Kijana msomi, J. Kayonge aeleza wanavyofanikiwa katika kilimo cha vitunguu



VIJANA wasomi wanaounda Taasisi ya Maendeleo ya Vijana Tanzania (TAYODA) wameeleza mafanikio wanayopata baada ya kuamua kujikita katika kilimo cha vitunguu tangu mwaka 2013, muda mfupi baada ya kumaliza elimu yao ya vyuo vikuu.

Vijana hao wanaomiliki shamba lenye ukubwa wa heka 300 katika kijiji cha Idodoma wilayani Mpwapwa mkoani Dodoma, wamewataka vijana wanaolalamika kukosa ajira, kuunga mkono kauli ya hivikaribuni ya Rais Dk John Magufuli inayowataka wafanye kazi badala ya kucheza pool toka asubuhi.

Akizungumza na wanahabari waliotembelea shamba lao hilo hivikaribuni, Mkurugenzi wa TAYODA, Jackson Kangoye alisema; “taasisi imefanikiwa kukuza mitaji ya vijana walioko mitaani kwa kupitia sekta hii ya kilimo.”

Alisema mwaka 2013 walipoanza na vijana 25 walifanikiwa kulima zao hilo katika shamba lenye ukubwa wa heka 30, wakaendelea kupata mafanikio yaliyowazesha kupata shamba lenye ukubwa wa heka 300 huku idadi ya vijana wanaojishughulisha na kilimo hicho ikiongezeka hadi 230 mwaka huu.

“Lengo letu katika kipindi cha miaka mitatu ni kuwaingiza katika shughuli hii vijana 2500 walioko mitaani bila kujali viwango vya elimu,” alisema.

Kangoye alisema wakiwa shambani vijana hao ugawanywa katika makundi ya watu watano ambapo kila kundi hupewa heka tano kwa msimu mmoja na kuzitumia kupata mitaji.

“Tangu tuanze kilimo hiki uzoefu wetu unaonesha kwa kila heka moja, tunazalisha kati ya gunia 80 na 120 za zao hilo ambalo uuzwa kwa kati ya Sh 120,000 na Sh 170,000 ambazo ni sawa na wastani wa Sh Milioni 10 na Sh Milioni 20 kwa heka,” alisema.

Alisema kiasi kinachobaki baada ya kutoa asilimia 25 ya pato lote linalokwenda katika taasisi hiyo kwa ajili ya kusaidia vijana wengine na gharama zote za matumizi, hutolewa kwa vijana hao kama mtaji wanaoweza kuutumia kujiendeleza katika kilimo hicho katika mashamba yao wenyewe.

Kangoye alisema zaidi ya vijana 120 wamekwishanufaika kiuchumi kupitia mpango huo kwa kuanzisha miradi yao ya kilimo cha vitunguu, pilipili, tikiti na nyanya.

Mmoja wa vijana aliyenufaika na mpango huo, Kassara Mageni alisema; “baada ya kumaliza Chuo Kikuu cha Dodoma mwaka 2012, sikutaka kubweteka kusubiri kuajiriwa. Nimehamia shamba, nalima na ninawasimamia vijana wenzangu kupitia taasisi hii ya TAYODA kujiletea maendeleo.”

Mbali na kujipatia mapato makubwa kutoka katika mashamba anayolima, alisema mpango wake ni kuhamishia maisha yake moja kwa moja katika kijiji hicho.

“Wasomi wengi tuna ndoto ya kupata mafanikio ya haraka tena kupitia kazi za kuajiriwa, bahati mbaya wengi wetu tunachelewa kufikia ndoto hiyo, niwajulishe wasomi wenzangu maisha yako huku, sekta ya kilimo ina fursa kubwa inayoweza kubadili maisha yetu vijijini na mijini,” alisema.

Kwa upande wake kijana mwingine, Gapi Yohana alisema kwa miaka miwili ambayo amefanya kazi na taasisi hiyo ameweza kuongeza ukubwa wa shamba lake kutoka heka moja hadi tano pamoja na kujiimarisha kiuchumi ikiwa ni pamoja na kununua pikipiki pamoja na kiwanja anachotarajia kukitumia kujenga nyumba yake ya kisasa.





Imenukuliwa kutoka kwenye blogu ya Frank Leonard