sauti zetu ili wabunge wengi zaidi Wazalendo wajitokeze na kukataaa posho hizi. Tunajua kuwa wapo miongoni mwao wabunge wazalendo ambao wataguswa na wito huu na kuuunga mkono hadharani.

Aidha tutaendelea kuwasemea kwa wananchi wabunge ambao bado hawataki kukataa posho hizi bila kujali vyama vyao. Tunawaomba wananchi kote nchini kutuunga mkono katika harakati hizi ili tuweze kuokoa mabilioni ya shilingi yanayopotea kila Bunge linapokaa Dodoma kupitia posho ya kitako (sitting allowance).
Ahsanteni sana.

ALLY SALUM HAPI - MWENYEKITI (0714 193161
MTELA MWAMPAMBA - KATIBU (0755 178927)