Jiji la Dar lampata Meya



KAIMU Mkurugenzi Jiji la Dar es Salaam Bi. Sara Yohana amemtanganza Isaya Mwita Charles ambaye ni Diwani wa Kata ya Vijibweni (CHADEMA) kutoka Wilaya ya Temeke kuwa Meya wa Jiji la Dar es Salaam.

Kaimu Mkurugenzi huyo alimtangaza mshindi huyo baada ya kuhesabiwa kura za uchaguzi uliyofanyika leo jijini Dar es Salaam ambapo mshindi alipata kwa kura 84 dhidi ya mgombea mweza kupitia chama cha CCM, Bw. Yenga Yusuph ambaye alipata kura 67 katika uchaguzi ambao kura 7 ziliharibika.

“Tunawashuruku wapiga kura wote mlioshiriki zoezi hili la upigaji kura kwa utulivu bila vurugu na kuweza kulifanikisha mpaka kumpata Meya wa Jiji hili,” alisema Bi Yohana.

Mshindi Mhe. Chacha aliwashukuru wapiga kura wa Vijibweni kwa kumchagua kuwa Diwani pamoja uongozi wa chama chake kwa kukubali kumpa nafasi ya kugombea kiti hicho.

“Nimejipanga kuleta maendeleo katika sekta ya elimu pamoja na kupambana na kero ya foleni katika jiji pia hakikisha wananchi wote maskini wanafaidika na mapato ya jiji hili katika kuendeleza miundombinu mbalimbali ,”alisema Chacha.

Mwenyekiti wa CHADEMA Bw. Freeman Mbowe alisema idadi ya wapiga kura tu inaonyesha wazi kuwa ushindi wa kiti hicho cha meya ni lazima uchukuliwe na CHADEMA sababu madiwani wengi wa Mkoa wa Dar es Salaam wanatoka katika chama hicho.





Isaya Mwita Charles, Meya wa jiji la Dar es Salaam (kushoto) akiwa na viongozi wa CHADEMA katika uchaguzi huo



Meya wa Jiji la Dar es Salaam Isaya Charles (katikati)akizungumza na wananchi juu ya kuwashukuru sana wapiga kura wake wa kata ya Vijibweni kwa kumchagua kuwa Diwani pamoja uongozi wa chama chake kwa kukubali kumpa nafasi ya kugombea kiti hicho, Jiji la Dar es Salaam.


Sehemu ya wafuasi wa CHADEMA waliojitokeza katika uchaguzi huo, leo Jijini Dar es Salaam.