Loading...
Monday

Mabalozi waanza kurejea; Waziri ataja mustakabali wao kwa mujibu wa kanuni

Mabalozi watatu wa Tanzania nje ya nchi wameanza kurejea nyumbani baada ya mikataba yao kuisha huku wengine wakiendelea na maandalizi.

Waziri wa wizara hiyo, Dk Augustine Mahiga aliwataja mabalozi ambao wamerejea nyumbani kuwa ni Dk James Msekela (aliyekuwa Roma, Italia) na Peter Kallaghe (aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Uingereza na kutangazwa kuhamishiwa Brazil) huku Dk Batilda Burian (aliyekuwa Tokyo, Japan) akielezwa kuwa yupo njiani kurejea.

“Kuwarudisha watu wengi kwa mkupuo ni gharama, ndiyo maana hawa wanarudi kwa awamu. Nafikiri siku za karibuni Dk Batlida atakuwa hapa nchini baada ya utaratibu kukamilika,” alisema Dk Mahiga ambaye aliwahi kuwa Balozi wa Tanzania kwenye ofisi ya Umoja wa Mataifa (UN).

“Kuwarudisha mabalozi na watumishi hawa ni gharama kwani wanahitaji marupurupu yao na kusafirisha mizigo na wakati mwingine haikuwa kwenye kasma yetu, lakini watarudi kwa kuwa tumeshapata fedha za kuwagharimia,” alisisitiza Balozi Mahiga.
 Alisema kuna aina mbili za mabalozi ambao ni wale wanaokuwa wafanyakazi wa wizara hiyo na wengine ni kutoka nje ya wizara.
  1. Alisema balozi akiwa mfanyakazi wa wizara hiyo huwa anakuwa na ukomo wa kuitumikia nafasi hiyo kisheria na kumpa Rais nafasi ya kumuongezea muda usiozidi miaka miwili ikibidi.
  2. Mabalozi ambao siyo wafanyakazi wa wizara hiyo, muda wao ukiishi wa kuitumikia nafasi hiyo na kama hawajafikia umri wa kustaafu, hurudishwa nchi na kupangiwa kazi nyingine.
Februari 15, mwaka huu, Rais Magufuli aliwateua aliyekuwa Waziri wa Sheria na Katiba katika serikali ya awamu ya nne, Dk. Asha-Rose Migiro, Waziri wa zamani wa Mambo ya Ndani, Mathias Chikawe na Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Dk. Ramadhan Dau kuwa mabalozi.

Tarifa ya Ikulu juu ya uteuzi wao iliyotolewa na Balozi Sefue ilieleza kuwa vituo vya mabalozi hao wapya vitajulikana baada ya taratibu husika za kidiplomasia kukamilika.

Dk. Mahiga alitolea ufafanuzi kuwa kuwapeleka na kuwarudisha watumishi ni gharama kubwa ambayo inahitaji maandalizi.

Hadi sasa baadhi ya vituo vya ubalozi vilivyo wazi ni:
  • London (Uingereza)
  • Tokyo (Japan)
  • Roma (Italia)
  • Brussels (Ubelgiji) kutokana na aliyekuwa Balozi Dk. Deodorous Kamala kuchaguliwa kuwa mbunge
  • Kuala Lumpur (Malaysia) kutokana na Balozi Dk. Aziz Mlima kuteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa na Brasilia, Brazil baada ya Balozi Francis Malambugi kustaafu.
Sehemu ya taarifa imenukuliwa kutoka kwenye magazeti ya MWANANCHI na NIPASHE

0 comments :

Post a Comment

 
Toggle Footer
TOP