Sehemu ya II: Wimbi la PhD za Heshima Tanzania – Utoposhwaji uliofumbiwa macho

Wimbi la PhD za Heshima Tanzania – Utoposhwaji uliofumbiwa macho
Sehemu ya Pili
Chuo Kikuu cha Oxford ni kati ya vyuo vitatu bora kabisa duniani na ndiyo Chuo Kikuu cha kwanza nchini Uingereza na katika ulimwengu wa nchi zinazoongea kingereza. Hali kadhalika, Oxford ni Chuo Kikuu cha pili kwa ukongwe duniani baada ya chuo Kikuu cha Bologna kilichoko kule nchini Italia. Ukifika katika mji wa Oxford pale Uingereza utashangazwa na chuo hiki kikongwe kwani kimesambaa karibu mji mzima kikiwa na shule (schools/colleges) kama 42 hivi na hivyo kuufanya mji wa Oxford kujulikana kama ”a University City”. Hakuna kumbukumbu zinazoonesha tarehe rasmi ya kuanzishwa kwa chuo hiki lakini kuna ushahidi unaonesha ufundishaji rasmi ulianza mwaka 1096 (miaka 920 iliyopita). Chuo hiki kilipanuka zaidi baada ya Mfalme Henry wa pili (Henry II) kutoa amri mwaka 1167 kwamba ni marufuku kwa vijana wa kiingereza kwenda kusoma katika chuo Kikuu cha Paris nchini Ufaransa na badala yake wasome Oxford. Oxford kiliendelea kuwa chuo Kikuu pekee nchini Uingereza hadi mwaka 1209 kulipotokea ugomvi kati ya wasomi waliokua katika chuo hiki na wenyeji wa eneo la Oxford uliopelekea baadhi ya wasomi kukimbia na kwenda kuanzisha chuo Kikuu cha Cambridge kilichoko Kaskazini Mashariki mwa Oxford. Vyuo hivi viliendelea kuwa vyuo vikuu viliwi pekee nchini Uingereza kwa miaka zaidi ya 600 vikilindwa na sharia ya kifalme hadi mwaka 1820 iliporuhusiwa kisheria kuanzisha vyuo vingine nchini Uingereza.
http://www.ox.ac.uk/sites/files/oxford/styles/ow_large_feature/public/field/field_image_main/aerial_oxford.jpg?itok=jQ67g78G
Sehemu ya majengo ya Chuo Kikuu cha Oxford

Shahada za heshima zinajulikana kitaalamu kama Honorary degree au “Honoris Causa” kwa lugha ya kilatini ikimaanisha “kwa ajili ya heshima” (for the sake of honour). Kwa lugha nyingine mtu aliyetunukiwa PhD ya heshima anapewa kwa kigezo cha heshima ambayo ameonekana anastahili.
Kumbukumbu zilizoko zinaonesha kwamba shahada ya kwanza ya heshima ilitolewa na Chuo Kikuu cha Oxford mnamo mwaka 1478 (karibu miaka 500 iliyopita). Heshima hii alipewa mtu aliyeitwa Lionel Woodville ambaye alikua maarufu na mwenye heshima kubwa kama Askofu kijana na Mkuu wa Cathedral Church of Saint Peter. Hali kadhalika, Lionel alikua shemeji ya mfalme Edward wa nne (King Edward IV) aliyekua anatawala kipindi hicho kule Uingereza. Mambo haya yalivyomfanya kuwa na hadhi ya jamii ya kifalme, utajiri mkubwa, na mtandano (connections) wa watu wenye ukwasi na maslahi mapana. Kwa kuyaona hayo, Chuo Kikuu cha Oxford kiliona kujishikamanisha na mtu huyu maarufu ni faida kwa chuo chao kwa namna nyingi na hivyo kikaamua kumtunuku shahada ya heshima ya PhD. Askofu Lionel “alipelekewa PhD nyumbani kwake” na mtumishi maalum wa chuo aliyekua amevalia kinadhifu sana na akiwa amebeba cheti cha shahada hiyo.  Jambo hili lilikua la ajabu kwani chuo hiki kilitupilia mbali taratibu zake ngumu za kumtunuku mtu PhD na kumtunuku Askofu Lionel PhD ambayo ilipewa hadhi sawa na PhD ya mtu aliyeingia darasani. Baada tu ya kupewa heshima hii, chuo kilipiga hatua moja zaidi na kumteua kuwa Mkuu wa Chuo (Chancellor of the University). Baada ya shahahada hii ya kwanza ya heshima ya PhD, chuo hiki kiliendelea kutunuku watu wengine kutoka familia za kifalme (noble families) au wale waliokua kwenye baraza la utawala la mfalme (the king’s court) na huu ulikua utamaduni wa karibu kila mwaka. Miaka ilivyoendelea, watu wengine maarufu waliingizwa katika mchakato huu wa kuheshimiwa.
Utamaduni huu wa kutoa shahada za heshima ulisambaa kwenye vyuo vingine vikuu na heshima hizi hazikua za PhD pekee bali zilikuwepo za Bachelor of Arts (B.A) na Masters of Arts (M.A) na walitunukiwa walipewa stahiki zote za kitaaluma zilizoambanata na shahada hizo. Hata hivyo utamaduni wa kutoa shahada za heshima kwenye vyuo vingi ulijitahidi kujikita katika kuwatunuku watu ambao michango yao kitaaluma na kijamii ilikua dhahiri. Kadiri siku zilizvyokwenda, wale walitunukiwa walishauriwa kutojitambulisha kama madokta mbele ya majina yao na waliambiwa kabisa kwamba heshima hizi haziwaongezei chochote kitaaluma au kupata faida katika maeneo yao ya kazi. Halikadhalika, walishauriwa kwamba kwenye wasifu wao (CV) waorodheshe shahada za heshima kama pongezi (awards) na wasiziorodheshe upande wa taaluma. Izingatiwe kwamba, PhD za heshima hutolewa hata kwa wasomi wenye shahda za PhD hasa wanapotambuliwa kwa michango yao mikubwa katika eneo maalum la kitaaluma au ubobezi wao. Katika ulimwengu wa elimu ya vyuo vikuu vya kisasa, degree za heshima zimekua ni za PhD tu na sio zile za BA na MA zimetupiliwa mbali kwani huenda zimeonekana hazitoi uzito wa kutosha. Nyingi ya PhD za heshima zinazotolewa huwa ni Doctor of Laws (LL.D.), Doctor of Letters (Litt.D), Doctor of Humane Letters (Litt.D), Doctor of Science (Sc.D.), Doctor of Divinity (D.D), Doctor of Music (D.Mus).
Mtu ambaye amevunja rekodi kwa kutunukiwa shahada nyingi zaidi za heshima duniani ni Padri/ Kasisi  Dr.Theodore Martin Hesburgh aliyefariki mwaka 2015 akiwa na miaka 98. Kasisi Theodore alikua Rais (president) wa chuo kikuu cha Kikatoliki cha Notre Dame kilichoko katika jimbo la Indiana kule Marekani. Chuo hiki ni kati ya vyuo vikuu maarufu sana duniani vilivyo chini ya kanisa na kilichopata mafanikio makubwa hasa katika kipindi cha miaka 35 cha uongozi/urais wa Kasisi Theodore. Kasisi Theodore alikua msomi aliyebobea katika Theology wa kiwango cha PhD lakini kutokana na mchango wake mkubwa katika taaluma na kazi zingine alizofanya ikiwa ni pamoja na kuteuliwa kama mara 16 na marais wa Marekani katika majukumu mbalimbali ya kitaifa, alitunukiwa PhD za heshima zaidi ya 150 na hivyo kuwa mtu aliyetunukiwa heshima hiyo kuliko mwingine yeyote yule katika historia.  
Hata hivyo, kadiri siku zilivyoendelea mbele, baadhi ya vyuo vilipunguza makali ya machakato wa utoaji wa shahda za heshima za PhD na kuanza kukumbatia maslahi yatokanayo na utoaji wa heshima hizo. Vyuo vingi hasa Marekani, vimejikuta wanatoa PhD za heshima kwa watu mashuhuri na maarufu (celebrities) na huku malengo yakiwa wamechepushwa. Badala ya heshima hizi kutolewa kutokana na vigezo (under merits) zimekua zikitolewa kimaslahi kwa kuwapa watu ambao hutegemewa kukisaidia chuo husika kifedha, kukitafutia “connections”, na kukifanya kuwa maarufu zaidi. Pamoja na ubora wa elimu wa vyuo vingi vya Ulaya na Marekani, swala la umaarufu wa chuo lina uzito mkubwa sana kwani wenzetu wamefanikiwa kuifanya elimu ya vyuo vikuu kuwa biashara inayolipa sana. Wale wanaoamini katika dini wanajua kitu kinachoitwa “roho iambatanayo na jambo”: hii ni hali inayojitokeza katika maisha ya mtu au kundi la watu kutokana na asili au chanzo ya kile wanachokifanya au kuamini. Kwa mtazamo huo, naweza kusema ile “Roho iliyokikumba chuo kikuu cha Oxford” kwa kutoa degree ya heshima kwa mtu maarufu kwa lengo la kutafuta maslahi, imeendele kutafuna vyuo vikuu na vingi kujikuta vinatoa heshima hizi bila vigezo vinavyoeleweka na badala yake kutanguliza maslahi, siasa, umaarufu, na kutukuza baadhi ya watu hasa wenye mamlaka (kiutawala au mali) katika nchi na jamii. Mbaya zaidi, kuna vyuo huko magharibi ambavyo wao hawana mpango na utoaji wa taaluma na badala yake wamejikita “katika biashara ya kuuza heshima”.
Mfumo wa Marekani ambao ni moja ya mifumo hurua sana katika mambo mengi duniani, umezalisha vyuo vingi vya kikanjana ambavyo ndani ya miaka kama 15 hivi iliyopita, vimekua vikifanya sana biashara ya kinachotwa “online degree” na utoaji wa “PhD za heshima”. Pamoja na kwamba vyuo vingi vinatoa heshima hizi duniani na hata Uingereza ambapo ndipo zilianzia bado zatolewa, lakini wamarekani ndio wamekua vinara wa biashara hii na wanaifanya “bila kumtazama nyani usoni”. Wahanga na wateja wakubwa wa biashara hizi wamekua ni watu wa nchi maskini na wenye elimu duni/ndogo kama ilivyo hapa kwetu na ndio mana soko letu la ajira, watumishi wa umma, wanasiasa, wafanya biashara, na kundi la viongozi wengi  wa dini, kumejaa watu wenye elimu zenye utata na maswali mengi.  
http://www.aceshowbiz.com/images/news/oprah-winfrey-receives-honorary-degree-at-harvard.jpg
Oprah Winfrey alipotunikiwa PhD ya heshima na Chuo Kikuu cha Harvard

Watu wana vyeti vya kutisha kuonesha kwamba wana degree hadi za uzamivu lakini uwezo wao wa kiakili, utendaji wao wa kazi, fikra zao, michango yao, na mengine mengi, havifanani kabisa na kile  wanachodai wanacho kupitia vyeti vyao. Wengi wa watu waliotunukiwa shahda za PhD za heshima hapa Tanzania, hawajatunukiwa na vyuo vyetu. Wengi wa watu hawa wametunukiwa na vyuo vya nje na hasa vyenye makao/asili ya Marekani. Pamoja na viwango vya kujikongoja vya vyuo vyetu, bado vimejitahidi sana kutofanya biashara ya kuwapa watu heshima wasizostahili. Mara nyingine kumeonekana kumekua na heshima ambazo zatolewa “kisiasa zaidi” na baadhi ya vyuo (hasa unaposikiliza vigezo wanavyodai wametumia kumtunuku mtu heshima), lakini bado hatujafikia kiwango ha kutisha.
Labda mtu waweza kujiuliza maswali kadhaa:
  1. Ni kwa nini watanzania na hasa viongozi wetu wameparamia hizi shahda za heshima?
  2. Wale wanaozitafuta wanapata faida gani?
  3. Jamii imechangiaje kuwafanya wengi zaidi wazitafute?
  4. Kwa nini jamii ya wasomi na mamlaka zinazohusika zimefumbia macho suala hili na hakuna anayekemea au kuchukua hatua?
Baada ya kutoa utangulizi wa asili ya shahada za heshima na mwelekeo wake, nitamalizia Makala hii kwa kuchambua wimbi la utoaji wa PhD za heshima hapa nyumbani.

Imeandikwa na Mwalimu MM - Waweza mwandikia kupitia mmmwalimu(at)gmail.com