Nape na Chongolo ni majipu CCM?

  • Gazeti la Uhuru ladidimia chini ya uongozi wao
  • Wadaiwa kuliyumbisha kiuongozi
  • Waweka makaim wasio na uwezo, wabadhirifu
  • Mtambo wa uchapaji wauzwa kinyemela kwa bei ya kutupa
  • Wafanyakazi wadai malimbikizo lukuki ya mishahara, likizo
  • Wastaafu washikilia nyumba za Kampuni hadi walipwe
WAKATI Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi Nape Nnauye, Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye akitamba kutumbua majipu katika vyombo vya habari vya Serikali, amedaiwa kushindwa kusimamia ipasavyo kuiinua kampuni ya Uhuru Publications Ltd (UPL), wachapishaji wa Magazeti ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Uhuru, Mzalendo na Burudani.

Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili umebaini kwamba, Nape anayeongoza Idara hiyo ya Itikadi na Uenezi yenye jukumu ka kusimamia vyombo vya habari vya CCM kwa takribani miaka mitano sasa, ameshindwa kusimamia ili kuiinua UPL baada ya kujenga uswahiba na kumwamini kupita kiasi Msaidizi wake, Godfrey Chongolo na hivyo kumbwagia usimamizi karibu wote wa kampuni hiyo ya UPL bila kumtamthimini.

Kufuatia hali hiyo, Chongolo ambaye ni Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Umma wa CCM, kwa kile kinachoonekana ni kwa kutumia vibaya madaraka yake yakiwemo ya Ukatibu wa Bodi ya Uhuru Media Group inayosimamia vyombo vya habari vya CCM, amedaiwa kuiua UPL, kwa kumshauri vibaya Nape na hivyo kuitumbukiza kampuni hiyo ikiwemo kutokuwa na uongozi imara kwa muda mrefu na badala yake kuweka makaimu wasio na sifa katika nafasi zote za juu ili kupata mwanya wa kufanya analotaka kwenye kampuni hiyo bila kubughudhiwa.

Moja ya mambo yanayodaiwa kufanywa na Chongolo ni kusimamia uuzwaji kinyemela mtambo wa uchapaji wa UPL, uliokuwa ukitumika kuchapisha magazeti ya Uhuru Mzalendo na Burudani wa Modern Newspaper Print (MNP) kwa bei ya kutupa na fedha za mauzo kuwa utata zilikokwenda.

Inaelezwa kwamba, mtambo huo wa uchapishaji ulikuwa ukisimamiwa na kampuni tanzu ya Modern Newspaper Printers (MNP) Limited, lakini kabla ya mtambo huo kuuzwa kampuni hiyo ya MNP ikavunjwa katika mazingira yanayoonyesha kuwa utaratibu haukufuatwa kama ifuatavyo;-
  1. Modern Newspaper Printers (MNP) Limited ni kampuni tanzu iliyoasisiwa na kumilikiwa na Shirika la Magazeti ya Chama (SMC) Limited na baadaye Uhuru Publications Limited (UPL). iliasisiwa mwaka 1995 kwa mkopo maalumu wa Benki ambapo katika ulipwaji wake, wafanyakazi walitakiwa kujifunga mikanda, ndani ya miaka minne, ikiwemo kusimamishwa kwa malipo ya aina mbalimbali ikiwemo likizo, jambo lililoridhiwa na wafanyakazi wakiamini kwamba hatua hiyo italeta maendeleo kwa kampuni na ustawi wao pia.
  2. Kwa kipindi chote cha uwepo wake, menejimenti ya kampuni hiyo tanzu ya MNP, ilikuwa ikiwajibika moja kwa moja kwa Uongozi au Menejimenti ya SMC na baadaye UPL hadi kifo chake.
  3. Hata hivyo, mtambo wa MNP umeuzwa bila wafanyakazi wa UPL kujulishwa, ambapo hata wakati mchakato wa uuzwaji wake ukifanyika hakukuwa na mrejesho wowote hata katika vikao vya kawaida vya wafanyakazi ambavyo vilikuwa na vimekuwa vikifanyika mara kwa mara.
  4. Kutokana na maelezo hayo, uuzwaji wa mtambo huo umewachia wafanyakazi maswali mengi juu yake, hasa ikizingatiwa kwamba kabla ya kununuliwa kwake waliombwa ‘kujifunga mkanda’ ili waweze kununua mtambo huo kwa manufaa ya kampuni, CCM na Watanzania kwa jumla, lakini wakati wa uuzwaji wa mtambo huo ulifanywa kwa siri kubwa, badala yake wafanyakazi walistukia baadhi ya vifaa na baadhi ya makabrasha yaliyokuwa kwenye ofisi ya MNP vikiletwa kuhifadhiwa UPL.
  5. Wafanyakazi wa UPL wanasema hawaridhiki na kile kilichofanyika maana hawajui mtambo ulivyouzwa, umeuzwa bei gani, fedha za uuzwaji wake zimetumikaje na mengi mengineyo yaliyofichika katika mpango huo. Wamekuwa na hadi sasa bado wanaiomba CCM ifanye uchunguzi wa kina kubaini mazingira yaliyosukuma kuuzwa kwa mtambo huo tena kwa siri kubwa, na kuweka hadharani (kama ilivyokuwa wakati wa ununuzi wake) fedha zilizopatikana na zilivyotumika.
  6. Wanasema wanaomba hivyo kwa sababu MNP kabla ya kuvunjwa na kuuzwa mtambo uliokuwa ukiifanya ifanye kazi, fedha zake zilitokana na UPL (wakati huo Shirika la Magazeti ya Chama Limited), hivyo kuna kila sababu ya kufahamu pia kile kilichopatikana baada ya kuuzwa kwake ni kipi na kiko wapi.
  7. Aidha, hofu juu ya mchakato wa uuzwaji kwa mtambo huo kugubikwa na ‘harufu chafu’ ilijionyesha tangu mpango huo ulipofanyika kwa sababu, hata baadhi ya vifaa vilivyokuwa katika ofisi za kampuni hiyo (MNP) kama kompyuta na nyaraka nyinginezo vilipotea katika mazingira ya kutatanisha.
  8. Uvunjwaji wa kampuni tanzu ya MNP ulifanyika pasipo kufuata sheria ikiwemo ya Usajili wa Kampuni inayosimamiwa na Wakala wa Usajili wa Majina na Leseni za Biashara (BRELA) na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
  9. Kutokana na Na. 8 hapo juu, suala hilo tayari limeshaleta matatizo na hata kuiweka njia panda UPL katika utayarishaji wa hesabu zake (Presentation of fixed assets and liaibilities from MNP Subsidiary). Kuendelea kuwepo kwa utata huo, suala hilo linaweza kuleta matatizo zaidi ya kisheria hata kwa mamlaka za nchi likiwemo suala la kodi.
  10. Pamoja na maelezo hayo, pia kuna malalamiko ya waliokuwa watumishi wa MNP ambao wameendelea kulalamikia malipo waliyopewa baada ya hatua ya uuzwaji wa mtambo. Wafanyakazi hao wanadai malipo hayo hayalingani na hali halisi na muda walioitumikia kampuni hiyo. Hili pia inatakiwa ufanyike uchunguzi na matokeo yake yajulikane maana malalamiko yao dhidi ya Chama ni makubwa na huenda yakawa na athari katika siku za usoni.
Uchunguzi umebaini kwamba kufuatia hali ya UPL kutokuwa na mtambo wake inalazimika kuingia gharama kubwa kwa kuchapisha magazeti yake katika mitambo ya watu binafsi ukiwemo wa JAMANA, ambao kila siku inalipa gharama za uchapaji, na kwa mwezi inatumia zaidi ya sh. milioni 55.6 (sh. 55,670,040/=) kwa kuchapisha magazeti ya Uhuru, Mzalendo na Burudani jambo ambalo linaisababishia kampuni madeni kwani kuna kipindi hushindwa kulipa fedha hizo kila siku na badala yake huchapa kwa mkopo jambo ambalo ni hatari kwa kampuni.

UONGOZI MBOVU

Chanzo chetu cha habari hii, kilisema uongozi mbovu ni miongoni tatizo kubwa ndani ya kampuni ya UPL, ambalo ni matokeo yaliyojiri chini ya uongozi wa Nape kama Mkuu wa Idara ya Itikadi na Uenezi na Chongolo kama Mkurugenzi wa Idara ya Mawasiliano ya Umma.

Inaelezwa kwamba, baada ya Mhariri Mtendaji aliyekuwepo, Josiah Mufungo kustaafu, Mnamo Machi 2014, CCM ilimteua aliyekuwa Mhariri Mkuu wa gazeti la Habari leo ambalo ni la Serikali Joseph Kulangwa, kuwa Mhariri Mtendaji wa Uhuru Publications Limited (UPL) ambapo chini ya uongozi wa Mhariri Mtendaji huyo, UPL ilianza kuonyesha matumaini kwa kuwa kiongozi huyo alionyesha kujitahidi kuiinua kampuni kwa kuanza kuziba mianya ya wizi aliokuta umekithiri ndani ya kampuni hasa kwenye Idara ya Biashara ambayo ndio idara inayotegemewa kwa ajili ya kuingiza kipato cha kampuni.

"Katika jitihada zake za kuboresha utedaji kazi na kudhibiti mianya ya wizi, alijaribu kufanya mabadiliko kwa kuwahamisha baadhi ya wakuu wa Idara ikiwemo ya Biashara, lakini alipotangaza hatua hizo, Chongolo, alizuia mabadiliko hayo, kumlinda Meneja Biashara Esther Paul ambaye siyo siri kuwa ni mpenzi wake", Kilisema chanzo chetu cha habari hii na kuongeza, "Kuanzia hapo Chongolo akishirikiana na watumishi wasio waadilifu, alianza kumfitini Kulangwa ili aonekane hafai kuongoza kampuni ya UPL, na kwa kuwa Chongolo ni mtu ambaye Nape alimpa jukumu la kusimamia vyombo vya habari vya CCM akionekana kumwamini sana, hivyo hakutilia shaka ripoti anazopata kutoka kwa Chongolo, naye aliafiki kuwa Kulangwa hafai.

Chanzo kilisema, kutokana na Bodi nayo ya UPL kushindwa kuwa na ubavu wa kuwakatalia Nape na Chongolo wazo lao la kumwondosha UPL Kulangwa kwa sababu hata Bodi yenyewe ya UPL ina walakini mkubwa, bila hata kutafakari kwa makini Juni 23, 2015, Bodi hiyo ilimsimamisha kazi Mhariri Mtendaji huyo hadi sasa.

"Ni ukweli ulio wazi hatua na Nape na Chongolo, kumuondoa Kulangwa kumekuwa ni pigo kwa UPL kwa kuwa si rahisi kumpata Mhariri Mtendaji mwenye sifa kama zake, kuwa mbali na kuwa mbunifu, mwenye kutetea haki na maslahi ya wafanyakazi bila ubaguzi na kuziba mianya ya wizi wa mapato ya kampuni, pia anaijua vizuri kampuni ya UPL kwa kuwa ndipo alipoanzia kazi ya Uandishi wa habari kabla ya kuhamia magazeti ya Majira na baadaye kwenda Habari leo kuwa Mhariri Mkuu", Kilidai chanzo hicho.

Waliongeza kwamba, "katika mda wake mfupi aliokuwa Mhariri Mtendaji katika UPL, Kulangwa alikuwa ameshaanza mikakati ya uwekezaji wa mali za kampuni ikiwemo nyumba tisa (9) zilizopo Dar es salaam, nyumba tatu (3) zilizopo Dodoma, nyumba moja iliyopo Morogoro na Shamba la ekari tatu (3) lililopo Nkuhungu Dodoma, Sasa kufukuzwa kwake kumezima ndoto za UPL kuinuka kwa sababu mbali ya kutegemea ruzuku ya CCM ambayo haipatikani kirahisi, Uwekezaji ndiyo njia pekee na mwafaka ambayo ingeiokoa UPL kutoka kwenye kitanzi cha kufa".

"Ni dhahri kwamba Nape na Chongolo wamechangia sana kuididimiza UPL na hii ilianza tangu mwaka 2012 kwa kumuondoa aliyekuwa Meneja Rasilimali Watu na Utawala Lucas Kisasa na kumpeleka kuwa Mratibu wa Chuo cha Siasa cha Ihemi, Iringa, akiwa amebakiza miezi minane tu ya kustaafu kazi. Hii ilifanyika tu ili kumuondoa ndani ya UPL kwa kuwa alikuwa akisimamia sheria na kuwa na msimamo wa kutokubali kuyumbishwa na viongozi hao", Walidai wafanyakazi hao na kuongeza.

"Mfano mwingine unaothibitisha kuwa Nape na Chongolo wamechangia kuididimiza UPL, ni huu; katika kikao cha wafanyakazi pamoja na Mwenyekiti wa Bodi ya Uhuru Media Group Adam Kimbisa kilichofanyika Juni 26, 2015 katika jengo la Makao Makuu ya Umoja wa Vijana wa CCM, Dar es Salaam, kutuliza mgomo wa wafanyakazi, pamoja na mambo mengine yaliyojadiliwa katika kikao hicho pia wafanyakazi walitoa taarifa kwamba kuna wizi katika Idara ya Biashara na kwa kuthibitisha hilo walikieleza kikao kwamba tayari Meneja wa Biashara Msaidizi Matangazo amesimamishwa kazi kwa ajili ya upotevu wa fedha. Katika hali ya kushangaza Nape alimtetea Meneja huyo kwa kusema kwamba fedha zenyewe alizoiba ni ndogo Sh.672, 000/= tu, sasa je kwa kauli hii kwa nini tusiseme kwamba anafuga wezi ndani ya kampuni kutokana na maslahi anayojua?" KilisemaChanzo chetu hicho cha habari hii.

Chanzo hicho kiliongeza kwamba katika kikao hicho pia kuna wafanyakazi walionyesha ushahidi wa nyaraka juu ya wizi unaofanyika kwenye kitengo cha matangazo, ambapo Mwenyekiti wa Bodi aliagiza ushahidi huo ukabidhiwe kwa Kaimu Mhariri Mtendaji Ramadhani Mkoma, kwa ajili ya kufanyiwa kazi lakini licha ya kukabidhiwa nyaraka hizo hakuna kilichofanyika hadi sasa na wafanyakazi wanaotuhumiwa katika ripoti hizo bado wapo.

Chanzo chetu kinaeleza kwamba baada ya kuondolewa Kulangwa, kampuni kwa sasa inaendeshwa kama ‘shamba la bibi’ kwa kuwa hakuna tena usimamizi thabiti wa taratibu na maslahi ya kampuni, kutokana na kwamba viongozi waliopo wanaonyesha kutojua vilivyo majukumu yao na hawana sifa.

Kinasema, hata Kaimu Mhariri Mtendaji aliyeko sasa Mkoma, amedhirihisha kufanya kazi kwa kutojiamini kuwa yeye ndiye msimamizi mkuu wa kampuni, kwa sababu amekuwa akionyesha kuwa bwana ndiyo kwa kila kinachofanywa na viongozi wa chini yake hata kama hakina tija kwa kampuni, mojawapo ya kutojiamini huko ni pale alipokubali Kaimu Meneja Rasilimali watu Paul Mg’ong’o kukarabati jengo la ofisi kwa gharama ya zaidi ya sh. Milioni saba ( sh. 7,671,000/=) wakati wafanyakazi hawajalipwa mishahara ya miezi mitatu na madeni mengine ya kisheria yakiwemo malipo ya waliostaafu.

"Kwa mfano kuanzia Mei 2011 hadi Juni 2015, kampuni imelimbikiza madeni ya kisheria ya wafanyakazi hadi kufikia zaidi ya sh. Bilioni 1.2, kiasi kwamba baadhi ya wafanyakazi wastaafu anaoishi katika nyumba za kampuni wamegoma kuondoka katika nyumba hizo hadi watakapolipwa fedha zao za kustaafu na madeni mengine, jambo ambalo hapo baadae wanaweza kuzihodhi kabisa nyumba hizo", kilisema chanzo chetu na kuzitaka nyumba zilizomo wastaafu hao wanaoidai Kampuni kuwa ni zilizopo Dar es Salaam, ya kwanza ipo Mwananyamala kwenye Plot Na. 82 Block 45 B, yapili ipo Mikocheni B, plot Na 559 na nyumba plot Na 1307/4 Block G iliyoko Tabata Mawenzi.

Mg’ong’o ambaye ni swahiba yake Chongolo, alilazimisha ukarabati huo ufanyike kwa kile kilichodaiwa kwamba alipata asilimia kumi kutokana na ukarabati huo, na hata vifaa vya ujenzi alikuwa akinunua yeye wakati yupo mnunuzi wa kampuni.

Chanzo chetu kinadai kwamba, kabla ya ukarabati huo, viongozi waliwadanganya wafanyakazi kwamba jengo litakarabatiwa kwa gharama ya sh. milioni 4,040,000/=. jambo ambalo halikuwa kweli, kwa kuwa taarifa zilizopo ni kwamba ukarabati huo umegharimu kiasi cha sh.7,671,000/= na bado ukarabati wenyewe haukukamilika jambo ambalo limekuwa kinyume na linatia mashaka.

"Kaimu Mhariri tendaji Mkoma alipaswa kukataa ukarabati huo kwa kuwa pamoja na kwamba ni kweli mfanyakazi anatakiwa kufanya kazi katika mazingiza mazuri na masafi lakini anatakiwa afanye kazi akiwa ameshiba na kuwa na uhakika wa maisha ya kesho yeye pamoja na familia yake na sio kufanyakazi katika nyumba nzuri akiwa na njaa halafu utegemee ufanisi wa kazi.
Unaweza ukajiuliza swali hili, hivi unaweza kukarabati nyumba yako wakati wanao wamerudishwa nyumbani wakidaiwa ada shuleni? Nadhani kama unaujua umuhimu wa elimu utakubaliana kwamba utalipa kwanza ada na kununua chakula halafu ndipo mambo mengine yatafuata", Kilisema chanzo chetu cha habari.

Chanzo chetu kilidai kuwa pia Meneja Rasmilimali na Utumishi aliyewekwa na uongozi wa Nape na Chongolo, Mg'ong'o ambaye kitaaluma si Mtawalani ila Mnunuzi (procure) naye uongozi wake unaitafuna UPL ikielezwa mifano mbalimbali ikiwemo kuchukua vifaa vya ofisi kupeleka nyumbani kwake na kutokuwa na kipaumbele katika matumizi ya fedha za kampuni.

Inadaiwa hivi karibuni amechukua kompyuta, kiti na meza na kuondoka navyo, jambo ambalo ni kinyumbe na utaratibu wa kiutawala na kiuongozi, na wakati anachukua vifaa hivyo vya kampuni alikataa kusaini na kuandika katika kitabu cha mlinzi kuwa anaondoka na mali hizo jambo ambalo lilimstua mlinzi na kuamua kuweka kumbulumbu hizo yeye mwenyewe.

Katika kutojali vipaumbele amewahi kuidhinisha kila kikao cha menejimenti wanachokaa pawe na posho ya sh 20,000/= pamoja na chips kuku hali akijua kuwa wafanyakazi hawajalipwa mishahara kwa mda mrefu na pia amekuwa akitumia madaraka yake vibaya, kwani pamoja na kupata posho ya usafiri ya sh 830,000/= kila mwezi amekuwa akitumia gari ya ofisi kwa shughuli zake binafsi.

Aidha, anayekaimu nafasi ya Mkaguzi Mkuu Caroline Kissamo pia hana sifa na hawezi kukagua kitu chochote wala kuandika ripoti yoyote kwa kuwa kisheria ripoti yake haitambuliki hadi awe na sifa za ukaguzi ambapo sifa mojawapo ni lazima awe na CPA ambayo hana.

MZIGO WA KULIPA MISHAHARA MARA MBILI KWA NAFASI MOJA

Chanzo hicho cha habari, kilisema, kutokana na maamuzi ya uongozi wa Kina Nape na Chongolo kuwasimamisha kazi viongozi waliokuwepo, kwa muda mrefu sasa kampuni imekuwa na mzigo mkubwa wa ulipaji mishahara mara mbili (Double payment), ambapo Mhariri Mtendaji aliyesimamishwa kazi Kulangwa, na Kaimu Mhariri Mtendaji Mkoma wote wanalipwa kiasi sawa cha mshahara na marupurupu mengine.

Kadhalika Meneja Rasilimali Watu na Utawala aliyesimamishwa Mpondachuma na anayekaimu nafasi yake kwa sasa Mng’ong’o nao wote wanalipwa kwa viwango sawa hali inayoelezwa ni kutokana na UPL kutokuwa na Uongozi makini tangu Bodi ya Wakurugenzi na kwamba kabla ya CCM kufikiria kuisaidia UPL katika suala la mtaji na upatikanaji wa mtambo ni vyema kampuni ikapatiwa viongozi makini, wachapakazi na wenye kujua masuala ya uongozi pia wenye taaluma zinazotakiwa katika kushikilia nafasi hizo katika nafasi zifuatazo:-

(i) Mhariri Mtendaji ambaye ndiye Mkuu wa Kampuni
(ii) Naibu MhaririMtendaji ambaye ndiye mkuu wa Idara ya Habari
(iii) Meneja Rasilimali Watu na Utawala
(iv) Meneja Biashara
(v) Mhasibu Mkuu
(vi) Mkaguzi wa Ndani Mkuu.

Nafasi hizo zinaweza kujazwa kwa CCM kuipatia kampuni watu wenye sifa au kwa kutoa idhini kwa kampuni kutangaza nafasi hizo ili kupata watu wenye, watu hao wakishapatikana ndipo kampuni iwezeshwe, kwani uongozi uliopo sasa hata kampuni ikipewa mtaji wa sh. bilioni 100 hakuna kitakachofanyika.

MADENI HEWA 

Chanzo chetu cha habari kilisema, Ili kampuni iweze kuondokana na baadhi ya wafanyakazi wabadhirifu ni lazima ufanyike ukaguzi wa miaka mitano nyuma, katika Idara ya Biashara ambapo kuna wasiwasi kuwa yapo madeni hewa kwa kipindi kirefu kwa kuwa tangu mwaka 2009 madeni yanasomeka ni bilioni mbili na zaidi hadi leo jambo ambalo linatia mashaka.

Pia ukaguzi huo uhusishe na idara zingine ikiwemo idara ya Fedha kwani kwa kipindi kirefu sasa kumekuwa na tofauti ya mahesabu baina ya idara mbili Biashara na Fedha, kwa kufanya ukaguzi huo itasaidia kuhakiki na kuwa na mahesabu ambayo yako sahihi na ukaguzi huo utasaidia kubaini wabadhilifu na hatua za kisheria ziweze kuchukuliwa dhidi yao. "Suala hilo lilishawasilisha na wafanyakazi kwenye kikao hicho cha 6/06/2015 alichokuwepo Nape na Mwenyekiti wa Bodi Kimbisa lakini hadi sasa hakuna hatua zozote ziizokwishafanywa, jambo ambalo linatia wasiwasi na maswali mengi kwamba kwanini hadi sasa ukaguzi huo haufanyiki?"Kiluliza chanzo chetu cha habari.