Mapitio ya magazeti Desemba 30, 2015


Kampuni za simu zatozwa faini; Wavietnam wa Halotel wakamatwa

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, (Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Watu wenye ulemavu), Bibi. Jenista Mhagama (Mb), akifuatilia maelezo ya wajumbe wa kikosi Maalum cha kukagua vibali vya Ajira za Wageni (hawapo pichani) wakati alipokutana nao Jijini Dar es Salaam tarehe 29 Desemba, 2015, (katikati) ni Naibu Waziri (Kazi, Ajira na Vijana), Anthony Mavunde na Katibu Mkuu (kazi na Ajira), Eric Shitindi.
NAIBU Waziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu, anayeshughulikia Kazi, Ajira na Vijana, Anthony Mavunde amebaini kuwepo kwa wafanyakazi wa kigeni, walioletwa na kampuni za simu za mkononi kufanya kazi zinazoweza kufanywa na Watanzania ikiwemo kufunga meza na viti vya kukalia.

Aidha, amebaini kuwepo kwa baadhi ya wafanyakazi wa Kampuni ya simu ya Halotel, raia wa Vietnam, ambao wanaishi nchini bila kibali cha kazi wala cha kuishi. Mavunde aliyabaini hayo jana wakati alipofanya ziara ya kukagua vibali vya ajira kwa wageni, baada ya tangazo lililotolewa na Waziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Walemavu, Jenista Mhagama.

Akiwa katika kampuni hiyo ya Halotel, Mavunde alibaini kuwepo kwa baadhi ya mapungufu, ikiwemo baadhi ya wafanyakazi kutopewa mikataba ya ajira na wenye ajira kutopewa nakala za mikataba yao.

Mavunde aliagiza viongozi wa kampuni hiyo, kuhakikisha kufikia leo wafanyakazi wote wanapewa mikataba huku nakala za mikataba hiyo, ikipelekwa ofisini kwake na pia kuwataka kulipa madeni ya wafanyakazi, hasa madereva, ya saa za ziada (overtime) haraka iwezekanavyo.

“Tumegundua kuwepo kwa mapungufu mengi katika kampuni yenu, hii ni pamoja na wafanyakazi wenu kutojiunga katika mifuko ya hifadhi ya jamii na kumekuwa na makato ambayo hayapo kwa mujibu wa sheria za kazi.

Lakini pia kuna wageni ambao wako katika hii kampuni yenu, wanafanya kazi ambazo zinaweza kufanywa na Watanzania, kwa mfano huyu anayefunga viti, hii kazi inafanywa na vijana wetu…kibali chake kinaisha kesho, naagiza asipewe kingine na aondoke,” alisema Mavunde.

Aidha, alisema katika masuala ya usalama mahali pa kazi, pia kuna mapungufu mbalimbali, ikiwemo wafanyakazi kutopewa mafunzo ya kukabiliana na majanga, vipimo vya afya na makosa mengine ambapo kwa mujibu wa sheria aliwatoza faini ya Sh milioni sita.

Hata hivyo, wakati akiendelea kutoa maagizo hayo, mmoja wa maofisa wa Ubalozi wa Vietnam, Mai Anh Thai aliingia katika ukumbi wa mkutano na kutaka kumkatisha Naibu Waziri kwa madai kuwa hakufuata utaratibu.

Kutokana na kuchafuka kwa hali ya hewa huko, ilimlazimu Mshauri wa kampuni hiyo ambaye jina lake halikuweza kupatikana mara moja, kumshauri ofisa huyo taratibu za ukaguzi zilivyo.

Baada ya kutoka katika kampuni hiyo, Mavunde na maofisa wa Uhamiaji, Wizara ya Kazi, Ajira na Vijana na askari walilazimika kufika katika nyumba ambayo iko Mikocheni, ambako inasadikiwa kuwa wapo raia wengi wa Vietnam wanaoishi hapo, huku wengine wakiwa hawana vibali vya kuishi wala vya kazi.

Walipofanya msako katika nyumba hiyo, baadhi ya raia hao walijificha na kufanikiwa kumkamata mmoja ambaye hakuwa na kibali chochote. Hata hivyo, mmoja wa walinzi wa nyumba hiyo alisema raia hao walikuwa wengi, lakini baadhi yao walitoroshwa juzi usiku.

Awali akiwa katika Kampuni ya Airtel, Mavunde aliwapiga faini ya Sh milioni nne kutokana na kuwepo na mapungufu mbalimbali katika masuala ya usalama na afya mahali pa kazi, ambazo wanapaswa kulipa ndani ya siku 14.

Aidha, aliwataka waajiri nchini kote, kuhakikisha wanasimamia sheria za kazi ili kujenga nchi ambayo haina misuguano. Mavunde alionya kuwa wanaobeza kuwa hiyo ni ‘nguvu ya soda’, wafute jambo hilo, kwani kazi hiyo ni endelevu.

Prof. Ndalichako ataja atakakoanzia ili kufufua kiwango cha elimu

Prof. Ndalichako (wa kwanza kushoto, nyuma ya Katibu Mkuu Kiongozi) katika picha ya pamoja na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzani Dkt. John Pombe Magufuli, Makamu wa Rais, Waziri Mkuu, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Katibu Mkuu Wa Kiongozi (walioketi) na Mawaziri (wote waliosimama) baada ya kuwapisha Ikulu jijini Dar es salaam Desemba 28, 2015. 
WAZIRI wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Prof. Joyce Ndalichako, amesema atafuatilia shule za Serikali ili kujua sababu za kufanya vibaya katika mitihani yao. Prof. Ndalichako ambaye aliwahi kuwa Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani (NECTA), amesema hayo juzi baada ya kuapishwa na Rais John Magufuli, kushika wadhifa huo.
“Kwa kuwa lengo langu ni kuona elimu bora inatolewa, nitafuatilia kujua sababu ya shule maalumu za Serikali kushuka kiwango chake katika ufaulu wa mitihani,” 
Kwa mujibu wa Prof. Ndalichako, shule hizo za Serikali hasa za vipaji maalum, ndizo awali kila mwanafunzi alipenda kwenda kusoma tofauti na sasa ndio maana anataka kujua kulikoni.

Shule hizo ni pamoja na Mzumbe, Ilboru, Tabora Wavulana, Tabora Wasichana, Kilakala na Msalato.

Ada holela, kukaa chini 

Kuhusu upandaji holela wa ada za shule binafsi, Prof. Ndalichako alisema atapambana na vyuo vikuu na shule binafsi, zinazofanya ujanjaujanja wa kupandisha ada tofauti na ile iliyoandikwa kwenye barua za kuwaita wanafunzi, jambo linalosababisha usumbufu kwa wazazi.

Alisema lengo lake ni kuhakikisha Tanzania inatoa elimu bora kwa wahitimu wa vyuoni na sekondari, itakayowawezesha kukidhi soko la ajira la kimataifa. Pamoja na ubora huo, Prof. Ndalichako alisema ataangalia uwepo wa miundombinu kwa wanafunzi wa kuanzia shule ya msingi na sekondari, ambako alikiri kuwa baadhi ya wanafunzi wanaketi chini na wengine wana matatizo ya mashimo ya vyoo.
“Inakuwaje shule yenye maelfu ya wanafunzi watumie shimo moja la choo, haya na mambo mengine yanakwaza wanafunzi wasipende shule na wengine wakatize masomo yao.
“Tunataka kuandaa mwanasayansi, hivi kweli mwanafunzi anayeketi chini anaweza kuwa mtaalamu mzuri wa sayansi? Ni lazima tuwezeshe shule zetu ziwe na miundombinu rafiki kwa wanafunzi” 
Pia alisema atashughulika na tatizo la baadhi ya vyuo kutoa kozi zinazoenda kinyume na ithibati walizopewa na mamlaka za elimu, jambo linalofanya wanafunzi wanaosoma kwenye vyuo hivyo kutotambuliwa na waajiri.

Askari Polisi ahukumiwa kifungo cha maisha jela kwa kulawiti

ASKARI Polisi mwenye namba G 9762 PC Daniel (24), amehukumiwa kifungo cha maisha jela, kulipa fidia ya Sh milioni mbili kwa mlalamikaji baada ya kupatikana na hatia ya kumlawiti mtoto wa kike mwenye umri wa miaka 13.

Daniel kutoka Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, alihukumiwa kifungo hicho katika Mahakama ya Wilaya ya Ilala mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi Mfawidhi, Said Mkasiwa.

Hakimu Mkasiwa alisema upande wa mashitaka ulileta mahakamani hapo mashahidi wanne kuthibitisha mashitaka hayo. Alisema baada ya Mahakama kusikiliza mashahidi hao, ilimuona mshitakiwa kuwa na kesi ya kujibu na kumtaka ajitetee.

Alisema Mahakama ilimtia hatiani mshitakiwa na kwamba katika mashitaka ya kwanza alihukumiwa kifungo cha miaka 30 jela, na mashitaka ya pili kifungo cha maisha. “Mahakama inakutia hatiani hivyo nakuhukumu kifungo cha maisha jela na kulipa faini ya Sh milioni mbili kwa mlalamikaji,” alisema.

Kabla ya kusomwa adhabu hiyo, Wakili wa Serikali Erick Shija aliiomba Mahakama kutoa adhabu kali kwa mshtakiwa iwe fundisho kwa watu wengine wanaofanya matendo kama hayo.

Wakili wa mshtakiwa aliyejulikana kwa jina la Manze, alidai mahakamani hapo kuwa mshtakiwa ni mkosaji wa kosa la kwanza na kwamba alifanya tukio hilo alipokuwa anatoka kwenye starehe ambazo chanzo chake ni pombe.

Katika mashitaka yake, ilidaiwa kuwa mshtakiwa alikabiliwa na mashitaka mawili ya kubaka na kulawiti. Katika mashitaka ya kwanza ilidaiwa Novemba 22 Mwaka jana, maeneo ya Tabata Maduka Mawili, wilayani Ilala, alimbaka mtoto mwenye miaka 13.

Pia ilidaiwa katika tarehe hiyo alimlawiti mtoto huyo kinyume na maumbile na baada ya tukio hilo, mshtakiwa alikimbia nyumbani kwake ambapo alikamatwa mkoani Tanga.


Sasa ni Profesa Joyce Ndalichako na siyo "Dokta" tena

Profesa Joyce Ndalichako
Profesa Joyce Ndalichako
WIZARA ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, imefafanua kuwa sifa ya kitaaluma ya waziri wa wizara hiyo ni Profesa Joyce Ndalichako; na siyo Dk Joyce Ndalichako.

Taarifa iliyotolewa jijini Dar es Salaam jana na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini cha wizara hiyo, ilisema tangu alipoteuliwa kushika wadhifa huo wiki iliyopita, kwa bahati mbaya sifa ya kitaaluma ya waziri huyo, imeendelea kujulikana kama Dokta.

“Tunapenda kuufahamisha umma kwamba cheo cha kitaaluma cha Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi Dokta Joyce Ndalichako kwa sasa ni Profesa Joyce Ndalichako”, ilisisitiza taarifa hiyo ya wizara, iliyotumwa kwa gazeti hili na Ofisa Habari, Oliva Kato.

Taarifa hiyo ilisema wafanyakazi wa wizara hiyo, wanampongeza waziri kwa uteuzi huo na wanaahidi kumpa ushirikiano katika kutekeleza majukumu yake kwa weledi na uadilifu katika kuendeleza sekta ya elimu na mafunzo nchini.

Mwl. Mndeme: Ni zipi athari za simu kwenye kujenga na kudumisha mahusiano ya kijamii?

NINI ATHARI YA SIMU ZA MIKONONI KATIKA KUJENGA NA KUDUMISHA MAHUSIANO YA KIJAMII?

Sehemu ya kwanza: Utangulizi na Chimbuko la Makala

Job:Chief of Party - Tanzania, International Center for AIDS Care and Treatment Programs

Organization: International Center for AIDS Care and Treatment Programs
Country: United Republic of Tanzania
Closing date: 15 Jan 2016

Job: Associate Director of Finance - Tanzania, International Center for AIDS Care and Treatment Programs

Organization: International Center for AIDS Care and Treatment Programs
Country: United Republic of Tanzania
Closing date: 14 Jan 2016

Job: Deputy Chief of Party - Tanzania, International Center for AIDS Care and Treatment Programs

Organization: International Center for AIDS Care and Treatment Programs
Country: United Republic of Tanzania
Closing date: 15 Jan 2016

Job: Senior Monitoring and Evaluation Manager - Tanzania, International Center for AIDS Care and Treatment Programs

Organization: International Center for AIDS Care and Treatment Programs
Country: United Republic of Tanzania
Closing date: 15 Jan 2016

Mahakama yawahukumu "Papaa Msofe", Alex Massawe, Makongoro NyerereMahakama Kuu Kitengo cha Ardhi, imetoa hukumu kwa mfanyabiashara Marijani Abubakar, almaarufu Papaa Msofe, Alex Massawe na Makongoro Nyerere kwa kosa la kughushi hati ya umiliki wa nyumba iliyopo Mikocheni jijini Dar, mali ya marehemu Onesphory Kituly aliyeuawa kwa kupigwa risasi na majambazi mwaka 2011.

Kesi hiyo iliyonguruma kwa takribani miaka saba tangu 2007, ilifikia tamati Desemba 22, mwaka huu na kuwakuta na hatia washtakiwa hao baada ya upande wa utetezi kushindwa kuwasilisha vielelezo vinavyowapa uhalali wa kumiliki nyumba hiyo.

Akisoma hukumu hiyo, jaji wa mahakama hiyo, John Nchimbi mbele ya wakili wa Msofe na wenzake, Majura Maghafu alisema kuwa baada ya kupitia hoja zilizowasilishwa na pande zote mbili, mahakama imeamua kumtangaza mke wa marehemu Onesphory, Mary Kituly kuwa mmiliki halali wa nyumba hiyo.

“Pia mahakama imewatoza fani ya shilingi milioni 300, Papaa Msofe, Massawe na Nyerere pamoja na asilimia 12 ya fedha hizo kama fidia ya gharama za uendeshwaji wa kesi hiyo,” alisema Jaji Nchimbi.

Mara baada ya kusomwa hukumu hiyo, mke wa marehemu, Mary aliangua kilio cha furaha na nduguze mbele ya jaji baada ya kuona haki imetendeka, kitu ambacho hakuwa akikitarajia.

“Yaani siamini macho yangu, maana jinsi kesi ilivyonisumbua kwa miaka saba, nimefarijika sana kwa haki kutendeka maana nilikuwa nikishindana na watu wenye pesa, damu ya mume wangu haijapotea bure, namshukuru Mungu kwa kweli,” alisema Mary alipokuwa akizungumza na waandishi wetu ambapo alimshukuru pia Rais John Magufuli kwani serikali yake inajali haki.

Msofe na wenzake walifunguliwa kesi katika mahakama hiyo mwaka 2007 baada ya kudaiwa kughushi hati ya nyumba kwa kuhamisha umiliki wa nyumba namba 288 iliyopo Mikocheni, Dar iliyokuwa ya marehemu Kituly na kuweka jina lake kisha kumuuzia Masawe kinyume cha sheria.

Ilidaiwa kuwa kabla ya kufariki dunia, marehemu Kituly alimkopa shilingi milioni 30 Msofe kwa dhamana ya hati ya nyumba hiyo kwa makubaliano ya kumrudishia kiasi hicho kwa muda wa miezi sita.

Inadaiwa kuwa baada ya miezi mitano, marehemu alipata kiasi hicho cha fedha na kurudisha kwa Msofe na kutaka hati yake, lakini alianza kuzungushwa kuanzia kipindi hicho hadi alipokufa kwa kuuawa na watu wasiojulikana mwaka 2011.

Oktoba 30, 2007, Msofe aliwatoa kwa nguvu marehemu, mke wake na watoto kwa madai kuwa nyumba hiyo imeuzwa kwa Massawe.

Panga, Pangua! Mabadiliko katika Jeshi la Polisi


Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), Ernest Mangu amelifumua Jeshi la Polisi nchini kwa kupanga na kupangua vigogo wake, huku baadhi wakipandishwa nyadhifa.

Pangapangua hiyo imewagusa pia maofisa waandamizi wa jeshi hilo walioko makao makuu, makamanda wa mikoa, wakuu wa upelelezi wa mikoa (RCO) na wakuu wa polisi wa wilaya (OCD).

Habari za uhakika kutoka ndani ya makao makuu ya Jeshi la Polisi zinasema pangapangua hiyo imewagusa pia wakuu wa vikosi, wakuu wa polisi wa vituo (OCS) na polisi wa vyeo cha chini.

Akizungumza na Mwananchi jana, msemaji wa polisi, Advera Bulimba alisema: “Mabadiliko hayo ni ya kawaida ya ndani, hayana uhusiano na kasi ya Rais John Magufuli ila kazi lazima ifanyike.”

Mabadiliko hayo yamekuja ikiwa ni siku chache baada ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kukutana na maofisa wa polisi kwenye Bwalo la Maofisa wa jeshi hilo Oysterbay jijini Dar es Salaam na kati ya mambo yaliyotajwa ni kukumbushana utendaji, uwajibikaji na mpango wa kulifumua jeshi hilo.

Chanzo chetu ndani ya Jeshi la Polisi kimedokeza kuwa orodha ya waliokumbwa na pangapangua hiyo ni ndefu na kwamba orodha ambayo Mwananchi iliiona ni sehemu tu ya maofisa hao.

“Nafikiri IGP ameamua kusuka upya safu ya uongozi ili kuboresha ufanisi katika utendaji wa kazi. Unajua jeshi lazima liendane na falsafa ya Rais Magufuli (John) ya Hapa Kazi Tu,” alidokeza afisa mwingine.

Mabadiliko hayo yamekuja wakati tayari makamanda wa polisi wa baadhi ya mikoa wakiwa wamebadilishwa katika vitengo walivyokuwa awali, wakiwamo Kikosi cha Usalama Barabarani, ili kuboresha utendaji wa jeshi hilo.

Mabadiliko

Katika mabadiliko hayo, Naibu Kamishina wa Polisi (DCP), Salehe Ambika amehamishwa kutoka kitengo cha Sheria na Huduma za Utafiti kwenda kuwa mkuu wa utawala.

DCP Robert Boaz amehamishwa kutoka kitengo cha intelijensia kwenda kuwa mkuu wa kitengo cha uhalifu wa kitaifa na uhalifu wa kupangwa au Transnational and Organized Crime (TOC).

Katika panguapangua hiyo, Kamishna Mwandamizi wa Polisi (SACP), Luteta Modest amehamishwa kutoka kitengo cha sheria kwenda kuwa mkuu wa kitengo cha sheria na huduma za utafiti.

Mkoa wa Kilimanjaro umetikiswa zaidi na mabadiliko hayo baada ya maofisa watano waandamizi kuhamishiwa vituo vipya na nafasi zao kuchukuliwa na sura mpya.

Kamanda wa polisi wa mkoa huo, Fulgence Ngonyani amehamishiwa Chuo cha Polisi Kilwa Road, na RCO Ramadhan Ng’anzi amehamishiwa mkoa wa Shinyanga kuendelea na wadhifa huo.

OCD wa Moshi, Mrakibu Mwandamizi Deusdedit Kasindo amepanda cheo na kwenda kuwa kamanda wa Mtwara, wakati mkuu wa kitengo cha FFU wa mkoa huo, amehamishiwa mkoa mwingine.

Katika mabadiliko hayo, kamanda wa mkoa wa Iringa, Kamishina Msaidizi Ramadhan Mungi amehamishiwa Kilimanjaro kuchukua nafasi ya Ngonyani anayekwenda chuoni.

Nafasi ya RCO wa Kilimanjaro imechukuliwa na SSP Black Magesa aliyekuwa OCD Korogwe.

Kamanda wa Mkoa wa Manyara, ACP Christopher Fuime amehamishiwa Kinondoni kuendelea na wadhifa huo, wakati kamanda wa Ruvuma, ACP Mihayo Miskhela amehamishiwa mkoani Tanga.

Pia, kamanda wa Mkoa wa Tanga, ACP Zuneri Mumbeki amehamishiwa Ruvuma kuendelea na wadhifa huo, huku kamanda wa Kinondoni, SP Camilius Wambura amehamishiwa Mkoa wa Manyara kushika wadhifa huo.

Maofisa wengine ni Gerald Ngichi, ambaye alikuwa OCD Magomeni, amehamishiwa Lindi, Nsekela M. Nsekela (OCD Nyang’wale sasa ofisa mnadhimu II Rorya, Nesto Msembele (OCD Mbalizi sasa Polisi Jamii Mbeya), William Malei (ofisa mnadhimu ll Kigoma, sasa OCD Korogwe), Melard Sindano (OCD Kigoma, sasa OCD Nyang’wale).

Wengine ni Patrilinius Mlowe (OC-CID Kwimba, sasa OCD Kawe, Edson Kasekwa (OCD Makambako, sasa OCD Kilolo), Agustino Titus (mnadhimu ll Morogoro, sasa OCS Malinyi).

Katika pangua pangua hiyo, Raphael Msela (ofisi ya RCO Kagera, sasa naibu RCO Kagera), John Samwel (OCS Malinyi, sasa ofisa mnadhimu II Morogoro), SP Debora Mrema (polisi jamii Mbeya, sasa OCD Mbalizi, SP Omari Mtungu (OCD Tanga, sasa OCD Moshi),SP Alfred Mwaikusa ambaye alikuwa OCS Singida sasa anakwenda kuwa OC-CID Serengeti.

Wengine ni SP Limited Mhongole ambaye alikuwa OC-CID Mbarali sasa anakuwa OCD Mbarali, ACP Jaffar Mohamed (RPC Pwani, sasa makao makuu) na ACP Peter Kakamba anakuwa RPC Iringa.

Pia ACP Mussa Taibu aliyekuwa RCO Shinyanga, sasa anapelekwa upelelezi makao makuu, SSP Pili Omari (OCD Kawe, sasa OCD Mwanga, David Chidingi (OCD Lindi, sasa OCD Magomeni, SSP Constantiono Mbugambi (OCD Mwanga, sasa OCD Ngara), SSP Jullius Lukindo (OCD Mbarali, sasa OCD Mvomero).

Taarifa ya CUF kuhusu taarifa ya 27.12.2015 - Maamuzi ya kikao cha CCM

Kufuatia taarifa iliyotolewa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) baada ya kikao cha Kamati Maalum ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya chama hicho iliyokutana Zanzibar juzi, tarehe 27 Desemba, 2015, waandishi wengi wa habari wametupigia simu wakitaka kujua Chama Cha Wananchi (CUF) kimepokea vipi taarifa ile.

Vikao vya CCM ni vikao vya CCM. Si kawaida yetu kutolea taarifa maamuzi ya vikao vya vyama vyengine. Hata hivyo, tunaelewa ni kwa nini kumekuwepo na shauku ya kusikia CUF inasema nini kwa sababu yale yaliyokuwemo kwenye taarifa hiyo yaligusia pia mazungumzo yanayofanyika Ikulu Zanzibar yanayolenga kupata ufumbuzi wa mgogoro wa uchaguzi uliofanyika tarehe 25 Oktoba, 2015.

Baada ya kuipitia taarifa ya CCM na mengine yaliyoelezwa na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM Zanzibar wakati akitoa ufafanuzi wa yale yaliyomo kwenye taarifa hiyo, CUF tunapenda kuwaeleza Wazanzibari na Watanzania kwa ujumla haya yafuatayo:

1. Taarifa yenyewe haionekani kama imeandaliwa na watu makini wala haioneshi kama walioitoa wanajua nini kilichopo. Hilo liko wazi kutokana na taarifa yenyewe kuwa na maudhui yanayopingana ambayo yamekuja kukorogwa zaidi na maelezo yaliyotolewa na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM Zanzibar mbele ya waandishi wa habari na kuoneshwa katika vituo kadhaa vya televisheni:

(a) Taarifa inawataka wanachama wa CCM wajiandae na uchaguzi wa marudio lakini papo hapo inaeleza kwamba kikao kimeridhia mazungumzo yanayoendelea Ikulu Zanzibar. Taarifa haisemi iwapo maamuzi ya vikao vya mazungumzo hayatakuwa na suala la kurudiwa uchaguzi, upi ni mwelekeo wa CCM.

(b) Taarifa inazungumzia uchaguzi wa marudio lakini papo hapo Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM Zanzibar anasema CCM haina imani na Tume ya Uchaguzi iliyopo na kwa hivyo uchaguzi huo wa marudio lazima ufanyike chini ya Tume mpya. Baada ya hapo hasemi Tume iliyopo ambayo muda wa utumishi wa Makamishna wake unalindwa kikatiba itaondolewa vipi na Tume mpya itapatikana vipi.

(c) Taarifa inawataka wanachama wa CCM wajiandae na uchaguzi wa marudio lakini Katibu wa itikadi na Uenezi anasema hata usiporudiwa ndani ya siku 90, bado Dk. Ali Mohamed Shein ataendelea kuwa Rais.

Nukta hizi tatu ambazo haziwezi zote kusimama kwa pamoja bila ya kupingana moja dhidi ya nyingine zinaonesha tu ni kwa kiasi gani viongozi wa CCM Zanzibar wamepoteza mwelekeo na hawana uhakika wa nini kitatokea katika kuondokana na mgogoro huu wa kutengenezwa.

2. Taarifa ya CCM haiwasaidii wanachama wa CCM wala wananchi wa Zanzibar kwa kuwapa matumaini ya kumalizika kwa mgogoro wa kutengenezwa wa uchaguzi wa Zanzibar na badala yake inaonekana imelenga kuwachanganya zaidi wananchi kwa maelezo yanayopingana.

3. Taarifa inaonyesha ni jinsi gani CCM kilivyopoteza mvuto kwa kujiweka mbali na wananchi. Taarifa hiyo inapongeza eti kuwepo kwa maendeleo ya kiuchumi na kijamii wakati wananchi wa Zanzibar, bila ya kujali itikadi zao za kisiasa, siyo tu wanumia kutokana na sera mbovu za CCM lakini sasa wanazidi kuteketea na maisha yao kuwa magumu zaidi kutokana na fadhaa (tension) na taharuki iliyopo katika nchi kutokana na kutokuwepo kwa Serikali yenye ridhaa yao.

Harakati za maisha zimeathirika sana huku bidhaa vikiwemo vyakula vikipanda bei. Viongozi wa CCM hawaonekani kujali hali hii mradi wao yao yanawaendea. Tabia hii ya CCM kutowajali wananchi wanyonge wa nchi hii ndiyo iliyopelekea wananchi kukiadhibu chama hicho katika uchaguzi mkuu na kupelekea mgombea wake wa Urais wa Zanzibar na wagombea Uwakilishi kushindwa vibaya kwa tofauti ya zaidi ya kura 25,831.

4. Taarifa inaendeleza utamaduni wa unafiki wa kisiasa kwa eti kuwapongeza viongozi wa CCM na jumuiya zake kwa kazi ya kukiimarisha chama chao huku wakijua kwamba viongozi wao hasa wale walioongoza Kamati ya Kitaifa ya Kampeni za CCM Zanzibar walishindwa kazi na kupoteza mwelekeo.

Matokeo ya kazi mbovu ya Kamati ya Kampeni ya CCM Zanzibar ni kukisababishia chama hicho kipigo kikubwa katika uchaguzi huo kilichopelekea kushindwa katika nafasi ya Urais wa Zanzibar kwa zaidi ya kura 25,831 na kupoteza viti tisa (9) vya Uwakilishi kisiwani Unguja mbali ya kutopata hata kiti kimoja kisiwani Pemba. Viongozi hao walishindwa kuwajibika licha ya kutumia mabilioni ya fedha walizopewa kwa ajili ya kampeni.

5. Katika maelezo yake ya ufafanuzi kwa waandishi wa habari, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM Zanzibar anaitupia lawama Tume nzima ya Uchaguzi ya Zanzibar kwa kushindwa kazi huku akijua na ikijulikana na kila mmoja kwamba tamko la kufuta uchaguzi limetolewa na Jecha Salim Jecha kinyume na Katiba, kinyume na Sheria ya Uchaguzi na kinyume na maadili ya kazi yake.

Katiba inataka Jecha achukuliwe hatua za kufukuzwa kazi kwa kuanza na kumuundia Tume Maalum ya kumchunguza, na siyo kutafuta mbinu za kumlinda kwa kuwaingiza wasiokuwemo.

6. Maelezo ya Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM Zanzibar kwamba Dk. Ali Mohamed Shein ataendelea kuwa Rais hata baada ya miezi mitatu ni kielelezo na ushahidi mwengine wa jinsi CCM isivyoheshimu Katiba.

Kwa hakika, hili suala la kutaja siku 90 ambalo linatajwa sana na CCM na wapambe wake haijulikani hata linatokea wapi. Hakuna pahala popote katika Katiba ya Zanzibar wala Sheria ya Uchaguzi ya Zanzibar panapotajwa sharti la kurudiwa uchaguzi ndani ya siku 90 kwa sababu Katiba yenyewe na Sheria ya Uchaguzi haina sehemu yoyote inayozungumzia kufuta uchaguzi na kufanya uchaguzi wa marudio.

7. Kwa ujumla, taarifa ya CCM Zanzibar iliyotolewa na Katibu wake wa itikadi na Uenezi inaonyesha jinsi chama hicho kisivyojali madhila wanayoyapata raia, fedheha iliyopata taifa na hali ya kiuchumi inayozidi kudorora kila siku Zanzibar ikiwaathiri mno wananchi wanyonge.

Baada ya uchambuzi huo wa taarifa ya Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM Zanzibar, CUF inapenda kuwaeleza Wazanzibari yafuatayo:
  1. Waipuuze taarifa hiyo ya Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM Zanzibar kwani haina lolote jipya zaidi ya kutaka kufunika kombe kutokana na hali ngumu inayotokana na hoja za viongozi wa ngazi za chini na wanachama wa CCM wanaotaka maelezo ya kwa nini chama hicho licha ya kutumia mabilioni ya shilingi kimeshindwa vibaya katika uchaguzi mkuu.
  2. Wazanzibari wasubiri taarifa rasmi ya matokeo ya mazungumzo yanayowahusisha viongozi wakuu wa kisiasa yanayofanyika Ikulu Zanzibar ambayo yamo katika hatua za mwisho kumalizika.
  3. Wampe nafasi Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dk. John Pombe Magufuli, ambaye anaendelea na juhudi katika ngazi za juu kabisa za kuhimiza kupatikana ufumbuzi wa haraka wa mgogoro wa uchaguzi wa tarehe 25 Oktoba, 2015.
  4. CUF inawahakikishia Wazanzibari kwamba haitotetereka na itasimamia kwa dhati maamuzi yao waliyoyafanya kwa njia za kidemokrasia kupitia uchaguzi mkuu wa tarehe 25 Oktoba, 2015 na italinda chaguo lao la Rais wa Zanzibar, Wawakilishi na Madiwani wao.
  5. Mwisho kabisa, inaendelea kuwapongeza Wazanzibari kwa kuonesha ukomavu wa hali ya juu wa kisiasa na kuendelea kutunza amani na utulivu wakati wakisubiri matokeo ya kazi kubwa waliyoifanya tarehe 25 Oktoba, 2015 ambayo inaashiria ujenzi wa Zanzibar Mpya.
HAKI SAWA KWA WOTE

ISMAIL JUSSA
KAIMU MKURUGENZI WA HABARI NA MAWASILIANO NA UMMA – CUF
29 DESEMBA, 2015

Wafanyakazi TPA watoroka! Wakamatwa 7 kwa upotevu wa makontena 11,884, magari 2,019

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhe. Prof. Makame Mbarawa akizungumza na uongozi wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), wakati alipotembelea bandarini hapo leo jijini Dar es Salaam.
BAADA ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kufanya ziara katika Mamlaka ya Bandari Nchini (TPA) na kubaini uondoshwaji wa wa kontena 329 bila kulipiwa kodi ya zaidi ya sh.bilioni 12, Mawakala wa Forodha walifanya ukaguzi kuona kama kuna upotevu wa mapato na kubaini jumla ya kontena 11,884 na magari 2019 yalitolewa bila malipo.

Makontena hayo yalitolewa katika bandari kavu ni MOFED 61, DICD 491, JEFAG 1, 450, AZAM 295, PMM 779, AMI 4384, TRH 4,424 ambazo kodi yake ni zaidi ya sh.bilioni 47.

Magari 2019 yalitolewa bila kulipa kodi katika kampuni za TALL 309, CHICASA 65, FARION 18, SILVER 97, MASS 171, HESU 1359 na kuinyima nchi kodi yenye thamani ya zaidi ya tsh.bilioni moja (1).

Akizungumza na wafanyakazi wa Bandari jijini Dar es salaam leo, Waziri wa Uchukuzi, Ujenzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa amesema wataendelea kuchukua hatua dhidi ya wale ambao wamehusika wakiwemo watumishi wanaoshiriki katika hujuma.

Wafanyakazi saba wa TPA wanashikiriwa na polisi kuhusiana na upotevu wa kontena hizo na kusababisha serikali kukosa mapato.

Waliotiwa mbaroni na jeshi la polisi baada ya kukamatwa leo ni John Elisante, Leticia Masaro, Christina Temu, Merina Chawala, Adnan Ally, Masoud Seleman na Benadeta Sangawe.

Wanaotafutwa kwa tuhuma za kusababisha upotevu wa kodi za serikali katika bandari ya Dar es Salaam ni Happygod Naftal, Nathan Edward, Aron Lusingu, Amani Kazumari, John Mushi, Valentine Sangawe, Benasweet Kamaina na Zainab Bwijo.

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhe. Prof. Makame Mbarawa akisisitiza jambo kwa viongozi wa TPA (hawapo pichani), alipokuwa akizungumza nao juu ya masuala mbalimbali ya utekelezaji wa majukumu yao.
Maafisa wa Wizara na Watendaji wa Mamlaka ya Bandari wakimsikiliza kwa makini Mhe. Waziri Mbarawa alipokuwa akitoa maelekezo ya kazi katika ofisi za Meneja wa Bandari mkoa wa Dar es Salaam.
  • via Michuzi blogUkaguzi wa vibali vya ajira kwa wageni kuanza

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, (Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Watu wenye ulemavu), Bibi. Jenista Mhagama (Mb), akifuatilia maelezo ya wajumbe wa kikosi Maalum cha kukagua vibali vya Ajira za Wageni (hawapo pichani) wakati alipokutana nao Jijini Dar es Salaam tarehe 29 Desemba, 2015, (katikati) ni Naibu Waziri (Kazi, Ajira na Vijana), Anthony Mavunde na Katibu Mkuu (kazi na Ajira), Eric Shitindi.
Serikali imeamua muda wowote kuanzia mwezi huu kuanza ukaguzi wa vibali vya Ajira za Wageni nchini, kufuatia muda wa siku 14 kuisha uliotolewa na serikali katika tangazo la utolewaji wa vibali vya kazi kwa wageni nchini lililotiwa saini Desemba 14, mwaka huu, na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, (Sera, Bunge, Kazi, Aiira, Vijana na Watu wenye ulemavu), Jenista Mhagama (Mb), ambaye aliwataka waajiri wote nchini kwa muda wa siku hizo wawe wametekeleza matakwa ya Sheria ya Kuratibu Ajira za Wageni nchini Na. 1 ya Mwaka 2015.

“Katika taarifa tuliyoitoa mwezi huu, tuliwajulisha waajiri wote wenye waajiriwa wageni ambao wana vibali vya kazi za muda (Carry on Temporary Assignment) na wale wote wasiokuwa na vibali vya ajira vilivyotolewa na kamishna wa kazi nchini kuwa wanatenda kosa. Kamishna wa kazi amepewa mamlaka kutoa vibali vya ajira kwa wageni wanaotaka kufanya kazi nchini. Hivyo hakuna mamlaka nyingine yoyote inayoruhusiwa kutoa vibali vya ajira kwa wageni,” amesema Mhagama

Amesema hayo, Tarehe 29 Desemba, 2015, Jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na kikosi maalum kitakachoendesha operasheni hiyo chenye wajumbe kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, Idara ya Uhamiaji na Wakala wa Usalama na Afya mahali pa kazi (OSHA), ikiwa lengo ni kufuatilia kama agizo lililotolewa na serikali limefuatwa na kuhakikisha taratibu zinazopaswa kufuatwa katika utoaji wa vibali vya ajira zinazingatiwa.

“Serikali ilitoa muda wa siku 14 kwa waajiri wote wawe wametekeleza matakwa ya Sheria Na. 1 ya mwaka 2015 vinginevyo hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.” Alisitiza Mhagama.

Mwezi Machi, mwaka huu Bunge la 10 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lilipitisha Sheria ya Kuratibu Ajira za Wageni nchini Na. 1 ya Mwaka 2015 (The Non-Citizens (Employment Regulation) Act)). Sheria imeanza kutumika rasmi tangu tarehe 15 Septemba, 2015. Sheria hiyo inaanzisha Mamlaka moja yautoajiwa vibali vya ajira kwa wageni na Mamlak ahiyo ni Kamishna wa Kazi.


RC aagiza Mganga Mkuu na Katibu wa hospitali Magu kuondolewa


Watumishi wa Afya wanaomiliki hospitali, kliniki, maduka ya dawa kuchunguzwa

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii,Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu akizungumza na Waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo kuhusiana na ugonjwa wa kipindupindu ulivyoweza kupungua ikiwa kukiwa na vifo vya watu 493 kwa Tanzania Bara.

SERIKALI imetangaza kuwachunguza waganga na wauguzi, wanaomiliki hospitali, kliniki na maduka ya dawa baridi ili kubaini kama wanahusika na upotevu wa dawa kwenye hospitali za Serikali.

Akizungumza ofisini kwake jana, Waziri wa Afya Ummy Mwalimu alisema Desemba 26 alipotembelea Hospitali ya Ocean Road, aliamua kuunda kamati ya watu watano kuchunguza kama wanahusika na upotevu wa dawa hospitalini hapo na sehemu nyingine.

Alisema bodi ya hospitali hiyo aliyoiunda wiki mbili zilizopita, nayo imeshaanza kufanya kazi ya kubaini chanzo cha uhaba wa dawa hospitalini hapo.

“Hata ukisoma tamko langu, hatukatazi watumishi wa umma wa sekta ya afya kumiliki hospitali, kliniki au maduka ya dawa, lakini tunachoangalia ni namna gani tunaondoa mgongano wa kimasilahi,” alisema.

“Nimeenda Ocean Road, wagonjwa wanakufa kwa kukosa dawa, tusubiri kamati itoe taarifa.”

Alisema katika ziara yake aligundua madudu mengi ikiwamo pia fedha za bajeti ya dawa zilizokuwa zikipangwa kwa ajili ya hospitali hiyo, kutofika kwa wakati zilizokuwa zikipangwa kwa ajili ya hospitali hiyo, kutofika kwa wakati.

Waziri Mwalimu alisema asilimia kubwa ya wagonjwa wanaotibiwa hospitalini hapo ni maskini,na kwamba watu wenye uwezo hutibiwa katika hospitali kubwa za kulipia na wengine wanatumia bima ya afya.

“Kwa kuwanyima dawa wanaokuja hospitali hizi ni sawa na kuwanyanyasa,” alisema Waziri Mwalimu.

“Bajeti ya dawa inayopangiwa hospitali hiyo imeonekana nyingi zilikuwa hazifiki kwa wakati. Nimeshamuagiza katibu mkuu wa wizara yangu ahakiki kila fedha zinazopelekwa kwa ajili ya kununua dawa wizarani.”

Waliofariki kwa ugonjwa wa kipindupindu ni 493

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii,Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu akizungumza na Waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo kuhusiana na ugonjwa wa kipindupindu ulivyoweza kupungua ikiwa kukiwa na vifo vya watu 493 kwa Tanzania Bara.
JUMLA ya watu 493 wamefariki dunia kwa ugonjwa wa kipindupindu Tanzania bara tokea ulipoibuka jijini Dar es salaam.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii,Wazee na Watoto Mhe.Ummy Mwalimu akizungumza na Waandishi wa habari ofisini kwake leo, amesema kuwa jumla ya watu 12,222 wameugua ugonjwa huo tangu ugonjwa huo wa mlipuko kuaza hapa nchini.

“Ugonjwa wa Kipindupindu umeanza tokea tarehe Desemba 15, 2015 katika mkoa wa Dar es salaam na kusambaa katika mikoa 21 ya Tanzania” Mhe. Mwalimu amesema.

Hata hivyo,Waziri huyo,amesema waathirika wa kipindupindu wameanza kupungua katika mikoa ya
Mwanza, Arusha, Mbeya na Dar es salaam.

Pia ameitaja Iringa na Kilimanjaro kuwa ni mikoa ambayo imeweza kuthibiti ugonjwa huo hatari.

Mwalimu akitoa takwimu za ugonjwa huo, amesema hivi sasa kuna wagonjwa wapya 76, hivyo idadi ya wagonjwa wapya imefikia 493 na kifo kimoja.

“Hadi sasa mkoa wa Morogoro vijijini unaongoza kwa wagonjwa 56, ukifuatiwa na Arusha (28), Rorya (22), Bunda (21) na Kigoma vijijini 17.” Mhe. Mwalimu amesema”

Aidha Mhe.Mwalimu ametoa agizo kwa wakuu wa mikoa na wilaya kuwa ni marufuku kuuza matunda yaliyokatwa barabarani,kuuza vyakula katika mazingira yasiyo safi na salama,huku akitaka kuandaliwa kwa taarifa za kila wiki kuhusu ugonjwa huo.

Akitoa rai kwa wakuu wa wilaya na mikoa, kuwa walete taarifa sahihi za mlipuko wa ugonjwa huo kwa ajili ya kuudhibiti. Na kwa kuwasisitiza watanzania kunywa maji safi na salama na kunawa mikono kwa maji safi na salama.
  • via Michuzi blog

TAMKO LILILOTOLEWA NA MHE. UMMY MWALIMU, WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO, KUHUSU HALI YA UGONJWA WA KIPINDUPINDU NCHINI 28 DESEMBA 2015


Ndugu Waandishi wa Habari,

Ninapenda kutoa taarifa kwa umma, kuhusu hali ya ugonjwa wa kipindupindu ulioanza tarehe 15 Agosti, 2015 katika mkoa wa Dar es Salaam na kusambaa kwa kasi katika Mikoa mingine 21 ya Tanzania Bara ikiwa ni pamoja na Pwani, Morogoro, Iringa, Kilimanjaro, Dodoma, Kigoma, Geita, Mara, Manyara, Arusha, Shinyanga, Tabora, Singida, Tanga, Lindi, Rukwa, Kagera, Katavi, Mbeya na Mwanza na Simiyu.

Tangu ugonjwa huu uanze, jumla ya watu 12,222 wameugua Kipindupindu, na kati yao jumla ya watu 196 wameshafariki kwa ugonjwa huu ambayo ni sawa na asilimia 1.6 ya waliougua. Mkoa ambao umekuwa na wagonjwa wengi tangu mlipuko uanze ni Dar es Salaam 4,652 (asilimia 38 ya wagonjwa wote) ukifuatiwa na Tanga 1,470 (asilimia12), Singida 1016 (asilimia 8) Mwanza 909 (asilimia 7), Mara 804 (asilimia 7) na Arusha 756 (asilimia 7).
Ndugu Waandishi wa Habari,

Katika kipindi cha wiki mbili za kwanza za mwezi Desemba 2015, mikoa ya Mbeya (Kyela), Arusha (Arusha Mjini) na Mara (Musoma Vijijini) ilikuwa inaongoza kwa kuwa na wagonjwa wapya wengi zaidi wa Kipindupindu. Kadhalika, mikoa ya Kigoma, Rukwa na Lindi ilianza kuripoti upya ugonjwa huu katika kipindi tajwa hapo juu. Aidha, Mikoa ya Tanga na Singida, ambayo hapo nyuma ilipata nafuu, sasa imeanza tena kuripoti ugonjwa huu.

Ndugu Waandishi wa Habari,

Hata hivyo, kasi ya ongezeko la ugonjwa imepungua katika mikoa ya Mwanza, Arusha na Mbeya na Dar-es-Salaam kutokana na juhudi zinazofanywa na wadau ambao kwa pamoja, wameshirikiana kudhibiti ugonjwa huu kwa karibu zaidi. Aidha, mikoa ya Iringa na Kilimanjaro imefanikiwa kudhibiti ugonjwa huu ambapo hakuna mgonjwa mpya kwa zaidi ya siku 30 zilizopita.

Ndugu Waandishi wa Habari,


Kwa mujibu wa taarifa ya tarehe 28 Desemba kumekuwa na wagonjwa wapya 76 na kufanya jumla ya wagonjwa wanaoendelea kupatiwa matibabu kwenye vituo vya kutolea huduma katika mikoa yote iliyoathirika kuwa 115 na kifo kipya kimoja (1). Halmashauri inayoongoza kuwa na wagonjwa wengi ni Morogoro Vijijini (12), Iramba (7), Simanjiro (7), Arusha Mjini (6) na Uvinza (4).

Ndugu Waandishi wa Habari,

Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, kwa kushirikiana na Sekta nyingine husika, wadau wa maendeleo na wadau wengine inaendelea kukabiliana na ugonjwa huu kwa njia mbalimbali. Ofisi ya Rais iliitisha kikao cha pamoja katika ngazi ya Mawaziri na pia iliitisha kikao kingine kwa kushirikisha Wizara yangu, TAMISEMI, Wizara ya Maji, DAWASCO, DAWASA, Wizara ya Elimu na Sekretariat ya Mkoa wa Dar-es-Salaam. Lengo lilikuwa ni kupanga mikakati jumuishi na ya haraka itakayoweza kufanikisha udhibiti wa ugonjwa huu.

Ndugu Waandishi wa Habari,

Kutokana na mwenendo wa mlipuko wa kipindupindu nchini, naendelea kusisitiza kuwa, maagizo niliyoyatoa tarehe 16 Desemba 2015 yazingatiwe na wananchi ili kudhibiti ugonjwa na kuokoa vifo vinavyotokana na ugonjwa huu. Maagizo haya ni pamoja na kunywa maji yaliyo safi na salama, kuepuka kula chakula kilichopoa au kuandaliwa katika mazingira yasiyo safi na salama, kunawa mikono kwa sabuni na maji safi yanayotiririka:-
– kabla na baada ya kula
– baada ya kutoka chooni
– baada ya kumnawisha mtoto aliyejisaidia
– baada ya kumhudumia mgonjwa

Aidha, ni muhimu kuhakikisha kuwa wananchi wanatumia vyoo wakati wote na kutokujisaidia ovyo katika vyanzo vya maji vya mito, mabwawa na ziwani.

Pia nasisitiza tena kuwa ni marufuku kuuza matunda yaliyokatwa na vyakula barabarani katika mazingira yasiyo safi na salama.

Aidha, maagizo niliyoyatoa hapo awali kwa Mamlaka za Mikoa na Halmashauri pamoja na watendaji ambao ni Waganga Wakuu wa Mikoa na Wilaya, Maafisa Afya yaendelee kutekelezwa na kutolewa taarifa kwa wakati.

Na kutokana na hili, nimeagiza kuandaliwa kwa taarifa ya mlipuko kwa kila wiki ili kupata hali halisi, na kila jumatatu wizara itatoa taarifa ya kila wiki ya ugonjwa.

Hitimisho

Kama nilivyosema hapo awali, kwa kuwa ugonjwa huu bado unaendelea kusambaa, mikoa ambayo bado haijaathirika ichukue hatua za tahadhari za kuzuia ili isipate mgonjwa yeyote wa Kipindupindu. Wizara itaendelea kufanya tathmini ya hatua zinazochukuliwa ili hatua stahiki zichukuliwe kuudhibti na kuutokomeza ugonjwa huu.
Nawashukuru kwa kunisikiliza.