Morogoro yapata Sheikh baada ya miaka mitatu

Abdallah Salim Mkang’ambe akipongezwa na wajumbe wa baraza la waislamu mkoa wa Morogoro baada ya kuchaguliwa 

Baraza la Waislamu Tanzania, mkoa wa Morogoro (BAKWATA) limemchagua Abdallah Salim Mkang’ambe kuwa shekhe wa mkoa huo baada ya kumshinda mpinzani wake katika uchaguzi wa kuchangua viongozi mbalimbali wa baraza hilo uliofanyika jana mkoani hapa.

Viongozi hao watadumu kwa miaka mitatu isipokuwa cheo cha shekhe wa mkoa ambacho ni cha kudumu.

Baraza la waislamu mkoa wa Morogoro limekosa nafasi ya sheikhe wa mkoa huo kwa kipindi cha miaka mitatu kufuatia aliyekuwa shekhe wa mkoa huo, Yahaya Juma Semwali kutenguliwa na aliyekuwa Mufti wa Tanzania Shekhe Issa Bin Shabaan Simba kutokana na madai ya kiongozi huyo kushindwa kuuletea maendeleo mkoa huo.

Msimamizi wa uchaguzi huo, Naibu Katibu Mkuu Kitengo cha Dini BAKWATA makao makuu, Mohamed Hamis alimtangaza Abdallah Salim Mkang’ambe kuwa shekhe wa mkoa wa Morogoro kwa kupata kura 34 baada ya kumshinda mpinzani wake, Iddi Husein Nyagongo aliyepata kura mbili.

Hamis alimtangaza, Mwishehe Ismail Mwishehe kuwa mshindi katika nafasi ya mwenyekiti wa halmashauri mji wa Morogoro kwa kupata kura 18 dhidi ya Mahseni Mbaraka Ahmed aliyepata kuwa 15 huku Rashid Hassan Chamile akiambulia kura tatu.

Kwa upande wa mjumbe wa hamlmashauri Taifa, Adam Rashid Yange alimshinda Mohamed Saidi Makala, wakati katika nafasi ya baraza la mashekhe waliopenya katika nafasi tano ni pamoja na Abdulrahman Pususa Kiswabi aliyepata kura 35.

Wengine ni Juma Hamza Hussein, kura 34, Juma Mohamed Odda, kura 33, Hassan Mamboleo Mzee, kura 33 na Twaha Swalehe Kilango, kura 28 huku Mikidadi Bakari Lyuba akishindwa kuingia katika safu hiyo kwa kupata kura 11.

Hamis alisema kuwa katika nafasi ya halmashauri kuu ya mkoa, wajumbe 10 ndiyo walioingia kuunda halmashauri hiyo baada ya kuvuka katika kinyang’anyiro cha wagombea 18.

Aliwataja wajumbe hao wa halmashauri kuu ya BAKWATA mkoa kuwa ni pamoja na Bakari Waziri Matua 31, Salum Mohamed Ngalima19, Saidi Okasha Kudurati 19, Omari Khamis Kindamba 24 na Khamis Khamis Ibrahim 19.

Wengine ni Hashim Suffy Swalehe 29, Yahya Mrisho Watuta 31, Ahmad Said Khayralla 32, Abushiri Mohamed Poyo 17 na Salum Hassan Chamile 21.