CHAMA cha wananchi CUF kimemuomba Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Pombe Magufuli kukataa kuhadaiwa na kutumia vibaya vyombo vya ulinzi na usalama pamoja na vikosi vya SMZ kwa kuwatia wananchi ghofu na kuanza kukimbia taifa lao jambo ambalo litaiweka nchi pabaya kimataifa.
Chama hicho kilisema hivi sasa tayari idadi kubwa ya majeshi pamoja magari na silaha kamili za kivita yameingia kisiwani Pemba kwa amri ya amiri Jeshi mkuu ambaye ni Rais Maguful na kudai kwamba jambo hilo limewatia ghofu kubwa wananchi na kutokujua khatma ya maisha yao.
Kauli hiyo ilitolewa na kaimu Mkurugenzi wa habari mahusiano na umma CUF Hamad Masoud Hamad alipokuwa akizungumza na wandishi wa habari huko Ofisini kwake Vuga Visiwani hapa.
“Kwa hili ambalo linatokea Pemba ambapo tayari wananchi wameshekimbilia misituni na kuanza kuangalia njia ya kueleka Shimoni, Kenya, Rais Magufuli hana pa kutokea na atawajibika kwa mujibu wa katiba na sheria pamoja na utaratibu wa kuendesha nchi tuluiojiwekea” alisema hamadi.
“Imekuwa ni idhilali kubwa tokea wananchi waikatae CCM na mateso makubwa kwao Visiwani Zanzibar kwa kuamua kufanya mabadiliko ya uongozi” aliendelea.
Alisema uharibifu na uvunjifu wa Amani ukitokea katika kisiwa cha Pemba JWTZ na Rais magufuli ndio ambao watawajibika na kubeba lawama kutokana na kupeleka idadi kubwa ya majeshi.
“Unapeleka majeshi na vifaa vya kivitaa katika sehemu ya nchi yako kama vile umevamiwa na majeshi ya kigeni kwa sababu tu watu wa Pemba wameikataa CCM, tunasema JWTZ ndilo litakalo beba lawama zoote,” alisema Hamad.
Sambamba na hilo hamad alifahamisha kwamba hivi sasa wanachi wa mkoa wa Kaskazini Pemba wameshaambiwa wasionekane nje ifikapo saa mbili usiku alidai jambo ambalo wananchi limewafanya wafikirie kukimbilia Mombasa Kenye.
“Jamani kwani kuna nini Pemba mpaka ifikie hali hii au kwa sababu wamekikataa Chama Cha Mapinduzi? Basi kwa hilo tushakikataa na tutaendelea kukitaa, endeleeni tu na mambo yenu,” alieleza Kaimu huyo mkurugenzi wa Habari CUF.
Alisema wanachokiandaa ni kuwafanya wananchi hao kukimbia makazi yao na kukimbilia Shimoni Kenya kama ilivyokuwa 2001 ambapo zaifdi ya watu 3000 walikimbilia huko.
“Hivi ninavyozungumza na nyinyi hali kisiwani Pemba ni tete kabisaa kwa watu hawana uhakika ya maisha yao” alisema.
Pia akizungumzia kuhusu kamatakamata iloingia kwenye kisiwa hicho alisema ni dhahiri kwamba Jeshi la Polisi linafanya kazi ya CCM badala ya kulinda wananchi na mali zao.
“Hivi nnavyozungumza na ninyi watu zaidi ya 50 tayari wameshakamatwa na kunyimwa dhamana hata makosa wenyewe hayana msingi,” alisema Hamad.
Alitaja baaidhi ya Majimbo ambayo watu hao wamekamatwa ni Pmaoja Konde watu 23, Chake Chake 6 wete 7 kiuyu watatu na kusema maeneo mengine bado hawajakamilisha kuorodhesha na kudai wote ni wananchama wa CUF.
Akizungumza kwa niia ya Simu RPC wa mkoa wa Kaskazini Pemba Hassan Nasir alikiri kuwakamata watu hao na leo waliwapeleka mahakamani na wamewarejesha rumande hadi uchaguzi upite.
“Sisi tumewakata watu ambao tunawashutumu kwamba wamehusika na uchomaji moto nyumba pamoja na majengo ya Serikali na hatujakamata wanachama wa CUF,” alieleza Nasir.
Alisema wanapokamata watu hawangalii kitambuylisho kama ni mtu Fulani asikamatwe bali wanakamta mtu yeyote wanayemshuku.
- Imeandikwa na Talib Ussi, Zanzibar