Loading...
Sunday

Mwl. Mndeme: Wimbi la PhD za Heshima Tanzania – Utoposhwaji uliofumbiwa macho

Sehemu ya Kwanza
Katika miaka ya karibuni, Tanzania imejikuta ni mhanga mkubwa wa kinachoitwa “kutunuku shahada (degree) za PhD za heshima” (honorary doctorate degree). Kama nitakavyoonesha  hapo baadaye, utoaji wa shahada za heshima si jambo geni katika vyuo vikuu duniani na hata vyuo vikuu vya hapa kwetu vimekua vikuwapa watu heshima hiyo kwa miaka mingi. 

Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere, alitunukiwa shahada za heshima na vyuo kadhaa duniani. Miaka ya nyuma kabla ya uchakachuaji wa heshima hizi kushika kasi, watu waliopewa PhD za heshima na vyuo vikuu walifanyiwa hivyo baada ya mchakato makini na ilikua nadra sana watu kuhoji zoezi na sababu za kutunukiwa kwao. 
Hata hivyo katika miaka ya karibuni, shahada hizi za heshima zimebadili kabisa mwelekeo wake kwani badala ya kutolewa na vyuo vikuu baada ya kufanya tafiti na kutazama vigezo walivyojiwekea, kwa sasa zimegeuzwa kuwa biashara. Kwanza kumeibuka “vyuo vikuu uchwara” duniani ambavyo biashara yao kuu ni “kuuza shahada za heshima”
Vyuo hivi hufuata watu kwenye jamii na kuwashawishi kwamba wanafaa kupewa heshima hiyo na hivyo kutakiwa kupitia “mchakato wao uchwara” ili wapewe heshima. Malengo ya kuwafuata watu hawa yanasukumwa na kutafuta fedha kupitia malipo toka kwa wanaotunukiwa heshima hizo, au kuwafuata watu wenye utajiri mkubwa na mtandao (connections) unaoweza kuvisaidia vyuo hivyo kupata misaada na umaarufu. Pili, kumeibuka wimbi kubwa la watu kwenye jamii kutafuta “vyuo vikuu uchwara” na kuwaomba/kuwashawishi wawape shahada za heshima kwa kupitia mgongo wa kuvisaidia vyuo hivyo kwa namna moja au nyingine au “kununua shahda ya heshima” hiyo kwa fedha.
C:\Users\User\Desktop\gwajima.jpg
Biashara ya shahada za heshima ilianza kupamba moto miaka ya 2000 mwanzoni na kasi kubwa kuongezeka ndani ya miaka kama 15 hivi iliyopita. Mwanzoni wanasiasa ndio walikua mstari wa mbele kutafuta heshima hizi za kubahatisha kwani ilionekana kuitwa “Dr Ukwasi Jipu” au “Dr Mtakamali za Kiiipu” ni kujijenga kisiasa na kujionesha kuwa msomi katika jamii bila kujali udokta huo unaendana na kujua kitu gani. Wanasiasa hawa walijua umuhim wa elimu katika kupata nafasi za kisiasa katika jamii lakini hawakua na uwezo na motisha ya kukomaa kutafuta elimu katika mchakato stahiki na hivyo kutafuta namna nyepesi ya kutokea. Baada ya jamii kuona wanasiasa wanafaidika na udokta uchwara unaopigiwa kelele na kulazimisha kutambuliwa hata kuliko wale walioutesekea darasani, watu wengi wakaanza kuutafuta. Miongoni mwa makundi makubwa yaliyoathirika na biashara hii ni wafanya biashara na viongozi wa baadhi ya madhehebu ya kikristo. “Wapakwa mafuta” hawa wamegundua kwamba mafuta waliyonayo ya kuitwa mtumishi, mchungaji, mwimbaji, askofu, nabii, mtume, na majina mengine, hayatoshi kuwapa heshima, mamlaka, na vitisho vya kutosha juu ya wanaowangoza na jamii kwa ujumla. Mbadala wake imekua ni kutafuta shahada za juu za heshima ili kunogesha vyeo vyao. Unajua tena: ina nguvu na mamlaka zaidi kuitwa “Mchungaji na Mtume wa Karne ya 23 Dr. MM” ukulinganisha na kuitwa “Mchungaji MM” bila vikorombwezo vingine!!! Udokta unaongeza “utukufu na mvuto”.
Wale wote waliopata nafasi ya kusoma vyuo vikuu vinavyoheshimu elimu na maadili ya taaluma, wanajua kwamba kupata shahada (degree) yoyote ile sio kazi rahisi. Ni zoezi gumu lenye changamoto nyingi na linalohitaji kujitoa, kupambana, kuvumilia, kujituma, na hata kupoteza baadhi ya fursa (opportunities) zingine za kimaisha (kama fedha, kazi, biashara, nk) kipindi ambacho unapambana kusoma. Kwa wastani, shahada ya kwanza ni safari ya miaka kuanzia mitatu hadi sita kulingana na kile mtu anachosomea na mtindo wa kusoma (parttime or fulltime). Unapoamua kutafuta shahada ya pili (uzamili) ni uamuzi wa kutafuta ujuzi na utaalamu mahususi zaidi unapolinganisha na unachokipata katika shahada ya kwanza. Shahada ya uzamili inalenga kukupa ujuzi/ufahamu mpana katika eneo moja la kitaaluma na uwezo wa uchambuzi wa mambo katika eneo husika. Zaidi ya kusoma kitu mahususi, shahada hii ya pili inakuandaa kama mtafiti na ndio mana unalazimika kufanya utafiti kama sehemu ya masharti ya kuhitimu. Shahada ya uzamili inaweza kukugharimu wastani wa mwaka mmoja hadi mitano kuimaliza.
Shahada ya tatu ambayo hujulikana kama ya Uzamivu au Doctorate (PhD) ndio ngazi ya juu kabisa ya kitaaluma kwa maana ya ubobezi. Shahada hii inalenga kumuandaa mtu kuwa mbobezi katika eneo fulani la kitaaluma kwa ngazi ya utafiti. Unaweza kubobea jambo kwa kulisomea/kulisoma au uzoefu wa kulifanyia kazi kwa muda mrefu lakini hiyo haitoshi kukufanya kuwa mbobezi kitaaluma. PhD ni ubobezi wa kitafiti unaojaribu kuelewa na kuelezea maarifa katika kiwango cha juu cha uchambuzi na uelewa.
PhD ni shahada ngumu kuliko zote (kwa maana ya mchakato wa kuisoma) na moja ya sababu kubwa ni ukweli kwamba hakuna mtu anayekufundisha kupata PhD kama ilivyo kwa shahada mbili za awali. PhD ni mradi au wazo la kitafiti lako mwenyewe (latakiwa lianzie kwako) na unalifanyia kazi kitaaluma chini ya ungalizi na usimamizi wa watafiti waliobobea katika eneo husika (wahadhiri waandamizi/maprofesa). Ingawa kuna PhD zinazojumuisha kufundishwa masomo/ courses darasani, lakini nyingi ya shahada hizi (hasa katika vyuo makini duniani) ni kazi za kitafiti pekee bila kuwa na masomo ya kufundishwa na kutahiniwa. Mtu aliyesoma PhD na kuhitimu, anategemewa awe na uelewa mkubwa na ubobezi katika eneo alilotafiti. Hali kadhalika, anategemewa awe na uwezo wa kufanya tafiti, kutoa mitazamo wa kisomi katika mazingira ya eneo la ubobezi wake, kufanya uchambuzi wa hali ya juu katika kuoainisha elimu nadharia na uhalisia wake katika jamii au mazingira ya kila siku. Antegemewa kufanya uchambuzi yakinifu na tunduizi kabla ya kutoa maoni yake pamoja na kuwa na uwezo wa kutazama mambo na mawazo ya wengine kwa tafakuri pana (reflective thinking) badala ya kukariri au kumeza kama yalivyo.
Mtu aliyehitimu PhD ya ukweli, anategemewa awe kapata mwanga zaidi wa mambo mengi (exposure) na awe mtu mwenye kuheshimu weledi wa taaluma ikiwa ni pamoja na kutumia ubobezi wake katika kutatua changamoto za kimaisha zinazoizunguka jamii aliyeko. PhD inasomwa kwa muda mrefu na inapitia michakato migumu sana ikiwa ni pamoja na kukosolewa kisomi na kuchambuliwa katika kiwango cha juu kwa lengo la kutazama ni mchango gani msomi husika anauleta kwenye jamii na taaluma yake. Kama vile haitoshi, kusoma PhD ni gharama kubwa sana kwa maana ya ada na gharama zingine zinazoendana na mazingira ya kusoma. Kwa mfano, kusomesha mtu mmoja kwa kiwango cha PhD kwa miaka minne katika nchi za Ulaya kama vile Uholanzi, Ujerumani, Uingereza na zingine, inagharimu karibu au zaidi ya shilingi Milioni mia tatu za kitazanzania (300,000,000) ikiwa ni gharama za ada, kuishi na mahitaji mengine ya lazima. Hizi sio fedha kidogo. Ukitazama ugumu wa mchakato wa kusoma PhD unaweza ukaelewa ni kwa nini shahada hii inasomwa na watu wachache sana duniani kote (nitaonesha zaidi sehemu ya pili ya makala).
Mtu aliyepitia mchakato wa kutafuta elimu kuanzia shahada ya kwanza hadi ya uzamivu (PhD) ana kila sababu ya kufurahia matunda ya kazi nzito aliyofanya na changamoto alizopitia kwa ushindi. Mara nyingi heshima hii na kutamhua ugumu wa kazi aliyoifanya. Moja ya njia ya kuonesha bidii yake kitaaluma ni kutambulishwa kwa utangulizi wa Dokta (Dr) mbele ya jina lake. Kote duniani, watu waliosoma hadi kiwango cha shahada ya PhD hupewa heshima na nafasi ya kipekee katika jamii na maeneo yao ya kazi na mengi hutegemewa kutoka kwao na ndio mana hata mishahara yao hupewa uzito zaidi ya wataalamu wengine katika maeneo ya ajira. Hivyo basi, wale wenye elimu ya chuo kikuu na haswa wa nagazi ya PhD wanawajibika kujitahidi kutunza heshima na matarajio ya jamii kwao kwa kuhakikisha wanaendeleza ubobezi wao na kuakisi taaluma na elimu yao katika maisha ya kila siku. Ndio mana mtu mwenye PhD anapofanya jambo la kipuuzi au ambalo lingeonekana ni la kawaida kwa watu wengine, husababisha malalamiko na hata wengine kuhoji ni nini umuhim wa kusoma kwa kiwango hicho iwapo elimu hiyo inashindwa kuakisiwa katika maisha ya kawaida. Waliopata PhD wanajua kwamba kuhitimu kwao sio mwisho wa kusoma bali ndio mwanzo wa safari ndefu na ngumu ya kukuza ubobezi wao kwa kusoma na kuandika kwa lengo la kusambaza maarifa na ujuzi wao kwa wengine. Ndio mana ni ajabu sana kuona mtu anadharau kiwango hiki cha eleimu kwa mtu aliyeipata kihalali na bila figisufigisu za udanganyifu.
Biashara ya PhD za heshima inadharau mchakato mgumu na wenye changamoto nyingi za kustahili heshima ya kutambulishwa kama Dokta (Dr) Inatia kichefuchefu unapowaona wafanyabiashara wa shahada za heshima walivyobadili heshima hii kuwa karanga huku wakiwaaminisha wale wanaozitafuta kwamba wana nafasi (status) sawa ya heshima na wale waliopata PhD darasani. Wanafanya makusudi kuwabebesha heshima itiokanayo na kazi ngumu ya kitaaluma kwa watu wasiostahili. Biashara hii imeharamishwa zaidi kwa kuacha misingi ya mchakato wa utoaji wa shahada hizi kwa watu wenye michango inayotambulika katika jamii au taaluma husika. Kibaya zaidi, wachuuzi hawa wa shahada za PhD za heshima pamoja na wanunuzi wao, wameamua kujitambulisha kwa heshima ya Udokta (kwa maana ya PhD holders) huku wengi wao wakiwa hawajui hata tafiti ni kitu gani na wengine hawajui mlango wa chuo Kikuu una rangi gani.

Makala hii itaendelea kwa kutoa vielelezo zaidi vya tatizo hili.
Mwalimu MM – waweza niandikia kupitia mmmwalimu(at)gmail.com
 
Toggle Footer
TOP