Karatasi za kupigia kura Zanzibar zarekebishwa makosa

Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha, amesema ZEC imefanya marekebisho ya katarasi za kura na zinatarajiwa kufika visiwani humo Machi 17, mwaka huu.

Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari aliyotolewa jana, Jecha alisema baada ya kubainika kasoro katika jina la mgombea wa Chama cha ADA-TADEA, ZEC imefanya marekebisho.

“Tunaishukuru Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa mashirikiano iliyoyaonesha katika kusahihisha kasoro zilizojitokeza na tunapenda kuwahakikishia wananchi na jumuiya za kimataifa kuwa uchaguzi utakuwa wa haki, huru na uwazi,” alisema Jecha katika taarifa yake.

Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) imeanza kutoa mafunzo ya kupiga kura kwa watu wenye ulemavu wa macho, kwa kutumika karatasi za wapigakura zilizokosewa jina la mgombea wa urais wa Zanzibar.

Uchunguzi wa Nipashe umebaini kuwa mafunzo hayo yalianza kufanyika jana mjini Zanzibar na kuratibiwa na Jumuiya ya Wasioona Zanzibar (ZANAB) chini ya ufadhili ya ZEC.

Karatasi za wapigakura ziliwasili Zanzibar Machi 11, mwaka huu, kutoka Afrika Kusini, lakini katika karatasi za wapigakura zimebainika kuchapishwa kimakosa jina la mgombea urais kupitia chama cha TADEA kwa kuandikwa Khatib Ali Khatib badala ya Juma Ali Khatib.

Mkufunzi wa mafunzo hayo, Fatma Dijaa Chersa, amethibitisha kufanyika kwa mafunzo hayo kwa watu wenye ulemavu wa macho kabla ya kufanyika uchaguzi wa marudio Jumapili ijayo.

Alisema washiriki 50 watapatiwa mafunzo juu ya upigaji kura kwa watu wenye ulemavu wa macho kwa kutumia karatasi za mfano za wapigakura, zikiwa na maandishi maalumu ya alama nundu, hatua ambayo itawawezesha watu wenye ulemavu kupiga kura bila msaada.

Alisema washiriki hao wamechaguliwa kutoka katika wilaya za Unguja na baadaye watatakiwa kwenda kusadia kuwaelimisha wenzao.

Hata hivyo, alisema kikosewa kwa jina la mgombea, hakutaleta madhara kutokana na watu wenye ulemavu wa macho kupiga kura kwa kuangalia jina la chama chumba namba cha mgombea badala ya jina la mgombea.

Hata hivyo, Mwenyekiti wa ZEC, Jecha Salim Jecha, alisema chagamoto uliyojitokeza ya kukosewa jina la mgombea katika karatasi za wapigakura, imeanza kufanyiwa kazi kwa kurekebisha makosa hayo.

“Tayari hatua stahiki zimeshachukuliwa, marekebisho yameshafanyika na karatasi zinatarajia kufika Machi 17 (kesho) mwaka huu,” alisema.

Uchaguzi Mkuu wa marudio Zanzibar umepangwa kutafanyika Jumapili, huku mjadala mkubwa Zanzibar kuhusu hatima ya karatasi za wapiga kura zilizochapwa kimakosa ukitawala.