Sehemu ya III: Wimbi la PhD za Heshima Tanzania – Utoposhwaji uliofumbiwa macho

Wimbi la PhD za Heshima Tanzania – Utoposhwaji uliofumbiwa macho
Sehemu ya Tatu
Nianze sehemu hii ya tatu ya makala hii kwa kuweka kumbukumbu sawa kwamba mimi sio mpinzani wa shahada za heshima. Nikiwa nimepata neema ya ufahamu kidogo kuhusu dhana ya taaluma na elimu kwa kiwango cha chuo kikuu, naelewa jinsi ambavyo heshima hii inaweza kutolewa kwa kuzingatia vigezo na kwa watu ambao wanastahili na ikawa na tija kwa anayeitoa na anayepewa. Shahada za heshima zinatambulika vema katika ulimwengu wa kisomi kote duniani kama namna ya kutambua mchango wa watu katika jamii kupia ubunifu, uongozi, utafiti, na mengine yenye kuleta mchango chanya katika kuboresha maisha ya mwanadamu, utamaduni wake, na mazingira yanayomzunguka. Kwa mfano: wakati natunukiwa shahada ya kwanza pale Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Rais Mstaafu Mzee Mkapa alitunukiwa shahada ya PhD ya heshima (Honoris Causa) kwa mchango wake katika kukuza Kiswahili katika kipindi cha uongozi wake. Pamoja na kwamba sijabahatika kusoma andiko la kisomi la sababu za kutunukiwa kwake, lakini nadhani hakuna mtu ambaye anaweza kuhoji ni kwa jinsi gani Rasi Mkapa aliheshimu lugha ya Kiswahili katika urais wake.
http://news.mak.ac.ug/documents/award.JPG
Mzee Mkapa akitunukiwa PhD ya heshima ya sheria ya Chuo Kikuu cha Makerere mwaka 2009.


Katika hotuba zake hasa zile za kila mwisho wa mwezi kwa taifa zilitolewa kwa Kiswahili kilichonyooka na ziliepuka kabisa kuchanganya na lugha ya kigeni hata pale ambapo ufafanuzi kwa lugha hiyo ungeweza kuweka mkazo au uelewa zaidi. Katika kipindi chake maneno mengi ya Kiswahili ambayo yalikua mageni kwa watu wengi yalipata umaarufu kupitia hotuba zake kama vile mshikadau (likaja kuwa mdau), teknohama (likaja kuwa tehama), utandawazi, ukwasi, asasi, uwekezaji,nk. Mzee Mkapa alitumia Kiswahili kwa ufasaha huku akijulikana  wazi kwamba ni msomi mwenye uwezo mkubwa sana wa matumizi ya lugha ya kingereza. Sidhani kama kuna mtu kipindi kile angeweza kutilia shaka uamuzi wa baraza la chuo la UDSM kuheshimu mchango wake kwa ustawai wa lugha yetu maridhwa ya Kiswahili. Kuna watu wengi hapa Tanzania ambao wamepewa shahada mbalimbali za heshima na vyuo vya ndani na nje ya nchi lakini naomba nisiwataje maana sio msingi wa mada hii.
Umakini katika kutoa na kupokea Shahada za Heshima.
Utoaji na upokeaji wa shahada za heshima sio jambo jepesi na halitakiwi kuchukuliwa kimzahamzaha na chuo kinachotoa heshima hiyo au yule anayepokea. Wale wanaoshiriki katika michakato hii kwenye vyuo vikuu wanajua ni kwa kiasi gani mchakato huu “unapitishwa kwenye moto” ili kuhakikisha chuo hakifanyi hivyo kwa aibu na kumpa mtu asiyestahili. Jambo hili hufanyika kwa umakini na usiri mkubwa sana na jopo la wahadhiri waandamizi


 • Baadhi ya vyuo huko Magharibi, majina ya watu wanaotarajiwa kupewa shahada za heshima katika mahafali yanayofuata pamoja na sababu za kuwatunuku huwekwa hadharani mapema kama namna ya kuweka uwazi zaidi katika mchakato.
 • Pamoja na kwamba utoaji huu wa shahada za heshima ni sehemu ya tamaduni katika mahafali ya vyuo vikuu kila mwaka, wakati mwingine vyuo makini huamua kutokutoa heshima hizi kwa miaka kadhaa iwapo mchakato wao hutapata mtu ambaye anastahili na anabeba heshima ya chuo chao.  Kwa mfano, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam pamoja na kuwa na umri wa miaka 55 sasa tangu kuanzishwa kwake, kimeshatoa shahada za heshima kwa watu wasiozidi 30. Hii inamaanisha, kuna miaka zaidi ya 25 ambapo chuo hiki kikongwe nchini hakikuona mtu anayestahili heshima yao na hivyo kutolazimisha kuitoa. Wakati vyuo vingine huko Magharibi huwa vinatunuku hadi watu 10 PhD za heshima kwa mwaka mmoja, sina hakika kama UDSM imewahi kutoa kwa zaidi ya mtu mmoja kwa wakati/mwaka mmoja.
 • Vyuo vikuu makini huchukua taadhari kubwa katika utoaji wa shahada za heshima kwani vyakua kwamba mtu anayepokea heshima yao huendelea kufungamana na chuo hicho na anabeba taseira ya chuo husika maisha yake yote. Ni aibu kwa chuo kutoa shahada ya heshima kwa mtu ambaye yuko kwenye hatari ya kufanya jambo la aibu kwenye jamii na hivyo kuaibisha chuo kilichomtunuku heshima
 • Shahada ya heshima ni mali ya chuo kilichoitoa kwa kuwa anayepewa hajahusika kwa vyoyote vile katika kuitafuta na kuipata. Hivyo, chuo husika kina uwezo wa kumnyang’anya (revoking) mpokeaji shahada ya heshima waliyompa iwapo itathibitika kwamba mwenendo wake haustahili heshima waliyompa. Vyuo hulazimika kufanya hivyo kama namna ya kujitenga na mambo maovu yamuhusuyo mtu huyo na kuendelea kutunza heshima na taswira yao kwenye jamii
 • Kwa mfano, Mchekeshaji maarufu nchini Marekani aitwaye Bill Cosby ameshatunukiwa PhD za heshima na vyuo zaidi ya 60. Hata hivyo siku za karibuni Cosby ameshutumiwa kwa udhalilishaji na kubaka wanawake zaidi ya 60 nchini humo kitendo aanachoshutumiwa kukifanya kwa miaka mingi. Kesi inayomkabili Cosby imepelekea vyuo kadhaa kati ya vilivyomtunuku PhD za heshima kumwondolea heshima hiyo kwa kufuta PhD waliyompa.
 • Kama njia ya kutunza heshima zao, baadhi ya vyuo duniani vimejiwekea sera ya kutokutoa kabisa shahada za heshima. Mingoni mwa vyuo hivyo ni vyuo bora kabisa duniani kama vile Stanford University (USA), Cornell University (USA), Massachusetts Institute of Technology (USA) na Rice University (USA).


Kwa upande mwingine, kila anayepewa taarifa ya kuteuliwa kupewa shahada ya heshima na chuo kikuu chochote kile, ana mambo kadhaa ya kuzingatia kabla hajakubali heshima hiyo. Ni vema kujipa muda wa kufanya utafiti kidogo na kujiridhisha ustahili wako wa heshima usika kabla ya kuipokea.
 • Ajipime na kujitizama iwapo anastahili shahada ya heshima anayopewa. Je, sababu za heshima hiyo zilizoainishwa zinalingana na anavyojiona au alichofanya kwenye jamii? Ni ajabu sana iwapo utaitiwa tuzo ya kuwa baba aliyeonesha mfano wa malezi mazuri kwa watoto na ukaikubali wakati hujawahi kuoa, huna watoto wa kuwazaa, na hujawahi kulea watoto tegemezi.
 • Hao wanaotaka kukupa shahada hiyo ni kina nani? Wanatambulikaje na heshima yao ikoje mbele ya jamii? Itakua ajabu sana pale utakapoitiwa tuzo ya kuwa kiongozi bora na kundi la wauza unga, au wakwepa kodi, au majambazi na ukaenda kuipokea kwa sababu tu inaonesha umeheshimiwa.
 • Je kuna kitu kilichojificha nyuma ya heshima unayopewa? Wanaoataka kukupa wana jambo la siri lililojificha nyumba ya heshima yao? Tutamshangaa waziri wa elimu au mkuu wa nchi kuitiwa PhD ya heshima na chuo cha nje ambacho kiko kwenye mchakato wa kutafuta kibali cha uwekezaji nchini na akaenda kuipokea.
 • Heshima hiyo ina tija gani kwako na itakupa taswira gani kwenye jamii unayoitumikia? Unaweza kusimama mahali na kuitetea heshima hiyo kwa maneno na matendo yako?
 • Je kuna jambo la mbeleni linalokuhusu ambalo laweza kuwa chanzo cha wengine kukufungamanisha nao kaa PhD ya heshima ili waje kufaidika nawe hapo baadaye?
 • PhD unayopewa unaigharamia au yaendana na masharti yoyote? Unatakiwa kuingia gharama zozote kwa maana ya fedha au rasilimali kuigharamia heshima unayopewa? Itakua ajabu sana chuo kimuitie PhD ya heshima mtu mwenye staha na shahiki ya kuheshimika kwenye jamii, halafu kumuhitaji alipie ada na gharama zingine za mahafali ya kumtunuku.
 • Je, wajiona ukisumbuliwa na “mchecheto” wa kujitambulisha kwa degree ya heshima mara utakapopewa? Unajiona ukitaka kuitumia kujitafutia maslahi kwenye jamii au kwa nafasi uliyo nayo? Unajiona ukiitumia kulazimisha heshima kwako? Ukiyaona haya, jua kabisa hukustahili heshima uliyopewa. Nimetazama taarifa za Mzee Mkapa na kukuta hadi sasa ametunukiwa PhD za heshima tisa na zingine ni za vyuo vinavyoheshimika duniani. Hata hivyo sijawahi kumsikia akijitambulisha au kutambulishwa kama Dr. Benjamini Mkapa.
 • Je, unashangazwa au kushtuka unapopata habari za kupewa heshima na chuo kikuu? Je wajiona kama hustahili na umependelewa? Unapata kitu (substance) kwa maana ya mchango wako ukilinganisha na zilizotolewa na wanaotaka kukuheshimu? Kama wajiona hivyo baada ya kutaarifiwa, ni wazi hustahili heshima hii.


Maswali haya na mengine, yanaweza kumsaidia mtu anayependekezwa kutunukiwa PhD ya heshima kuwa kwenye nafasi nzuri ya kukubali heshima hiyo au vinginevyo. Hulazimiki au kushurutishwa na mtu yoyote kukubaliana na kila pendekezo la chuo chochote kinachotaka kukutunuku shahada ya heshima.  Mara nyingine utajikuta umeonesha kwamba unastahili heshima zaidi ya unayotaka kupewa iwapo utatazama vigezo na kusema, “Nashukuruni sana kwa kunifikiria lakini nasitikita kwamba siko tayari kupokea heshima munipayo”


Mara nyingi (kama sio zote) kwa vyuo makini duniani, wale wanaoalikwa kupewa shahada za heshima, hutakiwa kutoa hotuba ya kisomi katika sherehe za mahafali husika. Muhusika huandaa hotuba katika mada mahususi na mara nyingine wengi hutoa hotuba zao zikielekea kwenye mwelekeo wa heshima waliyopewa. Pamoja na kwamba huu ni utamaduni wa tukio hili, kwa upande mwingine husaidia kumwelewa yule anayetunukiwa na ni kwa jinsi gani anastahili kile alichotunukiwa.


Ni vema kukiri kwamba, utoaji wa shahada za heshima hata katika vyuo vyenye heshima, umeingiliwa sana na maslahi ya kisiasa. Ndio mana wingi wa shahada za PhD za heshima umekua ukielekezwa kwa marais au wakuu wa nchi hata pale ambapo uongozi wao ulikua na utata na kukosa kukidhi viwango vya utawala bora. Vyuo vingi hasa katika nchi maskini vimekua vikishindana kuwatunuka wakuu wa nchi zao PhD za heshima huku ikijulikana kwamba wakuu hao wana mamlaka na maamuzi makubwa juu ya uendeshaji wa vyuo hivyo na viongozi wake. Wako watu wengi kwenye jamii wanaostahili  kutambulika ikiwa ni pamoja na wanasiasa/viongozi kama vile mabunge na mawaziri lakini ni ngumu sana kuona wakitambulika na vyuo kwa kutunukiwa PhD za heshima. Badala yake heshima hizo zimekua zikielekezwa kwa wakuu wa nchi na kuonekana kama hazina mashiko na kuhoji iwapo viongozi wa vyuo vikuu hawafanyi hivyo kwa lengo la kujipendekeza kwa mkuu wa nchi.


Katika sehemu ya nne na ya mwisho ya makala nitaonesha kwa vielelezo maigizo ya utoaji shahada za heshima hapa Tanzania.


Imeandikwa na Mwalimu MM - Waweza mwandikia kupitia mmmwalimu(at)gmail.com