![]() |
Kikaragosi kimenukuliwa na wavuti.com kutoka WhatsApp |
DOKTA DAU KUTEULIWA BALOZI: JE, AMEPENDELEWA AU AMEONEWA?
Kabla ya kuianza Kauli yangu ya leo yenye anuani tajwa hapo juu, niwaombe wasomaji wangu tufanye mambo matatu:
(a) Tukumbushane Waislamu kwamba ni haramu ‘kupendelewa’ kwani kupendelewa ni dalili ya huyo anayependelewa kutostahiki katika jambo fulani. Na pia kupendelewa kunalazimisha kudhulumiwa mwengine ili wewe upate huo upendeleo, jambo ambalo si zuri kwani Uislamu hautaki Muislamu amdhulumu mwengine kwa maslahi yake binafsi au ya jamii ya Kiislamu. Ieleweke kwamba Uislamu si dini ya usawa bali Uislamu ni dini ya uadilifu.
(b) Tushirikiane Watanzania wote kumuombea Rais wetu, Dokta John Pombe Jospeh Magufuli, Mwenye ezi Mungu amuepushe na tuhuma nzito ya kuwabagua Wislamu na Wakristo wasiokuwa katika dhehebu lake la Kikatoliki, na kuwapendelea zaidi Wakristo Wakatoliki na haswa wanaotokea ‘nyumbani’.
Tuhuma hizi hazifanani naye hata chembe kwani tabia yake ya kumuweka Mwenye ezi Mungu mbele na kumtaja sana kwenye hotuba zake inaonyesga ‘uchamungu’ ambao haukubaliani na tabia ya ubaguzi kwa misingi ya udini, madhehebu na ukanda.
Tumuombe sana Mwenye ezi Mungu amuepushe Rais wetu na tuhuma hizo.
(c) Tumpongeze sana Dokta Ramadhan Kitwana Dau kwa kuwa ‘mkimya’ baada ya kuipokea kwa mikono miwili taarifa ya kupewa ubalozi. Tunapaswa kumpongeza kwa hilo kwa sababu vyombo vya habari vimepokea kwa hisia tofauti uteuzi wa yeye kuwa balozi, na yameandikwa yakuandikwa pamoja na kusemwa yaliyosemwa.
Kitendo cha yeye kuwa mkimya, mtulivu na msikilizaji zaidi kumeonyesha ukomavu wake katika kuufahamu vyema mfumo wa uongozi.
Tukirudi katika anuani ya leo, jambo la msingi ni mjadala usio rasmi juu ya kitendo cha aliyekuwa Mkurugenzi wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), Dokta Ramadhan Dau, kuteuliwa kuwa Balozi, tukio ambalo ndio linahitimisha utumishi wake uliotukuka katika shirika hilo kubwa nchini.
Watanzania kupitia vyombo vya habari na mijumuiko isiyo rasmi wametofautiana sana juu ya uteuzi huo. Wapo walioupongeza na wapo walioubeza. Wale walioupongeza wanadai kwamba Dokta Dau amependelewa, na wale walioubeza wanadai kwamba Dokta Dau ameonewa.
Tukianza na wale walioupongeza uteuzi huo kwa hoja kwamba Dokta Dau amependelewa, wanadai kwamba:
(1) Dokta Dau amedumu katika shirika hilo kwa muda mrefu pengine kuliko mtu yeyote kwani ameweka historia ya kuwa Mkurugenzi wa Shirika aliyetumikia kwa muda mrefu. Aliteuliwa na Rais Mstaafu wa Awamu ya tatu, Mheshimiwa Benjamin William Mkapa, kuwa Mkurugenzi wa Shirika hilo mnamo mwaka 1997, na akaweza kulitumikia katika kipindi chote cha Mheshimiwa Mkapa kuanzia mwaka huo hadi alipoondoka madarakani mwaka 2005.
Ilipoingia Awamu ya nne chini ya Rais Mstaafu, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, bado Dokta Dau aliendelea kuwa Mkurugenzi wa Shirika hilo kwa mihula yote miwili (miaka kumi) ya uongozi wa Mheshimiwa Kikwete. Na hatimaye kuteuliwa kuwa Balozi katika Awamu hii ya tano chini ya Mheshimiwa Rais, Dokta John Pombe Magufuli.
Kutokana na utendaji wake uliotukuka na uliosheheni mafanikio makubwa, kwa hakika isingependeza kumpumzisha kwa kutengua nafasi aliyokuwa nayo bila ya kupewa nafasi nyengine yenye hadhi na heshima.
(2) Dokta Dau amependelewa kwa sababu Shirika hilo ni kubwa sana na kwa kuwa yeye ndiye aliyekuwa Mkurugenzi wake (na kwa kuwa ni mwanaadamu) ni makosa makubwa sana kumpa sifa ya umalaika kwamba eti ni mtakatifu aliyefanikisha tu na wala hana kasoro yoyote katika utendaji wake.
Hilo kamwe sio kweli kwani endapo ukipitishwa upembuzi yakinifu yanaweza kupatikana ‘majipu’ ambayo kama yakitumbuliwa yanaweza kumaliza uhai wa mgonjwa. Katika mazingira hayo halafu anapewa ubalozi, wanaamini Dokta Dau amependelewa sana.
(3) Dokta Dau amependelewa na wala hisia za kuondolewa kwake kuhusishwa na udini ni hoja isiyo na ‘mashiko’ kwa kuwa aliyemteua ni Rais Mstaafu, Mheshimiwa Benjamin William Mkapa, ambaye ni Mkatoliki na aliyemuondoa hapo ni Mheshimiwa Rais, Dokta John Pombe Magufuli, ambaye ni Mkatoliki pia.
Kama leo hii wanalalamikiwa Wakatoliki kwa kumuondoa Dokta Dau, ni vizuri kwanza zikatangulia pongezi kwa Wakatoliki hao kwani ndio waliomuweka pia.
Amma kuhusu hoja za wanaolaumu kwamba Dokta Dau ameonewa, msingi wa hoja zao umejengekea kutokana na historia njema ya Dokta Dau katika utumishi wake kwa Taifa la Tanzania.
Wanadai kwamba Dokta Dau ni miongoni mwa Waislamu wachache ambao hawauoni ‘kinyaa’ Uislamu wao, ni msomi aliyebobea mwenye uwezo na hadhi ya kimataifa. Pia ameongoza katika maeneo kadhaa ikiwemo Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) na kadhalika, kwa mafanikio na ufanisi mkubwa.
Pamoja na usomi wake na hadhi yake katika nafasi ‘nyeti’, bado anaona fakhri na heshimwa kubwa kujulikanwa na jamii kwamba yeye ni Muislamu. Na kamwe haoni tatizo kuvaa kanzu na koti siku ya Ijumaa, na wala haoni kwamba vazi hilo linampunguzia hadhi na heshima katika jamii ya kisomi (kama walivyojiweka Waislamu wengine ambao ni wasomi wa kisekula).
Kwa kipindi kirefu Dokta Dau amekuwa mkarimu sana kupitia mshahara wake na stahiki zake mbalimbali hadi kufikia kiwango cha kusifiwa hata na watu wasioijua hata sura yake.
Dokta Dau ni mnyenyekevu, anayehudhuria hafla na matukio mbalimbali ya dini yake ya Kiislamu huku akiwa na bashasha (mchangamfu) anapokutana na rafiki zake bila ya kujali wadhifa na uwezo alio nao.
Kutokana na hulka yake hiyo njema, Dokta Dau ni miongoni mwa Watanzania mwenye wapenzi wengi mnoo.
Na kutokana na yeye kuwa kinyume na Waislamu wengine wasomi wa kisekula kwa kujipamba vyema na kutounyanyapaa Uislamu wake, sehemu kubwa ya Waislamu, Wazee kwa Vijana, wanampenda sana Dokta Dau kwani anaondoa ‘ ombwe’ walilo nalo Waislamu wengi wasomi wa kisekula ambao wanaunyanyapaa Uislamu wao. Amejijengea himaya kubwa ya wapenzi kupitia tabia zake njema na wema anaowatendea wenzake.
Dokta Dau kwa utendaji wake uliotukuka katika Shirika la NSSF ameonyesha njia kwamba Waislamu nao wanaweza, tatizo linalowakumba ni kubaguliwa kutokana na wivu wa kiimani.
Kundi hili la Waislamu na baadhi ya wanajamii linaona kwamba Dokta Dau ameonewa kwa sababu:
(1) Pamoja na kuwa Rais Kikatiba anao uwezo wa kutengua uteuzi na kuteua upya katika eneo lolote ambalo ana mamlaka nalo, lakini alipaswa kuyafikiria mafanikio ya Shirika la NSSF na mchango mkubwa wa Dokta Dau katika mafanikio hayo.
Kitendo cha Mheshimiwa Rais, Dokta John Pombe Magufuli, kutengua uteuzi wa Dokta Dau kama Mkurugenzi wa Shirika hilo katika wakati huu ambao umepewa jina la ‘msimu wa utumbuaji wa majipu, kinailazimisha jamii hiyo iamini kwamba lipo lengo la kumdhalilisha Dokta Dau na huo ni uonevu kwa mtendaji huyo.
(2) Pamoja na heshima ya kazi ya ubalozi lakini kutokana na uwezo na utendaji uliotukuka wa Dokta Dau, baadhi ya wanajamii waliamini kwamba Mheshimiwa Rais Magufuli angemtumia msomi huyo bobezi kwa kumpa ubunge na kumteua kuwa waziri ili awatumikie zaidi Watanzania badala ya kwenda ‘kumficha’ ubalozini ambapo atasahaulika na jamii kwa muda mfupi sana.
Wanaendelea kuhoji kwamba: Hivi katika Baraza la Mawaziri la Mheshimiwa Rais Magufuli, hakuna nafasi ambayo Dokta Dau anaimudu? Kumpa Dokta Dau ubalozi ni ‘kumpandisha’ kimataifa lakini ni ‘kumfinika’ kijamii.
(3) Pia wapo wanaohoji kwamba; Je, haraka ya Mheshimiwa Rais Magufuli kumtoa upesi Dokta Dau imesababishwa na nini? Vipi ameshindwa hata kumvumilia afanikishe ufunguzi wa Daraja la Kigamboni na ndipo amteue kwa wadhifa huo wa Balozi? Kwani pamoja na wengi watakaotambuliwa kufanikisha ujenzi wa daraja hilo lakini Dokta Dau angekuwa ‘kinara’ wa sifa hizo. Je, ni kipi alichokiogopa Mheshimiwa Rais Magufuli mpaka akaharakisha ‘kumnyofoa’ Dokta Dau kwa kasi hiyo?
Kutokana na uharaka wa kumuondoa, utumishi wake uliotukuka kwa Taifa na kumuepusha na mafanikio ya Daraja la Kigamboni linalotarajiwa kufunguliwa mwezi huu wa Machi, Dokta Dau ameonewa na inaonekana ni mwanzo wa safari ya kuizima nyota yake katika jamii ya Watanzania.
Je, ni nini sababu ya kuyafanya hayo? Hicho ni kitendawili ambacho ni vigumu kukitegua kwa haraka kwani ni mapema mnoo kusema kwamba kilichotumika ni ile kanuni ya upangaji foleni kwamba ili ‘namba mbili’ awe namba moja, ni lazima ‘namba moja’ asiwepo; au kusema ni miongoni mwa ‘kampeni baridi’ kwamba wakati wa ‘Waswahili’ Waislamu umepita madhali ‘Mswahili Mkuu’ kamaliza muda wake basi na wa chini yake wamfuate huko huko mapumzikoni.
Yote kwa yote, niendelee kumhimiza Dokta Dau aendelee na ukimya wake pamoja na utii kwa mamlaka ya juu ya nchi yake, na Inshaallaah (Mwenye ezi Mungu akipenda) aende katika kituo chake atakachopangiwa na kamwe asikate tamaa na wala asipunguze hata nukta moja ya utiifu wake kwa Serikali ya nchi yake.
Popote awapo ayakumbuke maneno ya Wakale waliosema: “Udi kila ukichomwa ndio huzidi kutoa harufu nzuri”, “Dhahabu ikitaka kutengenezwa kitu kizuri huchomwa”, na “Mitihani ndio tanuri la kuyafikia mafanikio”.
Hii ndio Kauli yangu ya wiki hii na mjadala umefunguliwa.
Mwandishi wa makala haya ni Mwenyekiti wa ARRISAALAH ISLAMIC FOUNDATION
Unaweza kuwasiliana naye kwa namba: +255 754 299 749, +255 784 299 749.
---------
- Makala kutoka kwenye blogu ya Mohammed Said, "SHEIKH MUHAMMAD IDDI AMZUNGUMZA DR. RAMADHANI KITWANA DAU NA RAIS JOHN POMBE MAGUFULI"