FikraPevu: Nyalandu anastahili kuwajibishwaJANUARI 29, 2016 majangili wakitumia silaha nzito ya kivita aina ya AK47 walimpiga risasi na kumuua rubani Kapteni Roger Gower (37), pamoja na kuiangusha helikopta ambayo ilikuwa ikifanya doria katika pori la akiba la Maswa wilayani Meatu katika Mkoa wa Simiyu.

Kapteni Gower, raia wa Uingereza, alikuwa akiongoza chopa hiyo iliyokodiwa na kampuni ya Mwiba Holdings Ltd akiwa na msaidizi Nicky Bester, raia wa Afrika Kusini katika harakati za kuwasaka majangili walioua tembo watatu kwenye pori hilo.

Watu tisa walikamatwa na kushtakiwa wakihusishwa na tukio hilo. Washtakiwa hao ni Iddy Mashaka (49), Shija Mjika (38), Njile Gunga (28), Dotto Pangali (42), Moses Mandagu (48), Dotto Huya (45), Mwigulu Kanga (40), Mapolu Njige (50) na Mange Barumu (47).

Tayari Mahakama ya Wilaya ya Bariadi imekwishawahukumu washtakiwa wanne kati ya tisa kifungo cha jumla ya miaka 70 jela kutokana na tukio hilo huku washtakiwa wengine kesi zao zikiendelea. Hukumu hiyo ilitolewa Februari 11, 2016 na Hakimu Mary Mrio wa mahakama hiyo.

Lakini Njile Gunga, anayedaiwa kuitungua chopa hiyo amehukumiwa kifungo cha miaka 20 jela, huku akiwa anakabiliwa na kesi mbili ikiwemo ya mauaji pamoja na uhujumu uchumi ambazo zitasikilizwa katika Mahakama Kuu.

Wakati huu ambao Tanzania na dunia nzima inapambana kwa nguvu zote na ujangili, kamwe hakuna anayeweza kufurahia kuona majangili wakitanua wanavyotaka, lakizi zaidi hakuna aliye tayari kushuhudia damu isiyo na hatia ikimwagwa katika ardhi ambayo inafahamika kuwa ‘kisiwa cha amani’.

Mfuko wa Uhifadhi wa Friedkin (Friedkin Conservation Fund – FCF) wa Marekani unashirikiana na serikali ya Tanzania katika kukabiliana na majangili.

Licha ya kudunguliwa kwa chopa hiyo, lakini kumekuwepo na mambo mengi, yakihusu mfuko huo wa FCF pamoja na waziri wa zamani wa Maliasili na Utalii, Lazaro Samuel Nyalandu.

Taarifa mbalimbali ziliibuka mapema mwezi Februari 2016 kwamba wamiliki wa mfuko wa FCF ndio pia wanamiliki kampuni za uwindaji wa kitalii za Mwiba Holdings Ltd, Tanzania Game Trackers Safaris (TGTS) Ltd na Wengert Windrose Safaris. Mwiba Holdings Ltd ndiyo yenye leseni ya kuwinda katika Ranchi ya Wanyamapori ya Mwiba.

Kwa mujibu wa taarifa hizo, kumbukumbu zilizopo Wizara ya Maliasili na Utalii zinasema kampuni ya Mwiba Holdings Ltd ni miongoni mwa watuhumiwa wakubwa wa ujangili na kwamba kumekuwapo matukio kadhaa ya wafanyakazi wa kampuni hiyo kukamatwa wakiwa wameua wanyamapori na kukutwa na nyara za Serikali.

Lakini pamoja na kukamatwa kwao, kwa mujibu wa taarifa hizo, daima kesi zinazoihusu kampuni hiyo zimekwama kutokana na kinachotajwa kuwa ni urafiki wao wa karibu na Nyalandu, hasa wakati alipokuwa akiiongoza wizara hiyo.

Inaelezwa kwamba, wakati Nyalandu alipokwenda kutangaza nia ya kuwania urais na hata alipokuwa kwenye kampeni za ubunge, alikuwa akitumia helikopta inayodaiwa kutolewa na Wamarekani hao, taarifa ambazo hazikuwahi kukanushwa.

FikraPevu iliripoti Machi 26, 2015 kuhusu kukamatwa kwa gari la kampuni ya Wengert Windrose Safaris, lenye namba za usajili T 655 ARR ambalo lilikuwa na shehena ya magunia 11 ya dawa za kulevya aina ya bangi iliyokuwa ikisafirishwa kwenda nchi jirani ya Kenya.

Tukio hilo liliripotiwa na hata Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas, alikiri vijana wake kukamata shehena hiyo katika Wilaya ya Longido saa tano usiku na kumtaja dereva wa gari hilo, Sanka Faustine na maofisa wengine wa kampuni hiyo ambao walitiwa mbaroni.

“Mtuhumiwa mmoja amekamatwa na tunategemea kukamilisha upelelezi ili kumfikisha mahakamani. Tumemkamata katika mpaka wa Tanzania na Kenya akiwa katika harakati za kuvuka mpaka,” FikraPevuilimkariri Kamanda Sabas akisema.

Kampuni ya Wengert Windrose Safaris inamilikiwa na raia kutoka Marekani na ndiyo inayomiliki Kitalu cha Uwindaji wa Kitalii cha North Natron hapa nchini, ikiwa ni pamoja na kufanya doria katika mapori ya Akiba ya Kizigo, Maswa, Moyowosi, Ugalla na Pori Tengefu la Ziwa Natron.

Taarifa Zaidi kuhusu uswahiba wa Nyalandu na Wamarekani hao zinaeleza kuwa, akiwa waziri alimwamuru Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori wa wakati huo, Paul Sarakikya, kutoa Leseni ya Rais kwa familia ya Tom Friedkin (mmiliki wa kampuni hizi) kuwinda wanyamapori 700 katika vitalu nane na eneo la wazi la Makao. Leseni hizo zilitolewa bure bila kulipiwa hata senti.

Miongoni mwa wanyamapori waliokuwa kwenye orodha ya kuwindwa ni tembo, ambao wako hatarini kutoweka.

Lakini taarifa zinasema, Nyalandu alikiuka kifungu cha 38(7) cha Sheria ya Wanyamapori Namba 5 ya mwaka 2009 kwa kupuuza ukomo wa idadi ya vitalu vitano kwa kampuni moja baada ya kuimilikisha kampuni ya TGTS vitalu nane pamoja na eneo la wazi.

Lakini pia, pamoja na kutoa Leseni ya Rais (isivyo halali), Wamarekani hao waliwaleta watoto wadogo wenye umri chini ya miaka 18 kinyume cha kifungu cha 43(3) cha sharia hiyo.

Katika hali ambayo FikraPevu inaona kuna haja ya serikali kuchunguza ufisadi huo, inaelezwa kwamba Nyalandu alitoa vitalu hivyo kinyemela wakati sheria inaagiza kwamba kitalu kinapobaki wazi sharti kitangazwe kwanza na waombaji washindanishwe katika mfumo na utaratibu ulio wa haki na uwazi, kwa kuzingatia Kanuni ya Uwindaji wa Kitalii 18(1).

Kukamatwa kwa gari la kampuni ya uwindaji yenye uswahiba na Nyalandu likiwa na dawa za kulevya ni kashfa kubwa pamoja na jitihada zilizofanywa kukanusha na kuitakasa kampuni hiyo ya Wengert Windrose Safaris.

Watanzania wengi hawawezi kuamini kwamba Nyalandu ni muadilifu ikiwa taarifa zenyewe zinaonyesha wazi kwamba alikuwa akitumia madaraka yake vibaya kwa nia ya ‘kuwatumikia waliomtuma’.

Kitendo cha yeye kupewa chopa afanyie kampeni wakati wa uchaguzi nacho kinaongeza chumvi kwenye kidonda na kutia muhuri mashaka ya Watanzania dhidi ya uadilifu wa Mbunge huyo wa Singida Kaskazini (CCM), ambaye juhudi zake za kuikaribia wizara hiyo kwa kurejea tena kwenye Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii zinadaiwa kukwama alipojikuta akipelekwa kwenye Kamati ya Huduma za Jamii.

Kumbukumbu zilizopo zinaeleza kwamba, wakati alipokuwa kwenye Kamati hiyo katika Bunge la 9, wakati huo ikiongozwa na Job Ndugai, ziliibuliwa tuhuma kwamba Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) lilimpatia mamilioni ya fedha kupitia mradi wa ujirani mwema kwa ajili ya huduma za jamii katika eneo lake, fedha zambazo wachambuzi wa mambo walieleza kwamba zilimsaidia katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2010.

Wakati akiwa Waziri wa Maliasili na Utalii yapo madudu mengi yanayodaiwa kufanywa Nyalandu ikiwemo kuandaa mkataba na bilionea Howard Buffet wa Marekani unaodaiwa kuweka sharti kuwa ili tajiri huyo atoe misaada ya uhifadhi kwa Tanzania ni lazima yeye Nyalandu aendelee kuongoza Wizara ya Maliasili na Utalii.

Yapo madai pia kwamba, uamuzi wake wa kumfukuza Mkurugenzi wa Wanyamapori, Profesa Alex Songorwa na msaidizi wake Profesa Jafary Kidengesho ulitokana na shinikizo la Wamarekani wenye kampuni za uwindaji nchini baada ya kukwama kuwaweka mfukoni wasomi hao waliosaidia kuleta mabadiliko ya kiutendaji ndani ya Idara hiyo.

Kuambatana na msanii Anti Ezekiel hadi Marekani kwa gharama za serikali kwa maelezo kwamba alikwenda kusaidia kutangaza utalii nchini humo ni kashfa ambayo ilimchafua na kuichafua serikali nzima.

Pamoja na taarifa hizo kukanushwa, lakini bado wananchi wanaona kuwa mwanasiasa na kiongozi huyo hakuwa mwadilifu, achilia mbali kuisababishia Mamlaka ya Ngorongoro (NCAA) hasara ya Shs. 15 bilioni kutokana na kushinikiza mamlaka hiyo pamoja na Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) kutoza kiingilio mara moja bila kujali mtu ameingia hifadhini mara ngapi.

Kitendo cha kukaidi hukumu ya mahakama kinatajwa kuigharimu serikali hasara ya Shs. 80 bilioni katika kesi iliyofunguliwa kuhusu tozo kwenye hoteli zilizoko hifadhini, lakini bado mamlaka husika zikakaa kimya na kumwangalia tu.

“Hayupo kwenye uongozi, lakini bado serikali inao uwezo wa kuchunguza na kumshughulikia katika staili ile ile ya ‘kutumbua majipu’ kutokana na ukweli kwamba rasilimali alizokuwa akisimamia ni za umma na ikiwa ametumia madaraka yake vibaya hawezi kukwepa mkondo wa sheria,” baadhi ya wadau wa utalii wameieleza FikraPevu.

---
Makala kutoka FikraPevu