Makampuni 27 ya tanzanite yaliyobainika kukwepa ushuru yajiandae

Mwenyekiti wa Kamati za Ulinzi na Usalama za mikoa ya Arusha, Kilimanjaro na Manyara na Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro, Amos Makalla (aliyesimama) akizungumza na wajumbe wa Kamati za Ulinzi na Usalama za mikoa ya Arusha, Kilimanjaro na Manyara (hawapo pichani) ambazo zimeamua kufanya kazi kwa pamoja ili kudhibiti utoroshaji wa madini ya Tanzanite nje ya nchi. Wa kwanza kushoto ni Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini, Mhandisi Omar Chambo, wa kwanza kulia ni Katibu Tawala mkoa wa Manyara, Eliakim Maswi na wa pili kutoka kulia ni Mkuu wa mkoa wa Arusha, Daud Ntibenda.

KAMPUNI 27 za kununua na kuuza madini ya tanzanite mkoani Arusha zilizosajiliwa, zinachunguzwa na serikali baada ya kubainika kukwepa kodi ya zaidi ya Sh bilioni 150 na ziko hatarini kufutiwa leseni.

Akizungumza na gazeti hili (HABARILEO) kwa njia ya simu, Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mikoa mitatu ya Arusha, Kilimanjaro na Manyara, Amos Makalla alisema uchunguzi wa awali umegundua wafanyabiashara hao sio waaminifu katika kufanya biashara zao za madini kwani wamekwepa kulipa mabilioni ya kodi serikalini.

Makalla ambaye ni Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro alisema katika uchunguzi wao na vikao vyao vya Desemba 10 na Desemba 17, mwaka huu, kamati hiyo maalumu ilibaini mambo mengi makubwa juu ya udanganyifu na wizi mkubwa unaofanywa na wafanyabiashara wa tanzanite katika kukwepa kodi.

Alisema katika kufanya upekuzi wa kina wenye kujiridhisha, walibaini kuwa tayari kampuni 27 zimekwepa kulipa kodi hiyo ya Serikali ya zaidi ya Sh bilioni 150 tangu mwaka 2013/14. Kutokana na hali hiyo, alisema wametoa muda kwa kampuni za kununua na kuuza madini, madalali na wachimbaji kujisalimisha kwa kulipa kodi hadi Januari 5, mwakani vinginevyo serikali itachukua hatua kali za kisheria.

Alisema baadhi ya wafanyabiashara wakubwa wa tanzanite, madalali na wachimbaji wa madini hayo zaidi ya 5,000 wa Arusha, Manyara na Kilimanjaro sio waaminifu katika nyaraka zao za mapato na matumizi ya kila siku.

Kwa mujibu wa Makalla, katika nyaraka zao zinaonesha kutumia kiasi kikubwa cha fedha (returns) kila siku, lakini hawaoneshi kulipa kodi hata pale wanapopata madini na kutilia shaka nyaraka hizo.

Alisema kamati imejiridhisha na hali halisi ya ukwepaji kodi unaofanywa na wafanyabiashara wa tanzanite ambao wamekuwa wakifanya Mirerani (kunakochimbwa madini hayo pekee yanayopatikana Tanzania) kama shamba la bibi la kuvuna bila ya kulipa kodi sasa mwisho wa wafanyabiashara hao umefika.

“Nataka kukuambia kuwa kutatokeo mtikisiko mkubwa sana ambao haujawahi kutokea katika miaka mingi hapa nchini hususan hawa wafanyabiashara wa tanzanite kwani wamefanya Mirerani ni shamba la bibi la kuvuna mabilioni ya fedha bila ya kulipa kodi,” alisema Makalla na kuongeza: “Wakati wa wafanyabiashara wa tanzanite kukwepa kulipa kodi umekwisha, wanapaswa kujisalimisha wenyewe kwa kulipa kodi vinginevyo rungu la dola litawasaka walipo.”

Akizungumzia wageni kufanya kazi na kujaa migodini, alizitaka kampuni zote ziwe kubwa ama ndogo kuwaondoa wafanyakazi wote wasio na kibali kabla ya operesheni haijaanza baada ya Januari 5, mwakani.

Alisikitishwa kuona kazi zinazopaswa kufanywa na Watanzania zinafanywa na raia wa nje wakiwamo kutoka Kenya na bara Asia, zikiwamo za ulinzi migodini.


Tanzanite iliyokamatwa KIA yafikia Dola za Marekani 1,207,990


Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini Mhandisi Omar Chambo (wa kwanza kulia) akiangalia moja ya mashine zinazotumika katika shughuli za uchimbaji madini katika eneo la Mirelani mkoani Manyara wakati alipotembelea eneo hilo mara baada ya kumaliza kikao kikao chake na Kamati za Ulinzi na Usalama za mikoa ya Arusha, Kilimanjaro na Manyara ambazo zimeamua kufanya kazi kwa pamoja ili kudhibiti utoroshaji wa madini ya Tanzanite.
Na Teresia Mhagama na Asteria Muhozya

Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini, Mhandisi Omar Chambo ameeleza kuwa madini aina ya Tanzanite yaliyokamatwa yakitoroshwa nje ya nchi bila kuwa na vibali tarehe 15 Desemba, 2015 kupitia uwanja wa ndege wa Kilimanjaro (KIA) yamefikia thamani ya Dola za Marekani 1,207,990.

Katibu Mkuu alisema hayo jijini Arusha wakati wa kikao chake na Kamati za Ulinzi na Usalama za mikoa ya Arusha, Kilimanjaro na Manyara ambazo zimeamua kufanya kazi kwa pamoja ili kudhibiti utoroshaji wa madini ya Tanzanite na kufuatilia kwa karibu shughuli za uchimbaji na biashara ya madini hayo ili yanufaishe taifa.

Katibu Mkuu alisema kuwa Tanzanite hiyo ghafi yenye uzito wa gramu 2,015.59 ilikuwa ikitoroshwa na raia wa India, Jain Anurag aliyekuwa akitaka kuelekea mji wa Jaipur kwa kutumia shirika la ndege la Qatar.

“Nataka niwaeleze watanzania wanaoshirikiana na raia wa kigeni kutorosha Tanzanite kuwa wajiepushe na biashara hii haramu kwani hatua kali zitaendelea kuchukuliwa dhidi yao na hatuna mzaha katika hili,” alisema Mhandisi Chambo.

Alieleza kuwa madini hayo yaliyokamatwa yameshataifishwa kama ambavyo sheria na kanuni za madini zinavyoelekeza na kwamba zoezi hilo la ukamataji watorosha madini hufanywa na Wizara ya Nishati na Madini kupitia Wakala wake wa Ukaguzi wa Madini (TMAA) kwa kushirikina na Taasisi nyingine kama Mamlaka ya Viwanja vya Ndege, Jeshi la Polisi, Idara ya Usalama wa Taifa, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Idara ya Uhamiaji.

Aidha alieleza kuwa serikali itafuta leseni za wafanyabiashara wa madini watakaobainika kutorosha rasilimali hiyo nje ya nchi ikiwemo kuwakamata wachimbaji na wafanyabiashara wanaokwepa kulipa kodi stahiki kwa serikali.

“Ili kudhibiti utoroshaji madini unaofanywa na wafanyabiashara wenye leseni na wasio na leseni, wazawa na wasio wazawa, tumeshajipanga kwa kushirikiana na Kamati za Ulinzi na Usalama za mikoa mitatu ya Manyara, Kilimanjaro na Arusha ili kudhibiti hali hii na Tanzania ibaki kama kinara katika uzalishaji na uuzaji wa madini haya na sio nchi nyingine,” alisema Mhandisi Chambo.

Kuhusu wachimbaji wadogo nchini, alisema kuwa serikali itaendelea kugawa maeneo ya uchimbaji madini kwa wachimbaji hao ikiwa ni pamoja na utoaji ruzuku, uagizaji wa zana kama baruti na utoaji wa mafunzo huku akitoa angalizo kuwa wachimbaji hao wanapaswa kuwa waaminifu na kuhakikisha kuwa wanalipa kodi stahiki serikalini badala ya kusubiri kuchukuliwa hatua za kisheria.

Wakati huohuo Mwenyekiti wa Kamati za Ulinzi na Usalama za mikoa ya Arusha, Kilimanjaro na Manyara na Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro, Amos Makalla ametoa masaa 24 kwa raia wa kigeni wote wanaojihusisha na biashara ya madini ya Tanzanite na madini mengine kinyume cha sheria kuondoka nchini mara moja na watakaokaidi agizo hilo watachukuliwa hatua kali za kisheria.

Agizo hilo alilitoa baada ya Kamati hiyo kubaini kwamba uwepo wa wageni mbalimbali kutoka nje ya nchi hususani Kenya, Sri Lanka, Nepal na India ambao hujihusisha na biashara ya Tanzanite bila kuwa na leseni zinazowaruhusu kufanya hivyo na hatimaye hutorosha madini hayo kwenda nje ya nchi.

“Madini haya yanauzwa kama njugu hivyo tumeona kwamba sisi Kamati za Ulinzi na Usalama za mikoa hii mitatu tukishirikiana kuimarisha ulinzi tutakomesha suala hili, tunataka kuona watu watu wanaouza madini ni wale wenye leseni tu, na wachimbaji na wafanyabiashara wahakikishe wanalipa kodi stahiki kwani kuanzia tarehe Tano Januari operesheni ya kuwakamata itaanza,” alisema Makalla.

Vilevile alieleza kuwa wafanyakazi wa kigeni waliopo katika mgodi wa Tanzanite One unaomilikuwa na kampuni ya Sky Associates kwa kushirikiana na serikali ambao hawana vibali vya kufanya kazi na wale wenye vibali vya kufanya kazi ambazo zingeweza kufanywa na watanzania waondoke mgodini hapo.

“Mchango wa madini katika Pato la Taifa bado hauridhishi na sisi tunafanya kila jitihada ili Tanzanite hii ambayo inachimbwa Tanzania peke yake ifaidishe nchi, kila mwananchi anao wajibu wa kuhakikisha hili linafanikiwa, wadau wa madini wana wajibu wa kuhakikisha kwamba wanalipa kodi stahiki na kutoa taarifa za hujuma zozote zinazofanyika ambazo baadhi ya wazawa wanashirikiana na wageni kuiibia nchi rasilimali hii muhimu,” alisema Makalla.


Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini Mhandisi Omar Chambo (wa pili kulia) akitembelea baadhi ya vitalu vya uchimbaji madini ya Tanzanite katika eneo la Mirelani mkoani Manyara mara baada ya kumaliza kikao kikao chake na Kamati za Ulinzi na Usalama za mikoa ya Arusha, Kilimanjaro na Manyara ambazo zimeamua kufanya kazi kwa pamoja ili kudhibiti utoroshaji wa madini ya Tanzanite.Kulia kwake ni Afisa Madini Mkazi katika Ofisi ya Madini Mirelani, Mhandisi Henry Mditi.

Makamishna Wasaidizi wa Madini,Wizara ya Nishati na Madini, kutoka kulia ni Julius Sarota (Wachimbaji Wadogo), Latifa Mtoro (Uthaminishaji madini), Salim Salim (Uchumi na Biashara) pamoja na Mkurugenzi wa Sheria, Justus Mulokozi (wa kwanza kushoto) wakiwa katika kikao kilichojumuisha Kamati za Ulinzi na Usalama za mikoa ya Arusha, Kilimanjaro na Manyara (hawapo pichani) ambazo zimeamua kufanya kazi kwa pamoja ili kudhibiti utoroshaji wa madini ya Tanzanite nje ya nchi.

Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini Mhandisi Omar Chambo (wa kwanza kulia) akizungumza na baadhi ya wajumbe wa Kamati za Ulinzi na Usalama za mikoa ya Arusha, Kilimanjaro na Manyara ambazo zimeamua kufanya kazi kwa pamoja ili kudhibiti utoroshaji wa madini ya Tanzanite nje ya nchi.

Afisa Madini Mkazi katika Ofisi ya Madini Mirelani, Mhandisi Henry Mditi akitoa taarifa ya kazi zinazofanywa na Ofisi hiyo iliyopo katika wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara.Wanaosikiliza ni Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini, Mhandisi Omar Chambo (wa pili kushoto), Wa kwanza kushoto ni Kaimu Kamishna wa Madini, Mhandisi Ally Samaje. Wengine katika picha ni Kamishna Msaidizi wa Madini sehemu ya Uthaminishaji Madini, Latifa Mtoro (wa kwanza kulia) na wa pili kulia ni Mkurugenzi wa Taasisi ya Uunganishaji na Ushirikishi Wadau katika Tasnia ya Uziduaji (EISF), Catherine Lyombe.

Ripoti ya wataalamu waliokokotoa "ada elekezi shule binafsi" yakabidhiwa

TUME ya wataalamu waliokuwa wanakusanya maoni ya wadau wa elimu na kukokotoa ada elekezi kwa shule za msingi na sekondari zisizo za Serikali, wamemaliza kazi yao na tayari wamekabidhi ripoti hiyo kwa Serikali.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Profesa Sifuni Mchome alilithibitishia gazeti hili mwishoni mwa wiki kukamilika kwa kazi hiyo na sasa kinachofuata ni uchambuzi wa ripoti pamoja na kuangalia miongozo ya Serikali kabla ya ada elekezi kutangazwa na kuanza kutumika kwa majaribio mwakani Januari.

Wataalamu hao walipewa kazi na Serikali kuandaa ada elekezi baada ya kupata maoni ya wadau mbalimbali wa elimu wakiwemo wazazi, wananchi, wamiliki wa shule binafsi, walimu, asasi zisizokuwa za kiserikali, taasisi mbalimbali za umma na wadau wengine ambao wanaweza kusaidia katika ukokotoaji huo wa ada.

Katika ukokotoaji huo, wizara inaandaa mchanganuo wa gharama za kumsomesha mwanafunzi kuanzia elimu ya awali, darasa la kwanza hadi kidato cha sita kwa nia ya kutoa ada hiyo elekezi ambazo zitaendana na huduma itolewayo kwa shule zisizo za Serikali.

Alisema shule zitakazoteuliwa kuanza kutumika kwa ada hizo zitatangazwa pia na wizara hiyo baada ya kukutana na wamiliki wa shule hizo na kufanya nao mazungumzo.

Alisema majaribio hayo yatafanyika katika baadhi ya shule Tanzania nzima na sio katika baadhi ya mikoa tu.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na waliofika kumpokea baada ya kuwasili kijijini kwake Nndagala wilayni Luangwa kwa mapumziko mafupi Desemba 20, 2015. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

SERIKALI imekwishatenga kiasi cha sh. bilioni 137 kwa ajili ya kugharamia utoaji wa elimu ya bure kuanzia Januari hadi Juni, mwakani.

Kauli hiyo imetolewa jana jioni (Jumapili, Desemba 20, 2015) na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa wakati akizungumza na mamia ya wananchi waliofika kumsikiliza kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye uwanja wa uwanja wa mikutano wa Likangala wilayani Ruangwa, mkoani Lindi.

“Kazi ya utumbuaji majipu imezaa matunda kwani tumeweza kupata fedha za kugahrimia elimu ya bure ambayo iliahidiwa na Mheshimiwa Rais John Pombe Magufuli wakati wa kampeni. Fedha hiyo tunayo, na tumeshaanza kuisambaza kwa sababu tunataka shule zikifunguliwa Januari, 2016 watoto waanze kufaidika,” alisema huku akishangiliwa.

“Atakayezigusa fedha hizi na kuzitumia vibaya ni lazima tutamtumbua tu! Tumeshawapa maelekezo Wakurugenzi wa Halmashauri pamoja na Maafisa Elimu wao na kuwaonya kuhusu matumizi ya fedha hizo,” alisema.

“Hatuhitaji mwanafunzi achangishwe hela ya mitihani, na zile shilingi 10,000/- kwa ajili ya wanafunzi wanaosoma Sekondari nazo pia tutazipeleka. Na huu ni mpango wa dharura ambao haukuwemo katika bajeti ya mwaka 2015/2016, kwa hiyo tutalazimika kuziombea kibali,” alisema.

Waziri Mkuu Majaliwa alisema Serikali imekwishafanya hesabu za kubaini kiasi kinachohitajika kwa ajili ya milo ya watoto shuleni kwa wale walioko bweni na wale wa kutwa. Hesabu tunazo na tumebaini kuwa tutazimudu,” alisema huku akishangiliwa.“Serikali ilitoa ahadi kwa wananchi na sisi tumedhamiria kuzitekeleza. Tuliahidi elimu bure nasi tutaitekeleza,” alisema.

Naye Waziri wa Habari, Utamaduni, Wasanii na Michezo, Bw. Nape Nnauye amewataka madiwani wa jimbo la Ruangwa kuhakikisha wanamsaidia Waziri Mkuu Majaliwa kusimamia kazi za jimboni ili aweze kuwa huru kutekeleza majukumu ya kitaifa.

“Madiwani wa jimbo hili msaidieni Waziri Mkuu kusimamia shughuli za maendeleo ili wakati yeye anaendelea kutekeleza majukumu ya kitaifa, ya jimbo naye yawe shwari. Msaidieni kusimamia fedha za umma ziende kwenye miradi iliyokusudiwa ili wakati akitumbua majipu huko kwingine na huku pia yasiote,” aliongeza.

Kubenea aanika mkataba unaoonesha Coco Beach iliuzwa kabla ya Natty kuanza kazi Kinondoni


WAKATI Serikali ikimsimamisha kazi aliyekuwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni, Mhandisi Mussa Natty, kwa madai kuwa pamoja na mambo mengine alihusika kuuza ufukwe wa Coco Beach, sakata hilo limevaa sura mpya baada ya Mbunge wa Ubungo, Saed Kubenea na Diwani wa Kata ya Ubungo, Boniface Jacob, kuibuka na kutoa mktaba unaaonyesha kuwa eneo hilo liliuzwa kabla ya Mhandisi huyo kuanza kazi Kinondoni.

Mbunge huyo na Diwani ambao wote wanatoka Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), jana waliwaeleza waandishi wa habari kuwa, Natty kawajibishwa kwa sababu za kisiasa ikiwemo kutenda haki katika Uchaguzi Mkuu uliopita.

Katika uchaguzi huo, majimbo ya Wilaya ya Kinondoni yote yalichukuliwa na vyama vinaunda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), jambo ambalo viongozi hao walisema Natty alitakiwa kutangaza washindi kuwa ni wagombea wa CCM.

Akielezea suala hilo, Diwani wa Ubungo, Boniface Jacob, alisema tangu kumalizika kwa uchaguzi wameshuhudia wakurugenzi mbalimbali wa halmashauri ambazo wapinzani wameshinda wakishughulikiwa kwa mgongo wa kutumbua majipu.

“Nafsi zetu zinatusuta endapo tukikaa kimya huku tunaona wakurugenzi wa halmashauri wanashughulikiwa kwasababu walikataa kutekeleza maagizo haramu kipindi cha uchaguzi ikiwemo Kinondoni na wengine wa Mbeya, Iringa na Mtwara.

“Kama kuna ufisadi umetokea hatutamtetea mtu na kama kuna mtu tunaona anaonewa hatutakaa kimya na hili la Natty tunamwomba Rais John Magufuli aunde tume huru ambayo haitahusisha TAMISEMI wala Wizara ya Ardhi akiwemo Lukuvi (Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi), kwa sababu wana masilahi katika suala hilo,” alisema Jacob.

Alisema anashangazwa na tuhuma zilizotangazwa na Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Jumanne Sagini ya kumsimamisha kazi Natty.

Katika tangazo lake, SSagini alidai kuwa Natty anatuhumiwa kwa usimamizi mbaya wa ujenzi wa barabara, ukosefu wa uadilifu katika ubinafsishaji wa ufukwe wa Coco na malalamiko ya wananchi juu ya viwanja katika eneo la Kinondoni.

“Ukiangalia suala la barabara kitabu cha makabidhiano ya halamashauri cha mwaka 2010 kinaonesha mikataba yote ya barabara hizo, Natty aliingia kazini akaikuta mikataba ya barabara imekwishasainiwa na wakurugenzi waliomtangulia akiwemo Ndunguru (Raphael Ndunguru 2009-2011) na Fwema (Fortinatus Fwema 2011-2013).

“Ndunguru ndiye aliyeleta miradi ya lami nyepesi ambazo zinagharimu milioni 500 kwa kilometa moja baada ya kutoa hoja kuwa barabara za vumbi zinagharimu milioni 300 na mvua zikinyesha zinaharibika upesi hivyo bora ziwekwe lami nyepesi na ziwe zinafanyiwa ukarabati pale zinapoharibika.

“Hapo Natty anahusika vipi ikiwa waliomtangulia ndio walioidhinisha kiwango cha barabara na walijua lazima ziwe zinaharibika baada ya muda fulani,” alisema Jacob.

Kuhusu tuhuma ya malalamiko ya wananchi kuhusu viwanja alisema migogoro ya ardhi ilikuwepo tangu zamani na imeendelea kuwepo nchi nzima, hivyo madai hayo hayana mashiko.

Mkataba wa uuzwaji wa fukwe

Kwa upande wake Mbunge wa Ubungo, Saed Kubenea, alieleza namna ubinafsishwaji wa Coco beach ulivyofanyika ambapo alimtetea Natty na kusema kuwa mchakato wa kuuzwa kwa ufukwe huo ulianza muda mrefu kabla ya mkurugenzi huyo kushika wadhifa huo.

Kubenea alionesha mkataba wa makubaliano kati ya Baraza la Manispaa ya Kinondoni na Q- Consult Limited kampuni inayomilikiwa na mfanyabiashara Yusuph Manji ambaye ndiye mkurugenzi mtendaji wa kampuni hiyo.

Mktaba huo ulisainiwa Desemba 21, mwaka 2007 ambapo kwa upande wa Manispaa ya Kinondoni ulisainiwa na Naibu Meya wa wakati huo, Julian Bujugo na Mkurugenzi wa Manispaa ambaye alikuwa ni Noel Mahyenga huku upande wa Q-Consult ukisainiwa na S. Sampatihkumar na B. N. Arvind wote wakiwa wakurugenzi katika kampuni hiyo.Waziri Kitwanga akiri kupokea orodha ya majina ya askari waliogushi vyeti

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga akitoa majumuisho kwa waandishi wa habari mara baada ya kumaliza ziara ya kutembelea Magereza ya Mkoa wa Dar es Salaam. Katika ziara yake hiyo Waziri Kitwanga aliambatana na Waziri wa Sheria na Katiba, Dkt. Harrison Mwakyembe (katikati). Kulia ni Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza, CGP John Minja. (picha: Wizara)
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga, amepokea orodha ya majina ya askari waliogushi vyeti vya masomo na taaluma ambao walivitumia kuomba kazi.

Aliyasema hayo wakati akizungumza na Nipashe jijini Dar es Salaam jana, mara baada ya kutembelea kambi za mahabusu zilizoko Segerea, Ukonga na Keko.

Alisema katika orodha hiyo aliyokabidhiwa juzi wamo askari ambao walishafukuzwa kazi na wengine bado wanaendelea na kazi kama kawaida.

Waziri alisema atatoa orodha hiyo kesho Jumatatu na kuahidi kwamba watakaofukuzwa hawataachwa hivi hivi.

Waziri Kitwanga alisema hatua zaidi zitachukuliwa dhidi askari hao ikiwa ni pamoja na kufungulia kesi za kugushi nyaraka muhimu.

“Kugushi nyaraka hizi ni kosa na tunataka hawa wawe mfano kwa wengine wenye tabia kama hizi, serikali yetu ya awamu hii sio ile ya awali, hivyo sheria itafuata mkondo wake,”alisema Kitwanga.

Hata hivyo, Waziri Kitwanga alisema hajajua idadi kamili ya askari waliomo kwenye orodha aliyokabidhiwa lakini aliahidi kuwa kesho wote wanaohusika kwenye kadhia hiyo watawekwa hadharani.

Kwa upande wake, Waziri wa Katiba na Sheri, Dk Harrison Mwakyembe, ambaye aliambatana na Waziri Kitwanga kwenye ziara hiyo, aliwaonya watu wenye tabia ya kufanya kazi kwa mazoea.

Aliwataka watumishi wanaojihusisha na ubadhirifu wa fedha za umma kuacha mara moja kwa sababu serikali ya awamu ya tano haitawavumilia.

Alisema wamebaini ongezeko kubwa la mahabusu katika magereza wakati kesi zao nyingi hazisikilizwi kwa wakati.

Alisema changamoto nyingine ni uhaba wa nyumba za askari na aliahidi kuwa serikali itajenga nyumba 900.

“Tuna muda mfupi tangu tuingie ofisini changamoto hizi tunazichukua na tutazifanyia kazi na baada ya wiki moja tutarudi hapa tena kuangalia tumefanikiwa wapi na wapi bado,”alisema Dk. Mwakyembe.

Mawaziri Kitwanga na Dk Mwakyembe wazuru magereza makuu


Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga (kushoto) akisalimiana na Kamshina Jenerali wa Jeshi la Magereza,. John Minja wakati alipokuwa anawasili Gereza la Mahabusu Keko kwa ziara ya kikazi. Mwenye mawani ni Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Mbarak Abdulwakil, kushoto kwake ni Naibu Katibu Mkuu, John Mngodo.


Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga akikagua gadi maalumu iliyoandaliwa na Maafisa na Askari wa Gereza Keko alipofanya ziara ya kikazi ya kutembelea Magereza Makuu ya Mkoa wa Dar es Salaam.


Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga akizungumza na mahabusu na wafungwa waliopo Gereza la Wanawake Segerea, jijini Dar es Salaam alipofanya ziara katika Gereza hilo kujifunza shughuli mbalimbali za uendeshaji wa Magereza. Kulia kwake ni Waziri wa Sheria na Katiba, Dkt. Harrison Mwakyembe. Kulia ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Mbarak Abdulwakil, Kushoto ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Sheria na Katiba, Maimuna Tarishi. Wapili kulia ni Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza, CGP John Minja.


Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga (watatu kushoto) na Waziri wa Sheria na Katiba, Dkt. Harrison Mwakyembe (wapili kushoto) wakikagua jiko linalotumia gesi asilia kupikia vyakula vya wafungwa katika Gereza la Mahabusu Keko, jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza, CGP John Minja.


Msafara wa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga ukiwasili katika lango Kuu la Gereza Kuu Segerea, jijini Dar es Salaam kwa ziara ya kikazi kujifunza shughuli mbalimbali za uendeshaji wa Magereza.


Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga (wapili kushoto) na Waziri wa Sheria na Katiba, Dkt. Harrison Mwakyembe (kushoto) wakitoka Gereza la Wanawake Segerea baada ya kuzungumza na Mahabusu na Wafungwa wa Gereza hilo lililopo jijini Dar es Salaam.


Waziri wa Sheria na Katiba, Dkt. Harrison Mwakyembe (kushoto) akiangalia bidhaa zinazotengenezwa na wafungwa wa kike wa Gereza la Wanawake Segerea ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa program ya urekebishaji magerezani. Pembeni yake ni Mkuu wa Gereza Kuu Segerea, Kamishna Msaidizi wa Magereza, Abdalah Kiangi. Kulia ni Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga.


Waziri wa Sheria na Katiba, Dkt. Harrison Mwakyembe (kushoto aliyevaa suti) akipokea heshima kutoka gadi maalumu iliyoandaliwa na Maafisa na Askari wa Chuo cha Taaluma ya Urekebishaji cha Jeshi la Magereza mara baada ya kumaliza kufanya ziara ya kikazi ya kutembelea Magereza Makuu ya Mkoa wa Dar es Salaam.


Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga akitoa majumuisho kwa waandishi wa habari mara baada ya kumaliza ziara ya kutembelea Magereza ya Mkoa wa Dar es Salaam. Katika ziara yake hiyo Waziri Kitwanga aliambatana na Waziri wa Sheria na Katiba, Dkt. Harrison Mwakyembe (katikati). Kulia ni Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza, CGP John Minja.
  • Picha zote na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.

Ben Pol releases "Ningefanyaje" music video shot in South AfricaDar es Salaam, Tanzania - December 21, 2015 - The award-winning Tanzanian R&B crooner - Ben Pol outs the music video of his latest single – NINGEFANYAJE featuring ​Kenya’s Curvaceous Song Bird, Avril Nyambura and another Tanzanian artiste, R​ossie M​.

NINGEFANYAJE was produced by the talented producer Mswaki.

​The music video of NINGEFAN​​YAJE was shot in Pretoria, South Africa by one of Africa's biggest video director Justin Campos under his company Gorilla Films.

NINGEFANYAJE is based on true story happened to a close friend of Ben. It is an emotional song, which means "I Choose To Move On" despite the fact that he was madly in love with his girl. It also talks about how he could survive while the girl is no longer in the picture.

Watch ‘NINGEFANYAJE’


Jumapili mchana: Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu ashitukiza Bombo hospitali
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto, Mh. Ummy Mwalimu akizungumza na mmoja wa wahudumu wa afya (jina lake halikuweza kupatikana kiurahisi) wa dirisha la dawa katika Hospitali ya rufaa ya Bombo mkoani Tanga alipofanya ziara ya kushtukiza mchana wa leo Desemba 20, 2015.
  • Atoa wiki mbili wawe wamefunga mashine ya kukusanya mapato kwa njia ya Kielektroniki ili kudhitibiti upotevu wa mapato yanayotokana na wananchi kuchangia huduma za afya.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,Wazee na Watoto, Mh. Ummy Mwalimu akizungumza na mmoja wa wakina mama anayemhudumia mwanae katika wodi ya watoto Hospitali ya rufaa ya Bombo mkoani Tanga alipofanya ziara ya kushtukiza leo mchana Desemba 20, 2015.


Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,Wazee na Watoto, Mh. Ummy Mwalimu akimsikiliza mmoja wa akina mama aliyelazwa kwenye wodi ya wazazi wakati wa ziara ya kushtikiza aliyoifanya mchana wa leo Desemba 20, 2015 katika Hospitali ya rufaa ya Bombo mkoani Tanga.

Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Tanga (RMO), Dkt. Clement Marceli akimwelezea changamoto wanazokabiliana nazo katika Hospitali ya rufaa ya Bombo mkoani Tanga Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,Wazee na Watoto, Mh. Ummy Mwalimu (hayupo pichani).


Daktari aliyekuwa kwenye mafunzo, Dkt. Zuberi (Medical Intern) akitoa maelezo ya namna wanavyohudumia wananchi wanaofika hospitalini hapo Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,Wazee na Watoto, Mh. Ummy Mwalimu (kulia) aliyefanya ziara ya kushtukiza katika Hospitali ya rufaa ya Bombo, mkoani Tanga mchana wa leo Desemba 20, 2015 ambapo Waziri huyo alikutana na changamoto utoro wa madktari wa zamu kutokuwepo kwenye kituo chao cha kazi katika Hospitali ya rufaa ya Bombo, mkoani Tanga.
Mratibu wa Hospitali ya Rufaa ya Bombo, mkoani Tanga kutoka Idara ya Tiba, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,Wazee na Watoto, Dkt. Ibrahimu Maduhu (mwenye tai) akitoa maelezo kwa Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,Wazee na Watoto, Mh. Ummy Mwalimu namna wanavyokabiliana na changamoto ya kuzuia vifo vya mama na mtoto katika hospitali hiyo wakati wa ziara ya kushtukiza iliyofanywa na Mh. Ummy Mwalimu katika wodi ya wazazi leo mchana Dwsemba 20, 2015.


Baadhi ya madaktari waliokuwa mafunzoni wakizungumza na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,Wazee na Watoto, Mh. Ummy Mwalimu aliyefanya ziara ya kushtukiza katika Hospitali ya Rufaa ya Bombo, mkoani Tanga mchana wa leo Dwsemba 20, 2015.


Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,Wazee na Watoto, Mh. Ummy Mwalimu akipitia orodha ya mahudhurio ya zamu za Madaktari na Wauguzi ambao wengi hawakuwepo kazini wakati wa ziara yake ya kushtukiza katika Hospitali ya rufaa ya Bombo, mkoani Tanga aliyoifanya leo mchana Dwsemba 20, 2015.