Mbowe: Anafungwa mikono Rais na Kamati Kuu ya Chama cha Mapinduzi


Taarifa nzima ya habari ChannelTEN, Jumanne, Desemba 15, 2015


Taka zilizokusanywa Desemba 9 zizolewe kabla ya Desemba 20

Waziri George Simbachawene akizungumza na wafanyakazi wa wizara hiyo mjini Dodoma
WAZIRI wa nchi ofisi ya Rais Tamisemi, Utumishi na Utawala Bora, George Simbachawene amewaagiza wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya na wakurungenzi wote wa halmashari nchini kuhakikisha wanazoa taka zote zilizokusanywa wakati wa siku ya uhuru kabla ya tarehe 20 mwezi huu.

Kauli hiyo aliitoa wakati alipokuwa akizungumza na wafanyakazi wa Wizara hiyo wakati wa kikao cha kumkaribisha katika ofisi ya TAMISEMI mjini Dodoma. 

Alisema kuwa hataki kuona hadi ifikapo tarehe 20 ya mwezi huu kuwa uchafu unaendelea kulalamikiwa: 

“Hadi ifikapo tarehe hiyo sitaki kusikia uchafu bado haujaondolewa katika maeneo ulipokusanywa toka Siku ya Uhuru, lakini pia unapoondolewa huo kuna uchafu mwingine unakuja hivyo basi watendaji wanaohusika wahakikishe kuwa wanaanda maeneo ya kuupeleka,”alisema Simbachawene. 

Naibu Waziri wa wizara hiyo Suleiman Jaffo, aliwataka watumishi wa TAMISEMI kubadilika katika utendaji wao wa zamani ili waweze kuongeza ukusanyaji wa mapato na kuweza kuboresha maisha ya wananchi.

Mvua inapobisha hodi Dar es Salaam miaka nenda, miaka rudi, yale yale...

Kunazi na pilipili doria (sisi tunaita 'ngueda')

Pilipili doria

Kunazi
Picha za matunda yote zimenukuliwa kutoka ZanziNews blog.

Tinga Tinga Arts Group na Bricoleur Holdings Co. Ltd zasaini mkataba wa kazi

Mkurugenzi wa Kampuni ya Bricoleur Holdings ya nchini Japan, Bi. Yu Shiran (katikati) akiongea na Waandishi wa Habari (hawapo pichani) kuhusu kushirikiana kufanya kazi za sanaa na Kikundi cha Sanaa cha Tingatinga, leo katika Ukumbi wa Idara ya Habari (MAELEZO). Kulia ni Mwenyekiti wa Kikundi cha Sanaa (Tingatinga), Bwana Zachi Chimwanda na kushoto ni Mkurugenzi pia wa Kampuni ya Bricoleur Holdings ya nchini Japan, Bwana Shoji Tsuchiya.
Na Tupokigwe Marco na Mwanahamisi Matasi

Chama cha Sanaa cha uchoraji picha maarufu kama Tinga Tinga kimetiliana saini Mkataba wa Makubaliano wa miaka mitano wa kufanya kazi kwa pamoja na Kampuni ya Bricoleur Holdings Co. Ltd ya nchini Japan utakaokiwezesha chama hicho kunufaika kwa kuuza kazi zake Kimataifa.

Akiongea leo wakati wa utiaji saini wa Mkataba huo, Mwenyekiti wa Chama cha Sanaa cha Tinga Tinga, Bwana Zachi Chimwanda ameeleza kuwa, utiaji saini wa Mkataba huo utakua chachu ya maendeleo katika kuwakomboa wasanii wachoraji katika kipato chao na kuboresha hali zao za kimaisha kwakuwa kazi zao sasa zitakuwa zikiuzwa ndani na nje ya nchi.

Kwa upande wake Katibu Mtendaji wa Baraza la Wasanii la Taifa (BASATA), Bwana Godfrey Mngereza alieleza kuwa Mkataba waliosaini kati ya Tinga Tinga na watu wa Bricoleur Holdings Co. Ltd utaimarisha kazi za Wasanii katika fani ya uchoraji ikiwemo kuongeza vipato vyao.

''Sanaa ni kazi lakini pia ni biashara, imefika wakati kwa wasanii kufaidika na jasho lao, kampuni hii watakua wakitafuta masoko kule Japan ili kazi hizi za wachoraji toka Tanzania ziweze kununuliwa hali ambayo itawaongezea kipato'', alisema Mngereza.

Aliongeza kuwa Mkataba uliosainiwa kati ya pande zote mbili umepitia taratibu zote za kiserikali na Taasisi zinazohusika na mambo ya sanaa na maslahi ya msanii na msanii yule aliyehusika katika kuchora picha fulani atanufaika na mkataba huo.

''Kwa msanii atakehusika binafsi na uchoraji picha mkataba utamwezesha kujua atanufaika vipi na kwa muda gani'', aliongeza Mngereza.Kwa upande wake Mkurugenzi wa Kampuni ya Bricoleur Holdings Co. Ltd, Bi. Yu Shiran ameeleza kuwa mpango huo wa Mkataba kati yao na Tingatinga una lengo la kukitangaza Chama hicho cha wachoraji wa Tanzania Kimataifa.

‘Kwa kutumia taarifa za kidijiti za Tingatinga tutaweza kushirikiana na watengenezaji mbalimbali wa bidhaa, na ili kulithibitisha hili, sisi na Tingatinga tumekuwa katika mjadala wa takriban mwaka mzima sasa’, alisema Bi. Shiran.

Tinga Tinga Arts Group lilianzishwa nchini Tanzanja na Edward Saidi Tingatinga ambaye alifariki mwaka 1972 ambapo kwa sasa kundi hilo lipo maeneo ya Oysterbay jijini Dar es Salaam kikijihusisha na sanaa ya uchoraji.

Baadhi ya watuhumiwa kesi TRA watimiza masharti ya dhamana bilioni 2.1/=

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam imemuachia kwa dhamana aliyekuwa Kamishna wa Forodha na Ushuru wa Mamlaka ya Mapato (TRA), Tiagi Masamaki na vigogo wengine wawili wa mamlaka hiyo, baada ya Kamishna huyo kuwasilisha hati ya mali isiyohamishika ya Sh bilioni 2.12 kama moja ya masharti ya dhamana.

Hakimu Mkazi Mfawidhi wa mahakama hiyo, Cyprian Mkeha aliwaachia washitakiwa hao kwa dhamana baada ya kutimiza masharti, yaliyotolewa katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam.

Katika kesi ya msingi, washitakiwa wanane ambao ni wafanyakazi wa TRA pamoja na wafanyakazi wa Bandari Kavu (ICD) ya Kampuni ya Azam, wanakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi, kwa kula njama za kudanganya na kuisababishia serikali hasara ya Sh bilioni 12.7.

Washitakiwa walioachiwa kwa dhamana ni Masamaki, Mkuu wa Kituo cha Huduma kwa Wateja TRA, Habibu Mponezya na Meneja Udhibiti wa Forodha na Ufuatiliaji, Burton Mponezya, ambao waliwasilisha ombi la dhamana katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam.

Waliachiwa baada ya kutimiza masharti ya kila mmoja kutoa mahakamani hati ya mali isiyohamishika yenye thamani ya Sh bilioni mbili, kuwa na wadhamini wawili wa kuaminika waliosaini hati ya dhamana ya Sh milioni 20 na mmoja kati ya wadhamini hao ni mfanyakazi wa serikali.

Katika dhamana yake, Masamaki aliwasilisha hati ya mali isiyohamishika yenye thamani ya Sh bilioni 2.129 mali hiyo ipo katika eneo la Mikocheni na inamilikiwa na Sospeter Machunge ambaye aliwasilisha mahakamani hati ya kukubali, hati yake itumike kumdhamini Masamaki.

Habibu aliwasilisha hati mbili za mali zenye thamani ya Sh bilioni 2.129, ambapo hati moja ya mali yenye thamani ya Sh milioni 574 inamilikiwa na Salum Said, na nyingine ya Sh bilioni 1.55 inamilikiwa na Wakifu Abdallah.

Hata hivyo, Wakili wa Serikali Mwandamizi, alipinga hati hizo kupokelewa na kuhoji Abdallah amepata wapi mali zenye thamani hiyo akiwa na miaka 30. Abdallah alidai amerithi kutoka kwa baba yake na pia anajishughulisha na biashara ndogo ndogo.

Burton aliwasilisha hati mbili za mali zenye thamani ya Sh bilioni 2.3, moja ya mali yenye thamani ya Sh milioni 373 inayomilikiwa na Kampuni ya Theokratia Ltd, pamoja na hati ya mali yenye thamani ya Sh bilioni 1.6 inayomilikiwa na Sabah Salum, pia waliwasilisha hati za tathmini ya mali hizo.

Wamiliki wa mali hizo walikuwepo mahakamani na kuridhia hati zao zitumike kuwadhamini washtakiwa hao, pia washtakiwa hao walikuwa na wadhamini wawili ambao kila mdhamini mmoja alisaini hati ya Sh milioni 20 na kuwasilisha hati zao za kusafiria mahakamani.

Katika masharti mengine yaliyotolewa na Jaji Winifrida Korosso wa Mahakama Kuu, washtakiwa hao hawaruhusiwi kusafiri nje ya Dar es Salaam bila kibali cha Mahakama ya Kisutu na pia kila baada ya wiki mbili wanatakiwa kuripoti ofisi ya Mkuu wa Upelelezi Mkoa.

Baada ya washitakiwa hao, wanaowakilishwa na Wakili Alex Mgongolwa na Majura Magafu, kukamilisha masharti ya dhamana, Wakili Msigwa alidai upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika na kuomba tarehe nyingine ya kutajwa.

Hakimu Mkeha alisema washtakiwa watakuwa nje kwa dhamana na washitakiwa wengine, wataendelea kuwa rumande hadi Desemba 30, mwaka huu itakapotajwa tena.

Desemba 4, mwaka huu, Masamaki na wenzake walipandishwa kizimbani katika Mahakama ya Kisutu, wakikabiliwa na mashitaka ya kula njama ya kudanganya na kuisababishia serikali hasara ya Sh bilioni 12.7.

Wanadaiwa katika tarehe tofauti kati ya Juni mosi na Novemba 17, mwaka huu sehemu isiyofahamika, walikula njama za kuidanganya Serikali kuhusu Sh bilioni 12.7, kwa madai kuwa makontena 329 yaliyokuwa kwenye Bandari Kavu ya Azam (AICD), yametolewa baada ya kodi zote kufanyika, jambo ambalo si kweli.

Katika mashtaka mengine, inadaiwa kati ya siku hizo, kwa kushindwa kutekeleza majukumu yao vizuri, washtakiwa waliisababishia Serikali hasara ya Sh bilioni 12.7. Washtakiwa hawakuruhusiwa kujibu mashtaka na kurudishwa rumande kwa kuwa Mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo.
Watuhumiwa watatu wa uhujumu uchumi wakisindikizwa na Polisi wakitoka mahama kuu ya Tanzania jijini Dar es Salaam leo mara baada ya kupewa dhamana. Picha na Avila Kakingo/Michuzi blog


Kwa mujibu wa ITV

Mahakama kuu ya Tanzania imeridhia dhamana kwa washitakiwa watatu wa mamlaka ya mapato Tanzania TRA wanaokabiliwa na mashitaka ya kutoa makontena 329 bandarini bila kulipiwa kodi na kuisababishia serikali hasara ya shilingi bilioni 12.7.

Mbunge wa jimbo la Ubungo,(Chadema) Saed Kubenea akiwa na wanachama wa chama cha Demokrasia na Maendeleo, leo mara baada ya kusomewa shitaka lililokuwa likimkabiri katika mahakama ya Kisutu jijini Dar es Salaam leo.
Maamuzi hayo ya mahakama kuu ya Tanzania yametokana na ombi lililowakilishwa mahakamani hapo na washtakiwa watatu wakiongozwa aliyekuwa Kamishina wa Forodha wa TRA Bw Tiagi Masamaki. Jaji wa mahakama hiyo Bi Wilfrida Koroso, alisema dhamana kwa washitakiwa hao watatu iko wazi kama watatimiza masharti sita yakiwemo ya kulipa hundi ya shilingi bilioni 2.6 kila mmoja huku pia wakitakiwa kuwasilisha hati zao za kusafiri na kutakiwa kuwa na wadhamini watakaokuwa na uwezo wa kusaini hundi ya shilingi milioni 20 kila mmoja.


Katika hatua nyingine mbunge wa jimbo la Ubungo Mhe. Saed Kubenea amepandishwa kizimbani katika mahakama ya hakimu mkazi Kisutu Dar es Salaam akikabiliwa na shitaka la kutumia lugha ya matusi kinyume na sheria.

Akisoma shitaka mbele ya hakimu mkazi wa mahakama hiyo Thomas Simba, mwendesha mashitaka wa serikali Timon Vitalis ameiambia mahakama kuwa mnamo Desemba 14 mwaka huu katika eneo la EPZ mtuhumiwa huyo alitumia lugha ya matusi "we kibaka, we mjinga, mpumbavu, cheo chenyewe umepewa" maneno yaliyokuwa yakimlenga mkuu wa wilaya ya Kinondoni, ambapo kwa mujibu wa mwendesha mashitaka huyo amesema maneno hayo yangeweza kuhatarisha amani ikiwa ni kwa mujibu wa kifungu namba 89 (i) A cha kanuni ya adhabu sura namba 16 ya mwaka 2002 ambapo hata hivyo mshitaka huyo alikana shitaka hilo.

Mtuhumiwa huyo alikuwa akitetewa na jopo la mawakili watano wakiongozwa na wakili Peter Kibatala ambapo hata hivyo baada ya kukidhi vigezo vya dhamana aliachiwa nje.