Loading...
Tuesday

Balozi Sefue azungumza baada ya kung’oka Ikulu

Balozi Sefue atoa yake ya moyoni

ALIYEKUWA Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue amemshukuru Rais John Magufuli kwa kumwamini na kumpa nafasi ya kumsaidia katika kipindi chake cha mpito huku akisisitiza kwamba, atashirikiana na aliyeshika wadhifa huo, John Kijazi kujenga Tanzania mpya. Kwa upande wake, Katibu Mkuu Kiongozi Balozi, Kijazi, aliyeapishwa jana, alisema ataendeleza jitihada za Rais Magufuli kutumbua majipu, ikiwa ni moja ya njia ya kurejesha nidhamu kwa watumishi wa umma na Serikali kwa ujumla.

Viongozi hao walitoa kauli hizo jana Ikulu, Dar es Salaam, wakati wakizungumza na waandishi wa habari baada ya Rais Magufuli kumwapisha Kijazi kushika Ukatibu Mkuu Kiongozi. Sefue: Nimeheshimika Balozi Sefue ambaye alishiriki katika kumuapisha Dk Kijazi ikiwa ni ishara ya kumkabidhi wadhifa huo, alimshukuru Rais mstaafu Jakaya Kikwete, kwa kumpatia fursa ya kuwatumikia wananchi na kumteua kushika wadhifa huo aliouhitimisha rasmi jana.

Aidha, alimshukuru Dk Magufuli kwa kumpatia nafasi ya kuendelea kumsaidia mara baada ya kuchaguliwa na Watanzania kuwaongoza katika kipindi chote cha takribani miezi mitatu. “Namshukuru Rais Magufuli kwa kuniamini, haikuwa lazima kwake kuendelea na mimi lakini aliamua kuwa nami katika kipindi chake cha mpito ili niweze kumsaidia. Nashukuru sana najisikia nimeheshimika kuwa pembeni yake kwa kipindi chote hicho,” alisema Balozi Sefue.

Alimpongeza Dk Kijazi kwa kumpokea kijiti cha wadhifa huo wa Ukatibu Mkuu Kiongozi, akimuahidi kumpatia ushirikiano na ushauri atakapohitajika. “Nampongeza sana mwenzangu kupatiwa fursa hii, naamini awamu hii ya tano, kutokana na utendaji wake inaashiria mambo makubwa katika nchi yetu, naahidi kumpatia kila aina ya msaada mimi pamoja na makatibu wakuu viongozi waliomaliza muda wao kwa faida ya nchi yetu,” alisisitiza.

Kasi ya Kijazi Kwa upande wake, Katibu Mkuu Kiongozi, Dk Kijazi, alisema dhana ya utumbuaji majipu maana yake ni kujenga nidhamu ndani ya Serikali kwa kuhakikisha maeneo yote yenye kasoro yanarekebishwa. “Nitamsaidia Rais katika kufanikisha hili kwa sababu katika moja ya maeneo yanayopewa kipaumbele na Serikali ya Awamu ya Tano ni pamoja na suala zima la mapambano dhidi ya vitendo vya rushwa,” alisisitiza Dk Kijazi.

Alisema pamoja na kipaumbele hicho cha kupambana na rushwa, pia Serikali imeweka mkazo katika eneo la kuongeza kasi ya ukusanyaji wa mapato, hali ambayo itasaidia kuongeza pato la taifa na hivyo kutoa huduma bora kwa wananchi. Alisema ili nchi yoyote iendelee kiuchumi na maendeleo hayo yafikie wananchi wake, ni lazima ijikite katika kukusanya mapato yake ya ndani.

Alisema akiwa kiongozi na mtumishi mkuu wa Serikali, atahakikisha anaendana na kasi ya utendaji ya awamu ya tano katika kusimamia na kutekeleza kwa vitendo vipaumbele hivyo kwa ajili ya kuboresha uchumi wa nchi . Alisema atasimamia pia kujenga utumishi uliotukuka, wenye tija na nidhamu. “Namshukuru Mungu kutokana na uteuzi huu lakini pia namshukuru mheshimiwa Rais kwa kuniamini na kunipa kazi hii kubwa.

Kwa kuwa mimi ndiye mtendaji mkuu serikalini, nitawajibika na kuwa kiungo kikubwa kati ya Rais na wizara pamoja na idara zake,” alisema Balozi Kijazi. Alisema kwa mujibu wa majukumu ya kazi yake, anapaswa kufahamu kila wizara inafanya nini na kumjulisha Rais juu ya hali ya utumishi, mazingira ya watumishi pamoja na mwenendo wa nidhamu zao.

Alisema katika kutekeleza majukumu ya Baraza la Mawaziri ambalo naye ni mjumbe kutokana na wadhifa wake huo, ni jukumu lake kusimamia utekelezaji wa uamuzi unaofikiwa. “Nafahamu kuwa katika kutekeleza majukumu yote haya siwezi kufanya peke yangu. Kwa kuwa kila wizara ina mtendaji mkuu nitafanya nao kazi kwa ukaribu ili kujua yale yanayohitaji usimamizi na uamuzi ili kwa pamoja tufikie lengo la kuwatumikia wananchi,” alisema.

Wasifu wa Kijazi Kabla ya uteuzi huo, Balozi Kijazi alikuwa mwakilishi wa Tanzania nchini India, Singapore, Sri Lanka, Bangladesh na Nepal makazi yake yakiwa jijini New Delhi, India kuanzia mwaka 2007 na hivyo kumfanya kuwa Mkuu wa Mabalozi wote wanaowakilisha Tanzania nje ya nchi. Amekuwa Mkuu wa Mabalozi wa Afrika nchini India huku akitajwa kuwa mtetezi mkuu wa wanafunzi wenye asili ya Kiafrika nchini humo.

Kabla ya kuwa balozi, Kijazi alikuwa Katibu Mkuu , Wizara ya Ujenzi na baadaye Wizara ya Maendeleo ya Miundombinu kuanzia mwaka 2002 hadi 2006, kabla ya kuteuliwa kuwa Balozi ndani ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa na hatimaye kupangiwa kituo cha New Delhi, India. Kati ya mwaka 1996 hadi 2002, alikuwa Mhandisi Mwandamizi wa Ujenzi wa Barabara ndani ya Wizara ya Ujenzi kabla ya kupandishwa cheo na kuwa Mkurugenzi wa Barabara za Mikoa ndani ya Wizara hiyo hiyo.

Dk Kijazi alipata Shahada ya Sayansi ya Uhandisi wa Umma mwaka 1982 kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, na baadaye Shahada ya Uzamili katika Uhandisi wa Barabara Kuu kutoka Chuo Kikuu cha Birmingham, Uingereza mwaka 1992. Katibu Mkuu Kiongozi Kijazi, ana mke, Fransiscar Kijazi na wamejaliwa watoto watatu; David, Emmanuel na Richard Kijazi.

Katika hatua nyingine, Rais Magufuli ameagana na Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi (UNHCR) anayemaliza muda wake, Joyce Mends-Cole, Ikulu jijini Dar es Salaam. Pamoja mambo mengine, alimshukuru kwa kazi kubwa ya kuhudumia wakimbizi kwa kipindi chote alichokuwepo nchini.

Kwa upande wake, Cole alimpongeza Rais Magufuli kwa kazi nzuri inayofanywa na Tanzania kusaidia nchi zenye matatizo, hususan migogoro ya kisiasa ambayo husababisha watu wake kuwa wakimbizi. Pia amepongeza kuteuliwa kwa Rais mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamin William Mkapa, kusaidia usuluhishi wa mgogoro wa Burundi ambao umesababisha idadi kubwa ya wakimbizi kukimbilia Tanzania.

Siri za Balozi Sefue kung’oka Ikulu

ALIYEKUWA Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, ameelezea sababu zilimfanya Rais Dk. John Magufuli kumwondoa katika wadhifa huo.

Siri za kiongozi huyo kuondolewa zimeendelea kufichuka, huku mwenyewe akisema zama za mabadiliko chini ya uongozi wa Rais Magufuli ndizo zilizomwondoa Ikulu.

Rais Magufuli alitangaza kumn’goa Balozi Sefue juzi na kueleza kuwa atampangia kazi nyingine, huku akimtangaza Balozi Mhandisi John Kijazi kushika wadhifa huo.

Balozi Kijazi Ikulu ya Dar es Salaam katika tukio ambalo lilichukua takribani nusu saa likihudhuriwa na Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa na baadhi ya makatibu wakuu.

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya shughuli hiyo, Balozi Sefue alijibu maswali mawili tu huku akimtakia heri mrithi wake huyo.

Alisema anamshukuru Rais Magufuli kwa kumwamini katika kipindi alichoingia madarakani, lakini zimekuja zama za mabadiliko.

“Namshukuru Mungu kwa kuniwezesha kushika nafasi hii. Namshukuru Rais Magufuli aliyeniamini na kuendelea kufanya kazi na mimi… Awamu hii inawasilisha mabadiliko makubwa ndiyo maana naondoka…Namtakia mwenzangu kila la heri katika kazi zake,” alisema.

Hata hivyo wakati Balozi Sefue akijibu swali la pili aliloulizwa na mmoja wa waandishi wa habari kuhusu uzoefu wake kwa Rais Magufuli alipojibu ‘Hapa Kazi Tu’ ghafla walikuja maofisa wa usalama kumchukua na kisha kumsindikiza moja kwa moja hadi katika gari lake.

Katika tukio hilo la kumwapisha Balozi Kijazi, Rais Magufuli hakuwa amechangamka kama ambavyo amekuwa akionekana katika matukio mengine yanayofanana na hayo.

Rais Magufuli ambaye aliingia saa 4:15 ukumbuni na kisha kupigiwa wimbo wa Taifa na bendi ya polisi na baada ya hapo alimwapisha Balozi Kijazi akisaidiwa na Balozi Sefue mwenyewe ambaye alimpa kitabu cha kiapo na nyaraka za ofisi.

Tofauti na Magufuli, Balozi Sefue alionekana mchangamfu na hata kabla ya shughuli hiyo kuanza alikuwa akizungumza na Balozi Kijazi wakiwa wamesimama ndani ya ukumbi huo.

Wakati Sefue akieleza mabadiliko kama msingi wa yeye kuondolewa, habari ambazo gazeti hili limezipata toka Ikulu zinadai kuwa kuondolewa kwake kwa namna moja au nyingine kumechangiwa na uteuzi uliozua utata wa Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Hifadhi ya Jamii (NSSF), Dk. Carina Wangwe.

Inadaiwa Balozi Sefue kwa nafasi yake, alitoa baraka kwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Ajira na Wenye Ulemavu), Jenista Mhagama kuutangazia umma juu ya uteuzi huo, lakini baada ya muda mfupi akatangaza kuutengua.

Waziri Mhagama alimtangaza Dk. Carina mbele ya kikao cha menejimenti ya NSSF akiwa na naibu wake, Anthony Mavunde.

Dk. Carina alipaswa kuchukua nafasi ya aliyekuwa Mkurugenzi wa Mkuu wa shirika hilo, Dk. Ramadhan Dau ambaye aliteuliwa na Rais Magufuli kuwa balozi hivi karibuni.

Lakini baada ya saa tano kupita, Waziri Mhagama alitoa taarifa kwa vyombo vya habari, akisema teuzi huo umetenguliwa kwa kile alichodai baadhi ya taratibu zilikuwa hazijakamilika.

Kauli ya Waziri Mhagama, iliungwa mkono na Balozi Sefue ambaye alisisitiza kuwa uteuzi wa Dk. Carina ulikosewa na kwamba aliteuliwa kama mwangalizi tu na si kwa kushika nafasi hiyo nyeti ndani ya shirika hilo kubwa.

Baada ya uteuzi huo kutenguliwa yaliibuka mambo makubwa matatu yaliyotajwa kuwa nyuma ya uamuzi huo mgumu ambayo ni ukiukwaji wa sheria, utata wa uraia wake na uteuzi huo kufanywa na waziri badala ya Rais.

Hata hivyo ni jambo moja tu ndilo lililokanushwa ambalo ni utata wa uraia wa Dk. Wangwe ambapo Mamlaka ya Udhibiti wa Usimamizi wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii (SSRA), ilitoa ufafanuzi ikisisitiza kuwa Dk. Carina ni Mtanzania halisi kwa kuandikishwa tangu mwaka 1999.

Taarifa ya SSRA ilisema, Dk. Carina aliandikishwa kuwa raia wa Tanzania baada ya kukidhi vigezo vya kusailiwa (naturalisation)kwa mujibu wa kifungu cha 11 cha Sheria ya Uraia Na.6 ya mwaka 1995.

Taarifa hiyo, ilieleza Dk. Carina aliukana uraia wa Uganda, ikiwa ni pamoja na kurudisha hati ya kusafiria ya nchi hiyo aliyokuwa akimiliki.

Balozi Sefue aliyezaliwa Agosti 26, 1954 aliteuliwa na Rais mstaafu Jakaya Kikwete kuwa Katibu Mkuu Kiongozi Desemba 31, 2011 akimrithi Philemon Luhanjo. Kabla ya hapo alikuwa Balozi wa Kudumu wa Tanzania Umoja wa Mataifa New York, Marekani.

Hata hivyo Desemba 30 mwaka jana Rais Magufuli alimteua tena Balozi Sefue na kumwapisha katika nafasi hiyo aliyodumu nayo kwa siku 65 tu.

Balozi Kijazi aahidi kuendeleza utumbuaji majipu

Kwa upande wake Katibu Mkuu Kiongozi mpya, Balozi Mhandisi John Kijazi alisema lengo la kutumbua majipu ni kuisafisha Serikali na atamsaidia Rais Magufuli kwa kazi hiyo.

“Kuniteua maana yake ni kwamba amenipa heshima ameniamini. Haya yanayoendelea ya msamiati wa ‘kutumbua majipu’ maana yake ni kuleta nidhamu ya utendaji wa Serikali. Ni ujumbe mkubwa huu kwamba pale ambapo pana kasoro turekebishe na ndilo jukumu langu ambalo nitamsaidia Rais…” alisema Balozi Kijazi.

Akizungumzia majukumu yake kama Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Kijazi alisema atarejesha heshima ya utumishi wa umma.

“Kwanza kabisa mimi ndiye mkuu wa utumishi serikalini na ndiyo Katibu wa Baraza la Mawaziri na ndiye mtendaji mkuu katika ofisi ya Rais. Katika kila eneo kuna majukumu ambayo inabidi tuyafanye, kwa mfano katika utendaji katika Ofisi ya Rais, mimi nitahakikisha nakuwa kiungo kikubwa kati ya Rais na wizara zake ambazo zinaunda Serikali,” alisema Balozi Kijazi na kuongeza:

“Kama kiongozi mkuu wa utumishi Serikali napaswa kujua utumishi ukoje, mazingira ya utumishi yakoje, masuala ya nidhamu kwa watumishi yakoje, yapo ninayoyafanyia uamuzi katika ngazi yangu na yapo ambayo yatafanyiwa uamuzi katika ngazi ya juu” alisema.

Kwa upande wa baraza la mawaziri alisema ataendeleza jukumu la kuandaa vikao vyake na baadaye kufuatilia uamuzi uliokubaliwa.

“Siwezi kuyafanya haya peke yangu. Kila wizara ina viongozi, ina makatibu wakuu na viongozi wengine. Itabidi niwe nafanya kazi kwa karibu na viongozi hawa ili kujua yale yanayotokea katika wizara zao na kujua yale yanayohitaji uamuzi zaidi kuliko yale wanayofanya,” alisema.

Mbali na kusisitiza kuwafuatilia kwa karibu mawaziri katika utendaji wao, Balozi Kijazi alisema atasimamia ukusanyaji wa mapato ili kuhakikisha Serikali inakuwa na mapato ya kutosha.

“Nadhani mmeshaona mwelekeo wa Serikali yetu, yapo mambo ya kipaumbele ambayo Rais ameshaanza kuyafanyia kazi. Suala la makusanyo ya kodi na mapato ya Serikali, kwa sababu Serikali inaendeshwa kwa mapato, wananchi watahudumiwa vizuri kama mapato yapo ya kutosha,” alisema.

Kuhusu rushwa alisisitiza kuwa atamsaidia Rais Magufuli ili kuwa na utumishi wa umma uliotukuka.

“Suala la kupiga vita rushwa ndani ya vyombo vyetu vya serikali, idara zetu na wizara zetu, hilo Rais ameshatoa maelekezo hivyo ni jukumu langu kuhakikisha tunakuwa na utumishi uliotukuka, wenye tija na utumishi wenye nidhamu,” alisema na kuongeza:

“Lakini kuna utumishi wenye motisha (incentive) watumishi wanapaswa kuwa na motisha kwa majukumu waliyopangiwa,” alisema.
 
Toggle Footer
TOP