Dk Ndugulile achaguliwa kuwa Mwenyekiti wa IPU Advisory Group on HIV/AIDS and MCH

Mbunge wa Kigamboni Dkt Faustine Ndugulile amechaguliwa kuwa Mwenyekiti Kamati ya Ushauri ya masuala ya UKIMWI, Afya ya kina mama na Watoto ya Taasisi ya Mabunge Duniani (International Parliamentary Union - IPU).

Dkt Ndugulile amechaguliwa katika mkutano wa 134 wa Mabunge duniani unaoendelea mjini Lusaka, Zambia. Mkutano huu ulioanza tarehe 17 Machi unatarajia kuisha tarehe 23 Machi. Kabila ya kuchaguliwa kwake Dkt Ndugulile alikuwa ni Makamu Mwenyekiti wa Kamati hii.

Kamati hii inajumuisha wabunge wasiozidi kumi na mbili (12) ambao huteuliwa na Rais wa IPU kutokana umahiri na mchango wao katika masuala ya UKIMWI na masuala ya Afya ya Mama na Watoto. Wajumbe wengine wa kamati hii wanatoka nchi za Armenia, India, Bangladesh, Afrika Kusini, Rwanda, Italia, Ubelgiji, Austria, Sweden, Dominica na Marekani.

Majukumu ya Kamati hii n kushauri, kujengea uwezo na kuhamasisha Mabunge Duniani kuhusiana na na njia bora za kuboresha huduma za UKIMWI pamoja na Afya za kina mama na watoto.

Dkt Ndugulile ni daktari na mbobezi kwenye magonjwa ya maambukizi na pia kwenye Afya ya jamii. Pamoja na majukumu haya mapya, Dkt Ndugulile ni mwakilishi wa bara la Afrika katika Taasisi ya Kimataifa ya UKIMWI (International AIDS Society), mjumbe wa kamati ya wabunge duniani kuhusu masuala ya TB (Global TB Caucus) na Mwakilishi WA Bunge la Tanzania kwenye Bunge la Afrika (Pan African Parliament).