Rais Magufuli aliteua "Donald Trump"....

RAIS John Magufuli ameitimiza ahadi yake kwa kuchagua baraza dogo la mawaziri likilinganishwa na lile lililofura la awamu ya nne. Anachotuonyesha ni kwamba mawaziri wachache wanaweza wakafanya kazi sawa au pengine zaidi ya ile iliyokuwa ikifanywa na mawaziri wasio na hesabu.

Kwa kupunguza idadi ya mawaziri Magufuli anakuwa anapunguza matumizi halali ya fedha za umma pamoja na ubadhirifu wa fedha hizo. Hawa mawaziri wanazitafuna fedha za umma bila ya huruma; wanalipwa mishahara minono, wanalipiwa nyumba, gharama za matibabu nchi za nje wanapokuwa wao au walio wao wagonjwa, wanalipiwa magari, mafuta ya magari, mishahara ya madereva, wanalipiwa ulinzi pamoja na marupurupu kemkem yanayoingia akilini na yasioingia akilini. Ilimradi wanaula.

La kusikitisha ni kwamba kuna baadhi yao ambao hawatosheki, hawakinai. Hawaridhiki mpaka waitumbukize mikono yao katika tope za ufisadi. Ndiyo maana kuna wenye kuziona siasa kuwa ni uwanja wa kula na huzivaa siasa wakiwa na tamaa hiyo ya kuweza kuchota fedha za umma na kujitajirisha.

Kwa sababu hiyo wanasiasa wa aina hiyo, hasa waliokwishauonja uwaziri, huwa hawayajali maslahi ya wananchi. Wanakuwa tayari kuzikiuka haki za binadamu, kuzipinda sheria na kufanya kila wawezalo kuyang’ang’ania madaraka.

Kwa hivyo, Magufuli alipotangaza baraza lake lenye mawaziri wasio wengi kama wale wa Jakaya Kikwete Watanzania, kwa jumla, walimshangilia na kumpongeza kwa kutimiza ahadi.

Hata hivyo, japokuwa nia yake ya kupunguza gharama za serikali ni ya kupigiwa mfano na ilimpatia sifa ndani na nje ya nchi, kuna wachunguzi waliokosoa uteuzi wa baadhi ya mawaziri wake.

Kwa ufupi, wachunguzi hao wanakubaliana kwamba sura ya baraza hilo haipendezi wala haisisimui. Ni wazi kwamba Magufuli aliwateua baadhi yao kulipa hisani. Hili, bila ya shaka, si geni katika siasa na ni jambo la kawaida.

Kwa hivyo, hatutokosea tukisema kwamba uteuzi wa akina Dk. Khamis Kigwangalla (Naibu Waziri, Afya), January Makamba (Muungano na Mazingira chini ya Makamu wa Rais) na Nape Nnauye (Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo) ni kama malipo yao kwa kazi waliyoifanya wakati wa kampeni za uchaguzi wa urais.

Kazi yenyewe ilikuwa kumyanyasa Edward Lowassa, aliyekuwa mpinzani mkuu wa Magufuli katika uchaguzi huo akiwa mgombea wa Ukawa, muungano wa vyama vinne vya upinzani.

Mawaziri hao wametunukiwa nyadhifa hizo kuwa ni jaza yao kwa kazi waliyomfanyia Magufuli.

Uteuzi wa Nnauye, Katibu wa Uenezi na Itikadi wa Chama cha Mapinduzi (CCM), haukuwa wa busara kwa wizara nyeti aliyopewa. Uteuzi huo umezusha hofu na wasiwasi miongoni mwa wadau wa tasnia ya habari. Hofu yenyewe ni kwamba kwa machachari yake Nnauye anaweza kuigeuza wizara ya habari iwe chombo cha kuendeshea propaganda za CCM, asiweze kutofautisha baina ya wizara ya serikali inayotakiwa iwatumikie wananchi wote bila ya upendeleo na kitengo cha propaganda cha CCM.

Hilo haliwezi kuwa jambo zito kwa kiongozi kama yeye aliyethubutu wakati wa kukaribia uchaguzi mkuu kusema kwamba chama chake lazima kishinde hata kama kwa “goli la mkono”.

Tanzania imepata sifa mbaya karibuni kwa namna waandishi wa habari na vyombo vya habari vinavyohujumiwa Bara na Zanzibar. Mfano wa karibuni ni mashambulizi yaliyofanywa usiku wa kuamkia Desemba 3 kwenye steshini ya Redio ya Hits FM kilicho Migombani, Unguja.

Inasemekana kwamba watu wapatao 15 waliojifunika nyuso zao waliingia kwa nguvu katika studio za steshini hiyo wakavunjavunja zana za utangazaji na kisha wakaichoma moto steshini hiyo. Hadi sasa Polisi hawajamkamata mtu na wanaendelea kusema kuwa hawajui ni nani wahalifu waliofanya mashambulizi hayo.

Wananchi mitaani, ingawaje, wanasema kwamba lau mashambulizi hayo yangekuwa yamefanywa na mahasimu wa CCM isingelipita saa kabla ya wahalifu hao kutiwa mbaroni.

Jambo lililojitokeza wazi pale mawaziri wa mwanzo wa baraza la mawaziri wa Magufuli walipotangazwa ni jinsi Zanzibar isivyowakilishwa kwa usawa katika baraza hilo la serikali ya Muungano. Miongoni mwa mawaziri wa mwanzo waliotangazwa ni wawili tu wenye asili ya Zanzibar, Dk. Hussein Mwinyi, (Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa) na Profesa Makame Mbarawa (Maji na Umwagiliaji).

Uteuzi wa Mbarawa unashangaza kwa vile wizara aliyopewa si ya Muungano na nusu ya wizara ya Mwinyi, yaani Jeshi la Kujenga Taifa, haihusiki na Muungano.

Zaidi ya hayo, Magufuli amewachafua Wazanzibari na hata baadhi ya Waislamu, Visiwani na Bara, kwa kumrejesha William Lukuvi kwenye baraza la mawaziri. Itakumbukwa kwamba mwaka jana Lukuvi alitamka maneno yaliyoonekana na wengi kuwa ni ya uchochezi wakati alipokuwa kanisani wakati wa maadhimisho ya kutawazwa Askofu Joseph Bundala wa Kanisa la Methodist.

Alipokuwa akihutubu katika sherehe hizo Lukuvi alionya kwamba endapo wananchi wataukubali muundo wa Muungano wa serikali tatu basi jeshi litatawala nchi na Zanzibar itaukaribisha utawala wa Kiislamu na Waarabu.

Alipoyatapika matamashi hayo Lukuvi hakukaripiwa na wakubwa zake serikalini au katika chama chake. Wakati huo Lukuvi alikuwa Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Waziri Mkuu na alimwakilisha katika sherehe hiyo Waziri Mkuu wa wakati huo Mizengo Pinda.

Hakuna mkubwa wake yeyote aliyemtaka aombe radhi wala yeye mwenyewe hakutanabahi kwamba alikuwa amesema maneno ya kijinga, yasiyo na msingi na ya uchochezi. Badala yake aliyakariri hayo matamshi yake, tena kwa kibri, katika Bunge la Katiba, licha ya kutakiwa atubu na Askofu Bundala.

Tunaweza kuumithilisha ujinga wa Lukuvi na ule wa Donald Trump, mwanasiasa wa Marekani anayetaka chama chake cha Republic kimchague awe mgombea wake wa urais katika uchaguzi wa urais wa Marekani 2016. Sawa na Trump aliyependekeza hivi karibuni kwamba Waislamu wote wasiruhusiwe kuingia Marekani, Lukuvi amethibitisha kwamba ana ulimi usio na nidhamu na kwamba ni mtu mwenye chuki za kikabila na kidini.

Tafsiri ya wachunguzi ni kwamba kwa kumteua mtu kama huyo awe waziri wake, alichofanya Magufuli ni kama kuwazaba kibao Wazanzibari na hata Waislamu walioshtushwa na kukerwa na matamshi ya Lukuvi.

Uteuzi mwingine uliowavunja moyo Wazanzibari ni ule wa January Makamba kupewa wadhifa wa kushughulikia mambo ya Muungano. Wanamuona kuwa ni kiongozi mwenye kibri, asiyeielewa historia ya Muungano na kwamba kuwekwa chini ya Makamu wa Rais aliye mmoja wa wahafidhina wa Zanzibar huenda kukazidi kuchafua mahusiano baina ya Serikali ya Muungano na Zanzibar.

Magufuli alikuwa hana hila ila amkubali Samia Suluhu awe mgombea mwenza wake kwa vile ndiye aliyebebeshwa na vigogo vya chama chao. Inajulikana kwa nini wenye kuamua mambo walimtaka Samia awe mgombea mwenza wa Magufuli.

Umakamu wa Rais ni tuzo aliyotunukiwa Samia kwa msimamo aliouchukua katika Bunge la Katiba kuhusu suala la Zanzibar na la rasimu ya pili ya Katiba iliyopendekezwa na Tume ya Jaji Joseph Warioba. Jinsia yake, bila ya shaka, ilimsaidia akubalike kwa wengine miongoni mwa viongozi wa CCM, hususan kwa huko Zanzibar.

Inavyoonyesha hadi sasa ni kwamba wasaidizi wakuu wa Magufuli wa kuweza kumsaidia kuutanzua mgogoro wa kisiasa wa Zanzibar si watu ambao watakuwa na moyo wa kwenda kinyume na shinikizo za wahafidhina wa CCM, wa Visiwani na Bara.

Ikiwa hali ya mambo itathibitika kuwa hivyo basi mustakbali wa Zanzibar hauelekei kuwa mwema. Na usipokuwa mwema na mgogoro uliopo wa kisiasa ukiendelea hivi ulivyo bila ya kupatikana ufumbuzi wa haraka basi Magufuli atajikuta katika hali ngumu katika mahusiano yake na wafadhili wa Tanzania. Hali hiyo itazidi kutatanika iwapo viongozi sampuli ya Lukuvi wasipodhibitiwa wasitoe matamshi yanayoweza kuwa ya uchochezi.

Ahmed Rajab
RAIA MWEMA
Baruapepe: [email protected]

Waziri Kairuki aagiza wanaotakiwa kustaafu wasipewe mikataba serikalini

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-UTUMISHI na Utawala Bora Mhe. Angella Kairuki (Mb) akizungumza na watumishi wa Idara ya Uendelezaji Rasilimali Watu - Utumishi.
  • Imenukuliwa kutoka kwenye blogu ya Wizara - Utumishi

Mbeya: Binti akamatwa kwa alichokiandika Facebook

Mtu mmoja anashikiliwa na jeshi la polisi mkoani Mbeya kwa tuhuma za matumizi mabaya ya mtandao wa Face book.

Mtuhumiwa huyo aliyefahamika kwa jina la Carolne Kajela, alikamatwa jioni ya desemba 12, mwaka huu eneo la Uyole Jijini hapa, baada ya kuandika katika ukurasa wake wa Facebook kupitia kundi la Kwinyara Let’s talk kuwa, mmiliki wa mabasi ya Rungwe Express anaingiza mabasi hayo kupitia taasisi ya dini.

“Mtumbua majipu atumbue na hili.. mmiliki wa mabasi ya RUNGWE EXPRESS anapitisha mabasi kupitia taasisi moja ya kidin imbombo... jilipo,” unasomeka ujumbe huo, ambao mpaka anakamatwa ulikuwa umependwa na watu 35 na kuchangiwa maoni na watu 120

Taarifa kutoka ndani ya jeshi la polisi zinasema baada ya mtuhumiwa huyo kukamatwa na kuhojiwa, amekiri kosa na kuomba asamehewe kwani shetani alimzidi.

Mmiliki wa mabasi hayo Yohana Sonelo, alipohojiwa amekiri kampuni yake kupeleka mashitaka polisi na kwamba wanahitaji athibitishe alichokiandika mtandaoni, lasivyo sheria ya makosa ya mtandao namba 14 ya mwaka 2015 ambayo ilianza kutumika Septemba Mosi mwaka huu ifuate mkondo wake.

Kamanda wa polisi mkoani Mbeya, Ahmed Msangi, amethibitisha kumkamata mtuhumiwa huyo na kwamba taratibu za upelelezi zinaendelea kisha watapeleka jalada kwa mwanasheria wa serikali ili mtuhumiwa afunguliwe mashitaka na afikishwe mahakamani.

Kalulunga: Rais Magufuli hana imani na wabunge wa CCM

NIANZE kwa kuwatakia wasomaji wangu kheri ya maandalizi ya sikukuu ya Christmass ambayo inategemea kuazimishwa Desemba 25, mwaka huu.

Wakati huo huo niwatakie kila lakheri wazazi, nikiwemo mimi mwenyewe, wanaoenda kutimiza majukumu kwa watoto wao ambao wamebahatika kuchaguliwa kujiunga na sekondari mwakani 2016 na hata wale ambao hawakubahatika kupata alama za kuchauliwa.

Baada ya kheri hizo, huku tukielekea kuumaliza mwaka huu 2015 na kuuanza mwaka mpya 2016, tukiwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mpya, Dkt. John Magufuli, ni vema kila mmoja akaitazama jana yake na leo yake, kama somo la kesho yake.

Najiuliza kuwa je leo hii sote tungewekwa kwenye majeneza kisha kufunikwa ndani yake huku tukiambiwa tutafakari uwiano wa mema na mabaya tuliyoyatenda, huku kesho ukiwa ndiyo mwisho wa dunia, wangapi wangebaki bila machozi?

Ninachokiandika leo, kwa siasa za magharibi naamini kingeleta matokeo chanya ikiwa ni viongozi wa chama tawala pamoja na serikali chini ya jemedari wetu Rais John Magufuli kujitafakari na kutafakari walikotoka, walipo na waendako, badala ya kutafakari kumfanya baya mwandishi au kutafakari kufungia chombo cha habari.

Waswahili wanasema kuwa, kama umeshindwa kumtambua rafiki wa kweli, vivyo hivyo huwezi kumfahamu adui yako kuwa ni nani, hasa kama umekabidhiwa nafasi kubwa ya uongozi lakini hukupanga timu ya kufanya nayo kazi na cheo ulichopata kimetokea kama ndoto

Desemba 5, siku ya Alhamisi, mwaka huu, Rais Magufuli, aliwatangaza Mawaziri na manaibu Waziri wa baadhi ya wizara, huku akiacha kiporo cha wizara kadhaa.

Katika maelezo yake mwenyewe, alisema kuwa wizara ambazo amezibakiza, anaendelea kuwatafuta watakao weza kumudu wizara hizo ikiwemo wizara ambayo alikuwa akiiongoza yeye, Wizara ya miundombinu.

Hali ile kwetu sisi watu wa nyikani, imeleta sintofahamu nyingi
ikiwemo ya kwamba yawezekana kutokana na uadilifu kumezwa na rushwa Mkatika michakato ya kuwania uongozi hasa wa kisiasa, umempelekea Rais Magufuli na taasisi zake za ushauri ikiwemo idara ya usalama wa Taifa, kuwa na kazi ngumu kuwapata mawaziri wanaotokana na Chama Cha Mapinduzi (CCM) mwaka huu.

Yawezekana wengi ni wafanyabiashara ambao waliingia katika nyadhifa hizo kwa figisufigisu za rushwa kuanzia katika michakato ya kura za maoni majimboni.

Lakini sintofahamu hii, au shaka hii, inatiwa mkazo na idadi ya wabunge wa CCM waliopo ndani ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kuna wabunge zaidi ya 250, mawaziri wanatakiwa 34, lakini Rais na taasisi yake wanapata kazi ngumu kuwapata miongoni mwao.

Ni tafakuri ambayo inapaswa kuwaingia si wananchi pekee, bali hata wabunge wenyewe hasa wale ambao wanajifahamu kuwa walipita kwa rushwa kubwa kubwa hata kama vyombo husika vilivyokuwa chini ya Dkt. Edward Hoseah, havikufanikiwa kuwakamata.

Ninaamini kuwa baadhi waliingia kuwania nafasi hiyo kwa ajili ya kwenda kukinga biashara zao. Wengine waliingia kwa ajili ya kuingiza biashara zao nchini, chini ya kigezo cha kuwa na pasi za kusafiria za uheshimiwa (black passport).

Sina shaka kuwa bunge likivunjika leo, wabunge waliopo wengi wao hawatarejea kugombea majimboni, baada ya yale waliyokuwa wakiyatarajia kufifishwa na juhudi za Rais wa Watanzania wazalendo, Dkt. Magufuli.

Mpaka muda huu kutoweza kuchaguliwa mawaziri wote, pamoja na manaibu wake licha ya kuwepo subira ya mawaziri watakaotoka upande wa pili wa muungano, lakini ni wakati wa wabunge kujipima kuwa je wanaaminiwa na Rais Magufuli? Na kama hawaamini je wao ni waadilifu?

Ninaamini majawabu ya maswali mawili ya hapo juu yapo ndani ya uwezo wa wabunge wetu wa Jamhuri ya muungano wa Tanania, hasa wale wa chama dola, yaani CCM.

Tunapozungumzia serikali (kwa Tanganyika), tunazungumzia serikali za mitaa yaani Tamisemi ambayo imezoeleka inakuwa chini ya ofisi ya Waziri Mkuu, lakini chini ya muundo wa serikali ya Magufuli, Tamisemi amenyang’anywa Waziri Mkuu na sasa ipo chini yake mwenyewe, (ofisi ya Rais).

Nalo hili ni muhimu kamati kuu ya chama cha Dkt. Magufuli ikamsaidia Mheshimiwa Rais, kumpunguzia madaraka ingawa nafahamu kuwa, naye anafahamu kwamba urais siyo mtu binafsi bali ni taasisi.

Rais mstaafu, Dkt. Jakaya Kikwete, aliwahi kuonya kuwa matajiri
wajipime na kwamba wasiwe wana siasa, alishindwa kuisimamia kauli yake kwa vitendo.

Pamoja na dhamira yake njema, hakuweza kufanikiwa chini ya majaribio ya kauli mbiu zake chini ya Waziri Moses Nnauye, (msemaji wa chama kwa wakati huo bila shaka mpaka sasa), ile iliyosema vua gamba.

Rais Magufuli, pengine kwa kuwafahamu vema wabunge watokanao na chama kilichomdhamini nafasi ya urais, ameamua kujitenga na matajiri na wafanyabiashara ambao hapo baadae malengo yao ni kuipigania Katiba mpya na kuwa na mgombea binafsi atakayetokana miongoni mwao. Ameamua kuwa na mfumo tofauti sana, yawezekana ana mambo mawili.

Jambo la kwanza yawezekana hawaamini wabunge waliotokana na chama chake. Pili yawezekana anataka kuirejesha CCM mikononi mwa wakulima (wasio kuwa wafanyabiashara) na wafanyakazi ambao katika Tanzania ndiyo wengi ila wanalazimika kuwa waminifu wa kupokea rushwa kutokana na usalama wao pale wanapozikataa rushwa hizo nyakati za uchaguzi.

Kukomaa kwa rushwa nchini na kushindwa kudhibitiwa. Ulevi wa madaraka kwa watumishi wa umma na yafananayo na hayo, yanaonesha ni jinsi gani watanzania wenye utanzania katika mioyo yao wanavyotoweka kwa kasi katika nchi hii kila kukicha, ndiyo maana nasema Magufuli hawaamini wabunge wa CCM.

Waziri Kitwanga: Orodha ya wauza unga haitanisaidia, huna sheria ya kuwabana

Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, IGP Ernest Mangu akitoa taarifa mbalimbali za shughuli zinazofanywa na jeshi hilo kwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga (katikati), wakati Waziri huyo alipofanya ziara Makao Makuu ya Jeshi hilo, jijini Dar es Salaam kwa lengo la kuzungumza na Viongozi Wakuu wa jeshi hilo, ambapo walikubaliana kuweka mikakati zaidi ya kukabiliana na uhalifu nchini.
WAZIRI wa Mambo Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga amesema njia ya kudhibiti dawa za kulevya kuingia nchini ni kuweka mfumo wa kisasa wa kudhibiti uingiaji dawa hizo, kuwa na orodha ya waingizaji wa dawa ni kazi bure kutokana na kukosa mamlaka ya kisheria.

Kitwanga ameyasema hayo leo jijini Dar es Salaam wakati alipokutana na Maafisa Wakuu wa Jeshi la Polisi, amesema katika kukabiliana na uingizaji wa dawa za kulevya ni kuweka mfumo imara na jeshi la polisi lazima lijipange katika udhibiti huo.

Kitwanga amesema kuwa mfumo wa kiteknolijia ukiwekwa hautabagua mtu yeyote au mkubwa katika madaraka awe mdogo wakishajulikana watachukuliwa hatua za kisheria bila kuangaliwa nafasi walizo nazo.

“Orodha ya wauza unga ukiwanayo haitasaidia na kufanya hivyo ni kuhisi, lakini huna sheria ya kuweza kuwabana katika orodha hiyo” amesema Kitwanga.

Kitwanga amesema kuwa katika mambo waliyojpanga nayo na jeshi la polis ni kuhakikisha wanaimarisha ulinzi katika bandari ili kuweza kudhibiti utoroshaji wa vitu mbalimbali ambavyo vinatoka bila utaratibu.

Hata hivyo amewataka polisi watu washitakiwe kwa kesi walizo nazo na sio kuwabambikia watu wasio na hatia kusababisha kufungwa kwa kesi zisizowahusu.

Kitwanga amesema utoroshaji wa madini,jeshi la polisi haliwahusu wakihitajika na Wizara ya Nishati na Madini watafanya hivyo katika kukabiliana na utoshaji huo.

Aidha amesema kati ya askari 45,000 ni askari 10,000 ndio wenye makazi hivyo wanatarajia kujenga nyumba 5000 ikiwa nia nia askari wote kukaa katika makambi ni rahisi kuweza kuhitajika kwa muda wowote.
  • Imenukuliwa kutoka Michuzi blog

Rais Magufuli, Makamu Suluhu wazungumza na Maalim Seif kuhusu Zanzibar

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akizungumza na Maalim Seif Sharif Hamad, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Ikulu jijini Dar es Salaam. Rais amemshukuru Maalim Seif na amemsihi waendelee na mazungumzo hadi suluhisho la muufaka lipatikane.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amekutana na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Mgombea Urais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharrif Hamad, leo tarehe 21 Desemba, 2015 Ikulu Jijini Dar es Salaam kufuatia maombi yake ya siku nyingi.

Mazungumzo ya viongozi hao pia yamehudhuriwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan.

Viongozi hawa kwa pamoja wamejadili hali ya kisiasa Zanzibar na wamefurahishwa na hali ya usalama na utulivu inayoendelea. Aidha, Mhe. Rais Magufuli amewapongeza Rais wa Zanzibar Mhe. Dkt. Ali Mohamed Shein, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, na viongozi wote wanaoshiriki katika mazungumzo ya kuleta hali ya uelewano Zanzibar.

Rais Magufuli pia amewapongeza na kuwashukuru wananchi wa Zanzibar kwa kudumisha amani na utulivu wakati wa mazungumzo baina ya viongozi wa CUF na CCM yakiendelea huko Zanzibar.

Katika mazungumzo hayo Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar Maalim Seif Sharrif Hamad amemueleza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania juu ya hali ya siasa Zanzibar kadiri anavyoielewa yeye na Rais Magufuli amemshukuru Makamu huyo wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar kwa taarifa yake nzuri huku akimsihi waendelee na mazungumzo hadi suluhisho muafaka lipatikane.

Majadiliano yanayoendelea yanatoa fursa ya kudumishwa kwa utulivu na sifa njema ya nchi yetu. Wote kwa pamoja wamewaomba wananchi waendelee kuwa watulivu ili kutoa nafasi ya majadiliano yanayoendelea kufikia hatma njema. Wameelezea matumaini yao kuwa vyama vya CCM na CUF haviwezi kushindwa kupata suluhu ya mgogoro huo.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amemuhakikishia kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano itahakikisha kuwa amani na utulivu unaendelea kudumishwa Zanzibar.

Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU.

21 Desemba, 2015
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiwa katika picha na Maalim Seif Sharif Hamad ,Makamu wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar pamoja na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama Samia Suluhu Hassan.


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akimkaribisha Maalim Seif Sharif Hamad ,Makamu wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Ikulu jijini Dar es Salaam na kufanya Mazungumzo kuhusu hali ya kisiasa ya Zanzibar. Katika Mazungumzo hayo viongozi wote wamefurahishwa na hali ya usalama na utulivu inayoendelea.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiagana na Maalim Seif Sharif Hamad ,Makamu wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Ikulu jijini Dar es Salaam, wakwanza kushoto ni Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama Samia Suluhu Hassan.


Wizara yapiga marufuku kutumia wajenzi wasiosajiliwa Bodi ya Wahandishi Tanzania

Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Edwin Ngonyani (kushoto), akitoa maagizo mbalimbali kwa uongozi wa Bodi ya Mfuko wa Barabara nchini, alipotembelea bodi hiyo, Dar es Salaam juzi, kujua utendaji wake. Kulia ni Meneja wa bodi hiyo, Joseph Haule.

Na Richard Mwaikenda

NAIBU Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Edwin Ngonyani, amepiga marufuku kwa Halmashauri zote nchini, kuwatumia wajenzi wa barabara wasiosajiliwa na Bodi ya Wahandisi nchini (ERB).

Mhandisi Ngonyaji alichukua hatua hiyo alipofanya ziara ya kujua utendaji wa Bodi ya Mfuko wa Barabara nchini, Dar es Salaam juzi, ambapo alielezwa na Meneja wa Bodi hiyo, Joseph Haule, kuwa barabara nyingi kwenye halmashauri zinajengwa chini ya viwango kwani wanaopewa tenda hawana utaalam wa ujenzi wa barabara.

Alisema kuwa, kuanzia sasa halmashauri ziachane kabisa kuwatumia mafundi wasio na utaalam, bali wawatumie wahandisi waliosajiliwa na Bodi ya Wahandisi nchini, ili barabara zijengwe kwa viwango vinavyotakiwa, na watakaokaidi agizo hilo wanyimwe fedha za mgao kutoka kwenye bodi hiyo.

Pia , Mhandisi Ngonyani, ameitaka bodi hiyo, kutokutuma fedha za ujenzi wa barabara kwa halmashauri yoyote ambayo imetumia fedha walizopelekewa na kuzitumia kinyume cha malengo yaliyokusudiwa.

Amemwagiza Meneja wa Bodi hiyo, kuzichukulia hatua halmashauri zote ambazo zimetumia fedha hizo tofauti na malengo yake ikiwa ni pamoja na kutopelekewa fedha hadi hapo watakapoziresha walizozitumia.

"Ongezeni nguvu zaidi katika kusimamia matumizi ya fedha za mfuko wa barabara kwa halmashauri ambazo fedha hizo zinatumiwa kwa shuguli zisizo za barabara", alisisitiza Mhandisi Ngonyani.

Naye Meneja wa Bodi ya mfuko huo, Joseph Haule, alielezea mafanikio ya mfuko huo tangu ianzishwe miaka 15 iliyopita kwamba kuwa mapato yameongezeka kutoka sh. bilioni 73 mwaka 2005 hadi sh bilioni 752.

"Kutokana na kupanda kwa mapato mtandao wa barabara umeboreshwa kwa kiwango kikubwa kwa kuwa barabara nyingi zimejengwa kutokana na kipato hicho", alisema Meneja Haule.

Aidha, Meneja wa Bodi ya mfuko huo, Haule, alisema kuwa mfuko huo ambao chanzo chake kikubwa ni ukusanyaji wa fedha kutoka sehemu ya mauzo ya mafuta ya petroli na dizeli nchini, Bodi italitia mkazo katika ufuatiliaji wa matumizi ya mfuko kuhakikisha vyanzo vipya vya mapato vinapatikana.

Alisema kuwa, katika kuhakikisha ufuatiliaji wa usimamizi wa fedha hizo unatekelezwa, mfuko tayari umezichukulia hatua halmashauri tatu zikiwemo za Kinondoni, Songea Vijijini na Bukoba Vijinini ambazo zimetumia fedha za mfuko wa barabara kinyume na malengo yaliyokusudiwa.

Alisema Bodi ya Mfuko wa Barabara ilianzishwa kwa lengo la kukusanya mapato, kufuatilia matumizi ya fedha hizo na kugawa kwenye taasisi ambapo asilimia 63 zinapelekwa Wakala wa Barabara wa Serikali (Tanroads) kwa ajili ya matengezo barabar kuu na za mikoa, asilimia 30 katika halmashauri 166 kwa ajili ya ujenzi wa barabara za halmashauri na asilimia 7 zinapelekwa wizara ya ujenzi


Meneja wa Bodi ya Mfuko wa Barabara, Joseph Haule akijibu baadhi ya hoja.


Mhandisi Edwin Ngonyani
  • Picha, habari tumeshirikishwa na Richard Mwaikenda

Rais Magufuli ashiriki mazishi ya dada wa Rais mstaafu Kikwete


Rais Mstaafu Dkt Jakaya Mrisho Kikwete akiweka udongo kaburini wakati wa mazishi ya dada yake, Marehemu Tausi Khalfani Kikwete kijijini Msoga wilaya ya Chalinze Mkoa wa Pwani leo Jumatatu Desemba 21, 2015


Rais John Pombe Joseph Magufuli akiweka udongo kaburini wakati wa mazishi ya dada yake Rais Mstaafu Dkt JAkaya Kkikwete, Marehemu Tausi Khalfani Kikwete kijijini Msoga wilaya ya Chalinze Mkoa wa Pwani leo Jumatatu Desemba 21, 2015


Rais Mstaafu Alhaj Ali Hassan Mwinyi akiweka udongo kaburini wakati wa mazishi ya dada yake Rais Mstaafu Dkt Jakaya Kkikwete, Marehemu Tausi Khalfani Kikwete kijijini Msoga wilaya ya Chalinze Mkoa wa Pwani leo Jumatatu Desemba 21, 2015


Rais Dkt John Pombe Joseph Magufuli, Marais Wastaafu Alhaji Ali Hassan Mwinyi na Dkt Jakaya Mrisho Kikwete wakishiriki katika dua wakati wa wa mazishi ya dada yake Rais Mstaafu Dkt Jakaya Kikwete, Marehemu Tausi Khalfani Kikwete kijijini Msoga wilaya ya Chalinze Mkoa wa Pwani leo Jumatatu Desemba 21, 2015


Rais Dkt John Pombe Joseph Magufuli na Rais Mstaafu kt Jakaya Mrisho Kikwete wakiondoka makaburini baada ya mazishi ya dada yake Rais Mstaafu Dkt JAkaya Kikwete, Marehemu Tausi Khalfani Kikwete kijijini Msoga wilaya ya Chalinze Mkoa wa Pwani leo Jumatatu Desemba 21, 2015

  • Picha:Ikulu

COSOTA, CMEA kuanza kulipa wanamuziki mirahaba Januari 2016

Afisa Mtendaji Mkuu wa Chama Cha Hakimiliki Tanzania (COSOTA) Doreen Sinare akielezea umuhimu wa wanamuziki kujisajili kwao kupitia Kampuni iliyopewa jukumu la kuendesha zoezi usajili, Copyrights Management East Africa Limited (CMEA) ilikuweza kupata haki zao kutokana na kazi zao.
Chama cha Hakimiliki Tanzania (COSOTA) kwa kushirikiana na kampuni ya kusimamia kazi za wanamuziki nchini Copyrights Management East Africa Limited (CMEA) wataanza kulipa mirabaha ya wanamuziki na wadau wake kuanzia mwakani.

Rais Magufuli atoa sehemu ya mshahara wake kumsaidia mtoto BarakaMapitio ya magazeti mbalimbali, Jumatatu, Desemba 21, 2015