Loading...
Sunday

Bandari kuongozwa na "mtu kutoka nje" asema Waziri

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa amesema serikali inatafuta mtendaji mkuu wa Mamlaka ya Bandari nchini (TPA) kutoka nje ya shirika hilo ili kuongeza ufanisi.

Waziri huyo ambaye alikuwa akizungumza mkoani hapa wakati akiwa katika ziara ya kikazi, alisema katika kuhakikisha TPA inaongeza tija kiutendaji, serikali imedhamiria kumtafuta mtu kutoka nje.

Prof Mabarawa alisema mtu huyo atatakiwa kuwa mzalendo, mwenye mlengo wa kibiashara na atakayeweza kuifufua mamlaka hiyo kwa kasi ya utendaji iliyopo sasa serikalini.

“Wafanyakazi msiogope mabadiliko," alisema na kueleza zaidi, "lazima tupate mtu kutoka nje mwenye utaalamu wa uchumi na biashara wa kutuendeshea mamlaka hii kwani kweli bandari hakuna kitu sasa hivi. 
"Tunataka tupate Sh. trilioni moja (sasa) bila umakini itakuwa ni kazi bure wakati serikali ipo katika mkakati wa kukusanya kodi kikamilifu kwa maendeleo ya Taifa.
"Mabadiliko haya tumeyafanya TRL na matunda yake tunayaona.”

Februari 2 mwaka huu, Waziri Mbarawa alimteua Masanja Kadogosa kuwa Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Reli (TRL), kuchukua nafasi ya Mhandisi Elias Mshana ambaye amestaafu.

Kabla ya kushika wadhifa huo mpya, Kadogosa alikuwa Mkurugenzi Idara ya Mikopo Benki ya Rasilimali Tanzania (TIB).

Wakati akimtambulisha kwa watendaji wa shirika hilo, Prof. Mbarawa aliwaomba maofisa hao wa TRL kumpa Kadogosa nafasi ya kulijua shirika na utendaji wake.

Wakati huo huo, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa ameiagiza Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA) mkoa wa Tanga kuhakikisha inapata mzabuni wa ujenzi wa bandari mpya ya Mwambani ili kurudisha imani ya wananchi kwa serikali yao.

Prof. Mbarawa alisema mradi wa Bandari hiyo mpya umekuwa mwiba kwa wananchi wa mkoa wa Tanga kutokana na kuonekana kuwa ni ahadi isiyotekelezeka hivyo kuondoa imani yao katika utendaji wa serikali.

Waziri huyo alisema ni ukweli usiopingika kwamba uchumi wa mkoa huo unategemea zaidi sekta ya bandari na kulegalega kwake kunakwamisha maendeleo ya wananchi.

“Ni uzembe tu wa hali ya juu (kwani) sioni sababu ya kukosa mzabuni kwenye mradi kama huu wakati ninyi wote ni wataalamu," alisema Prof. Mbarawa. "Kwa nini manafanya kazi kwa mazoea?

"Sitaki kusikia hii habari... nataka mzabuni apatikane, kazi ianze. Huu ubabaishaji siyo wa awamu yetu hii ya hapa kazi tu.”

Taarifa iliyosomwa hivi karibuni na Kaimu Meneja wa TPA mkoani hapa, Kapteni Andrew Matilya ilisema kukosekana kwa udhamini wa serikali na kutaka wawekezaji wajilipe wenyewe kutoka katika mradi ni miongoni mwa sababu zilizokwamisha kupata mzabuni wa ujenzi wa bandari mpya ya Mwambani.

Matilya alisema zabuni hiyo ilitangazwa kwa mara ya kwanza Machi 27, 2014 na kurudiwa Januari 27 mwaka jana lakini hakujatokeza mzabuni hata mmoja.

Mwaka 2011 TPA iliajiri kya URS Scott Wilson ya Uingereza kwa ajili ya kufanya upembuzi yakinifu wa kujenga Bandari mpya ya Mwambani, kazi iliyokamilika Agosti 2012.

Makadirio yaliyofanywa na kampuni hiyo yalionyesha kuwa hadi kufikia mwaka 2028, shehena ipitayo katika bandari ya Tanga itaongezeka kufikia tani milioni 4.5 kwa mwaka tofauti na sasa ikihudumia tani 700,000.

Hivyo ili kukidhi mahitaji , upembuzi yakinifu huo ulipendekeza ujenzi wa bandari yenye gati tatu kwa awamu ya kwanza itakayohudumia shehena mchanganyiko na kontena.

Eneo la Mwambani liliainishwa na kuwekwa jiwe la utambuzi na serikali mwaka 1975. Eneo hilo lina ukubwa wa hekta 174.2 ambapo zaidi ya shilingi bilioni 2.59 zililipwa kwa wananchi kama fidia.
 
Toggle Footer
TOP