Loading...
Saturday

Kamishna Abbas Irovya akitangaza mabadiliko ya maafisa katika idara ya uhamiaji


IDARA ya Uhamiaji, imetangaza mabadiliko makubwa ya uhamisho wa maofisa wake kutoka makao makuu, mikoani mpaka wilayani, yakihusisha vigogo walio makao makuu na mikoani mpaka wilayani.

Msemaji wa Uhamiaji, Kamishna Msaidizi Abbas Irovya, alisema jana kuwa Kaimu Kamishna Jenerali wa Uhamiaji, Victoria Lembeli, amewabadilisha vituo vya kazi maofisa waandamizi 14 wa mikoa na wilaya kwenda vituo vingine vya kazi.

Mbali na maofisa hao waandamizi, uhamisho huo kwa mujibu wa Kamishna Irovya, pia umewahusu maofisa wengine 200 ikiwa ni sehemu ya kuipanga upya idara hiyo na kujiimarisha kiutendaji.

Vigogo Kamishna Irovya aliwataja maofisa waandamizi na walikopelekwa kuwa ni DCI Faustine Nyaki kutoka Iringa kwenda Mwanza na DCI Remigius Pesambili kutoka Mwanza kwenda kuwa Ofisa Mfawidhi wa Ofisi ya Uhamiaji Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere.

Wengine ni DCI Rose Mhagama anayetoka Njombe kwenda Mtwara, DCI Charles Habe anayetoka Geita kwenda Njombe kuwa Ofisa Uhamiaji wa Mkoa. DCI Assa Mwansansu, yeye anatoka kuwa Mfawidhi Kitengo cha Hati za Ukaazi anahamia mkoani Pwani na aliyekuwa Ofisa Uhamiaji Wilaya ya Ilala, Naibu Kamishna Safina Muhindi, amehamia Morogoro kuwa Ofisa Uhamiaji wa Mkoa.

Wengine ni DCI Wilfred Marwa ambaye alikuwa Naibu Ofisa Uhamiaji wa Mkoa wa Tanga, amehamia Geita kuwa Ofisa Uhamiaji wa Mkoa, wakati DCI Evaristi Mlay, ambaye ni Ofisa Uhamiaji Wilaya ya Kinondoni, amehamia Same kwenda kuwa Ofisa Uhamiaji wa Wilaya na DCI Frank Mwakifuna anayetoka Same anahamia Kinondoni.

Irovya aliwataja maofisa wengine waliohamishwa kuwa ni DCI Pily Mdanku aliyekuwa Ofisa wa Pasipoti Makao Makuu, yeye amehamishwa kuwa Ofisa Uhamiaji Wilaya ya Ilala, wakati DCI George Goda, anayetoka Kitengo cha Hati za Ukaazi Makao Makuu na anaenda Temeke kuwa Ofisa Uhamiaji wa Wilaya na Jafari Kisesa anatoka Temeke na anahamishiwa Tanga ambako anaenda kuwa Ofisa Uhamiaji wa Mkoa.

Julieth Sagamiko ametoka Kitengo cha Pasipoti Makao Makuu, anahamishiwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) kuwa Mfawidhi wa kituo hicho. Aidha, Naibu Ofisa Uhamiaji Mkoa wa Kagera, Kamishna Msaidizi Hosea Kagimbo, amehamishiwa Kituo cha Uhamiaji Holili kuwa Mfawidhi wa kituo hiho.

Maofisa 200 “Pamoja na orodha hiyo, Idara ya Uhamiaji inaendelea na utaratibu wa kuwabadilisha vituo vya kazi maofisa zaidi ya 200 kutoka sehemu mbalimbali nchini, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa agizo la Waziri wa Wambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga,” alisema Kamishna Irovya.

“Uhamiaji imefanya mabadiliko hayo wakati inashutumiwa kuwa maofisa wake watendaji wamekuwa wakichukua rushwa katika utoaji wa hati za makazi kwa wageni pamoja na utoaji wa hati za kusafiria.

Shutuma hizo zilifanya hadi Rais John Magufuli kuwasimamisha kazi Kamishna Jenerali wa Uhamiaji, Sylvester Ambokile na Kamishna wa Utawala na Fedha, Piniel Mgonja.

Baada ya viongozi wa idara hiyo kusimamishwa, Waziri anayesimamia idara hiyo Charles Kitwanga aliagiza watumishi wa Idara ya Uhamiaji walioko katika viwanja vya ndege vya kimataifa vya Julius Nyerere (JNIA), Dar es Salaam na Kilimanjaro (KIA), wahamishwe na kupelekwa maeneo mengine nchini, wakiwemo wale wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano.

Katika maagizo ya waziri huyo, alisisitiza kuwa anataka kuwepo na mabadiliko makubwa katika vitengo mbalimbali vya Idara ya Uhamiaji, ili kuboresha huduma na kuimarisha uadilifu katika vitengo hivyo.

Waziri alitaka uhamisho huo uguse viwanja vya ndege, Kitengo cha Pasipoti, Uhasibu, Hati za Ukaazi na Kitengo cha Upelelezi, vyote vya Makao Makuu ya Uhamiaji jijini Dar es Salaam.

Pia aliagiza wakuu wote wa vitengo vya upelelezi vya wilaya zilizopo jijini Dar es Salaam, Tunduma, Mtukula, Holili na Kasumulo, wahamishiwe maeneo mengine, wakiwemo watumishi wote waliokaa kwa zaidi ya miaka mitatu katika vituo hivyo.

“Hatua hii inayochukuliwa ni mwanzo tu wa mabadiliko makubwa yatakayofanywa katika Idara ya Uhamiaji ili kuboresha huduma zinazotolewa na Idara hii ambayo ni moja ya Idara muhimu za Serikali,” alisisitiza Kitwanga wakati akitangaza maagizo hayo. 

0 comments :

Post a Comment

 
Toggle Footer
TOP