Loading...
Monday

Matawi 5 ya CUF Zanzibar yachomwa moto

Zikiwa zimesalia siku 13 kabla ya kufanyika uchaguzi wa marudio Zanzibar, matawi matano ya Chama cha Wananchi (CUF), yamechomwa moto Kisiwani Pemba na Unguja, imefahamika.

Akizungumza na Nipashe mjini hapa, Naibu Katibu Mkuu wa Chama hicho, Nassor Ahmed Mazrui, alisema matawi hayo yalichomwa moto kwa nyakati tofauti usiku wa kuamkia jana na juzi.

Alisema tangu Zanzibar kuingia katika mgogoro wa uchaguzi mkuu baada ya kufutwa matokeo, matawi na maskani ya chama hicho yamekuwa yakichomwa moto na kuvunjwa na aliodai kuwa Askari wa Vikosi vya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ).

Alidai kuwa hujuma hizo zimekuwa zikifanywa na askari hao na hakuna hatua ambazo zimekuwa zikichukuliwa tangu kuanza kwa matukio hayo.

Mazrui alisema vitendo vya kuchoma moto matawi ya chama, vinakwenda kinyume cha misingi ya demokrasia na utawala bora.

Aliyataja matawi yaliyochomwa moto kuwa ni Tawi la Mkanyageni, Kiwapwa katika Jimbo la Ziwani, Kiuyu Minungwini Jimbo la Kojani, Ofisi ya Jimbo Wingwi, Maskani ya Kinowe Kisiwani Pemba na Maskani ya Mwanakwerekwe, kisiwani Unguja.

“Tumeripoti sana matukio haya polisi, lakini hakuna hatua zinazochukuliwa kwa wanaofanya hujuma hizo,” alisema Mazrui.

Alisema taarifa walizopokea kutoka kwa wananchi, zilieleza kuwa magari ya askari wa vikosi yalionekana nyakati za usiku yakizunguka kabla ya kutokea matukio hayo.

Alisema bado ni mapema kufahamu hasara iliyopatikana lakini alisema tangu kufutwa kwa matokeo ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 25, mwaka jana, wanachama wake wamekuwa wakipigwa mbali na kuchomwa moto matawi na maskani ya chama hicho.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kaskazini Pemba, Hassan Nassir, alithibitisha kutokea kwa matukio hayo na kueleza kuwa polisi wameanza kufanya uchunguzi.

Alisema hadi sasa bado haijafahamika watu wanaochoma moto matawi hayo licha ya kushutumiwa kwa askari wa vikosi Zanzibar.

Hata hivyo, alikiri matukio hayo kuwa na uhusiano mkubwa na mambo ya siasa na kuwataka wananchi kutoa ushirikiano ili kufanikisha kuwakamata watu wanaofanya vitendo hivyo.

“Tumeanza kufanya uchunguzi wa kuwasaka watu waliochoma moto maskani na matawi ya CUF,” alisema Kamanda Nassir.

Kwa upande wake, Waziri Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Vikosi vya SMZ, Haji Omar Kheir, jana hakupatikana kuzungumzia suala la askari wake kuhusishwa na uchomaji moto wa matawi hayo ya CUF, baada ya simu yake kutopokewa, licha ya kuita mara kadhaa.
 
Toggle Footer
TOP