Kasheshe la mwekezaji wa NMC Arusha vs serikali


Serikali imeshindwa kuipokonya kampuni ya Monaban Trading & Farming uendeshaji wa Shirika la Usagishaji la Taifa (NMC) tawi la Arusha na badala yake, katika mazingira tata, imeongezewa miaka 10 kuanzia 2014.

Habari ambazo Mwananchi imezipata zinasema kuwa tangu mwaka 2008, wajanja wachache serikalini wamehusika katika njama za kuzuia shirika hilo kurejea mikononi mwa Serikali na baadaye kukabidhiwa kwa Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko (COPB).

Taarifa kutoka kwa viongozi kadhaa na nyaraka mbalimbali zinaonyesha kuwa katika kikao chake cha Novemba 7, 2008, Baraza la Mawaziri lilijadili na kushauri mali zote za NMC zilizoko chini ya mwekezaji huyo zichukuliwe na kukabidhiwa kwenye bodi hiyo baada ya kuona uwekezaji huo haukuwa na tija kwa Taifa.

Mali za NMC zilizotakiwa kukabidhiwa kwa Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko tangu mwaka 2008 ni mashine za unga zenye uwezo wa kuzalisha tani 47,000 kwa mwaka, maghala yenye uwezo wa kihifadhi tani 38,000 pamoja na nyumba kadhaa. Mali zote za NMC zilizopo Arusha zinakadiriwa kuwa na thamani ya zaidi ya dola 100 milioni za Marekani, zikiwa katika eneo lenye ukubwa wa heka 4,489.

Mbali ya mashine na maghala, NMC inamiliki nyumba za wafanyakazi mjini Arusha ambazo mpaka sasa hazijulikani ziko chini ya nani.

NMC ni moja ya mashirika ya umma yaliyoshindwa kujiendesha ambayo yaliwekwa chini ya Tume ya Rais ya Kurekebisha Mashirika ya Umma (PSRC). Baadaye PSRC ilivunjwa na likaundwa Shirika Hodhi la Mali za Mashirika ya Umma (CHC) na lilikabidhiwa mashirika machache ambayo hayakubinafsishwa, likiwamo tawi la NMC mkoani Arusha.

CHC ilifanikiwa kurejesha mali za NMC zilizokuwa katika mikoa ya Iringa Aprili 2011; Mwanza, Aprili 2012 huku mali za Dodoma zikirejeshwa Agosti 2013. Lakini mali za NMC Arusha hazikurejeshwa na badala yake zikaachwa kuendelea kuwa mikononi mwa mwekezaji ambaye Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA).

Agosti 23, 2007 kampuni ya Monaban iliingia mkataba wa miaka mitano na NMC wa kukodisha mali zote za shirika hilo zilizopo eneo la Unga Limited, yakiwamo maghala na kinu cha kusaga unga.

Juni 23 mwaka 2014, mwekezaji huyo aliingia mkataba mwingine na CHC ambao unatarajiwa kuisha mwaka 2023.

Ingawa uamuzi ulifikiwa mwaka 2008 na ukasisitiziwa Februari 4, 2011 na aliyekuwa Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Profesa Jumanne Maghembe alipokuwa akizindua COPB, hakuna kilichofanyika na badala yake ni mawaziri wa Serikali ya Rais Jakaya Kikwete kushindana kuandika barua zinazopingana kuhusu uwekezaji NMC.

Juni 24, 2014 ilipewa mkataba mwingine wa miaka 10 ambao unatarajiwa kuisha mwaka 2023. Mkataba huo mpya uliongezwa huku Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko ikiwa imeshamwandikia barua katibu mkuu wa Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika Novemba 20, 2013 kumueleza kuwa hawautambui mkataba wa NMC na Monaban kwa kuwa serikali iliuona kuwa hauna manufaa kwa Taifa.

Vilevile, Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko katika barua hiyo kwa katibu mkuu ikimtahadharisha kuwa kukosekana kwa msimamizi wa mali za NMC zilizopo Arusha kutaikosesha serikali mapato, kwa kuwa Monaban hailipi tozo kutokana na shughuli inazoendesha.

Barua juu ya barua

Mwaka 2013, CHC ilimwandikia barua katibu mkuu wa Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika kumtaarifu kuhusu mali hizo na kwamba wanataka kutekeleza agizo la Baraza la Mawaziri la kukabidhi mali hizo kwa Bodi.

Katika barua hiyo Agosti 16,2013, ambayo nakala yake ilipelekwa Bodi ya Nafaka na Mazao Mchaganyiko walieleza kuwa kazi hiyo wataifanya Agosti 31, 2013.

Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko, kupitia barua ya Agosti 29, 2013 ilikubali kukabidhiwa mali hizo kama ilivyokubaliwa na Baraza la Mawaziri.

Mwkaa huo Agosti 30, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko, Elimpaa Kiranga alifika mjini Arusha akiwa ameambatana na Ofisa Ugavi wa Bodi, Alfan Semindu na Mwanasheria wa Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika, Ernesto Doriye kwa ajili ya makabidhiano.

Hata hivyo, makabidhiano hayo yalikwama kufanyika kutokana na maagizo kutoka ofisi ya mkuu wa Mkoa wa Arusha ambayo yalitaka kusitishwa kwa shughuli hiyo mpaka itakapojulikana hatima ya fedha zilizotumiwa na Monaban kuwekeza kwenye kiwanda hicho.

Baada ya makabidhiano kushindikana, Septemba 23, 2013, Bodi hiyo iliamua kulifikisha suala hilo kwa Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika.

“Mheshimiwa waziri, kutokana na suala hili la makabidhiano ya mali katika kinu cha Arusha kutokamilika kwa agizo la uongozi wa Mkoa wa Arusha, napenda kuliwasilisha suala hili kwako kwa hatua zaidi ili liweze kutafutiwa ufumbuzi wa haraka, Bodi ikabidhiwe mali hizi kama ilivyoagizwa na Serikali,” inasema barua hiyo iliyotiwa saini na Kiranga.

Septemba 19, 2013 Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Sophia Kaduma alijibu barua ya Kiranga akielekeza mali za NMC Arusha zikabidhiwe kwa Bodi hiyo kama ilivyoagizwa na Serikali.

Katika barua hiyo, Wizara ilipendekeza baada ya Bodi kukabidhiwa inaweza kuipangisha Monaban kwa mkataba wa muda mrefu ili iweze kurejesha fedha ilizowekezwa katika kinu hicho.

Baada ya Stephen Wasirra kuteuliwa kuwa waziri, alikutana na viongozi wa Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko Februari 3, 2015, mjini Dodoma na aliiagiza taasisi hiyo ya serikali ikabidhiwe kinu cha Arusha kama ilivyoagizwa na waraka wa Baraza la Mawaziri namba 40/2008.

Juhudi za Bodi kukabidhiwa kinu hicho zilififia Novemba 27, 2013 baada ya ofisi ya Waziri Mkuu, kupitia kwa aliyekuwa Waziri wa Nchi, Uwezeshaji na Uwekezaji, Mary Nagu kutoa maagizo tofauti kwa CHC kwamba kampuni ya Monaban ipatiwe maghala yote ya kuhifadhia nafaka na kwamba iwe mkodishaji pekee hadi uamuzi wa Serikali juu ya kinu hicho utakapotolewa.

Katika barua hiyo, ofisi ya Waziri Mkuu ilishauri kuwa mwekezaji huyo asibughudhiwe katika shughuli zake. Uamuzi huo ulikinzana moja kwa moja na ule wa Baraza la Mawaziri ambao ulitolewa miaka sita iliyopita kwamba mali za NMC zirejeshwe serikalini.

Mkanganyiko huo uliivutia Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) ambayo ilianza kufuatia kujua kama kuna harufu ya rushwa. “Suala hilo lipo lakini linashughulikiwa na makao makuu, mimi siwezi kulizungumzia kwa kuwa nitaingilia uchunguzi,” alisema kamanda wa Takukuru Mkoa wa Arusha, Juventus Baitu.

Mkurugenzi wa Monaban Trading and Farming Co Ltd, Philemon Mollel alipoulizwa kuhusu suala hilo alisema ameshindwa kukabidhi kwa kuwa mpaka sasa ametumia fedha nyingi kuwekeza katika kinu hicho na hajui hatima yake.

Alisema alipoingia mkataba wa upangaji aliwekeza Sh6.2 bilioni kwa ajili ya ukarabati wa kinu cha kusaga ngano na kwa utaratibu maalumu fedha hizo zingerejeshwa kupitia tozo iliyopaswa kulipwa.

Mollel alitaja uwekezaji alioufanya katika eneo hilo kuwa ni kujenga ukuta kuzunguka kiwanda, kuweka sakafu ya matofali madogo kwenye eneo lote, kutengeneza na kuweka mashine ya kusaga na kuweka mfumo wa majitaka, kukarabati na kuweka mashine yenye uwezo wa kusaga mahindi na mtama tani 120 tofauti na ile iliyokuwapo awali iliyokuwa na uwezo wa kusaga tani 60.

Uwekezaji mwingine ni mashine ya kukamua mafuta ya alizeti, kuweka jenereta lenye uwezo wa kuzalisha umeme wa KVA 300, kuchimba kisima cha maji na kuanzisha kiwanda cha kisasa cha mikate.

Alipoulizwa sababu za kutumia fedha nyingi kuwekeza katika kiwanda ambacho si mali yake, Mollel alisema alifanya hivyo akiamini kuwa yeye ni Mtanzania mzalendo atauziwa kama walivyouziwa watu wengine mali za NMC sehemu mbalimbali nchini.

Hata hivyo, alisema ana matumaini ya kupatikana ufumbuzi suala hilo baada ya Waziri wa Viwanda na Biashara, Charles Mwijage kutembelea kiwanda hicho hivi karibuni na kuahidi kuwa atalifanyia kazi.

Kiranga alipoulizwa alisema wana matumaini makubwa kuwa suala hilo litakwisha na kwamba sasa Serikali itaanza kunufaika na mali zake ambazo zilikuwa zinatumika kwa maslahi ya mtu mmoja.