Katuni: Kauli mbiu za viongozi wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki


Katuni za Danni Mzena za "Politiks"


Kauli ya Zitto kuhusu uteuzi wa Prof. Muhongo


Waliosema Ufisadi ni Mfumo ndio wanasema leo Prof. Muhongo hafai kuwa Waziri sababu ya Tegeta Escrow. Sijui lini mahakama ilimhukumu Muhongo! Sijui lini Muhongo kawa Mfumo. Tujifunze kuweka akiba.

Prof. Sospeter Muhongo alikuwa Waziri wa Nishati na Madini wakati wa sakata la ‪#‎TegetaEscrow‬. Kamati ya Bunge ilipendekeza na Bunge kuazimia kuwa Muhongo avuliwe madaraka yake ya Uwaziri. Prof. Muhongo alijiuzulu. Akafanyiwa uchunguzi na Kamishna wa Maadili kutamka kuwa hakukutwa na kosa la kimaadili. Unajengaje hoja kuwa hana haki ya kuteuliwa kuwa Waziri? Keshaadhibiwa kwa kosa la awali, kwa kujiuzulu. Sheria ipi inasema hana haki ya kuteuliwa tena?

Niliongoza Kamati ya PAC. Nina uhakika Waziri muhongo kwenye sakata lile alishauriwa vibaya na kujikuta anatetea ubadhirifu. Lile nifunzo kubwa kwake na ninavyomuona sasa hatarudia tena makosa yale. Kuna mambo ya msingi lazima afanye sasa

1) Azuie kuanzia sasa malipo ya 'capacity charges' kwa kampuni ya kitapeli ya IPTL na atumie sheria kutwaa mitambo ya IPTL na kumilikisha TANESCO

2) Amtake Waziri wa Mambo ya Ndani na Jeshi la Polisi kumkamata mara moja anayejiita mmiliki wa IPTL na afunguliwe mashtaka ya utapeli, wizi wa udanganyifu na uhujumu uchumi; huyo mmiliki na washirika wake ambao ni raia wa Tanzania

3) Amtake Gavana wa Benki Kuu na FIU kuichukulia hatua za kisheria Benki ya Stanbic ikiwemo kupiga faini ya kurejesha fedha zote zilizokua kwenye akaunti ya Tegeta Escrow.

Hizo ndio hoja za msingi na sio uteuzi wa Prof. Muhongo. Mwenye ushahidi dhidi ya Muhongo si aende Mahakamani? Tuache siasa za porojo porojo

Kauli ya ACT-Wazalendo kuhusu yanayoendelea Burundi


CHAMA CHA ACT-WAZALENDO KINAITAKA TANZANIA NA JUMUIYA YA AFRIKA MASHARIKI KUKOMESHA MAUAJI NCHINI BURUNDI


1. Chama cha ACT-Wazalendo kinasikitishwa sana na maujai yanayoendelea nchini Burundi na hasa Mji Mkuu wa nchi hiyo Bujumbura. Hali hii ya mauaji imesababishwa kwa kiasi kikubwa na uamuzi wa Rais wa sasa wa nchi hiyo Ndugu Piere Nkurunzinza kuendelea kugombea na hatimaye kuchaguliwa kuwa Rais wa nchi hiyo katika mazingira yaliyovunja demokrasia na utawala bora.

2. Tangu machafuko nchini Burundi yaanze zaidi ya watu 100 wameshauawa kufikia wiki hii na wengine kadhaa kujeruhiwa. Aidha, wimbi la wakimbizi kutoka Burundi linarudi kwa kasi na wengi wao wakikimbilia nchini Tanzania.

3. Bahati mbaya sana Jumuiya ya Kimataifa na hasa Jumuiya ya Afrika Mashariki ambapo Burundi ni mwanachama, haikuchukua hatua za maana za kuzuia kuchafuka kwa utawala wa kidemokrasia na utawala wa sheria nchini Burundi, na wala haichukui hatua stahiki kuzuia mauaji yanayoendelea. Hii ni kinyume kabisa na Mkataba unaounda Jumuiya ya Afrika Mashariki ambao unatoa kipaumbele cha juu kulinda uhai na haki za raia katika Jumuiya hiyo

4. Kutokana na hali ya kisiasa na usalama nchini Burundi, na kwa kuzingatia nafasi ya kihistoria ya Tanzania katika kutafuta na kufanikisha Mkataba wa Amani nchini Burundi, na kwa kuzingatia nafasi yake katika Jumuiya ya Afrika Mashariki na Umoja wa Afrika, tunaitaka serikali ya Tanzania, kwa hali kubwa ya dharura, ichukue hatua zifuatazo:

a. Iitake serikali ya Jamhuri ya Burundi kukomesha mara moja maujai yanayoendelea nchini humo na kuwahakikishia raia wa nchi hiyo usalama

b. Iitake serikali ya Jamhuri ya Burundi kuitisha mkutano wa wadau wote wa siasa na utawala nchini humo ili kujadili mustakabali wa nchi hiyo kisiasa na kijamii, ikiwemo uwezekano wa kuunda serikali ya Umoja wa Kitaifa itakayosimamia Katiba ya Burundi kuelekea uchaguzi wa kidemokrasia

c. Itumie nafasi yake katika Jumuiya ya Afrika Mashariki kuitakaJumuiya hiyo kuzuia machafuko nchini Burundi na kuhakikisha kwamba utawala wa demokrasia na utawala wa sheria unazingatiwa nchini humo

5. Chama cha ACT-Wazalendo kinasisitiza kuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki itakosa uhali wa kuendelea kuwepo kwake kama itaendelea kuwa Jumuiya ya viongozi wa nchi zinazounda Jumuiya hiyo na kishindwa kusimamia haki za kuishi na haki za kiraia za wananchi wa Afrika Mashariki.

Venance Msebo
Katibu wa Kamati ya Mambo ya Nje
ACT-Wazalendo
Jumatano, 16 Desemba 2015

Katuni: Sijui lini anakuja huku...


Abiria 367 wanusurika kifo baada ya boti ya Royal kuungua moto karibu na PembaRais Magufuli asema "ole" akieleza fedha za kutuma mashuleni kwa ajili ya elimu bure zimepatikana


Twaweza to launch report on Citizens views on security and radicalization

Waziri Mwigulu, "Nahitaji majawabu, siyo majibu"

Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi Mhe. Mwigulu Nchemba akisalimiana na watumishi wa wizara yake mapema hii leo alipowasili ofisini kwaajili ya kuzungumza na watumishi wa wizara hiyo.

Walimu Wakuu kufukuzwa kazi - Naibu W. Elimu

Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Mhandisi Stella Manyanya (wa pili kulia) akikata utepe na Makamu wa Rais wa Kampuni ya Total, Jean-Christian Bergeron (wa tatu kulia) wakati wa hafla ya kukabidhi madawati 1000 yaliyotolewa kama msaada na Total kwa ajili ya Shule 10 za mikoa ya Dar es Salaam na Pwani. Makabidhiano hayo yalifanyika wilayani Bagamoyo jana. Kulia ni Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA), Prof. Naomi Katunzi (kulia) na Kushoto anayeshuhudia ni mwanafunzi wa shule ya msingi Nianjema ya Bagamoyo, Ramadhani Issa. (Picha na Francis Dande)
SERIKALI imesema itawafukuza kazi walimu wakuu wa shule zote za msingi ambazo wanafunzi wake watashindwa kusoma, kuandika na kuhesabu kabla ya kuingia darasa la tatu.

Tamko hilo la serikali lilitolewa mjini Bagamoyo Mkoa wa Pwani na Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, mhandisi Stella Manyanya wakati akipokea msaada wa madawati 1,000 kutoka kwa kampuni ya mafuta ya Total yatakayosambazwa katika shule 10 za mikoaya Dar es Salaam na Pwani.

Akizungumza wakati wa hafla hiyo, naibu waziri huyo alisema ili kuwa na elimu bora katika hatua za awali lazima wanafunzi kuanzia ngazi ya chekechea wajue kuhesabu, kusoma na kuandika kwa viwango vyao huku akisisitiza kwamba kabla ya mwanafunzi kuingia darasa la tatu lazima kusoma, kuandika, kuhesabu na kuelewa anachokifanya.

“Ni fedhaha unamkuta mwanafunzi wa darasa la tatu hajui kusoma kwa nini? Lazima kuna uzembe mahali sasa hili ni agizo na utekelezaji wake unaanza… tutapita huko kwenye mashule kukagua hili, tukibaini wapo wanafunzi hawajui hizi KKK hatuna sababu ya kuendelea na huyo mwalimu
mkuu.
“…Tutamwambia atupishe akafanye shughuli nyingine, lazima walimu wawajibike,” alisema Injinia Manyanya baada ya kuwapa karatasi wasome na kuhesabu baadhi ya watoto wa shule za msingi waliokuwepo kwenye hafla hiyo na kusema elimu bora ni pamoja na kujua kusoma, kuandika, kuhesabu na kuelewa.

Naibu Waziri huyo pia aliipongeza Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA), kwa kuhamasisha wadau mbalimbali kuchangia katika elimu hasa suala la madawati, ujenzi wa mabweni huku akisema taifa lina upungufu wa madawati 1,349,090 ambayo gharama yake ni sh bilioni 182.1 hivyo aliwaomba wadau wa elimu kuchangia.

Akizungumza kabla ya kukabidhi madawati hayo, Makamu wa rais wa Kampuni ya Mafuta ya Total, Jean-Christian Bergeron alisema gharama ya madawati hayo ni sh milioni 78 huku akibainisha kwamba kwa miaka mitatu kampuni yake imechangia madawati 3,000 yenye tahamani ya sh milioni 234 ambapo wanafunzi 9,000 wamenufaika nayo.
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Mhandisi Stella Manyanya (kushoto) akiwa amekaa katika madawati yaliyotolewa kama msaada na Kampuni ya Total. Katikati ni Makamu wa Rais wa Kampuni ya Total, Jean-Christian Bergeron, madawati 1000 yaliyotolewa na kampuni hiyo yakiwa na thamani ya shs. milioni 78 kwa ajili ya Shule 10 za mikoa ya Dar es Salaam na Pwani. Wa pili kushoto ni mwanafunzi wa shule ya msingi Nianjema ya Bagamoyo, Ramadhani Issa.


 

Bashe 'awapiga tafu' wafanyabiashara wadogo wa Nzega


Leo Mbunge wa jimbo la Nzega mkoani Tabora, Hussein Bashe alizuru Stendi Kuu ya Mabasi na kukutana na vikundi tofauti vya akina mama wa wafanyabiashara ndogondogo.

Ofisi ya Mbunge imewataka kuanzisha umoja wao haraka na kuwawezesha na fedha za kufungilia akaunti benki kisha kupewa elimu ya ujasiriamali ili waweze kujiendesha kwa faida.


Taarifa ya kusimamishwa kazi Mhandisi Mussa Natty


Taarifa ya Rais Magufuli ya kutengua na kuteua Mkurugenzi Mkuu TAKUKURUTanzania na Japan zasaini mkataba wa shilingi bilioni 210 za umeme

Katibu Mkuu Wizara ya Fedha Dkt. Servacius Likwelile na Balozi wa Japani nchini Bw. Masaharu Yoshida wakibadilishana hati ya mkataba wa mkopo wa Shilingi Bilioni 210 kwa ajili ya mradi wa Umeme kati ya Tanzania na Kenya.

SERIKALI ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imesaini mkataba na Serikali ya Japani kiasi cha shilingi bilioni 210/= kwa ajili ya maendeleo ya mradi wa njia ya kusafirishia umeme kati ya Tanzania na Kenya ambao utasaidia upatikanaji wa umeme wa kutosha.

Mkataba huo wa masharti nafuu ulisaininiwa na Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango na Mlipaji Mkuu wa Serikali Dkt. Servacius Likwelile na Balozi wa Japani nchini Tanzania Bw. Masaharu Yoshida jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kusaini mkataba huo Dkt. Likwelile alisema kuwa fedha hizo zitaelekezwa katika kusambaza nyaya za umeme zenye KV400, na urefu wa kilometa 414.5 kati ya Singida na Namanga kupitia Babati na Arusha.

Alisema kuwa kukamilika kwa mradi huo kutachochea maendeleo ya jamii na uchumi nchini kwa kuleta muungano wa kibiashara katika nchi za Afrika Mashariki.

Naye Balozi wa Japani nchini Tanzania Bw. Masaharu Yoshida alisema kuwa mkopo huo utafanikisha kusambaza nyanya za umeme zenye urefu wa takribani kilometa 508 kati ya Tanzania na Kenya ambapo Tanzania itasambaza kilometa 415 wakati Kenya itakuwa na kilometa 93.

Japani imekuwa ikisaidia Tanzania katika miradi ya umeme kwa muda mrefu, miradi ambayo tayari imekamilika ni pamoja na usambazaji umeme Zanzibar, mradi wa usambazaji nyaya za umeme mkoani Kilimanjaro na mradi wa kutengeneza nyaya mpya za umeme jijini Dar es Saalam.

IMETOLEWA NA WIZARA YA FEDHA
KITENGO CHA MAWASILIANO

16/12/2015.


Katibu Mkuu Wizara ya Fedha Dkt.Servacius Likwelile na Balozi wa Japani nchini Bw.Masaharu Yoshida wakisaini mkataba wa mkopo. Nyuma yao kushoto ni Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini Eng. Omar Chambo, kulia ni Waziri wa Mambo ya Nje wa Japani Seiji Kihara wakishuhudia tukio hilo katika ukumbi wa Wizara ya Fedha Jijini Dares Salaam.

Katibu Mkuu Wizara ya Fedha Dkt.Servacius Likwelile akitoa ufafanuzi wa matumizi ya mkopo wa bilioni 210 baada ya kusaini mkataba wa mkopo huo katika ukumbi wa Wizara ya Fedha jijini Dar es Salaam.

Muhimbili yafunga mashine nyingine ya kipimo cha CT scan

HOSPITALI ya Taifa Muhimbili (MNH) inafunga mashine nyingine ya CT- Scan ambayo inategemewa kuanza kutoa huduma kesho mchana.

"Hivyo kufikia jumatatu ijayo Hospitali hiyo itakuwa na mashine mbili za CT-Scan ambazo zitakuwa zinafanya kazi hatua ambayo itaboresha zaidi utoaji wa huduma kwa wagonjwa ambao wanatakiwa kupimwa kwa kutumia mashine hiyo," amesema Waziri wa Afya , Maendeleo ya Jamii, Jinsia , Watoto na Wazee, Ummy Mwalimu.

Waziri Mwalimu ameyasema hayo leo wakati alipotembelea mashine za CT-Scan na MRI katika hospitali hiyo.

Pamoja na mambo mengine Waziri huyo ameshauri ripoti za wagonjwa wanapimwa kwa kwa kutumia mashine hizo zitolewe haraka ili kuwapunguzia gharama za kukaa muda mrefu wagonjwa wanaotoka katika mikoa mingine.

Akizungumzia kuhusu mashine ya CT-Scan na MRI ambazo zimeharibika Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa MHN Profesa Lawrence Mseru amesema juhudi za kutengeneza mashine hizo zinafanyika na kwamba kifaa cha CT- Scan kilichoharibika kitaingia leo usiku wakati spea ya MRI imeshawasili na matengenezo yanaendelea.

Mashine ya CT-Scan hupima wastani wa wagonjwa 40 hadi 60 kwa saa 24 wakati MRI hupima wagonjwa 20 kwa siku.