Amboni Estates Ltd yafutiwa umiliki wa shamba la mkonge

picha hii si ya shamba linalozungumziwa katika habari
Serikali imefuta hatimiliki ya shamba la mkonge la Kikwetu, mkoani Lindi baada ya mmiliki wake kampuni ya Amboni Estates Ltd, kushindwa kuliendeleza.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, aliyasema hayo alipokuwa akizungumza na wakazi wa manispaa hiyo wakati wa mkutano wa hadhara uliofanyika uwanja wa Ilulu mjini hapa juzi.

Shamba hilo linalodaiwa kupewa hati ya umiliki wa miaka 99 na baadaye kampuni ya Tasco kabla ya kuchukuliwa na Mohamed Enterprieses Tanzania Ltd lilikuwa likizalisha mkonge kwa ajili ya kutengeneza magunia na bidhaa zingine.

Akizungumza katika mkutano huo, Waziri Mkuu Majaliwa alisema kupitia mamlaka aliyopewa kisheria, Rais Magufuli (pichani) amefuta leseni ya umiliki wa shamba hilo na kuwa chini ya serikali.

Majaliwa alisema tayari shamba hilo lipo huru na kampuni ya BSG ipo huru kujenga mitambo itakayotumika kusafishia gesi asilia kwenye eneo hilo.

Kuhusu uendelezwaji wa kiwanda cha kuzalisha saruji cha Meis ambacho ujenzi wake umesimama kwa muda kutokana na sababu mbalimbali zikiwamo za kisiasa, Majaliwa alisema kazi hiyo inatarajiwa kuanza tena muda mfupi ujao baada ya kupatikana kwa wataalam.

Alisema kujengwa kwa viwanda ndani ya mji huo, kutasaidia kupunguza tatizo la upatikanaji wa ajira kwa wananchi wa Mkoa wa Lindi na vitongoji vyake.

Shamba la mkonge la Kikwetu lililopo ndani ya Manispaa ya Lindi awali lilikuwa linamilikiwa na kampuni ya Amboni Estates Ltd halafu Tasco na baadaye Mohamed Enterprieses Tanzania Ltd ya jijini Dar es Salaam.

Ahukumiwa kwa alichokiandika Facebook kuhusu uvamizi wa kituo cha polisi Tanzania


Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imemhukumu Bruno Kimaryo, kifungo cha miaka miwili jela baada ya kupatikana na hatia ya kusambaza ujumbe katika mtandao wa kijamii wa kuyapongeza majambazi yaliyovamia Kituo cha Polisi cha Stakishari na kuua polisi. Aidha, mshtakiwa huyo ametakiwa ama kulipa faini ya Sh. 600,000 kwa kosa hilo. 

Katika tukio la Stakishari lililotokea Julai 12, mwaka huu, majambazi yalivamia kituo hicho na kuua polisi wanne na raia watatu pamoja na kupora bunduki 20 aina ya Sub Machine Gun (SMG). 

Hukumu hiyo ilitolewa jana na Hakimu Mkazi Mkuu, Waliarwande Lema, baada ya kupitia ushahidi uliotolewa na mashahidi watano wa upande wa mashtaka. Alisema vielelezo vitano na utetezi wa mshtakiwa vinaonyesha kuwa Bruno alifurahia kitendo kilichofanywa na majambazi hao na alitamani kila kituo cha polisi kivamiwe.

Alisema mshtakiwa huyo katika ujumbe wake huo alitumia viunganishi vya maneno yasiyokuwa ya kibinadamu ya auawe, avamiwe na kuwa utetezi wake unaungana na maelezo ya onyo aliyoyatoa polisi hayaonyeshi kusikitishwa wala kuhurumia polisi.

Hakimu Lema alisema kama mshtakiwa angekuwa anapeleka ujumbe kwa polisi wachukue tahadhari, angeupeleka katika mamlaka husika, lakini kutokana na lugha aliyoitumia, mahakama hiyo inamtia hatiani.

Hata hivyo, mshtakiwa huyo alifanikiwa kulipa faini na kukwepa adhabu ya kifungo.

Awali, ilidaiwa kuwa Julai 13, mwaka huu, jijini Dar es Salaam, mshitakiwa huyo anadaiwa kusambaza machapisho ya uchochezi kinyume cha Sheria ya Magazeti kwa nia kuleta ushawishi na kueneza chuki katika mtandao wa kijamii wa Facebook.

Taarifa ya kusimamishwa kazi Kaimu Mkurugenzi ORCI


Uamuzi wa mwisho wa NEC kuhusu uteuzi wa madiwani viti maalumu Kyerwa


Taarifa ya kusimamishwa kazi Mtendaji Mkuu BRT


OFISI YA RAIS

TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA - TAMISEMI

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Ndugu wanahabari nimewaita hapa leo ili mnisaidie kufikisha ujumbe kwa wananchi kuhusu mradi wetu wa Mabasi yaendayo Haraka katika Jiji la Dar es Salaam (DART – BRT). Kama mnavyofahamu Serikali ilianzisha mradi huu ili kupunguza msongamano wa magari barabarani kwa madhumuni ya kurahisisha usafiri na usafirishaji katika Jiji letu.

Kutokana na kukamilika kwa sehemu ya ujenzi wa miundombinu ya Awamu ya Kwanza ya mradi, Serikali iliamua tuwe na mtoa huduma wa mpito (Interim Service Provider) kabla ya kumpata mtoa huduma wa kudumu (Service Provider). Mtoa huduma wa mpito alipaswa kupatikana kwa mujibu wa Sheria ya Manunuzi ya Umma. Hata hivyo, Serikali imebaini ukiukwaji wa wazi wa sheria hiyo wakati wa kumpata mtoa huduma wa kipindi cha mpito.
Kufuatia hali hiyo nimeamua kumsimamisha kazi kuanzia leo tarehe 23 Desemba, 2015, Mtendaji Mkuu wa DART, Bi. Asteria Mlambo ili kupisha uchunguzi.

Sababu za kumsimamisha kazi ni:
i. Kushindwa kuzingatia Sheria ya Manunuzi ya Umma wakati wa kumpata mtoa huduma katika kipindi cha mpito;
ii. Kushindwa kuchukua hatua hata pale alipobaini kuwa mtoa huduma wa mpito amekiuka masharti ya mkataba wa kutoa huduma ya mpito; na
iii. Kufanya maamuzi makubwa pasipo kuishirikisha Bodi ya Ushauri ya DART.

Aidha, Serikali inatambua kuwa wapo watumishi wa DART ambao hawakumshauri vizuri Mtendaji Mkuu. Watumishi hao watachunguzwa na kuchukuliwa hatua na Kaimu Mtendaji Mkuu atakayeteuliwa.

Nimemwagiza Katibu Mkuu Ofisi ya Rais TAMISEMI kuendelea na taratibu za kinidhamu dhidi ya Mtendaji Mkuu aliyesimamishwa kazi.

Naitumia nafasi hii kuwahakikishia kuwa Serikali itaendelea kuchukua hatua kwa haraka na uangalifu ili mradi huu uweze kuanza kutoa huduma bora ya usafiri kwa wakazi wa Dar es salaam bila kuchelewa zaidi. Aidha, natoa rai kwa wananchi kuitunza na kuithamini miundombinu ya DART kwa kuwa imegharimu fedha nyingi kwa manufaa yao.

Imetolewa na:-
George B. Simbachawene,
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - TAMISEMI

Taarifa ya kusitishwa kwa siku 14 zoezi la "bomoa bomoa"


Taarifa ya kusimamishwa kazi Mkurugenzi Mkuu RAHCO


Rais wa Jamhuri ya Jamhuri wa Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amemsimamisha kazi Mkurugenzi Mkuu wa kampuni hodhi ya rasilimali za reli Tanzania (RAHCO) Mhandisi Benhadard Tito ili kupisha uchunguzi wa kina kufuatia ukiukwaji mkubwa wa taratibu za manunuzi uliobainika katika mchakato wa utoaji wa zabuni ya ujenzi wa reli ya kati.

Akitoa taarifa kwa vyombo vya habari, Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Sefue amesema, Rais Magufuli amefikia uamuzi huo baada ya kuitisha kikao cha wataalamu kutoka Wizara na Taasisi mbalimbali za serikali ambazo zinahusika katika utekelezaji wa Mradi wa Ujenzi wa Reli ya kati kwa kiwango cha kisasa yaani “Standard Gauge”

Amesema pamoja na kumsimamisha kazi Mkurugenzi Mkuu wa RAHCO, Rais Magufuli ameivunja bodi ya RAHCO baada ya kujiridhisha kuwa haikutekeleza ipasavyo wajibu wake katika kusimamia mchakato wa zabuni hiyo na badala yake imeonekana kutetea kilichofanyika.

Aidha Rais Magufuli amemtaka Mkurugenzi Mkuu wa RAHCO Mhandisi Benhadard Tito kutoa ushirikiano kwa vyombo vya serikali vitakavyofanya uchunguzi zaidi kuhusu mchakato wa Zabuni hiyo.

Pia ameiagiza Mamlaka ya udhibiti wa manunuzi ya umma (PPRA) kuchunguza na kuchukua hatua dhidi ya kampuni za ukandarasi zilizopewa zabuni ya ujenzi huo endapo itathibitika kuwa zimeshiriki katika ukiukwaji wa sheria.

Katika hatua nyingine Balozi Sefue amesema, Rais Magufuli amevunja bodi ya Mamlaka ya Reli Tanzania (TRL) kutokana na kutoridhishwa na jinsi bodi hiyo ilivyoshughulikia ripoti ya uchunguzi wa mchakato wa ununuzi wa mabehewa ya treni.


Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, 
IKULU
22 Desemba, 2015

Sehemu ya pili ya walioteuliwa kukamilisha Baraza la Mawaziri la Rais Magufuli

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amemalizia kujaza nafasi za uteuzi wa Mawaziri na Naibu Waziri alizobakiza wakati akitangaza baraza la Mawaziri la kwanza katika awamu ya tano ya utawala wake.

Uteuzi huo ni kama ifuatavyo;
  1. Profesa Jumanne Maghembe – Ameteuliwa kuwa Waziri wa Maliasili na Utalii.
  2. Dkt. Philip Mpango – Ameteuliwa kuwa Waziri wa Fedha na Mipango (Ni baada ya kumteua kuwa Mbunge).
  3. Mhandisi Gerson Lwenge – Ameteuliwa kuwa Waziri wa Maji na Umwagiliaji.
  4. Dkt. Joyce Ndalichako – Ameteuliwa kuwa Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi. (Ni baada ya kumteua kuwa Mbunge)
  5. Mheshimiwa Hamad Masauni – Ameteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi
  6. Prof. Makame Mbarawa – Amehamishwa kutoka Wizara ya Maji na Umwagiliaji na kwenda Wizara ya Ujenzi, uchukuzi na Mawasiliano
Katika hatua nyingine Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amewatakia heri watanzania wote katika Sikukuu za Maulid, Christmas na Mwaka Mpya na kuwataka washerehekee kwa amani na utulivu.

Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU

23 Desemba, 2015