Loading...
Friday

Baraza la Madiwani latangaza Monduli kuacha kukarabati magari kwa wakala wa serikali

Monduli, Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Monduli mkoa wa Arusha, limetangaza kujiondoa kutengeneza magari yake,wakala wa serikali wa ufundi na umeme (TEMESA), kutokana na gharama kubwa ya vipuri tofauti na bei halali za soko.

Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Monduli, Isack Joseph alitoa maamuzi hayo, baada ya kupokea taarifa ya matengenezo hafifu na malipo makubwa ya magari ambayo ilitolewa na Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Ephraem Ole Nguyaine.Joseph alisema haiwezekani TEMESA wawauzie kioo (wind Screen) cha gari kwa sh 900,000 wakati kioo hicho kinauzwa sh. 300,000 na pia wamefanya matengenezo kwa ya magari kwa sh 2 milioni hadi milioni 3 wakati matengenezo hayo gharama yake ni kati ya 600,000 na Sh1 milioni.

“huu ni mfano hai na gharama hizi, zimetumika katika gari STK 2223 na tuna risiti zote jambo ambalo tunaamini ni wizi,” alisema.

Mwenyekiti huyo, alisema wao waliamini TEMESA kwa kuwa ni taasisi ya serikali ingefanyakazi nzuri lakini wao sasa ndio wamekuwa tatizo na kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.

Awali Mkurugenzi wa halmashauri hiyo Ole Nguyaine alisema tayari ameandika barua ya malalamiko hayo kwenda kwa katibu Tawala mkoa wa Arusha na TEMESA makao makuu, kulalamikia malipo ya matengenezo hafifu.

Katika barua hiyo, pia halmashauri hiyo, imelalamikia tatizo la kuchelewa kutengenezwa magari kutokana na kutaka kuliwa kabla hali ya kuwa mfumo wa malipo ya halmashauri kwa sasa haiwezekani.

“Pia TESEMA wanakataa kujaza fomu za TIMS pamoja na matengenezo kufanyika kwao, hali ya kuwa halmashauri zinatakiwa kufuata utaratibu wa TIMS kwenye matengenezo ya magari” alisema.

Kutokana na mapungufu hayo, baraza hilo limeagiza halmashauri kutafuta utaratibu mwingine wa kutengeneza magari ambao unapunguza matumizi ya fedha za umma yasiyo ya lazima ili fedha hizo zifanye kazi ya maendeleo.

Hata hivyo, hakuna afisa wa TEMESA mkoa wa Arusha ambaye alikuwa tayari kuzungumzia malalamiko hayo, kwa maelezo kuwa barua za malalamiko zipo ngazi za juu.
  • Taarifa ya Mahmoud Ahmad, Monduli.
 
Toggle Footer
TOP