Loading...
Saturday

Bunge laeleza sababu za Bulaya kukamatwa Mwanza usiku na kumsafirisha hadi DarMbunge wa jimbo la Bunda Mjini, Esther Bulaya (Chadema), alikamatwa juzi usiku akiwa akiwa hotelini jijini hapa na kusafirishwa jana kama mhalifu kwenda Dar es Salaam, kwa amri ya Bunge.

Bulaya alikamatwa wakati vikao vya Kamati Kuu na Baraza Kuu la Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) vikiendelea.

Baada ya kukamatwa, Bulaya aliwekwa mahabusu ya Kituo Kikuu cha Polisi Mwanza, kabla ya jana saa 4.30 asubuhi kupakiwa kwenye gari la polisi chini ya ulinzi mkali hadi uwanja wa ndege wa Mwanza, kwa ajili ya kupelekwa Dar kujibu tuhuma zinazomkabili.

Bulaya alisindikizwa na magari kadhaa ya polisi likiwamo Toyota Landcruiser T 387 DCP ya Ofisa Upelelezi wa Mkoa, PT 3643 na T 916 ASC.

Kwa mujibu wa habari kutoka kwa watu wa karibu na Mbunge huyo, Bulaya alikamatwa kutokana na amri ya Spika wa Bunge, Job Ndugai, kwa madai kwamba hakuhudhuria kwenye Kamati ya Maadili ya Bunge iliyomuita kumuhoji.

“Siku ambayo Bulaya alitakiwa kwenda kuhojiwa na Kamati ya Maadili ya Bunge, alikuwa mgonjwa na taarifa ziliwasilishwa kwenye kamati hiyo, lakini tunashangazwa na Spika Ndugai kutoa kibali cha kukamatwa,” alisema mmoja wa viongozi wa Chadema aliyeomba kutotajwa jina.

Akizungumza na Nipashe Jumapili, kiongozi huyo wa Chadema alisema lengo la Ndugai ni kuvuruga vikao vya chama ambavyo vinaendelea jijini Mwanza ili kumpata Katibu Mkuu atakayerithi mikoba ya Dk. Wilbroad Slaa.

Akizungumzia kadhia ya kukamatwa kwa Bulaya, Mbunge wa Kawe, Halima Mdee (Chadema), alisema jana kuwa wanafanya utaratibu wa kumwekea dhamana mwenzao.

“Ndiyo tunaingia hapa, hatujafahamu tatizo lililosababisha mwenzetu kukamatwa, lakini tunataka kuzungumza na mkuu wa kituo ili tuelewe kama kuna uwezekano wa kuachiwa kwa dhamana ama la,” alisema Mdee.

Katika Kituo cha Kikuu cha Polisi Mwanza, Jeshi la Polisi liliimarisha ulinzi mkali na wananchi walioruhusiwa kukatisha eneo hilo ni wale waliokuwa wakipeleka chakula kwa jamaa zao.

RPC KAMUGISHA 

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Justus Kamugisha, alisema vijana wake walimkamata Bulaya baada ya kupata waranti kutoka Dar es Salaam.

“Hapa tunapozungumza, tayari Bulaya tumemsafirisha kuelekea Dar es Salaam, wanakomhitaji na taarifa zaidi zinaweza kupatikana huko,” alisema Kamugisha.

MWENYEKITI MBOWE

Naye Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Freeman Mbowe, akihutubia Baraza Kuu, pamoja na mambo mengine alielezea jinsi polisi walivyovamia hoteli aliyokuwa amefikia Bulaya.

Alisema baada ya majibizano ya muda mrefu, aliamuru viongozi wa Chadema waruhusu Bulaya kukamatwa ili kuondoa purukushani hizo.
"Polisi walionyesha barua kutoka kwa Spika Job Ndugai aliyeagiza mbunge huyo akamatwe popote alipo nchini," alisema Mbowe.

"Kosa lake ni kupinga kuzuiwa kurushwa moja kwa moja vipindi vya Bunge na alishindwa kwenda kwa kuwa tarehe zilizopagwa alikuwa kwenye kesi yake mjini Bunda."

Mbowe ambaye ni kiongozi wa kambi rasmi ya upinzani bungeni alisema wabunge wengine waliotakiwa kuhojiwa na Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Maadili ni Tundu Lissu, Paulin Gekuli na Godbless Lema.

NAIBU SPIKA

Naibu Spika wa Bunge, Dk. Akson Tulia, alipoombwa na gazeti hili kuzungumzwa kukamatwa kwa Bulaya, alisema atafutwe Ndugai, ambaye hata hivyo licha ya jitihada za kumtafuta kwa simu yake ya mkononi, hakupatikana hewani.

Naye Katibu wa Bunge, Thomas Kashilila, alipotafutwa kupitia simu yake ya mkononi, alikata simu na kutuma ujumbe mdogo wa maneno ‘Nitumie ujumbe nitarudi kwako punde’, lakini pamoja na kutumiwa ujumbe hakuweza kujibu chochote licha ya kupigwa mara kwa mara simu yake.
 
Toggle Footer
TOP