Loading...
Saturday

Kasulu yasimamisha maafisa 3 wa wakala wa misitu

KAMATI ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma, imewasimamisha kazi na kuwakamata maafisa watatu wa Wakala wa Misitu Tanzania, TFS, katika wilaya hiyo kosa la kufanya udanganyifu katika uvunaji wa mazao ya misitu wilayani humo kufuatia kukamata zaidi ya mbao elfu moja zikiwa zimevunwa kinyume cha sheria.

Akizungumza baada ya ukaguzi wa ghafla uliofanywa katika kijiji cha Mvugwe na kukamata mbao hizo, Mwenyekiti wa kamati hiyo ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Kasulu, Gerald Guninita, amewataja maafisa hao kuwa ni Meneja wa Wakala wa Misitu Wilaya ya Kasulu Donald Slaa, na wafanyakazi wawili wa TFS William Skoi na Jonathan Kaiza.

Alisema mbao zilizokamatwa zimebainika kutogongwa muhuri wa serikali ambao hugongwa kwenye mbao na kwamba kibali cha mmoja wa wafanyabiashara kinaonyesha anatakiwa kuwa na mbao 150 lakini amekutwa akiwa na zaidi ya mbao 700.

Aidha alisemaa uchunguzi wa awali umeonyesha kuwa maafisa hao walikwenda kuhalalisha mbao hizo kwa kugonga muhuri sehemu ya mbao hizo nyumbani kwa mfanyabiashara badala ya kugonga zikiwa porini baada ya kupasuliwa kama sheria zinavyotaka.

Alisema kutokana na hali hiyo kamati ya ulinzi na usalama wilaya imejiridhisha kuwa maafisa hao wamekwenda kinyume cha sheria na taratibu hivyo wamekabidhiwa polisi ili wachunguze na kuwafungulia mashtaka na kwamba vitendo vinavyofanywa na maafisa hao ni hujuma kwa kuwa walikuwa wakishirikiana na wafanyabiashara kuvuna raslimali misitu katika wilaya hiyo.

Aliongeza kuwa pamoja na maafisa hao polisi pia inamshikilia mfanyabiashara Fera Jumanne na wanamtafuta Kenedy Masatu kuhusiana na tuhuma za kuvuna mbao bila kibali.

Hata hivyo akizungumza na waandishi wa habari mfanyabiashara Kenedy Masatu, alisema ana vibali vyote vinavyomruhusu kufanya biashara hiyo na kwamba hatua ya baadhi ya mbao kugongwa muhuri na nyingine kutogongwa inatokana na uwingi ambapo mgongaji hulazimika kugonga asilimia kubwa ili kuhalalisha nyingine.

”Hapa kuna mbao nyingi ni vigumu kugonga zote kutokana na mazingira yake lakini asilimia 99 ya mbao zimegongwa hivyo na ambazo hazijagongwa ni kutokana na kuwa katika mazingira yasiyofaa” alisema mfanyabiashara huyo.

---

 
Toggle Footer
TOP