Matatizo ya wasomi na vijana: Tunaamini mtaji ni fedha, tunasahau mtaji wa kwanza ni akili

Gerald Magooge
Gerald Magooge

Miongoni mwa vilio vinavyotawala kila kukicha katika Taifa letu hususani miongoni mwa vijana, ni suala la ukosefu wa ajira.

Takwimu za hivi karibuni za Serikali kuhusu ajira zinaonyesha kuwa kila mwaka jumla ya vijana 1,200,000 wanamaliza mafunzo ya elimu katika ngazi mbalimbali za elimu. Kati yao ni vijana 200,000 pekee ndiyo wanaofanikiwa kupata ajira katika sekta iliyo rasmi, huku 1,000,000 wakiwa hawajulikani wanakoelekea baada ya kumaliza masomo.

Ukweli ni kwamba kundi hili la zaidi ya vijana milioni moja linalotemwa na vyuo vyetu kila mwaka, limezagaa mitaani likiwa halina kabisa mbinu mbadala za kujinasua kutoka katika lindi la umaskini licha ya kutumia miongo mingi darasani na rasilimali nyingi za Taifa katika kuwaondolea adui ujinga vichwani mwao.

Ni kundi hili la vijana ambalo ukibahatika kukutana nalo mtaani utakuta limebeba makabrasha makubwa ya vyeti na nyaraka mbalimbali za kitaaluma zenye kuonyesha ufaulu wao mzuri darasani. Hata hivyo, ukiwategea sikio na kusikiliza maongezi yao hakuna utakachoambulia zaidi ya malalamiko dhidi ya Serikali na taasisi za binafsi kwa kuwanyima ajira au kutoa ajira kwa upendeleo. Ukitaka kuoga mvua ya matusi basi jaribu kuwagusia suala la kujiajiri hususani katika sekta ya kilimo iliyojaa fursa lukuki.

Wasomi hawa wa makabrasha watakuambia uwape mtaji wa kujiajiri wakimaanisha fedha bila kujua kwamba fedha ni silaha ya mwisho kabisa katika masuala ya ujasiriamali na biashara. Kwao baada ya kuwapa fedha na kuhakikisha wamezishika mkononi ndipo huanza kutafakari nini cha kufanya kupitia fedha hizo!

Vijana wetu hawa wamekuwa wakilalamikia upatikanaji mgumu wa mashamba kwa ajili ya kilimo, ilhali ukienda katika bonde la Mto Ruvu au Mto Rufiji mkoani Pwani unakodishiwa mashamba kwa bei ya kutupwa na wenyeji wa maeneo hayo waliojaa ukarimu usio na kifani!

Tunaona jinsi mikoa ya Lindi na Mtwara inavyoinukia kwa kasi kiuchumi kutokana na ugunduzi wa gesi asilia na ujenzi wa viwanda kikiwamo Kiwanda cha Saruji cha Dangote. Kiwanda hiki kinaelezwa kuwa miongoni mwa viwanda vikubwa vya saruji barani Afrika. Ni wazi kwamba viwanda hivi vitavutia ongezeko la watu kutoka mataifa mbalimbali kwa ajili ya kusaka ajira. Ziko wapi harakati za kifikra za vijana wetu waliomaliza vyuo katika kuhakikisha wananufaika na fursa mbalimbali za kiuchumi zilizoanza kuzalishwa na viwanda hivi?

Mbuga zetu za wanyama zilizotapakaa kila kona ya nchi hii zimejaa mahoteli ya kifahari yanayoishia kuagiza nyanya, pilipili na mchicha kutoka ughaibuni kwa kuwa wakulima wetu hawalimi kwa kuzingatia viwango vya ubora vya kimataifa, wako wapi vijana makini wenye kuiona hii fursa na kuamua kuifanyia kazi? Mpaka sasa Serikali inaendelea kuchanja mbuga kupeleka umeme maeneo ya vijijini kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA). Hii ni fursa mpya kwa vijana hasa wasomi kwa kushirikiana na wenzao ambao hawakubahatika kufika mbali kielimu kuanzisha viwanda vidogo vidogo vya kusindika mazao ya chakula kwani umeme utakuwa wa uhakika.

Matatizo ya wasomi na vijana

Tatizo la vijana wengi barani Afrika, ni kupenda maisha ya mkato na ya mteremko. Wasomi wetu hawataki kuumiza vichwa na kujitosa katika uwanja wa mapambano ya kiuchumi kama ilivyo kwa wenzetu wa mataifa mengine.

Wakati vijana wenzetu wakiumiza vichwa kubuni programu mbalimbali za Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) kama Whatsapp, Facebook na Instagram, vijana wa Kitanzania na Afrika kwa jumla tunabuni makundi mapya ya kupiga soga katika mitandao hiyo!

Vijana wa sasa hatushauriki, hatuambiliki na hatukubali kukosolewa. Tukipewa wazo la kuanzisha biashara ya kufyatua tofali tutataka tupewe mashine za kufyatulia, lori la kusombea mchanga, saruji za bure, fedha za kujilipa posho na kisha tuchimbiwe kisima cha maji. Na bado tutalalamika kwamba hatujatafutiwa masoko ya matofali hayo!

Wengi tunaamini kuwa mtaji ni fedha, tunasahau kuwa mtaji wa kwanza maishani ni akili. Kama wahitimu wa Tanzania na vijana kwa jumla, hatutabadili fikra na mitazamo kuhusu maisha, mitaji ya kifedha kutoka serikalini au kwa wahisani haitakuwa na tija. Shime vijana, tuache kulalamika kila mara na badala yake tutumie matatizo hayo kama fursa za kufanikiwa katika maisha.
  • Imeandikwa na Gerald Magooge na kuchapishwa katika gazeti la MWANANCHI. Magooge ni mhitimu wa biashara Chuo Kikuu Dodoma, aliyeamua kujiajiri katika sekta ya kilimo. 0716 78 45 77