Mambo 3 ambayo Anna Mghwira angependa kumwona Rais Magufuli akiyapa kipaumbele

Anna Mghwira
Anna Mghwira
Aliyekuwa mgombea wa urais kwa tiketi ya ACT – Wazalendo, Anna Mghwira amesema iwapo atakutana na Rais John Magufuli atamweleza mambo matatu ambayo haonekani kuyapa kipaumbele katika utawala wake likiwamo la kuharakisha mchakato wa Katiba Mpya.

Mghwira alisema Dk Magufuli ameanza vizuri uongozi wake kwa kutekeleza mambo mengi ambayo hata yeye alipanga kuyafanya iwapo angekuwa Rais lakini yapo baadhi yanayotakiwa kurekebishwa.

Katika mahojiano maalumu yaliyofanyika hivi karibuni, Mghwira alisema Katiba lingekuwa la kwanza kumweleza Dk Magufuli kwani mpaka sasa hajaonyesha mwelekeo wa kuendeleza mchakato wake licha ya kutangaza kwamba angechukua hatua.

Mwenyekiti huyo wa ACT – Wazalendo alisema ingekuwa vyema angeanza sasa kutekeleza mchakato huo ambao ulikwama katika hatua ya kupigia kura Katiba inayopendekezwa baada ya uandikishaji wapigakura kuchelewa mwaka jana.

Akizindua Bunge la Kumi na Moja Novemba mwaka jana, Dk Magufuli alisema ataendeleza mchakato wa Katiba Mpya bila kueleza kinagaubaga hatua atakayoanzia kutokana na Katiba Inayopendekezwa kupingwa na sehemu kubwa ya wanasiasa na watetezi wa haki za binadamu.

“Serikali iliyopo itusaidie kupata Katiba Mpya, halisi, inayokubalika na yenye maoni ya Watanzania na siyo hiyo Katiba Inayopendekezwa iliyopatikana kwa misingi ya vyama,” alisema.

Mchakato huo uanzie katika hatua ipi? Kwa Mghwira, unapaswa kuanzia katika Rasimu ya Katiba Mpya iliyotolewa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyokuwa ikiongozwa na Jaji Joseph Warioba kwa kuwa ndiyo yenye maoni ya wananchi.

Alisema mchakato huo ulikwamia hapo licha ya kwamba hata katika hatua za awali za ukusanyaji maoni kulikuwa na upungufu.

Mara kadhaa Mghwira ameonekana kumshawishi Rais kuendeleza mchakato huo kwani alifanya hivyo Dk Magufuli alipokuwa akikabidhiwa cheti cha ushindi wa urais Oktoba 29, mwaka jana.

Mghwira aliyeshika nafasi ya tatu katika uchaguzi huo, alitaja jambo la pili ambalo Rais Magufuli anatakiwa kulitekeleza kuwa ni kurasimisha mfumo wake wa utumbuaji majipu katika utumishi wa umma ili ufuate misingi ya kisheria badala ya kuongozwa na utashi wa kisiasa.

“Kwa mfano, kama sheria ya bandari ilitoa mwanya kutokana na vifungu vyake, au wasimamizi wa bandari wameitumia vibaya sheria kujinufaisha kama ilivyotokea sasa mpaka wametumbuliwa, hatua zilizochukuliwa zilitakiwa ziingie kwenye sheria.

“Hii itafanywa ama kwa kuboresha sheria au kutungwa mpya kwa kuipeleka bungeni na alitakiwa afanye hili ndani ya siku 100 ofisini ili tumpime” alisema Mghwira.

Alisema kinachofanyika sasa katika uboreshaji wa mfumo wa utumishi wa umma ni hatua za kisiasa kwa kuwa akija kiongozi mwingine anaweza kuwarudisha vigogo wote waliotumbuliwa kwa kuwa hakuna sheria itakayomzuia.

Alisema hivi sasa kila wakati wananchi wapo makini kusikiliza taarifa ya habari kuona nani katumbuliwa kana kwamba kutumbuliwa kwa vigogo hao kutawapatia shibe jambo ambalo siyo sahihi.

Alisema Rais anatakiwa akaimishe madaraka kwa viongozi wa chini katika utumbuaji majipu kadri awezavyo na azuie utumbuaji kwa misingi ya masilahi binafsi.

Katika jambo la tatu, mwanasheria huyo alisema hadi sasa Dk Magufuli hajaonyesha kuwa ni mtu wa wanawake kwa kujali usawa wa kijinsia katika uteuzi wa nafasi mbalimbali za uongozi.

“Ama haoni, haelewi au hataki... kwa vyovyote vile lipo mojawapo hapo. Siwezi kumsemea lakini ni mzito na yupo tofauti na mtizamo wa Hayati Baba wa Taifa (Mwalimu Julius Nyerere) aliyekuwa anatafuta ubora katika uteuzi wa wanawake lakini yeye anaonyesha uongozi ni wanaume.” Alisema ameteua wanawake wachache na kwamba kuna haja kuwaongeza.

Alipoulizwa iwapo kuna tatizo katika uteuzi wa wanaume wengi, alisema hakuna lakini wanatakiwa kuonyesha kuwa ni viongozi bora kuliko wanawake 100 walioachwa.

Alisema hata kama Dk Magufuli angeteua wanawake wote, nchi isingetetereka kwa kuwa kwa miaka zaidi ya 50 wanaume wameongoza na hakuna kilichobadilika.

“Wanawake katika nchi hii ni wengi kuliko wanaume, asiwapuuze. Kuna msemo unaosema ‘usipuuze nguvu ya wajinga walioungana’. Wanawake tunachangia pato kubwa la Taifa, tunalea watoto wa Taifa la kesho... hivyo atushirikishe na sisi katika uongozi,” alisema Mghwira.

Kuhusu mikakati ya kudhibiti mianya ya ukwepaji kodi na ukuzaji uchumi, alisema Serikali ya Awamu ya Tano inafanya vizuri lakini inatakiwa ibane mianya yote ya wizi badala ya kusimamia tu Bandari ya Dar es Salaam wakati mipaka mingi nchini ipo wazi na bidhaa zinaingizwa kwa magendo.