Katibu Mkuu wa CHADEMA ni Dk Vincent Mashinji

Vincent B. Mashinji, MD, (Clinical Advisor & TB/HIV lead, UMSOM-IHV)
Vincent B. Mashinji, MD, (Clinical Advisor & TB/HIV lead, UMSOM-IHV)
Vincent Mashinji, daktari wa binadamu (MD) ameteuliwa kuwa Katibu Mkuu mpya wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na kisha kupitishwa na Baraza Kuu la CHADEMA, katika kikao chake kilichokaa jijini Mwanza.

Dk Mashinji anachukua mikoba iliyoachwa na Dk Wilbrod Slaa aliyejiengua katika chama hicho mwaka jana, miezi michache tu kabla ya kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu wa Tanzania 2015, baada ya chama hicho kumpitisha Edward Lowassa aliyetokea CCM kuwa mgombea kiti cha Urais wa Tanzania kupitia vyama vinavyounda UKAWA (Umoja wa Katiba ya Wananchi).

Katika Kikao cha Baraza Kuu kilichofanyika usku wa Jumamosi, Machi 12, 2015 Mwenyekiti wa chama, Freeman Mbowe alilitangaza jina la Dk. Mashinji ambalo liliungwa mkono na wajumbe wa baraza.

Jina la Dk. Mashinji halikuwa miongoni mwa wanachama wa CHADEMA ambao walikuwa wanatarajiwa kumrithi Dk. Slaa kwani waliokuwa wanatabiriwa kukalia kiti hicho walitajwa kuwa ni Salum Ally Mwalimu, Frederick Sumaye, Benson Kigaila, John Mnyika, Dk. Marcus Albanie na Prof. Mwesiga Baregu.

Akizungumzia uteuzi wake, Dk Mashinji alisema Mbowe alimwalika katika chakula cha mchana (bila kutaja siku) na kumdokeza juu ya kumpa nafasi hiyo. “...sikuamini lakini Mbowe akaendelea kunisisitizia.” Aliesema Mashinji.

Dk. Mashinji anakuwa katibu mkuu wa nne wa CHADEMA tangu chama hicho kianzishwe baada ya Bob Makani, Dk. Walid Aman Kabourou na Dk Slaa.

Mara baada ya kuchaguliwa, Dk Mashinji aliwataka wanachama wa CHADEMA kushirikiana katika kujenga mfumo badala ya kuliacha jukumu hilo kwa watu wachache tu.

Dk Mashinji ambaye alishiriki katika kuandaa Ilani ya Uchaguzi ya CHADEMA na UKAWA kwa ujumla katika Uchaguzi Mkuu uliopita, aliahidi kujifunza na kusema kuwa atashaurika.

‘Kipaumbele chetu ni katiba ya wananchi. Ni kitu cha kwanza tutakachokisimamia. Tunachohitaji kwa sasa ni kufumua mfumo wa kiutawala kwa kuwa kumekuwa na mwingiliano wa kimajukumu. Kingine ni kwenda kuuwezesha umma uweze kutambua haki zao na uwe tayari kutetea haki zao," alisema Dk Mashinji,

Wasifu wa Mhe. Dk Mashinji...