Yule jamaa Magufuli alimzungumzia kazuia maji, jumba lake limebomolewa na DAWASCO


Na Eleuteri Mangi-MAELEZO

Zoezi la kubomoa nyumba na majengo yaliyoingia ndani ya ya hifadhi ya miundombinu ya bomba la maji kutoka Ruvu Chini limeendelea mwishoni mwa wiki ili kuhakikiha kunakuwepo usalama wa bomba hilo na kuwapatia wakazi wa jiji la Dar es salaam na maeneo ya mkoa wa Pwani uhakika wa maji ifikapo Februari, 2016.

Bomo bomoa hiyo ya mwishoni mwa wiki ilihusisha maeneo ya Salasala ambapo baadhi ya nyumba, karakana na uzio vyote viljengwa ndani ya hifadhi ya miundombinu hiyo ya maji.

Akizungumzia ubomoaji huo, Mkurugenzi wa Usimamizi na Ufundi wa Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka Dar es Salaam (DAWASA), Romanus Mwang'ingo alisema kuwa ni wajibu wa wakazi wa maeneo hayo kuvunja sehemu za makazi yao yaliyoingia ndani ya hifadhi ya mradi kwa hiyari ama nyumba hizo kuvunjwa baada ya kukaidi agizo la kubomoa ili kupisha ujenzi wa bomba la maji kutoka Ruvu Chini hadi jijini Dar es salaam.

“Umbali sahihi unaopaswa wakazi hao kujenga makazi yao kutoka lilipo bomba la maji ni mita 15 kila upande ambapo hatua hiyo inapelekea kuwa jumla ya mita 30 ya umbali unaotakiwa ili kuhakikisha kunakuwepo na usalama na kuruhusu matengenezo mengine tofauti na hali ya awali ambayo huwezi hata kufanya kazi maana bomba limepita ndani ya uzio na makazi ya watu ambayo ni hatari kwa usalama wa maisha yao na mali zao” alisema Mwang'ingo.

Vile vile Mwang’ingo alizitaja changamoto zilizochangia kuchelewesha kukamilika kwa mradi huo kwa wakati ni kuwepo kwa kesi zilizofunguliwa na wananchi kuzuia ufanisi wa kazi hiyo ambapo kulikuwa na kesi 17 katika mahakama mbalimbali katika maeneo hayo ikiwemo mahakama ya ardhi.

Kwa mujibu wa Mwang’ingo hadi sasa DAWASA imeshinda kesi 13 na kupewa haki ya kutumia njia hiyo kukamilisha upanuzi wa mradi na zimebaki kesi nne ambazo bado zipo mahamani na zimefikia hatua mbalimbali kulingana na taratibu za kimahakama.

Kwa upande wake mkazi wa Salasala Mhandisi Josephat Nakapange ambaye sehemu ya nyumba yake pamoja na uzio vipo ndani ya hifadhi hiyo ya bomba la maji kutoka Ruvu Chini hadi Dar es salaam alisema kuwa yeye hana tatizo wala ugomvi na mradi huo, wamepokea maelekezo na wanayafanyia kazi.
“Hivi sasa ninavyoongea mafundi wapo kwenye eneo langu wanaendelea na zoezi la kutoa mabati na baadaye kuvunja kuta zilizo ndani ya umbali unaotakiwa kuachwa wazi kwa ajili ya mradi wa bomba la maji” alisema Josephat.

Aidha, Josephat aliongeza kuwa ni vema ziwekwe alama katika maeneo yote yanayotakiwa kuachwa wazi ambayo yapo ndani ya hifadhi ya mradi ili kuepusha usumbufu na gharama zisizo za lazima kwa wakazi ulipopita mradi huo.
Maeneo yaliyohusishwa na ubomoaji huo mwishoni mwa wiki ni pamoja na Bunju, Bondeni, Boko, Tegeta, Mbezi Intacheki, na Mbezi Tangibovu ili kuruhusu kukamilisha ujenzi wa bomba hilo la maji kutoka Ruvu Chini ha jijini Dar es salaam.


Kazi ya kubomoa baadhi ya nyumba ikiendelea mwishoni mwa wiki eneo la Salasala jijii Dar es salaam ili kupisha ujenzi wa bomba la maji kutoka Ruvu Chini.

Tingatinga likisukuma na kung’oa miti na jengo eneo Salasala iliyo ndani ya hifadhi ya bomba la maji kutoka Ruvu Chini hadi jijini Dar es salaam jijii Dar es salaam.

likisukuma na kung’oa mnazi eneo Salasala ambao upo ndani ya hifadhi ya bomba la maji kutoka Ruvu Chini hadi jijini Dar es salaam jijii Dar es salaam.

Tingatinga likisukuma na kung’oa mnazi eneo Salasala ambao upo ndani ya hifadhi ya bomba la maji kutoka Ruvu Chini hadi jijini Dar es salaam jijii Dar es salaam.

Mafundi wakiendelea kubomoa nyumba iliyopo eneo la Salasala kwa hiyari ya mmiliki wa nyumba hiyo ili kupisha ujenzi wa bomba la maji kutoka Ruvu Chini.

Tingatinga likishushwa tayari kwa kazi ya bomobomoa eneo la Salasala jijii Dar es salaam ili kupisha ujenzi wa bomba la maji kutoka Ruvu Chini hadi jijini Dar es salaam.

Usafi wa mazingira waendelea katika soko la Mwana Kwerekwe, ZanzibarAskari wetu na mifagio yao


Kila akisikia jina la Rais analia...


Chahali: #Magufuli ni Tumerejeshewa Nyerere na Sokoine


Makala hii imechapishwa katika jarida la Raia Mwema toleo la wiki hii lililotoka tarehe 25/11/2015, lakini kwa sababu nisizoelewa tovuti ya jarida hilo haijawa-updated kwa wiki kadhaa sasa. Kwa vile makala ninazotuma gazetini hufanyiwa uhariri kabla ya kuchapishwa, yawezekana makala iliyopo gazetini ikawa na tofauti kidogo na hii.

MAKALA YA RAIA MWEMA TOLEO LA NOVEMBA 25, 2015

“Hotuba hii ya Rais Magufuli ni moja ya hotuba bora kabisa katika historia ya siasa za Tanzania.” Hili lilikuwa hitimisho langu katika mtandao wa kijamii wa Twitter mara baada ya Rais John Magufuli kumaliza kulihutubia Bunge wiki iliyopita, huko Dodoma.

Na kwa hakika watu kadhaa waliafikiana na hitimisho hilo. Kilichovutia wengi waliosikia hotuba hiyo, katika shughuli ya ufunguzi wa Bunge la 11, sio tu mpangilio wa hotuba yenyewe bali pia jinsi kila alilotamka lilivyoonyesha bayana kuwa lilitoka moyoni mwake kwa dhati kabisa.

Rais alianza hotuba yake hiyo kwa kuorodhesha matatizo mbalimbali aliyobaini wakati wa kampeni zake Urais ambapo alizunguka takriban Tanzania nzima. Alitoa uchambuzi wa kina wa matatizo hayo kabla ya kuelezea kwa undani ni kwa jinsi gani serikali yake itayashughulikia. Ilikuwa ni zaidi ya hotuba ya kisiasa, na pengine ingeweza kabisa kuwa mhadhara wa kitaaluma uliofanyika katika lugha nyepesi na ya kueleweka.

Moja ya vitu vilivyonivutia sana katika hotuba hiyo ni jinsi Rais Magufuli alivyoweza kutupatia jibu la swali ambalo kwa miaka kadhaa lilionekana kuwatatiza viongozi wetu mbalimbali: “Kwanini Tanzania ni masikini licha ya utajiri lukuki wa raslimali ilionao.” Alieleza bayana na kwa kirefu jinsi ufisadi, rushwa na uhalifu vinavyochangia kukwamisha maendeleo ya taifa letu. Kadhalika, alifafanua, kwa kutumia takwimu halisi, jinsi mabilioni ya fedha yalivyotumika visivyo kwa matumizi yasiyo muhimu na yaliyo nje ya uwezo wa taifa letu masikini.

Kwa hakika ilikuwa hotuba ya kihistoria iliyofunika kabisa utovu wa nidhamu wa hali ya juu ulioonyeshwa awali na wabunge wa upinzani ambao walitumia muda mwingi kabla ya hotuba hiyo kuzomea na baadaye kuamiriwa kutoka nje ya ukumbi huo.

Lakini kwa vile sio rahisi kumridhisha kila mtu, baadhi ya wenzetu waliosikiliza hotuba hiyo walidai kuwa eti “haina tofauti na hotuba nyingine kadhaa zilizokuwa nzuri kuzisikiliza lakini zikaishia kuwa maneno matamu tu.” Wengine walikwenda mbali zaidi na kudai kuwa hata mtangulizi wa Rais Magufuli, Rais Mstaafu Jakaya Kikwete naye pia alianza urais wake kwa hotuba za kutia moyo kama hizo lakini mengi ya aliyoahidi, hususan lile la ‘Maisha Bora kwa Kila Mtanzania,’ yaliishia kuwa ahadi tu.

Sikubaliani kabisa na wakosoaji hao, japo hoja zao zinaweza kuwa na mantiki kidogo. Ni kweli kwamba ukosefu wa hotuba za kuvutia si moja ya matatizo yanayoikabili nchi yetu. Wengi wa wanasiasa na viongozi wetu ni mahiri sana wa maneno lakini tatizo huwa katika kutafsiri maneno yao kuwa vitendo.

Wakosoaji hao hawapo sahihi kwa sababu, kama nilivyoeleza awali, hotuba hiyo ilikuwa ya kutoka moyoni.Ilikuwa hotuba ya kiongozi anayeguswa na yanayoisibu nchi yake, kiongozi mwenye uelewa wa changamoto zinazoukabili uongozi wake, na mwenye dhamira thabiti ya kukabiliana na changamoto hizo.

Kuna mbinu moja muhimu ya kubaini iwapo mtu anaongea ukweli au anahadaa, nayo ni kumwangalia usoni. Tangu kuanza kwa kampeni zake za urais na hadi wakati wa hotuba hiyo ya wiki iliyopita, uso wa Rais Magufuli wakati anaongea unaonyesha bayana kuwa kila neno linalotoka mdomoni mwake ni la dhati, linatoka moyoni na si sehemu ya porojo tulilozowea kutoka kwa wengi wa wanasiasa na viongozi wetu. Mtaalam yeyote wa kubaini ukweli na uongo hatoshindwa kuafikiana nami kuwa uthabiti wa kauli za Magufuli upo wazi kwa yeyete anayemwangalia usoni wakati anaongea.

Lakini pia, hotuba hiyo ilikuwa mwendelezo wa ishara nzuri zilizoanza kujitokeza siku moja tu tangu Rais Magufuli aingie ofisini, ambapo alifanya ziara ya kushtukiza Wizara ya Fedha, kabla ya kufanya ziara nyingine kama hiyo katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili. Na siku ya uzinduzi wa Bunge, alitukumbusha enzi za (Waziri Mkuu wa zamani) hayati Edward Sokoine, aliyesifika kwa uchungu wa mali za umma, baada ya kuamuru zaidi ya shilingi milioni 200 zilizochangwa kwa ajili ya hafla ya mchapalo ya sherehe za uzinduzi wa Bunge jipya zielekezwe kwenye ununuzi wa vitanda katika hospitali ya Muhimbili, na kiasi kidogo tu kitumike kwa ajili ya hafla hiyo.

Kimahesabu, chini ya wiki tatu tangu aingie madarakani, Rais Magufuli ameshaokoa jumla ya shilingi milioni 900 kutokana na hatua alizochukua dhidi ya matumizi yasiyo ya lazima. Kwa kasi hii, tuna kila sababu ya kutarajiwa kuiona nchi yetu ikipaa kiuchumi, na hatimaye Watanzania kunufaika na neema lukuki ambayo nchi yetu imejaaliwa kuwa nayo.

Sina shaka kuhusu uwezekano wa mafanikio ya hatua za Rais Magufuli huko serikalini. Licha ya kuwa na Waziri Mkuu mchapakazi mzoefu, Majaliwa Kassim Majaliwa, kuna kila dalili kuwa baraza la mawaziri ambalo hadi wakati ninaandaa makala hii lilikuwa halijatangazwa, litasheheni wachapakazi kama yeye. Kwahiyo, kazi ya kurejesha nidhamu serikalini, kupunguza matumizi yasiyoendana na umasikini wetu na kupambana na ufisadi ina dalili kubwa za mafanikio.

Eneo ambalo Rais Magufuli hawezi kufanikiwa peke yake pasipo ushirikiano wa Watanzania wote ni nje ya serikalini na huko ‘mtaani.’ Mara kadhaa nimekuwa nikisisitiza umuhimu wa wananchi kujenga kasumba ya kudai haki na stahili zao badala ya kuona haki/stahili hizo ni kama fadhila au upendeleo flani. Wenzetu huku Ughaibuni wamejenga desturi ya kutokubali huduma au bidhaa inayotolewa chini ya kiwango wanachostahili. Haki na stahili za mpokea huduma ni miongoni mwa vitu vinavyopewa umuhimu mkubwa huku tulipo.

Haitokuwa rahisi kwa Rais Magufuli au wasaidizi wake kwenda kila sehemu kuwezesha au kuharakiasha upatikanaji wa huduma. Jukumu hilo linapaswa kusaidiwa na wananchi wenyewe ambao mara nyingi ndio wahanga wakubwa wa huduma mbovu. Kadhalika, watoa huduma nje ya serikali wanapaswa kutambua kuwa hizi ni zama mpya, na asiyeweza kuendana na kasi ya Rais Magufuli na ajiweke kando.

Lakini mchango mkubwa zaidi wa wananchi wote unahitajika zaidi katika kupambana na ufisadi, rushwa na uhalifu mwingine nje ya serikali. Wakati Rais ameahidi kukabiliana na ‘mapapa’ wa uhalifu kama kwenye biashara hatari ya madawa ya kulevya, pasipo wananchi kumsaidia kwa kuwatenga wahusika na kuwaripoti - badala ya kuwasujudia na kuwapa majina ya heshima kama ‘wazungu wa unga’ au ‘mapedejee’ – basi tutamkwamisha, na nchi yetu itaendelea kuumizwa na vitendo hivyo viovu.

Kadhalika, ili kauli-mbiu ya ‘Hapa Ni Kazi Tu’ iweze kuleta matokeo kusudiwa na kuwa ya ufanisi ni muhimu kwa kila Mtanzania kuachana na dhana fyongo ya kusaka mafanikio kwa njia za mkato, turejee zama za Ujamaa na Kujitegemea ambapo waliokula bila kuvuja jasho tuliwaita ‘kupe.’ Sote tuchape kazi, tuache kufanya ‘ujanja ujanja,’ tuone fahari kuwa na shughuli halali badala ya kuamini kuwa ufisadi, rushwa, uhalifu,nk ndio njia rahisi na sahihi za kufikia mafanikio kwa haraka.

Baada ya kumpoteza Baba wa Taifa Marehemu Mwalimu Julius Nyerere aliyetujengea misingi imara ya taifa letu, japo sasa inamong’onyoka kwa kasi, na mzalendo wa daraja la kwanza, Marehemu Sokoine, sala/dua zetu katika wimbo wetu wa taifa katika maneno “Mungu Ibariki Tanzania…” zimesikika, na Mwenyezi Mungu ametuletea ‘Nyerere na Sokoine mpya’ kupitia kwa Rais wetu mpya Dkt Magufuli. Tusijiangushe wenyewe kwa kutotumia ipasavyo fursa hii adimu.

Nimalizie makala hii kwa wito ‘wa kitaalamu’ kwa ndugu zangu wa Idara ya Usalama wa Taifa, ambao pamoja na majukumu mengine, wana dhamana ya ulinzi wa Rais wetu na viongozi wengine wakuu kitaifa. Kama alivyosema mwenyewe, vita aliyoanzisha dhidi ya kila vitendo na kasumba zinazolikwaza taifa letu ni nzito na inawagusa watu wazito. Kwa vile yayumkinika kusema kuwa vitendo vya rushwa,ufisadi na uhalifu vimefikia hatua ya ‘kimafia,’ basi ni muhimu kuimarisha ulinzi wa Rais wetu (na viongozi wengine wanaopatiwa ulinzi) kwa sababu ‘tupo vitani.’

Simaanishi kuwa ulinzi uliopo una mapungufu lakini angalizo hili linazingatia ukweli kwamba ‘vita’ hiyo inagusa maslahi ya wengi, maslahi ya ‘kupe’ lukuki walioigeuza Tanzania yetu kuwa ni ‘shamba la bibi,’ la kuvuna wasichopanda, sambamba na wahalifu wanaoingiza, kuuza na kusafirisha madawa ya kulevya kana kwamba ni bidhaa iliyoidhinishwa na Shirika la Viwango la Taifa (TSB), majangili wanaoshindana kuua wanyamapori wetu na kusafirisha nyara za serikali, na wahalifu wengineo.

Rais Magufuli ameahidi kutotuangusha, basi nasi tusimwangushe.

Hapa Ni Kazi Tu!

Barua-pepe: [email protected]
Twitter: @chahali

Katuni: Naniliu alivyotua bandarini...


Mkuu wa Mkoa Kilimanjaro: "Sitaki kusikia likizo kwa DC, Wakurugenzi na Wakuu wa Idara"Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Amos Makalla amepiga marufuku likizo za Wakuu wa wilaya, Wakurugenzi na Wakuu wa Idara kwenye mkoa wake ili kutekeleza kwa vitendo hotuba na maagizo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk John Pombe Magufuli.

RC Makalla aliyasema hayo jana katika kikao cha kazi na wakuu wa wilaya, wakurugenzi wa halmashauri, wakuu wa idara wa halmashauri na Kamati ya Ulinzi na usalama ya mkoa huo kwa ajili ya kupeana mikakati ya majukumu ya kuwatumikia Wana Kilimanjaro na Watanzania kwa ujumla, ikiwa ni hatua nzuri ya kwenda na kasi ya Dk Magufuli.

Baadhi ya watendaji wa Mkoa Kilimanjaro wakimsikiliza kwa makini Mkuu wa Mkoa huo, Aamos Makalla alipozungumza nao jana. Katika kikao hicho, RC Makalla alipiga marufuku likizo kwa Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi na Wakuu wa Idara ili kujipanga na maagizo yaliyotolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk John Pombe Magufuli.

Alisema kuwa Dk Magufuli ameagiza mambo mengi mazuri na yenye kuhitaji utendaji uliotukuka, ikiwamo elimu bure, mikakati ya kubana matumizi, kupambana na maradhi mbalimbali, ugonjwa wa kipindupindu, usimamizi wa pembejeo na kuzuia pia matukio mbalimbali yenye kugharimu pesa, sanjari na mapambano ya dawa za kulevya na uwadijibikaji kazini.

“Hakuna muda wa kupoteza katika kufanyia kazi maagizo ya rais Magufuli, hivyo sote kwa pamoja tunapaswa kujipanga na kwenda na kasi ya serikali yetu ili kuhakikisha kwamba nchi yetu inapiga hatua kubwa kama yalivyokuwa makusudio yetu ya kuhakikisha watoto wanasoma bure, hivyo sitaki kusikia likizo kutoka kwa Ma DC, Wakurugenzi na Wakuu wa Idara katika Mkoa wetu wa Kilimanjaro. “Suala la kubana matumizi, pembejeo kwa wakulima, vita ya madawa ya kulevya na mengineyo yanapaswa kuanza sasa, huku tukihakikisha kwamba maadhimisho ya siku ya Uhuru yanajikita zaidi kwenye suala zima la usafi kuanzia kaya, mtaa au kijiji na kwingineko,” Alisema Makalla.

Katika hatua nyingine, RC Makalla alionyesha kukerwa na ugonjwa wa kipindu kipindu na kusema kuwa kamwe hataki kuona ugonjwa huo unaingia kwenye Mkoa wake wa Kilimanjaro, akiwataka wataalamu wa afya na watendaji wa serikali kujipanga kikamilifu.

Kwa mujibu wa Makalla, endapo watajipanga imara katika suala zima la usafi, usimamizi wa rasilimali na utendaji uliotukuka katika maeneo yao, Mkoa huo utazidi kupiga hatua kubwa kiuchumi, hivyo kufanikisha kwa vitendo dhamira kubwa ya Dk Magufuli ya kuwakwamua wananchi wake na Watanzania kwa ujumla. RC Makalla ni miongoni mwa viongozi wa juu wanaopambana kwenda na kasi ya Rais Magufuli, ikiwa ni siku chache tangu alipoapishwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, huku wananchi wengi wakionyesha kuwa na Imani kubwa na rais huyo wa awamu ya tano.

Ujumbe wa Katibu Mkuu Kiongozi kwa Watendaji Wakuu na Afisa Masuhuli


Waandishi wa habari wa gazeti la JamboLeo wakabidhiwa mifagioWaandishi wa habari wa gazeti la Jambo Leo, wakifurahia kupata fagio walizokabidhiwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Zahanati ya Mji Mwema Kigamboni, Dar es Salaam, Omary Kombe (kulia), katika hafla iliyofanyika katika chumba cha habari cha gazeti hilo, Dar es Salaam. 

Kombe ametoa msaada huo kuunga mkono maelekezo ya Rais Dk. John Magufuli ya kufuta sherehe za Sikukuu ya Uhuru ili wananchi washiriki siku hiyo kufanya usafi wa mazingira kwa lengo la kutokomeza ugonjwa wa kipindupindu nchini. (PICHA NA RICHARD MWAIKENDA)


Tumeshirikishwa taarifa hii na Richard Mwakienda (shukurani)

Walioahimshiwa TRA mikoani na Waziri Mkuu jana wasiamishwa kazi

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

WATUMISHI WENGINE WATATU WASIMAMISHWA KAZI TRA

Ni kuipsha uchunguzi wa tuhuma zinazowakabili

SERIKALI imewasimamisha kazi watumishi watatu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ambao jana iliamriwa kwamba watahamishiwa mikoani. Watumishi hao ni Bw. Anangisye Mtafya, Bw. Nsajigwa Mwandengele na Bw. Robert Nyoni.

Uamuzi huo umetolewa leo (Jumamosi, Novemba 28, 2015), na Waziri Mkuu Majaliwa Kassim Majaliwa ili kupisha uchunguzi zaidi wa tuhuma zinazowakabili. Kama ilivyo kwa wenzao sita waliosimamishwa kazi jana (akiwemo aliyekuwa Kamishna Mkuu), nao pia hawaruhusiwi kusafiri kwenda nje ya nchi hadi uchunguzi utakapokamilika.

“Kazi ya kuwachunguza ilianza jana ileile na sasa, tumeona hawa watu wanapaswa kuwa nje ya utumishi ili kupisha uchunguzi ufanyike kwa uhuru zaidi,” alisema Waziri Mkuu.

Pia Waziri Mkuu amemuagiza Kaimu Kamishna Mkuu wa TRA, Dkt. Philip Mpango atekeleze maagizo hayo kwa kuwaandikia barua watumishi hao.

Jana mchana, Waziri Mkuu alifanya ziara ya kushtukiza kwenye bandari ya Dar es Salaam akiwa na nia ya kukagua namna shughuli zinavyoendelea kwenye bandari hiyo hasa kwenye maeneo ya kupokelea mizigo kutoka nje ya nchi.

Katika kikao kilichofanyika bandarini hapo na kuhudhuriwa na baadhi ya viongozi wa Serikali, Waziri Mkuu aliamua kuwasimamisha kazi maafisa watano na TRA kutokana na ‘upotevu’ wa makontena 349 yenye thamani ya zaidi ya sh. bilioni 80/-.

Waziri Mkuu alisema upotevu huo unasababishwa na mchezo unaofanyika baina ya wafanyabiashara na watumishi wa TRA ambao wanaruhusu makontena kupita bila kulipiwa ushuru na hivyo kuikosesha Serikali mapato.

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
2 MTAA WA MAGOGONI,
S.L.P. 3021,
11410 DAR ES SALAAM
JUMAMOSI, NOVEMBA 28, 2015.