Loading...
Monday

Fedha ya kuipatia ATCL ndege 2 tayari - Waziri: Tutawaondoa wapiga dili wote waliohujumu

Air Tanzania - The Wings of Kilimanjaro!

WAZIRI wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa amesema serikali iko kwenye mpango kabambe wa kulifufua Shirika la Ndege la Taifa la Tanzania (ATCL) ili kuiwezesha nchi kumiliki ndege zake kama awali na kwamba watumishi ambao walibainika kulihujumu kamwe hawatapata nafasi tena ya kutumikia.

Alisema mpango uliopo kwa sasa ni kuanza na ununuzi wa ndege mpya mbili ili kulipa uhai shirika.

Aliyasema hayo wakati wa ziara yake ya kikazi mkoani Tanga iliyolenga kukagua shughuli za Uwanja wa Ndege wa Tanga na idara nyingine za wizara hiyo zikiwemo Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA), Mamlaka ya Viwanja vya Ndege (TAA) na Mamlaka ya Usafiri wa Anga (TCAA).

“Kwa kuwa tayari fedha ipo na imeshatengwa kwa ajili ya ndege hizo, hatua inayoendelea sasa ni kuzungumza na wataalamu na iwapo tutakubaliana basi Air Tanzania itaanza kufanya kazi kwa kasi mpya,” alisema.

Aliongeza kuwa, uwepo wa ndege mbili ina maana kwa siku kutakuwa na uwezekano wa wastani wa kusafiri safari nyingi zaidi katika maeneo mbalimbali nchini, yakiwemo yenye vivutio vya utalii. Aidha, amewataka watanzania kuwa wazalendo kwa kutumia usafiri wa ndege hizo za serikali.

Akizungumzia ilivyojipanga kukabili hujuma ambazo zimetajwa kuliathiri shirika, alisema Air Tanzania mpya haitaajiri watumishi ambao kumbukumbu zao za ajira zinaonesha walifanya madudu ndani ya shirika hilo.

“Tayari wizara inao mwongozo. Tutawaondoa watumishi wote wabovu ambao walihujumu shirika ili kutoa fursa ya kuanza upya na wale ambao walikuwa wazalendo katika kutimiza majukumu yao ya kazi kwa maslahi ya watanzania na taifa kwa ujumla. 

“Kuna wale wapiga dili, taarifa zao ninazo na ninawajua hivyo wasitegemee kabisa kubaki tutakapofufua shirika. Ni afadhali tukawa na watu hata kumi, lakini wachapa kazi na wazalendo kuliko kuwa na watu wahuni ambao wanajali maslahi yao binafsi,” alisisitiza.

0 comments :

Post a Comment

 
Toggle Footer
TOP